Monday, July 29, 2013

Hali tete na tata ya kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT)- Hatua ambazo nimeanza kuzichukua

Katika siku za karibuni nimepokea malalamiko kuhusu hali tete na tata katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) kinachosimamiwa na kuendeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam. 

Kufuatia malalamiko hayo, nimechukua hatua zifuatazo mpaka sasa: Mosi, tarehe 15 Julai 2013 nilifanya ziara ya ghafla kujionea hali halisi, sehemu ya ziara hiyo inaweza kutazamwa kupitia: 
http://www.youtube.com/watch?v=JuPGoz-JI-I , ambapo nilibaini kwamba hatua za haraka zinahitajika. 

Nimeshuhudia hali ya uchafu ikiwemo utiririkaji wa maji machafu ndani ya Kituo cha Mabasi ambayo yanatuama na hadi kubadilika rangi na kuwa ya kijani ambapo ni hatarishi kwa abiria na watu wanaofanya shughuli zao ndani ya kituo. Pia, kuna vyoo vichache ukilinganisha na idadi ya abiria na watumiaji wengine wa Kituo. Hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Nimejulishwa hali ya usalama ndani ya kituo ni tete; usalama ndani ya kituo ni mdogo sana kwa abiria na nimepewa taarifa za matukio ya uhalifu ambayo yamesababisha pia madhara kwa abiria.

Nimetembelea kituo na kukuta kuna usumbufu mkubwa sana kwa abiria na watumiaji wengine wa Kituo baada ya maeneo ya awali ya kupumzikia kwa abiria na wasindikizaji kubomolewa. 

Thursday, July 25, 2013

Chenge (Mb) amesema kodi ya kadi za simu (SimCardTax) ni sahihi kwa utafiti wao; aulizwe kupitia 0754782577 atoe maelezo zaidi na vielelezo vya ziada

Leo tarehe 25 Julai 2013 chombo kimoja cha habari kimemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Andrew Chenge (Mb) akisema kwamba uamuzi kuhusu kodi/tozo ya kadi/laini za simu haukuwa wa kubahatisha. Chenge amesema kwamba kamati yake ilifanya utafiti wa kina na kisha kufikia uamuzi wa kuona tozo hiyo ni sahihi.

Ni muhimu akatakiwa kupitia namba yake 0754782577 atoe maelezo zaidi kuhusu usahihi wa tozo hiyo na aeleze ni wapi wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kupata vielelezo vya utafiti walioufanya.

Aidha, wenye maswali kuhusu nini hasa kilijiri kwenye kamati ya bajeti mpaka kamati hiyo ikakataa jedwali la marekebisho nililowasilisha tarehe 27 Juni 2013 kabla ya muswada wa sheria ya fedha kupitishwa bungeni tareheb 28 Juni 2013 kwa kuwa yeye ambaye ndiye msemaji wa kamati ameanza kutoa majibu. 

Pia, aeleze iwapo yupo tayari kumshauri Spika aruhusu kamati ya bajeti ikutane kwa dharura wiki ijayo kufanya kazi ya kupitia matumizi ya Serikali kwa lengo la kuanisha maeneo ambayo Serikali inaweza kubana matumizi kwa haraka kufidia pengo la bilioni 178 zinazotafutwa kwenye tozo hiyo ya simu. Hatua hii itawezesha kodi hiyo kuacha kutozwa bila ya kulazimika hata kuongeza vyanzo vingine vya fedha iwapo Serikali inasuasua kupanua wigo wa mapato.

Friday, July 19, 2013

Kufuatia kauli za Serikali magazetini kuhusu mimi na kodi ya umiliki wa kadi za simu; nijibu tu kwa ujumla kwamba SITAACHA. Badala yake naomba kuwapatia namba zao: Makamba 0767783996 na Mgimwa 0754/0684765644, tunachohitaji ni kauli ya Serikali kuwa kodi imesitishwa na itaondolewa na sio siasa chafu.

Kwa mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba kwamba; “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:

Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha walau kidogo kwa maendeleo.

Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.

Wednesday, July 17, 2013

Kodi ya kadi ya simu (SimcardTax): Maoni ya awali ya wananchi juu ya hatua za kuchukuliwa

Nawashukuru kwa maoni ambayo mmenitumia kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kufuatia kuanzishwa kwa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa wamiliki wa simu za kiganjani/mkononi.

Bado naendelea kuchambua maelfu ya maoni yaliyotolewa katika mijadala na niliyotumiwa kwa barua pepe. Nitoe mrejesho wa awali kwamba kwa muktasari mapendekezo niliyoyachambua mpaka sasa yanapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa:

Monday, July 15, 2013

Mnyika aponda sera za michezo za CCM

Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema ukosefu wa maandalizi ya mapema katika micheo kunatokana na sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiko kunakoibua matokeo mabovu katika sekta hiyo hususan kwa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, aliyasema hayo jana wakati akizindua michuano ya Mama Kevin Cup kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe (DUCE), jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema katika ilani ya uchaguzi ya Chadema 2010, waliahidi masualaya michezo hususan Tanzania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia Brazil mwakani endapo wangekabidhiwa cnchi, lakini kutokana na baadhi ya maeneo kutowataka waingie serikali mpya, hayo yameshindikana chini ya sera mbovu za CCM.

Saturday, July 13, 2013

Mkutano wa hadhara leo Julai 13, 2013 Dar es Salaam!

Msimamo wetu kuhusu rasimu ya katiba mpya na mustakabali wa taifa utatolewa leo Jumamosi ya Julai 13, 2013 kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Ukombozi-Manzese kuanzia saa 8 mchana.

Hotuba zitatolewa na viongozi mbalimbali wakiwemo Dr.W.Slaa, T.Lissu, M.Marando nk nathibitisha nami nitakuwapo kuwakaribisha Jimboni Ubungo.

Wananchi wote mnakaribishwa. Njoo wewe, njoo na yule!

Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli!

Muhimu: Shule ipo jirani na Manzese TipTop. Maelekezo wasiliana na: M/Kt wa Kata ya Manzese Ali Makwilo 0784-691449 au 0715-691449 au 0769-658593

Thursday, July 11, 2013

KAULI YA WAZIRI WA FEDHA KUHUSU KODI YA LINE ZA SIMU NI KIELELEZO CHA UDHAIFU WA SERIKALI NA UZEMBE WA BUNGE; NIANDIKIE SASA KUHUSU HATUA ZA KUCHUKUA JUU YA SUALA HILI KUPUNGUZA MZIGO WA GHARAMA ZA MAISHA KWA WANANCHI

Katika kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha amesema kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya simu ni ya wabunge. 

Kauli inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa Wizara yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu udhaifu wa Rais (na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala yanayohusu maandalizi ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa taifa wa maendeleo na ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa wananchi. Kwa kauli hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea kujihidhirisha.

Kauli hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge.

Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo. Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.