Wednesday, November 28, 2012

MUHIMU SANA: Tujitokeze leo kutoa maoni yetu rasimu ya gesi

Leo 29th Novemba, 2012 kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni Mahala: Makumbusho ya Taifa (Mkabala na Chuo cha IFM) tufike kutoa maoni yetu juu ya rasimu ya sera ya gesi asili Tanzania. Neema ya kuwa na rasilimali ya gesi tunapaswa kuipanga na kujua namna gani kama taifa tunufaike. Mawazo na busara zetu ni za muhimu sana. 

Monday, November 26, 2012

Shime tujitokeze kutoa maoni yetu kupata Katiba Mpya!


Rejeeni mikutano ya hadhara na vikao mbalimbali ndani ya jimbo letu la Ubungo katika kata mbalimbali ambapo nilihamasisha elimu juu ya haja na hoja za mabadiliko ya katiba.

Sasa zamu ya jimbo letu imefika kutoa maoni.

Toa sasa na himiza wananchi wenzako wengine nao washiriki kutoa maoni.

Endapo utakosa fursa ya kutoa maoni yako katika mikutano na Tume ya Katiba. Hakikisha unatoa bado maoni yako kwa njia hizi: Facebook hapa: http://www.facebook.com/pages/Tume-ya-Mabadiliko-ya-Katiba-Tanzania/323414977745643?fref=ts  au Ingia hapa ujaze maoni yako: http://www.katiba.go.tz/index.php/toa-maoni-yako/wanaoishi-ndani-ya-nchi au baruapepe: katiba@katiba.go.tz

Pia kwa watanzania wenzetu waliopo nje ya nchi, huu pia ni wakati wenu wa kutoa maoni kwa kupitia: Facebook hapa: http://www.katiba.go.tz/index.php/toa-maoni-yako/wanaoishi-nje-ya-nchi au Ingia hapa ujaze maoni yako: http://www.katiba.go.tz/index.php/toa-maoni-yako/wanaoishi-ndani-ya-nchi au baruapepe: katiba@katiba.go.tzRATIBA YA MIKUTANO YA MAONI YA KATIBA JIMBO LA UBUNGO.
NA.

KATA

TAREHE

MAHALI
MUDA WA MKUTANO
KUANZA
KUMALIZA
1
KIMARA

27/11/2012
BAHAMA TRA
3:00 ASB
6:00 MCH
UBUNGO
S/MSINGI MSEWE
8:00 MCH
11: JIONI
2
KIBAMBA

28/11/2012
S/MSINGI KILUVYA
3:00 ASB
6:00 MCH
MBEZI
S/MSINGI MBEZI
8:00 MCH
11:00 JIONI
3

GOBA

02/12/2012
ZAHANATI YA GOBA
3:00 ASB
6:00 JIONI
4
KWEMBE

03/12/2012
KIBAMBA HOSPITAL
3:00 ASB
6:00 MCH
SINZA
UWANJA WA TP
8:00 MCH
11: JIONI
5

SARANGA

04/12/2012
STENDI YA BONYOKWA

8:00 MCH

11: JIONI
6

MSIGANI

05/12/2012
UWANJA WA TANESCO

3:00 ASB

6:00 JIONI
7

MANZESE

07/12/2012
UWANJA WA BAKHRESA

8:00 MCH

11: JIONI
8

MABIBO

10/12/2012
S/MSINGI MPAKANI

3:00 ASB

6:00 JIONI
9

MBURAHATI

11/12/2012
S/MSINGI MBURAHATI U/KIFA

3:00 ASB

6:00 JIONI
10
MAKUBURI

13/12/2012
U/NJIA PANDA MABIBO HOSTEL

3:00 ASB

6:00 MCH
MAKURUMLA
GOMBERO
8:00 MCH
11: JIONI

MUHIMU: naomba wananchi wakati mkituma/toa maoni yenu, mnitumie pia nakala kwa simu: 0715-37 95 42 au baruapepe: mbungeubungo@yahoo.com kwa kuratibu na kurahisisha shughuli za ufatiliaji kwani kwa mujibu wa sharia ya mabadiliko ya katiba ilivyo sasa wabunge ni wajumbe wa Bunge la Katiba hivyo napaswa kupata nakala ya maoni ya wananchi pia juu ya katiba mpya niweze kuwakilisha kwa hatua hiyo ikifika.

Pia, napaswa kupata maoni yao kuhusu mchakato wa kupata katiba mpya ili niyazingatie wakati natekeleza wajibu wa kuwakilisha wananchi, kutunga sheria na kusimamia tume na serikali kwa ujumla wake ili nchi ipate katiba mpya na bora kwa maendeleo ya wananchi.Maslahi ya Umma Kwanza!

John Mnyika
Mbunge Jimbo la Ubungo

Saturday, November 24, 2012

Mnyika amlilia Odira Ongara


Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ametoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Mzee Odira Elizaphan Hamathe Ongara na kumweleza Marehemu kuwa alikuwa mtu mwenye msimamo katika nafasi za uongozi na utumishi wa umma alizowahi kuzishikilia wakati wa marais watatu wa Tanzania; Nyerere, Mwinyi na Mkapa.

Friday, November 23, 2012

SIRI HADHARANI KUWEZESHA HATUA ZA ZIADA ZA KISHERIA KUCHUKULIWA DHIDI YA MHANDO NA WENZAKE

Nimeamua kuchukua hatua ya kuiweka hadharani ripoti hii ya SIRI ya ndani ya Shirika la Umeme (TANESCO) ya maoni ya kisheria juu ya ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi niliyoitoa tarehe 1 Novemba 2012.

Kwa mujibu wa nyaraka hii ni wazi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) William Mhando amefanya makosa mengi yanayohitaji hatua za ziada za kisheria ikiwemo ya mgongano wa maslahi, utovu wa uaminifu, kushindwa kutangaza maslahi na matumizi mabaya ya ofisi; matendo ambayo ni ya kifisadi.

Makosa hayo na mengine ni kinyume cha sheria mbalimbali za nchi ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sheria ya Ununuzi wa Umma na sheria nyingine.

Hivyo, kwa kuwa Bodi imekataa kuwa haitachukua hatua za zaidi za kisheria juu yake natoa kauli ya ziada kwamba mamlaka zingine zinazohusika zichambue Taarifa hii sanjari na Taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuchukua hatua za kisheria zilizochini ya mamlaka hizo.

Monday, November 12, 2012

SABABU ZA AWALI ZA KUKATA RUFAA DHIDI YA UAMUZI WA SPIKA WA TAREHE 9/11/2012 WENYE MWELEKEO WA ‘FUNIKA KOMBE’


Baada ya habari kutolewa jana na leo juu ya uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma kwamba baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari na wananchi kwa simu na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii sababu za kusimama bungeni tarehe 9 Novemba 2012 mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba muongozo.

Nalazimika kutoa ufafanuzi huu nje ya bunge baada ya mkutano wa bunge kuahirishwa bila Spika kunipa fursa ya kusema jambo hili bungeni kwamba nilitaka muongozo wake kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) na 5 (2) kuwa nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake kutokana na kuwa na maudhui kadhaa yasiyozingatia katiba ya nchi, sheria mbalimbali za nchi, kanuni za kudumu za bunge, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge letu.

Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa nilitaka niombe muongozo wake kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini ilivyovunjwa, hivyo Spika anapaswa bado kueleza kwa umma iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine au kuelekeza kamati nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na madini yenye athari kwa maisha ya wananchi wakiwemo wa Jimbo la Ubungo.

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nasisitiza kwamba Spika anapaswa kurejea barua yangu ya toka mapema Oktoba ambayo mpaka sasa haijapatiwa majibu, hoja niliyoiwasilisha bungeni na kuungwa mkono ya jambo lililohusu haki za bunge  na miongozo niliyoomba bungeni kuhusu masuala ya nishati kwa nyakati mbalimbali katika mkutano wa Bunge uliomalizika  na kutoa kauli kwa umma.

Kwa kuwa katika uamuzi wake Spika wa Bunge ameeleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter  Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliackim Maswi wametoa maelezo yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali uwepo wa kamati ya bunge kwa ajili ya kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya bunge ni suala linalohitaji uamuzi wa haraka.

Aidha, katika uamuzi wake Spika zaidi ya kutoa onyo kali kwa Katibu Mkuu na Wabunge hakutoa onyo kwa Waziri wa Nishati na Madini wala hakueleza chochote  iwapo alipokea ushauri kutoka kwa Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu ukiukwaji wa kanuni uliofanywa na Spika mwenyewe bungeni wakati wa kadhia nzima.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Spika anaweza kutoa taarifa bungeni wakati wowote  na taarifa yake haijadiliwi hivyo sehemu kubwa ya taarifa ya tarehe 9 Novemba 2012 ilikuwa ni maelezo kuanzia sehemu ya kwanza mpaka sehemu ya pili.

Uamuzi wa Spika unapatikana sehemu ya tatu ya maelekezo hususan kifungu cha 6.12 ya kwamba “tuhuma husika hazikuweza kuthibitishwa” na baadaye kufuatiwa na uamuzi wa Spika kuhusu watoa tuhuma katika vipengele (a), (b), (c) na (d).

Nakusudia kukata rufaa ili taarifa kamili ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kuwasilishwa kwa ukamilifu wake kwenye kamati husika ya kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa kamili kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu’ zijulikane na masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa ‘funika kombe’.

Yapo masuala ya ziada ambayo binafsi niliyaeleza mbele ya kamati ndogo chini ya kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje ya bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria husika , hata hivyo taarifa kamili ikiingia bungeni kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa mujibu Kwa Ibara ya 100 ya Katiba ya Nchi.

Aidha, nitaka rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu’ kilichotolewa kwenye uamuzi wa Spika hakilingani na ‘makosa’ ambayo yameelezwa kuwa na  uzito wenye kuathiri “kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge waliohusishwa”.

Spika amefanya uamuzi wake chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza kuwa iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli Spika amepewa fursa ya kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano.

Aidha nitakata rufaa kwa kuwa waliodaiwa kutoa kutoa tuhuma bila ushahidi walipaswa kujieleza kwa tuhuma hizo kabla ya kuhukumiwa kwa misingi ya kanuni za haki ya asili zilizopo pia katika katiba ya Nchi na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge; hata hivyo Spika amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo kali’ kinyume na masharti ya kanuni ya 5 (1).

Ikumbukwe kwamba Spika katika maelezo yake amesisitiza kuwa Kamati Ndogo ilipewa hadidu rejea moja tu, “Kuchunguza na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana”, baada ya kuchunguza kwa mujibu wa hadidu rejea hiyo na kuwasilisha ripoti yake Spika alipaswa kama kuna ukiukwaji mpya wa kanuni uliobainika kutokana na uchunguzi huo kuanzisha mchakato wa adhabu.

Binafsi niliitwa kwa maandishi kuisaidia kamati ndogo katika uchunguzi wake kutokana na maoni niliyowasilisha bungeni ya kwamba  “….Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa inafanywa ndani na nje ya Bunge ili uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni yaliyokosa zabuni kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme…”.

Sijawahi kuandikiwa au kuitwa popote kutakiwa kujieleza kwa ‘kuisemea tuhuma bungeni bila ya kufanya utafiti kupata ukweli’ na maelezo hayo niliyoyatoa bungeni hayakukiuka kanuni yoyote ya bunge kama ambavyo nitathibitisha wakati nitakapokata rufaa.

Kwa upande mwingine nitakata rufaa kwa kuwa adhabu aliyopewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi hailingani na ukubwa wa makosa anayodaiwa kuyafanya, ikiwa ni kweli amevunja haki za bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge kwa ajili ya kujihami dhidi ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika.

Kadhalika kwa Spika ameeleza kuwa mbinu aliyotumia ni pamoja na kutaka kuwalipa fedha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini shilingi milioni mbili kwa kila mjumbe madai haya ni ya jaribio la kufanya ufisadi wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyokuwa kwenye kashfa ya Katibu Mkuu aliyemtangulia David Jairo hivyo Spika alipaswa kupendekeza kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria.

Uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna tofauti na maamuzi yaliyotangulia ambayo yamesababisha mpaka sasa Serikali haijawasilisha bungeni ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanywa na kamati teule ya Bunge.

Ni vizuri ikakumbukwa kwamba katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tarehe 27 Julai 2012 nilisisitiza kwamba  “ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.

Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.

Mchakato huu ungewezesha kupata ukweli wa ziada kibunge kuliko utaratibu uliotumiwa na Kamati Ndogo na Spika.

Nitaeleza masuala ya ziada nitakayoyakatia rufaa na kauli yangu kuhusu maelezo na uamuzi wa Spika juu ya Waziri na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.

John Mnyika (Mb)
10/11/2012

Wednesday, November 7, 2012

KAULI YA WAZIRI KIVULI WA NISHATI NA MADINI KUHUSU MATATIZO YA MAFUTA YANAYOENDELEA NCHINI

Katika kipindi cha ziadi ya wiki tatu nchi imekuwa katika matatizo makubwa ya upungufu wa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli hali yenye athari kwa uchumi wa nchi na usumbufu na gharama za ziada kwa wananchi.

Katika kipindi hicho viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wakiwemo Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na taasisi zilizochini ya Wizara hiyo hususan Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) wamekuwa wakitoa taarifa zenye mkanganyiko kuhusu matatizo yanayoendelea.

Hivyo, nasisitiza Waziri Mkuu kwa madaraka yake ya ibara ya 51 ya katiba ya udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa shughuli za siku hata siku wa kazi za Serikali na kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni badala ya kutoa tu kauli bungeni aagize Waziri wa Nishati na Madini awasilishe hoja ya taarifa ya Serikali juu ya utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu mafuta na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali juu ya matatizo ya mafuta yanayoendelea.

Juu ya uhaba wa mafuta nchiniNa Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge wa Ubungo (Chadema)John Mnyika akihoji Kiti cha Spika juu ya serikali kushindwa kuleta bungeni kauli ya serikali juu ya mkakati wa kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini Tanzania.

Uhaba wa mafuta jana umewakimbiza kwenye kikao cha Bunge mjini Dodoma asubuhi, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na naibu mawaziri wake George Simbachawene na Steven Masele.

Waziri huyo na naibu mawaziri wake hawakuwepo bungeni leo wakati Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika akiitaka serikali itoe sababu ya kutokuja bungeni leo kutoa tamko la serikali jinsi inavyoshughulikia suala la uhaba wa mafuta nchini.

Spika wa Bunge Anne Makinda alimlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusimama na kujibu hoja ya Mnyika aliyemtaka Spika kulazimisha serikali ijibu hoja yake pamoja na mkakati wa serikali wa kutatua uhaba wa mafuta nchini.Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilazimika kunyanyuka na kusema kwa ufupi kuwa serikali ilikuwa ikijiandaa na kuja na hoja nzito ya kueleza umma mikakati kabambe ya kutatua uhaba wa mafuta nchini.

Sera ya gesi itafsiriwe kwa Kiswahili

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwaagiza maofisa wake kuitafsiri sera ya gesi asili iliyoandikwa kwa kiingereza badala ya Kiswahili ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitolea maoni.

Hatua hiyo ya Mnyika imekuja baada ya wizara ya Nishati na Madini kutoa matangazo kwenye magezeti kuhusu rasimu ya sera ya gesi asilia ikiwa katika lugha ya Kiingereza.