Saturday, April 12, 2014

MAONI YA WAJUMBE WALIO WA WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA [Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Bunge Maalum, 2014]


UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”[1]

Mafuriko yanayoendelea katika jiji la Dar es Salaam

Nipo bungeni lakini nimepokea taarifa za mafuriko katika maeneo mbalimbali jimboni kama Kibamba, Malambamawili, Makoka nk Nimeshatoa maelekezo kwa Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Mbunge Ubungo kufatilia kwa ukaribu na kuzitaarifu mamlaka husika kwa hatua za haraka. Kwa maeneo mengine yenye mafuriko tafadhali mpeni taarifa kupitia: 0715-379542 au 0784-379542

Sunday, April 6, 2014

Sijaridhika na majibu ya Mkuu wa Mkoa kuhusu mgogoro unaoendelea juu ya usafiri wa pikipiki/bodaboda na bajaji katikati ya jiji la Dar es Salaam

Tarehe 4 Aprili 2014 Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Said Meck Sadiq amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba hawezi kusitisha kwa muda agizo lake la kukataza pikipiki/bodaboda na bajaj kuingia katikati ya Jiji. Mkuu wa Mkoa amenukuliwa akisema kwamba hawezi kufanya hivyo kwa kuwa agizo hilo si la kwake bali la sheria ambayo ameamua kuisimamia.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo kufuatia taarifa yangu ya tarehe 2 Aprili 2014 niliyoeleza kuwa nimemwandikia ujumbe kutaka asitishe kwa muda utekelezaji wa tamko alilotoa tarehe 3 Machi 2014 ili kupisha mazungumzo baina ya Serikali, wahusika wa Bodaboda na Bajaji na wadau wengine muhimu ili kupata ufumbuzi.

Kufuatia kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa nimeipitia kwa mara nyingine tena kifungu kwa kifungu Sheria inayohusika ambayo ni The Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act; sheria namba 9 ya mwaka 2001. Hakuna kifungu chochote katika sheria hiyo kinachokataza pikipiki/bodaboda au bajaj kuingia katika maeneo ya katikakati ya jiji. Hivyo Mkuu wa Mkoa anapaswa kutoa ufafanuzi kwa umma ni sheria ipi hiyo ambayo anaitumia na kifungu kipi hicho cha sheria ambazo kinamzuia kutengua agizo lake.

Ujumbe kwa Wananchi wa Chalinze:

Leo jumamosi 05 Aprili 2014 ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze na kesho jumapili 06 Aprili 2014 ni siku ya wananchi kupiga kura. Kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze wa kata mbalimbali mnaoweza kupata ujumbe kwa njia ya mtandao nawajulisha kwamba nitazungumza nanyi katika mkutano wa hadhara leo. 

Kampeni za Chalinze zilizinduliwa na Katibu Mkuu Dr Wilbroad Slaa na zitafungwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Said Issa Mohamed (ZNZ) akiwa na Dr Slaa. Kwa wapenda demokrasia na maendeleo popote mlipo ziungeni mkono timu za viongozi, wanachama na wapenzi kwenye kata na vijiji mbalimbali. Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mratibu Mohamed kupitia 0784246764 au 0784246764.

Wasiokuwa na mtandao naamini timu zetu za kampeni ya chini kwa chini na zenye magari ya matangazo kwa pamoja zitakuwa zimeshawaalika kwa kuzingatia ratiba ya kampeni. Tutahutubia kufunga kampeni kupitia mkutano utakaofanyika eneo la Chalinze Mjini (Sokoni) kuanzia saa 8 mchana na mpaka 12 Jioni nikiwa na viongozi wengine wa kitaifa.

Thursday, April 3, 2014

TAARIFA KWA UMMA

Tangu tarehe 3/3/2014 Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Meck Sadiq ilipotoa tamko la kupiga marufuku biashara ya kusafirisha abiria maeneo ya mijini kwa kutumia usafiri wa bodaboda na bajaji kumekuwa na mgogoro baina ya vijana wanaofanya kazi hiyo kwa upande mmoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa upande mwingine.

Aidha, kufuatia kauli hiyo watumiaji wa kawaida wa pikipiki na bajaji nao wamekuwa wakipata usumbufu wa kukamatwa kamatwa na kusumbuliwa wakidhaniwa kwamba ni sehemu ya biashara ya usafiri kwa kutumia bodaboda na bajaji.

Kadhalika, kuanza tamko hilo limezusha usumbufu kwa abiria ambao walikuwa wakitumia vyombo hivyo vya usafiri kama mbadala wakati huu ambapo ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo kwa Haraka (BRT) imeambatana na ongezeko la foleni katika barabara zinazoelekea mjini.

Kwa upande mwingine pamekuwepo na utata kuhusu mipaka ya Eneo la Katikati ya Mji (Central Business District- CBD) linaloguswa na amri hiyo.

Kwa kuwa mwezi mmoja umepita bila mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi na Serikali yenyewe, nimeamua kuingilia kati ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.