Tuesday, March 17, 2009

Ardhi na Maendeleo ya mgeni njoo mwenyeji akonde!

Ardhi na Maendeleo ya mgeni njoo mwenyeji akonde!

Na John Mnyika

Wahenga walisema, mgeni njoo mwenyeji apone. Msemo huu, ni ishara ya baraka njema inayoletwa na wageni chini ya ukarimu wa kiafrika. Hata hivyo, yapo maeneo ambayo ujio wa wageni ama wa mambo mageni umezua hasara kwa upande wa wenyeji. Tunayaona hayo katika maeneo ya uwekezaji ambayo wenyeji wameondolewa kwa shuruti kupisha wageni bila kupata manufaa ya kutosha kutokana na ujio wa wageni hao. Hayo yamejitokeza katika sekta za uchimbaji madini, uwindaji na maeneo mengine yanayohusiana na rasilimali za taifa. Hapo ndio unapoweza kuzuka msemo mpya wa mgeni njoo mwenyeji akonde. Si dhamira ya makala yangu ya leo kuzungumzia hayo ya wageni katika maeneo ya rasilimali wengi wao wakiwa kutoka nje, leo nataka nizungumze kuhusu wageni wa ndani katika sekta ya ardhi.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Ardhi ni msingi wa maendeleo. Hata hivyo, pamoja na kutambua hayo, mpaka sasa sera za serikali inayoongozwa na CCM zimejikita katika kuweka ardhi mikononi mwa serikali badala ya umma. Watanzania wanaoamini kwamba wanamiliki ardhi ni wapangaji tu katika ardhi husika kwa miaka ambayo imetajwa ndani ya hati za umiliki. Unahitajiika msukumo mbadala wa kubadili sera ili kuwe na mfumo wa kuwezesha raia kumiliki ardhi kikamilifu. Hii nayo, si hoja kuu ya makala yangu ya leo.

Chini ya mfumo huu huu tulionao sasa, wako watanzania ambao ni wamiliki wapangaji katika ardhi na kipindi chao cha kumiliki ardhi hiyo bado hakijamalizika lakini serikali inaitaka ardhi yao kwa sababu moja au nyingine.

Hawa wako maeneo mbalimbali ya nchi. Katika mkoa wa Dar es salaam pekee mijadala ya masuala kama haya imetapakaa katika maeneo ya Kigamboni, Tabata, Kurasini, Kibamba na kadhalika. Katika maeneo yote haya wananchi wanapaswa kuhamishwa kupisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Leo najadili eneo la Kwembe kwa kuzingatia msemo wa ‘mgeni njoo mwenyeji akonde’. Ama kwa hakika hakuna anayepinga maendeleo. Maendeleo yanavyopiga hodi kokote ni faida kwa wenyeji kama ambavyo ni faida pia kwa taifa kwa ujumla.

Kijiji cha Kwembe sasa kikiwa na hadhi ya mtaa, kiko katika kata ya Kibamba, Wilaya ya Kinondoni katika Mkoa wa Dar es salaam. Mjadala kuhusu yanayojiri katika mtaa huu unaweza kusaidia watanzania wengine wa maeneo mbalimbali ambayo wanakumbwa na masuala kama hayo hayo.

Izingatiwe kwamba mtaa huu uko katika kata ambayo huko nyuma palijitokeza mgogoro mwengine wa ardhi wakati wa uhamishaji na ulipaji fidia wa wananchi walioko katika eneo la Luguruni kupisha ujenzi wa mji mpya(satellite town).

Mgogoro huu wa awali ulifungua macho watanzania kuhusu ufisadi uliopo katika mfumo wa ardhi hususani katika tathmini na ulipaji fidia kwa wananchi. Ilibainika wazi kwa ushahidi wa nyaraka kwamba kuna watu walilipwa fidia zisizostahili, chini ya mtandao ambao ulihuisha maofisa wa ardhi. Waziri wa Ardhi wa wakati huo, John Magufuli, alipatiwa orodha kamili ya wahusika wa ufisadi huo na aliikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU). Hata hivyo, mpaka leo serikali haijaeleza hatua zilizochukuliwa kwa watu hao. Pengine sasa ni wajibu wa Waziri aliyefuatia wa Ardhi, Zephania Chiligati kueleza kuhusu hatua zilizochukuliwa. Lakini waziri mpya sasa anatuhumiwa kutumia nafasi ya kiserikali kutoa viwanja kisiasa kwa wafanyakazi wa taasisi zinazomilikiwa na CCM ambayo yeye ni Katibu Mwenezi, katika eneo hilo hilo. Kwa upande mwingine pia, ilibainika kuwa wapo wananchi ambao walipunjwa fidia zao kutokana na kutofahamu haki zao na kukiukwa kwa taratibu. Hii iliilazimu serikali kufanya tathmini na kulipa fidia upya. Wakati wananchi wa eneo hilo wakichekelea kulipwa fidia zao upya kwa mujibu wa haki, malipo hayo kwa upande mwingine ni hasara kwa mradi na serikali kwa ujumla kutokana na ulipaji wa fidia kufanyika mara mbili. Kwa vyovyote vile, sehemu ya hasara hiyo inabebwa kwa kodi yangu mimi na wewe. Mradi huo wa Luguruni pekee umeigharimu serikali shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ulipaji fidia pekee. Kiasi hiki ni mara tatu ya jumla ya fedha zote zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mikopo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo katika mkoa mzima wa Dar es salaam.

Kama vile taifa halijajifunza na hasara hii, jirani kabisa na Luguruni katika eneo la Kwembe pameibuka sakata lingine. Watendaji wa wizara ya Ardhi wameingia kisiri siri katika maeneo ya wananchi, na kuanza mchakato wa kuthaminisha mali za wananchi kinyume na taratibu ili kuwahamisha. Tayari wapo wananchi ambao walianza kulipwa fidia bila kufuata taratibu na bila haki zao kulindwa. Nyuma ya mchakato wote palikuwa na upokeaji rushwa na uporaji wa kitapeli wa ardhi ya wananchi. Suala hili lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kutokufahamu haki na wajibu wao katika masuala ya ardhi. Hivyo, baadhi ya wanasiasa na watumishi wasio waamininifu wakatumia mwanya huo kufanya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Ushahidi wa mambo hayo ulidhihirika wazi katika mikutano ya umma.

Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999(Namba 4 na 5 kwa mijini na vijijini) pamoja na kanuni zilizotokana na sheria hiyo zinaeleza bayana misingi muhimu ya kuzingatiwa katika masuala la ardhi. Ardhi inapaswa kutumika kwa ajili ya uzalishaji ama makazi kwa maendeleo endelevu. Katika hali hiyo, katika kuwaondoa wananchi katika ardhi yao, inapaswa kuzingatiwa kwamba ardhi ina maslahi kwao na maslahi yoyote yana thamani inayopaswa kurejeshwa. Hivyo, wananchi wanapopaswa kuhamishwa, uhamishwaji huo lazima uende na fidia kamili na kwa wakati. Sheria na kanuni husika zinataka pia raia wawezeshwe kushiriki katika kutoa mamuzi yanayohusika na umiliki wa ardhi. Kwa upande wa Kwembe hili nalo halikufanyika na hivyo kubatilisha mchakato wa fidia zilizoanza kulipwa.

Ili kutekeleza azma hiyo, kifungu namba 109 cha sheria kimempa mamlaka waziri husika kuandaa kanuni kuhusu ulipaji wa fidia. Mnamo mwaka 2001 Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Gideon Cheyo alitunga kanuni kwa notisi namba 78 ya kwenye gazeti la serikali la tarehe 4 Mei mwaka 2001. Hii ni nyaraka ambayo kila mtanzania aliyopo katika eneo ambalo anapaswa kuhamishwa kwa sababu mbalimbali anapaswa kuisoma.

Kanuni hizo ambazo zinatumika mpaka sasa zimeeleza bayana kwamba msingi wa tathmini katika ulipaji na ulipwaji wa fidia ni bei ya soko, ya ardhi na maendelezo ambayo yamefanyika. Kwa maneno mengine, hii ni dhana ya mgeni njoo mwenyeji apone badala ya ile ya mgeni njoo mwenyeji akonde kama ilivyoanza kufanywa katika eneo la Kwembe.

Kanuni zimekwenda mbali zaidi kwa kueleza vigezo vya kukubaliana ‘bei ya soko’. Baadhi ya vigezo vilivyotajwa ni pamoja na mauzo ya karibuni ya ardhi inayoendena na ardhi inayotaka kuuzwa sasa, thamani ya uzalishaji unaofanyika na njia nyinginezo zilizoelezwa. Vigezo hivi havikuzingatiwa katika ulipaji wa fidia ulioanza Kwembe.

Fidia pia imeelezwa kwamba inapaswa kuhusisha si tu thamani ya ardhi bali pia mambo mengine kama usafiri wa kuhama, kodi ya miezi 36(miaka mitatu), faida iliyopotea na usumbufu. Katika eneo la Kwembe, wapo wananchi waliotuhumiwa kuwa waliwapa rushwa watumishi wa ardhi ili wawaandikie fidia kubwa. Lakini walikuja kubaini baadaye kwamba walipewa fidia ya ardhi pekee pamoja na rushwa yao, kiwango ambacho walipwa kupewa kwa haki yao kabisa kilikuwa kikubwa kuliko walichopewa kwa kutoa rushwa. Walidhani wamepata, kumbe walikuwa wamepatikana. Huu ni mfano halisi wa jinsi ambavyo, utamaduni wa ufisadi katika taifa letu unavyoathiri mifumo ya haki. Yaliyotokea Kwembe ni funzo kwa raia kuhusu umuhimu wa utamaduni wa uwajibikaji kama kimbilio la haki za msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Matokeo ya ufisadi huo na matumizi ya madaraka ni baadhi ya wananchi kulipwa fidia kisirisiri kwa kiasi kidogo kwa ekari. Wakati hayo yakifanyike, jirani kabisa na Kwembe eneo la Luguruni thamani ya ardhi iliyofanyika kwa uwazi na kufuata taratibu baada ya nguvu ya umma kuanika ufisadi wa awali ilikuwa ni shilingi elfu 30 kwa mita moja ya mraba. Izingatiwe kwamba ekari moja ina mita za mraba takribani elfu nne. Ndio maana wapo wananchi wa eneo hilo la Luguruni ambao walilipwa takribani milioni mia moja. Pamoja na kuwa eneo la Kwembe si barabarani kama ilivyokuwa Luguruni, bado wananchi walistahili kulipwa fidia stahili inayoendana na thamani halisi ya ardhi na mali zao kwa wakati huu. Hata hivyo, kwa kuruhusu ufisadi, uvunjaji wa sheria/kanuni na matumizi mabaya ya madaraka, baadhi ya wananchi walikaribia kuzikosa haki zao.

Chini ya mchakato wa fidia unaofuata sheria na kanuni, wananchi wanapaswa kujaza fomu namba moja ya ukaguzi kwa ajili ya uthamini wa fidia. Fomu hii ipaswa kujazwa maelezo kuhusu kiwanja, nyumba, maendelezo, matumizi, mazao nk. Hivyo fomu hii inapaswa kujaziwa katika eneo la fidia ili mwishoni ijazwe mmiliki na kiongozi wa eneo. Fomu hii huambatana na picha na michoro. Lakini kwa upande wa Kwembe, watumishi wasio waaminifu, waliwaita wananchi wizarani na kujaza fomu hizo huko. Hatua ambayo inabaditilisha fomu zenyewe ambazo zilishaanza kutumika kulipia fidia. Fedha hizo zilizolipwa kwa njia hii ya kifisadi, ni wazi kwamba zinaweza kupotea na serikali kupata hasara kama ilivyotokea kwa Luguruni.

Maelezo ya fomu ya kwanza huhamishwa katika fomu ya kijani, ambayo nyuma huwa na mchanganuo wa uthamini. Fomu hii ni zana ambayo inaweza kutumiwa vizuri kulinda rasilimali za serikali. Kama fomu hii isipojazwa vizuri, raia anaweza bado kubaki na mali yake na wakati huo huo akawa shahidi upande wa serikali kulinda mali ya umma dhidi ya maofisa wanaotumia mianya kama hiyo kujinufaisha. Ili fomu hii iweze kutumika kutoa fedha za umma kwa ajili ya kulipa fidia inapaswa kuwa na saini za ngazi mbalimbali za utayarishaji na uidhinishaji. Ikiwemo saini ya mthamini mkuu wa serikali na muhuri wake. Kwa upande wa Kwembe, malipo ya awali ya fidia yalitolewa bila kuwa na saini za wahusika, kwa tafsiri ya haraka hizi fedha zilizotolewa pamoja na kuwa zilitoka kwenye mikoba ya umma, zilitolewa na watu binafsi sio serikali. Namna pekee ya kulinda ardhi ya wananchi, na fedha za umma katika mazingira kama hayo ni kufanya uchanguzi wa kina na kuchukua hatua kwa wahusika wote.

Baada ya mambo yote hayo kufunuka, viongozi wa serikali kama kawaida walianza kutumiana mipira. Wakati waziri husika akieleza kwamba mradi uko chini ya wilaya, mkuu wa wilaya yeye alitoa tamko la kutokuwa na taarifa zozote. Hata hivyo, fomu za fidia zilizotolewa zinaeleza kwamba zimetolewa na halmashauri ya manispaa ya Kinondoni. Taifa linaweza kujifunza mambo kadhaa kutokana na sakata linaoendelea Kwembe, na masakata kama hayo yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mosi, ufisadi ni adui wa haki. Wananchi wanaweza kukosa haki zao tu kutokana na mfumo wa rushwa ambao umeota mizizi katika jamii yetu. Hivyo, jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mmoja kwa manufaa yake yeye binafsi na kwa taifa kwa ujumla. Pili, wananchi kutokufahamu sheria na kanuni mbalimbali kunatoa mianya kwa viongozi wasio waadilifu kupitisha taratibu. Tatu; sera za zimamoto huleta mzigo mkubwa wa fidia katika taifa. Laiti kama sera za maendeleo ya makazi zingeweka mkazo katika mipango ya ujenzi wa miji ya muda mrefu na kulinda viwanja vinavyotengwa kwa kazi maalumu, nchi isingebeba mzigo mkubwa wa fidia zinazojitokeza mara kwa mara kwa ajili ya kupisha miradi ya maendeleo. Izingatiwe kuwa fidia hizi hulipwa toka fedha za za walipa kodi ambazo zingeweza kutumika kupeleka maendeleo katika maeneo mengi zaidi. Nne, nguvu ya umma ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Hivyo, kila wanapopata kero ya msingi, wananchi wanapaswa kuungana pamoja, pale ambapo viongozi wa kuchaguliwa wanapoashindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatetea bado wananchi wanafursa ya kusukuma hatua kuweza kuchukuliwa kwa kutumia njia mbadala. Ushujaa wa wananchi wa Kwembe wa kwenda kutoa taarifa TAKUKURU kwa ajili ya kulinda mali zao na fedha za umma na kuwakataa viongozi wasio waadilifu, unapaswa kuigwa na wengine katika maeneo mengine. Maendeleo katika sekta ya ardhi yaje sambamba na kulinda haki za wenyeji. Wageni waje lakini wenyeji wasikondeshwe.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com

Tuesday, March 3, 2009

Richmond, Dowans and Operesheni Safisha Mafisadi

Richmond, Dowans na Operesheni Safisha Mafisadi

Na John Mnyika

Kwa muda wa wiki mbili nimekuwa kikifuatilia na kutafakari mjadala unaoendelea kuhusu ununuzi wa mitambo ya kufua umeme ya Dowans mintaarafu hofu ya taifa kukumbwa na tatizo la uhaba wa umeme. Aidha katika kipindi hicho nimekwepa kuandika hadharani mawazo yangu kuhusu suala hilo. Katika kipindi chote hicho nimekuwa nikizungumza na walio katika korido za mamlaka na maamuzi kueleza mawazo yangu. Nikiamini kwamba waliouanzisha mjadala huu, watauhitimisha kwa kuzingatia mahitaji ya taifa na hisia za umma. Badala yake mjadala huu, kama moto wa nyikani, umeendelea kushika kasi na kuchukua sura mbalimbali.

Pamoja na kuwa na uhuru wangu, kama mtanzania; natambua kwamba kwa upande mwingine sehemu ya uhuru huo imeshikiliwa na taasisi ambazo mimi ni sehemu ya uongozi. Bahati njema, taasisi hizo bado hazijatoa misimamo yao. Kati ya taasisi hizo, ni CHADEMA. Bahati nzuri zaidi ni kuwa chama hiki kimejitambulisha kuwa ni cha demokrasia, kinachotoa fursa ya uhuru wa mawazo. Ndio maana, mwaka 2007 ulipozuka mjadala baada ya Rais Kikwete Kamati ya kupitia sheria, sera na mikataba ya madini, maarufu kama Kamati ya Bomani, umma ulishuhudia mjadala mkali baina ya viongozi wa CHADEMA. Mjadala huo ulichangiwa na dhamira ya kuundwa kwa kamati hiyo, muundo na uteuzi wa Mbunge kupitia CHADEMA, Zitto Kabwe katika kamati hiyo. Mjadala huo ulioibua mambo kadha wa kadha ya msingi ulihitimishwa kwa msimamo wa pamoja wa chama uliobeba fikra mbadala.

Kwa mara ya kwanza nilizungumza kuhusu hili suala la Richmond mwaka 2006, wakati huo serikali ilikuwa ni kwanza imeweka dhamira ya kununua mitambo hiyo. Wakati huo, tukiwa kwenye kongamano la vijana tuliweka msimamo wetu bayana kuwa Richmond ni kampuni ya kitapeli, na mchakato mzima wa tenda umegubikwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Serikili na CCM wakati huo ilikanusha, na kwa ujumla onyo letu lilionekana kuwa ni ‘kelele za mlango’, ‘uzushi’ na ‘upinzani wa maslahi ya taifa’. Kwa kuwa ukweli ni mmoja na haugawanyiki, ni hoja hoja zile zile baadaye zikaja kubebwa na Kamati Teule ya Bunge, maarufu kama Kamati ya Mwakyembe na baadaye kubarikiwa na maazimio ya Bunge.

Lakini ‘geuka nyuma’ hii ya Bunge na serikali inayoongozwa na CCM haikuja hivi hivi. Ni baada ya heka heka za vyama vya upinzani, vyombo vya habari na wadau wengine. Ni baada ya kuanza kwa ‘uasi wa umma’ kulikofuatiwa baada ya kupitishwa kwa ‘udikteta wa uwingi’; bajeti iliyoongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi, kuzimwa kwa hoja Buzwagi iliyowasilishwa na Zitto; kuwekewa mizengwe kwa hoja ya ufisadi wa Benki Kuu(BOT) iliyokuwa iwasilishwe na Dr Slaa; na kwa ujumla, hotuba mbalimbali za kambi ya upinzani za wakati huo zilizozungumza suala la Richmond ikiwemo ile bajeti mbadala. Nguvu hiyo ya umma iliunganishwa na ziara ya ushirikiano wa upinzani, iliyoratibiwa na kufadhaliwa na CHADEMA, ambayo ilianzia uwanja wa Jangwani kwenye mapokezi ya Zitto Kabwe baada ya kusimamishwa na kuhitimishiwa Mwembe Yanga, ambapo Orodha ya Mafisadi ilisomwa na Dr Slaa. Hiyo ilikuwa ni Septemba 15 mwaka 2007. Toka wakati huo, mpaka wakati huu; taifa haliko kama lilivyokuwa. Tulizoea kwamba tabaka tishio kwa uhai wa taifa, ni kupatuka kwa pengo kati ya matajiri na masikini. Lakini sasa mstari umechorwa katika taifa, kati ya mafisadi na waadilifu; baina ya maisha ya ufisadi na utamaduni wa ufisadi. Mawaziri wa Serikali na makada wa CCM nao wakaanza ziara za ‘kuelezea uzuri wa bajeti’,ambazo kwa muda mwingi zaidi zilihusisha kujibu hoja za ufisadi-kuanzia Richmond, Benki Kuu(EPA, Majengo pacha nk), Buzwagi, Rada; orodha ni ndefu. Wakaambulia ‘uasi’ na ‘upinzani’ toka kwa umma, ulioambatana na ‘zomea zomea’ katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Neno ‘ufisadi’ likawa msamiati wa kila kaya, na mafisadi wakatambulika rasmi kuwa ni maadui wa taifa.

Pima joto za vyombo vya dola na vile vya ushushushu zikaona bayana kwamba uwepo wa serikali madarakani upo mashakani. Namna pekee ya kutokea ikawa ni kusikilizwa kwa sauti ya wengi; kama isemavyo, sauti ya watu; sauti ya Mungu. Kamati ya Bomani ikaundwa, Kamati Teule ya kuchunguza suala la Richmond ikaundwa; Ofisi ya Rais ikatoa tamko kuhusu EPA iliofuatia kuundwa kwa Kamati. Kadiri nguvu ya umma, ilivyokuwa ikishinda mtandao wa mafisadi na kuilazimisha serikali kuanza kuchukua hatua ndivyo ambayo mafisadi nao wakaanza kuchukua hatua. Vita baridi ikazuka katika taifa letu, vita ambayo inaendelea mpaka hivi leo.

Mafisadi, mawakala na vibaraka wao nao wakarudi mezani kujipanga upya. Wakaja na mikakati mipya. Mkakati wa awali ukawa kukanusha madai yote na kutishia kwenda mahakamani, mkakati huo ukashindwa. Mkakati ukafuata wa kuwachafua vinara wa kupinga ufisadi, nao ukashindwa. Hatimaye kamati husika zikamaliza kazi yake. Kutokana na taarifa ya Kamati mojawapo, Waziri Mkuu akalazimika kujiuzulu; baraza la mawaziri likavunjika lenyewe kwa kitendo hicho. Matokeo ya Kamati hizo ni baadhi ya watuhumiwa kupelekwa mahakamani. Kwa bahati mbaya, wakati yote hayo yanafanyika mihimili ya ufisadi huo iliyojikita katika mfumo wa chama kinachotawala na kwenye dola yenyewe; bado iko barabarani inapanga mikakati mipya kila kukicha.

Mara baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Lowassa kujiuzulu, wengine tulijitokeza hadharani na kutaka yeye na maswahiba wake wakamatwe na kufunguliwa mashtaka. Na wakati huo tulionya kuhusu mkakati wa mafisadi kujisafisha na wasiwasi wa mafisadi kuligawa taifa. Toka tuseme hayo, mpaka leo wakina Lowassa na watuhimiwa wengine wa matumizi mabaya ya madaraka wako barabarani wakati wenzao wakina Mramba na Yona wako mahakamani. Tulionya kuhusu kutikishwa kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki, wakati ulipotolewa msamaha kwa wezi wa fedha za EPA waliorejesha fedha zao, hata wachache waliokacha kurejesha fedha walipopelekwa mahakamani tuliendelea kupaza sauti kutaka mafisadi halisi wa Kagoda wapelekwe mahakamani.

Matokeo ya mafisadi kuendelea kutamba barabarani badala ya kuwa mahakamani ni kupata fursa ya kupanga na kutekeleza mikakati. Ukitafakari kinachoendelea hivi sasa, inaonyesha bayana kwamba iko Operesheni Safisha Mafisadi (OSAMA) katika taifa letu. Mkakati ule ule uliotumiwa na wanamtandao, wa kumwingiza Rais Kikwete madarakani wa kumsafishia mteule wao njia na kujenga matumaini mapya, huku wakichafua wapinzani wao wote-wa nje na ndani ya chama chao ndio ambao unaendelea hivi sasa.

Baada ya kushindwa OSAMA ya kupita majimboni kujisafisha; sasa OSAMA mpya ikabuniwa. Mikakati hiyo ikahusisha pia kuanzishwa kwa wimbi la magazeti ya uchafuzi na utetezi. Mikakati hiyo ikahusishwa kuzushwa kwa mijadala mingine yenye kuligawa taifa ili kuondoa fikra za taifa katika mjadala wa ufisadi. Mkakati huu ukahusisha mpaka baadhi ya watu wa kada mbalimbali kufadhiliwa kufanya ziara za kusafisha mafisadi, na kushambulia wenye kupinga ufisadi. Hapa ninapoandika makala hii, mikutano ya hadhara inaendelea katika baadhi ya mikoa nchini ikiwa na ajenda hiyo. Mafisadi wenyewe sasa wako nyuma ya barokoa, wakiendesha mambo kwa mbali kwa kutumia vibwebwezo (remote control) walilichezesha taifa na baadhi ya viongozi wake, kuanzia wa kisiasa mpaka wa dini; ngoma wasizozielewa.

Pamoja na kuwa na orodha ndefu ya kashfa ya za ufisadi katika taifa letu, bado Mkataba wa Richmond, na kujiuzulu wa Lowassa ni matukio yaliyopiga muhuri kwenye mioyo ya watanzania. Kwa wataalamu wa OSAMA, ushindi na kubadili nyoyo za wananchi katika suala hili, ni hatua moja kubwa katika ujio wao mpya na kutezwa harakati zote zilizokwishafanyika mpaka hivi sasa.

Baada ya mkakati wa kumsafisha Lowassa, mlango unaonekana kwa sasa ni kupitia kuibariki mitambo ya Dowans. Fungua za kuingilia mlango huo ni kuinuua mitambo hiyo. Wakati mzuri wa kufanya hivyo, ni kipindi ambacho taifa lina hofu ya uhaba wa umeme siku za usoni. Ili Dowans na maswahiba wake waonekane kuwa ni wakombozi wa Taifa!

Kwa yoyote aliyewahi kusoma kitabu cha Confession of the Economic Hitman (ungamo la kuwadi wa kiuchumi- kwa tafsiri yangu), wanaweza kupata picha la mfumo wa kifisadi unavyoweza kufanya kazi katika suala kama hili.

Makuwadi hao wakajifunika katika kivuli cha maslahi ya taifa na nia njema ya kulinasua taifa kwenye shaka ya kukumbwa na baa la uhaba wa umeme, wakaenda katika Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ambayo mwenyekiti wake ni Mbunge Zitto Kabwe. Wakamwaga takwimu na maelezo yao, kwa ustadi na ushawishi mkubwa. Mdadisi yoyote wa mambo akichambua wajumbe wanaounda kamati hiyo, kwa kuangalia michango yao bungeni- hususani michango yao wakati wa mjadala wa Bunge kuhusu ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Richmond unaweza kubashiri kilichojiri na kitakachojiri. Wapo wabunge wa jamii ya Zitto Kabwe, wao wakati wote wanachotazama ni nguvu ya hoja na kutazama ukweli na daima wamekuwa wakitanguliza zaidi maslahi ya taifa pengine hata kuliko maslahi ya vyama vyao. Hawa walishawishiwa na TANESCO kwa hoja, na hivyo kuanza kuhoji maamuzi ya Kamati zingine za bunge kuhusu suala hilo hilo. Lakini hawakutaka kufanya maamuzi ya mwisho, wametaka kamati zikutune ili ukweli uweze kujulikana. Kundi hili, wakipata muda wa kutafakari ukweli wa ziada na kupata taarifa sahihi, hubadili msimamo wao.

Halafu wako wabunge jamii ya Peter Selukamba, ambao msimamo wao wa kutetea ya mfumo wa utawala na wakati mwingine kuwatetea watuhumiwa wa ufisadi pamoja na ufisadi wao inajulikana bayana. Katika ya kundi hili, wapo wanaonufaika na ufisadi na wapo pia mawakala wa ufisadi. Hawa ni wazi watamshinikiza zaidi Mwenyekiti wa Kamati ili matakwa yao yatimie. Ni katika ule usemi kwamba katika siasa, hakuna rafiki wala audui wa kudumu; kuna maslahi ya kudumu.

Halafu kuna kundi la wabunge wengine wachache, ambao wao kwa kawaida yao hawana kawaida ya kuchotwa na yanayowasilishwa; wanakwenda mbali zaidi. Wao walishafanya maamuzi, na hawaoni haja ya kamati hizo kukutana. Kwao wao, kwa kusikiliza maelezo ya TANESCO na kupitia taarifa za Kamati nyingine, wameshaweka misimamo yao moyoni- kununua mitambo ya Dowans, hapana!. Hakika suala hili litaendelea kuigawa kamati husika, sitashangaa wakiendelea kupingana hadharani, na katika maeneo mengine wajumbe wakiwa na mgawanyiko wa namna hii wanaweza kupigiana kura za kutokuwa na imani.

Inawezekana mimi si mtu mwafaka kuchambua ama kutoa mawazo kuhusu suala hili kwa kuwa msimamo wangu kuhusu suala hili tayari unajulikana. Lakini naandika makala haya kuchochea mjadala zaidi na hatimaye taifa liweze kufanya maamuzi kwa kuzingatia fikra mbadala. Naandika makala hii kutaka wabunge wetu na serikali wasikilize sauti ya umma

Eneo ambalo kampuni ya Richmond ilikuwa iweke mitambo yake, lipo ndani ya jimbo la Ubungo. Ni eneo hilo hilo ambalo kampuni ya Dowans imeweka mitambo yake. Katika jiografia ya Dar es salaam mitambo ya Dowans iko pembeni ya Makao Makuu ya TANESCO ukipita tu mataa ya Ubungo. Kwa kuzingatia mazingira hayo, mwaka 2008 tuliitisha Kongamano la Wakazi wa Ubungo, kujadili masuala mbalimbali ya wananchi katika sekta za ardhi, umeme na wafanyakazi. Katika suala la umeme, mjadala kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Kamati ya Bunge kuhusu Richmond ulichukua nafasi kubwa kwa kurejea tatizo la bei kubwa na uhaba wa umeme nchini. Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa kongamano hilo. Kama wakazi wa jimbo hilo, tuliazimia kwamba kwa kuwa imethibitika kwamba mkataba na Richmond ulikuwa batili, hata mkataba wa mrithi wa mkataba batili yaani Dowans nao unapaswa kutafakariwa ubatili wake. Hivyo, tuliazimia mitambo ya Dowans itaifishwe na serikali, iuzwe kufidiwa gharama za fedha ambazo serikali imeshalipa mpaka sasa kwa Richmond/Dowans. Ilibainika pia kwamba tayari kwenye mchakato huo, serikali ilikwishalipa takribani bilioni 30; ziada ya yale malipo ya milioni 152 kwa siku ambayo yalikuwa yakitolewa. Fedha hizo ni nyingi kiasi cha kutoa shilingi milioni moja kwa kila mkazi mtu mzima wa kata ya Ubungo. Ama ni sawa na kununua mitambo kamili ya umeme kwani kwa taarifa mbalimbali mitambo kama hiyo inapatikana kwa bei ya dola milioni 14. Baada ya Kongamano hilo, azimio hilo pamoja na maazimio mengine yalisambazwa kwa umma kupitia mikutano ya hadhara, na kukabaliana kwamba Oktoba 14, 2008 pangefanyika maandamano ya wakazi wa Ubungo kushinikiza utekelezaji wa matakwa hayo ya umma.

CHADEMA jimbo la Ubungo ikaratibu maandamano ya wakazi, kuelekea kwenye kampuni za Dowans na TANESCO ambazo ziko jirani; lakini polisi walikataa kutoa kibali cha maandamano hayo. Sababu pekee ambayo ilitolewa ni kuwa Oktoba 14 ni siku ya Nyerere, hivyo vyama havipaswi kufanya maandamano ya siku hiyo kukumbuka mchango wa Baba wa Taifa katika kupiga vita ufisadi. Badala yake, polisi ikaelekeza watanzania wote wakashiriki pamoja katika uwanja ambao serikali imeandaa maadhimisho!

Baadaye ikafutiwa na taarifa ya Waziri Mkuu Pinda kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge na kupelekwa kwa mtuhumiwa mmojawapo wa Richmond mahakamani. Sambamba na hilo, mjadala wa ununuzi wa mitambo hiyo ukashika kasi, mwanzoni ukibebwa na Waziri wa Nishati, Bwana Ngeleja na kupingwa na Kamati husika chini ya Uenyekiti wa Shelukindo; sasa umeibukia kwenye kamati ya Zitto.

Pamoja na suala la uhalali wa mitambo ya Dowans ukirejea ubatili wa mitambo wa Mkataba wa Richmond. Liko pia suala la umiliki wa kampuni ya Dowans!. Kamati ya Bunge. Kamati ya Mwakyembe ilijulisha bunge kuwa ilitaarifiwa nje ya kiapo kuwa Richmond ni mradi wa kina Lowassa na Rostam Aziz. Pamoja na kuwa kwenye majumuisho yake, Kamati ilikwepa kutaja moja kwa moja mmiliki wa Richmond. Lakini mfuatiliaji yoyote anaweza kuthibitisha uhusiano wa karibu kati ya Lowassa na Rostam Aziz na makampuni ya Richmond na ile ya Dowans, ukirejea kutajwa kwa kampuni ya Caspian. Mduara huu wa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka pekee, unaweza kubatilisha azma ya kununua mitambo toka kampuni hiyo. Pengine kamati zote tatu, ile teule na hizi za kudumu zingeingia kwa undani kuhusu suala hili na kupendekeza hatua timilifu leo taifa lisingekuwa linayubishwa kama penduli! Hoja wala isingekuwa uhalali au uharamu wa kununua mitambo chakavu kwa kurejea sheria ya manunuzi ya umma; hoja ingekuwa ni ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na uhujumu wa uchumi wa taifa.

Wataalamu wa OSAMA, wamefanikiwa kuzifunika hoja hizi kwa hoja tamu ya matazimio ya uhaba wa umeme na haja ya kutanguliza maslahi ya taifa katika mjadala huu. Nakubaliana na Zitto kwamba nchi iko na litaendelea kuwa mashakani kutokana na uhaba wa umeme, na kwamba tunahitaji suluhu ya kitaifa. Lakini ili tupate suluhu hiyo, tupanue wigo wa fikra zetu. Tuichambue asili ya tatizo lenyewe, ukosefu wa maono, sera na mipango ya muda mrefu katika sekta ya umeme chini ya utawala wa CCM, na ombwe la dhamira ya kisiasa ya kutekeleza hata ile miradi iliyopo tayari. Tatizo hili linakuzwa zaidi na uzembe na ufisadi wa kutumia tatizo la umeme kama kivuli cha kujinufaisha. Tumeona hivyo katika IPTL, Kiwira, RICHMOND na tutaendelea kuona hivyo katika Dowans. Katika hili, ni muhimu kwa Zitto na Kamati yake kujinasua na mtego wa kisiasa. Kama ni kutetea maslahi ya taifa, ni umma upi huo wanaoutetea kama umma wenyewe umeshatamka kwamba hautaki mitambo ya Dowans na kwamba Richmond ni ufisadi? Kamati za bunge zitumie muda mrefu zaidi kujadili mbinu za kulinasua taifa katika suala hili, badala ya kutumia kodi zetu na muda wa watanzania kujadili Dowans pekee. Kwa bahati mbaya, taifa limeingizwa katika mizengwe hii na TANESCO. Mwaka 2001, ripoti za kiserikali zilikwisha tabiri kuhusu upungufu wa umeme mwaka 2006 na hata mwaka 2009; lakini miaka mitano baadaye watawala hawakuongoza taifa kujiandaa badala yake wahujumu uchumi wa taifa kupitia kashfa ya Richmond mwaka 2006. Watawala hao, bado wako nyuma ya pazia wakisuka mipango ya kurejea- na makuwadi wao wako bado kwenye korido za Mamlaka za Wizara ya Nishati na hata TANESCO yenyewe wakiendelea kuwa mawakala wa hujuma kwa watanzania. Wanajipenyeza kila mahali na kufanya kila jitihada za kutoa taarifa za uwongo za kuwahadaa wabunge wetu kubariki maamuzi tenge ya serikali. Sasa tuko mwaka 2009, hata baada ya watawala kukumbushwa Februari 2008 kuhusu haja ya kujiandaa na dharura ya umeme bado leo Machi 2009, mwaka mmoja baadaye na miaka takribani nane toka tahadhari ya awali tunalazimishwa kuamini kwamba hii ni dharura ya hali ya juu. Hali Kama hii inafanya wengine tuamini kwamba kuna kikundi cha watu, kinaacha matatizo ya taifa kuweka mianya ya dharura ili kuhalalisha kupitishwa kwa sheria na kupitishwa kwa zabuni kwenya mazingira yanayowawezesha kutimiza malengo yao ya kiuchumi na kisisiasa. Ndio maana, wakati taarifa zikiwa zinaonyesha kwamba katika ya mikoa itayokumbwa na uhaba wa umeme ni Mwanza ambapo kuna mitambo ya umeme ambayo muda wake wa kukodishwa imeisha. Pamoja na utata wa bei na mikataba ya mitambo hiyo, bado hatusikii ikijadiliwa kununuliwa au kukodishwa tena kama ambavyo Dowans inavyopigiwa upatu na TANESCO. Historia ya Taifa letu itufundishe, wataalamu kama Chenge ndio ambao walitumia nafasi zao akiwa mwanasheria mkuu wa serikali kulisukuma taifa katika mikataba kanyaboya ikiwemo katika ununuzi wa RADA. Sasa kama watalaamu kama Dr Idrissa Rashid wamekwishatajwa kwamba walipewa mlungula katika mgao wa rushwa ya RADA ni vyema tukautazama kwa jicho la mashaka utamu wa takwimu na maelezo wanayotupatia kuhalalisha manunuzi makubwa mengine.

Kwangu mimi hoja kuu sio bei ya mitambo ya Dowans. Maana najua pamoja na kuwa bei ya bilioni 30 inayotajwa inakaribia mara mbili ya bei ya kawaida. Bado maajabu yanaweza kufanywa na Dowans ya kupunguza bei zaidi kwa sababu mbili. Kwanza kiuchumi, tayari walishatunufaika na malipo ya awali ambayo yalikwishafanyika. Hivyo, wanaweza kuiuza mitambo hiyo kwa bei ya kutupa. Pili; kisiasa, serikali kununua mitambo ya Dowans ni jambo lenye maslahi makubwa kwa walionyuma ya kampuni hiyo, na wote wanaozongwa na “Mzimu wa Richmond”. Hivyo, kundi hilo linaweza kuwa tayari hata kuitoa mitambo hiyo bure kwa kuwa uamuzi wowote wa kuisafisha kampuni ya Dowans ni mtaji muhimu kwa OSAMA. Kwa OSAMA ununuzi wa mitambo hiyo, sio tu bezo kwa harakati dhidi ya Richmond/Dowans bali utakuwa pia mzigo wa taswira hasi ya kisiasa kwa wote watakaoendelea kupigia debe ununuzi huo.

Jambo lingine ninalokubaliana na Zitto ni kuwa kuna makundi ndani ya CCM. Sasa tunalazimishwa kuamini kwamba makundi hayo yametokana na vita dhidi ya ufisadi, na kwamba makundi hayo ni kati ya kundi la mafisadi na kundi la ‘waadilifu’. Na kwamba CCM sio chafu, ila kuna baadhi ya wanachama wake ndio wachafu!. Kadiri mahubiri haya mapya, ambayo sasa yameanza kutengezewa majukwaa na ziara- ya kujilindia majimbo katika uchaguzi ujao, ndivyo ambayo taifa litatoka katika mstari thabiti ambao taifa lilianza kuuchora nje ya mipaka ya vyama. Makundi ya CCM yapo, yakitokana na sababu mbalimbali; lakini kubwa zaidi ikiwa ni migogoro ya kimaslahi na kimadaraka. Lakini mwisho wa siku, utawala ni utawala. Ndio maana wengine tulihoji, nguvu na makeke yaliyotumika wakati wa mjadala wa Richmond Bungeni lakini nje ya hapo nguvu hiyo imethibitika kuwa ni ya soda. Ukisikiliza kauli mbili za Dr Mwakyembe za hivi karibuni, ile ya kutamka kwamba wananchi kumnyima kura Kikwete mwaka 2010 ni kuwapa ushindi mafisadi; na ile ya wiki hii ya kwamba kauli za Zitto kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Dowans ni sehemu ya Operesheni Sangara. Ukitafakari sana kauli hizi, mtiririko wa matukio na masuala yanayojadiliwa; unaweza kupata taswira ya mambo yaliyokatika akili za wanasiasa wetu.

Tukiacha mijadala ya watu na matukio inayoendelea hivi sasa, kuna masuala mawili yanapaswa kujadiliwa na hatua za haraka kuchukuliwa kila moja kwa peke yake na kwa uzito wake. Mosi, jitihada pana za haraka zifanyike za kutafuta umeme wa kufidia pengo linalotarajiwa, nje ya mjadala wa ununuzi wa mitambo ya Dowans. Kwa hakika, Mkurugenzi wa TANESCO, Dr Iddrissa Rashid ameshindwa kuishauri serikali vizuri katika hili. Kwa uzembe huu, na matumizi mabaya ya madaraka yaliyofanyika hapo nyuma, sio mwelekeo bora wa TANESCO chini yake. Pamoja na kufikiria dharura, kamati za bunge ziisimamie serikali kutekeleza mipango ya muda mrefu; ya sera zenye maono katika sekta ya umeme. Ni aibu kwa taifa lenye rasilimali kama Tanzania kuwa na uhaba wa umeme. Pili; turejeshe utamaduni wa uwajibikaji na uadilufu kwa kuchukua hatua kamili dhidi ya wahusika wa Richmond, na kufunua pazia linalofunika kampuni ya Dowans. Kesi ya Gire mmoja, huku wakina Gire mwingine, Lowassa, Rostam nk wako uraiani ni kuendelea kuahirisha matatizo. Suala hili liende sambamba na kuendeleza mijadala mingine kama ile ya Kagoda, Meremeta, Deep Green nk. Mizizi ya Operesheni Safisha Mafisadi ni lazima ikatwe kwanza, ama sivyo tutaendelea kutumbukizwa kwenye mijadala yenye kupunguza imani na heshima baina ya watanzania wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com