Friday, June 30, 2017

MUHIMU: Nini maoni yako juu ya miswada iliyowasilishwa kwa hati ya dharura


MUHIMU:

Nawaomba wananchi wenye maoni/maboresho juu ya miswada (rasilimali+madini) iliyowasilishwa bungeni wanitumie kwa:

mbungekibamba@gmail.com‬

ISOME kupitia link hii: http://parliament.go.tz

John John Mnyika,
Waziri Kivuli-Nishati na Madini,
Mbunge wa Jimbo la Kibamba


Monday, June 5, 2017

TANZIA: Mzee Philemon Ndesamburo


04 Juni, 2017: Niliweza kuwasili salama Moshi, KDC nyumbani kwa Mzee wetu Philemon Ndesamburo tayari kwa ajili ya shughuli ya kumpumzisha Mzee. Nikisaini kitabu cha maombolezo. 

Mwenyezi Mungu amjalie pumziko jema la milele.

John John MNYIKA,
Mbunge-Jimbo la Kibamba,
Moshi, Juni 05, 2017

Friday, June 2, 2017

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA JOHN JOHN MNYIKA (MB), KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2016/2017 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/ 2018

(Inatolewa chini ya 99(9) ya kanuni za Bunge, Toleo la Mwaka, 2016)
  1. A. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Awali ya yote niungane na wenye mapenzi mema katika kuomba ulinzi wa mwenyezi Mungu wakati wa kutimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuishauri na kuisimamia Serikali kwa Wizara ya Nishati na Madini juu ya bajeti ya mwaka 2016/2017 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, nitumie fursa hii kuwatakia waislamu wote mfungo mwema katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Spika, Nitambue mchango Mheshimiwa John Heche, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini alioutoa katika maandalizi ya hotuba hii. Aidha tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kupona na kurejea katika utekelezaji wa majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa familia ya marehemu Mzee Philemon Ndesamburo, wanachama wa CHADEMA kote nchini, wananchi wa Moshi Mjini, wabunge na watanzania wote walioguswa na msiba huu. Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake kama mmoja wa waasisi wa chama chetu, Mbunge Mstaafu na Mfanyabiashara Mashuhuri. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema.

  1. B. MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA MADINI, MAFUTA NA GESI ASILIA

Mheshimiwa Spika, Novemba 4, 2016 Mheshimiwa Rais alipokuwa akizungumza na watanzania kupitia vyombo vya habari, ikulu jijini Dar es salaam alinukuliwa akisema hakuwahi kuzungumzia katiba mpya wakati wa kampeni zake, kwa hiyo siyo kipaumbele chake na kwamba anachotaka kwanza ni kunyoosha nchi.