Saturday, September 3, 2011

Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje; mchango wangu bungeni

MKUTANO WA NNE-Kikao cha Thelathini na Moja – Tarehe 22 Julai, 2011

JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ina umuhimu wa pekee sana wakati huu dunia iko kwenye mwelekeo wa ubeberu na ubepari, hivyo iongezwe fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya kulinda maslahi ya Taifa Kimataifa.


Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kazi yake, inahitajika kufanyike mabadiliko ya kisheria na kitaasisi ili kuweka mkazo katika diplomasia ya uchumi na usalama.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kitabu cha bajeti, Volume II, Fungu 34; Wizara ieleze sababu za kupanda kwa Kasma 220800 Kifungu 1002, hizi zimepanda kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na mwaka 2010/2011 na 2011/2012. Kifungu 2006 ielezwe hatua zilizochukuliwa kurekebisha ongezeko la matumizi ya zaidi ya 832 milioni nje ya bajeti iliyopitishwa na Bunge (Ubalozi wetu London). Kifungu 2009- hatua za kumaliza masuala ya nyuma yaliyotolewa na CAG ya takribani 451 milioni kuhusu Ubalozi wetu Moscow. Hatua zilizochukuliwa kurekebisha kasoro za mawasiliano na sekta mbalimbali kuwezesha utekelezaji wa miradi inayodhaminiwa na Serikali ya China na Taasisi/Makampuni yake, hii ifanyike kwa kutumia vizuri rasilimali zilizotengwa kwenye Kifungu 2014. Kifungu 2027; hatua zilizochukuliwa kushughulikia kasoro ya milioni 865 kutumiwa bila idhini.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Volume IV, Fungu 34, Kifungu 1604, Kasma 6391, kwenye utekelezaji 2009/2010, 2010/2011 na malengo 2011/2012, napenda kujua hatua zilizochukuliwa kwa Ubalozi wetu Kigali kulipa nyumba miezi saba bila kutumika, ukarabati wa Ubalozi wetu Nairobi na ujenzi kwenye kiwanja Upper Hill.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya kulinda maslahi ya kiuchumi ya nchi yetu,
mkazo uwekwe kwenye Balozi za nchi ambazo tuna maslahi mengi ya kiuchumi kwa 87 kurejea Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano. Aidha, safari za nje za viongozi zipunguzwe ukubwa wa misafara na idadi ili kuweka mkazo kwenye safari zenye tija. Haiwezekani kwa safari zote kati ya 2005-2010 kwa kisingizio cha kutafuta wawekezaji halafu tumeshindwa kuweka mstari wa mbele kuondoa kero ya umeme na upatikanaji wa gesi asilia.


Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ijikite katika kuepusha uongozi wetu kutumiwa
na makuwadi wa kiuchumi bila maslahi ya Taifa na rasilimali zake kulindwa kwa
kiwango cha kutosha hususani kwenye ardhi, madini, gesi n.k Kampuni kama Good Works International zichunguzwe kwa ajili ya maslahi ya umma.


Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ishirikiane na Wizara ya Afya, NSSF na balozi wa India kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Apollo.


Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza ushiriki wa Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kwenye maendeleo; Wizara ishirikiane na mamlaka nyingine
kuhakikisha inafanyika sensa rasmi.


Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya kiusalama yapewe kipaumbele katika kazi
za Wizara. Serikali itoe kauli kuhusu malalamiko ya Askari wa Tanzania katika vikosi vya kuleta amani vya UN hususani nchini Lebanon na Sudan (Darfur). Malalamiko hayo yanahusisha kuchelewa kwa mishahara na kupelekewa malipo pungufu ya mikataba. Malalamiko hayo yameshaandikwa kwa Rais na Waziri wa Ulinzi badala ya haki zao kulindwa, wameandikiwa Waraka toka Makao Makuu ya Jeshi wa kuwatishia kuwa watarudishwa na kufukuzwa kazi. Ni muhimu Wizara ya Mambo ya Nje ikaingilia kati ili kuhakikisha masharti yote na stahili zote zilizomo kwenye mikataba ya kulinda amani baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa UN yanatekelezwa.


Aidha, kwa ajili ya kusafisha taswira ya Tanzania Kimataifa, ni vizuri Serikali ikatoa kauli ya hatua ambazo imechukua kuhusu tuhuma za baadhi ya Watanzania kuhusika na biashara ya silaha haramu. Mathalani Ripoti ya Timu ya Wataalamu wa Baraza la Usalama la UN ya tarehe 26 Januari 2006. Pia mkataba wa tarehe 17 Agosti 1997 kati ya Kampuni ya Executive Outcomes Inc. na Tanzania kwenye mradi wa madini kupitia mradi wa Meremeta, suala ambalo limehusishwa na usafirishwaji wa silaha haramu Congo (DRC) kati ya 1997 mpaka 2007.


JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kupitia kifungu hiki cha Mshahara wa Waziri, ningeomba kupata ufafanuzi kuhusu jambo moja
la Kisera. Ninaelewa kwamba, jukumu mojawapo la Kisera la Wizara hii ni kujenga taswira pana ya nchi yetu Kimataifa. Sasa kuna suala mahususi ambalo nililiuliza kuhusiana na tuhuma juu ya Watanzania kushiriki kwenye masuala ya uuzaji wa silaha haramu ambazo zinachafua taswira ya nchi yetu.


Ninaelewa kwamba, Mheshimiwa Membe, analifahamu jambo hili, kwa sababu
mwaka 2000 lilijadiliwa kwenye Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa na mwaka wa 2006 lilijadiliwa vilevile Umoja wa Mataifa. Sasa ningependa kupata kauli ili tusichafuke kama Watanzania, kwa sababu ya matendo ya watu binafsi kuhusiana na tuhuma hizi hususan tuhuma zinazoihusu Kampuni ya Meremeta, kwa sababu wengi wamezoea kufikiria kwamba, ilikuwa ni kashfa sijui ya utoroshaji wa madini peke yake na ufisadi wa pesa za Watanzania shilingi bilioni 100, lakini kuna tuhuma nzito vilevile za kuhusiana na utoroshaji wa silaha. Kwa hiyo, ninaomba ufafanuzi kuhusu hilo.


WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi kabisa kusema kwamba, Watanzania na hasa Wizara yetu, wanayo haja ya kujua nini kinachoendelea na kuthibitisha madai mbalimbali yanayotolewa kama hili ambalo limetolewa na Mheshimiwa Mnyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala alilolisema Mheshimiwa John Mnyika ni zito,
linastahili kutoa majibu ya uhakika na nilivyojiandaa leo katika shughuli hizi, suala la silaha na suala la Meremeta, halikuwepo kwenye vocabulary yangu. Tunaomba suala hili tulitafutie muda ili tuweze pengine kulitolea majibu, sitaweza kutoa majibu ya haraka haraka kwa swali zito.

MWENYEKITI: Ahsante

Friday, September 2, 2011

Kuhusu kukatwa maji Goba

Taarifa kuhusu kukatwa maji kata ya Goba na tuhuma za kamati ‘kutafuna’ m 18

Naomba kutoa taarifa ya awali kuhusu ufuatiliaji ambao nimeufanya na hatua ambazo nakusudia kuzichukua kuhusu maji kukatwa katika kata ya Goba na tuhuma juu ya kamati ya maji Goba ‘kutafuna’ kiasi cha shilingi milioni 18 zilizotolewa tarehe 28 Agosti 2011 na hivyo kulimbikiza deni la kiwango hicho DAWASCO.

Mara baada ya kuingia ofisini tarehe 29 na 30 Agosti 2011 nimefuatilia na kubaini kwamba maji yamekatwa kwenye kata ya Goba kutokana na DAWASCO kuidai kamati ya mradi wa maji shilingi 18,108,478. Aidha, katika kufuatilia deni hilo nimepata taarifa za Kamati ya Maji kuwasilisha malalamiko DAWASCO ya kutokukubaliana na kiwango hicho cha deni na pia kwa Manispaa ya Kinondoni kuhusu matatizo ya kiutendaji na kifedha katika mradi huo wa maji ikiwemo ya upotevu wa fedha.

Naomba kutoa taarifa kwamba katika ufuatiliaji wangu nimebaini kwamba Matatizo ya Maji katika Kata ya Goba kama ilivyo katika kata zingine katika Jimbo la Ubungo na Mkoa wa Dar es salaam kwa ujumla yanatokana na matatizo ya kimfumo, kiuongozi, kifedha na kiutendaji yanayosababishwa na Kamati ya mradi wa Maji Goba, DAWASCO, DAWASA, Halmashauri za Jiji la Dar es salaam na Wizara ya Maji ambayo nimekuwa nikiipa taarifa na kutaka iingilie kati kwa nyakati mbalimbali.

Ikumbukwe kwamba tarehe 31 Januari 2011 niliitisha Kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo na kuwaweka pamoja wananchi pamoja na wadau wa msingi ili kuunganisha nguvu ya pamoja kukabiliana na matatizo mbalimbali ikiwemo la maji katika kata ya Goba ambalo mgogoro katika kamati ya mradi umedumu kwa zaidi ya miaka mitano. Pamoja na kuwasilisha ripoti ya kongamano husika wa DAWASCO, DAWASA, Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Maji hatua muhimu kuhusu matatizo katika mradi wa maji Goba na maeneo mengine hazikuchuliwa kwa wakati.

Ili kuweza kuzisukuma mamlaka husika kutimiza wajibu tarehe 27 Februari 2011 nilifanya mkutano na wananchi ambapo risala ya wananchi pamoja na ripoti ya ukaguzi wa mradi wa mradi wa maji Goba ya mwaka 2007 zilizosomwa ambazo zilieleza bayana matatizo yaliyokuwepo kwenye kamati ya maji pamoja na mradi kwa ujumla ikiwemo yaliyohusu upotevu wa fedha. Maazimio mbalimbali yalifikiwa ikiwemo ya kuitishwa kwa mkutano wa watumiaji wa maji kwa ajili ya kuvunja kamati iliyokuwepo na kuunda kamati mpya. Tarehe 6 Machi 2011 nilishiriki mkutano wa watumiaji Goba ulioitishwa na diwani na mtendaji wa kata ambao wananchi walifikia uamuzi wa kuvunja kamati ya awali na kuunda kamati mpya. Pamoja na kuundwa kwa kamati hiyo nilibaini matatizo ya mradi yaliyoendelea hivyo tarehe 21 Machi 2011 nilimuandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni barua yenye kumb.na. OMU/MJ/005/2011 kumtaarifu kuchukua hatua za haraka kuhusu mradi wa maji Goba ikiwemo kukutana na kamati husika. Hata hivyo, toka wakati huo Manispaa ya Kinondoni ambayo ndiyo yenye mradi kwa mujibu wa sheria haikuchukua hatua zinazostahili. Hivyo; tarehe 2 Septemba 2011 nitachukua hatua za ziada za kukutana na meya, mkurugenzi na uongozi mwingine wa manispaa ili kuweza kuchukua hatua za haraka kuhusu tuhuma zilizotolewa, kuhakikisha madeni yanalipwa kwa wakati na huduma ya maji inarejeshwa kwa wananchi.

Tarehe 1 Juni 2011 niliandika barua kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) yenye kumbu. Na. OMU/MJ/007/2011 ya kutaka kupatiwa maelezo kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa kushughulikia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Ubungo toka Kongamano la Maji na toka niwasilishe taarifa kwa mamlaka husika tarehe 15 Machi 2011.

Katika barua hiyo nilitaka hatua pia kuhusiana na mradi wa maji Goba kwa kuwa pamoja na kuwa mradi kuwa chini ya Manispaa ya Kinondoni na Kamati ya wananchi kutokana na malalamiko ya muda mrefu ambayo yamehusisha pia tuhuma dhidi ya watendaji wa DAWASCO kuhusu uharibifu wa mita na ufisadi uliofanyika kati ya mwaka 2005 mpaka 2010.

Katika barua hiyo nilitaka pia DAWASCO na DAWASA wafanyie kazi pendekezo la eneo husika kuhudumiwa moja kwa moja na DAWASCO kutokana na ongezeko kubwa la watu na pia mradi wa sasa kununua maji toka DAWASCO na kuwauzia maji wananchi kwa bei kubwa zaidi. Hivyo, iwapo DAWASCO isipotoa majibu ifikapo tarehe 3 Septemba 2011 ikiwemo kuhusu malalamiko juu ya deni la maji katika kata ya Goba nitawaongoza wananchi wa kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo kwenda makao makuu ya DAWASCO wiki ijayo ili kuunganisha nguvu ya umma hatua za haraka zaidi ziweze kuchukuliwa.

Ni muhimu mamlaka husika zikazingatia kwamba Kamati ya Maji Goba haikuridhika na kiwango cha deni hilo kwa kuwa tarehe 9 Agosti 2011 iliwasilisha malalamiko kwa Meneja wa DAWASCO Kawe kutokana na mabadiliko ya ghafla ya kupanda kwa Ankara za Maji kutoka Tshs. 1,761,967 ya kipindi cha Februari 2011 kufikia 18,108,478 mwezi Julai.

Katika Barua hiyo Kamati ya Maji Goba ilimtaka meneja au wataalamu wake kufanya ukaguzi wa mwenendo wa mita ili kuweza kupunguza kiwango hicho cha deni. Kamati ya Maji Goba imetoa maelezo kwamba tarehe 8 Machi 2011 kamati mpya ilipoanza kazi mita hiyo namba 090080215 ilisoma Qm 8210 (kwa miezi tisa) lakini ghafla toka Machi mpaka Juni 2011 ikasoma Qm 11,954 (kwa miezi minne) na Juni mpaka Julai Qm 12,212 (mwezi mmoja). Pia, kamati ya Maji Goba iliileza DAWASCO kuwa katika siku 154 ambazo kamati imefanya kazi haikuweza kupeleka maji kwa wananchi katika siku zote kutokana na kupasuka kwa mara kwa mara kwa bomba kuu la DAWASCO, mgawo wa kitaifa wa umeme na kukatwa mara kwa mara kwa umeme katika eneo la Tanki Bovu kutokana na kuhamishwa mtandao wa umeme kupisha ujenzi wa Barabara Kuu ya Bagamoyo. Hivyo, katika kipindi husika wametoa maji kwa takribani siku 70 kwa wastani wa saa 7 mpaka 9 kwa siku hali ambayo inajenga mashaka ya ziada ya kamati kwamba kiwango hicho cha deni la milioni 18 hakilingani na matumizi halisi ya maji ambayo mradi umeyatumia.

Kuwa upande mwingine, nyaraka za kiofisi zinaonyesha kwamba Kamati ya Maji Goba iliwahi kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe 22 Mei 2011 ambayo haikufanyiwa kazi yenye kueleza matatizo katika uendeshaji wa mradi ambayo yalihitaji Halmashauri kuingilia kati kwa kuwa kimsingi eneo hilo la Goba linahudumiwa na mradi ulio chini ya Manispaa pamoja na kupata maji kutoka DAWASCO.
Kamati ya Maji Goba ililalamika kutokupata ushirikiano toka kwa uongozi wa kata hususani Diwani na Afisa Mtendaji na kueleza mgogoro uliokuwepo miongoni mwa baadhi wajumbe wa kamati. Mgogoro huo ni pamoja na mvutano kuhusu utaratibu wa ukusanyaji na matumizi ya fedha za mradi kati ya mweka hazina wa kamati na viongozi wengine katika kamati husika. Kutokana na hali hiyo Mhandisi wa Maji wa Manispaa kwa niaba ya Mkurugenzi alimsimamisha katika nafasi hiyo mweka hazina na kaimu mweka hazina akateuliwa lakini Afisa Mtendaji akakataa hali ambayo ilifanya mradi kuwa na watunza fedha wawili hali ambayo inaelezwa kusababisha upotevu wa fedha.

Kufuatia hali hiyo Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ilimuita mkaguzi wa ndani ya manispaa kufanya ukaguzi ambao mpaka sasa taarifa yake haijatolewa. Aidha, WDC pia uliunda kamati ya kufuatilia mfumo mzima wa uendeshaji wa mradi iliyoanza tarehe 2 Juni 2011 lakini mpaka sasa taarifa yake haijatolewa. Kamati ya Maji Goba iliandika barua kwa mtendaji wa kata kuomba kikao cha wananchi tarehe 12 Juni 2011 ili kuweza kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa mujibu wa muongozo hata hivyo kamati ilizuiwa kufanya mkutano wa wananchi mpaka kwanza uchunguzi uweze kukamilika.

Itakumbukwa kwamba Gazeti la Tanzania Daima toleo la tarehe 29 Agosti 2011 lilikuwa na habari yenye kueleza kwamba Kamati ya Maji kata ya Goba katika Manispaa ya Kinondoni inatuhumiwa ‘kutafuna’ kiasi cha shilingi milioni 18.

Habari hiyo imeeleza kwamba kukosekana kwa kiwango hicho cha fedha kumesababisha Ankara ya maji ya mradi wa maji Goba inayodaiwa na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) kufikia deni la shilingi milioni 18 na hivyo DAWASCO kuwakatia maji wananchi wa kata ya Goba na maeneo jirani yanayohudumiwa na mradi huo wa maji.

Habari hiyo imenukuu kauli yangu niliyohojiwa kwa simu nikiwa njiani kutoka bungeni Dodoma kuwa nitafuatilia chanzo cha matatizo hayo na nitachukua hatua pindi nikifika Dar es salaam; taarifa hii ya awali ni sehemu ya kutimiza wajibu huo na nitatoa taarifa ya ziada baada ya kuchukua hatua zaidi.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Dar es salaam-01/09/2011