Wednesday, April 25, 2012

Hatuna Serikali, tufanye mapinduzi

Nilisema 2010: AMUA; Uwajibikaji kwa Maslahi ya UMMA kwanza. Kilichodhihirika kwenye mkutano uliomalizika wa bunge ni kuwa hatuna serikali. Nimerejea toka Dodoma, nawatakia heri ya kumbukumbu ya Muungano. Tufanye mapinduzi, tuwang’oe mafisadi kwa nguvu ya umma.

Monday, April 9, 2012

Mkutano wa Manzese na masuala ya kuyawasilisha bungeni

Nashukuru wananchi mliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara Manzese Bakhresa; kura mlizopiga za wazi kuwa hata uchaguzi ukirudiwa leo mtanichagua kwa kura nyingi zaidi zimenipa imani ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi. 

Asanteni kwa kuchangia 193,000 kwa ajili ya kesi ya kupinga ushindi wetu ikiwa ni ishara ya kuwa mko tayari kuendelea kulinda kura mlizopiga kwa hali na mali. 

Nitafikisha pia ushauri wenu kwa CHADEMA kuhusu umuhimu wa kuharakisha kwenda vijijini, kujijenga ngazi ya chini kwa kuwa na matawi na ofisi na kuanzisha chombo cha habari cha chama.

Mkutano wa Bunge unaanza kesho, nitatimiza wajibu mlionituma wa kuwawakilisha kwa kuwasilisha masuala mliyonieleza: Hoja Binafsi kutaka hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji; Ombi la wazalishaji wadogo na wafanyabiashara ndogondogo kwa ajili ya kuchangia katika kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi; Swali juu ya hatma ya kupandishwa hadhi kwa barabara kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya pembezoni na kupunguza msongamano. 

Naendelea kukaribisha maoni yenu kuhusu miswada minne ya sheria inayotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huu wa bunge. Maslahi ya umma kwanza.

Sunday, April 8, 2012

Pasaka ni kuacha utumwa kupata uhuru

Pasaka ni kutoka katika utumwa na kuwa katika uhuru wa kiroho, kimwili na kiakili. Nawatakia maisha mema yenye upendo, furaha na mafanikio. Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.

Saturday, April 7, 2012

Rambirambi ya Kanumba na matukio mengine ya leo

Natoa pole kwa wasanii na wapenzi wa tasnia ya filamu nchini kwa kifo cha ghafla cha Steven Kanumba, nimetoka nyumbani kwa marehemu Sinza Jimboni Ubungo kutoa rambirambi; tutaendelea kuwa pamoja kwa kadiri mipango ya mazishi itavyopangwa.


Kwa sasa naelekea kwenye mkutano wa hadhara Manzese Bakhresa saa 10 Jioni, nitatumia fursa hiyo kujibu maswali ya wananchi na pia kupokea masuala ya kuzingatia katika uwakilishi kwenye mkutano wa saba wa bunge utaotarajiwa kuanza tarehe 10 Aprili 2012.

Nawatakia Wazanzibar na Wabara wote heri katika siku ya kumbukumbu ya Mzee Karume. Maslahi ya Umma Kwanza.

Wednesday, April 4, 2012

Matokeo ya Mkutano wa Mbunge na Wafanyabiashara Ndogondogo

Tarehe 04/04/2012 nilifanya mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500 walioondolewa katika kata ya Ubungo.

Nilianza kwa kuwaeleza wazi kwamba siungi mkono biashara kufanyika katika maeneo hatarishi na maeneo yasiyoruhusiwa kisheria; hata hivyo nimekutana nao kwa kuwa: Mosi; waliniita hivyo nimefika kuwasikiliza kwa kuwa kazi yangu ni kuwakilisha wananchi wote. Pili; kuwaeleza sijaridhika na namna ambavyo serikali imetekeleza zoezi hilo bila kutimiza ahadi zake kwa wafanyabiashara ndogondogo na bila kutushirikisha au walau kutupa taarifa yoyote wakati wowote viongozi wa kuchaguliwa wa eneo husika. Tatu; kukubaliana hatua za pamoja za kuchukua ili kupata mwelekeo muafaka kwa kuzingatia haki, utulivu na fursa kwa waathirika kuendelea na shughuli za kujikimu bila kuwa katika maeneo hatarishi.

Baada ya utangulizi huo niliwapa fursa ya kutoa hoja au kuuliza maswali ambayo masuala mengi yalielezwa au kuulizwa. Baadhi ya masuala na maswali hayo ni:

Stella Mbuba-Yeye alieleza kuwa hawajakutana na serikali na kukubaliana maeneo mbadala kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari. Anasema baada ya kusikia matangazo kwenye vyombo vya habari kuwa kuna maeneo mbadala wametengewa walikwenda kwa mtendaji tarehe 29 Machi 2012 lakini wakajibiwa kuwa ‘aliyewaleta eneo hilo ndiye atayewapeleka anakokujua na mkiendelea kuuliza tutawaitia polisi’.

Mkutano wangu na "wamachinga" wa Ubungo leo 04.04.2012

Nikiwa naongea na kujadiliana na wafanyabiashara ndogo ndogo "wamachinga" walioondolewa maeneo yaUbungo. Pembeni ni Diwani wa Ubungo, Bw. Boniface
Wafanya biashara ndogo ndogo wakiwa wanafatilia mkutano huu

Muhimu: Taarifa yangu kwa kina itafata baadae

Sunday, April 1, 2012

Hongera Joshua!Hongera CHADEMA!Hongera wananchi!


Hongereni wananchi wa Arumeru Mashariki!

Mmedhihirisha kuwa uongo, ufisadi na usanii hauwezi kushinda ukweli, uadilifu na umakini!

Asanteni kwa kuunganisha nguvu ya umma na makamanda wote mliiongoza mapambano mpaka kimeeleweka.

Nawashukuru kwa kutuongezea nguvu ya kuwawakilisha bungeni kwa sasa, ushindi huu ni ishara ya ushindi wa 2015.

Maslahi ya Umma Kwanza.

Ukweli, uadilifu na umakini umeshinda Arumeru Mashariki

Hongereni wananchi wa Arumeru Mashariki, mmedhihirisha kuwa uongo, ufisadi na usanii hauwezi kushinda ukweli, uadilifu na umakini.

Asanteni kwa kuunganisha nguvu ya umma na makamanda wote mliiongoza mapambano mpaka kimeeleweka.

Nawashukuru kwa kutuongezea nguvu ya kuwawakilisha bungeni kwa sasa, ushindi huu ni ishara ya ushindi wa 2015. Maslahi ya Umma Kwanza.

CCM inategemea matusi, mafisadi na wamwagaji damu; 'kudumisha amani na utulivu' ni maneno ya kuficha matendo yao maovu


Wabunge: Highness Kiwia na Salvatory Machemli

CCM ni chama chenye kukumbatia matusi, mafisadi, uongo na umwagaji damu; maneno yao juu ya amani na utulivu ni ya kuficha matendo maovu ya viongozi wake.

Poleni wananchi wa Mwanza na wapenda demokrasia na maendeleo kote nchini. Nami nimesikitishwa na naalani tukio la wabunge Highness Kiwia na Salvatory Machemli kushambuliwa kwa mapanga na mawe usiku wa kuamkia leo mara baada ya kampeni za uchaguzi wa udiwani unaofanyika leo. Hakika tukio hili halitaishia kusikitika na kulaani, tutachukua hatua za ziada. Naendelea na mawasiliano na mashauriano na viongozi wakuu walioko Arumeru Mashariki na maeneo mengine na tutaeleza hatua zitazofuata.

Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kwamba tukio hilo la Mwanza limefanywa na WanaCCM, ushahidi wa tuhuma za kihistoria unathibitisha kwamba CCM na serikali yake imekuwa na kawaida ya kumwaga damu nyakati za chaguzi kwa njia mbalimbali ikiwemo kwa kukata viongozi wa CHADEMA mapanga, sasa wamefikia hatua ya kushambulia viongozi wa wananchi; wabunge.

Niliwahi kutahadharisha miaka michache nyuma kwamba kadiri CCM inavyoelekea kuondoka madarakani rangi yake halisi kinyume na maneno yao ya kinafiki ya ‘kudumumisha amani na utulivu’, matendo yao halisi yatajihidhirisha ya kuwa chama na serikali inayokumbatia vitisho, vurugu na umwagaji damu kama njia ya kujaribu kujiokoa na kukataliwa na umma. Wanafanya hivyo kwa kutumia vyombo vya dola na vikosi vya chama chao vya vitisho, vurugu na umwagaji damu.