Friday, May 25, 2012

Shamrashamra za Ushindi wa Kesi ya Mnyika jana

Shangwe!!Mnyika akinyanyuliwa juu baada ya Jaji kumtangaza ni Mbunge halali wa Ubungo tena.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mh. John Mnyika akiwa amebebwa juu juu na wanachama wa CHADEMA  pamoja na washabiki wake nje ya mahakama kuu Kanda ya Dar es salaam jana mara baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili kuhusiana na ushindi wake kwenye Uchanguzi mkuu wa mwaka 2010.

Mnyika akipongezwa na baadhi ya Jamaa waliofika mahakamani hapo.

Wanachama wa CHADEMA pamoja na washabiki mbalimbali wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo  Mh Mnyika wakishangilia Ushindi wa Kesi ya Mbunge wao.

Askari polisi walikuwepo pia kuhakikisha ulinzi wa kutosha katika njia walizopita wapenzi wa CHADEMA kusherehekea ushindi wa Mbunge wa Ubungo.

Mh Mnyika alipokuwa akiwasili mahakamani jana asubuhi.

 Mnyika akisindikizwa kuingia mahakamani jana asubuhi,kushoto ni Diwani wa Sinza, Bw.Renatus Pamba.

 Akisalimiana na Mwenyekiti wa CHADEMA,Mh Freeman Mbowe ndani ya mahakama jana.


PEOPLEEEEEEES!!!!!!!!!

Kutoka Page ya Twitter ya Mnyika:


Ushindi huu ni wetu sote kwani ktk kura elfu60+ ifahamike yangu ni moja tu!Hivyo ushindi huu ni faraja kwa wote walioguswa na ushindi 2010.

Wednesday, May 23, 2012

Kumbukumbu:Mnyika Ushindi Ubungo 2010 Video 5

Kumbukumbu:Mnyika Ushindi Ubungo 2010 Video 4

Kumbukumbu:Mnyika Ushindi Ubungo 2010 Video 3

Kumbukumbu:Mnyika Ushindi Ubungo 2010 Video 2

Kumbukumbu:Mnyika- Ushindi Ubungo 2010 Video 1


Hukumu kesho itakuwa mahakama kuu kivukoni na sio mahakama ya kazi akiba

Nimepokea taarifa kwamba hukumu ya kesi ya uchaguzi dhidi ya ushindi wetu Jimbo la Ubungo kesho tarehe 24 Mei 2012 itatolewa katika Jengo la Mahakama Kuu (Kivukoni- Court No. 1) badala ya jengo ilipo mahakama ya kazi (akiba) ambapo kesi iliendeshwa. Kama tulivyotafuta kura pamoja, tukapanga mstari kupiga kura pamoja na tukakesha kuzilinda pamoja tujumuike pamoja kujua hatma ya kura zetu. Hukumu ya kesi inatarajiwa kuanza kusomwa saa nne asubuhi hata hivyo ni muhimu kuwahi mapema zaidi asubuhi kwa ajili ya itifaki za kuingia mahakamani. Maslahi ya Umma kwanza

Tuesday, May 22, 2012

Ufisadi TANESCO, mikataba mibovu na mpango wa dharura wa umeme-majibu kwa Waziri Mpya wa Nishati na Madini

Toka waziri na manaibu waziri wapya wa wizara ya nishati na madini wateuliwe kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini sikutoa maoni yoyote kwa sababu ya kuwapa muda wa kuingia ofisini na kuanza kazi.


Kwa nyakati mbalimbali Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo toka ateuliwe ameeleza kuwa atakuwa waziri wa matendo kuliko maneno, na kwa kuanzia amezungumza kuhusu sekta ndogo ya umeme na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 20 Mei 2012 na 21 Mei 2012.

Amenukuliwa akitoa ahadi za maneno kuhusu masuala yafuatayo: Kushughulikia orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO; Kusimamia mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ya umeme; Kuagiza watumike wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wa nje; Kuharakisha utekelezaji wa mipango ya umeme.

Nasubiria kuona matendo na nitahoji utekelezaji wa ahadi husika kwenye mkutano wa nane wa bunge unaoanza tarehe 12 Juni 2012 kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli wa nishati na madini na mbunge wa Jimbo la Ubungo yalipo makao makuu ya TANESCO.

Hata hivyo, katika kuchukua hatua za vitendo kuhusu masuala hayo Waziri wa Nishati na Madini na manaibu wake wapitie kumbukumbu za kibunge na mchango wetu kwa nyakati mbalimbali kwa Wizara ya Nishati na Madini kupata hatua za vitendo zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu sekta ndogo ya umeme kwa upana wake; na kwa machache niliyoyanukuu kutoka kwenye vyombo vya habari ni muhimu wakazingatia yafuatayo:

Mosi; kushughulikia orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO

Waziri Muhongo azingatie kuwa hii si mara ya kwanza kwa orodha ya watuhumiwa wa ufisadi ndani ya TANESCO kuwasilishwa Wizara ya Nishati na Madini, katika siku za karibuni agizo lingine la kuwasilisha orodha lilitolewa mwaka 2010 na mwaka 2011 wafanyakazi wa TANESCO wakazungumza tena kwa uchungu kuhusu ufisadi ndani ya shirika hilo la umma na mafisadi wanaohusika. Ni muhimu Waziri akarejea pia katika orodha ya siri iliyowasilishwa mwanzo na iwapo kuna majina ya watuhumiwa wa ufisadi yamejirudia kwa mara nyingine tena achukue hatua za vitendo za kuitoa orodha hadharani na pia kutaka maelezo toka kwa vyombo vya uchunguzi vya kiserikali na mamlaka za nidhamu za watumishi hao kupata maelezo ya hatua ambazo zilichukuliwa toka orodha hizo ziwasilishwe.Waziri Muhongo azingatie pia orodha hiyo haipaswi kuhusu watumishi wa TANESCO pekee kwa kuwa ufisadi ndani ya shirika hilo unatokana na msukumo wa ufisadi toka kwa watuhumiwa wa ufisadi wa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na pia wataalamu kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali. Baadhi ya majina yao yametajwa pia bungeni kwa nyakati mbalimbali hivyo anachopaswa kufanya ni kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ya bunge ya mwaka 2008 juu ya mkataba baina ya TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC na ya mwaka 2011 kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni na kuhusu uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi nchini.

Pili; Kusimamia mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ya umeme

Waziri Muhongo azingatie ahadi za maneno za kufanya mapitio ya mikataba mibovu kwenye sekta ndogo ya umeme zilianza toka mwaka 2008 hivyo anachopaswa kusema ni kueleza hatua za vitendo vilizofikiwa katika kufanya mapitio ya mikataba kwa kurejea rai yangu ya mara kwa mara kuwa toka mijadala miwili muhimu inayogusa sekta ndogo ya umeme kufungwa mwaka 2010 na ni miaka minne toka maazimio yapitishwe na bunge kuhusu masuala husika. Baadhi ya maazimio hayo ni Azimio Na. 3, ambalo liliagiza kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua. Pia, Azimio Na. 13, “Serikali izihusishe Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara ili kuondokana na utaratibu uliopitwa na wakati kwamba Mikataba ya Kibiashara ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe. Aidha, Serikali ihakikishe kuwa, Kamati zote za Bunge zinapitia Mikataba mikubwa ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima”. Azimio hili halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu wake matokeo yake ni kwamba serikali katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2012 kumeendelea kuwa na usiri katika hatua za awali za maandalizi ya mikataba na pia mikataba mingi mikubwa haijafanyiwa mapitio. Kwa utaratibu wa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988 pamoja na kanuni na taratibu za bunge, kamati au mbunge anaweza kuomba kwa serikali kupitia kwa ofisi ya bunge nakala ya mikataba baada ya kusainiwa hali ambayo hailiwezeshi bunge kutimiza kikamilifu wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 ya kuisimamia serikali katika hatua zote muhimu.Tatu; kuagiza watumike wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wa nje

Namuunga mkono Waziri Muhongo katika azma ya kutumia wataalamu wa ndani kabla ya wataalamu wan je, hata hivyo ni muhimu Waziri akarejea kwenye hotuba yetu bungeni ya tarehe 15 Julai 2011 na kuzingatia masuala ya msingi ya kuwezesha utekelezaji wa agizo hili kwa kuweka mifumo muhimu kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, Waziri Muhongo apanue wigo wa dhana hii ya kuwashirikisha wataalamu na makampuni ya ndani sio tu kwenye kutumia wataalamu washauri bali mkazo uwekwe pia kwenye makandarasi na ununuzi unaofanywa na mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwemo TANESCO ili kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ajira nchini. Hata hivyo, katika kutumia watalaamu hao wa ndani pamoja na kupanua wigo wa wazabuni kutoka ndani, Waziri Muhongo awezeshe ukaguzi maalum ili wataalamu na makandarasi waliohusika katika ufisadi dhidi ya TANESCO na mashirika mengine yaliyochini ya Wizara ya Nishati na Madini waondolewe katika orodha (black listing).

Nne; kuharakisha utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.

Waziri Muhongo ameahidi kusimamia kwa kusimamia ongezeko la uzalishaji na usambazaji wa umeme na katika kufanya hivyo pamoja na mipango ya muda mrefu atoe taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme kabla ya mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012.

Waziri Muhongo azingatie kuwa matatizo ya sasa ni matokeo ya udhaifu wa kisera na kiutendaji kuanzia wakati wa Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi na baadaye kwa Rais awamu ya tatu Benjamin Mkapa ambapo TANESCO iliwekwa kwenye orodha ya mashirika ya kubinafsishwa na hivyo serikali kuacha kuwekeza kikamilifu katika uzalishaji wa umeme pamoja na matengenezo ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji. Aidha, ni katika kipindi hicho hicho kuliibuka matatizo pia ya ufisadi kwenye uwekezaji katika sekta ya nishati kama ya IPTL, Kiwira, Net Group Solution nk. Awamu ya nne ya Rais Kikwete nayo ikaongeza zaidi mzigo kwa TANESCO kupitia miradi mingine ya kifisadi kama ya Richmond na sasa kuna tuhuma mpya za ufisadi kuhusu utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme.

Mpango wa Dharura uliwasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011, ahadi ya serikali ilikuwa kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011 na kuweka orodha ya mitambo ya kununua kabla ya oktoba 2012. Pamoja na kuwa na mpango wa gharama kubwa wa dharura ambayo unahusisha kwa sehemu kubwa suluhisho la muda mfupi la kukodi mitambo, bado utekelezaji wa mpango wenyewe nao unasuasua hali inayodhihirisha kuendelea kwa uzembe na udhaifu katika serikali. Hata mitambo iliyofungwa nayo haina uhakika wa kuwa na uwezo wa kuendeshwa wakati wote uliopangwa kutokana na madeni TANESCO ambayo inadaiwa, serikali kushindwa kutekeleza kikamilifu ahadi ilizotoa kwa TANESCO na pia upungufu wa gesi kwa ajili ya kuendeshea mitambo husika na kuwa tishio kwa nchi kuingia gizani katika siku za usoni. Kati ya miradi ambayo utekelezaji wake umesuasua kinyume na ahadi za serikali bungeni ni pamoja na kununua mtambo wa MW 150 wa NSSF na kununua mitambo ya MW 100 wa TANESCO Ubungo.

Kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na takribani MW 660 unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Waziri Muhongo arejee tahadhari niliyotoa bungeni kuhusu gharama kubwa za mpango wa dharura wa umeme na kupendekeza vyanzo mbadala vya fedha ambavyo serikali ilivipuuza. Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Julai 2011 nilieleza bungeni vyanzo mbadala vya kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bila kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme. Hata hivyo, tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Siku hiyo nilirudia kumsomea Waziri Mkuu kumbukumbu ya Bunge (Hansard) ya ahadi yake ya tarehe 18 Julai 2011 ambayo haikuitimiza, inaelekea serikali ilitoa ahadi hewa ndio maana haikutaka kabisa kubadili msimamo.

Waziri Muhongo aonyeshe kwa vitendo kwamba utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini umebadilika kwa kurejea masuala muhimu na kuyazingatia kwenye makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013; kauli yangu kuhusu masuala mengine ya gesi asili, mafuta na madini nitayaeleza katika hatua za baadaye.

Imetolewa tarehe 21 Mei 2012

Hatua saba za haraka zinazopaswa kuchukuliwa na Waziri Mpya wa Maji

Toka mabadiliko ya Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya maji yafanyike sikutoa maoni yoyote nikisubiri wateule hao kuanza majukumu yao na kutoa kauli zao kwa umma kuhusu namna walivyojipanga katika kushughulikia matatizo ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam ambalo miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.


Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Nilitarajia Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe aanze kazi kwa nguvu ili kurejesha imani juu ya utendaji wake uliochafuka kutokana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika aliyoiongoza awali kugubikwa na tuhuma mbalimbali kwa mujibu wa taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na madai mengi yaliyotolewa bungeni hususani katika mkutano wanne mwaka 2011 na mkutano wa saba mwaka 2012.

Badala yake amerudia ahadi zile zile kama zilizotolewa na Waziri aliyemtangulia Prof. Mark Mwandosya kwa nyakati na maeneo mbalimbali kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 kuhusiana na hatua za utatuzi wa matatizo ya maji safi na maji taka katika Jiji la Dar es salaam ambazo utekelezaji wake unasuasua zaidi ya mwaka mmoja toka zitolewe.

Aidha, siku chache baada kuapishwa Naibu Waziri wa Maji Dk. Binilith Mahenge alifanya ziara ya kutembelea vyanzo vya uzalishaji wa maji na kutoa kauli kuhusu utekelezaji wa miradi, lakini wiki moja baadaye Waziri wa Maji naye akafanya ziara katika vyanzo vile vile na kurudia kauli zenye mwelekeo ule ule ambayo ni matumizi mabaya ya muda na rasilimali nyingine za umma zilizotumika katika ziara hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Hivyo, baada ya kurejea ofisini kutoka katika ziara hiyo ya vyanzo vya ruvu juu na ruvu chini na kufanya mikutano na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) natoa mwito kwa Waziri Maghembe kuueleza umma hatua saba za haraka zaidi za Wizara ya Maji kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.

Katika ya hatua hizo ambazo Waziri Maghembe anapaswa kuzisimamia katika Wizara ya Maji ni; Mosi, kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.

Pili; kuwasilisha bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.

Tatu; Waziri Maghembe aeleze hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara yake kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.

Nne; Waziri Maghembe akubaliane na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.

Tano; Waziri Maghembe ahakikishe Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Wizara ya Maji ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.

Sita; Waziri Maghembe awezeshe Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kabla ya mkutano wa nane wa bunge ulipangwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa mchakato wa bajeti.

Saba; Wizara ya Maji ihakikishe Serikali inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.

Imetolewa tarehe 20 Mei 2012

Saturday, May 19, 2012

Kwenda mahakamani 24 Mei na "Get Together" baada ya Hukumu

Nashukuru wote mliojumuika katika mkutano wa leo wa kata na matawi jimboni Ubungo, nimefarijika na azimio lenu la kuja kwa wingi mahakamani tarehe 24 Mei kusikiliza hukumu dhidi ya kura zenu.

Nimevutiwa pia na azimio la kuwa na ‘get together bottle party’ siku hiyo hiyo baada ya hukumu ‘kwa utawala binafsi’.

Kwa swala na sala mlizoswali na kusali leo kwa pamoja, naamini Mwenyezi Mungu atawezesha kutolewa hukumu ya haki.

Sunday, May 13, 2012

Buriani mwanahabari na mwanamichezo Rachel Mwiligwa

Marehemu Rachel Mwiligwa hakuwa tu mwandishi na mhariri wa habari za michezo na burudani bali alishiriki michezo na buradani kwa vitendo. Mara ya mwisho kukutana naye ni wakati wa bonanza TP Sinza yeye akiwa mratibu; nitashiriki katika maziko yake. Naungana na familia na tasnia nzima ya habari katika kipindi hiki cha majonzi; Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema

Saturday, May 12, 2012

Waziri Kigoda anusuru viwanda walivyovibinafsisha kwa kuanza na cha Nguo Urafiki

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdalah Kigoda anapaswa kuweka kipaumbele katika kunusuru viwanda vilivyo katika hali mbaya kutokana na matatizo yaliyotokana na ubinafsishaji pamoja na ufisadi katika mchakato wa uwekezaji ili kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi na kuongeza ajira nchini.
Waziri Kigoda atumie nafasi hiyo kurekebisha kasoro ambazo serikali za awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa ambayo yeye alikuwa mmoja wa mawaziri akiwa ofisi ya rais mipango na ubinafsishaji ilizisababisha.Waziri Kigoda amehusika katika ubinafsishaji wa viwanda, kuratibu urekebishaji wa mashirika ya umma na kusimamia kisera utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa; kuteuliwa uwaziri wa viwanda na biashara kuwe ni fursa kwake ya kurekebisha makosa ya awali.Nimemkaribisha kutembelea Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kabla ya mkutano wa bunge la bajeti unaotarajiwa kuanza tarehe 12 Juni 2012 ili kushughulikia udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro katika mchakato wa ubinafsishaji.Waziri wa Viwanda na Biashara azingatie kuwa matatizo ya kiwanda cha urafiki ni zaidi ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi pamoja na ufisadi uliokithiri unaohitaji uchunguzi maalum.Aidha mchakato wa kutafuta mwekezaji mpya unaoendelea hivi sasa unaohusu kampuni ya China iliyokuwa ikimiliki hisa asilimia umegubikwa na utata na wakati huo huo kuna mchakato mwingine wa kinyemela wa kutaka kuuza hisa asilimia 49 zinazomilikiwa na Serikali kwa niaba ya Watanzania.Kama inavyofahamika, moja ya viwanda vikubwa vya nguo hapa nchini vilivyojengwa wakati wa Awamu ya Kwanza ya Utawala wa nchi yetu chini ya Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiwanda cha Nguo cha Urafiki ambacho kilijengwa miaka michache baada ya uhuru kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka nchi ya China. Baadaye kiwanda kilibinafsishwa kiholela na sasa kinaendeshwa kwa ubia kuanzia mwaka 1997 ambapo serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 49 ya hisa huku asilimia 51 zikiwa chini ya kampuni ya nchini China.Pamoja na kuwa mwenye hisa nyingi ndiye anawajibika zaidi katika uendeshaji wa kiwanda kiuendeshaji na maslahi ya wafanyakazi, serikali kwa kuwa na hisa 49% kwa niaba ya watanzania ina wajibu wa pekee wa kufuatilia kwa karibu hali ya kiwanda kama sehemu ya kulinda viwanda vya ndani, kudhibiti hasara kwa serikali na kuzuia upotevu wa mali za umma. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka kumi wajibu huu umekuwa hautekelezwi ipasavyo hali ambayo imedidimiza kiwanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri uzalishaji pamoja na kupunguza ajira.Baada ya kubaini hali hiyo tarehe 4 Februari 2011 nilitembelea Kiwanda cha Nguo cha Urafiki Ubungo na kufanya mazungumzo na wafanyakazi pamoja na wawakilishi wa menejimenti. Kutokana na mkutano huo na vyanzo vingine nilipata maelezo ya kina kuhusu hali mbaya ya kiwanda ikiwemo kusimama kwa uzalishaji wa nguo na maslahi duni ya wafanyakazi.Kufuatia taarifa hizo nilichukua hatua ya kuziandikia mamlaka husika kuweza kuchukua hatua za haraka kunusuru hali ya kiwanda. Kutokana na mamlaka husika kuchelewa kuchukua hatua nilikwenda mbele zaidi kwa kutumia mamlaka ya kibunge kuhoji mawaziri husika wakati wa mkutano wa nne wa Bunge wakati wa kujadiliwa kwa bajeti za wizara mbalimbali mwaka 2011.Baadhi ya Wizara nilizozitaka kuchukua hatua ni pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha hususani ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali ya Mashirika ya Umma (CHC), Wizara ya Kazi na Ajira na mamlaka zingine. Hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa zimekuwa za kususua na hazionyeshi kama serikali inayachukulia matatizo ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa uzito unaostahili.Pamoja na kuitaka serikali kuchukua hatua pia nilitoa mwito kwa kamati husika za bunge kuchukua hatua ambapo kamati ya Viwanda na Biashara iliitikia mwito huo na Novemba 2011 ilitembelea kiwanda na kushuhudia ukweli wa madai ambayo tumekuwa tukiyatoa kuhusu hali mbaya ya kiwanda. Kamati hiyo ilitoa kauli ya kutaka uchunguzi wa ziada ufanyike hatua ambayo haijatekelezwa mpaka hivi sasa.Izingatiwe kuwa kabla ya Kuingia ubia, Serikali ilifanya ukarabati mkubwa wa mitambo kwa gharama za walipa kodi watanzania. Aidha, mara baada ya ubia serikali ya Tanzania iliingia mkataba mwingine na Serikali ya China wa mkopo wa dola milioni 27 (zaidi ya bilioni 30) kwa ajili ununuzi wa mitambo mipya badala yake kwa sehemu kubwa fedha hizo zikatumika kununua mitambo chakavu.Matokeo yake uzalishaji ukaanza kupungua na wafanyakazi wakaanza kupunguzwa na hivyo kusababisha kushuka kwa mapato ya serikali na kuongezeka kwa matatizo ya ajira. Pia, kutokana na matatizo hayo baadhi ya mitambo imeondolewa na kuuzwa kinyemela kama vyuma chakavu hali ambayo imesababisha wafanyakazi kupewa likizo wengi bila malipo na wengine kwa malipo pungufu kwa visingizio mbalimbali. Kutokana na hali hiyo nilizitaka Wizara na Mamlaka husika kuchunguza madai hayo na kuongeza ukaribu wa serikali katika uendeshaji wa kiwanda husika.Kwa upande mwingine maslahi ya wafanyakazi nayo yamezidi kuwa duni badala kuboreshwa baada ya ubia kuingiwa na hivyo kushusha motisha ya ufanyaji wa kazi. Pia wafanyakazi hawalipwi mishahara kwa viwango vipya vilivyotangazwa na serikali katika hatua za awali. Hali hizi zimesababisha migogoro mbalimbali kati ya kampuni na serikali kwa upande mmoja na wafanyakazi walioko kazini na walioachishwa kwa upande mwingine na hivyo kuongeza mizigo ya madeni kupitia hukumu za mahakama, mamlaka zingine na madai lukuki. Kufuatia hali hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi, nilitoa mwito kwa Wizara na Mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kumaliza matatizo ya wafanyakazi katika Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ili kuelekeza nguvu katika uzalishaji.Katika mikutano ya tatu na nne ya Bunge kwa nyakati na njia mbalimbali nilizieleza pia Wizara na mamlaka mbalimbali za serikali kuwa hali mbaya ya kiwanda inahusisha pia kukosekana kwa udhibiti katika mali za kampuni na pia kiwanda kuanza kufanya shughuli ambazo ziko nje ya kazi ya msingi ya ubia wa uzalishaji wa nguo. Niliitaka serikali kuchunguza na kuchukua hatua juu ya shughuli zinazoendelea kufanywa na Kiwanda cha Nguo cha Urafiki nje ya mikataba na misingi ya ubia mathalani: upangishaji wa Nyumba za wafanyakazi, upangishaji wa maeneo ya wazi, upangishaji wa maghala ya kiwanda, uuzaji wa nyumba za wafanyakazi, mfano mzuri ni nyumba 50 za THB eneo la Manzese, na ukodishaji wa maeneo kwa ajili ya kufanya biashara ya mafuta. Hali hii imeambatana na uingizaji wa bidhaa za nje kwa mgongo wa kampuni ya Urafiki na zingine tanzu kinyume na ubia wenye msingi wa kulinda na kuendeleza viwanda vya ndani hali ambayo imeleta athari katika uchumi wa taifa na kupunguza ajira za uzalishaji.Kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwa Serikali kuingilia kati kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki. Aidha, kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki kama ili kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda vingine. Hata hivyo, mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na Wizara na Mamlaka husika hali ambayo imefanya niendelee kutaka uwajibikaji wa serikali hata baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri.John Mnyika (Mb)

11/05/2012

Monday, May 7, 2012

"Toa Kitabu Kisomwe"-mimi nimeanza, wewe je?

Jana jumapili tarehe 6 Mei 2012 nimekabidhi zaidi ya vitabu mia saba (700) kama ishara ya kuanzisha Programu ya Taarifa iitwayo “Toa Kitabu Kisomwe”, hii ni miezi mitatu baada ya kusambaza kwa wananchi wa jimbo la Ubungo vitabu 4500 ikiwa ni pamoja na nakala za katiba ya nchi na vitabu kuhusu mchakato wa katiba mpya; na kufanya jumla ya vitabu ambavyo nimesambaza mpaka sasa kuwa zaidi ya elfu tano (5,000).


Lengo ya Programu ya Taarifa ya “Toa Kitabu Kisomwe” ni kusambaza jumla ya vitabu visivyopungua elfu hamsini (50,000) ndani ya Manispaa ya Kinondoni katika kipindi cha mwaka ili kuchochea uhuru wa kifikra na kuchangia katika ustawi wa wananchi.

Kwa mtazamo wangu akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Hivyo kushirikiana kuwezesha elimu bora na uhuru wa kifikra ni msingi muhimu wa kuchochea maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Elimu bora sio majengo pekee bali ni pamoja na walimu bora na mazingira bora ya kusomea na kujifunzia yenye vifaa vya kujifunzia na vitabu vya kiada na ziada.

Hivyo, harakati za kusimamia uwajibikaji wa serikali kuu, serikali za mitaa na mamlaka nyingine zinazohusika na sekta ya elimu hususani kwenye shule, vyuo na vyuo vikuu vya umma zinapaswa kuendelezwa.

Tuendelee kuhakikisha rasilimali zinazotengwa ikiwemo ruzuku ya elimu ya msingi na sekondari na mikopo ya elimu ya juu zinakuwa za kutosha, zinatolewa kwa wakati na zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kudhibiti mianya ya ufisadi.

Wakati, tukisimamia uwajibikaji huo wa serikali tutambue masuala matatu muhimu; mosi, jukumu la kuboresha mazingira ya elimu kwenye elimu rasmi ya darasani sio wa serikali pekee bali ni wajibu wa wote katika jamii.

Pili, izingatiwe kuwa sehemu kubwa ya wananchi hawajapata elimu rasmi hivyo ni muhimu kuwa na mifumo ya elimu kwa njia nyingine mitaani na vijijini ili kuchochea zaidi maendeleo.

Tatu, hata kwa wenye elimu rasmi inafahamika kuwa elimu haina mwisho hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujisomea ili kuendeleza uhuru wa kifikra.

Katika muktadha wa masuala hayo matatu, niliungana na Asasi ya Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative-UDI) kuzindua Programu ya Taarifa inayohusisha kukusanya vitabu vya kiada na vya ziada kutoka wa watu mbalimbali na taasisi mbalimbali na kuvisambaza katika taasisi za elimu kwa ajili ya wanafunzi kusoma na maeneo maalumu kwa ajili ya wananchi kujisomea.

Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kwamba ukimpa mtu samaki umemlisha kwa siku moja lakini ukimfundisha kuvua umemlisha kwa maisha yake yote. Nikisisitiza mantiki ya msemo huo naweza kusema pia kwamba ukimpa mtu chakula cha kawaida umemshibisha kwa muda mfupi lakini ukimpa chakula cha kifikra umemuwezesha kwa muda mrefu; huu ndio msingi utakaoongoza Programu ya Taarifa; “Toa kitabu kisomwe”.

Kupitia programu hii tunaomba taasisi au mwananchi yoyote mwenye kitabu chochote popote ambaye yuko tayari kukitoa ili kisomwe iwe ni cha kiada au cha ziada awasiliane UDI ili iweze kufikisha kitabu hicho kwa walengwa.

Ukipenda unaweza kuweka saini kwenye kitabu hicho kama kumbukumbu kuwa taasisi yenu au wewe ndiye uliye “Toa kitabu Kisomwe” au unaweza pia kutueleza kitabu hicho unapendekezwa kipelekwe wapi ndani ya Manispaa ya Kinondoni ili kiweze kusomwa kwa ufanisi.

Sisi mpango wetu ni kusambaza vitabu hivyo kwenye maktaba za shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa upande wa elimu ya kiada na kusambaza kwenye maktaba za jumuia, ofisi za serikali za mtaa, taasisi za kijamii na vijiwe vya kudumu kwa upande wa elimu ya ziada.

Naamini kwamba kwenye kaya mbalimbali za Manispaa ya Kinondoni vipo vitabu makabatini au masandukuni ambavyo ama ni vya kiada vilivyoachwa baada ya walengwa wa awali kupanda ngazi moja ya elimu kutoka ile ambayo walikuwa wakisoma au ni vya ziada ambavyo tayari wahusika walishavitumia na vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa walengwa wengine wenye kuvihitaji hivyo; “Toa Kitabu Kisomwe”.

Aidha, naamini pia kwamba Jiji la Dar es salaam lina makao makuu ya taasisi mbalimbali ambazo hutoa vitabu mbalimbali kwa ajili ya kusambaza nchini lakini wakati mwingine hushindwa kuwafikia walengwa katika ngazi ya chini jijini hivyo UDI kwa kuwa taasisi ya ngazi ya chini inaweza kuwa kiungo kizuri cha kuwezesha vitabu husika kuwafikia walengwa; “Toa Kitabu Kisomwe”.

“Toa kitabu kisomwe” kupitia ofisi ya UDI iliyopo Kimara Kona au wasiliana na UDI kupitia Afisa Taarifa (0768503331 au 0715745874) au barua pepe ubungo2005@yahoo.com kutoa kitabu husika.

Nilitumia pia fursa hiyo kuitaka serikali kutoa kauli kuhusu hatua iliyofikiwa katika kusambaza vitabu na vifaa vingine vilivyonunuliwa kutokana fedha iliyorejeshwa baada ya ufisadi wa Rada kubainika.

Pia, nilitoa pia mwito kwa wananchi katika mchakato wa maoni ya katiba mpya kuhakikisha haki za elimu na taarifa zinatolewa kikamilifu na kulindwa kikatiba tofauti na katika katiba mbovu ya sasa ambayo imetaja haki hizo na kuziwekewa mazingira ya kupokonywa na serikali kujitoa katika wajibu wa kisheria wa kuhakikisha zinapatikana. Wakati mabadiliko hayo yakisubiriwa serikali iharakishe kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya uhuru wa taarifa ambayo ni nyenzo muhimu ya kupambana na ufisadi na kuchochea maendeleo nchini.

Hatua tulizochukua kurejesha maji Golani ya Msewe; Goba bado kuna vikwazo

Jana tarehe 6 Mei 2012 tulifanya mkutano na wananchi wa mtaa wa Msewe kata ya Ubungo kuhusu mradi wa maji katika eneo la Golani taarifa ilitolewa kuhusu hatua ambazo tumechukua mpaka na kuwezesha maji kurejeshwa katika eneo la Golani, ambapo mpaka kufikia juzi tarehe 5 Mei 2012 tayari Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) ilikuwa imesukuma maji kwa ajili ya wananchi wa eneo husika kuanza kupata maji.


Pia katika mkutano huo taarifa ya ukaguzi maalum wa mradi wa maji wa Golani kwa kipindi cha Novemba 2007 mpaka Machi 2012 ilitolewa kwa wananchi ambayo ilieleza kasoro zilizopo kwenye mradi ambazo zimekwamisha wananchi kupata maji kwa muda mrefu ikiwemo kutofuatwa kwa muongozo wa muundo wa kamati za maji ili wananchi waweze kuchukua hatua zaidi.

Aidha taarifa hiyo pamoja na mambo mengine ilieleza kwa kina kuhusu kuwepo kwa ‘matumizi hewa’ ya zaidi ya milioni 63, mapato ya zaidi ya milioni 89 kukusanywa kwa kutumia nyaraka zisizo sahihi na kulimbikizwa kwa deni la maji hali ambayo ilifanya Kampuni ya Maji-Safi na Maji-Taka (DAWASCO) kuwakatia maji wananchi wa eneo la Golani. Kufuatia taarifa hii maamuzi mbalimbali yalifikiwa na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa.

Katika kipindi cha kati ya mwaka 2007 mpaka 2011 kwa nyakati mbalimbali eneo la Msewe-Golani limekuwa na matatizo ya maji kutokana na malalamiko ya wananchi nilifanya ufuatiliaji na kubaini kwamba chanzo cha matatizo hayo ni udhaifu katika uendeshaji wa mradi wa maji katika eneo husika.

Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Kata ya Ubungo pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na ambapo pamoja na mambo mengine ilikubaliwa hatua za haraka zichukuliwe kuwezesha wananchi wa eneo husika kupata maji.

Kufuatia mazungumzo hayo Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob, Diwani wa Viti Maalum Jimbo la Ubungo Joyce Muya na watendaji wengine wa kata na mitaa walifanya mkutano na wananchi wa eneo husika tarehe 26 Februari 2012 ambapo ilisomwa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa maji wa Golani kwa kipindi cha Oktoba 2007 mpaka Machi 2012, taarifa ambayo ilikataliwa na wananchi na kutaka ufanyike ukaguzi maalum wa mapato na matumizi ya mradi huo.

Matatizo ya maji katika Jimbo la Ubungo na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam yamedumu kwa muda miaka mingi kutokana na udhaifu wa usimamizi katika vyombo vinavyohusika na utoaji wa huduma husika. Pamoja na changamoto zilizopo katika maeneo yanayohudumiwa moja kwa moja na mabomba ya DAWASCO na DAWASA yapo pia matatizo katika miradi inayoendeshwa na vyama vya watumiaji maji pamoja na kamati za wananchi ambazo zinapaswa kusimamiwa na Manispaa.

Matatizo kama ya mradi wa Golani yamejitokeza pia katika mradi wa maji Goba kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 hali ambayo ilihitaji kuunganisha wananchi kuweza kuchukua hatua. Kwa upande wa mradi wa maji Goba hatimaye DAWASCO ilikubali kurejesha maji kwa wananchi baada ya hatua ambazo tulichukua zilizowezesha Manispaa ya Kinondoni kuingilia kati. Mpaka sasa taratibu zinazoendelea kwenye mradi wa maji Goba ni uwekaji wa mfumo mbadala wa mabomba ya maji pamoja na mita ili kuepusha wizi wa maji na malimbikizo ya madeni kama ilivyokuwa katika siku za nyuma.

Hata hivyo, kasi ya urejeshaji wa maji imekuwa ndogo kutokana na udhaifu wa kiutendaji wa idara ya maji ya manispaa ya Kinondoni suala ambalo mamlaka husika zimetoa maagizo ya hatua za kuchukuliwa ili kuwezesha maji kurejea kwa haraka. Kwa upande mwingine, tofauti na mradi wa maji Goba hakuna kasoro za miundombinu zilizobainika mpaka sasa kwa upande wa mradi wa maji wa Golani na hivyo kufanya huduma ya maji kurejea mapema zaidi. Natoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mamlaka zote za kiserikali zinasimamiwa ipasavyo kuongeza ufanisi katika miradi ya maji.

Friday, May 4, 2012

Fidia ya barabara ya Ubungo Kibangu mpaka Makuburi Makoka imeanza kulipwa; nitaendelea kuisimamia serikali kwa hatua zaidi

Fidia kwa wananchi wa wa Kibangu kuwezesha mchakato wa ujenzi wa njia mbadala kwa wakazi wa Mitaa ya Ubungo – Kibangu na mwongozo katika Kata ya Makuburi inaendelea kulipwa kufuatia barabara iliyokuwa ikitumika kuzolewa na maji kutokana na kuwa pembeni ya mto Gide.Mpaka leo tarehe 3 Mei 2012 jumla ya shilingi 122,543, 264 zimelipwa kwa nyumba chache zilizobaki na yamesalia malipo ya milioni 64 tu ili notisi kwa wakazi waliosalia iweze kutolewa na hatimaye barabara iweze kufunguliwa hatua za matengenezo ziweze kufuata.


Hivyo, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Manispaa ya Kinondoni kuharakisha malipo ili kuepusha gharama za fidia kuongezeka kwa kuzingitia kuwa iwapo malipo yangefanyika kwa wakati mwaka 2010 gharama za fidia zingekuwa milioni 80 tu lakini sasa zimeongezeka mpaka kufikia zaidi ya milioni 180.


Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Makuburi pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na hatimaye nikafanikisha wananchi hao kukutana na watendaji wa Manispaa na fedha zao za fidia kutengwa.

Hata hivyo, kabla ya kukabidhiwa fedha hizo baadhi yao walikataa kiwango ambacho walikuwa wamekubaliana awali kwa maelezo kwamba thamani za nyumba zao zimepanda baada ya serikali kuchelewa kuwalipa kwa miaka mingi, hawajaridhika na kiwango cha riba kilichowapa nyongeza kwa miaka husika kwa kutozingatia bei ya soko.

Niliendelea kufuatilia suala husika kupitia mikutano ya baraza la madiwani tarehe 25 Februari na 28 Februari 2012 na Manispaa iliahidi kufanya majadiliano nao tena kuweza kutoa nyongeza na kufanya malipo mwezi Machi 2012.


Ikumbukwe kwamba Tarehe 7 Februari 2011 nilimuandikia barua Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Mkuchika kumkumbusha kwamba katika Kikao cha kumi na nne cha Mkutano wa Ishirini wa Bunge la Tisa mnamo tarehe 23 Juni 2010 Waziri wa TAMISEMI wa wakati huo aliahidi bungeni kwa niaba ya serikali kukamilisha mchakato wa ujenzi wa njia mbadala kwa wakazi wa Mitaa ya Ubungo – Kibangu na mwongozo katika Kata ya Makuburi , kufuatia njia iliyokuwa ikitumika kuzolewa na maji kutokana na kuwa pembeni ya mto Gide.


Nilitaka ahadi hiyo itekelezwe kwa haraka kutokana na adha ambao wananchi wa eneo husika wanaipata hivi sasa na pia kutokana na ukweli kuwa kuanzia mwaka 2005 kwa nyakati tofauti serikali ngazi mbalimbali imekuwa ikiahidi kujenga njia mbadala kwa ajili ya eneo husika.


Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilishafanya tathmini ya gharama za ukarabati huo ambao utahusisha kazi za ujenga kingo za mto kwa kutumia Gabions kujaza kifusi na kushindilia. Kwa ujumlawake gharama hizo zilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi 836,458,000/=.


Aidha mpaka kufikia Juni 2010 malipo ya nyumba nne yalishafanywa ambayo yaligharimu shilingi 16,240,262/= ambapo wananchi (2) walilipwa fidia zao. Kilichokuwa kimebaki ni kukamilisha utaratibu wa malipo ya nyingine zilizobaki kwa wakazi waliobaki ambazo kwa mujibu wa tathmini ya wakati huo ilikuwa shilingi 80,195,307/=.

Hukumu ya kesi yetu tarehe 24 Mei; tumuombee Jaji

Tumemaliza majumuisho ya kesi dhidi yetu. Hukumu imepangwa kutolewa tarehe 24 Mei 2012. Mawakili wote wawili wa upande wa utetezi wametimiza wajibu wao.


Pamoja na kuwa mawakili kwa ujumla walizungumza kwa zaidi ya saa saba, namnukuu kiduchu Wakili wetu Mbogoro: “Mshindi wa uchaguzi anatokana na maamuzi ya watu wengi, haki ambayo huipata kwa nadra kila baada ya miaka mitano na ni mchakato unaotumia fedha nyingi za walipa kodi. Hivyo kiwango cha uthibitisho wa madai yoyote lazima kiwe bila ya shaka yoyote………mlalamikaji Hawa Ng’umbi amesema mwenyewe mahakamani kuwa hana tatizo na matokeo ya toka vituoni, malalamiko yake sio juu ya nani mshindi. Kwa kawaida kesi za uchaguzi hufunguliwa na wenye kupinga ushindi wanaodai kuwa wangeshinda wao iwapo sheria zisingekiukwa; kama hapingi matokeo ya vituoni ambayo majumuisho yake ndio yamempa Mnyika ushindi; tunaweza kujiuliza tuko hapa kwa ajili gani?”

Tuungane pamoja katika sala na swala kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Jaji Upendo Msuya afanye maamuzi ya haki.

Tuesday, May 1, 2012

Daraja Golani-Suca na Barabara Mburahati-Mabibo

Mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa daraja la Golani-Suka anapaswa kuanza mapema ujenzi wa daraja hilo muhimu linalounganisha kata za Kimara na Saranga ili kupunguza kero kwa wananchi hasa wakati wa mvua.


Mwezi huu wa Aprili nimefuatilia kuhusu hatma ya daraja hilo na hatimaye mkataba wa ujenzi wa daraja husika umesainiwa kati ya Manispaa ya Kinondoni na Mkandarasi Kika Co. Ltd kwa gharama za shilingi milioni 447.

Hata hivyo, ujenzi wa daraja husika haujaanza suala ambalo linahitaji Manispaa ya Kinondoni kumsimamia kwa karibu mkandarasi husika ili ujenzi uanze kwa haraka kwa kuwa mchakato wa zabuni ulianza kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2012.

Izingatiwe kwamba kutokuwepo kwa daraja katika eneo hilo mwaka miaka mingi kumefanya mawasiliano katikati maeneo hayo kuwa magumu nyakati za mvua na kusababisha madhara ya kibinadamu na mali wananchi wanapovuka mto katika eneo hilo wakati wa mafuriko.

Baada ya kuwawakilisha wananchi kutaka ujenzi wa daraja hilo lilingizwa kwenye bajeti ya Manispaa ya Kinondoni kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hata hivyo miezi ikiwa imebaki takribani miwili kabla ya mwisho wa bajeti husika ujenzi wa daraja hilo ulikuwa haujaanza bado.

Hatua kama hiyo inahitajika pia kwa barabara ya Mburahati mpaka Mabibo NIT ambayo inapaswa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa imetengewa kiasi cha shilingi milioni 504 kwa ajili ya kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro .

Tathmini ya utekelezaji wa bajeti inaonyesha kwamba kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni ndogo pengo ambalo linapaswa kuzibwa kwa kusimamia kwa karibu miradi inayopaswa kuanza katika muhula uliobaki wa mwaka wa fedha 2011/2012.

WAFANYAKAZI, UWAJIBIKAJI na KESI za UCHAGUZI

Mei Mosi, niko ofisini tukiendelea na kazi lakini nimeona niandike machache kutokana na maswali ambayo nimeanza kuulizwa juu ya maoni yangu kutokana na hotuba ya Rais na juu ya masuala ya kesi za uchaguzi. Mengine zaidi tutaelezana baada ya kazi jimboni;


WAFANYAKAZI: Nawatakia heri katika siku ya wafanyakazi; risala iliyosomwa kwa JK sehemu kubwa ni mambo yaleyale ambayo Rais amekuwa akielezwa na wafanyakazi miaka kadhaa mfululizo , aeleze amefikia wapi kwa takwimu katika nyongeza ya mishahara, punguzo la kodi nk. Mei Mosi ya 2011 alitoa maneno matupu kwa wafanyakazi kuwa wasubiri bajeti, nikasema ilikuwa ahadi hewa na kweli ikiwa ni usanii hata bungeni. Sasa amerudia tena kauli zile zile. Kuhusu mfumuko wa bei, maneno ya Rais yamedhihirisha kwamba tatizo letu kubwa zaidi si la kiuchumi bali ni udhaifu wa uongozi, ufisadi na kutetereka kwa misingi ya utawala wa sheria katika sekta muhimu za nishati na kilimo. Sijaridhika pia na maelezo aliyotoa kuhusu namna serikali inavyoshughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana. Ni vizuri tu Rais akarejea ushauri na mapendekezo yetu kuhusu masuala yote matatu ya wafanyakazi, mfumuko wa bei na ajira kwa vijana tuliyotoa ndani na nje ya bunge kwa nyakati mbalimbali na kuisimamia vizuri serikali kuhakikisha yanatekelezwa.

UWAJIBIKAJI: Kuhusu uwajibikaji kutokana na taarifa za CAG na mijadala ya bungeni, historia aliyoieleza Rais Kikwete ya toka 2007 imedhihirisha nilichokisema siku chache zilizopita kuwa hatuna serikali na mamlaka ya Rais hayatumiki vizuri kwa maslahi ya umma, inaonyesha taarifa zote Rais; hata hizi zilizojadiliwa mwaka 2012 Rais alikuwa nazo toka 2009/2010, angetumia vizuri madaraka yake kwa mujibu wa katiba vyombo vya dola na mamlaka zingine zingeshachukua hatua. Lakini ameendelea kusema tu serikali imepokea mapendekezo kutoka bungeni na inayafanyia kazi huku uzembe na ufisadi ukiendelea kutamalaki katika utumishi wa umma toka Orodha ya Mafisadi (List of Shame) itolewe mpaka sasa. Tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kusimamia uwajibikaji mpaka kieleweke.

KESI ZA UCHAGUZI: Nashukuru Mbassa ameshinda Biharamulo, Sumbawanga Mjini tumepata jimbo wazi la kwenda kulikomboa; Ubungo tutakwenda mahakamani kesho kwa ajili ya kupatiwa mwenendo wa kesi (court proceedings) kwa ajili ya kufanya uwasilishaji wa mwisho (final submission) kabla ya hukumu kutolewa. Maslahi ya UMMA kwanza