Wednesday, August 1, 2012

BUNGE LISIZUIWE KUINGILIA KATI MGOGORO KATI YA WALIMU NA WANAFUNZI DHIDI YA SERIKALI KWA KISINGIZIO CHA KESI KUWA MAHAKAMANI

Tarehe 1 Agosti 2012 niliieleza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia swali langu la msingi bungeni kwamba serikali hutoa ruzuku (capitation grants) kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari za Umma zikiwemo za Jimbo la Ubungo, japo utekelezaji wa sera husika huwa unasuasua sana kwa kiwango kilichowekwa kutokulingana na mahitaji halisi ya wanafunzi; viwango vinavyotengwa katika Bajeti ni chini ya vinavyotajwa kwenye Sera na Fedha hazitolewi zote isipokuwa hutolewa kidogo kidogo na hazifiki kikamilifu mashuleni; nikahoji ni lini serikali itarekibisha hali hiyo ili kuboresha elimu nchini.

Ofisi ya Waziri Mkuu katika majibu yake imekiri kwamba kweli viwango vya ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari havijafikiwa mpaka sasa na hata fedha zinazotengwa kwa mujibu wa bajeti hazitolewi kwa kiwango kilichopitishwa na bunge kwa kile alichoeleza kuwa ni makusanyo ya Serikali.

Niliuliza maswali mawili ya nyongeza; nilihoji ni lini serikali itatekeleza sera husika kwa kuwa upungufu wa ruzuku kwa shule za umma ni kati ya vyanzo vya kuporomoka kwa elimu kutokana na kuathiri uendeshaji wa shule ikiwemo upatikanaji wa vifaa shuleni, na kwa kuwa kwenye vyombo vya habari jana na leo kati walimu na wanafunzi wameeleza kwamba hali hiyo ni kati ya sababu za mgomo unaoendelea hivyo nikata serikali itoe kauli bungeni ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoendelea.

Hata hivyo Spika wa Bunge alimkataza Naibu Waziri asijibu swali kuhusu mgogoro kati ya walimu na wanafunzi dhidi ya serikali na kutaka kujibiwa kwa swali ya lini ruzuku itaanza kutolewa kwa kuzingatia viwango vya sera hata hivyo serikali ilitaja kiwango cha fedha ya ruzuku kwa mwaka wa fedha 2012/2013 bila kueleza iwapo viwango kwa mujibu wa sera vitafikiwa kwenye ngazi zote ikiwemo katika shule za msingi.

Kwa mara nyingine tena Bunge limezuia kupewa taarifa kuhusu masuala hayo kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani hatua ambayo inadhihirisha kwa mara nyingine tena umuhimu wa kusikilizwa kwa rufaa niliyokata tarehe 31 Julai 2012 ili suala la mgomo wa walimu, madai ya wanafunzi na hatma ya sekta ya elimu lijadiliwe kwa dharura bungeni.

Nimefanya hivyo kwa niaba ya walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu katika Jimbo la Ubungo na Tanzania kwa ujumla ili bunge lipewe fursa ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba kuisimamia serikali itekeleze madai ya walimu na kuepusha athari za migogoro inayoendelea katika shule za umma nchini.

Tarehe 30 Julai 2012 kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo na maamuzi na Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai ya kukataa hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 47 ya kuahirishwa kwa Shughuli za Bunge kujadili jambo la dharura la mgomo wa walimu na yatokanayo na mgomo huo kwa kutumia kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 ambayo inamkataza mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama.

Nimewasilisha rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) kueleza kutoridhika na uamuzi wa Naibu Spika wa kutumia kanuni ya 64 (1) (c) kudhibiti Bunge kutumia uhuru na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya nchi; sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge na kanuni nyingine za Kanuni za Kudumu za Bunge kwa sababu tatu.

Mosi, Suala la yatokanayo na mgomo wa walimu hususani hali tete ya sekta ya elimu kwenye shule za umma haliko mahakamani, kilichopo mahakamani ni mgogoro kati ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na serikali kuhusu madai ya walimu:

Pili, hata masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Tatu; izingatiwe pia kuwa masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kwa kuzingatia sababu nilizozieleza, nimeomba kamati ya kanuni ibatilishe maamuzi yaliyofanyika na kutoa pia muongozo wa kikanuni; hivyo nimeomba Katibu wa Bunge amtaarifu Spika kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa.

Wako katika kuwawakilisha wananchi,


John Mnyika (Mb)

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, CHADEMA

01 Agosti, 2012

3 comments:

Anonymous said...

gud responsibilities

no said...

hongera kaka kwa kutupigania wanyonge,lakini naomba msaada wako kuhusu sheria za usalama bararani,makosa ya pikipiki hutizwa faini ya sh.ngapi kwa kosa moja maana hapa morogoro kuna zoezi linaendelea hatulielewi

Anonymous said...

big up kaka mnyika na wao wana haki ya kusikilizwa kama watumishi wangine. hongera sana kwa kuwatetea wanyonge.