Monday, February 22, 2010

Kauli ya Waziri Mkuu Pinda juu ya Rostam Aziz ‘imepinda’ na ‘inapindisha’ mambo

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewashauri wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora wasimkatae Mbunge wao Rostam Aziz wakati wa uchaguzi mkuu ujao kwa kusikia maneno yanayosemwa bungeni, badala yake wazingatie kile alichowafanyia. “Iwapo mnataka kumchagua tena Rostam zingatieni amewafanyia nini katika ubunge wake. Msisikilize kile kinachosemwa bungeni juu yake. Bunge lina mambo yake, mimi kama Waziri Mkuu nafahamu mambo ya pale bungeni,” alisema Waziri Mkuu. (Chanzo, Habari Leo-Gazeti la umma).

Kauli hii ya Pinda ‘imepinda’ na inajaribu ‘kupindisha’ mambo:
Kwanza amefanya kampeni za kumnadi mbunge wa chama chake CCM kwa kutumia cheo chake cha Uwaziri Mkuu katika ziara ya Kiserikali inayogharamiwa na kodi za wananchi wote bila kujali itikadi; huu ni ubaguzi na matumizi mabaya ya madaraka kwa mujibu wa katiba na sheria.
Pili, amebeza bunge kuwa lipuuzwe kwa kuwa linayoyajadili hayana maana kwa wananchi hivyo wazingatie yanasemwa bungeni. Ni muhimu angeyataza hayo ‘mambo yake’ ya bunge ambayo yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anayafahamu. Huku ni kudharau hadhi ya bunge kwa mujibu wa katiba na sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge.
Tatu; kwa hiyo kwa mantiki ya waziri mkuu ni kwamba mtu akifanya ufisadi na/ama matumizi mabaya ya madaraka lakini akatumia sehemu ya fedha zake kwenda kuwafanyia kuwafanyia wananchi wa jimbo lake ‘mambo kadhaa’ basi huyo aendelee tu kuwa na haki zote za kuwa kiongozi wa umma.

Waziri Mkuu akasome tena Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka namba 13 ya mwaka 1984( iliyofuta sheria namba 9 ya mwaka 1983) pia akasome Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 5 ya mwaka 2001 na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini namba 11 ya mwaka 2007; halafu ajibu kwanza tuhuma kuhusu Richmond, Dowans, Kagoda nk kabla ya kuanza kutoa kauli za kusafisha watuhumiwa waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi (List of Shame). Lakini siwezi kushangaa sana, ni Waziri Mkuu Pinda huyu huyu alilidanganya bungeni kuwa Meremeta ni Siri ya Jeshi hivyo hawezi kujibu chochote; kampuni yenye tuhuma ya ufisadi wa mabilioni mengi kuliko kashfa ya akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu (BOT). Huwa najiuliza, kama huyu ni Pinda maarufu kama mtoto wa Mkulima anayetajwa pia kuwa ni mtumishi wa usalama wa taifa; ni nani atakayesimama ndani ya Serikali na CCM kusimamia maadili na uwajibikaji?

Haya ndio matokeo ya uongozi kuingia madarakani kwa kufadhiliwa na watuhumiwa wa ufisadi. Narudia tulichosema mwaka 2005: Mabadiliko ya Kweli, hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa Ari, Nguvu na Kasi(ANGUKA) mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema (ccm) Tanzania yenye neema haiwezekani. Tunahitaji mabadiliko ya uongozi na mfumo wa utawala kuondoa hodhi(monopoly/dominance) ya chama kimoja katika bunge, halmashauri na siasa za nchi kwa ujumla. Waziri Mkuu Mizengo aache 'mizengwe' ya kisiasa, awaachie wananchi wawe huru kuwahukumu viongozi kwa maneno na matendo yao sio tu majimboni mwao; bali ndani na nje ya nchi yetu.

Wednesday, February 10, 2010

Bunge Leo-Kiwira+Richmond: Unafiki wa kisiasa ama ndio uzalendo wa kisasa?

Natazama na kusikiliza kinachoendelea bungeni sasa hivi mintaarafu kuwasilishwa kwa Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu Kiwira na Richmond kama zilivyowasilishwa na Dr Mwakyembe na Shellukindo.

Ninaweza kuielezea hali hii kwa kukubaliana na msemo wa wahenga kwamba CCM, serikali yake na Bunge linahodhiwa na chama hicho limeamua kufanya kinachoitwa ‘funika kombe, mwanaharamu apite’. Watoto wa mjini wanaweza kuelezea hali hiyo kuwa ni ‘tumepigwa mchanga wa macho’. Bunge limerejea kule kule kwa kuwa kama mchezo wa kuigiza kwa kuruhusu usanii wa kisiasa wa serikali; kipeo cha juu cha unafiki wa wanadamu.

Kamati umeshatangaza kwamba imeshaliza kazi yake, Bunge nalo litangaze kufunga huo mjadala kwa bunge zima badala yake sasa ufuatiliaji uachwe kwa kamati za kisekta. Kwa hiyo sasa ripoti za utekelezaji zitapelekwa kwenye kamati za kisekta kwa kuwa kamati husika imesharidhika mpaka sasa kwa utekelezaji ambao serikali imefanya mpaka sasa.

Wakati Kamati ikiyasema hayo inasema kuhusu Kiwira kuwa inaendelea kumshauri CAG afanye ukaguzi kuhusu bilioni 17 zilizoingizwa na serikali kwenye kiwira .(Tujiulize, muda gani agizo hili lilitoka? Kwanini mpaka sasa ukaguzi haujafanyika). Kwa maneno mengine, baada ya serikali kuamua kuuchukua upya mgodi, tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka za kina Mkapa, Yona na wenzao sasa sinaelekea kufunikwa kwa nguvu zote.

Usanii mkubwa zaidi unajidhihirisha kwenye sakata zima la Richmond, ambayo mitambo yake dada ya Dowans ipo mpaka sasa hapa jimboni ubungo. Zikitafutwa kila namna za kuingiza mitambo husika kwenye mkondo wa kuhudumia na kulipwa na serikali ya Tanzania.

Kamati inakiri kwamba ni kweli kuna double payment kwenye ulipwaji wa dola milioni tatu kwa kampuni ya Dowans, kamati inasema tu kwamba inaishauri serikali hizo fedha zirudishwe. (Toka kwa kampuni ya Dowans- ambayo kama ilivyo kwa Richmond inaonyesha kwamba ni kampuni hewa, uhalali wa usajili wake una mushkeli mkubwa). Kamati inatamka kwamba watendaji husika mamlaka zao za kinidhamu zimeona hawana hatia. Kamati inasema viongozi wa kisiasa wakina Msabaha, Karamagi nk uchunguzi wa ndani kuhusu ushiriki wao kwa ajili ya kuwajibishwa umeshakamilika, lakini sasa serikali imeanza uchunguzi wa nje wa kimataifa unaendelea. Kamati inatamka kwamba sasa suala hili likikamilika lipelekwa kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Usalama( Sasa sio Bungeni tena). Ajabu sana! Suala hili lilianza mwaka 2007; maazimio ya Bunge ni kujiuzulu kwa Lowassa ilikuwa 2008; mpaka leo uchunguzi unaendelea.

Kituko kikubwa zaidi ni hitimisho la Kamati, kwamba kuhusu kumwajibisha Mkurugenzi wa TAKUKURU Hosea kwa TAKUKURU(Wakati huo TAKURU) kuisafisha Richmond; kwamba kamati haiwezi kulizungumzia tena suala hilo na wala haitarajii bunge ilizungumzie kwa kuwa Hosea naye anawachunguza wa bunge(rejea tuhuma kuhusu posho mbili). Hivyo kamati inasema suala hili sasa inaachiwa mamlaka ya juu zaidi(Soma Rais Kikwete). Ningeweza kuchambua azimio moja baada ya lingine katika ya maazimio 13 ambayo yalibaki kabla ya 23 (Hata yale 10 mengine yalikuwa mchanga wa macho).

Lakini yatosha kusema kwamba suala hili ni ishara kwamba sasa makundi ndani ya CCM (lile linalojiita la wapambanaji dhidi ya ufisadi na lile linaloitwa la mafisadi) yanakaribiana kufunika tofauti zao kwa maslahi ya chama chao na utawala wao tunapoelekea uchaguzi wa mwaka 2010 ama pengine huo ndio uzalendo?. Inaonyesha kamati ya chama (party caucus) imefanya kazi yake kwa kile kinachoitwa ‘kuchukua maamuzi magumu (soma mabovu/bomu). !. Hii inaweza kutoa ishara kuhusu nini kitatokea kwenye ripoti ya Kamati ya Mwinyi na mwelekeo wa chama hicho tawala kwa ujumla. Haya ni madhara ya kuwa na hodhi (dominance/monopoly) ya chama kimoja bungeni.

Hii ni changamoto kwa umma tunapoelekea katika uchaguzi mkuu. Tukumbuke maneno ambayo CHADEMA tuliyasema mwaka 2005; Kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa letu, hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale kwa Ari, nguvu na Kasi mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema(ccm), Tanzania yenye neema haiwezekani. Tuunganishe nguvu ya umma kuchagua viongozi mbadala wenye dira na uadilifu tuweze kujenga taifa lenye uwajibikaji kwa kubadili mfumo wa utawala; mabadiliko ya kweli yanawezekana. Tuwe wakala wa mabadiliko tunayotaka kuyaona; Mwenyezi Mungu atuwezeshe kufika salama.