Nimeziandikia
mamlaka husika za Serikali kutoka ofisini na kwenda kukagua wa ubovu wa
barabara za Kimara-Mavurunza-Bonyokwa, Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani- Mabibo
External, Makuburi-Kibangu-Makoka ili kuweza kufanya maamuzi ya matengenezo ya
haraka.
Nimechukua
hatua hiyo baada ya kuona hali halisi ya barabara hizo nilipozitembelea kati ya
tarehe 24 na 25 Agosti 2012 na pia kutokana na maoni ya wananchi niliokutana
nao katika tarehe hizo kwenye kata za Kimara, Mabibo na Makuburi.
Kwa
upande wa Barabara ya Kimara-Mavurunza-Bonyokwa ambayo tayari Wizara ya Ujenzi
imekubali kuihudumia, leo tarehe 27 Agosti 2012 nitapeleka barua kwa meneja wa
TANROADS Mkoa wa Dar es salaam kutaka hatua zake kwa hali mbovu ya barabara
hiyo pamoja na kuwa kero wa wananchi inamwaibisha Rais Kikwete mbele ya wakazi
husika kwa kuwa alitembelea mwaka 2010 na kuahidi itajengwa kwa kiwango cha
lami.
Aidha,
mwaka 2011 ilifanyiwa matengenezo ya kawaida lakini kwa sasa imeharibika tena
kufuatia mvua zilizonyesha, hali mbovu ya barabara hiyo inaathiri pia hatua za
kupunguza msongamano kwenye barabara ya Morogoro wakati huu ujenzi wa mradi wa
mabasi yaendayo haraka (DART) unapoendelea kwa kuwa barabara hiyo hutumika kama
njia mbadala kutoka Manispaa ya Kinondoni mpaka Manispaa ya Ilala.
Kuhusu
barabara Ubungo Maziwa-Kisiwani Darajani-Mabibo External leo nitamkumbusha Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya barabara kwa mkoa
afuatilie kutoka mfuko wa barabara fedha za ujenzi wa daraja kwa dharura kwa
kuwa kwa hali ya sasa na uzito wa magari yanayopita daraja linaweza kuvunjika
na kusababisha maafa. Aidha, asimamie pia utekelezaji wa upande wa TANROADS kwa
kuwa fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo zilishatengwa katika bajeti ya
mwaka wa fedha 2011/2012 na nyingine katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.
Kwa
upande wa barabara ya Makuburi-Kibangu-Makoka mpaka sasa matengenezo yanasubiri
malipo yafanyike ya fidia ya nyumba chache zilizobaki kiasi cha shilingi
milioni 64, suala ambalo Manispaa ya Kinondoni inapaswa kulitolea kauli kwa
kuwa lilipaswa kukamilika katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe
30 Juni 2012, leo nimemuagiza katibu msaidizi wa mbunge kufuatilia suala hilo
katika ofisi za Manispaa. Mpaka kufikia tarehe 3 Mei 2012 jumla ya shilingi
milioni 122 zilikuwa zimeshalipwa kama fidia, hivyo Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Manispaa ya
Kinondoni kuharakisha malipo ili kuepusha gharama za fidia kuongezeka kwa
kuzingitia kuwa iwapo malipo yangefanyika kwa wakati mwaka 2010 gharama za
fidia zingekuwa milioni 80 tu lakini sasa zimeongezeka mpaka kufikia zaidi ya
milioni 180.
Wakati hatua za haraka za serikali zikisubiriwa
kuwezesha matengenezo makubwa nitawaeleza karibuni utaratibu kwa kushirikiana
na madiwani kwa ajili ya kuunganisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine
ili kufanya matengenezo madogo kupunguza kero.
Izingatiwe
kuwa tarehe 24 na 25 Agosti 2012 nimekwenda mitaa mbalimbali ya kata 12 kati ya
14 za Jimbo la Ubungo kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa ya watu na
makazi na kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya.
Aidha
wananchi niliokutana nao wamepata fursa ya kuuliza maswali kuhusu hatua
iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na mrejesho
kuhusu mkutano wa nane wa bunge ambapo pamoja na kupata majibu nimepokea pia
mapendekezo ya masuala ya kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia
jimboni katika kipindi cha mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa
mkutano wa tisa wa bunge na pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013.
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
27/08/2012
1 comment:
Mbunge wangu nakushukuru sana kwa mrejesho huu muhimu na wa kueleweka. Tunasubiri tu utekelezaji wa haraka wa hatua hizi. Naamini kabisa kuwa kama madiwani wetu wakifuatilia kwa karibu hatua ambazo umeshazichukua ni wazikuwa wahusika watakuwa punctual.
Barabara yetu ya kuja makoka angalau kwa sasa inapitika bila tabu nyingi baada ya greda kuchimba lakini hatua zaidi hasa kuweka mitaro na kusawazisha pamoja na kuwa na outlet ya kuaminika kuingia Mandela Road ni muhimu ili kuongeza idadi ya daladala ziendazo makoka na kurasimisha njia ya daladala. Hivi vitapunguza adha kwa wananchi na kujenga imani ya wananchi kwa serikali.
Hata hivyo mbunge wangu jambo muhimu ni kwa wananchi kuwa na imani na wewe mbunge ambaye walikuchagua kwa kura nyingi na imani kubwa. Usikubali kurudishwa nyuma na madiwani. Wao ndiyo mikono na miguu yako kwa wananchi, wao ndiyo macho na masikio yako kwa wananchi. Wakilala wao wananchi watapoteza imani na sisi CHADEMA.
Tunwajibika sote kwa maendeleo yetu.
Emmanuel P Lema
box 35041 DSM
0717/0767 151125/0686 878384
Post a Comment