Sunday, February 27, 2011

Risala ya Wananchi wa Goba kwa Mbunge

RISALA YA WANANCHI WA GOBA KWA MH. JJ MNYIKA, MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO (27 February, 2011)

1.0 Utangulizi:
Awali ya yote tunamshukuru Mungu aliyekusaidia kupita katika ushindaji mgumu wa kuwawakilisha wananchi katika jimbo la Ubungo. Tunawashukuru pia wananchi walioshiriki katika harakati za uchaguzi ambao matokea yake leo ndio nguvu yako inayokuwezesha kusimama kutuwakilisha Bungeni, Serikani na zaidi kuwa kiongozi miongoni mwetu katika kujadili fursa na kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii yetu.

Tunatambua kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoainisha mgawanyo wa madaraka wewe sio kiongozi wa serikali wala wa chama bali ni kiongozi-mwakilishi wa wananchi. Hii ni pamoja na waliokuchagua na amabao hawakukuchagua na wa vyama vyote. Ndivyo tunavyoamini pia kwa diwani Mh. Kissoky kwa ngazi ya kata. Tunakukaribisha Kata ya Goba yenye changamoto nyingi. Tunamkaribisha pia Mh. Kissoky na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake tena.

Kwa kutambua hivyo, risala hii imeandikwa na wananchi wenye itikadi tofauti za vyama vya CCM, CHADEMA, CUF na vinginevyo wakifungamanishwa na dhamira moja tu ya kuleta maendeleo na kupambana na ufisadi, uonevu na matumizi mabaya ya dhamana za uongozi na madaraka. Kwetu sisi hakuna bei yeyote ya kununua utu wetu zaidi ya ukweli, uwezo wa utendaji kazi na uadilifu. MASLAHI YA JAMII DAIMA YATATANGULIA MASLAHI BINAFSI. MASLAHI YA NCHI NA YA WANANCHI YATATANGULIA MASLAHI YA CHAMA NA ITIKADI.

2. Matarajio ya Wananchi Kwa Ujio Wako
Tunashukuru katika barua yako ya kutuarifu juu ya ujio wako uliweka vipaumbele vya ziara yako katika Kata ya Goba. Tunakufahamu wewe ni mtu msikivu, makini na mwenye uwezo wa kubaini mambo mengi yanayotokea katika jamii. Hatuhitaji kukuambia kila kitu kwa sababu mengine unayafahamu na katika kampeni zako uliahidi kuyatafutia ufumbuzi. Tunategemea kusikia kutoka kwako mipango na mikakati juu ya utengenezaji wa miundo mbinu na hasa barabara kuu na zile ndogo ndogo zinazoingia na kutoka katika maeneo na mitaa yetu tunayoishi. Tunamashukuru Mungu kwa Kuchanguliwa kuwa Waziri-Kivuli wa Nishati na Madini. Hii itakupa nafasi nzuri ya kuwasaidia wananchi ambao bado wanahitaji kuunganishwa na umeme. Swala la Usalama, Elimu ya watoto na vijana wetu na usalama wa raia na mali zao vinahitaji tu upeo wa kioungozi na maono ya kuunganisha nguvu za wananchi. Tunaamini hilo utalipa uharaka wa kutosha.

Mh. Mbunge, pamoja na hayo yote swala la maji hatuwezi kuliacha kuwa la kawaida kwa sababu maji ni uhai na linagusa maisha na uhai wa kila kiumbe cha Mwenyenzi Mungu. Ni Bora ukakosa maji kwamba hayapo lakini ikifikia mtu akakunyima maji yakiwa yanapita mbele yako tena kwa ukatili tu ni uuaji. Inapofikia mtu ananyeshea matofali kwa ajili ya biashara zake huku majirani zake wakiwemo wazee, wajane na yatima wakiwa wanahangaika kutafuta walau ya kunywa au kupikia chai, hatutakuwa na lugha nyepesi zaidi ya kusema ni ukatili tunaotakiwa kupambana nao kwa nguvu zote hadi pumzi yetu ya mwisho. Tunaamini watu wanaochukia maovu katika jamii hupata upinzaji mkubwa na hata kuzushiwa kesi kwa kutumia mfumo wa sheria au/na utawala. Hiyo imeshatokea kwa wenzetu wachache amabo wamezushiwa tuhuma za kutaka kuweka sumu kwenye maji. Zaidi ya mwaka mmoja sasa waliotuhumu hawajaweza kuthibitisha.

Kama ambavyo umesoma katika taarifa ya ukaguzi wa mradi wa maji ya octoba 2007 tatizo hili limekuwa kubwa kila kukicha. Tunaamini ungekuwa unayafahamu yaliyoendelea kutokea kati ya octoba 2007 mpaka leo ungehuzunika sana . Tunaamini pia sehemu kubwa ya wananchi hawana hizi taarifa kwani zinahuzunisha sana. Tunasema hivi kwa sababu sehemu ya watendaji wa mradi wa maji walikuwa msitari wa mbele kuandamana mwaka 2007 kwenda kwa Mkuu wa Wilaya (Colnel Massawe) na Mkuu wa Mkoa (Kandoro) wakiwatuhumu wanakamati waliokuwa chini ya Ndugu Lupenza. Leo hii watu hawa ni wakatili na waonevu wa kutisha wasiosikiliza la mtu yeyote isipokuwa kiongozi wao mkuu ambaye ameendelea kutumia dhamana za uongozi wake wa kata na Manispaa kuhakikisha wananchi wanendelea kusulibiwa bila huruma. Sisi hatuwezi kupigana lakini uongozi ni dhamana yenye mwisho. Hata walioko kwenye mradi watafikia mwisho na hata viongozi nao wana ukomo wao. Shida ni kwa vipi wataendelea kuishi ndani ya jamii waliyoistesa utakapofika ukomo wa uongozi wao nao wakigeuka kuwa wahitaji sawa na wengine.

Mh. Mbunge tunapojifariji ni sehemu ya kibinadamu inayolenga kupunguza maumivu ya nafsi ambayo yumkini yangeweza kuamsha mitafaruku na jazba zinazoweza kuleta shida katika jamii. Lakini tunafahamu ziko sheria na taratibu zinazomlamzimisha mwananchi au kiongozi wa ngazi yeyote kuishi na kutenda kwa mujibu wa taratibu hata kama hazipendi. Hilo ndilo tunalotaka kusikia kutoka kwako na kwa wananchi waliokusanyika hapa leo. Tunaamini pia kwenye nguvu ya umma pale ambapo suluhisho halitafikia mwisho mwema katika kipindi cha kawaida cha uvumilivu wa mwanadamu. Tunaamini kuwa wanakamati ya maji wamejizatiti kuthibitishia umma kuwa ni watu wasafi na wale wanaowasema ni kwa sababu ya chuki binafsi au uelekeo na maslahi ya kiitikadi/kichama. Kwa sababu hiyo tuhuma zetu tumezifanyia utafiti ambao hatuna mashaka nao.

Madai yetu kwa Kamati ya Maji

I. Kamati hii sio halali-
Kamati hii ilichanguliwa na mkutano wa wananchi (Mkutano wa Mh Keenja (Mb) na Kisoky -Diwani)) tarehe 21 Octoba 2007 na ikaongezewa wajumbe tarehe 27 Octoba 2007. Ilipaswa kufanya ukaguzi wa shughuli za kamati ya kwanza na kuweka mfumo mzuri na kurudi kwa wananchi kutoa taarifa. Kwa kipindi cha miaka 3 na miezi mitano haijarudi kwa wananchi. Hata kwa kutumia kanuni za uendeshaji wa miradi midogo ya maji vijijini haifuati sheria ya uendeshaji na utoaji wa taarifa. Ngvu za kamati, jeuri na ukatili unaashiria kuwepo kwa nguvu kubwa nyuma yao. Tunasema hivyo kwa sababu katika kipindi hiki chote juhudi kubwa imefanyika ili kilio cha wananchi kitatuliwe na mamlaka halali za kiuongozi lakini hatukuzikilizwa. Hii ni pamoja na kutumia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TAKUKURU. Hii inaonyesha kupotea kwa maadili katika ngazi mbalimbali ndani ya jamii. yetu

II. Uhujumu wa Mradi
Katika ukaguzi wa mradi wa Maji Octoba 2007, tulionyesha wasiwasi wetu juu ya uwezekano mkubwa wa kuwepo ushirikiano wa kihujuma kati ya watendaji wa mradi na watendaji wa DAWASCO. Hii ilitokana na ukweli kuwa wakati kumbukumbu za DAWASCO zilikuwa zinaonyesha maji yaliyouziwa mradi kuwa mita za ujazo 67,640 (31/10/2007) matumizi ya maji kwa kutumia mita za wateja wachache zilionyesha kiasi cha maji kilichoingia kwenye mradi kuwa zaidi ya lita za ujazo laki mbili (200,000). Hatuna uhakika kama kuna hatua zozote za kiutawala au kisheria zilizochukuliwa kufuatilia na/au kukomesha uharibifu huu.

Yumkini ndio sababu tatizo hili sasa limeongezeka kwa kiwango cha kutisha. Kuna kila dalili ya ushiriakiano wa kifisadi kati ya watendaji wa mradi na watendaji wachache wa Dawasco. Utafiti wetu umejengwa juu ya nguzo zifuatazo;

a. Kuwa, ni ukweli usiopingika kuwa idadi ya watu waliounganishwa maji na matumizi ya maji ni kubwa zaidi mwaka 2010 kuliko ilivyokuwa mwaka 2006/2007;
b. Kiwango cha maji tunachouziwa na DAWASCO kimeshuka toka mita za ujazo 4,335 kwa mwezi March 2008 na kufikia mita za ujazo 1,100 (Oct 2008)
c. Tunamshukuru Mungu pia hata kwa kuwapa upofu wa fikra wanaohusika kwani kuanzia August 2008 matumizi ya maji ya units 1,100 yanalingana kwa kila mwezi. Kwa mienzi 26 inayoishia Dec, 2010 wastani wa mauzo ya maji toka Dawasco kwenda kwenye mradi ni mita za ujazo 884. Akili ya kawaida inakataa kukubali uovu huu unaojengwa kwenye mbinu dhaifu.

d. Katika kipindi cha miaka 6 ya mradi mita tatu tofauti zimetumika na DAWASCO. Yumkini ziliharibika au ni kupoteza ushahidi.

e. Ili kujiridhisha na kutowapa nafasi ya kudanganya tulilazimika kupata bill ya umeme (kutoka TANESCO) unaotumika kusukuma maji pale tangi-bovu. Tulitaka tujiridhishe kama watu wameacha kutumia maji kwa asilimia 75% kama inavyosomeka kwenye invoice ya DAWASCO . Tulitaka kujua-Je nao umeme unaosukuma maji umepungua kwa kiwango hicho hicho. Tungekuta ni hivyo tungejiridhiridha kwa sehemu lakini ilikuwa kinyume kabisa. Kama inavyoonyeshwa kwenye jedwali hapa chini ni kuwa units za umeme ziliongezeka toka wastani wa 2,500 (Oct 2007-May 2008) mpaka units 4,000 (June 2008-Octoba 2008). Kwa uwiano huu inaonyesha matumizi ya majini yalizidi karibu mara mbili hivi. Huu ni uthibitisho tosha kuwa matumizi ya maji yamekuwa yakiongezeka ila bahati mbaya tu hawakuweza kuzishawishi machine za kidigitali za TANESCO zibadilishe kiwango cha units za umeme

Jedwali 1: Matumizi ya Maji na Umeme
Mwezi Mita za Ujazo-Maji Units za Umeme
1 Novemba 2007 –Jan. 2008 8,756 6,520.40
February 2008 7,308 3,121.20
March 2008 5,610 3,697.90
April 2008 2,039 1,455.70
May 2008 1,038 2,672.80
June 2008 709 2,512.70
July 2008 800 4,178.50
August 2008 1,100 4,434.60
September 2008 1,110 4,658.90
October 2008 1,100 3,826.30

f. Sababu nyingine inayotufanya tuamini kuwa kuna ushrikiano wa kifisadi kati ya watendaji wa mradi na DAWASCO ni huu ufuatao. Eti kwa kipindi cha miaka miwili na miezi miwili (miezi 26) inayoishia Decemba 2010 DAWASCO wamefungulia maji mita za ujazo 22,973 sawa na units 884 kwa mwezi. Kiwango hiki ni kidogo kuliko mita za ujazo 24,751 zilizouzwa na DAWASCO kwa miezi saba tu ya kati ya Nov 2007-May 2008. Hili jambo ni kubwa na yumkini laweza kuhitaji nguvu na mamlaka makubwa zaidi ya kiutawala na kisheria
g. Uhujumu wa Mradi Miongoni mwa Wafanyakazi wa Mradi – Mh. Mbunge kuna viashiria vingi vinavyoonyesha jitihada za mfanyakazi binafsi dhidi ya wenzao au kikundi cha wawili au watatu dhidi ya waliobaki. Si nia ya sisi wananchi kuingilia maisha binafsi lakini yanapoingilia haki za wananchi sisi hatutanyamaza. Hatuna haki ya msingi au ya kisheria kuuliza kwa nini Ndugu G. W. Rwegasira (Mwenyekiti wa Mradi) na Bi Lilian B. Mavika (Katibu wa Mradi) wamefungua na kumiliki akaunti ya pamoja benki. Pia hatujui ilifunguliwa lini na kwa makusudi gani. Lakini tunayo haki ya kuuliza ni kwa nini pesa za mauzo ya maji zilipwe kwenye accounti hiyo binafsi?. Kama inavyoonekana kwenye Payment Voucher ya tarehe 28 sept. 2008 –wawili hao walilipwa kiasi cha shillingi laki tano (TZS 500,000) kwa cheki namba 000630 ya sekondari ya St Joseph Millenium. Huyu ni mteja mkubwa ambaye mpaka tunaandika risala hii alishatumia zaidi ya mita za ujazo 5,000 ambazo ni sawa na TZS (5,000 x 2,500) – TZS 12,500,000. Hatujui hizo nyingine zimelipwaje. Tunaomba jambo hili lifuatiliwe kwa makini.
h. Uhujumu kwa Ushirikiano na Wananchi wachache miongoni mwetu wasiokuwa waaminifu – Mh Mbunge katika kufuatilia matatitizo ya maji pamoja na madhaifu yaliyokuwepo kwenye kamati iliyotangulia tuligundua kuwa wapo wananchi miongoni mwetu ambao waliunganishiwa maji bila mita au kuchepua (divert) ili yasisomeke kwenye mita. Pia tuligundua watu waliokuwa wakitumia maji huku mita zao zikiwa zimeharibika. Zipo fununu pia kuwa watu hawa wana ushiriakiano na mafundi bomba. Jamii inawafahamu ila kuna woga wa kutajana kwani baadhi ya watu hawa wana nguvu za kifedha. Pamoja na woga lakini wanaobebeshwa mzigo wa maji ni watu maskini wakiwepo wajane na yatima wasiokuwa na kipato kwa kulipia ndoo ya shs 50/- badalaTZS 17/- zinazoruhusiwa na EWURA au wastani wa shs 25/- au 30/- amabayo ingetosha kabisa kulipa gharama nyinginezo kama kungekuwepo na uadilifu.
Mradi wa Maji Sasa ni Kisu cha Kuikata na Kuipasua Jamii: Mh Mbunge tunakueleza kwa masikitiko na uchungu mkubwa kuwa mradi huu wa maji ni fimbo ya kisiasa au itikadi. Ni chombo cha uhasama na kulipizana visasi. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mtu au au kikundi kilichoonekana kutokumunga mkono Mh. Diwani Kisoky katika kutetea nafasi ya uongozi basi wameadhibiwa kwa kuzuiliwa kupata maji, kuharibu connections zinazokwenda majumbani mwao n.k. Adhabu zina maumivu tofauti. Moja Wana CCM ambao walionekana kutokuunga mkono Bwana Kisoky na wale wanaoonekana kuwa wa itikadi tofauti. Bahati nzuri mafundi bomba ni jeuri na katili wakiwa na uwezo wa kusema chochote mahali popote na kwa yeyote kwani wanao ulinzi.
Hatuna wasiwasi na tunachokisema kwani wenzetu waliweza kuzuliwa kesi ya kuweka sumu kenye maji na kukamatwa na polisi usiku wa saa 9. mpaka leo hawajafikishwa mahakamani. Jambo hili ni la hatari kwani linaweza kusababisha chuki miongoni mwa jamii. Tunafahamu kuwa viongozi wa Kata wangekuwa wameitisha mkutano wa wananchi hii kamati iliyokusudiwa kuwa ya muda ingeshabadilishwa na jamii isingekuwa inaendelea kupata mateso na manyanyaso ya kiwango hiki. Udhaifu wa kamati hii umeendelea kulindwa kwa pazia la kiitikadi. Lakini wanaoumia ni Wana CCM na wengine. Hatujawahi kusikia kuwa wana CCM wana bei tofauti ya maji au miongoni mwetu tunao wana CCM hatujawaji kurudishiwa kiasi fulani kwa siri. Wote tumeendelea kuadhibiwa

3.0 Mapendekezo:
Sisi tumewasilisha kilio chetu kwa niaba ya wananchi. Mh. Umma uliopo mbele yako watoe mapendekezo
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Taarifa ya Ukaguzi ya Wananchi ya mwaka 2007 unaweza kuisoma kupitia: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/taarifa-fupi-ya-ukaguzi-wa-uendeshaji_27.html

Taarifa fupi ya ukaguzi wa uendeshaji wa mradi wa maji Goba

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ameitisha mkutano wa wananchi wa kata ya Goba utakayofanyika eneo la Goba mwisho mwembemadole siku ya jumapili tarehe 27 Februari 2011 kuanzia saa 9 alasiri mpaka sasa 12 jioni.

Mkutano huo utajadili ajenda mahususi za maendeleo kuhusu maji, barabara na ulinzi. Hata hivyo, inatarajiwa kwamba ajenda ya maji itachukua uzito mkubwa katika mkutano huo kutokana na malalamiko mbalimbali ambayo yamewasilishwa kwa ofisi ya mbunge na wananchi mbalimbali.

Katika Mkutano huo Mbunge wa Ubungo anatarajiwa kutoa fursa ya ripoti ya ukaguzi kuwekwa hadharani ripoti ambayo haikutolewa kwa wananchi toka mwaka 2007 ukaguzi ulipokamilika.
Itakumbukwa kwamba kwa kipindi cha miaka takribani mitano pamekuwa na malalamiko kuhusu maji yakihusisha pia tuhuma mbalimbali kuhusu mradi wa maji. Kutokana na hali hiyo tarehe 21 Oktoba 2007 palifanyika mkutano wa wananchi ambapo pamoja na mambo mengine iliazimiwa kwamba kamati iliyokuwa ikihusika na mradi wa maji isimamishwe kwa muda kuruhusu ukaguzi wa uendeshaji wa mradi.

Kutokana na uamuzi huu wananchi waliunda kamati ya muda ya kupitia uendeshaji wa mradi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa uongozi na wananchi kabla ya tarehe 27 Oktoba 2007.
Kamati hiyo ilipewa majukumu kadhaa ikiwemo: Kupitia mahesabu na mfumo wa uendeshaji wa mradi kwa msaada wa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mkaguzi wa Manispaa (auditor) ili kutoa maoni juu ya madhaifu, mfumo na/au namna bora na endelevu ya kuuendesha mradi huu na Kuwasilisha mapendekezo kwa timu ya uongozi na wananchi ili kutoa fursa ya majadiliano na maamuzi katika mkutano uliopendekezwa kuwa tarehe 27 Oktoba 2007.

Hata hivyo, pamoja na ukaguzi husika kukamilika toka mwaka 2007 mkutano wa wananchi haukuitishwa katika tarehe husika wala tarehe nyingine yoyote katika kipindi cha miaka zaidi ya mitatu mpaka hivi sasa wala ripoti husika haijawahi kutolewa hadharani.

Hivyo, Mbunge mpya wa Ubungo ameamua kuitoa ripoti hiyo hadharani kupitia mkutano na wananchi pamoja na mtandao kama ifuatavyo ili mjadala uweze kufanyika ili kukubaliana hatua za kuchukua katika mazingira ya sasa mwaka 2011:


TAARIFA FUPI YA UKAGUZI WA UENDESHAJI MRADI WA MAJI GOBA

1.0 Utangulizi:

Tarehe 21 Octoba 2007 wananchi wa Kata ya Goba Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar re Salaam walishiriki katika mkutano wa mashauriano na viongozi mbalimbali wa Kata na Mbunge wao (Jimbo la Ubungo) Mh. Charles Keenja. Mkutano huu uliitishwa na Mh. Kisoky ,Diwani wa Kata ya Goba kama sehemu ya kufuatilia maagizo na ushauri wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kufuatia malalamiko ya matatizo ya maji yaliyokuwa yamefikishwa ofisini kwake na baadhi ya wananchi. Mh. Diwani aliwaalika pia viongozi watendaji wa Kata ya Goba pamoja na wa mitaa yote minne ya Kinzudi, Goba, Kulangwa na Matosa. Pamoja na kwamba wananchi kwa ujumla walikuwa na mambo kadhaa na ambayo Mh. Mbunge Keenja alipata fursa ya kufafanua na kuyatolea majibu, agenda kubwa ilikuwa ni kukatiwa maji na DAWASCO kutokana na kulimbikiza deni linalofikia shillingi millioni kumi na tano (TZS 15,000,000)

Kufuatia malalamiko na manung’uniko toka kwa wananchi zikiwepo tuhuma za ubadhirifu ilionekana ni hekima kuisimamisha kwa muda kamati hii ili kuruhusu ukaguzi wa uendeshaji wa mradi. Kwa maana hii uongozi kwa pamoja na wananchi watakuwa wameshiriki kwa vitendo kusimamia utawala bora badala ya kutuhumu bila uthibitisho. Kwa upande mwingine wajumbe wa kamati ya mradi wa maji watapata nafasi ya kujibu hoja mbalimbali zitakazoibuliwa na ukaguzi huu. Kutokana na uamuzi huu wananchi walipendekeza kamati ya muda ya kupitia uendeshaji wa mradi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa uongozi na wananchi kabla ya tarehe 27 Octoba 2007. Kamati hii ilitakiwa kufanya mambo matatu;

I. Kushirikiana na Mh. Mbunge na Diwani kupata/kukopa fedha kiasi cha millioni nne (TZS 4,000,000) kulipia sehemu ya deni la TSZ millioni kumi na tano (15,000,000) kama sharti la Dawasco kuirejesha mita ya maji pale Tangi bovu kwenye kianzio au muunganisho na bomba kubwa;
II. Kupitia mahesabu na mfumo wa uendeshaji wa mradi kwa msaada wa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mkaguzi wa Manispaa (auditor) ili kutoa maoni juu ya madhaifu, mfumo na/au namna bora na endelevu ya kuuendesha mradi huu,
III. Kuwasilisha mapendekezo kwa timu ya uongozi na wananchi ili kutoa fursa ya majadiliano na maamuzi katika mkutano uliopendekezwa kuwa tarehe 27 October, 2007.

1.1 Wajumbe wa Kamati waliopendekezwa ni hawa wafuatao:
I. Ndugu Ibrahim Mabewa –Mtendaji wa Kata ya Goba (Mwenyekiti)
II. Ndugu Emanuel Meso Chacha -Mjumbe/Katibu
III. Ndugu Hamisi Deule –Mjumbe
IV. Ndugu Mama Mwazani Ramadhani- Mjumbe
V. Ndugu Willy Muro Mjumbe-Mtaalamu wa mambo ya fedha na ukaguzi
VI. Auditor toka Manispaa ya Kinondoni ambae Mh. Mbunge angemwomba kwa mkurungenzi – Aliteuliwa jumatatu ya 22octoba 2007- Ndugu Paul Kandokando

Kamati hii ilifanya kazi ilizopangiwa na kuwasilisha taarfia za awali katika kikao cha Mbunge na wananchi kilichofanyika wiki moja baadaye yaani tarehe 27 Octoba 2007. Ikiwa imefanikiwa kutimiza jambo moja muhimu la kuunganishiwa maji na DAWASCO kamati iongezewe nguvu za utendaji ili iweze kumalizia kwa haraka majukumu yaliyosalia na kuyatolea taarifa katika mkutano wa wananchi ambao ungeitishwa baadaye. Mh. Mbunge aliwasihi wananchi waendelee kuwa na subira na alikuwa anawahi kikao cha Bunge mjini Dodoma. Wananchi walipendekeza wajumbe wafuatao kuongezwa kwenye kamati ili kuharakisha mategemeo na makusudio ya kuwa na mradi endelevu. Wajumbe walioongezwa na mitaa wanayotoka kwenye mabano ni hawa wafuatao

VII. Mama Rose Basaka (Mjumbe- Kizundi)
VIII. Ndugu Rwegasira (Mjumbe-Kinzudi
IX. Maulidi Selemani –(Mjumbe-Goba)
X. Mama Mnandi(Mjumbe-Goba)
XI. Ndugu Wambura –(Mjumbe-Kulangwa)


2.0 Matokeo na Taarifa ya Ufuatiliaji na Ukaguzi:

2.1 Kulipia na Kuunganishiwa Mita na Dawasco
Tunasihi kwa niaba ya wananchi tumshukuru Mh. Mbunge Keenja akishirikiana na diwani kwa jitihada kubwa walizofanya kupata mkopo wa shillingi millioni nne (4,000,000) toka Manispaa ambapo iliwezesha kulipa sehemu ya deni siku moja tuu baada ya kikao cha jumapili;

2.2 Ukaguzi wa Mfumo (systems audit), Utendaji (Performance audit) na Utawala wa fedha (Financial audit)

Tarehe 22 October,2007 wajumbe wanne wa kamati wakiongozwa na Mwenyekiti (Mtendaji wa Kata) na Auditor toka Manispaa walikubaliana nini kifanyike kutokana na uharaka wa taarifa, ukubwa wa eneo la mradi kijiografia na mazingira halisi ya ukaguzi. Kamati hii iliafiki kuwa ili kupata matokeo mazuri ya kazi hii yafuatayo yanastahili kufanywa;

2.2.1 Kupata uthibitisho na uwiano wa maji yaliyonunuliwa toka DAWASCO na yale yaliyouzwa kwa wateja kwenye vioski (mabomba ya wananchi) na yale yaliounganishwa majumbani. Malinganisho haya yanatoa fursa ya kubaini upotevu wa bidhaa (yaani maji) kwa njia ya kuvuja (leakages), yanayotumika kuosha ndoo kwenye vituo n.k

2.2.2 Ili kupata uthibitisho huu (2.2.1 hapo) juu ilibidi timu ya ukaguzi ipitie vituo vyote vya wananchi na majumbani na kusoma mita, kupata uthibitisho wa gharama za maji, malipo ya billi n.k.


2.2.3 Kulinganisha taarifa hapo juu (confirming) na taarifa na ripoti za kamati, pamoja na nyingine muhimu zikiwepo za DAWASCO.

2.3 Mfumo na Utendaji
Tulipitia wateja wapatao toka vituo mbalimbali. Sehemu nyingine tuliwakuta wenye nyumba na mahali pengine hatukuwakuta. Kwa sababu hii hatukuweza kupata maelezo muhimu juu ya gharama za kuunganishiwa na ulipaji wa bili ili kupata uthibitisho wa jumla ya fedha iliyopkelewa. Kwa sehemu kubwa tuliweza kulinganisha kiwango kilichotumika na bili za August, Septemba na Octoba 2007 kwa wale waliokuwa nazo. Mahojiano na wateja pamoja wasimamizi wa vituo vya wananchi ni kama yafuatayo;

2.3.1 Malipo ya Ankara za Maji na Utoaji wa Risiti – Idadi kubwa ya wateja tuliowatembelea walikiri kuwa wamekuwa wakilipa gharama za maji kila wanapopewa bili lakini hawakuwa wanapatiwa risiti. Wakati mwingine wakiuliza wanaadiwa kuwasilishiwa baadaye ahadi ambazo hazikutekelezwa. Huu ni udhaifu mkubwa kwa wananchi/wateja kutokujua wajibu wao au tu mwendelezo wa utamaduni wa kupuuzia mambo muhimu. Pale ambapo kamati ilipatiwa bili za mwezi tulijaribu kuona kama kulikuwa na malimbikizo. Hii ni kwa sababu bili inaonyesha salio la kipindi kilichopita na gharama mpya ya mwezi. Bili tulizopitia zinaonyesha kuwa kwa sehemu kubwa wateja walikuwa wanalipa ankara zao kwa wakati.

2.3.2 Kuunganishiwa Maji- Ukaguzi unaonyesha kuwa mfumo wa maombi ya kuunganishiwa maji pamoja na malipo haukuwa na uwazi. Yumkini ndio sababu ya kuunganishiwa maji kwa malipo tofauti. Kutokana na mahojiano na wateja tulishuhudiwa kuwa baadhi wameunganishiwa kwa TZS 160,000, wengine TZS 210,000; TZS 310,000; TZS 500,000 mpaka TZS 700,000.

2.3.3 Usimamizi wa Vituo/Mabomba ya Wananchi – Kila kituo kina watu wanaoitwa kamati ya maji ambapo wajumbe wake husimamia uuzaji wa maji kwa wananchi. Kwa kipindi kirefu ndoo moja ya lita ishirini iliuzwa kwa TZS 40/- hadi hivi karibuni ilipopandishwa na kuwa TZS 50/-. Baada ya mauzo msimamizi wa mradi ndugu Msasa alikuwa anawapitia wauzaji na kukusanya mapato kwa utaratibu tuliouona kuwa ni dhaifu. Baadhi ya wauzaji wana daftari wanazoandikia mapato wakati wengine hawana. Kwa kuwa hakuna leja inayoonyesha kiwango cha maji yaliyouzwa na kwa kwa kuwa hakukuwepo na risiti basi uwezekano wa kuthibitisha mapato kwenye vioski vya wananchi ni mgumu.

Baadhi ya vituo hivi kwa mfano Mbuyuni (Kwa Sanya) havina mita na wananchi wanauiziwa maji kwa utaratibu ambao hatukujua ni kwa vipi waliweza kufahamu kiwango cha maji na fedha zilizopatikana. Baadhi ya mita za kwenye vituo ni mbovu ambapo vingine zilishabadilishwa mara zaidi ya moja lakini hatukuweza kupata mita za zamani. Kwa sababu hii imekuwa vigumu kupata kiwango cha maji kilichouzwa kwa kila kituo.

2.3.4 Mabomba ya Majumbani- Tunashawishika kutokuamini kama baadhi ya wateja si washiriki wa tuhuma wanazoelekeza kwa kamati. Pili tumegundua kuwa wapo watu walounganishiwa katika eneo la Mbezi Juu/Tangi Bovu. Tulikuta baadhi ya nyumba zikiwa na mita mbovu japokuwa wanapata maji. Hatukuweza kutambua bili ya maji inatolewaje wakati mita imeharibika. Baadhi ya Ankara zinatia shaka. Mfano wakati mjumbe mmoja wa kamati alikiri kwenye mkutano wa wiki iliyopita kuwa anacho kisima cha lita 25,000 na amekuwa akiuza maji, mita yake ilionyesha kuwa amechota maji uniti 11 tu sawa na lita 11,000. Kwa tafsiri nyingine hajawahi kuchota maji yonayofikia hata nusu yakisima chake tangu mradi uanze.

Mahali pengine, mteja ambaye amekuwa akiuza maji kwa wingi na kwa muda mrefu eneo la Kunguru mita yake imesoma unit 125 tu. Tunashawishika kuamini kuwa upo utaratibu wa kudivert maji nje ya mfumo wa mita kwani hata kamati iliporudi kwa mteja mwenye unit 11 tulikuta ameshaingoa. Hii ina maana kuwa hata tulipofungulia maji siku ya jumatano yaliyoingia kwake hayana kumbukumbu yeyote.

2.3.5 Usomaji wa Mita Tangi Bovu – Usomaji wa mita kuu tangi bovu ulikusudia kuoanisha na kuthibitisha kama kuna uhusiano kati ya maji yaliyonununuliwa kutoka DAWASCO NA YALE YANAYOONYWESHWA NA ANKARA TULIZOZIPITIA KATIKA Vituo. Kutokana na ukaguzi wetu mita kuu ya Tangi Bovu ilichukuliwa na DAWASCO walipokata maji tarehe 4/octoba/2007 ikiwa inaonyesha matumizi ya mita za ujazo 67,640. Idadi hii ndio inayoonekana kwenye bili ya DAWASCO iliyosainiwa tarehe 22 october 2007 ya mmoja wa wateja. Kiwango hiki cha maji kimeambatanishwa na fedha zilizolipwa na kamati ya maji kuanzia Octoba 2005 na kuonyesha kuwa DAWASCO inadai TZS 15 millioni.

Kamati hii haikuwa na uwezo wa kupitia nyaraka za DAWASCO kuthibitisha kama walikosea au la. Lakini ukaguzi wetu unatia shaka kubwa kutokana na yafuatayo;

Leja iliyopo Tangi Bovu (tumeambatanisha vivuli) ambayo inasainiwa na mlinzi na mwendesha machine Ndugu Mustapha Jumanne inaonyesha kuwa tarehe 5 Decemba mwaka jana (2006) DAWASCO ilikuwa imeuzia mradi wa maji Goba mita za ujazo 38,565.5 kuanzia octoba 2005 ambapo kiwango hiki kilifikia mita za ujazo 67,640. Ukilinganisha na usomaji wa mita majumbani kwa watu walounganishiwa maji na vioski vya wananchi kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na matumizi yanayoonyweshwa na mita ambayo yanazidi mita za ujazo 200,000. Hii ni tofauti kubwa ambayo ambayo inahitaji nguvu kubwa zaidi ya kisheria na kiutawala kuichunguza.

Yumkini tofauti kubwa hapo juu yaweza kuwa mita za wateja ni mbovu lakini ni vigumu kuamini kwa nini mteja akubali kuendelea kutumia mita mbovu. Na hata kama akikubali msimamizi wa mradi anampaje bili ya mwezi na yeye analipa kwa utaratibu upi ukizingatia pia kuwa hakuna risiti?


3.0 Majumuisho na Ushauri Wetu

3.1 Mradi haukuendeshwa kwa utashi wa kutosha kuthibitisha kama kulikuwa na nia na dhamiri njema ya kutoa huduma hii muhimu;
3.2 Maji yaliyotumika hayawezi kuwa mengi kuliko yaliyouzwa na DAWASCO. Kuna walakini mkubwa ambao mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua;
3.3 Kuna fununu kuwa wapo watu waliounganishiwa maji kwa siri hasa Tangi Bovu na Sehemu ya Mbezi Juu. Tumekubali fununu kwa kuwa hili ni tatizo sugu linaloikabili DAWASCO na mashirika mengine ya maji ya Miji ya Tanzania.Tusingeweza kukataa kupokea fununu kwa kuwa zinalingana na matatizo sugu yanayotangazwa na vyombo vya habari sehemu mbalimbali. Kamati haikuwa na mamlaka ya kuingia nyumbani kwa watu na kuchimba ili kuthibitisha. Lakini hiki ni kianzio muhimu kwa kamati mpya au ile ya zamani ikiwa ni utashi wa wananchi na viongozi kuirejesha kwenye utendaji.
3.4 Uthibitisho wa Kimazingira (Circumstantial evidence) unaonyesha wapo wananchi waliokula njama (collusion) za kujipatia maji kwa kuyaingiza kwenye visima bila kupitia kwenye mita. Haingii akilini mtu ana visima vikubwa huku akiuzia majirani maji mwaka mzima na mwishowe awe na mita inayosoma ujazo wa mita 125.
3.5 Mfumo wa uuzaji wa maji katika vituo unaashiria ushirikiano usiokuwa wa kiuadilifu kati ya mkusanyaji wa fedha na baadhi ya wauzaji. Ni vigumu kuamini uhusiano wa kiutendaji kwa mtu anayeuza maji kwenye kituo kisichokuwa na mita huku akiendelea kukabidhi chochote alichokipata bila hata ya maandishi huku mpokeaji wa fedha akiwa haitaji uthibitisho zaidi.

3.6 Kwa ujumla mfumo (system), utendaji (performance) na utawala wa fedha (financial management) ulikuwa ni dhaifu sana kiasi ambacho kimoja hakikumsaidia mwenzake. Kwa maana nyingine kulikuwa hakuna mfumo ulioruhusu utendaji mzuri wa kazi na kwa kwa kuwa utendaji ulikuwa dhaifu basi utawala na usimamizi wa fedha uliharibiwa kwa manufaa binafsi au ya kikundi cha watendaji.

3.7 Uwezo wa kuthibitisha kiwango cha ubadhirifu kinahitaji yafuatayo;

3.7.1 Uwepo muda wa kutosha kufuatilia kila mtu aliyeunganishiwa maji atoe taarifa ya fedha yote aliyolipa;
3.7.2 Kamati za maji kwenye vioski vya wananchi wahojiwe kueleza ni kiasi gani na kwa uthibitisho kiasi walichokabidhi kwa mkusanyaji wa fedha;
3.7.3 Uthibitisho toka DAWASCO kama kweli kiwango kinachoonyeshwa kwenye bili yao ni halali. Kama ni halali basi mita zote za wananchi zitakuwa ni mbovu au zimetengenezwa kwa utaratibu tofauti na mfumo wa dunia (international standards) wa kupima matumizi ya maji.
3.7.4 Mamlaka za kiutendaji (administration/government) zenye nguvu za kisheria zipitia bomba lote kuona watu waliounganishiwa maji kwa siri. Kinyume na kutokufanya wananchi maskini wataendelea kulipishwa gharama kubwa kufidia ubadhirifu wa watu wachache, yumkini wenye uwezo mkubwa tu wa fedha.

Taarifa hii imeandikwa na:

1. Imanuel Willy Muro (Mjumbe kamati ya Maji-Goba
2. Paul Kandokando –Auditor wa Manispaa ya Kinondoni

Nov 2007

Monday, February 21, 2011

Tamko langu la awali kuhusu kuwekwa X katika majengo ya pembeni ya Barabara ya Morogoro

Katika kipindi cha wiki moja mfululizo kuanzia tarehe 11 mpaka 17 Februari 2011 nikiwa bungeni Dodoma nimekuwa nikipokea simu na sms toka kwa wananchi wakilalamikia hatua ya wafanyakazi wa wakala wa Barabara Mkoa wa Dar es salaam (TANROADS) kupita katika nyumba zao zilizopembezoni mwa barabara ya Morogoro bila wakazi kupewa notisi na kuweka alama za “X” ama “BOMOA TNRD”.

Aidha nimesoma kwenye baadhi ya vyombo vya habari (mf. NIPASHE Toleo na. 056929 la tarehe 18 Februari 2011 Uk 1 na 8) habari yenye kichwa “bomoa bomoa nyingine kukumba wakazi wa Ubungo/Dar”

Habari hiyo imemnukuu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es salaam, James Nyabakari akiwataka watu wote waliojenga kwenye hifadhi ya Barabara kubomoa wenyewe na kwamba serikali haitawalipa kwa kuwa ni wavamizi na kwamba watakaolipwa ni wale tu ambao serikali itahitaji maeneo yao.

Taarifa zinazoelezwa ni kwamba alama hizo zimewekwa mita 90 pande zote mbili za barabara kuanzia maeneo ya Ubungo mpaka Kimara, na kwamba hali hiyo itawagusa pia wananchi wa Mbezi mpaka Kiluvya katika hatua za baadaye.

Nikiwa mwakilishi wa wananchi wa maeneo husika nimeshangazwa na hatua kubwa kama hizi za kiserikali kuchukuliwa bila kufanyika kwa mikutano ya umma ama walau kutoa taarifa ya kuelimisha umma kuhusu mipango husika inayotarajiwa kufanyika. Aidha nimeshangazwa zaidi na hatua kama hizo kuchukuliwa bila walau wawakilishi wa wananchi kama wenyeviti wa mitaa, madiwani na wabunge kuelezwa kwa kina mipango inayokusudiwa kufanyika na athari zake kwa wananchi wa maeneo husika. Utendaji kazi wa namna hii ni kinyume na misingi ya utawala bora inayotaka uwazi na pia ni chanzo cha migogoro isiyo ya lazima katika jamii.

Nachukua fursa hii kutoa mwito kwa serikali ngazi ya wizara ya ujenzi, mkoa na wilaya kuhakikisha kwamba mikutano na wananchi inafanyika ama walau matangazo kwa umma yanatolewa kuhusu suala husika.

Aidha mamlaka husika za kiserikali zitoe maelezo ya wazi kuhusu wananchi wanaostahili fidia na kutoa notisi ya muda wa kutosha kwa wakazi wenye majengo yanayostahili kubomolewa ili kupitisha barabara ya mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (DART) na mipango mingine.

Katika kufanya hivyo Serikali izingatie kuwa wapo wakazi wengi wenye kustahili kulipwa fidia kutokana na historia ya Barabara hiyo ya Morogoro kuliko ambavyo suala hili linavyotazamwa kijuujuu.

Ikumbukwe kwamba Mwaka 1932, wakati wa mkoloni, ilitungwa sheria ya barabara nchini, sheria hii inatambua na kuelezea uwapo wa barabara za umma nchini. Kiambatanisho cha sheria hii kinaitaja barabara itokayo Morogoro mpaka Iringa, maarufu kama barabara ya Morogoro kama barabara ya umma, pamoja na mambo mengine, sheria hii inampa waziri mwenye dhamana na barabara uwezo wa kuamua juu ya upana muafaka wa barabara za umma kwa kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali.

Mnamo mwaka 1967, waziri mwenye dhamana ya barabara nchini alitoa notisi namba 161 kwenye gazeti la serikali, kupitia tangazo hilo upana wa barabara uliongezwa kutoka futi 33 za mwaka 1932 na kufikia futi 75, hii ni kutoka katikati.

Sheria hii ya mwaka 1967 ndio umekuwa msingi wa 'bomoa bomoa' na 'chukua chukua' inayotekelezwa na serikali chini ya mwavuli wa kile kinachojuulikana kama upanuzi wa barabara ya Morogoro. Hata hivyo ni vyema ikumbukwe kuwa tangazo hilo la serikali halikueleza juu ya maeneo yanayo milikiwa na watu binafsi.

Hivyo mamlaka husika zirejee kwamba utekelezaji wa sheria hauzingatii kikamilifu wakazi ambao wameyamiliki maeneo hayo kabla ya mwaka 1967 ambao kimsingi sheria hii imewakuta,hivyo wanahaki ya kulipwa fidia. Pamoja na ukweli kuwa katika miaka hiyo majengo yalikuwa bado hayajatamalaki lakini sehemu kubwa ya ardhi ilikuwa ni ama mashamba ya watu au maeneo ya ufugaji ambayo kwa muda wote huo yamekuwa yakirithishwa au kuuzwa vizazi hadi vizazi mpaka kufikia hatua ya sasa ya kuendelezwa. Kwa serikali inayofuata sheria zinazojali haki, watu hawa wanastahili fidia kwa kuwa sheria hii iliwakuta.

Ikumbukwe pia kwamba baada ya Barabara ya Morogoro kukamilika miaka ya mwanzoni mwa sabini, serikali ya Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilianzisha kote nchini vijiji vya ujamaa na kuhamishia watu katika vijiji hivyo. Maeneo ya kati ya Ubungo na Kiluvya yalikuwa sehemu ya vijiji hivyo na watu wakahamishiwa katika maeneo hayo kwa ajili ya makazi. Dar es salaam ilitangazwa kama eneo la mjini mwaka 1985 bila ya wananchi wa maeneo husika kushirikishwa kwa ukamilifu.

Hivyo ni muhimu kwa mamlaka husika kurejea ukweli kwamba Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kifungu cha 15 kinatambua haki za watu walioishi katika vijiji kati ya tarehe 1 Januari 1970 na tarehe 31 Disemba mwaka 1977; hivyo kimsingi haki za wananchi wa eneo kati ya Ubungo na Kiluvya walioanza makazi yao katika kipindi husika zinapaswa kuthaminiwa na kulindwa.

Mamlaka husika zikumbuke kwamba mwaka 2001 bila kuzingatia sheria hiyo ya ardhi Wizara ya husika iliingilia makazi ya wananchi na kuongeza ukubwa wa eneo la hifadhi ya barabara kuwa mita 120 kila upande wa Barabara ya Morogoro.

Izingatiwe pia kwamba mwaka 2009 Waziri wa Miundombinu wa wakati huo Dr Shukuru Kawambwa alitoa kanuni kupitia gazeti la serikali namba 21 na 23 la Januari 2009 zilizopunguza eneo hilo kutoka mita 120 mpaka mita 60 kwa pande zote mbili za barabara katika maeneo mengi, mchakato huu nao ulifanyika kimya kimya bila wananchi kupewa taarifa za wazi na za kina.

Katika kanuni hizo maeneo mengi ya barabara ya Morogoro nchi nzima yametengwa kuwa mita kati ya 30 na 60 kwa pande zote mbili isipokuwa ya kutoka Ubungo mpaka Kiluvya ambayo yametengwa kwa kiwango kikubwa zaidi bila kuzingatia kwamba baadhi ya maeneo hayo yalishatolewa kihalali kwa wananchi kupitia sheria nyingine kama maeneo ya makazi kama nilivyoeleza awali. Hivyo, katika mazingira hayo, ikiwa serikali ina mpango wa kuongeza ukubwa wa barabara ziada ya eneo ambalo tayari lilishatolewa kwa wananchi na wajibu wa serikali kuhakikisha wananchi hao wanapata fidia stahili.
Baada ya sheria zingine kuwapa haki ya kuanzisha vijiji na baadaye miji Serikali iliwapa uhalali zaidi wa kuwa na makazi rasmi katika maeneo hayo kwa kuwapelekea huduma za msingi ambazo kisheria hutolewa maeneo halali yanayo tambulika kisheria. Serikali imewawekea miundo mbinu ya umeme, maji, simu na wengine wamepewa mpaka hati miliki na wizara ya ardhi. Iweje wizara ya ujenzi imwambie mtu kuwa ardhi anayo imiliki si halali wakati amesha milikishwa ardhi hiyohiyo na wizara ya ardhi? Au wizara ya ujenzi na ile ya ardhi ziko chini ya serikali mbili tofauti?

Kimsingi mimi kama mwakilishi wa wananchi wa eneo husika, naunga mkono suala la miradi ya maendeleo katika maeneo yetu; hata hivyo miradi hiyo lazima izingatie vile vile haki na stahili za wananchi wanaoondolewa kupisha miradi husika. Na ni muhimu kwa mchakato mzima kuwa shirikishi na taarifa sahihi kutolewa kwa wakati. Hivyo, pamoja na mikutano na taarifa ambazo nahimiza mamlaka husika kuzitoa na mimi kwa upande wangu nitatembelea maeneo yanayogusudiwa kubomolewa na nitafanya mikutano na wananchi kuhusu suala husika pindi nikirejea Dar es salaam. Aidha, natoa rai kwa wananchi wote wa maeneo husika ambao wanaamini kwamba haki zao zinavunjwa waweze kuunganisha nguvu ya umma katika kuhimiza uwajibikaji na kufuatilia stahili zao kama sehemu ya kutimiza wajibu wao wa kiraia kwa maendeleo ya kaya zao na taifa kwa ujumla.

Imetolewa safarini toka Dodoma tarehe 20 Februari 2011:

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo

Saturday, February 19, 2011

Mrejesho kuhusu Uwakilishi wa Mbunge wa Ubungo Bungeni katika Mkutano wa Pili

Waraka wa kwanza kwa Wananchi wa Jimbo la Ubungo: Mrejesho kuhusu uwakilishi wa Mnyika bungeni katika mkutano wa pili.


Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2) Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi ya kuishauri na kuisimamia serikali. Katika kutimiza wajibu huu kwa nafasi yangu ya ubunge wa Jimbo la Ubungo niliwawakilisha wananchi wenzangu kwenye Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi ulioanza tarehe 8 Februari na kuahirishwa tarehe 18 Februari 2011. Naomba nitoe mrejesho kwa muktasari kuhusu ushiriki wangu katika vikao vya mkutano husika wa bunge.


Katika kikao cha kwanza tarehe 8 Februari wakati wa mjadala juu ya Azimio la kufanya Mabadiliko katika Kanuni za Bunge toleo la 2007 niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni 68 (7) kuhusu haja ya kiongozi wa kampi rasmi ya upinzani kupewa nafasi ya kuzungumza na nikatoa hoja kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (b) kwamba mjadala uahirishwe mpaka kwanza kiongozi wa upinzani apewe nafasi ya kuzungumza kama zilivyo mila na desturi za uendeshaji wa Bunge. Spika alilazimika kumpa kiongozi wa upinzani nafasi ya kuzungumza pamoja na kuwa tayari alikuwa amefunga orodha ya wachangiaji hapo awali bila kumpa nafasi. Baada ya hotuba ya kiongozi wa upinzani nilishiriki kutoka bungeni ili kutoshiriki maamuzi ambayo yalilenga kuminya demokrasia ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na pia kutoa fursa kwa wabunge wa chama tawala kuchagua wenyeviti wanaowataka kuwakilisha kambi rasmi ya upinzani kwenye kamati za muhimu za usimamizi wa fedha za umma kinyume na misingi ya utawala bora.


Katika kikao cha tatu tarehe 10 Februari mara baada ya maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni ya 68 (7) kutokana na kauli ya Spika ya kumtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuthibitisha papo kwa papo bungeni juu ya uongo wa Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni 63 (3) (4) na 68 (1). Nilimueleza Spika kwamba Lema hakutumia kanuni 68 (1) ya ‘kuhusu utaratibu’ kama Spika alivyodai bali alitumia kanuni 68 (7) ya kuomba muongozo wa Spika wa hatua gani za kuchukua iwapo kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu analidanganya bunge. Aidha nilimkumbusha Spika kuwa alishatoa muongozo kuwa alete taarifa hivyo hakupaswa kutoa ushahidi wa papo kwa papo. Kauli yangu ilimfanya Spika atoe mwongozo mwingine wa kumtaka Lema awasilishe maelezo yake tarehe 14 Februari katika kikao cha asubuhi.


Katika kikao cha nne tarehe 11 Februari nilitoa mchango wangu wa papo kwa papo bungeni wakati wa hoja ya kujadili Hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge jipya. Katika hotuba hiyo niliwashukuru wananchi na kuzungumzia suala la viongozi kuepuka kupandikiza mbegu ya udini, haja ya kukabaliana na mfumuko wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha, suala la kufufua viwanda na jitihada za kukabiliana na matatizo ya maji katika jimbo la Ubungo. Nilianza hotuba hiyo kwa kuweka katika kumbukumbu za historia namna tulivyoshinda Ubungo kwa nguvu ya umma ya wazee, wanawake na vijana pamoja na vikwazo vya kikatiba na kisheria. Katika hotuba hiyo nimetaka vyombo vya ulinzi na usalama vimshauri Rais na viongozi wengine kuacha kutoa kauli za mara kwa mara ambazo kimsingi ndizo zinazopandikiza udini. Aidha nimeitaka serikali kuwasilisha taarifa ya hali halisi kuhusu mfumuko wa bei na hatua ambazo inapendekeza zichukuliwe ili kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha ambapo kunaweza kuleta migogoro katika taifa. Nilidokeza kuhusu mwelekeo wa kufa kwa kiwanda cha Urafiki Ubungo na kueleza kusudio la kuwasilisha maelezo binafsi kuhusu suala husika. Nilieleza Bunge kuhusu Kongamano la Maji Ubungo na kueleza dhamira yangu ya kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutatua kero husika. Sikuendelea zaidi kwa kutokana na muda wa dakika kumi kuisha hata hivyo niliwasilisha mchango wa ziada wa maandishi kuhusu ufisadi hususani kuhusu Dowans na Kagoda na michezo ikiwemo suala la kurudishwa kwa viwanja vya umma ambavyo vimehodhiwa na chama kimoja baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi ( Bonyeza hapa kusoma hotuba husika: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/hotuba-yangu-bungeni-katika-mkutano-wa.html )


Katika kikao cha tano tarehe 14 Februari mara baada ya kipindi cha maswali na kauli za mawaziri Spika aliruhusu moja kwa moja Hoja ya Kujadili Hotuba ya Rais ya kufungua bunge kuendelea. Nilitaka muongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni 68 (7) na 63 (6) ambayo inatoa fursa ya mbunge kutoa uthibitisho wa ukweli bungeni ili Lema apewe nafasi ya kuwasilisha maelezo yake bungeni katika kipindi hicho cha asubuhi kama alivyoelekeza Spika mwenyewe katika kikao cha tatu. Hata hivyo, Spika alitoa muongozo mpya kuwa Lema awasilishe maelezo na ushahidi wake kwa maandishi ofisini kwake. Katika kikao hicho pia niliuliza swali la nyongeza baada ya majibu ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa Swali namba 65 ambapo nilihoji kwa kuwa waraka wa kutengua utaratibu wa wahitimu wenye stashahada wenye kupaswa kurudia mitihani michache kufanya hivyo wakiwa kazini ulisambazwa ukiwa umechelewa huku wakitakiwa kulipia ada ya mitihani na kujiandaa je serikali iko tayari kutoa muda wa nyongeza zaidi ya uliotangazwa wa mwezi Aprili? Katika majibu yake naibu waziri alieleza kwamba serikali itatoa muda mwingine wa walimu hao kufanya mitihani yao ikiwa wakishindwa kufanya mwezi Aprili hata hivyo serikali iliwahimiza wafanye hivyo wakati huu ili kuepuka ushindani wa nafasi za ajira utakaokuwepo kipindi kijacho.


Katika kikao cha sita tarehe 15 Februari mara baada ya kauli za Mawaziri ambapo Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya umeme nchini na utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi kifupi na cha kati nilitoa hoja ya dharura kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (e) na kanuni ya 47 ili bunge lijadili jambo la dharura la mgawo wa umeme unaolikumba taifa. Nilitaka jambo hilo lijadiliwe kwa kutoa maelezo ya namna linavyowathiri maisha ya wananchi waliowengi na pia kuathiri uchumi wa taifa. Pia, nilieleza kwamba katika kauli yake Waziri ameeleza hatua za dharura zinazotaka kuchukuliwa na serikali ambazo nyingine kimsingi sio za dharura na pia zinahusisha matumizi makubwa ya fedha za wananchi ambazo nilizikadiria kuwa ni zaidi ya bilioni 300 nje ya bajeti ya serikali hivyo ni muhimu bunge likajadili. Spika wa Bunge akaikataa hoja hiyo pamoja na kuwa iliungwa mkono na idadi ya wabunge inayohitajika badala yake akanitaka kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nikazungumzie mambo hayo kwenye kikao cha kamati husika hapo baadaye. Kimsingi nilitaka suala hilo lijadiliwe kwa sababu katika maelezo yake Waziri alitaja kuwa serikali inakusudia kukodi mitambo ya dharura ya MW 260 (hii ni mitambo ambayo gharama yake ni kubwa sana, na inaweza kuchelewa isije wakati wa dharura kama ilivyokuwa kwenye sakata la Richmond), pia Waziri hakuzungumzia kabisa kuhusu mitambo ya Dowans ambayo asubuhi ya siku hiyo nilizungumza LIVE na TBC1 na kutaka serikali iitaifishe mitambo husika kwa kutumia sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo ili iiwashe kwa dharura na kupunguza pengo la MW 120 wakati taifa likiendelea kufanya maamuzi ya namna ya kufidia kiwango kitachobaki. Aidha mjadala huo ungewezesha pia kutaka waziri awajibike kwa kutochukua hatua za mapema za kukabiliana na kinachoitwa dharura ambacho kilishafahamika toka mwaka 2006, 2008 na 2009 na maamuzi ya kuondokana na hali hiyo yakafanyika lakini hayakutekelezwa kwa wakati ( Bonyeza hapa kwa kauli ya awali kuhusu Dowans na mgawo wa umeme: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/mitambo-ya-dowans-itaifishwe-waziri.html)


Katika kikao cha saba tarehe 18 Februari niliuliza Swali la Nyongeza kutokana na majibu ya Swali namba 85 kwa Wizara ya Maji. Kwenye swali langu la Nyongeza kwanza nilimkosoa Naibu Waziri kwa kutaja majina ya miradi ya maji ambayo iko Kigamboni na kueleza kwamba ni ya Ukonga na kumweleza Naibu Waziri kuwa pamoja na uwekezaji wa fedha za miradi ya maji za Benki ya Dunia na Wadau wengine wa maendeleo kwenye Ruvu Juu na Ruvu chini ikiwemo kuweka mtandao mpya wa mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya wachina; bado maji kwenye kata za Kwembe, Kibamba, Msigani, Mbezi, Saranga, Kimara nk maji hayatoki kwa pamoja na mambo mengine upotevu wa maji na wafanyabiashara wanauza maji bei juu kujiunganishia kinyemela; je Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa? Naibu Waziri alijibu kwa kunipongeza kwa kuweka kipaumbele cha kwanza suala la maji katika kazi zangu na kuahidi kutembelea miundombinu husika kwa kushirikiana nami. Pia, niliuza Swali namba 91 kwa niaba ya Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi kwa Wizara ya Fedha kuhusu kero za upatikanaji wa mafao ya wastaafu na mirathi kwa watumishi waliokufa kazini. Baada ya majibu ya Waziri kueleza kwamba sababu ni matatizo ya mawasiliano ukiwemo udhaifu katika mfumo wa kumbukumbu kwa upande wa watumishi wanaohudumiwa na mifuko; niliuliza maswali mawili ya nyongeza, moja kuhusu namna ambavyo serikali imepanga kuondokana na matatizo hayo ya mawasiliano na kumbukumbu hasa kwa kuwa wapo wastaafu na marehemu ambao kumbukumbu zao zote zimekamilika lakini bado kuna kero nyingi katika kupata mafao na mirathi. Pili, niliuliza swali la kutaka tamko la serikali kuhusu wastaafu wengine ambao hawahudumiwi na mifuko kama wale wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki ambao mpaka sasa wanahangaika kuhusu mafao yao. Serikali ilijibu kuwa haina tamko la kutoa kwa sasa kwa kuwa inasubiri kwamba suala la Wastaafu wa Afrika Mashariki lipangiwe jaji mwingine katika mahakama ya rufaa kama walivyoomba.


Kwa muktasari huo ni mrejesho kuhusu ushiriki wangu ndani ya vikao vya mkutano wa pili wa bunge la kumi. Hata hivyo, kuna masuala mengine yanayohusu ushiriki wangu katika shughuli nyingine za kibunge nje ya vikao kwa nafasi zangu zingine kama Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA, Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam, Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo, Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani-Nishati na Madini na nafasi nyinginezo ambayo sijayaeleza katika taarifa hii. Nawashukuru sana wote walitoa maoni kwenye Mikutano ya Mbunge kuwasikiliza na kuzungumza na Wananchi tuliyoifanya Mbezi mwisho na Manzese Bakhresa siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano wa pili wa bunge, sehemu ya masuala mliyonituma nimeyawasilisha. Hata hivyo yako mengine kutokana na ufinyu wa muda na kubanwa na kanuni sikupata wasaa wa kuyawasilisha ikiwemo suala la hoja ya mchakato wa katiba mpya ambalo nililitolea kauli ya tahadhari baada ya serikali kukubaliana nami mchakato husika kuanzia bungeni kwa kutungwa kwa sheria (Rejea kauli yangu ifuatayo: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/tahadhari-kuhusu-serikali-kupeleka.html). Nawashukuru kwa kuniunga mkono. Tuendelee kuwasiliana, kushauriana na kushirikiana.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

Tahadhari kuhusu serikali kupeleka muswada wa katiba mpya bungeni

Nimepokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kama nilivyokuwa nikitoa mwito kwa nyakati mbalimbali.

Nimepokea kwa tahadhari kwa kuwa bado kauli za serikali kuhusu mchakato husika zina utata kwa kuwa hotuba ya Rais Kikwete ya tarehe 5 Februari 2011 pamoja na kutaja kuwa katiba mpya itapitishwa kwa kura za maoni, haikueleza iwapo Mkutano Mkuu wa Kikatiba utaitishwa katika hatua za awali za mchakato husika. Utata huu unaongezeka zaidi kwa kuwa Waziri Mkuu Pinda akilihutubia bunge tarehe 8 Februari 2011 pamoja na kueleza kwamba muswada kuhusu mchakato husika utawasilishwa kwenye mkutano wa tatu wa bunge mwezi Aprili, ameelezea kuwa sheria husika itahusu kuundwa kwa tume.

Natoa kauli ya kuitaka serikali iwapo muswada unaopelekwa bungeni mwezi Aprili iwapo utaweka utaratibu wa kuitishwa kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba kuanzia hatua za awali pamoja na mwishowe kupigwa kwa kura kwa kura za maoni. Ni muhimu kwa tume ya mchakato wa katiba kuandaliwa hadidu rejea zake na kuundwa na mkutano wa kikatiba ambao utaweka tunu/misingi muhimu kabla ya kuanza kwa mchakato, ili tume ikusanye maoni, ipeleke rasimu kwa mkutano mwingine wa kikatiba na hatimaye katiba ithibitishwe kwa kura ya maoni. Natoa mwito pia kwa serikali kutoa ufafanuzi iwapo sheria husika inayokusudiwa kutungwa itagusa marekebisho ya katiba ibara ya 98 ili kutoa uhalali kwa katiba mpya kupitishwa na umma kupitia mkutano wa kikatiba na kura za maoni badala ya bunge pekee ambalo kwa sasa ndicho chombo chenye mamlaka ya mabadiliko ya katiba.

Pamoja na kauli nilizozisoma kwenye vyombo vya habari za hivi karibuni zikinukuu ofisi ya bunge na hoja ya katiba, bado taarifa yangu ya hoja husika niliyoiwasilisha tarehe 27 Disemba 2010 bado ipo katika ofisi husika na nitamwandikia katibu wa bunge kupata majibu rasmi kuhusu suala husika kabla ya kutoa kauli kuhusu hatma ya mimi kuwasilisha maelezo ya hoja na hoja husika kama nilivyotakiwa na ofisi husika.
Ikumbukwe kwamba msimamo wa awali wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu mabadiliko ya katiba alioutoa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 17 Disemba 2010 ulikuwa na kumshauri Rais aunde jopo shirikishi ili kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Kutokana na msimamo huo tarehe 19 Disemba 2010 nilifanya Mkutano na waandishi wa habari na kupinga msimamo huo na kueleza kwamba ni muhimu kwa mchakato wa katiba mpya kuanzia bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika badala ya kuundwa kwa jopo shirikishi la wataalamu kama alivyotaka Waziri Mkuu. Aidha katika mkutano huo nilipingana na azma ya Waziri Mkuu Pinda ya kutaka marekebisho ya katiba badala yake nikaitaka serikali itangaze rasmi kuanzisha mchakato wa katiba mpya. Katika Mkutano huo na waandishi wa habari nilidokeza kuwa kutokana na serikali kutoa msimamo wa kutokupeleka hoja au muswada wa serikali bungeni wa kuratibu na kusimamia mchakato husika nitalazimika kupeleka hoja binafsi bungeni ili bunge litipishe maazimio ya kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya ili hatimaye kuwezesha kutungwa kwa sheria ya kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Tarehe 27 Disemba 2010 nilitekeleza azma hiyo kwa kuwasilisha taarifa ya hoja kwa katibu wa bunge ya kutaka kuwasilisha hoja ili bunge lipitishe azimio la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kupitisha utaratibu wa kisheria wa kuratibu na kusimamia mchakato mzima. Katika Mkutano wangu na waandishi wa habari siku hiyo nilieleza kwamba baadhi ya mambo ya msingi yatayozingatiwa katika hoja binafsi ni pamoja na kuhakikisha kwamba kunatungwa sheria ya kuwezesha kuitishwa kwa mkutano mkuu wa taifa wa kikatiba, tunatunga sheria ya kuwezesha tume ya kuratibu mchakato husika kuundwa kwa sheria ya bunge badala ya kuteuliwa na Rais, kutoa kwa mujibu wa sheria elimu ya uraia kwa umma kuhusu maudhui na mchakato husika na kuweka utaratibu wa kisheria wa kuwezesha kufanyika kwa kura za maoni.

Tarehe 31 Disemba 2010 Rais Jakaya Kikwete akilihutubia taifa akatangaza kukubaliana na suala la kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya na kutangaza dhamira yake kuwa ya kuunda tume ya kusimamia mchakato husika na hatimaye vyombo vya kikatiba kufanya mabadiliko husika.

Tarehe 2 Januari 2011 nilitoa kauli yangu kwa umma ya kuitaka serikali kutoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Rais Kikwete na kueleza bayana iwapo serikali inakubaliana na hoja ya kupeleka suala husika ili mchakato uratibiwe na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge itayaozingatia kufanyika kwa mkutano wa kitaifa wa katiba, kuundwa kwa tume kwa mujibu wa sheria badala ya uteuzi wa Rais na hatimaye kufanyika kwa kura za maoni; na nikaeleza bayana kwamba wakati nasubiria ufafanuzi wa serikali taarifa yangu ya hoja binafsi kuhusu katiba inaendelea.

Tarehe 7 Januari 2011 badala ya kutoa ufafanuzi na kueleza azma ya serikali kupeleka suala husika bungeni Rais Jakaya Kikwete akarudia tena mbele ya mabalozi kwenye hafla ya mwaka mpya kuwa anakusudia kuunda moja kwa moja tume ya kuratibu na kuongoza mchakato mzima wa maoni bila kuhusisha bunge katika hatua za msingi.
Kutokana na serikali kuendeleza msimamo huo tarehe 9 Januari 2011 nilitoa tamko kwa umma la kupinga utaratibu wa Rais kuunda moja kwa moja tume ambapo ni kuendeleza hodhi ya serikali na kusababisha mapitio (review) ya katiba na hivyo kuendeleza kasoro za msingi kama zilivyojitokeza katika vipindi vilivyopita. Katika tamko langu hilo nilieleza wazi kuwa kama serikali itaendelea na msimamo wake wa kutaka kuunda tume ya Rais badala ya mchakato husika kuanzia bungeni hali hiyo itadhihirisha serikali kutokuwa na dhamira ya kuandikwa kwa katiba mpya na umma wenyewe. Kutokana na hali hiyo nilitoa tamko ya kuendelea na uamuzi wangu wa kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili mchakato husika uanzishwe kwa maazimio ya bunge na kusimamia kwa sheria itayotungwa na bunge.

Siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa bunge (ambao umeanza tarehe 8 Februari 2011 ) hatimaye serikali kupitia Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda imeeleza dhamira ya kulipeleka suala la mchakato wa katiba mpya bungeni kupitia kuwasilisha muswada wa serikali na hivyo kubadili msimamo wa awali wa kutaka kuunda moja kwa moja tume ya Rais na kukubaliana na sehemu ya hoja yangu ya kutaka mchakato husika kuanzishwa na kusimamiwa kwa sheria iliyotungwa na bunge.

Wakati wote nimekuwa nikisisitiza kuwa ipo haja ya suala hili la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Rais Jakaya Kikwete akihutubia Mkutano wa CCM tarehe 5 Februari 2011 alitoa kauli kuwa Kiserikali matayarisho yanaendelea ya kupeleka Bungeni Mswada wa Sheria wa kuanzisha mchakato wa katiba mpya ikijumuisha kuundwa kwa Tume ya kuongoza mchakato huo. Aidha katika Mkutano huo Rais Kikwete aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura ya maoni itakayoidhinisha katiba hiyo.
Kwa upande mwingine Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisoma tamko la serikali bungeni tarehe 8 Februari 2011 alisema kwamba serikali katika kuitikia mwito wa wananchi kuundwa kwa katiba mpya imetangaza kuwa itawasilisha bungeni muswada wa kuundwa kwa tume itayoratibu mchakato wa katiba mpya katika mkutano wa tatu wa bunge la kumi Aprili mwaka 2011.


John Mnyika
Mbunge Ubungo
09/02/2011- Dodoma

Mitambo ya Dowans itaifishwe, Waziri ajieleze kuhusu mgawo wa umeme

Naomba kutoa taarifa kwa umma kwamba sijawahi kutoa kauli popote ya kushauri Dowans ipewe mkataba wa miezi mitatu kama ilivyonukuliwa na chombo kimoja cha habari.

Gazeti la Mtanzania toleo namba 5388 la tarehe 16 Februari 2011 limeandika katika ukurasa wake wa kwanza kwamba “ Wabunge: Dowans iwashwe”; “January, Mnyika washauri mkataba wa miezi mitatu”.

Gazeti la Mtanzania limetaja kuwa chanzo chake ni mahojiano ya kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na TBC1 asubuhi ya tarehe 15 Februari 2011.

Napenda watanzania wenzangu wakumbuke kwamba kipindi hicho kilirushwa LIVE na katika kipindi husika hakuna kauli yoyote niliyoitoa ya kutaka mitambo ya Dowans iwashwe kwa mkataba wa miezi mitatu badala yake niliitaka serikali itumie sheria hususani ya uhujumu uchumi kuiwasha mitambo husika kwa maslahi ya taifa.

Katika kipindi hicho nilitoa kauli hiyo na kueleza kwamba nisingependa kwenda ndani zaidi katika hatua kwa wakati huo. Kauli yangu hiyo imenukuliwa kwa usahihi na Gazeti la Mwananchi toleo namba 03888 la tarehe 16 Februari 2011 katika ukurasa wa nne.

Ningependa kutumia fursa hii kusisitiza mtazamo wangu kwamba ni muhimu ili kupunguza adha ya mgawo wa umeme serikali itumie mamlaka yaliyopo kwenye katiba na sheria ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi, sheria ya kupambana na rushwa, sheria ya mali zilizopatikana isivyo halali nk itaifishe mitambo hiyo haraka iwezekanavyo na kuiwasha kwa maslahi ya umma.

Ikumbukwe kwamba kampuni ya Dowans ilirithi mkataba toka kampuni ya Richmond ambayo ilithibitishwa kwa maazimio ya bunge kuwe ilipata mkataba katika mazingira ya ukiukwaji wa sheria ikiwemo sheria ya kupambana na rushwa. Pia, hata kampuni yenyewe ya Dowans kuna utata kuhusu usajili, umiliki na uhamasishaji wa mkataba wake kama suala zima likitazamwa kwa undani wake yakirejewa yaliyojiri Costa Rica na Tanzania.

Kampuni ya Dowans kama inataka kuepusha kutaifishwa basi wamiliki wake popote pale walipo duniani wajitokeze hadharani wakiri kwamba walipotoshwa na Richmond pamoja na vyombo vya kiserikali wakati wa kuhamishwa mkataba ili wajijengee uhalali wa kufanya majadiliano ikiwemo ya kufuta madai ya fidia inayotaka kutolewa kwa mujibu wa hukumu ya ICC.

Aidha wakati mjadala kuhusu MW 120 za Dowans ukiendelea na kwa kuwa kiasi hicho hakiwezi kuziba pengo la takribani MW 240 ambalo linakabili taifa hivi sasa, ni muhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua ambayo serikali inataka kuchukua ya kukodi mitambo ya MW 260. Aidha, Waziri atoe ufafanuzi wa kutokukamilika kwa mipango ya serikali wakati ambapo dharura ya umeme ilijulikana toka mwaka 2002, serikali ikaijadili kwa kina mwaka 2006, bunge likapitisha maazimio mwaka 2008 na serikali ikaahidi tena mwaka 2009 kuweka utaratibu wa kukabiliana na dharura hiyo. Katika muktadha huo ni muhimu kwa bunge kupata fursa ya kujadili kwa kina suala la umeme katika mkutano unaoendelea wa bunge kama jambo la dharura ili kuweza kulinusuru taifa. Nitatoa tamko la kina hivi karibuni kwa nafasi yangu ya uwaziri kivuli kuhusu suala la umeme kwa kuzingatia hali ya mgawo inavyoendelea sanjari na kupanda kwa gharama za nishati hiyo kunakoongeza ugumu wa maisha kwa watanzania walio wengi baada ya majadiliano na baraza kivuli na mamlaka nyingine husika.

Imetolewa Dodoma leo tarehe 16/02/2011

John Mnyika (Mb)
0784222222

Hotuba yangu Bungeni katika Mkutano wa Pili

Mchango wangu wa papo kwa papo bungeni wakati wa hoja ya kujadili Hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge jipya. Mchango huu niliutoa tarehe 11 Februari 2011 katika kikao cha nne cha mkutano wa pili wa Bunge la kumi katika hotuba hii niliwashukuru wananchi na kuzungumzia suala la viongozi kuepuka kupandikiza mbegu ya udini, haja ya kukabaliana na mfumumo wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha, suala la kufufua viwanda na jitihada za kukabiliana na matatizo ya maji katika jimbo la Ubungo.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kutoa mchango rasmi, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako tukufu kuingiza kwenye historia ya Taifa hili kwamba safari yangu kufika hapa ilikuwa ndefu kidogo, ilianza mwaka 2005. Lakini, kwa sababu ya udhaifu wa mifumo yetu ya kikatiba na ya kisheria ya usimamizi wa haki, safari hii imekuwa ya miaka mitano na nimefika leo hapa kwa nguvu ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wazee wa Jimbo la Ubungo bila kujali tofauti za vyama, Jimbo lenye wakazi - wapiga kura 450,000 ambao waliona wanitume mtoto wao nije kuwawakilisha. Nawashukuru vile vile wakinamama wa Jimbo la Ubungo, wanawake ambao katika kipindi kigumu sana cha kampeni walikuwa wakiniombea kwa Mwenyezi Mungu na leo nimefika hapa salama. Lakini, zaidi niwashukuru vijana wenzangu wa Tanzania nzima na Jimbo la Ubungo, vijana wa mtaani, vijana wafanyakazi na vijana wa vyuo vikuu ambao walikuwa tayari kukesha kwa siku tatu kulinda ushindi mpaka tukatangazwa. Ahadi yangu kwao ni kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitano cha utumishi wangu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumza leo tukiwa wakati pekee sana kwenye historia ya Taifa letu. Tunazungumza ikiwa ni miezi michache kuelekea kuadhimisha miaka 50 toka Taifa letu lipate uhuru. Lakini tunazungumza wakati ambapo Taifa likikabiliwa na mgawo wa umeme miaka 50 baada ya uhuru, Taifa likikabiliwa na matokeo mabovu ya wanafunzi miaka 50 baada ya uhuru, Taifa likikabiliwa na kupanda kwa hali ya juu kwa gharama za maisha ambapo kunasababisha tishio la migomo mbalimbali. Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu tunazungumza leo wakiwa wamerudishwa nyumbani kwenye vyuo mbalimbali, migomo ya wafanyakazi na mambo mengine yote haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yangeweza kutupa sababu ya kukata tamaa. Lakini, mimi ninayo sababu ya kuwa na matumaini. Nina matumaini kwa sababu tupo kwenye chombo hiki na natarajia kwamba hatutaendekeza itikadi na maslahi ya vyama, badala yake tutasimamia maslahi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na upungufu wake, Ibara ya 63 inazungumza kwamba hiki ndiyo chombo kikuu kwa niaba ya wananchi waliotutuma chenye wajibu wa kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, naomba nieleweke tu hapa, tunapokosoa, tunapounga mkono, ni sehemu ya kuishauri Serikali, ni sehemu ya kuisimamia Serikali. Natarajia kwamba Wabunge kwa umoja wetu hatutajigeuza kuwa na jukumu la Serikali, badala yake tutaendelea kuwa na jukumu la kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwanza, mimi ningeomba niishauri Serikali kwa kweli. Ili tuweze kufika Desemba 9 tukiadhimisha uhuru tukiwa na sababu ya kuadhimisha uhuru kwa maana ya kusherehekea, lazima Serikali iamue kwa dhati, Bunge lijalo la mwezi Aprili, lilete mapendekezo ya msingi wakati tunatengeneza vipaumbele vya bajeti ya safari hii. Ni mambo gani ya haraka ambayo kama Taifa tunaweza tukafanya kwa umoja wetu, kwa makubaliano yetu ili ikifika Desemba, pamoja na yote yaliyojitokeza miaka 50 iliyopita, tuseme walau hapa tuna sababu ya kujivunia; na nitasema machache:- (Makofi)


[MHE. JOHN J. MNYIKA]

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Rais na nitaichangia kwa uchache wa maneno. Rais amezungumza vipaumbele mbalimbali. Ukurasa wa 12 na 13 amegusia suala la umoja wa kitaifa na hili ni jambo ambalo hatupishani kwa sababu hata Ngao ya Taifa letu inasema Uhuru na Umoja. Lakini, kuna jambo moja mimi ningependa nitoe tahadhari, suala la udini. Hotuba ya Rais ukurasa 12 inazungumza kwamba Tanzania ni moja, watu hawabaguani, kwa hiyo Tanzania hakuna mgawanyiko hata wa kidini. Lakini ukurasa wa 13 unasema kuna mpasuko wa kidini. Mimi ningeomba vyombo vya Ulinzi na Usalama vikamshauri Rais kwamba kadri viongozi wa juu tutakavyoendelea kupiga kelele nyingi sana za udini, ndiyo kadri tunavyopandikiza mbegu ya udini kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuja kwenye kikao hiki, nimezunguka vijiweni, nimekaa vijiweni, Watanzania ni wamoja kweli kweli, tusije viongozi ndiyo tukasababisha mgawanyiko miongoni mwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie eneo lingine: Rais amezungumza kuhusu kukuza uchumi na ukurasa wa 15 amezungumzia suala la kupanda kwa bei ya mafuta n.k kwenye Soko la Dunia na chakula kama sehemu ya matatizo ya kimaisha ambayo yalitokea mwaka 2007. Mimi ningeomba tu Serikali ituletee taarifa Bungeni kuhusu hali halisi. Takwimu hapa kwa mujibu wa hotuba ya Rais inaonyesha kwamba mfumko wa bei ni asilimia 4.2. Wakati Rais anazungumza, bei ya sukari kilo moja ilikuwa shilingi 1200/=, leo tunazungumza kilo moja imepanda mpaka shilingi 2000/=. Gharama za maisha zinapanda kwa ari, kasi na nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ikatuletea pendekezo la namna gani Tanzania inakabiliana na tatizo hili la kupanda kwa gharama za maisha. Tunaweza kuwalaumu wanafunzi kwa nini wanagoma kwamba wanalipwa 5000/= lakini wanalalamika, huku bei ya chakula inapanda! Sasa kuwalaumu wafanyakazi kwa nini wanalalamika, wanataka kuandamana, bei ya umeme imepanda, kama hatutadhibiti kupanda kwa bei, tunatengeneza mgogoro kwenye Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais amezungumza kuhusu kufufua viwanda, mimi niseme tu kwamba kazi hii ni nzito, inahitaji vile vile kama Taifa tuzungumze hivyo viwanda vilivyokufa vilikufaje. Mimi pale Jimboni kwangu Ubungo kuna Kiwanda cha Urafiki ambacho Tanzania ilikuwa inamiliki mwanzoni, sasa hivi ina hisa 49 peke yake. Kiwanda kinaelekea kufa, uzalishaji sasa hivi ninavyozungumza, wafanyakazi wamepewa likizo, tena wamepewa likizo kwa asilimia 50 tu ya malipo. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili la Urafiki nitaliletea maelezo kwa sababu ni suala la kina sana, kuuzwa kwa mitambo n.k. Nitawaletea maelezo.

Mheshimiwa Spika, lakini, itoshe tu niingie kwenye eneo la msingi ambalo ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Ubungo, nayo ni maji. Mheshimiwa Rais, amezungumza kuhusu ongezeko la mgawo wa fedha za bajeti kwenye maji na amezungumza kuhusu Miradi ya Benki ya Dunia. Lakini, mimi nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Maji na nimwahidi tu kwamba tulifanya kongamano la maji tarehe 31 Ubungo, tukayajua matatizo na nitaleta taarifa kamili kwake kama ambavyo tumekubaliana na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano. Tunahitaji, pamoja na mipango ya muda mrefu ya ujenzi wa mabwawa ya Kidunda, miradi ya Kimbiji, Mpera n.k. Mheshimiwa Spika, nashukuru! (Makofi)

Monday, February 14, 2011

Katika Utumishi wa Uwakilishi


Nikiwawakilisha wananchi wenzangu wa Jimbo la Ubungo mlionipa ridhaa.
"Maslahi ya Umma Kwanza"

Saturday, February 5, 2011

Mkutano wa Hadhara Kukusanya Maoni: 06/02 Manzese Bakhressa

Ndugu zangu wananchi,
Miongoni mwa ahadi zangu kwenu wakati nikiomba ridhaa ya uwakilishi katika chombo cha maamuzi ilikuwa ni kuhakikisha nachochea katika kukuza uwajibikiji na utawala wa kidemokrasia wakilishi.

Nitakuwa na mkutano wa hadhara wa kukusanya maoni yenu na kusikiliza ninyi wananchi ambao mmenipatia ridhaa niwawakilishe bungeni kabla ya kwenda kuanza vikao vya kibunge.

Nitazimiza ahadi na utashi wangu wa kuwa na mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi kabla ya kwenda katika vikao vya bunge. Na zaidi kutoa tunu na thamani halisi ya uongozi wa uwakilishi kwa ninyi kunituma kuwa sauti yenu katika kufanya maamuzi!

Mkutano utakuwa J2 06/02/2011 Mahala:Manzese Bakhresa Muda:Kuanzia saa 10 mpaka 12 jioni.

Ikumbukwe Dodoma kazi zinaanza kuanzia tarehe 7, mkutano tarehe 8.

Tuhimizane kujitokeze kwa wingi. Tushirikiane.Inawezekana. Tufanye sasa!

Maslahi ya Umma Kwanza!!

Baruapepe kwa Ofisi ya Mbunge: mbungeubungo@yahoo.com

Thursday, February 3, 2011

RIPOTI YA KONGAMANO LA MAJI JIMBO LA UBUNGO TAREHE 31.01.2010

Utangulizi:
Kongamano la maji jimbo liliandaliwa na Ofisi ya Mbunge jimbo la ubungo ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Maji Ubungo (Rwegalulila). Kongamano lilikua na mada kuu mbili; Mosi ni sera, sheria na mikakati ya sekta ya maji safi na maji taka- fursa na changamoto kwa wananchi wa jimbo la ubungo. Pili, hali halisi ya upatikanaji wa maji jimbo la ubungo na wajibu wa wadau mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la maji.

Zaidi ya wadau 200 walishiriki kongamano na kupata fursa ya kujadili hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kukabiliana na kero zinazohusu sekta ya maji katika muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Pamoja na kuwa wadau muhimu kama Dawasco na Wizara ya Maji walitumiwa mwaliko kushiriki na kutoa mada katika kongamano hilo cha kushangaza hawakuweza kushiriki kabisa na sababu zilizotolewa hazikua na msingi wowote lakini kongamano liliendelea na kufikia kutoa maazimio.

Wadau waliohudhuria:
Pamoja na wadau wakuu kwa maana ya Wizara ya Maji na Dawasco kushindwa kufika na kutoa mada lakini wadau zaidi ya 200 waliweza kuhudhuria na kushiriki katika kongamano, hawa ni pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wirara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni, Ewura, Ofisi ya Ubunge Jimbo la Ubungo, Maafisa Watendaji, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa mbalimbali, Asasi za kiraia kama HakiElimu, Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI), Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT) na wadau wa maendeleo kama Care International, Wawakilishi wa Uongozi wa Chuo cha Maji pamoja na wanafunzi, Vyombo vya Habari pamoja na wananchi mbalimbali.

Mjadala:
Mwenyekiti wa kongamano alianza kwa kuchokoza mjadala kwa kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kama ifuatavyo;
i. Kinachotakiwa kufanyika kutatua kero ya maji katika jimbo la Ubungo: mwenyekiti aligusia mipango ya muda mrefu ya utatuzi wa kero ya maji kama ilivyoainishwa katika ripoti ya Mkukuta ya July 2010 kuwa kero ya maji inatakiwa kuwa imekwisha ifikapo mwaka 2013. Pia kuchimba visima vikubwa Kimbiji na bwawa la Kidunda kama ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 24.05.2010 alipotembelea Kimara na pia tarehe 17.10.2010 na 28.10.2010 alirudia ahadi hiyo hiyo. Hili kwa Mwenyekiti/ Mbunge ni suluhisho la muda mrefu

ii. Tafiti zilizofanywa na watu mbalimbali; mwenyekiti aligusia kuwa wapo wananchi ambao ni wakazi wa jimbo la ubungo ambao kwa umoja wao na kuguswa na tatizo sugu la maji waliamua kufanya tafiti zao za kitaalamu ambazo zililenga kutatua kero ya maji na kugundua kuwa kwa siku wananchi katika jiji la Dar es Saalam wanahitaji kutumia lita 450,000 milioni kwa siku lakini kwa sasa ni lita 300,000 milioni ndizo zinazozalishwa. Kwa maana hiyo lita 150,000 milioni ni pungufu ya mahitaji yanayohitajika kwa ajili ya kukidhi haja ya huduma hii. Hata hivyo tafiti hizo hizo zinaonyesha kuwa 50% ya maji yanayozalishwa kwa sasa yanapotea bila kuwafikia wananchi. Hata hivyo mwenyekiti alishauri kuwa ili kuanza kutatua kero hii ya maji kwa muda mfupi ni vizuri sasa mikakati ikawekwa ili kuzuia upotevu huo wa maji ambao ni wa kiasi kikubwa sana. Upotevu huu wa maji husababishwa na viunganishi visivyo halali katika mtambo wa Ruvu juu ambao hufikia 15% kwa mtambo husika pekee.

iii. Ziara ya Mbunge makao makuu Dawasco; katika ziara ya Mbunge makao makuu ya Dawasco mnamo tarehe 19 Januari 2011 na kuelezwa pamoja na mambo mengine kuwa kero ya maji katika jimbo la ubungo husababishwa na mazingira ya kijiografia ambapo kuna miinuko inayosababisha maji kutokufika maeneo hayo kutokana na presha ya maji kuwa ndogo. Mwenyekiti/ Mbunge alishauri kuwa Liongezwe “tank” lingine au lile la Uluguruni ambalo halifanyi kazi lianze kutumika. Kama tatizo ni “pump” ya kusukuma maji ili kuwe na presha ya kusukuma maji ni vizuri “pump” inunuliwe ili kutatua kero ya maji kwa muda wa kati.

iv. Vioski vya maji; ilishauriwa na mwenyekiti kuwa vibanda hivi vya kuuzia maji ambavyo vipo na vimefungwa vifunguliwe na pia viongezwe vingine katika maeneo mbalimbali ya jimbo. Pia bei ya maji katika vioski hivi idhibitiwe ili kuepuka upangaji wa bei holela ambao huwaathiri wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa huduma hii. Hili lilishauriwa kuwa suluhisho la muda mfupi.

v. Ujenzi wa visima, changamoto kubwa iliyopo katika ujenzi wa visima ni kuwa maeneo mengi ni ya miinuko kwa hiyo inabidi kuchimba visima kwa kina kirefu ambapo husababisha kutumia kiasi kikubwa cha fedha. Pia maji yanayopatikana katika maeneo mengi ni ya chumvi hivyo kuwa ni changamoto nyingine.

vi. Suluhisho la muda wa kati; mwenyekiti alidokeza kuwa sehemu kubwa ya jimbo la Ubungo inahudumiwa na mtambo wa Ruvu juu kasoro maeneo ya Goba, Mburahati na Mabibo ambayo huhudumiwa na mtambo wa Ruvu chini. Pia mwenyekiti aligusia kuwa serikali ya Marekani kupitia mpango wa MCC imetoa fedha kwa ajili ya kuongeza bomba lingine likini fedha hizo hazitoshi kwa kuwa hazifiki hata bilioni 200. Ili kupata suluhisho la muda wa kati mwenyekiti aliwaomba washiriki kujadili; Je hatuna vyanzo mbadala katika mapato ya serikali ili kutatua tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam?

vii. Majukumu ya wadau; mwenyekiti alipendekeza majukumu kwa wadau wachache katika kutatua kero ya maji;

 Manispaa ya Kinondoni: mwenyekiti alitoa pendekezo kwa Manispaa kujenga visima kwenye maeneo ya pembezoni na kushauri kuwa kwa mwaka jana Manispaa ilitarajia kujenga visima 7 idadi ambayo alisema ni ndogo sana kulingana na mahitaji yaliyopo.

 Ewura: sheria inayounda Dawasa inawataka Ewura kudhibiti matumizi na bei ya maji kwenye miradi iliyopo chini ya jumuia za wananchi lakini changamoto kubwa iliyopo ni utekelezaji, na aliwakaribisha washiriki kwa ajili ya mjadala juu ya swala hilo.

 Vyombo vya habari: wanatambulika kama wadau muhimu sana katika swala la huduma ya maji. Mwenyekiti aliwaomba wanahabari kushughulikia kwa karibu swala la maji ili kuleta msukumo wa uwajibikaji na hatimae kutatua kero hii ya muda mrefu.

MAAZIMIO YA KONGAMANO
Baada ya mjadala mrefu uliodumu kwa takribani masaa matatu ukiendeshwa na Mwenyekiti ambaye pia ndiye aliyechokoza mada husika, kongamano lilifikia maazimio yafuatayo kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika jimbo la ubungo;

i. Kongamano limelaani kitendo cha Dawasco kutohudhuria na kutoa mada bila sababu ya msingi huku wao wakiwa ni wadau wakubwa wanaolalamikiwa na wananchi katika kadhia hii nzito na ya muda mrefu sana. Juhudi kubwa ilifanywa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo kuwasiliana na Dawasco Makao Makuu na waliahidi kushiriki na kutoa mada lakini mpaka siku ya kongamano ofisi haikupokea ujumbe wa aina yoyote kuhusu ushiriki wao. Mawasiliano yalifamyika tena siku hiyo ya kongamano na ndipo walipokiri kuwa hawatashiriki kwa kuwa kazi yao ni ya kitaalamu na hivyo hawatakiwi kushiriki makongamano ya kisiasa. Hata hivyo kongamano hilo halikuwa la kisiasa bali wadau mbalimbali bila kujali dini au itikadi za vyama walishiriki na kutoa maoni yao na hata mamlaka ya serikali Ewura walishiriki, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nao pia walishiriki na kutoa maoni. Kwa kuzingatia hayo ndipo kongamano lilipofikia uamuzi wa kuwalaani Dawasco kushindwa kushiriki katika kongamano hilo lenye kutoa mwelekeo/utatuzi wa tatizo sugu la maji.

ii. Utendaji wa Dawasco utazamwe upya kimuundo
ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi. Hii ni kutokana na maeneo mengi kukosa maji huku wananchi wakiendelea kulipia bili za maji, hakuna mgawo wa maji ulio rasmi kwa maeneo yote ambapo huchangia maeneo mengine kuwa na maji muda mwingi na mengine kukosa kabisa, watendaji wa Dawasco kuwajibu vibaya wananchi pindi wanapofuatilia matatizo ya maji, watendaji wa shirika hilo kuwa na ushirikiano na wafanyabiashara wa maji nahata wengine kutuhumiwa kumiliki magari yanayouza maji. Haya na mengine yaliwafanya washiriki kuazimia kuwa kuna haja ya kulifanyia shirika tajwa maboresho makubwa ili kukidhi mahitaj ya wananchi.

iii. Watu wanaotumia bomba ambazo wameziunganisha na bomba kuu la maji bila idhini ya shirika (illegal connections) wafichuliwe mara moja na kuchukuliwa hatua na mianya hiyo ya upotevu wa maji ifungwe ili kuwezesha maji kuwafikia wananchi walio wengi. Hii ni pamoja na malalamiko yaliyotolewa kuwa wapo wafanyabiashara waliojiunganishia maji kwa ajili ya kuwauzia wananchi wanaokosa huduma hiyo. Vile vile maeneo ya Kibamba maji yanatumiwa kumwagilia bustani za michicha na miche ya miti, hii ni kwa sababu ya uunganishwaji kiholela wa maji katika bomba kuu.

iv. Wananchi wenye “pump” binafsi za kuvutia maji; hawa nao watazamwe upya kwa sababu wanafanya maji mengi kubaki katika maeneo yao na hivyo kufanya wale wasokua na kifaa hicho kupata maji kidogo au kukosa kabisa. Hali hii inawafanya wachache kuhodhi huduma ya maji na kufanya wengi kuzidi kutaabika. Hivyo swala hili linahitaji kutazamwa upya na ikiwezekana wazuiwe kutumia vifaa hivyo.

v. Sera ya Maji; hitaji la mabadiliko katika Sera ya Maji ili kuyatoa maeneo mengi ya Jimbo la Ubungo kutoka kuwa kwenye miradi ya maji vijijini na kuwa kwenye miradi ya maji mjini. Hii ni kutokana na maeneo mengi ya jimbo kushindwa kunufaika na miradi mingi ya maji kwa kuwa sera inayatambua kama maeneo ya vijijini.

vi. Kamati za Maji kila kata ziundwe upya na zipewe nguvu ya kisheria tofauti na sasa ambapo huwa zinakua za muda kutokana na mradi husika (interim committees). Madiwani walipewa jukumu la kuhakikisha sheria ndogondogo zinatungwa ili kuzipa nguvu kamati za maji. Pia kongamano liliazimia kuwa kamati ziwe zinapeleka ripoti Manispaa kuhusiana na hali halisi ya upatikanaji wa maji ili mamlaka husika zichukue hatua za haraka.

vii. Mradi wa barabara katika Kata ya Manzese uliharibu miundombinu ya Maji na bado ukarabati wa kurudisha mabomba yaliyoharibika haujafanyika. Kongamano liliazimia kuwa miundo mbinu yote iliyohariwa ifidiwe na kurudishwa ili wananchi waendelee kupata maji.

viii. Maeneo ya miinuko mabwawa na visima vya maji vijengwe ili kuwaondolea wananchi kero ya kukosa maji kwa sababu ya kijiografia.

ix. Mitaa mipya itengewe maeneo ambayo ni maalumu kwa maji taka; hii ni kwa sababu jimbo la ubungo kuna mitaa mingi sana ambayo ni mipya na haina maji taka. Hii itatunza mazingira lakini pia itazuia magonjwa ya mlipuko.

x. Kata ya Kwembe haina miundombinu ya maji kabisa na hivyo wananchi kuendelea na kupata adha ya kununua maji ya madumu kwa bei ghali sana. Pia Msakuzi maji yanauzwa shilingi 500 hali inayofanya wananchi kuishi maisha magumu sana.

xi. Vyanzo vya maji vitumike vizuri hii ikiwa ni pamoja na wananchi kuwa na utamaduni wa kuhifadhi maji ya mvua kitaalamu.
xii. Ewura; Pamoja na kuwa Ewura wana uwezo wa kudhibiti bei ya maji katika vioski na sehemu zinazomilikiwa na jumuia za wananchi bado nguvu kubwa iongezwe kuhakikisha maji yanauzwa kwa bei iliyokubaliwa. Na pia uandaliwe utaratibu wa kudhibiti pia bei za wafanyabiashara ya maji ambao hununua kwa bei ya jumuia na kuuza maji hayohayo kwa wananchi kwa bei kubwa mno.

xiii. Nguvu ya pamoja ya wananchi inahitajika ili kubuni miradi ya maji na pia kuweka mikakati ya kila mara na kushirikisha mamlaka husika kutatua tatizo hili.

xiv. Kongamano linatoa muda wa mwezi mmoja kwa Dawasco kuanza kutatua kero ya maji kwa hatua za muda mfupi ili kupunguza kero ya maji. Wakishindwa kufanya hivyo Mbunge wa Jimbo la Ubungo atalazimika kuwasilisha hoja binafsi Bungeni kuhusiana na tatizo hili katika kikao cha mwezi Aprili 2011.

HITIMISHO
Kamati ya maji ya kongamano iliundwa ikiwa na mwakilishi mmoja kutoka kila kata 14 za jimbo na pamoja na madiwani wote kutokana na wadhifa wao na hivyo kufanya idadi ya wajumbe kufikia 28. Kamati itashughulikia utekezaji wa maazimio na pia kuibua kero mbalimbali za maji katika maeneo ya jimbo la Ubungo. Kamati itafanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo.

Tuesday, February 1, 2011

Shukrani kwa Kongamano la Maji

Ndugu wananchi, wadau wa maji(wataalamu na taasisi),

Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mwitikio mzuri mliotoa kwa Kongamano la Maji 31.01.2011. Nawashukuru wote ambao walishiriki katika tukio, pia ambao walitoa mchango na maoni yao kwa njia ya simu, facebook na blogu. Asanteni sana!

Muda si mrefu, taarifa ya kina na picha za tukio zima zitakuwa humu kwa matumizi ya umma.

Hakika Umoja ni Nguvu, Tuzidi kushauriana, na kuungana katika kutafuta suluhu ya kero ya Maji na kero nyingine zinazokabili jimbo letu la Ubungo.

Daima maslahi ya Umma Kwanza.

©John J. MNYIKA.