Sunday, February 23, 2014

TAARIFA KWA UMMA: SAKATA LA FIDIA YA ENEO LA MLOGANZILA

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ameendelea kufuatilia kuhusu fidia ya ardhi ya wananchi wa kata ya Kwembe waliohamishwa baada ya kulipwa fidia ya maendelezo pekee kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila.

Kwa upande mwingine, Mbunge Mnyika ameendelea pia kuhoji katika mamlaka mbalimbali juu ya kauli za viongozi wa Serikali kutamka kwamba eneo hilo lipo katika Mkoa wa Pwani badala ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar Es Salaam.

Tarehe 19 Januari 2014 Mbunge Mnyika alifika katika kata ya Kwembe na kukutana na wananchi kusikiliza malalamiko yao na mara baada ya mkutano huo alizikutanisha kamati mbili zinazofuatilia suala hilo.

Kufuatia hatua hiyo, Mbunge Mnyika aliwasiliana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwakumbusha kutekeleza ahadi zao za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo kufuatia hatua ya mbunge kuhoji suala hilo bungeni kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2011 mpaka 2013. (Baadhi ya rejea kutoka Kumbukumbu Rasmi za Bunge-Hansard zimeambatanishwa).

Saturday, February 22, 2014

Maoni yangu kuhusu matokeo ya kidato cha nne wa mwaka 2013


Maoni yangu kuhusu matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2013 yaliyotangazwa na kuelezwa kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.17 yamedhihirisha tahadhari niliyotoa kuhusu mabadiliko ya viwango vya ufaulu yaliyotangazwa na Serikali tarehe 30 Oktoba 2013.

Serikali kwa barakoa (veil) ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) imeamua kulificha taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa (Bad Results of Now). Hivyo, wachambuzi wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili nchi ijue hali halisi kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuweka wazi kwa umma ripoti za uchunguzi zilizoundwa kuwezesha wananchi kuihoji Serikali iwapo kupanda huko kwa ufaulu ni matokeo ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza au ni kiini macho cha mabadiliko ya wigo wa alama na madaraja?

Ukweli ni kuwa hali ya mazingira ya kujifunza na kujifunzia katika shule nyingi za msingi na sekondari hasa za umma sio nzuri kutokana na kutokuwa na vitabu vya kutosha, maabara za kutosha, waalimu wenye sifa wapo wa kutosha na kuboresha maslahi ya waalimu ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa siku nyingi.

Thursday, February 20, 2014

Rasilimali na mchakato wa kuandika Katiba Mpya

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa wadau wote wa masuala ya rasilimali kuzingatia kwamba rasimu ya katiba haijazingatia masuala ya msingi kuhusu haki ya wananchi kumiliki na kunufaika na rasilimali za nchi. Hatua hii ni kinyume na mapendekezo niliyoyatoa bungeni tarehe 22 Mei 2013 na maoni yangu niliyoyatoa mbele ya tume ya mabadiliko ya katiba pamoja na maoni yaliyotolewa na wadau wengine mbalimbali. 

Katika hotuba yangu ya Bungeni nilitaka Serikali isitishe kuendelea kunadi leseni za vitalu vya gesi mpaka kwanza mchakato wa katiba mpya ukamilike na pawepo sera na sheria zitazoongozwa na katiba mpya. Nilieleza kwamba katiba mpya inapaswa kuwa na ibara mahususi ya haki za wananchi kuhusu rasilimali ikiwemo ardhi, madini, gesi, mafuta, maji, misitu na maliasili zingine. Hata hivyo, katika rasimu ya katiba sura ya nne sehemu ya kwanza inayohusu haki za binadamu hakuna haki yeyote iliyotolewa kwa wananchi kuhusu kumiliki na kunufaika na rasilimali. Nitapendekeza kwa Bunge Maalum ibara mahususi kurekebisha udhaifu huo

Kwanini ni muhimu tushirikishe wananchi katika kutunga kanuni za Bunge Maalum

Kwenye kikao cha juzi cha Bunge Maalum nilipendekeza umuhimu wa suala la ushirikishwaji wa wananchi na wadau mbalimbali katika kutengeneza kanuni (Soma hapa: http://goo.gl/b0nQVA) . Wapo wenye mtazamo kwamba kanuni kwa kuwa ni za Bunge Maalum, kuandaa na kupitisha rasimu hiyo ni suala la wajumbe wenyewe pekee; hakuna ulazima wa wadau wala umma kushirikishwa.

Hata hivyo, kwa uzito na unyeti wa kanuni zenyewe na kwa kuzingatia kwamba mjumbe anapaswa kuzingatia maoni ya aliyemtuma ni muhimu umma ujue na kushiriki.

Pia, izingatiwe kwamba Bunge Maalum linapoendelea upo wakati wadau na wananchi wanataka kufuatilia kuhakikisha maoni na maslahi yao yanazingatiwa na wajumbe wao.

Hivyo, ni muhimu kushirikishwa kupata kuwezesha kanuni kuruhusu fursa hiyo. Ni wajulishe tu kwamba rasiu ya Katiba kuchakachuliwa badala ya kuboreshwa. Nitafanya uchambuzi wa vifungu hivyo vibovu na hatimaye nitawasilisha mapendekezo ya maboresho kwa Bunge Maalum.

Wednesday, February 19, 2014

Uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga: CHADEMA yamekea pingamizi CCM!

CHADEMA imemuwekea pingamiza mgombea wa CCM kwamba sio raia wa Tanzania. 

Kazi imeanza!

Mkakato wa Katiba Mpya: Wadau washirikishwe kutunga kanuni Bunge la Katiba

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amesema atawasilisha mapendekezo ya kutaka ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ibadilishwe, ili wadau washirikishwe kwenye mchakato wa kutunga kanuni za Bunge hilo.

Mnyika alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Alisema ratiba iliyotolewa inaonyesha kwamba baada ya kusomwa kwa tangazo la kuitisha Bunge hilo na uchaguzi wa mwenyekiti wa muda, kazi ya kutunga kanuni itaanza.

Mnyika alisema kanuni ndiyo msingi wa kufikia mwafaka wa kuboresha rasimu ya Katiba badala ya kuchakachua na kwamaba ili zisitungwe kanuni mbovu ipo haja ya wadau wote wanaohusika na mchakato wa Katiba mpya ndani na nje ya Bunge kushiriki. 

“Nakusudia kuwasilisha mapendekezo kwamba ratiba ya Bunge ifanyiwe mabadiliko ili kuwapo na kikao cha kusikiliza umma (Public hearing), juu ya kanuni hizo ili mawazo ya wadau yazingatiwe katika maandaluzi ya kanuni kabla ya Bunge kupitisha azimio la kuridhia kanuni hizo,” alisema Mnyika.

Tafakari ya leo!


Tuwe wepesi wa kusikia si kusema wala kukasirika.

Tuwe watendaji sio wasikiaji tu.

Dini safi ni matendo mema.


-Funzo toka Yak. 1:19-27

Fursa kwa kijana kufanya kazi Ofisi ya Mbunge

Feb 2014 ni mwaka 1 toka nilipowasilisha Bungeni Hoja Binafsi ya kupendekeza Bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka kuboresha upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiwaji wa Maji Taka katika jiji la Dar es Salaam. Soma hapa: http://goo.gl/Q770zm Natumia fursa hii kutangaza nafasi ya kazi ya mwezi 1 ya kutathmini mafanikio na vikwazo kwa kijana wa ndani ya Jimbo la Ubungo (Mwanamke au Mwanaume) aliyetayari kufanya kazi ya mwezi 1 ya kutathmini hatua za haraka juu ya suala la Maji ndani ya jiji la Dar es Salaam afike Ofisi ya Mbunge, Halmashauri ya Kinondoni.

John J. Mnyika
Mbunge wa Ubungo
19.02.2014

Tuesday, February 18, 2014

Hon. John Mnyika's witness statement regarding The Election of Tanzania’s East African Legislative Assembly

IN THE EAST AFRICAN COURT OF JUSTICE
FIRT DIVISION
AT ARUSHA
REFERENCE NO.07 OF 2012
(In the matter of interpretation of Article 50 of the Treaty for the Establishment of the East African Community)
BETWEEN
ANTON CALIST KOMU………………….CLAIMANT
AND
THE HONOURABLE ATTORNEY GENERAL OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA…………………….......RESPONDENT


WITNESS STATEMENT OF JOHN MNYIKA

I, John Mnyika Member of Parliament of the United Republic of Tanzania for Ubungo Constituency, make the following witness statement regarding The Election of Tanzania’s East African Legislative Assembly members:

I wrote a letter dated 8th February 2012 with reference no. OMU/BJMT/004/2012 to the Clerk of The Parliament of United Republic of Tanzania requesting amendment  to be  made in the third schedule of the Parliamentary Standing Orders (The East African Legislative Assembly Election Rules).

I made those proposals commensurate with the requirement of sections 3(3)(a) and (b) of the eighth schedule made under standing order 115 of the Parliamentary Standing Orders (2007 Edition).

I requested the Clerk to recall what transpired in the Election of East African Legislative Assembly that was conducted in the Parliament of the United Republic of Tanzania on the 2nd of November 2006. 

In that particular election complains arose and were raised that indicated the need for amendment of the East African Legislative Assembly Election Rules of the Parliament of the United Republic of Tanzania. I also drew to the attention of the Clerk that The East African Assembly had passed the EALA elections Act of 2011.

Monday, February 17, 2014

Mrejesho wa leo Februari 17: Jitihada za kuboresha barabara jimboni Ubungo na mengineyo

1. Barabara ya Goba-Mbezi Louis nawaomba wananchi wenzangu mfuatilie matengenezo yaliyoanza na kutoa mrejesho; lami kidogo nayo itaanza. Tuungane kupendekeza nyongeza bajeti hii

2. Barabara ya Malambamawili-Msigani naombeni tathmini ya matengenezo yaliyofanyika; ujenzi wa lami utaanzia kipande cha Kinyerezi-Kifuru. Kwa hii sasa ni hatua.

3. Barabara ya Bonyokwa-Mavurunza Kimara mwisho; nimewasiliana na Manispaa ya Kinondoni kukumbusha utekelezaji wa ahadi ya matengenezo. Majibu kesho.

4. Barabara ya Matete-Jeshini-Golani haikutengewa fedha KMC, nimewatumia ujumbe TANROADS wakishughilikia Msewe wasogee

5. Barabara ya Mavurunza-Golani-Msewe-Matete hali ya barabara ni tete. Nimewasiliana na diwani Pascal Manota na kumtumia posho ya leo kuweka mafuta grader. Ikiwa unatumia barabara za Mavurunza-Golani-Matete wasiliana na Diwani 0713792966 utuunge mkono sasa; mamlaka zingine nazo tunazifuatilia

Friday, January 31, 2014

Mwito kwa wananchi kutoa maoni kuhusu sheria ndogo

 
Nimerejea jimboni kikazi, pamoja na ufuatiliaji kuhusu kasoro za ujenzi unaendelea katika Barabara ya Morogoro na matengenezo yanayohitajika katika barabara zinaunganika na barabara hiyo katika maeneo ya pembezoni kupunguza foleni, lipo suala linalohitaji mjadala na maoni ya haraka toka kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Tangu mwaka 2013 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa katika mchakato wa kutunga sheria ndogo nne: ya matumizi ya barabara, ushuru wa masoko, ada na ushuru na ushuru wa huduma. Mwanzoni mwa mwaka huu 2014 katika kikao cha Baraza la madiwani ilibainika kwamba sheria hizo zilikaribia kupitishwa bila ya ushirikishwaji wa kutosha wa wadau na wananchi.

Halmashauri iliongeza muda wa kupokea maoni; hata hivyo muda ukiwa unaelekea ukiongoni, ikiwa imesalia takribani wiki moja, tathmini ya ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo inaonyesha kwamba sheria hizo hazijasambazwa vya kutosha kwa wananchi na wadau kwa ajili ya kutoa maoni yao katika kata na mitaa mbalimbali.

Hivyo, ofisi ya mbunge Jimbo la Ubungo leo tarehe 31 Januari 2014 itafanya kazi ya kusambaza Sheria hiyo kwa njia mbalimbali kwa ajili ya wadau na wananchi kupitia na kutoa maoni yao. Mkazi wa Jimbo la Ubungo anayehitaji kutoa nakala anaweza kuwasiliana na Katibu Msaidizi Aziz Himbuka kupitia 0784379542 au 0715379542 au kwa kuwasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni moja kwa moja.

Wednesday, January 22, 2014

Ufafanuzi kuhusu upanuzi na mgogoro wa kuhusu upana wa barabara ya Morogoro

Kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2004 na 2013 nimezungumzia haja ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro kutoka Jimboni Ubungo kupitia Kibaha mpaka Chalinze na mgogoro uliodumu muda mrefu kuhusu upana wa Barabara hiyo.

Ningependa kutoa ufafanuzi kwamba nyakati zote nimeunga mkono upanuzi wa Barabara hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo kuwa njia sita (tatu kwenda na tatu kurudi).

Hata hivyo, mara nyingi nimekosoa masuala manne kuhusu upanuzi na mgogoro kuhusu upana wa barabara ya Morogoro:

Mosi, Serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Mwaka 2012 na 2013 Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli amekuwa akirudia kauli kwamba ujenzi wa Dar Es Salaam-Chalinze express road kuanza. Katika mkutano wangu na wananchi jimboni tarehe 19 Januari 2014 kuhusu ujenzi wa Barabara hiyo, nimesisitiza kwamba fedha za ujenzi wa barabara hiyo hazijatengwa hivyo ujenzi hauwezi kuanza. Badala yake nilifafanua kwamba Serikali inachokifanya kwa sasa ni kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa kutafuta fedha na kujenga. Hivyo, ni muhimu Serikali ikawaeleza wananchi ukweli na kuharakisha kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa miaka mingi.

Wednesday, January 15, 2014

TAARIFA KWA UMMA: Kero ya maji Dar na taarifa za kina


Rais Jakaya Kikwete amwondoe Prof. Jumanne Maghembe nafasi ya Waziri wa Maji kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka za kuongeza upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam na nchini kwa ujumla.

Rais Kikwete azingatie kwamba tarehe 10 Januari 2014 nilimtumia ujumbe Waziri Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, kufutia maelezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Hawa Sinare kuhusu sababu za kuchelewa kwa miradi ya maji Jijini na majibu ya Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) Jackson Midala kuhusu kujirudia kwa matatizo ya maji; Rais Kikwete akumbuke ahadi yake ya kuitisha kikao Ikulu kujadili masuala maji mwezi Machi 2013 ambayo mpaka sasa hajaitekeleza.

Ikumbukwe kwamba mara baada ya kujirudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam niliwasiliana na mamlaka husika ziweze kuchukua hatua na pia nilitaka Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo za matatizo hayo.

Taarifa kwa Umma-Nishati ya Umeme


Kufuatia ukimya wa Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka nyingine tangu nitoe mwito kwao tarehe 9 Januari 2014 juu ya ongezeko la bei ya umeme; namshauri Rais Jakaya Kikwete katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kumtaka Waziri Prof. Sospeter Muhongo kujieleza kwake na kwa umma kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.

Rais Kikwete akumbuke kwamba Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.

Kinyume na kauli za Waziri Prof. Muhongo; Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania hatua ambazo nazo zina athari katika uchumi na maisha ya wananchi.

Thursday, January 9, 2014

Waziri Prof. Maghembe ajiuzulu: DAWASA/DAWASCO warejeshe huduma ndani ya wiki moja katika maeneo yaliyokuwa yakipata mgao wa maji kabla

Nimemtumia ujumbe Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kumshauri ajiuzulu kutokana na kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam kinyume na maelezo yake ya uongo aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.

Aidha, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Mamlaka zinazohusika na huduma ya maji jijini (DAWASA na DAWASCO) watoe maelezo kwa umma juu ya sababu za kweli za matatizo ya maji kujirudia rudia katika Jiji la Dar Es Salaam.

Pia, wajieleze kwa umma ni kwanini wananchi wasipendekeze Rais awachukulie kwa uzembe, kuisababishia hasara Serikali, kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kukosa maji mara kwa mara ambayo ni huduma ya msingi ya binadamu na malighafi muhimu katika uzalishaji.

Itakumbukwa kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam, nikipendekeza Bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka.

Iwapo hoja hiyo ingejadiliwa na maazimio yote kutekelezwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar Es Salaam mpaka hatua ya sasa yangekuwa yamepungua katika maeneo mbalimbali kutokana na hatua ambazo nilipendekeza zichukuliwe.

Kauli ya awali kuhusu ongezeko la bei za umeme

Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania.

Maamuzi hayo ya Bodi ya EWURA ambacho ni chombo cha Serikali yamethibitisha kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.