Saturday, March 31, 2012

Turekebishe kwanza kanuni ndipo tufanye Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki!

Siku chache zilizopita tarehe 28 Machi 2012 niliwasilisha kwa katibu wa bunge mapendekezo ya mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge Nyongeza ya Tatu (The East African Legislative Assembly Election Rules) kwa mujibu wa kifungu cha 3 fasili ya 3 (a) ya kanuni husika za bunge toleo la mwaka 2007.

Malengo ya mapendekezo niliyowasilisha ni: Mosi, kupanua wigo na kuboresha mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa kuwakilisha vyama vya upinzani na kambi rasmi ya upinzani bungeni. Pili; kuwezesha uwepo wa uwakilishi wa vijana katika bunge la Afrika Mashariki. Tatu; kupanua wigo na kuboresha mchakato wa upatikanaji wa wajumbe kwa kuzingatia jinsia. Nne; kuanza mchakato wa kufanyia marekebisho kanuni za bunge la Tanzania za uchaguzi wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia maudhui ya muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki.

Marekebisho hayo yatawezesha kuzingatiwa kadiri iwezekanavyo uwakilishi wa kambi na pande zote (shades of opionion), makundi maalum na uendelevu na kumbukumbu ya kitaasisi (continuity and institutional memory) katika wakati huu ambapo uchaguzi husika una umuhimu wa pekee ambapo jumuiya ya Afrika Mashariki ipo katika soko la pamoja na majadiliano ya kuwa na sarafu moja yanaendelea hali ambazo zina athari kwa nchi na wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Thursday, March 29, 2012

Mnyika: Mpango wa Dharura wa Umeme


Utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme unasuasua kutokana ombwe la uongozi katika serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete hususan udhaifu wa kiuratibu ulioonyeshwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na uzembe wa kiutendaji wa Wizara ya Nishati na Madini.

Izingatiwe kwamba kwa nyakati mbalimbali kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa nyakati mbalimbali tulieleza umuhimu wa serikali kuchukulia dharura ya umeme kwa uzito wake na kuunda chombo maalum kitakachohusisha wadau na kupewa msukumo na uongozi mkuu wa nchi katika kupanga na kutekeleza mkakati wa taifa wa kuondoa janga hili linalojirudia.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda mara zote alikataa mapendekezo hayo huku akisema kwamba serikali iwajibike iwapo itashindwa kutekeleza mpango huo kwa wakati. Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja naye alieleza bungeni kuwa baada ya mpango huo kupita na kuwa na uhakika wa fedha kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na mabenki binafsi miradi hiyo yote itatekelezwa kwa wakati.

Kutokana na mipango hiyo kutotekelezwa kwa wakati Waziri Mkuu Pinda na Waziri Ngeleja kukiri kwamba walitoa taarifa potofu kwa bunge na kwa umma ilibidi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kurekebisha mwelekeo wa mambo katika utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme.

Wednesday, March 28, 2012

Serikali ijieleze kwa wananchi juu ya utafutaji na uchimbaji wa Urani

Wizara ya Nishati na Madini inayoongozwa na Waziri William Ngeleja ieleze wananchi hatua iliyofikiwa katika kuboresha mifumo ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi kuhusu utafuataji na uchimbaji wa madini ya urani ili kuhakikisha umiliki, manufaa na usalama.

Aidha Wizara ieleze hatua ambazo zimefikiwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato; kama ambavyo nilihoji Bungeni tarehe 15 Julai 2011.

Pia hatua iliyofikiwa na serikali kufanya marekebisho ya sheria kuweka mipaka ya kiwango cha wigo wa mikopo katika mitaji katika madini kwenye mahesabu ya kodi, kuwezesha kuondolewa kwa riba ya mikopo kwa makampuni yanayohusiana na kuhakikisha kodi ya mauziano ya makampuni makubwa ya madini ya kimataifa hata kama yamefanyika nje ya nchi.

Itakumbukwa kwamba kwa nafasi yangu ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini nilieleza masikitiko yetu juu ya maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo litaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia itahatarisha usalama.

Monday, March 26, 2012

Mahakamani:Kesi kupinga ushindi wangu 26/03/2012


Nikiwa natoka mahakamani, nyuma yangu ni wakili anayenitetea, Bw. Mbogolo

"Nguvu ya Umma......Peoples Power!!"
"Sauti ya watu, sauti ya MUNGU"


Wakili wangu, Bw. Mbogolo akiwa anatoka akimsabahi Mshtaki, Bi. Hawa Nghumbi (CCM)

Kutembea kutoka mahakamani kwenda ofisini na wananchi waliofika mahakamani
"A walk from Court to Office"

Mkutano wa hadhara wa Kimara Mwisho 25/03/2012


Nikihutubia umati wa wananchi Kimara Mwisho


Nikipitia hoja na maswali mbalimbali zilizoletwa kwa maandishi


Wananchi waliojitokeza kushiriki mkutano wa hadhara Kimara mwisho

Saturday, March 24, 2012

Ratiba ya Mbunge kukutana na wananchi leo Kwembe na Saranga/Kimara

Ratiba yangu ya kukutana na wananchi jimboni Ubungo leo jumapili tarehe 25 Machi 2011: Saa 9 mpaka 10 nitakuwa Kata ya Kwembe Mtaa wa Luguruni Msakuzi kwa Mbokomu kuhusu Umeme na Maji kupitia mkutano wa kuunganisha nguvu za pamoja na wananchi kuwezesha hatua kuchukuliwa na DAWASCO na TANESCO.


Mkutano wa Hadhara Kimara mwisho Saa 9:00 mpaka 12 Jioni kutoa mrejesho kuhusu maji, barabara na kesi ya kupinga ushindi wetu. Mkutano utaanza na hotuba za viongozi wa chama jimbo la madiwani wa kata za Saranga na Kimara, mimi nitaanza kuhutubia kuanzia saa 11 jioni na kutakuwa na fursa ya kuniuliza maswali ya papo kwa papo na kuwasilisha masuala mbalimbali ya kuzingatiwa na mbunge na chama katika mkutano wa saba wa bunge. Nimeitika mwito, natarajia uwepo wenu. Maslahi ya Umma Kwanza.

Katizo la umeme DSM, maeneo yatakayokatizwa Jimbo la Ubungo

Jumapili tarehe 25 Machi kutakuwa na katizo la umeme kwenye baadhi ya maeneo ya DSM kuanzia saa 2 Asubuhi mpaka  10 jioni.
Kwa Jimbo la Ubungo katizo litahusu maeneo yafuatayo: Sinza, Goba, Ubungo Kisiwani, Mabibo Jeshini,  Makuburi (External, Barabara ya Mandela, Mabibo Hosteli, Kibangu).
Hivyo usishike waya wowote uliokatika badala yake toa taarifa kwa ofisi za kanda za TANESCO Kinondoni Kaskazini (Mikocheni):0716768584; 0784768584 au Kinondoni Kaskazini (Magomeni): 0768985100; 0784271461; 0784078837 au 0788379696.
Sababu zilizotajwa na TANESCO: Kuunga line ya msongo mkubwa wa 132kV katika kituo cha kupoozea umeme Ubungo na Kufunga LBS kwenye njia ya FZ3-1&2 na U1 ili kurahisisha uzimaji wa line wakati inapopata hitilafu na kurahisisha kugundua eneo la hitilafu kwa urahisi na haraka. Maslahi ya Umma Kwanza.

Kampeni Vijibweni Kigamboni na Migogoro ya Ardhi DSM

Leo jumamosi 24/03 niliweka kambi Kata ya Vijibweni, nawashukuru wananchi wa Kigamboni kwa kuunganisha nguvu ya umma. Asubuhi tulianza kwa maandamano mpaka Soweto, mchana nikaendesha mafunzo ya awali ya mawakala wa kampeni ya mtu kwa mtu pamoja na ulinzi wa kura katika uchaguzi. Jioni nikahutubia mkutano wa hadhara Kisiwani na usiku nimefanya kikao na makamanda kuwapa mikakati ya ziada ya ushindi. Askari wakiwa vitani walio nyumbani wajibu wao ni kuwapelekea mahitaji, endeleeni kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya M4C. Nimemsikiliza Isaya Mwita Chalres Diwani Mtarajiwa wa Kata ya Vijibweni kupitia CHADEMA, kijana msomi wa shahada ya uchumi mwenye uwezo wa kuwakilisha na kuisimamia serikali kwenye ngazi ya serikali za mitaa katika baraza la madiwani; anahitaji kuungwa mkono zaidi kwa kuwasiliana na timu ya kampeni kupitia 0714225960 au 0756091748 kwa ajili ya maelezo na maelekezo na mnipe mrejesho kupitia mnyika@chadema.or.tz. Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke.


Nimezungumza na wananchi wa Kata ya Vijibweni bila kujali tofauti za vyama, dini, kabila, jinsia na hali zingine wako tayari kwa mabadiliko ya kweli. Matatizo ya mipango miji na migogoro ya ardhi yanawaunganisha. Serikali imevamia katika maeneo yao na kutaka kutwaa ardhi ya ekari zaidi ya 200 bila kuwashirikisha wala kufuata taratibu za kisheria. Aidha, wana mgogoro baina yao na wawekezaji wakubwa wengine yakiwa na makampuni ya kigeni yaliyotwaa ardhi, huku serikali ikishindwa kuwashirikisha na kufanya usimamizi bora wa rasilimali hii muhimu. Wapigakura wanaiamini CHADEMA kuwa ni chama chenye kuweza kuwawakilisha wananchi, kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa. Nimewaomba watupe Diwani Isaya Mwita Chalres awe kiungo kati ya CHADEMA na wananchi wa Vijibweni katika Jimbo la Kigamboni ambalo kwa sasa halina mwakilishi wa kuchaguliwa na wananchi katika ngazi ya kata yoyote kupitia CHADEMA. Nimewapa fursa ya kuuliza maswali, tukawajibu na hatimaye wakapiga kura za wazi za kuchagua mabadiliko na kuwa tayari kuunganisha nguvu ya umma kuhakikisha ushindi; M4C, kwa pamoja tutashinda.

Nimeguswa na wananchi waliotoka maeneo mengine ya jirani na Kata ya Vijibweni ya Pembamnazi, Kisota na Kibada waliokuja baada ya kusikia ningehutubia na kunieleza kuhusu migogoro katika maeneo yao na mashaka yao kuhusu mwelekeo wa mji mpya wa Kigamboni. Maelezo yao yamenirejesha kwenye migogoro ya miaka mingi niliyoikuta ya ardhi katika jimbo la Ubungo mathalani ya Kata ya Kwembe, Kata ya Kibamba na mingine ambayo nimeiwasilisha kwa mamlaka husika na naendelea kuisimamia serikali ipatiwe ufumbuzi. Hivyo, nitaendelea kufuatilia kupata kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni lini atakutana nasi kuhusu migogoro ya ardhi Dar es salaam kwa ujumla na pia kauli ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka ni lini atatembelea jimboni Ubungo kuipatia ufumbuzi migogoro tajwa kwa walivyoniahidi katika Mkutano wa nne wa Bunge mwezi Agosti mwaka 2011. Kukithiri kwa migogoro ya ardhi jijini Dar es salaam ambapo kunachangiwa pamoja na mambo mengine udhaifu katika mipango miji na kukithiri kwa ufisadi katika sekta ya ardhi ni bomu la wakati linalohitaji hatua za haraka. Maslahi ya Umma Kwanza.

Kampeni kuelekea uchaguzi wa Udiwani Kata ya Vijibweni,Temeke

Nikiwa namnadi mgombea wetu wa Udiwani CHADEMA kata ya Vijibweni Ndg.Isaya Mwita Charles
Nikisisitiza kwanini tunahitaji mtuunge mkono ewe mwananchi kuhakikisha kata ya Vijibweni inapata diwani toka CHADEMA. Manispaa ya Temeke ni pekee mkoa wa Dar es Salaam isiyokuwa na Diwani yoyote wa kata wa CHADEMA! Inawezekana....tuungane sasa kuhakikisha anapatikana Ndg. Isaya Mwita Charles anakuwa diwani na kuleta fikra mbadala zenye kuharakisha maendeleo!

Friday, March 23, 2012

M4C: Vijibweni-Halmashauri ya Temeke Jimbo la Kigamboni

M4C: Kwa kipindi cha mwaka mmoja cha utumishi wa umma nimeshuhidia umuhimu wa kuchanganya vyama katika mabaraza ya madiwani katika kuongeza uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma katika serikali za mtaa ambazo ndio zinashughulikia kwa kiwango kikubwa masuala ya maendeleo katika maeneo yetu. Leo jumamosi 24/03 nitahutubia kwenye kampeni za uchaguzi wa udiwani kata ya vijibweni Manispaa ya Temeke Jimbo la Kigamboni. Tuunge mkono kwa kuwasiliana Kilewo 0714225960 au 0756091748 kwa ajili ya maelezo na maelekezo. Tushiriki kufanya mabadiliko tunayoyataka.
Wednesday, March 21, 2012

Soma, Shiriki na Shirikisha na wengine kuwezesha mabadiliko ya kweli

Soma, Shiriki na Shirikisha na wengine: Mabadiliko Arumeru Mashariki (Arusha) na Vijibweni (DSM) yatawezeshwa na wewe, mimi na wenzetu.


Kesi ya uchaguzi wa Ubunge Ubungo imenifanya nishindwe kurudi Arumeru Mashariki mapema kwa kuwa nawajibika kuandaa ushahidi na mashahidi. Kiroho nipo pamoja na makamanda wengine katika mapambano kuhakikisha Nassari anaungana nasi kupunguza hodhi ya chama kimoja bungeni. Katika siku hizi ambazo nalazimika kuwepo DSM, kiakili na kimwili pamoja na kesi na majukumu mengine ya kibunge naelekeza nguvu katika uchaguzi wa udiwani kata ya Vijibweni Jimbo la Kigamboni Manispaa ya Temeke.

Marafiki zangu na wote mnaouniunga mkono mlio Arusha naomba muwezeshe uwepo wangu kiroho kwa kushiriki katika harambee ya kuchangia chama itakayofanyika Naura Spring Hotel tarehe 23 Machi 2012 kuanzia saa 1 Usiku. Wasilianeni na Mwigamba 0784815499 au 0713953761 kwa maelezo na maelekezo. Mkishashiriki mnipe mrejesho kuhusu ushiriki wenu kupitia mnyika@chadema.or.tz ili Mungu akipenda nikija Arumeru Mashariki mwishoni mwa kampeni kuongeza nguvu tuweze kuonana. Hakuna Kulala; Mpaka Kieleweke.

Marafiki zangu na wote mnaoniunga mkono katika Jiji la Dar es salaam naomba mshirikiane nami kwa hali na mali kuhakikisha kwamba Manispaa ya Temeke ambayo ndio pekee katika mkoa wa Dar es salaam isiyokuwa na Diwani yoyote wa kata wa CHADEMA inapata walau mwakilishi mmoja kutoka chama mbadala. Wasilianeni na Kilewo 0714225960 au 0756091748 kwa ajili ya maelezo na maelekezo na mnipe mrejesho kupitia mnyika@chadema.or.tz. Kwa kipindi cha mwaka mmoja cha utumishi wa umma nimeshuhidia umuhimu wa kuchanganya vyama katika mabaraza ya madiwani katika kuongeza uwajibikaji kwenye usimamizi wa fedha za umma katika serikali za mtaa ambazo ndio zinashughulikia kwa kiwango kikubwa masuala ya maendeleo katika maeneo yetu. Tuunganishe nguvu ya umma kuwezesha mabadiliko ya kweli. Shiriki sasa na shirikisha na wengine; Maslahi ya Umma Kwanza.

John Mnyika (Mb), Mkurugenzi wa Habari na Uenezi (CHADEMA)-22/03/2012

Michango kwa ajili ya Barabara ya Maziwa-External Mandela, kifusi sasa; lami itafuata

Kwa watumiaji wa Barabara ya Mkato ya Maziwa mpaka External Barabara ya Mandela; tuunganishe nguvu ya pamoja kuwezesha matengenezo ya dharura ya kuweka kifusi wakati tukiendelea kufuatilia barabara husika ijengwe kwa kiwango cha lami.


Watendaji wa Manispaa ya Kinondoni wametueleza kuwa barabara ya External haiwezi kupitishwa grader kusawazishwa kwa kuwa ina mabaki ya lami; hivyo suluhisho ya muda mfupi linapaswa kuwa ni kuweka kifusi.

Manispaa imekubali kutoa malori kwa ajili ya kubeba kifusi; hata hivyo wameeleza kuwa hakuna bajeti ya kununua na kusambaza kifusi kwa haraka. Jana tarehe 20 Machi 2012 nilimjulisha Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob akutane na kamati ya wananchi iliyoanza jitihada mbalimbali kuangalia nini tunachoweza kufanya kwa kuunganisha nguvu ya umma.

Diwani amenijulisha kwamba gharama zinazohitajika kuweka na kusambaza kifusi ni milioni moja; nimeshampatia 10% ambayo ni sawa na laki moja kazi iendelee. Nawaandikia kuwaomba watumiaji wa Barabara hiyo ambayo ni ya mkato na yenye kupunguza foleni, tuunganishe nguvu za pamoja kukamilisha matengenezo yanayoendelea.

Wasiliana na Diwani 0712239595 kwa ajili ya maelezo na maelekezo ya kuwasilisha mchango wako; ukishaunganisha nguvu yako tafadhali tujulishe kupitia mbungeubungo@gmail.com ili kuhakikisha uwajibikaji.

Mtakumbuka kuwa gazeti la Habari leo la tarehe 18 Machi 2012 katika ukurasa 5 lilikuwa na habari “Wataka Ubungo-Mandela kutengenezwa”, Habari hiyo imeeleza kuwa “Wakazi wa Ubungo katika Manispaa ya Kinondoni, wamemuomba mbunge wa Jimbo hilo John Mnyika, kushughulikia tatizo la Ubovu wa Barabara inayounganisha eneo la Ubungo Maziwa na Barabara ya Mandela ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa kero”.

Kufuatia habari hiyo kwa kazi waliyonipa wananchi ya kuwawakilisha na kuisimamia serikali na vyombo vyake katika kuwezesha maendeleo nilitoa wiki moja kwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutimiza wajibu wa kushughulikia ubovu wa barabara husika.

Nikaeleza kuwa iwapo baada ya wiki moja Manispaa itakuwa haijaanza kuifanyia matengenezo barabara iliyolalamikiwa basi nitachukua hatua za kuunganisha nguvu ya umma kuwezesha matengenezo yanayohitajika.

Kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi kazi za utekelezaji ziko chini ya vyombo vya serikali kuu na serikali za mitaa; kazi ya mbunge ni kuvisimamia vyombo husika kuwezesha maendeleo.

Wananchi wa kata ya Ubungo na maeneo mengine ya Manispaa ya Kinondoni wanalipa kodi na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 kumetengwa fedha za matengenezo ya barabara hivyo ni wajibu wa Manispaa kutumia mafungu hayo kwa haraka kufanya ukarabati au kama Manispaa haina fedha itangaze kufilisika ili vyanzo vingine viweze kutumika.

Hivyo, kama katika kipindi hicho cha wiki moja nilieleza iwapo Manispaa itakuwa haijatoa kauli ya lini matengenezo ya barabara husika yataanza nitawajibika kwa kutumia nafasi yangu ya ubunge kuunganisha wananchi na wadau wa maendeleo katika eneo husika kuweza kuanza kushughulikia ubovu wa barabara husika kwa dharura kwa kutumia vyanzo vingine vya fedha nje ya kodi.

Aidha, wakati tukichukua hatua za dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero , suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami.

Kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.

Niliziandikia mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele vyake na sasa imetengewa fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.

Hivyo, nichukue fursa hii pia kutoa mwito kwa TANROADS kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka huu wa 2012 ili kupata suluhisho la kudumu zaidi la kuondoa kero ya ubovu wa barabara husika na kuchangia katika kupunguza msongamano katika Jimbo la Ubungo.

Aidha, pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External.

Hivyo, ni muhimu watendaji wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao wakaeleza hatua ambayo imefikiwa katika kushughulikia maombi hayo kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Nitumie nafasi hii pia kurudia kutoa mwito kwa Wizara ya Ujenzi kueleza kwa wananchi hatua iliyofikiwa katika kupandisha hadhi barabara za Dar es salaam za kupunguza msongamano na kutumia nyongeza ya mapato iliyopatikana kwenye ushuru wa barabara kuanza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami mwaka huu wa 2012. Maslahi ya Umma Kwanza.

Sunday, March 18, 2012

WIKI YA MADAI YA MAJI

Mwito wa kushiriki wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii:

Nimerejea toka Afrika Kusini nilipokuwa kikazi na kukuta Wizara ya Maji imezindua maadhimisho ya Wiki ya Maji kuanzia tarehe 16 Machi na kilele kitakuwa Siku ya Kimataifa ya Maji tarehe 22 Machi 2012.

Ujumbe wa mwaka huu ni “Maji na Usalama wa Chakula”, hata hivyo tunahimizwa kuadhimisha ujumbe mpya bila kuelezwa matokeo ya ujumbe wa mwaka mmoja uliopita wa “Maji kwa ajili ya Miji: Kukabiliana na changamoto mbalimbali mijini”.

Kazi ya wabunge na bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika kuwezesha maendeleo kwa kutumia rasilimali za umma na za wadau wengine.

Kwa nafasi hiyo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo na wa Jiji la Dar es salaam kwa ujumla kwamba badala ya kuadhimisha sherehe za maji bila ya maji kila mmoja ashiriki kwa namna mbalimbali katika Wiki ya Madai ya Maji.

Kila mmoja anaweza kushiriki kwenye wiki hii ya madai ya maji kwa njia mbalimbali, njia mojawapo ambayo natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuitumia ni kushiriki madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii kwa kuandika barua pepe kwa bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA) kuitaka ifanye kazi ipasavyo ya kuharakisha upatikanaji wa maji kwa mujibu wa sheria, kanuni, mipango na mikataba.

Waandikie wajumbe wa bodi ya DAWASA madai ambayo unataka wayafanyie kazi katika eneo lako na nakala ya barua pepe hiyo kuituma kwa mbungeubungo@gmail.com kwa ajili za hatua zaidi za kibunge za uwakilishi na usimamizi.

Bodi ya DAWASA ni kama ifuatavyo: Mwenyekiti Dr. Hawa E. Sinare(e.sinare@rexattorneys.co.tz), Makamu Mwenyekiti-Alhaj Said H. El-Maamry-elmaamry@cats-net.com, wajumbe: Bw. Laston Msongole (lmsongole@mof.go.tz), Bi. Mary Mbowe (mrymboowe@yahoo.co.uk) , Bi. Christine Kilindu(christinekilindu@cti.co.tz), Bw. Daniel Machemba (dmachemba@tccia.com, dmachemba@gmail.com), Alhaj Bakari Kingobi (brmkingobi@yahoo.com), . Mary G. Musira(drtc@cats-net.com), B. Florence S. Yamat (yamatf@dawasa.co.tz), Mh. Amina N. Mkilagi (Mb), Mhandisi. Archard Mutalemwa-Afisa Mtendaji Mkuu (dawasaceo@dawasa.co.tz).

Tuungane pamoja kutaka serikali kuu na serikali za mitaa zitumie wiki hiyo kutoa maelezo kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza miradi ya maji na pia kuharakisha uzinduzi wa miradi ilicheleweshwa.

Njia hii ya kuunganisha nguvu ya umma kwa kutumia TEHAMA (SMS, facebook, twitter, email na njia nyingine) tuliitumia tarehe 1 Disemba 2011 wakati wa kuhamasisha umma kushiriki mkutano wa wadau uliotishwa na EWURA kuhusu ombi la TANESCO kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu ya bei iliyokuwepo).

Hatimaye umeme ulipandishwa lakini si kwa kiwango hicho cha awali bali kwa wastani wa 40% kwa kuzingatia pia viwango vya utumiaji. (Suala la Umeme nimeanza kuchukua hatua zingine kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kutokana na matatizo yanayoendelea kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa umeme na nitatoa kauli kuhusu mgawo wa umeme unaoendelea kinyemela).

Izingatiwe kuwa nilipanga kwenye wiki hii ya madai ya maji kuunganisha nguvu ya umma kwa kuwaongoza wananchi kukutana na serikali na mamlaka nyingine zinazohusika hata hivyo itabidi kutumia njia mbadala za kuwasilisha madai.

Hii ni kwa sababu kuanzia kesho tarehe 19 Machi 2012 nitakuwa mfululizo mahakamani kwenye kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Ubungo wa mwaka 2010. Hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea nitaendelea kutumia njia nyingine za kibunge kuchukua hatua kuhusu masuala ya maji lakini natoa mwito kwa wananchi nanyi kwa upande wenu kila mmoja kuchukua hatua zinazowezekana katika wiki hii ya madai ya ya maji. Umoja ni Nguvu.

Maadhimisho ya Wiki ya Maji bila ya Maji

Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji kuwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Uchakavu na wa miundombinu kutokana na mabomba kutokarabatiwa ipasavyo pamoja na uharibifu katika mitandao ya maji wa kujiunganishia kinyemela na kiholela umesababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji mpaka kufikia kati ya asilimia 40 hadi 45.

Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni asilimia 18 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa kama Sinza mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Katika muktadha huo hakuna sababu ya kusherekea wiki ya maji bila maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla hivyo Wizara ya Maji na mamlaka nyingine husika zitumie wiki hii kutoa majibu ya msingi kwa wananchi kuhusu namna ambavyo wataongeza kasi ya kushughulikia kero ya maji.

Itakumbukwa kwamba akihutubia Bunge mwezi Juni mwaka 2010 wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka wa fedha 2010/11 Waziri Mark Mwandosya aliahidi kwamba usanifu wa bwawa la Kidunda linatarajiwa kutoa mchango mkubwa wa utatuzi wa kero ya maji kwa wananchi wa Ubungo lingekamilika mwezi Septemba mwaka huo wa 2010; lakini mwezi Machi 2011 Waziri Mwandosya kauli tofauti kuwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa hilo utakamilika mwezi Juni mwaka 2011 na ujenzi mwaka 2013.

Kwa sababu hiyo, ni muhimu kuendelea kuwasilisha madai ili taratibu zote za msingi zikakamilishwa mwaka huu wa 2012 kwa haraka; hivyo pamoja na kutenga bilioni sita kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa ajili ya ulipaji fidia iongeze fedha kwa ajili ya ujenzi kuanza. Maamuzi haya yafanyike pia kuhusu kuharakisha upanuzi wa Bomba la Ruvu Chini na ujenzi wa bomba jipya toka Ruvu Juu kama Serikali ilivyoahidi bungeni wakati wa kujibu swali langu la msingi tarehe 13 Aprili 2011.

Aidha, DAWASA ambayo ndiyo mamlaka yenye dhamana ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam ieleze ni lini maeneo ya pembezoni yenye mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina hususani ya Kimara Bonyokwa, King’ong’o, Mbezi kwa Msuguri, Malambamawili yataanza kutoa maji.

Kama hatua za dharura, DAWASA iharakishe kukamilisha uchimbaji wa visima virefu nane vyenye kuweza kuhudumia kwa ujumla wakazi zaidi ya elfu thelathini wa Kimara Mavurunza, Bonyokwa, Kilungule na King’ong’o kama ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Mei mwaka 2010.

Visima hivi ni suluhisho la dharura wakati tukiendelea kufuatilia suluhisho la kudumu linalopaswa kuhusisha pamoja na mambo mengine kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikataba, kudhibiti ufisadi unaofanywa katika mtandao ikiwemo kukabiliana na upotevu wa maji unaondelea na kupanua miundombinu.

DAWASA ieleze pia mpango ilionao wa kumalizia maeneo ambayo hayakufikiwa na mtandao wa mabomba ya maji hususani ya pembezoni ya Saranga, Makoka, Msakuzi, Kibamba, Kwembe, Msakuzi, Goba, Mpiji Magohe, Makabe, Msumi, Kilungule nk.

Kwanini madai ya sasa ya maji yaelekezwe DAWASA kwa niaba ya Serikali?

Ni muhimu ikazingatiwa kuwa kwa mujibu wa katiba ibara ya 8 mamlaka na madaraka yote ni ya umma, serikali na vyombo vyake vinafanya kazi kwa niaba; hivyo wiki hii ya madai ya maji iwezeshe kuongeza msukumo katika kazi za kuboresha upatikanaji wa maji kwa njia mbalimbali.

Njia mojawapo ni pamoja na kuwasilisha madai ya mamlaka husika na kutaka majibu kuhusu kazi ambazo zinafanyika na katika wiki hii ya madai ya maji, pamoja na kuwa wahusika wa masuala ya maji ni wengi kwenye sekta ya umma na sekta binafsi; ni muhimu nguvu zielekezwe kwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASA).

Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya DAWASA (Dar es salaam Water and Sewerage Authority Act no.20 of 2001) kifungu cha 22 DAWASA ndio chombo kikuu cha utekelezaji wa mipango na sera za serikali kuhusiana na maji, ugavi wa maji, huduma za maji taka na uhifadhi wa maji katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla.

Tarehe 1 Julai 2005 DAWASA ilitoa mkataba wa ukodishaji (lease agreement) kwa DAWASCO ambao unaitaka DAWASCO kuendesha miundombinu ya maji na kuhakikisha matengenezo ya mtandao wa maji katika jiji la Dar es salaam.

Hata hivyo, uhusiano wa DAWASA na DAWASCO ni kama wa mwenye duka na muuza duka; ambao kunaweza kuwa na matatizo ya muuza duka lakini lakini panaweza kuwa na matatizo ya uhaba wa bidhaa na duka lenyewe ambayo kimsingi yanamhusu mwenye duka.

Hivyo, katika wiki hii ya madai ya maji nguvu zielekezwe kwenye kuisimamia DAWASA ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha sheria tajwa inatumia kodi za wananchi wote ikiwemo ambao hawapati huduma ya maji toka kwao na pia tozo za wateja wanaopata maji kwa mgawo, hivyo DAWASA inawajibika kuhakikisha huduma zinapatikana kwa kuzingatia sheria, kanuni, mikataba na mipango.

Bodi ya DAWASA inapaswa kwa kuzingatia mamlaka yake kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Sheria tajwa na majukumu mengine ya DAWASA kwa kurejea vifungu vya 6, 7 na 8 vya sheria husika kuhakikisha huduma ya maji safi na maji taka inapatikana kwa wananchi.

Mtakumbuka kwamba Machi Mosi 2012 niliungana na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) katika kata saba Jimboni Ubungo kwenye kazi za kuboresha upatikanaji wa maji.

Tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na wanahabari na kutaka hatua za ziada kuchukuliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) na Wizara ya Maji.

Nashukuru kwa hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na DAWASCO na EWURA katika masuala kadhaa; hata hivyo sijaridhika na namna ambavyo DAWASA na Wizara ya Maji wanavyoshughulikia masuala ya maji katika maeneo mengi; hivyo wiki ya madai ya maji kupitia mitandao ya kijamii itumike kuongeza msukumo wa umma kabla ya kuchukua hatua zaidi za kibunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 10 Aprili 2012.

John Mnyika (Mb)

Jimbo la Ubungo

18/03/2012

Friday, March 9, 2012

Mamlaka ya Urais yawezeshe uwajibikaji kumaliza mgogoro wa Serikali na Madaktari

Jana tarehe 8 Machi 2012 asubuhi nilitoa tamko kwa niaba ya CHADEMA la kutaka kauli ya haraka ya Rais Jakaya Kikwete ya kutengua uteuzi wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hadji Mponda na Naibu Waziri wa wizara husika Dk. Lucy Nkya kutokana na udhaifu wao mkubwa wa kiongozi waliouonyesha katika kushughulikia mgogoro wa madaktari ambao umedumu kwa muda wa takribani miezi miwili.

Nilieleza kusitikitishwa na ukweli kwamba Rais Kikwete toka mgogoro utokee hajatumia ipasavyo mamlaka yake ya kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 34 na 35 na tarehe 5 Februari 2012 aliahidi kwamba atazungumzia kwa kina suala la mgomo wa madaktari lakini badala yake akalizungumza kwa ufupi tarehe 29 Februari 2012 katika hotuba yake kwa taifa bila kuchukua hatua za msingi hali inayoashiria ombwe la uongozi.

Nilieleza kuwa iwapo Rais Kikwete haitatoa kauli viongozi wakuu wa CHADEMA wataeleza hatua za ziada ambazo chama kitachukua kuiwajibisha serikali. Jioni Serikali ilieleza kuwa leo Rais angezungumza na wazee wa Dar es salaam, na leo imetolewa taarifa kuwa atazungumza nao kesho.

Jana usiku na leo asubuhi masuala kadhaa yameendelea kuhusu mgogoro huu, mosi; hukumu ya mahakama ya kazi, pili; uamuzi wa serikali na wadau wake kufanya propaganda dhidi ya madaktari tatu; uamuzi wa serikali kufanya mawasiliano na uongozi wa madaktari.

Friday, March 2, 2012

DAWASCO kufuata ratiba ya mgawo, ndani ya wiki moja DAWASA, EWURA na TANESCO nao wachukue hatua

Kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali na vyombo vyake kuwezesha maendeleo. Naomba niwape mrejesho kwa muktasari; Machi Mosi tulikuwa pamoja na DAWASCO kwenye kata za Sinza, Makurumla, Mburahati, Msigani, Mabibo, Saranga, Kwembe na Makuburi tukifanya kazi za kuboresha upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Itakumbukwa kwamba Septemba 2011 baada ya kwenda DAWASCO na wananchi maji yalianza kupatikana kwa kuzingatia ratiba ya mgawo kwenye maeneo zaidi ambayo hapo awali yalikuwa hayapati mgawo; hata hivyo mara baada ya mafuriko ya Disemba kisingizio cha kuharibika kwa miundombinu kikafanya ratiba husika kutokuzingatiwa kwa mwezi mzima wa Januari na mwezi Februari; hali ambayo ilirejesha kwa kiwango kikubwa pia biashara ya kinyemela ya maji.

Baada ya kuchukua hatua ikiwemo kuiandikia DAWASCO tarehe 14 na hatimaye kuwapa muda siku tatu kutoa majibu kwa umma DAWASCO ilieleza kuwa pamoja na mafuriko ratiba ya mgawo kwenye maeneo kadhaa ya Dar es salaam ilishindwa kuzingatiwa kutopata umeme wa uhakika kwenye mitambo yao ya Ruvu na pia kuharibika kwa pampu moja Ruvu Juu.

Tuliendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na hatimaye DAWASCO ilikamilisha matengenezo ya pampu husika hata hivyo bado kuna maeneo ambayo yalishindwa kupata mgawo kutokana hujuma katika miundombinu zikiwemo za mitandao haramu ya maji katika maeneo mbalimbali.