Thursday, March 25, 2010

Tamko letu kuhusu ajali ya leo Kata ya Kibamba Wilaya ya Kinondoni

Taarifa kwa Umma: Kwa niaba ya Uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam; natuma salamu za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa wote kufuatia ajali mbaya iliyotokea leo asubuhi Kibamba jijini Dar es salaam ikihusisha Lori la Mafuta na Hiece iliyokuwa na abiria.

Aidha tunatoa mwito kwa serikali na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya ajali za mara kwa mara katika eneo la Kibamba ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Ikumbukwe kuwa mwezi Disemba mwaka 2007 ajali nyingine ilitokea eneo la Kibamba Hospital ikihusisha malori na kusababisha vifo vya watu saba akiwemo mjamzito na wengine 11 kujeruhiwa.

Aidha mwezi Aprili 2008 Bunge jumla ya watu 181 wamepoteza maisha kwa kugongwa na magari kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2007 katika eneo la kuanzia Kibamba mpaka Ubungo kwenye mataa.

Ikumbukwe kuwa Mei 2009 madereva wawili walikufa baada ya magari yao kugongana uso kwa uso huko maeneo hayo hayo ya Kibamba.
Itakumbukwa pia kwamba mwezi Januari 2010 watu 18 walijeruhiwa vibaya katika ajali ya gari iliyotokea katika barabara ya Morogoro eneo la Kibamba Darajani (barabara ina mteremko kuelekea darajani) ambapo magari matano yaligongana kwa pamoja.

Imetolewa tarehe 25 Machi 2010:

John Mnyika-0754694553; mnyika@chadema.or.tz
Mwenyekiti wa Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum (CHADEMA)

Saturday, March 20, 2010

Natangaza rasmi dhamira ya kugombea ubunge 2010

Ni wakati wa mabadiliko ya kweli; tuwajibike

Utangulizi

Wapendwa wananchi wezangu na marafiki zangu ndani na nje ya jimbo la Ubungo. Ninayofuraha kuwatangazia rasmi dhamira yangu ya kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Nimefikia uamuzi huu baada ya kusikia maoni ya wengi wenu na kuisikiliza pia nafsi yangu katika kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka 2009 mpaka mwanzoni mwa mwaka 2010. Wakati wa kampeni bado, hivyo sitazungumzia kwa sasa ahadi zangu kwenu wala ilani ya chama; lakini inatosha kuwaambia tu kwamba: ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike. Naamini katika kuwa na uongozi bora wenye dira na uadilifu wa kuwezesha uwajibikaji katika kusimamia rasilimali za umma ikiwemo kodi zetu na mali asili za nchi yetu kwa ajili ya kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote.


Nautambua wajibu; tushirikiane

Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu).

Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.

Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.

Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria unaosubiriwa kutungiwa kanuni. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.

Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii.

Nilisema wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, na narudia leo. Kipaumbele cha wananchi wa Jimbo la Ubungo ni kupata mbunge mkweli, mwadilifu, mwajibikaji, mwenye dira, atayewasilikiliza na kuwawakilisha ipasavyo. Iwe ni wananchi wa Kwembe, Mloganzila na maeneo mengine yenye migogoro ya ardhi. Ama wale wa Saranga, Baruti na kwingineko kwenye matatizo ya maji huku mabomba makubwa ya maji yakipita jimboni na uwepo wa Chuo cha Maji, na Wizara ya Maji ndani ya jimbo letu. Iwe ni wale Bonyokwa, Mpiji Magoe na kote kwenye udhaifu wa mipango miji na matatizo ya usafiri huku Chuo cha Usafishaji cha Taifa kikiwa ndani ya jimbo hili hili.

Iwe ni wafanyakazi wa Kiwanda cha Urafiki hapa Ubungo ama wa sekta umma na wa binafsi waoishi ndani ya jimbo hili wenye kubebeshwa mzigo mkubwa wa kodi na kuzongwa na maslahi duni. Iwe ni wafanyabiashara ndogo ndogo wanawake kwa vijana pale Manzese, Makurumla na kwingineko; iwe ni wanafunzi wa sekondari na vyuo Mbezi na Ubungo ambao kwa ujumla wake wanaishi katika mazingira yenye mifumo dhaifu yenye kudorora kwa ubora na upatikanaji nafuu wa huduma za kijamii.

Iwe ni mwananchi wa Jimbo la Ubungo anayeathirika kwa bei na mgawo wa umeme huku akipita na kuona mitambo ya kampuni feki ya Dowans inayotakiwa kurejesha mabilioni iliyolipwa mara mbili (double payment) na serikali; mitambo ambayo imeendelea kukaa pembeni na makao makuu ya TANESCO yaliyopo jimbo la Ubungo bila kutaifishwa. Iwe ni mtanzania wa kawaida anayeelemewa na mzigo wa kodi na kupanda kwa gharama za maisha. Wote wanahitaji mbunge wa kuwasikiliza, kuwawakilisha, kushiriki kutunga sheria bora na kuziwajibisha mamlaka zinazohusika. Tanzania bila mafisadi inawezekana. Huu si wakati wa kuahidi nitafanya nini kwa kuwa si kipindi cha kampeni. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Tunahitaji mabadiliko ya kweli kuliko ahadi kedekede utekelezaji legelege

Natambua kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (pamoja na ubovu wake) imetaja katika ibara ya 9 Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha: kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa; kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa; kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumyonya mtu mwingine; kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa ulinganifu na kwa pamoja; kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini; kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondosha umaskini, ujinga na maradhi. Misingi hii na mingine, haitekelezwi wala kuzingatiwa kikamilifu kutokana na ombwe la uongozi, udhaifu wa kitaasisi na upungufu wa uwajibikaji. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Aidha naelewa kuwa katiba hiyo hiyo (pamoja na mapungufu yake) inatamka katika Ibara ya 63 kifungu cha pili na cha tatu kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia maswali, mijadala, kuidhinisha mipango (zikiwemo bajeti), kutunga sheria na kuridhia mikataba.

Madaraka hayo ya bunge na majukumu ya wabunge hata baada ya uongozi wa awamu ya nne kuahidi kuyatekeleza kwa ari, nguvu na kasi mpya na Spika wa Bunge kuahidi kuyasimamia kwa kasi na viwango; hali kwa sehemu kubwa iko vile vile; ahadi kedekede, utekelezaji lege lege.

Hasara kwa taifa iliyotajwa kwenye orodha ya mafisadi (list of shame) na ile inayotokana na ufisadi kwenye serikali za mitaa pekee kwa ujumla wake inafikia takribani trilioni mbili. Hivyo Tanzania ni nchi tajiri wa rasilimali huku wananchi walio wengi wakiishi katika lindi la umasikini na ugumu wa maisha.

Naamini hali hii inachangiwa na kufilisika kiitikadi na kidira kwa chama tawala, hodhi (monopoly) ya chama kimoja bungeni, bunge kukosa uhuru wa kikatiba na udhaifu wa taasisi za kusimamia uwajibikaji. Hali hii inachochewa pia na udhaifu wa kiuongozi ikiwemo uzembe wa sehemu kubwa ya wabunge wengi wao wakiwa wameingia kwa nguvu ya ufisadi katika uchaguzi wa mwaka 2005 na hivyo kukosa nguvu ya kimaadili na dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli. Hata wale wachache wenye dhamira ya kufanya mabadiliko wanadhibitiwa na kamati za chama chao (party caucus) chenye mmomonyoko wa kimaadili. Hivyo, harakati za ukombozi zinapaswa kuungwa mkono na watanzania wote wakiwemo wanachama wa chama hicho wanaokerwa na hali ya mambo. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Tuchukue hatua; kwa pamoja tunaweza

Jukumu lililo mbele yetu la kuwezesha mabadiliko ya kweli ni kubwa linalohitaji hatua za haraka kujitoa sadaka na kutumia talanta kuanzia sasa mpaka wakati wa uchaguzi Oktoba 2010; kabla ya majukumu makubwa zaidi kuanzia wakati huo na kuendelea. Kwa pamoja tunaweza, pamoja tutashinda.

Hatua ya kwanza ni kuhakikisha kila mmoja mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ama atayefikisha umri huo wakati wa uchaguzi kama bado hajajiandikisha anajitokeza kujiandikisha katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unaonza katika Mkoa wa Dar es salaam kuanzia kesho tarehe 22 mpaka 27 Machi, 2010 ikiwa ni awamu ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu. Aidha kwa waliohama makazi, huu ndio wasaa mwafaka pia wa kwenda kubadilisha taarifa zenu ili muweze kupiga kura katika maeneo mliyopo.

Hatua ya pili ni kushiriki kwa hali na mali katika kujenga oganizesheni ya chama mbadala. Kuhamasisha wagombea mbadala kujitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali, kuwaunga mkono na kueneza ujumbe wa matumaini wa mabadiliko kwa watanzania wengine katika maeneo yenu. Izingatiwe kuwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili mpaka Julai ni cha wagombea kuonyesha nia, kuchukua fomu ndani ya vyama, kampeni za ndani ya vyama, kuingia katika kura za maoni na uteuzi kufanywa na vyama vyao kwa kuwa serikali mpaka hivi sasa imekataa matakwa ya umma ya kutaka wagombea binafsi waruhusiwe.

Kampeni kwa umma zinatarajiwa kuanza baada ya wagombea kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwezi Agosti na zinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka 2010. Hatua muhimu wakati huo ni pamoja na kushiriki katika kampeni kwa hali na mali, kupiga kura na kuunganisha nguvu ya umma katika kulinda kura. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Haturudi nyuma kamwe; matumaini yapo mbele

Mwaka 2005 Mwezi Machi kama huu nilipochukua fomu kwa mara ya kwanza kugombea ubunge, CHADEMA haikuwa na mtandao imara katika jimbo la Ubungo tofauti na sasa ambapo ina mtandao madhubuti na ipo fursa bado ya kuufanya kuwa mzuri zaidi. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Hivyo Disemba 2005 (pamoja na kukubalika kwa wananchi) baada ya mvutano wa siku kadhaa matokeo ya uchaguzi yalitangazwa kwa shuruti bila kupitia utaratibu wa kupitia na kujumlisha kituo hadi kituo na kufanya jumla ya wapiga kura waliotangazwa kupiga kura katika ubunge kuzidi wale waliopiga kura za urais kwa zaidi ya kura elfu thelathini (30,000) katika uchaguzi uliofanyika katika siku moja.

Kutokana na hujuma hizo na nyinginezo zilizohusisha pia ufisadi katika uchaguzi niliamua kufungua kesi namba moja ya mwaka 2006 katika Mahakama Kuu kupinga matokeo hayo. Kesi ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikipigwa danadana za kiufundi bila kuingia katika kusikiliza msingi wenyewe wa kesi.

Wakati najiandaa kutangaza rasmi dhamira ya kugombea nikitazama mbele kwa matumaini, nimepokea simu toka kwa Wakili wangu katika kesi hiyo Ndugu Tundu Lissu akinieleza kwamba hatimaye Mahakama Kuu imepanga kuwa kesho tarehe 22 Machi 2010 ndio siku ambayo mahakama itatoa hukumu juu ya kesi hiyo.

Bila kuingilia uhuru wa mahakama, nieleze wazi tu kwamba kwa mtiririko wa mambo mpaka sasa hukumu hiyo itahusu zaidi ombi langu la kuondolewa kuweka dhamana ya milioni tano kama sharti la kufungua kesi na kupita kwa muda toka kesi ifunguliwe badala ya utata wa matokeo na kasoro za uchaguzi husika.

Hata hivyo kwa miaka takribani mitano ambayo nimekuwepo katika siasa na kushiriki katika chaguzi mbalimbali za kiserikali, mmoja nikiwa kama mgombea na zingine nikiwa kwenye timu za kampeni nimejifunza kuwa pamoja na uwepo wa katiba na sheria mbovu zenye kusababisha tume ya uchaguzi kutokuwa huru na kukosekana kwa uwanja sawa wa kisiasa kwa ujumla; bado vyama mbadala vinaweza kuunganisha nguvu ya umma kupata kura nyingi na kushinikiza mshindi kutangazwa pale ambapo kunakuwa na mikakati thabiti, oganizesheni makini na uongozi mahiri. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.

Naweza nikalazimika kutangaza upande wa kugombea

Tunahitaji mabadiliko ya uongozi na mfumo wa utawala ili kutumia vizuri kodi za wananchi na rasilimali za taifa kuwa na miundo mbinu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuwezesha ustawi wa wananchi.

Badala ya kuelekeza nguvu zaidi katika azma hii, serikali ya sasa inaongeza nguvu katika matumizi ya anasa na mzigo mkubwa wa gharama za utawala na sasa inajadili kuongeza zaidi idadi ya wabunge.

Mathalani mwaka wa fedha 2009/2010 kiasi cha bajeti kilichotengwa kwa ajili ya Bunge ni shilingi bilioni 62 ambayo ni sawa na wastani wa zaidi ya milioni 190 kwa kila mbunge kwa mwaka. (Pato la mtumishi wa umma wa kima cha chini halifiki hata asilimia 1% ya fedha hizo).

Ndio maana binafsi siungi mkono ongezeko la majimbo lisiloangalia tija na ufanisi wa wabunge katika kutimiza majukumu ya msingi ya kibunge. Kwa mtizamo wangu, tunapaswa kupunguza idadi ya majimbo ya uchaguzi badala ya kuyaongeza kwa kufanya wilaya za sasa za kiutawala ndio ziwe kitovu cha mgawanyo wa majimbo.

Mathalani, wilaya ya Kinondoni badala ya kuwa na majimbo matatu ya Kawe, Kinondoni na Ubungo iwe na jimbo ni jimbo moja tu la Kinondoni. Badala yake Halmashauri ya Kinondoni bila kushirikisha vyama vya siasa ilipeleka mapendekezo kwa Baraza la Mashauriano la Mkoa (RCC) wa Dar es saaalam ambalo nalo limepeleka mapendekezo ya kugawa majimbo kadhaa ya mkoa huu likiwemo jimbo la Ubungo.

Kwa mujibu wa mapendekezo yao Kata za Kimara, Makuburi, Mbezi na Kibamba zimependekezwa kuwa kwenye jimbo la Kibamba toka Jimbo la sasa la Ubungo. Kwa msingi huo wanapendekeza sasa jimbo la Ubungo libaki na kata za Mabibo, Manzese, Makurumla, Ubungo, Sinza na Mburahati na kuongezewa pia kata ya Kigogo (ambayo kwa sasa iko ndani ya Jimbo la Kinondoni).

Kwa hiyo, pamoja na kutangaza dhamira yangu ya kugombea ubunge katika eneo ambalo ni Jimbo la Ubungo; haiwezekani kwa sasa kutangaza kwa hakika nitagombea katika jimbo gani mpaka pale Tume ya Uchaguzi itakapotangaza maamuzi yake kuhusu mgawanyo wa majimbo baada ya kupokea mapendekezo hayo toka kwa serikali. Iwapo Tume ya uchaguzi italigawa jimbo la Ubungo nitalazika kutangaza upande ambao nitagombea. Ni wakati wa mabadiliko; tuwajibike.


Hitimisho:

Maneno na matendo yangu katika harakati za umma katika kipindi cha mwaka 2000 mpaka 2005 wakati nikiwa kwenye uongozi wa kijamii katika asasi za kiraia na katika kipindi cha mwaka 2005 mpaka 2010 nikiwa kiongozi wa kisiasa yanaweza kurejewa kama msingi wa kuashiria ni watu gani nitawawakilisha na masuala gani nitayasimamia katika uongozi wa umma kabla hata sijateuliwa rasmi na kutoa hotuba katika kampeni. Naomba uwasiliane nami kwa kunitumia ujumbe kupitia johnmnyika@gmail.com au 0784222222 tuwe pamoja hatua kwa hatua katika safari ya ushindi. Ni wakati wa Mabadiliko; tuwajibike mpaka kieleweke.

Wenu katika demokrasia na maendeleo;


John Mnyika
Jimboni Ubungo-21/03/2010


Thursday, March 11, 2010

Heshima ya mwisho kwa Anna Daraja

Leo tarehe 11 Machi 2010 ni siku ambayo marehemu Anna Daraja (Mke wa Balozi Mstaafu Andrew Daraja) amepewa heshima za Mwisho jijini Dar es salaam kabla ya kusafirishwa kwa ajili ya maziko.

Kwa niaba ya Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA na niaba yangu binafsi natoa salamu za rambirambi kwa mwanadiplomasia Balozi Daraja, familia yake na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine.

Kwa upande mwingine, namkumbuka Mama Daraja kama mkazi mwenzetu ndani ya Halmashauri ya Kinondoni aliyekuwa karibu na jamii ya eneo lake kabla ya mauti kumkuta kwa kuchomwa na kisu nyumbani kwake Kimara Temboni. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema.

John Mnyika: Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar es salaam (CHADEMA).

Wednesday, March 10, 2010

Maandalizi ya Uandikishaji wa Wapiga Kura Mkoa wa Dar es salaam yaanza na kasoroTAARIFA KWA UMMA: Serikali izingatie Katiba, Sheria na maelekezo katika maandalizi ya uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la Kudumu la wapiga kura katika Mkoa wa Dar salaam. Tarehe 9 Machi 2010 Vyombo vya Habari hususani gazeti la Tanzania Daima vimemnukuu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam William Lukuvi akifungua semina ya uboreshaji wa daftari katika mkoa husika. Aidha katika semina hiyo Lukuvi alitangaza kwamba zoezi la uandikishaji litafanyika katika mkoa wa Dar es salaam kwa ufanisi mkubwa.

CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam tunaungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam katika kuwahimiza wananchi wote wenye miaka 18 na kuendelea ama ambao watakuwa wamefikisha miaka 18 mwezi Oktoba na wale waliohama makazi yao kujitokeza kujiandikisha wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura utakaofanyika katika mkoa wa Dar es salaam kuanzia tarehe 22 mpaka 27 Machi, 2010.

Hata hivyo CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam hatukubaliani na kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba zoezi hilo litaendeshwa kwa ufanisi kwani tayari ofisi yake imeanza kufanya kasoro katika hatua za mwanzo ambazo kama hazitarekebeshwa kwa haraka zitavuruga zoezi hili muhimu kwa ustawi wa demokrasia katika mkoa wa Dar es salaam na taifa kwa ujumla.

CHADEMA Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalumu Dar es salaam tumeshangazwa na hatua ya uongozi wa Mkoa kuendesha mafunzo ya waandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura bila kuwashirikisha kikamilifu wadau katika maandalizi ya awali kama katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na maelekezo ya uandaaji wa daftari la wapiga kura yanavyoitaka serikali kufuata.

Tunamtaka Mkuu wa Mkoa azingatie kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 74 vifungu vya 14 na 15; maofisa waandikishaji, maofisa waandikishaji wasaidizi na waratibu wa mikoa hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.

Ili kuweza kuzingatia msingi huu wa katiba ya nchi ambayo viongozi walioko madarakani wameapa kuilinda maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu kipengele cha 2.2 na 2.4 yanataka vyama vya siasa vipewe fursa ya kutoa maoni kuhusu waandikishaji kabla ya kuanza kazi yao rasmi ili kuweza kuwawekea mapingamizi wale ambao wamekiuka masharti hayo ya katiba ya nchi.

Kitendo cha Mkuu wa Mkoa William Lukuvi kufungua semina ya mafunzo ya waandikishaji ambao vyama havijapewa fursa ya kuwatolea maoni na kuwawekea mapingamizi kama katiba, sheria na maelekezo yanavyohitaji kinaweza kutafsiriwa kuwa ni kutoa mwanya kwa makada wa chama tawala kuratibu zoezi la uandikishaji jambo ambalo linaweza kuruhusu hujuma za kiuchaguzi wakati wa uandikishaji kama zile zilizojitokeza Visiwani Zanzibar.

Hivyo, tunamtaka Mkuu wa Mkoa William Lukuvi kuwasilisha majina ya waratibu wa uandikishaji wa wapiga wa Mkoa na waandikishaji katika Manispaa/Wilaya mbalimbali kwa vyama vya siasa ili kuweza kuwatolea maoni na mapingamizi kama itahitajika.

Aidha tunamtaka azielekeze Halmashauri za Wilaya za mkoa wa Dar es salaam kufanya vikao rasmi na vyama vya siasa kujadili maandalizi ya mchakato wa uandikishaji kama kipengele cha 7.1 cha Maelekezo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kinavyoeleza. Pia awatake wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwasilisha majina ya waandikishaji wasaidizi ili kuweza kuwatolea maoni na mapingamizi kama itabainika wamekiuka Katiba ya Nchi ibara ya 74(14) na (15).

“Mkuu wa Mkoa Lukuvi azingatie kuwa Tume ya Uchaguzi imetoa maelekezo rasmi kwake ambayo kifungu cha 7.2 kinaelekeza kuwa vyama vya siasa vyote vyenye usajili wa kudumu vina haki na wajibu katika mchakato mzima wa uandikishaji wa wapiga kura ikiwemo kuwahamasisha raia wenye sifa kujiandikisha, kusahihisha taarifa na kukagua daftari husika. Hivyo, tunamtaka Mkuu wa Mkoa azingatie Katiba, Sheria, Maelekezo na misingi ya kidemokrasia kama kweli anataka zoezi liwe huru na lenye ufanisi”.

Imetolewa tarehe 10 Machi, 2010:John Mnyika-0754694553; mnyika@chadema.or.tz
Mwenyekiti wa Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum (CHADEMA)
Na Mwakilishi wa wenyeviti wa mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala- Kanda Maalum ya Kichama Dar es salaam.


Sunday, March 7, 2010

Tamko la Mnyika kuhusu Taarifa ya SMVU

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TAARIFA YA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA


UTANGULIZI:

Tarehe 24 Februari 2010 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Rais- Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitoa taarifa kwa umma kuhusu habari iliyotoka katika Gazeti la Jambo Leo Jumapili tarehe 21 Februari 2010 iliyokuwa na kichwa cha habari “ Mkapa Kitanzini-adaiwa kuvunja katiba bila kuwajibishwa”.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamishna wa maadili ilitolewa kama tangazo la kulipia katika gazeti la Mtanzania la ijumaa tarehe 26 Februari, 2010; na baadaye taarifa hiyo ikachapwa kama Tangazo la kulipia tena katika magazeti mengine likiwemo Mwananchi, magazeti ya serikali nk. Karibuni kabisa, tangazo hilo likatolewa kwa mara nyingine kwa kulipia katika gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa Machi 5 mwaka 2010.

Maudhui ya tangazo hilo hususani matumizi ya maneno kama ‘nia mbaya’, ‘uongo’ na kiwango cha kutolewa kwake katika magazeti mbalimbali kukanusha habari iliyoandikwa na gazeti moja ni dalili ya propaganda ambazo zinafanyika kwa kutumia fedha za umma hivyo ni muhimu nikatoa taarifa hii kwa umma kufanunua masuala kadhaa ya msingi ya kuzingatiwa.

Taarifa ya sekretariati ya viongozi wa umma imekanusha habari iliyoandikwa na Jambo Leo tarehe 21 Februari 2010 lililomnukuu “John Mnyika-Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA kwamba alisema kuwa Rais Mkapa hakutaja mali zake baada ya kutoka madarakani.”

Taarifa ya Sekretariati ya Maadili wa Viongozi wa Umma iliendelea kusema kwamba “Sekretariati inathibitisha kwamba Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliwasilisha tamko lake alipoacha wadhifa wake wa Rais wa awamu ya tatu kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) D cha Sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995”.

Taarifa hiyo ya Sekretariati ya maadili ya umma ilimalizia kwa “kuwaelekeza wahariri na wanasiasa wa aina ya ‘Mnyika’ kuwasiliana na uongozi wa sekretariati” ili kupata usahihi na ukweli wa taarifa za mali na madeni ya viongozi.

“Nimeshangazwa na Sekretariati ya maadili ya umma kutoa tamko bila kurejea kauli zangu kamili kama ambavyo nilizitoa kwenye kipindi cha Kipima Joto kilichorushwa katika kituo cha luninga cha ITV ijumaa tarehe 19 Februari 2010 pamoja na Jambo Leo kudokeza kuwa chanzo cha habari yako ni kipindi husika.”

Izingatiwe kuwa Majadiliano katika kipindi hicho kilichorushwa moja kwa moja (live) yalihusu swali “ Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma; Je, zinasaidia?”, na kwamba ilitangazwa katika kipindi husika kuwa sekretariati ilialikwa katika kipindi cha siku hiyo lakini haikutuma mwakilishi yoyote.


HOJA ZILIZOPASWA KUTOLEWA MAELEZO NA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA:

Katika kipindi husika nilitoa kauli ya kumtaka Rais Kikwete kuchukua hatua yeye binafsi pamoja na ofisi ya Rais ikiwemo Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu tuhuma zifuatazo ambazo kwa miaka kadhaa zimekuwa zikitawala miongoni mwa umma hususani katika vyombo vya habari:

Kwamba katika kushughulikia suala la mmomonyoko wa maadili katika uongozi wa umma ikiwemo suala la ufisadi lazima tuweke malengo ya muda mfupi na malengo ya muda mrefu. Malengo ya muda mrefu ni kubadili mfumo wa utawala kwa kufanya mabadiliko ya uongozi, kuweka dira ya pamoja, maadili ya taifa, utamaduni wa uwajibikaji na kufanya mabadiliko ya katiba yenye kujenga taasisi. Wakati tukisubiri mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana pia na uchaguzi wenye kupunguza nguvu ya chama kimoja katika vyombo vya maamuzi, hatuwezi kama taifa kuacha ufisadi na ukiukwaji wa maadili ukaendelea badala yake tunaweza kutumia katiba na sheria zilizopo kuchukua hatua za haraka.

Kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 132 imeweka msingi wa kuundwa kwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba Ibara ya 70 kuwasilisha taarifa ya mali na kifungu cha 71 kinataja sababu za kukoma kuwa mbunge kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma. Lakini kila mwaka Sekretariati imekuwa ikilalamika kwamba wapo viongozi ambao hawajazi. Na mwaka 2008 na 2009 Waziri husika alilieleza Bunge kuwa kuwa kuna ambao hawajajaza fomu husika; lakini mpaka sasa hakuna aliyeondolewa kwenye nafasi kwa sababu hiyo. Nikaendelea kueleza kwamba pamoja na kuwa Sheria husika imekinzana na katiba kwa kueleza adhabu nyingine chini ya kuondolewa madarakani; sekretariati haijawahi kueleza adhabu ambazo imezitoa. Hivyo, nikaitaka sekretariati ieleze wazi hatua ambazo imechukua; jambo ambao katika taarifa yao kwa umma hawajaligusia kabisa.

Kwamba jambo la msingi ni kuwa tunahitaji viongozi wetu wasimamie utawala wa sheria na suala hili la maadili ya viongozi wa umma, wakalaumiwa haipaswi kuwa Sekretariati ya maadili bali watawala hususani Rais wa nchi. Na nikanukuu kifungu cha 5 kipengele cha (1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma ya mwaka 1995 ambacho kinasema bayana kuwa itakuwa ni wajibu wa Rais kuchukua hatua zitakazoleta mabadiliko ya maadili yenye lengo la kuweka msingi wa kuongeza imani kwa wananchi kuhusu uadilifu wa viongozi. Hivyo, nikatoa kauli ya kumtaka Rais Kikwete yeye mwenyewe au kupitia ikulu au Wizara ya Utawala bora kueleza hatua ambazo zimechukuliwa kwa viongozi ambao wanatuhumiwa kukiuka kanuni za maadili ya uongozi wa umma. Nikatoa mfano kwamba Rais Mstaafu Mkapa amekuwa akituhimiwa kufanya biashara ikulu na kwenye kashfa ya Kiwira; Je, ni hatua gani ambazo Rais ameelekeza zichukuliwe zaidi ya kusema kwamba aachwe apumzike (jambo ambalo ni ishara ya kupuuza misingi ya kikatiba na kisheria inayotaka uwajibikaji wa viongozi wawapo madarakani na hata wanapostaafu) ? Nikakumbusha kwamba Rais Mstaafu Mkapa alipoingia madarakani alitaja mali zake zote hadharani, lakini alipotoka hakutaja mali zake zote. Tuhuma zinazotolewa juu ya Mkapa zile za ufisadi na hata za kutotaja mali zote ni za uvunjaji wa Katiba na Sheria; hatua gani zimechukuliwa? Pia, nikatoa mfano mwingine wa Adrew Chenge(Mb) ambaye uchunguzi wa SFO ya Uingereza umebaini kuwa ana akaunti nje ya nchi; je fedha zote zilitangazwa kwenye tamko lake la mali na madeni? Iwe ametangaza au hakutangaza sekretariati ilipaswa kuchukua hatua ya kumchunguza kwa kuwa sheria haisemi tu Sekretariati ipokee taarifa bali ina mamlaka ya kuchunguza ukweli wa taarifa husika na uhalali wa kimaadili wa umiliki wa mali. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikujibu tuhuma za msingi zaidi ya kusema tu kwa ujumla kuwa Rais Mstaafu Mkapa alitangaza mali zake kwa kujaza fomu zinazotolewa na chombo hicho.

Kwamba wapo wanaojenga hoja kuwa kama watu wanatuhuma dhidi ya viongozi basi wakakague mali katika sekretariati au wawasilishe malalamiko rasmi; hoja hii haizuii Rais na Sekretariati kuwajibika kwa kuwa Sheria hiyo hiyo inatamka kwamba tuhuma zinazotakiwa kushughulikiwa ni pamoja na Sekretariati yenyewe kuanzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazohusu viongozi wa umma zikiwemo ambazo zimejitokeza katika vyombo vya habari. Hivyo, Rais Kikwete na Sekretariati wanawajibika kueleza kwa umma ni hatua gani zimechukuliwa kwa viongozi wa umma ambao tuhuma zao zimekuwa zikitajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ikiwemo wale waliotajwa hadharani kwenye Orodha ya Mafisadi (list of shame) toka Septemba 15 mwaka 2007. Nilieleza kwamba hata kwenye kashfa ya Richmond, TAKUKURU wakati huo ikiitwa TAKURU pamoja na kutoa ripoti mbovu ya kuusafisha mchakato wa zabuni hiyo bado ilikiri kwamba RICHMOND ilikuwa ikipata taarifa za ndani ya serikali. Viongozi wa umma waliokuwa wakitoa taarifa za umma kinyemela kwa Richmond ili kushinda zabuni ni wazi walikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma lakini hakuna hatua ambazo sekretariati ilichukua hata baada ya taarifa hizo kutolewa kwenye vyombo vya habari. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikujibu suala hili katika taarifa yake.

Kwamba kwenda kukagua ama kuhakiki daftari la mali na madeni ya viongozi wa umma kunapoteza maana kwa kuwa Kanuni zilizotungwa na Serikali vipengele cha 6 na 7 vinaelekeza bayana kuwa ukishakagua mali husika huruhusiwi kuzizungumzia hadharani (ambayo masharti makubwa ya ziada pamoja na Sheria ya maadili ya viongozi wa umma). Nilikumbusha kwamba Wanaharakati walifungua kesi ya kikatiba mahakama kuu Aprili 2008 kupinga vipengele tajwa kesi ambayo mpaka sasa hukumu yake haijatolewa. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikulitolea taarifa suala hili pia.

Msingi mkuu wa hoja zangu nilizotoa ni kwamba uwepo wa kanuni za maadili pekee hauwezi kusaidia iwapo kanuni hazisimamiwi, na pia hauwezi kusaidia iwapo kanuni ni mbovu. Nilieleza bayana kwamba sheria na kanuni husika hazina meno ya kutosha lakini hata yale meno kidogo yaliyopo hayang’ati; kwa kuwa hakuna hatua stahili zinazochokuliwa. Kwani mpaka sasa Sekretariati haijawahi kutoa taarifa ya yoyote kuhusu aliyewahi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutokutangaza mali zake ama kutoa taarifa za uongo katika fomu husika. Hivyo, pamoja na udhaifu wa sheria, changamoto kubwa zaidi ni kutokusimamiwa kwa utawala wa sheria ambao katika suala hili la maadili wahusika wakuu katika kusimamia sheria husika ni ofisi ya Rais hususani sekretariati ya maadili ya viongozi wa umma.

MASWALI NA MASUALA YA ZIADA AMBAYO OFISI YA RAIS NA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA WANAWAJIBIKA KUYAJIBU NA KUYATOLEA TAARIFA:

Mosi; Watanzania wenzangu na mamlaka husika zizingatie kwamba msingi wa tuhuma nilizotoa tarehe 19 Februari 2010 kuhusu Mkapa kufanya biashara Ikulu, matumizi mabaya ya madaraka katika mchakato wa Kiwira na kutokutoa taarifa za mali zake zote na madeni yake baada ya kutoka madarakani ni kutolewa kwa tuhuma hizo mara kadhaa mwaka 2006, 2007, 2008 na 2009 bila kutolewa majibu kamili na Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma au Rais Mstaafu Mkapa mwenyewe. Tuhuma kuwa Rais Mstaafu hakutaja mali zake zilianza kutolewa bungeni na Fatma Maghimbi (Mb) wakati akichangia mjadala kuhusu Hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa tarehe 30 Disemba 2005 wakati akizundua bunge. Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma haikutoa tamko wakati huo. Viongozi wengine waliowahi kutoa tuhuma hiyo hadharani na kunukuliwa na vyombo vya habari ni pamoja na: Profesa Ibrahim Lipumba (Tanzania Daima-20/04/2008); Profesa Mwesiga Baregu (Mwananchi-21/11/2009). Aidha taarifa kwamba Rais Mstaafu Mkapa hajawahi kutangaza mali zake baada ya kutoka madarakani ziliandikwa pia na wanahabari kadhaa mathalani: Rai (12/1/2006); Tanzania Daima (01/04/2009) nk. Hivyo, Sekretariati ya Maadili ya Umma inapaswa kueleza Rais Mstaafu Mkapa alijaza lini hasa tamko juu ya mali zake? Na kwanini Sekretariati haikutoa taarifa katika kipindi chote toka mwaka 2006 pamoja na tuhuma hiyo kuandikwa na vyombo mbalimbali vya habari mpaka pale Gazeti la Jambo Leo lilipozirudia katika toleo lake la Jumapili tarehe 21 Februari 2010 ? Tamko la Sekretariati limekidhi sehemu ya matakwa ya sheria husika lakini halijakidhi mahitaji ya umma na misingi ya uwajibikaji hivyo, kupitia tamko hili natoa mwito wa Rais Mstaafu Mkapa mwenyewe kutaja mali zake hadharani kama sehemu ya ‘ukweli na uwazi’ ambao amekuwa akihimiza toka mwaka 1995 alipoingia madarakani katika kipindi chake cha kwanza cha Urais.

Pili; kwa kuwa Sekretariati ya Maadili ya Umma imejitokeza rasmi kutoa kauli ya kujibu kwa niaba ya Rais Mstaafu Mkapa, naiomba ijibu maswali yafuatayo ambayo umma umekuwa ukijiuliza na yako ndani ya mamlaka ya sekretariati husika kuyazungumzia: Je, Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma imehakiki mali zote na madeni ya Rais Mkapa ili kuthibitisha usahihi na ukweli wa taarifa zilizowasilishwa? Je, mali zilizotajwa zinajumuisha pia mali zinazotajwa kumilikiwa na Rais Mkapa na mkewe zikihusishwa na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma mathalani kufanya biashara Ikulu kupitia kampuni ya ANBEN, kujiuzia bei chee mgodi wa umma katika kashfa ya Kiwira ambayo Rais Mkapa alitajwa kuwa mmoja wa wanahisa? Je, Sekretariati ilichukua hatua gani baada ya tuhuma hizo kutolewa hadharani na kwenye mamlaka mbalimbali ikiwemo bungeni zikihusisha pia kukiuka kifungu 12(1)(a) kinachokataza kiongozi kutumia taarifa zinazopatikana kwenye uongozi wa umma kwa manufaa binafsi? Suala hili linahusu pia tuhuma dhidi ya Andrew Chenge (Mb) katika kashfa ya Rada zinahusu pia kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma kifungu 12(e) kwa kupokea maslahi ya kiuchumi wakati wa manunuzi na mikataba. Sekretariati imepewa mamlaka kwa mujibu wa sheria husika kifungu 18(4) kuanzisha na kufanya uchunguzi wa tuhuma hata kama hakuna mtu aliyekwenda kuwasilisha malalamiko rasmi na pia inaweza kuchunguza tuhuma hata zilizotoka kwenye vyombo vya habari kwa mujibu wa kifungu 22(4). Hivyo, Sekretariati inapaswa kueleza umma toka tuhuma zitolewe hadharani kupitia Orodha ya Mafisadi (List of Shame) Septemba 15 mwaka 2007 uchunguzi gani imeukamilisha na hatua kuchukuliwa kwa watajwa wote? Izingatiwe kuwa pamoja na uchunguzi wa awali unaoweza kufanywa na Sekretariati kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kifungu 22(2); uchunguzi kamili unafanywa na baraza ambalo kwa mujibu wa kifungu 26(5) linapaswa kufanya uchunguzi wake hadharani ili umma uweze kufahamu.

Tatu; Sekretariati itoe taarifa ya kueleza bayana imechukua hatua gani kwa viongozi wa umma ambao hawajataja mali na madeni yao au wametoa taarifa za uongo kama ilivyoelezwa kwa miaka kadhaa na sekretariati yenyewe pamoja na Ofisi ya Rais ( Rejea- Habari Leo 12/1/2007, 26/1/2007; 29/1/2007; Mwananchi 18/09/2007 na taarifa zingine zilitolewa kwenye vyombo vya habari mwaka 2008 na 2009). Aidha ikumbukwe kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Hawa Ghasia wakati akiwasilisha makadario ya bajeti ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/2009 alitoa ahadi kuwa Serikali ingewachukulia hatua za kisheria viongozi wa umma 3,186 kwa kuwa hawakurudisha fomu za tamko la mali. Pia, Taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(Utawala Bora)-Sofia Simba mwaka 2008 ilisema kwamba serikali inachunguza baadhi ya viongozi baada ya kubaini wana mali zaidi ya walizotaja kwenye fomu baada ya kuhakiki mali za viongozi 260 tu kati ya viongozi zaidi ya 7000 ambao ilipaswa kuhakiki mali zao. Sekretariati ni muhimu pia ikatoa taarifa ya kuuleza umma kwanini haikagui mali za viongozi wote kama inavyohitajiwa kwani hapo kabla iliwahi kueleza kupitia kwa kamishna wake mkuu kwamba ina uhaba wa fedha za kuweza kutekeleza kwa wakati zoezi hilo la kisheria ( Habari Leo- 18/09/2007). Badala ya kutumia fedha nyingi za walipa kodi kwenye kutoa matangazo ya maneno ni muhimu kwa sekretariati kuwekeza katika kufanya vitendo vya uhakiki, uchunguzi na kuchukua hatua stahili kwa manufaa ya umma. Sekretariati ikumbuke kuwa Rais Kikwete aliagiza toka mwaka 2007 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM kwamba mali zote za viongozi wa umma zitahakikiwa na kuchunguzwa badala ya utaratibu wa zamani wa kuorodhesha tu kwenye daftari.

Nne; Natambua kwamba Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewaelekeza wahariri na wanasiasa wa aina ya “Mnyika” kuwasiliana na uongozi wa sekretariati ili kupata taarifa za mali na madeni ya viongozi. Kabla sijatoa tamko la kukataa ama kukubali maelekezo hayo kuna masuala ambayo wahariri na wanasiasa ambao Sekretariati imewabatiza jina la ‘aina ya Mnyika’ ni lazima tukapatiwa ufafanuzi. Sekretariati ituhakikishie kwamba hata baada ya kupitia taarifa za kumbukumbu hizo za mali na madeni ya viongozi tutaendelea kutumia uhuru wetu wa kikatiba wa haki ya kupata na kutoa taarifa kama ulivyotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 vipengele (a) (b) (c) (d) badala ya kuzibwa mdomo kutoendelea kuzungumzia mali hizo baada ya kukagua daftari. Izingatiwe kuwa Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka aliyopewa na Sheria kifungu 20(3) alishatunga kanuni zenye vipengele 6(1) (2) na 7(2) (c) vinavyokataza mwananchi kuzizungumzia popote taarifa hizo baada ya kuzikagua . Kwa upande mwingine, sekretariati ituhakikishie kwamba itatoa taarifa zote kwa wakati kwa kadiri ya tukavyohitaji kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kifungu 20(1)(2) taarifa zote zinapaswa kuingizwa kwenye daftari ambalo linaweza kukaguliwa na umma kwa nyakati zote zinazofaa. Hivyo Sekretariati itoe kwanza tamko kuwa imefikia wapi kuwaruhusu Viongozi wa Vyama vya Upinzani ambao kwa barua yenye kumbukumbu CCTN/TC/DSM/UF/2008/002 ya mwezi Aprili 2008 waliomba kukagua matamko ya mali za viongozi hususani waliotuhumiwa kwa ufisadi lakini mpaka sasa inakaribia miaka miwili sekretariati haijaruhusu daftari la mali husika kukaguliwa likiwemo tamko la Rais Mstaafu Mkapa . Ikumbukwe kwamba viongozi wa vyama walikwenda kwenye Sekretariati na kutimiza masharti yote ikiwemo kujaza fomu na kufanya malipo ya ada ya ukaguzi; Sasa Sekretariati inawahakikishia kwa kiasi gani wahariri na wanasiasa ‘aina ya Mnyika’ kwamba tukienda hivi sasa tutapatiwa taarifa kuhusu Mkapa na wengine ama utakuwa ni mwendelezo mwingine wa kufunika mijadala ya umma kwa kisingizio cha kusubiria ‘taarifa sahihi’ kutoka kwenye sekretariati hiyo?. Wakati tukisubiria maelezo na maelekezo ya ziada toka Sekretariati ya Maadili ya Uongozi wa Umma tutaendelea kuandika na kuzungumza kuhusu suala hili kama sehemu ya kuhamasisha uwajibikaji wa viongozi na kutetea rasilimali za taifa.


Imetolewa tarehe 07 Machi 2010 na:
John Mnyika
mnyika@chadema.or.tz
0754694553