Tuesday, August 28, 2012

DAWASCO NA DAWASA WASHUGHULIKIE MATATIZO YA MAJI MBEZI


Nimefuatilia Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na kujulishwa kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa kuhusu matatizo ya maji yanayoendelea katika maeneo mengi ya kata za Mbezi Luis na Msigani kwa takribani wiki tatu kufuatia ratiba ya mgawo wa maji kuathiriwa na kuhamishwa kwa huduma ya maji kutoka katika bomba la maji la inch 24 mpaka la inch 30. Hali hiyo imeathiri zaidi maeneo ya Magari Saba, Kibanda cha Mkaa, Kwa Msuguri, Temboni na maeneo mengineyo. 


Aidha, kuhusu maghati ya umma na maeneo ya pembezoni ambayo yalikuwa na matatizo makubwa ya maji kabla hata ya kipindi husika ikiwemo maeneo ya Bwaloni na Msingwa, nimeiandikia barua Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kuwaalika kufanya nao ziara ya kikazi mapema iwezekanavyo katika maeneo husika kwa ajili ya kutoa maelezo ya kiutendaji kuhusu hali iliyopo na kueleza mipango inayopaswa kutekelezwa ya kupata ufumbuzi wa haraka.

Natoa taarifa hii kwa kuzingatia kuwa tarehe 25 Agosti 2012 nilipokutana na wananchi katika eneo la Mbezi kwa Msuguri wakati nikiwa katika kazi ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa, kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya na kupata mapendekezo yao kuhusu masuala ya kuyapa kipaumbele baada ya kurejea kutoka katika mkutano wa nane wa Bunge nilielezwa kuhusu matatizo ya maji katika maeneo tajwa.

Kufuatia maswali yaliyoulizwa na masuala yaliyoelezwa nilitoa majibu ya ujumla kwamba: Mosi, kuhusu matatizo yaliyojitokeza nilieleza kuwa chanzo chake ni marekebisho yaliyokuwa yakiendelea ya kuondoa baadhi ya watu waliokuwa wamejiunganisha maji kinyemela katika mabomba makuu pia kuhamisha huduma kwa wananchi wa maeneo tajwa kutoka bomba la inch 24 mpaka la inch 30, hata hivyo kwa kuwa matatizo hayo yameendelea niliahidi kuwasiliana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na kutoa majibu ya hatua za kuharakisha huduma ya maji kurejea katika hali ya kawaida.

Pili, kuhusu maeneo ambayo yalikuwa hayatoki maji hata kabla ya wiki tatu ikiwemo baadhi ya maghati ya umma na maeneo ya pembezoni nilieleza chanzo cha hali hiyo kwa kadiri ya majibu niliyoelezwa na DAWASCO nilipofanya nao ziara katika kata ya Msigani tarehe 1 Machi 2012 na kwa kuwa matatizo katika maeneo hayo yanahitaji hatua kubwa zaidi niliahidi kwamba nitawaalika Watendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) ili kufanya nao ziara ya kikazi karibuni kuweza kutafuta ufumbuzi.

Izingatiwe kwamba kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali na vyombo vyake kuwezesha maendeleo, na katika muktadha huo Machi Mosi 2012 niliungana  pamoja na DAWASCO kwenye kata za Sinza, Makurumla, Mburahati, Msigani, Mabibo, Saranga, Kwembe na Makuburi kufuatilia kazi za kuboresha upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Kupitia ushirikiano huo tuliona bayana kwamba mtandao wa biashara haramu ya maji unaohusisha kujiunganisha mabomba ya maji kinyemela nao unachangia katika matatizo ya maji katika baadhi ya maeneo, mathalani tuliona mota za biashara hizo katika  maeneo ya kata ya Makurumla hususani mtaa wa Kagera, Makuburi kwenye nyumba yenye matanki yaliyounganishwa chini chini kwa ajili ya biashara ya maji na Kata ya Saranga eneo la Kimara B ambapo mtandao wa maji ulitolewa toka kwenye maeneo ya wananchi na kupelekwa nje ya makazi ya watu kwenye mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa maji. Mitandao hiyo ilianza kukatwa na majalada yalifunguliwa polisi kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua za kijinai.

Hali hiyo ilishamiri kutokana pia na vishoka na tulikubaliana kwamba kuanzia wakati huo yoyote anayekwenda kugusa bomba la DAWASA lazima kwamba aripoti kwenye serikali za mitaa na pia popote anapofanya kazi hizo lazima awe na kitambulisho cha DAWASCO na pia kadi ya kazi (job card) yenye saini ya meneja wa eneo ya kueleza aina ya kazi na ruhusa iliyotolewa kuifanya. Nachukua fursa hii kuwakumbusha wananchi kuchukua hatua dhidi ya yoyote anayekwenda kinyume na makubaliano hayo kama ilivyo kwa wahalifu wengine wanaokiuka sheria.

Katika kazi tulizofanya Machi Mosi 2012, ilionekana bayana kwamba bado yapo maeneo ambayo mtandao wa mabomba ya wachina hautoi maji kutokana na msukumo mdogo na matatizo ya mfumo mzima, kama ilivyo katika majimbo yote ya Dar es salaam, Kwa upande wa Jimbo la Ubungo hali hii imeathiri maeneo ya Malambamawili, kwa Msuguri, Makoka na mengine. Aidha, yapo maeneo ambayo hayakufikiwa kabisa kwenye awamu ya kwanza ya utandazaji wa mabomba husika mathalani ya Msingwa, Mbezi Msumi na mengineyo katika jiji la Dar es salaam.

Haya ni masuala yanayohusu mwenye mali na miundombinu ambaye ni Serikali kupitia Wizara ya Maji na DAWASA, zaidi ya DAWASCO ambayo pamoja na kuwa nalo ni shirika la umma ni mwendeshaji tu. (Maji DSM ni kama duka, kuna mwenye bidhaa ambaye anawajibika kujaza duka lake ili wateja wasikose-DAWASA na muuza duka ambaye ana kazi ya kuuza duka lenye bidhaa chache-DAWASCO malalamiko mengi ya wateja yanamuangikia yeye).

Kufuatia hali hiyo niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge hoja Binafsi kwenye mkutano wa nane wa Bunge uliomalizika kutaka bunge lipitishe maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam; hata hivyo hoja hiyo haikupangiwa kujadiliwa bungeni kutokana na ufinyu wa muda baada ya ratiba ya bunge kufanyiwa marekebisho na kipengele cha hoja za wabunge kuondolewa. Kutokana na hali hiyo, wakati nikisubiri mkutano tisa wa bunge unaofuata niendelee na kazi zingine ikiwemo kuwaandikia DAWASA ili wafike jimboni Ubungo na kuchukua hatua kwa masuala ya maendeleo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Wenu katika uwakilishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
27 Agosti 2012




3 comments:

Anonymous said...

Nakushukuru Mbunge wetu Mnyika kwa jitihada za maksudi uzifanyazo za kututatulia kero zinazotusibu wanachi wa jimbo lako la Ubungo. Tutashukuru zaidi na zaidi endapo kero hii itatatuliwa maana wanamalamba mawili tuna hali mbaya sana. Tunakuoba usikate tamaa kutokana na vikwazo unavyokumbana navyo katika kutuwakilisha huko, tunakuombea pia Mungu akutangulie katika kazi zako na akupe busara na hekma katika utekelezaji wa majukumu yako.

Mkazi wa Malamba mawili

Anonymous said...

Salaam Mheshimiwa.
nikiwa mkazi wa Mbezi Makabe Mjimpya napenda kukutaarifu kuwa, sisi wa kazi wa eneo hili tuna matatizo makubwa yafuatayo mabayo kwa sasa ni sugu na hatuoni kama kuna dalili ya kupatiwa suluhusho.
- Tatizo la bara bara kutoka Mbezi Mwisho stand ya Zamani, bara bara hii hatujui ni nani hasa ,mwenye jukumu la kufanyia matengenezo hii barabara, ina makorongo na mara ya mwisho kutengenezwa ni muda mrefu hata hatujui. Tunashukuru kwa daraja kutengenezwa lakini bara bara ni tatizo kusababisha dala dala kupandisha nauli kwa ajili ya ubovu wa bara bara.

- Tatizo la maji, hili ni tatizo sugu kwa eneo letu la mji mpya, tumekuwa kwenye mikono ya wanfanya biashara ya maji kwa sababu tu hatuna na mna ya kupata maji. hi hatuwezi kuweka tank kubwa na kuweza kutusambazia maji, sisi tunaweza kuchangia hilo tunahitaji viongozi thabiti tu. Inasemekana wafanya biashara wa maji ndio wanaohujumu miradi ya maji nen hili, tunakuomba Mbunge wetu simamia hili tutakuunga mkono.

Ni mimi mpiga kura wako, mkazi wa Mbezi Makabe Mji mpya.

giaonhan247 said...

Thanks for sharing, nice post! Post really provice useful information!

FadoExpress là một trong những top công ty chuyển phát nhanh quốc tế hàng đầu chuyên vận chuyển, chuyển phát nhanh siêu tốc đi khắp thế giới, nổi bật là dịch vụ gửi hàng đi nhậtgửi hàng đi pháp và dịch vụ chuyển phát nhanh đi hàn quốc uy tín, giá rẻ