Thursday, June 30, 2011

Hoja Binafsi kuhusu uvamizi wa viwanja vya wazi vya umma

Mtakumbuka kwamba mwezi Machi 2011 niliwaeleza kwamba nimewasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni hoja binafsi kuhusu uvamizi/uuzwaji wa viwanja vya wazi ili ipangiwe tarehe ya kuwasilishwa na kujadiliwa kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Hata hivyo, toka wakati huo uongozi wa Manispaa umekuwa ukipiga danadana hoja hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa pamoja na kuwa katika kipindi husika kumefanyika vikao viwili vya baraza la madiwani. Katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kinondoni cha kawaida cha tarehe 18 Juni 2011 hoja hii haikuingizwa kwenye taratibu kama kanuni zinavyohitaji. Ili kuongeza msukumo kwa hatua kuchukuliwa kwa haraka zaidi kama sehemu kuisimamia serikali naomba kuwajulisha kuwa nimeamua kuchukua hatua zifuatazo:

Mosi; kutumia bunge kuhoji kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa na serikali kuu baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi. Hii ni kwa sababu ufisadi uliofanyika katika ardhi umehusisha pia baadhi ya maofisa wa serikali kuu hususani wa Wizara ya Ardhi. Aidha, mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti yamehusisha pia masuala ambayo mengine yako juu ya halmashauri yakitaka hatua kutoka kwa jeshi la polisi ngazi za juu, TAKUKURU ngazi za juu, uongozi wa Mkoa wa Dar es salaam, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI nk. Ili ufuatiliaji uwe rahisi, nitataka ripoti nzima ya kamati ambayo mpaka sasa imefanywa kuwa siri; iwekwe hadharani.

Pili; Kuiwasilisha hoja binafsi husika kwa umma (nakala inafuata hapa chini); ili hatua zisipochukuliwa katika kipindi cha miezi hii miwili ambayo nipo bungeni Dodoma tuanze maandalizi nikirejea tushirikiane na madiwani wa kata husika kuunganisha nguvu ya umma katika mitaa yenye viwanja husika mpaka kieleweke. Wakati mimi nikiendelea na hatua za kibunge, naendelea na mawasiliano na madiwani pamoja na uongozi wa manispaa ili nao waharakishe kuanzia sasa kuchukua hatua kupitia kamati mbalimbali za manispaa kwenye masuala ambayo wana mamlaka nayo kabla ya kikao kijacho cha baraza la madiwani.HOJA BINAFSI KUHUSU UUZWAJI/UVAMIZI WA VIWANJA VYA UMMA KWENYE BAADHI YA KATA ZA JIMBO LA UBUNGO KATIKA MANISPAA YA KINONDONI

Maelezo ya Hoja

Nawasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 19 ya Kanuni za kudumu za Halmashauri na kanuni nyingine kwa nafasi yangu ya ujumbe wa baraza husika kuwa:

KWA KUWA katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 mpaka 2010 pamekuwepo malalamiko mbalimbali ya wananchi kuhusu uvamizi ama uuzwaji wa viwanja vya umma maarufu kama viwanja vya wazi katika maeneo ya kata mbalimbali za jimbo la Ubungo.

KWA KUWA kutokana na malalamiko hayo tumekuwa tukitoa shinikizo wa serikali kuweza kuchukua hatua za haraka ikiwemo kwa kuweka hadharani baadhi ya taarifa za uuzwaji ama uvamizi wa viwanja vya umma.

KWA KUWA hatimaye tarehe 24 May 2010 Rais Jakaya Kikwete wakati akifanya majumuisho ya ziara ya kukagua hali ya maji katika mkoa wa Dar es Salaam alikiri kuwa yapo maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa na kuwa madiwani wanahusika na sakata hilo.

KWA KUWA kufuatia kauli hiyo ya Rais na malalamiko ya umma Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitembelea Manispaa ya Kinondoni tarehe 15 Juni 2010 na kubaini mapungufu kadhaa ya kiutendaji kuhusiana na masuala ya ugawaji wa ardhi yakiwemo maeneo ya umma yaliyozoeleka kuitwa viwanja vya wazi.

KWA KUWA kufuatia malalamiko mengi ya wananchi aliyoyapokea na pia kufuatia habari mbalimbali zilizotolewa na vyombo vya habari aliunda kamati maalumu ya kuchunguza maeneo yote ya wazi yaliyovamiwa katika mkoa wa Dar es Salaam. Kamati hiyo iliundwa tarehe 18 Juni 2010 na pamoja na mambo mengine ilipewa hadibu za rejea ambazo ziliiongoza kamati tajwa kufanya kazi yake.

KWA KUWA taarifa ya tume hiyo ilibaini kuwa Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na maeneo mengi ya wazi yaliyovamiwa. Maeneo hayo yanahusisha pia viwanja vya wazi katika kata mbalimbali za jimbo la Ubungo ambalo mimi ni mbunge wake na mjumbe wa baraza la madiwani.

Msingi wa Hoja

Ninaomba kuwasilisha hoja binafsi katika baraza hili ili kupata maelezo na vielelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa na Manispaa kuhusu maelekezo ya kamati katika maeneo yafuatayo;

Kiwanja Na. 1022 Kitalu E Sinza. Kamati ilibaini kuwa katika kiwanja hiki kuna Ofisi ya Afisa Mtendaji na banda lenye vyumba vitano vya biashara na msingi wa jengo ambalo halijakamilika. Kamati ilishauri pamoja na mambo mengine kuwa ufanyike uchunguzi wa kipolisi kwa kuwa eneo hilo bado lipo wazi. Nataka kujua kama huo uchunguzi umefanyika na nini kimebainika katika uchunguzi huo.

Eneo karibu na kiwanja Na. 636 Kitalu E Sinza. Eneo lilibainika kuwa wazi ila limemegwa pande zote mbili na kuna matofali machache yamewekwa. Kamati ilielekeza kuwa Halmashauri irudishe mipaka ya kiwanja hiki na hatua ya kulitangaza kama eneo la wazi kwa mujibu wa sheria.Je Halmashauri imesharekebisha mipaka na kulitangaza eneo kuwa wazi? Na kama bado Halmashauri ina mpango gani wa kutekeleza agizo hilo na lini?

Eneo karibu na viwanja Na. 281, 282, 283 na 287 Sinza B. Eneo hili limejengwa ofisi ya Mtendaji kata Sinza D. Kamati ilishauri kuwa eneo lililobaki litangazwe kama eneo la wazi kwa mujibu wa sheria na sehemu ilipojengwa ofisi ya kata eneo hilo lipimwe.
Naomba kupata maelezo kama ushauri huo wa kamati umetekelezwa na Halmashauri.

Eneo karibu na viwanja Na. 411, 413,414 na upande mwingine kinapakana na 698 na 609 Sinza Block D, sehemu kubwa ya eneo hili ipo wazi na pia kimechimbwa kisima cha umma na kuna jiwe la msingi lenye shina la wakereketwa wa chama cha mapinduzi (CCM). Kamati ilishauri eneo lipimwe na kutumika kama eneo la wazi kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa sheria. Je halmashauri imeshapima eneo hilo na kuwaondoa wavamizi hao waliobainika?

Kiwanja Na. 814, 818 Sinza Block D. eneo hili hutumika kama makazi ya watu na ndiyo waliondeleza eneo hilo. Kamati ilishauri Halmashauri kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini uhalali wa umiliki wa wananchi hao. Je uchunguzi huo umeshafanyika na kama ndiyo, uchunguzi huo ulibaini nini na baraza la madiwani lilipokea taarifa hiyo?

Eneo jirani na viwanja Na. 480 na 481 Sinza Block D. Eneo hili lipo wazi na kamati imeshauri Halmashauri eneo hili lipimwe ili libaki kuwa wazi kwa matumizi yaliyokusudiwa. Je Halmashauri imepima eneo hili na kulitangaza kuwa wazi ili kuepuka wavamizi?

Eneo jirani na kiwanja Na. 37 Sinza Block D ambalo kumejengwa msikiti na mmiliki wake hajulikani. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri wafanye uchunguzi wa kina kubaini uhalali wa umiliki huu na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi huo umeshafanyika?

Eneo jirani na viwanja Na. 75 na 77 Sinza Block D. Eneo hili limezungushiwa ukuta na mtu binafsi. Halmashauri ilishauriwa kufanya uchunguzi ili kubaini uhalali wa umiliki wa eneo hili na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi umefanyika na ni hatua gani zilizochukuliwa?

Eneo linalopakana na viwanja Na. 63, 99 Sinza Block D ambalo limejengwa Kanisa la Assemblies of God, Shule ya chekechea, ofisi ya CCM, gereji na pia kuna jengo la ghorofa limejengwa hapo. Halmshauri pia ilishauriwa kufanya uchunguzi wa kina na hatua stahiki zichukuliwe ili kubaini uhalali wa umiliki wa taasisi hizo (kanisa na CCM) na watu binafsi. Je uchunguzi huo ulishafanyika na hatua gani zilizochukuliwa?

Eneo lililopo mkabala na kiwanja Na. 475 Sinza B ambapo kumejengwa shina la wakereketwa wa CCM, mama lishe na pia kuna biashara ya pool inaendelea. Halmashauri ilishauriwa ifanye uchunguzi wa kina na hatua stahiki zichukuliwe. Je ushauri huo ulizingatiwa na Halmashauri?

Eneo karibu na kiwanja Na. 23 Sinza C. Eneo hili hutumika limejengwa ofisi ya Afisa Mtendaji wa mtaa na pia kuna vibanda vya biashara. Kamati ilipendekeza kuwa sehemu ya ofisi imegwe na eneo lililobaki lipimwe na kutangazwa kama eneo la wazi. Je Halmashauri imezingatia ushauri huo?

Eneo karibu na kiwanja Na. 24 Sinza C, ambalo limengwa makazi ya watu. Halmashauri pia ilishauriwa ifanye uchunguzi wa uhalali wa umiliki na hatua stahiki zichukuliwe. Je Halmashauri imezingatia ushauri huu na ni hatua gani walizochukua?

Eneo karibu Na. 765, 789, 790, na 797 Sinza C. Hapa kuna sehemu hutumika kama maegesho ya magari na pia kuna kibanda cha kukaangia chipsi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri itoe amri kuwa wamiliki wa magari kuondoa magari yao na pia upimaji ufanyike na kulitangaza eneo hilo kuwa wazi. Je Halmashauri imeshawaondoa wamiliki wa magari hayo na kuwa wasiendelee kulitumia eneo hilo? Je upimaji na kulitangaza eneo hilo kuwa wazi umeshafanyika?

Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na. 21, 23, 25, 27, 29 Sinza B. Eneo hili kuna shina la wakereketwa wa CCM ,vibanda vya mama lishe, sehemu za kutengenezea mageti, magenge na kontena la kuuzia vinywaji vikali na baridi. Halmashauri ilishauriwa kuwaondoa wavamizi hawa ili eneo libaki kuwa wazi. Je Halmashauri imeshawaondoa wavamizi hawa?

Eneo la wazi lililozungukwa na viwanja Na.72-74. Eneo limewekwa shina la wakereketwa wa CCM Kawawa kuna mama lishe na vioski. Kamati ilibaini kuwa eneo hili kwa mujibu wa mipango miji ni la wazi na kuishauri Halmashauri iwapeleke mama lishe kwenye maeneo yanayostahili na kupima eneo husika na kulitangaza kuwa wazi. Je nini kimefanyika mpaka sasa na je eneo limeshapimwa na kutangazwa kuwa wazi?

Eneo la wazi linalozungukwa na viwanja Na. 1, 2, 89, 90, 141 na 142 Sinza E. Katika eneo hili kumejengwa nyumba za makazi, Baa na asilimia ndogo ya eneo lipo wazi (baadhi ya namba ya viwanja hivyo ni 655 na 690). Kamati ilishauri kuwa Halmashauri iendelee na uchunguzi na hatua stahiki zichukuliwe. Je uchunguzi huo ulishafanyika?

Eneo la kiwanja cha michezo na Shule ya Msingi Sinza E. Kiwanja kimemilikishwa kwa CCM na kuna vibanda vimejengwa kuzunguka eneo lote na ndani linatumika kama maegesho ya magari. Kamati ilishauri kuwa eneo litumike kwa matumizi yaliyopangwa na shughuli ambazo hazihusiani ziondolewe. Je Halmashauri imeshawapa taarifa CCM kuhusu hili na kutangaza eneo husika kutumika kwa matumizi yaliyopamgwa?

Eneo la wazi jirani na viwanja Na. 77, 79, 81, 151-154, eneo hili limejengwa makazi ya watu na sehemu za biashara. Kamati imeshauri kuwa Halmashauri ifanye uchunguzi wa kina na kuchukua hatua zinazostahiki. Je Halmashauri imechukua hatua gani mpaka sasa?

Viwanja Na. 9 na 10 Sinza A. Wamiliki wa viwanja hivi viwili wamefunga barabara ya kuingia eneo la wazi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri ichukue hatua ya kufungua barabara husika ili eneo la wazi litumike kwa matumizi yaliyopangwa. Je Halmashauri imeshafungua barabara hiyo? Na kama bado nini kinachelewesha utekelezaji huo?

Kiwanja Na. 846 Sinza A. Eneo hili limejengwa nyumba ya makazi na biashara. Katika eneo hili taratibu za kubadili matumizi inasemekana zilifuatwa; je ni kweli?

Jirani na viwanja Na. 38, 40, 44, 46 na 48 Mtaa wa Kibesa Makurumla. Eneo hili limejengwa ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Makurumla. Kamati ilishauri kuwa eneo la ofisi limegwe na taratibu ya kubadilisha matumizi zifuatwe na eneo lililobaki litangazwe kuwa wazi na litumike kama sehemu ya starehe na michezo kwa mujibu wa sheria. Halmashauri imefikia hatua gani juu ya kutekeleza ushauri huo?

Jirani na viwanja Na. 18 na 19 Mtaa wa Malala Makurumla. Kuna wavamizi wasiorasmi wanalitumia eneo hili kama gereji. Kamati ilishauri kuwa wavamizi waondolewe na kutokana na uhaba wa maeneo ya wazi katika maeneo hayo, eneo hilo litumike kama kiwanja cha wazi. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala kwa ajili ya gereji husika ?

Jirani na viwanja Na. 73, 78, 80, 82, 84 na 86 Mtaa wa Mengo Makurumla, eneo hili limevamiwa na wavamizi wasiorasmi. Ushauri wa kamati ni sawa na uliopo hapo juu. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala kwa wajasiriamali husika?

Eneo la wazi lililopo Mtaa wa Kagera Makurumla limevamiwa na na kuna ofisi ya CCM Tawi la Karume Kata ya Makurumla na pia kuna banda linalotumika kama sehemu ya biashara. Kamati ilibaini kuwa wahusika walishapewa notisi ya kuondoka na hivyo Halmashauri ichukue hatua ya kuwaondoa wavamizi hao. Je Halmashauri imewaondoa wavamizi hao?

Eneo la wazi nyuma ya Ubungo terminal (“buffer zone” ya reli) limejengwa vibanda vya biashara. Kamati ilibaini kuwa eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya reli hivyo basi vibanda hivyo viondolewe ili kuacha eneo litumike kama ilivyokuwa imepangwa. Je Halmashauri imeshaweka utaratibu mbadala wa kuwapa wafanyabiashara hao maeneo ya biashara ikiwa bado kuna azma ya kuboresha matumizi ya reli kwa usafiri wa ndani ya mkoa wa Dar es salaam?

Eneo lipo jirani na kiwanja Na. 148 ambalo limejengwa nyumba ya makazi ya kudumu ya mtu binafsi. Kamati ilishauri kuwa Halmashauri iwasilishe taarifa kuhusu mwendelezaji huyo na kama ni mvamizi apelekewe notisi na kumtaka aondoe jengo hilo. Naomba kujua kama taarifa ya Halmashauri ilishawasilishwa au la.
Nyuma ya jengo la RUBADA na Kanisa la KKKT na Anglikana. Eneo hilo limejengwa shule ya msingi Ubungo Plaza kwa mpango wa MMEM. Kamati ilishauri kuwa eneo lililobakia litumike kwa matumizi michezo na burudani na si vinginevyo. Je, hatua zipi zimechukuliwa?

Na viwanja vingine vya kata zingine za jimbo la Ubungo kwa kadiri ya ripoti ya Kamati/Tume iliyoundwa na Mkoa wa Dar es salaam na taarifa za nyingine.

Kwa kuwa maeneo hayo yalitengwa kwa mujibu wa sheria (Public Recreation Grounds Cap. 320) na kwa kuwa maeneo hayo ni muhimu kwa ajili ya matumzi ya umma naomba kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitisha maazimio mahususi kuhusu viwanja husika kwa lengo la kulinda sheria na hazi za wananchi kuhusu ardhi.

Aidha naomba kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Manispaa ya Kinondoni lielezwe hatua za kisheria na kiutawala ambazo zimechukuliwa kwa wahusika kutokana na uvamizi na/au uuzwaji huo.

Naomba pia kutoa hoja kwa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitisha maazimio yatakayowezesha vitendo vya namna hiyo kutojirudia ikiwemo kwa kupitia kata zingine na kuchukua hatua stahili.

Kadhalika naomba kutoa hoja baraza la madiwani wa Manispaa ya Kinondoni lipitishe azimio kwamba mamlaka husika ziweze kufanya ziara ya kutembelea viwanja husika ili kuweza kuchukua hatua na kuhakikisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati husika.
Naomba kutoa hoja kwamba baraza la madiwani lipitishe azimio la kutaka kuletwa mapendekezo ya mpango kabambe wa matumizi endelevu ya viwanja vya umma katika Manispaa ya Kinondoni.

Naomba kutoa hoja;John Mnyika (Mb)
Mjumbe wa Baraza la Madiwani
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
19 Machi 2011

Marekebisho niliyowasilisha kupunguza bei ya mafuta

MHE. JOHN MNYIKA (22/06/2011) : Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuwasilisha mabadiliko ambayo yanahusu kifungu cha (8) cha Muswada wa Sheria ya Fedha ukurasa wa (5) na yanahusiana vile vile na ukurasa wa (2) wa schedule iliyowasilishwa na Serikali kipengele cha (e).


Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu yanakusudia na nitasoma: “In clause eight which relates to the fourth schedule by inserting under heading 27.10 and just before its code 27.10, the following particulars, particulars nyingine ziko kama ambavyo zimeelezwa na Serikali isipokuwa kwenye sehemu ya new excise rate ambapo napendekeza kwamba iwe ni shilingi 300.30 kwa upande wa mafuta ya taa na shilingi 115/= kwa upande wa gas oil.


Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa mapendekezo haya, hoja ambayo Serikali imeikubali ambayo ni ya wananchi na imetolewa na Kambi ya Upinzani ni kushusha gharama za maisha. Hoja hii imekuwa na sura mbili kwa upande wa suala hili tunalozungumza la mafuta, kuna suala la tozo za mafuta na kuna suala la kodi za mafuta, lakini ukiyatazama sasa mapendekezo ya Serikali yaliyoko kwenye ukurasa wa pili wa schedule ya kupandisha kodi ya mafuta ya taa kutoka shilingi 52/= mpaka shilingi 400.30 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya takriban 600%, wakati huo huo kupunguza kodi ya mafuta haya mengine ikiwemo dizeli kwa kiwango kidogo sana cha kutoka shilingi 314/= mpaka shilingi 215/= peke yake ambayo ni sawasawa na punguzo la sh 99/=, peke yake kwenye kodi iliyoko kwenye mafuta


Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba halikujikita kwenye lile lengo la msingi la kupunguza gharama za maisha, bali imelenga lengo la msingi lingine ambalo na lenyewe naliunga mkono la kupunguza uchakachuaji ambao umekuwa ukiligharimu Taifa hasara ya sh. bilioni takriban 50, gharama ya uharibifu wa magari na kuharibu biashara ya usafirishaji wa mafuta. Ni hoja ambayo naiunga mkono lakini namna ambavyo imechukuliwa na Serikali imelenga kuondoa uchakachuaji bila kuelekea kwenye suala la kupunguza bei za mafuta.


Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naunga mkono kabisa msimamo na maoni ya wote kwamba tusiguse kodi ya ushuru wa magari kwa maana ya fuel levy shilingi 200/= kwa sababu inatusaidia kwenye kujenga barabara zetu. Lakini pamoja na kuacha kugusa fuel levy Serikali imeshindwa kufanya uamuzi mgumu wa kukubali kugusa kwa kiwango kikubwa zaidi kidogo excise duty ili kuweza kwenda kweli kupunguza bei ya mafuta.


Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa marekebisho haya ya kuwianisha bei ya mafuta na bei ya petroli yazingatiwe ili usimwongezee mzigo sana mtu anayetumia mafuta ya taa na wakati huo huo usimwongezee mzigo mtumiaji wa daladala, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri.

Nakala ya Jedwali la Marekebisho unaweza kuipata kupitia: http://mnyika.blogspot.com/2011/06/schedule-of-ammendments-on-finance-bill.html

Schedule of Ammendments on Finance Bill

SCHEDULE OF AMMENDMENTS TO BE MOVED BY HON. JOHN JOHN MNYIKA MEMBER OF PARLIAMENT FOR UBUNGO COSTITUENCY AT THE SECOND READING OF THE BILL ENTITLED “THE FINANCE ACT, 2011”

Made under standing order 86(9), 86(11) and 88(2)

A Bill entitled “The Finance Act, 2011 “ is amended as follows:

A in clause 8 which relates to the “Fourth schedule” by inserting under Heading 27.10, and just before its code 2710. 1 941, the following particulars: First row; Its Code- 271.19.31; Description- Illuminating Kerosine (IK); Unit-1; Old excise- Tshs. 52.00; New excise rate- Tshs. 300.30. Second row ; Its Code- 2710.19.31 ; Description- Gas Oil (Automotirc light, ambar for High speed engines; Unit-1; Old excise-Tshs. 314.00; New excise rate- Tshs. 115.00

In Clause 17 by deleting and substuting for it the following new clause. 17 The Principal Act is amended in paragraph 1 of the second schedule by deleting item “w” and substuting for it with the following: (w) Payment of withholding tax on dividend arising from investment in the export processing zone and special economic zone during initial period of five years.

In clause 21: The last sentence is amended by deleting the word; “ten” after of before years and substuting it with “five” to read “during initial period of five years.

In clause 32; Ammendment is done by maintaining the wording of paragraph 8(2), particularly “National Housing Corporation” by deleting sub clause (a); Renumbering sub clause (b), (c) and (d).


John Mnyika, (MP)
UBUNGO CONSTITUENCY
DODOMA – 22 JUNE, 2011

Wednesday, June 29, 2011

Niliyochangia katika mjadala wa bajeti 2011/2012

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Lakini kwanza niseme tu kwamba nimesikia michango humu Bungeni inayosema mambo mawili makubwa. Kwanza inasema Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ameiga kutoka mawazo ya Serikali bila kuishukuru Serikali kwa mawazo yake, lakini pili mawazo kwamba CHADEMA kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani haikutekeleza ilani yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali imeiga mawazo mengi sana kutoka kwa CHADEMA, ni jambo zuri na kwa sababu mawazo haya yako kwenye Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 na hayapo kwenye ilani ya CCM.

Serikali kwenye hotuba ya Waziri wa Bajeti imezungumza kuhusu mchakato wa Katiba mpya ambayo haipo kwenye Ilani ya CCM, bali iko kwenye Ilani ya CHADEMA na Serikali imeiga, ni vizuri. Serikali imezungumza kuhusu kupunguza gharama za maisha ambayo haijachambuliwa kwa kina kwenye Ilani ya CCM, lakini humu imechambuliwa na CHADEMA imeeleza ni namna gani ambavyo kuna haja ya kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.

Serikali imeiga wazo la wingi wa posho na CHADEMA ilizungumza kwa kina sana na kwa takwimu kuhusu ukubwa wa posho na haja ya kuunganisha posho, kupunguza posho na kadhalika ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi na kusukuma mbele maisha na wakati huo huo kuweka uchumi sawa.

Hili wazo nalo Serikali imelichukua, lakini imelichukua ndivyo sivyo. Sasa mimi niseme tu kwamba ni vizuri watu wakawa wanasoma ilani za vyama vingine ili kujua asili ya haya mawazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwepo na wazo kwamba hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikutekeleza ilani hii. Kuna mambo humu tumeyasema kwenye hotuba ya Kambi na ninaomba tu Serikali iyachukue kwenye bajeti ijayo kama haiingizi sasa ambayo yamo kwenye Ilani na ambayo ni mambo yanayotekelezeka japo awali walisema hayatekelezeki.

Tulisema elimu bure na tulisema bure Kidato cha Kwanza mpaka Kidato cha Sita na tukasema elimu ya juu tunavunja Bodi ya Mikopo, tunatengeneza mamlaka nyingine ya ugharamiaji wa elimu kwa mfumo tofauti.

Kwenye bajeti ya mwaka huu, Msemaji wa Kambi Rasmi ameeleza kwa kina ni namna gani ambavyo tutagharamia elimu kwenye shule za umma za kutwa, ni namna gani watoto wa kike watasoma bure na tumeeleza kwamba yanatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu jambo lingine la msingi kwamba kuna mambo walikuwa wanasema hayatekelezeki kwamba huwezi kushusha Pay As You Earn kodi ya wafanyakazi mpaka 9%. Sisi tumeteremsha na tunaomba Serikali ikubali hili wazo na tumeonyesha jinsi gani ambavyo linatelekezeka kwa ajili ya kutetea maslahi ya wafanyakazi.

Tumezungumza muda mrefu kwenye Ilani kuhusu haja ya kutoa pension kwa wazee ikasemekana kwamba wazo hili halitekelezeki. Tumeeleza jinsi gani ambavyo suala la kutoa pension kwa wazee wote inawezekana kabisa. (Makofi)

Kwa hiyo, naiomba tu Serikali katika haya mawazo ambayo hayapo katika bajeti ya Serikali na yenyewe katika hitimisho la Waziri ayatolee kauli na kuyaingiza kwenye utekelezaji. Kuna wengine wamesema kwamba bajeti kivuli haijazungumza kuhusu suala la kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi na kumwondolea mzigo Mtanzania maskini.

Kuna mchumi mmoja anaitwa Rostow, tatizo ni kwamba bajeti hizi zinaweza zikawa zinasomwa kama vitabu vya A, E, I, O, U, tusome kiuchambuzi wa kiuchumi. Unapozungumza kuinua viwanda ni lazima utengeneze kitu kinachoitwa pre-conditions for take off, kwamba uweke msingi ili uwekezaji kwenye viwanda uende kwa nguvu kubwa zaidi.


Ukiangalia falsafa ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo mimi naiunga mkono, kwa kweli imejikita katika kuhakikisha gharama za uzalishaji zinapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza kutaka uwekezaji mkubwa kwenye gesi na hili naomba Waziri katika majumuisho yake alitolee kauli kwa sababu kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini naelewa kwamba ujenzi wa bomba kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam na baadaye Tanga ambao ungepunguza sana gharama za uzalishaji ikiwemo kwenye viwanda hivi vya cement kama cha Wazo Hill pale Dar es Salaam na viwanda vingine, bomba hili Serikali ya China iko tayari kuingiza pesa kwa condition kwamba Serikali ya Tanzania iwekeze bilioni 181 kama 15% ya mtaji. Nimepitia Vitabu vyetu vyote hivi vya Bajeti ya Maendeleo na kadhalika, hiki kitu hakipo. Mimi niwaombe tu kwamba kama tunataka kupunguza gharama za uzalishaji, ikiwemo uzalishaji wa cement lazima tu-invest kwenye gesi na falsafa ya mchango wetu ambao mimi nauunga mkono ni kwamba tulinde viwanda vya ndani, hiyo ndiyo principle. Viwanda vyetu vya saruji, iwe ni Mbeya, Tanga au Dar es Salaam vingeweza kuwekewa mazingira ya kupunguza cost za uzalishaji na kulinda na kumsaidia Mtanzania kwenye ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie eneo lingine, mimi siungi mkono bajeti hii iliyo mbele yetu mpaka Serikali itoe maelezo ya kina sana na siungi mkono siyo kwa sababu niko Upinzani, kwa sababu kuna hoja Serikali imeleta nyingi tu hapa katika Mikutano iliyopita nimeziunga mkono, Maazimio yale ya SADC, UNESCO na mambo mengine, lakini hili siungi mkono na siungi mkono kwa sababu wananchi wa Jimbo langu walionileta hapa, wamenituma nisiunge mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Waziri kusoma Hotuba ya Bajeti, mimi niliandika kwenye ukurasa wangu wa mtandao kwamba hotuba hii ya Waziri imejaa matumaini hewa na bajeti ni ya kiini macho na nilisema hivyo kutokana na takwimu za bajeti yenyewe. Ukichukua kwa mfano suala dogo tu la tozo la faini kwa Madereva kwa mfano kwa watu wanaoendesha vyombo vya usafiri, Waziri alisema kwamba faini inapanda mpaka shilingi 50,000, Muswada wa Sheria ya Fedha unasema faini inapanda mpaka shilingi 300,000, Kitabu cha Mapato ya Serikali, Kitabu cha Mapato ukiangalia faini sehemu ya Wizara husika inaonesha Serikali haikusudii kugeuza leseni na faini hizi kama chanzo cha mapato lakini mantiki ya kupandishwa kwa kiwango hiki iko wapi? Madereva wa pikipiki wa Mbezi, Madereva taxi wa Ubungo na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri wa daladala na kadhalika wamenituma katika hili nisiunge mkono bajeti kwa sababu hii unless hiki kitu kiondolewe. Tatizo siyo ukubwa wa faini, faini ya shilingi 20,000 tu sasa hivi iliyopo, ama 40,000 ama ngapi, tatizo ni enforcement ya Sheria, rushwa iliyotapakaa. Kwa hiyo, unapoongeza kiwango cha faini, unaongeza tu kiwango cha rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kwamba, kweli ajali ziko nyingi hata kwenye pikipiki kule Dar es Salaam ajali zinaongezeka sana lakini tufikirie zaidi. Mimi ningeshukuru kama Waziri angekuja na mkakati kwamba sasa tunahakikisha kupitia Chuo cha Usafirishaji pale Dar es Salaam tunatoa mafunzo kwa Madereva pikipiki, Idara yetu ya Traffic inakwenda kutoa mafunzo inafanyaje mambo kama haya, ningetarajia kwamba haya ndiyo yangekuwa kipaumbele. Kwa hiyo, katika hili siungi mkono kwa sababu hiyo niliyozungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inasema kwamba kipaumbele ni nishati na kadhalika, lakini ni maneno. Nimezungumza suala la bomba la gesi ambalo linahitaji investment ya bilioni 181 na ningeweza kuzungumza mengine lakini kwa sababu nina platform nyingine ya Uwaziri Kivuli nitazungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kwenye eneo lingine la msingi sana ambalo linafanya nisiunge mkono bajeti hii. Bajeti inasema principle kubwa tunakwenda kupunguza gharama za maisha kwa wananchi, tunapunguzaje kwa sababu gharama zetu zinapanda kwa sababu ya nishati ikiwemo mafuta na umeme, basi tunapunguza tozo kwenye mafuta. Kauli hiyo ni kauli ya kiini macho ndiyo maana Waziri alipotoa hoja yake akasema ufafanuzi atautoa tarehe 22 wakati tutakapojadili Muswada wa Sheria ya Fedha, nimeupitia huu Muswada tutakuja kuujadili baadaye, lakini principle ya kukuza tozo haiwezi kusaidia kushusha kwa kiwango kikubwa bei ya mafuta sababu tozo zote za taasisi hizi SUMATRA, TBS changanyanga na EWURA na kila kitu haifiki 3% ni 2.3% tu ya bei ya mafuta. Tozo za makampuni binafsi ya mafuta ni 2% jumla ya tozo zote hazifiki hata 5%. Sababu kubwa ya bei ya mafuta kuwa juu kwenye Taifa letu ni ukubwa wa kodi, asilimia 26 ya bei ya mafuta kwa lita ni kodi, ni takribani shilingi 600. Sasa Muswada huu haujagusa kodi, hotuba haijagusa kodi, vitabu vya mapato havijaigusa kodi kwa sababu hiyo bei ya mafuta itashuka hata Serikali ikijitahidi vipi kati ya shilingi 100 mpaka shilingi 200 ugumu wa maisha utaendelea kuwa pale pale kwa ari, kasi na nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kuhusu nishati ya gesi ambayo ingetumika majumbani kama LPG, gesi hii kama watu wangeitumia ingepunguza bei ya nishati nyingine. Tunazungumzia kuhusu gesi kutumika kwenye magari ambayo ingeshusha nusu ya nauli Dar es Salaam au nusu ya gharama. Investment kwenye gesi na miundombinu ya gesi siyo bomba tu lile na mitandao ya gesi, vituo vya kujazia mafuta ya gesi na kadhalika ni kama vile imeachiwa TPDC tu peke yake na hiyo retention ya 50% kama tunataka kupunguza gharama za maisha lazima pamoja na kupunguza kodi kwenye mafuta twende kuwekeza kwa nguvu sana kwenye nishati mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema tutapunguza gharama za maisha kwa sababu tutapunguza bei ya chakula, tutafungua strategic grain reserve na mambo mengine yamezungumzwa sana humu kwenye hotuba, lakini ni matumaini hewa na kwa fact kama kwenye mwaka huu wa fedha uliomalizika, Serikali imefungua ghala, Serikali ikifungua ghala maana yake mimi na wewe na Mtanzania mwingine tunaingia loss kwa sababu yale mahindi tumeyaweka mle kwenye ghala kwa pesa zetu, ime-inject kwenye soko lakini bei haijashuka. Niwaeleze tu siri moja na Waziri ukitaka nitakuletea taarifa kimaandishi, bei haishuki Manzese pale kwa sababu chakula kinachotolewa hiki cha kutoka katika hii grain reserve watu wanabeba wanakwenda kuuza nje kwa bei kubwa zaidi, kwa hiyo haishushi sembe pale Dar es Salaam, sijui Makurumla sijui wapi sembe haishuki, enforcement iko weak. Kwa hiyo, nitaunga mkono hoja kama haya yatatolewa ufafanuzi wa kina sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii kuna mambo humu ya maji, barabara na kadhalika na kwa kwetu sisi Dar es Salaam mtu ukisikia maji, barabara na kwa Ubungo kulivyo na shida ya maji mtu anaweza kusema kwa nini huyu anakataa kuunga mkono bajeti wakati bajeti inazungumza kuhusu maji, barabara, tatizo ni matumaini hewa maana kuna tofauti kati ya maneno na matendo. Ukiingia sasa kwenye Kitabu cha Bajeti cha Maendeleo cha Wizara ya Maji, ile specific section ya Wizara ya Maji, ukiangalie investment ambayo imewekwa pale kwa ujenzi wa bwawa la Kidunda ambayo ingesaidia siyo watu wa Morogoro tu kwa sababu Kidunda iko Morogoro, ingeboresha flow ya maji kwenye Ruvu Juu ambayo inge-service watu wa Ubungo kuanzia Kiluvya, Kwembe na kwingineko, investment ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija mradi wa Kimbiji na Mpera, Mkuranga na Kigamboni ambao utasaidia vilevile Ubungo na maeneo mengine ya Dar es Salaam, Serikali ilisema hata kwenye Baraza la Mawaziri najua Mheshimiwa Pinda atakubaliana na mimi walisema kwamba sasa tutaingiza pesa za ndani ili tatizo la maji Dar es Salaam liishe, lakini ukiangalia 35 bilioni ni expectation za pesa za nje. Mimi nitaunga mkono hoja tu kama kweli tukidhamiria kwa dhati kutenga rasilimali kwa ajili ya kuboresha hii miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri amesema kwenye hotuba yake kwamba sasa hii bajeti inakwenda kuondoa tatizo la foleni Dar es Salaam, lakini ukipitia bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwenye kifungu kinachohusika na decongestion of Dar es Salaam, kupunguza foleni Dar es Salaam, kimetengewa bilioni tano peke yake, sisi wa Dar es Salaam nikiwemo mimi wa Ubungo ambao takribani 80% ya mapato yanatoka kwetu five billion decongestion, 20 billion fly over, siungi mkono hoja mpaka tupate kwanza ufafanuzi wa kina kutoka kwenye Serikali, ahsante. (Makofi)

Chanzo: Hansard-Tarehe 16 Juni 2011 Kikao Cha Sita Mkutano wa Nne

Monday, June 27, 2011

Tahadhari na kauli za Pinda kuhusu Katiba Mpya

Tarehe 25 na 26 Juni 2011 Vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitangaza kwamba katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazinduliwa tarehe 26 Aprili 2014 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
Kufuatia ahadi hiyo ya Waziri Mkuu, baadhi ya wananchi wa Ubungo na vyombo mbalimbali vya habari mmetaka kupata kauli yangu kuhusu tamko husika. Naomba kuwasilisha kwenu maoni yangu yafuatayo:

Pamoja na kutambua kwamba hatimaye Serikali imetangaza muda rasmi wa ukomo wa kukamilika kwa mchakato husika bado ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inapaswa kupokelewa kwa tahadhari na anapaswa kutoa kauli ya kina bungeni itayoambatana na kuweka ratiba katika mipango, maazimio na sheria.

Hii ni kwa sababu katika Hotuba yake bungeni kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge ya mwaka 2011/2012 Waziri Mkuu Pinda hakueleza tarehe hiyo badala yake alitoa tu kauli ya ujumla kwamba “Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba dhamira inatekelezwa ili nchi yetu iwe na katiba mpya kabla ya mwaka 2015”. Hivyo, ni muhimu ukomo huo wa Aprili 2014 kuwasilishwa rasmi bungeni kupitia kauli ya serikali au kupitia majumuisho ya hotuba ya Waziri Mkuu kabla ya mjadala wa muswada wa sheria na uzingatiwe katika mipango, maazimio na sheria.

Ikumbukwe kwamba tarehe 19 Disemba 2010 na 27 Disemba 2010 kupitia mikutano na wanahabari wakati nikieleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi kuhusu mchakato wa katiba mpya na kutoa taarifa ya hoja husika nilieleza bayana kwamba kati ya mambo ambayo yanapaswa kupangwa na bunge ni pamoja na muda wa mchakato wa katiba mpya; suala ambalo lisingezingatiwa katika mchakato uliotangazwa awali kufanywa na serikali bila kuanzia bungeni.

Nilieleza wasiwasi wa wadau mbalimbali kuwa ukomo wa muda usipowekwa kwa mujibu wa sheria ama maazimio ya bunge, serikali inaweza kuchelewesha mchakato mzima kwa kutoa visingizio mbalimbali ili usikamilike mapema kuwezesha maandalizi ya kisheria na kitaasisi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia katiba mpya.
Aidha umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa kupitia Semina Elekezi kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa kwa tahadhari kwa kuwa imeambatana na kauli tata kuhusu mchakato mathalani serikali kutokuwa na uhakika kuhusu wakati ambapo muswada wa sheria ya mapitio ya sheria ya marekebisho ya katiba wa mwaka 2011 utawasilishwa bungeni.

Waziri Mkuu Pinda amenukuliwa akisema kwamba muswada huo utawasilishwa bungeni mwishoni mwa mkutano wa nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa au mwanzoni mwa mkutano wa tano wa bunge utakaofanyika Oktoba 2011; wakati katika mkutano wa tatu wa bunge Waziri Mkuu aliahidi kwamba muswada huo utarejeshwa katika mkutano wa nne wa bunge.
Ikumbukwe kwamba tarehe 30 Machi 2011 nilitoa tamko la kueleza kushtushwa na maudhui ya muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011 (The Constitutional Review Act 2011) uliochapwa katika gazeti la serikali toleo No. 1 Vol. 92 la tarehe 11 Machi 2011.

Nilieleza kwamba maudhui ya muswada huo yamedhihirisha tahadhari niliyotoa mara kadhaa kwamba serikali haina dhamira ya kweli ya kuhakikisha panakuwepo na mchakato mzuri wa kuwa na katiba mpya; matokeo yake ni muswada huo uliowasilishwa kwa hati ya dharura kuondolewa katika ratiba ya kupitishwa katika mkutano wa tatu wa bunge kutokana na shinikizo la wadau mbalimbali. Hivyo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kutoa kauli bungeni kueleza bayana iwapo hati ya dharura ya muswada huo ilifutwa basi muswada husika uwasilishwe kwa kufuata taratibu za kawaida kwa mujibu wa kanuni za bunge.

Pia, umma unapaswa kuipokea kwa tahadhari ahadi hiyo ya Waziri Mkuu kwa kuwa imeambatana na kutolewa kwa maelekezo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala kuhusu maudhui ya mchakato wa katiba na kipi kinakusudiwa kufanywa na serikali wakati ambapo bado sheria haijapitishwa na bunge.

Maelekezo hayo ya Waziri Mkuu Pinda yanadhihirisha kwamba tayari serikali imeshachukua msimamo kuhusu mchakato utakaotumiwa kuandika katiba mpya hiyo; hali inayoashiria kuwa serikali ina dhamira ya kulitumia bunge kama muhuri (rubber stamp) ya kupitisha mchakato ambao tayari ulishapitishwa ndani ya serikali na maelekezo ya utekelezaji kuanza kutolewa kwa watendaji wa serikali ngazi ya chini kabla ya sheria kupitishwa.

Ikumbukwe kwamba tarehe 30 Machi 2011 nilitahadharisha kwamba muswada uliowasilishwa bungeni umelenga kuhalalisha yote ambayo yalitangazwa kufanywa na Rais kuhusu mchakato wa katiba mpya na kupingwa na wadau mbalimbali na yanataka kupewa uhalali kwa sheria inayotaka kutungwa na bunge kupitia muswada huo; mchakato ambao Waziri Mkuu Pinda ameurejea katika hotuba yake.

Kadhalika umma unapaswa kuipokea ahadi hiyo ya Waziri Mkuu Pinda kwa tahadhari kubwa kwa kuwa imeambatana na maelekezo ya kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya wawe mstari wa mbele kuongoza mchakato huo wakati inaeleweka wazi kwamba wadau mbalimbali wamelalamikia mamlaka waliyopewa watendaji wa serikali katika mikutano ya kukusanya maoni kuhusu katiba kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa awali ambao wananchi walitaka vifungu husika vibadilishwe.

Ikumbukwe kwamba watendaji hao wamelalamikiwa kwa miaka kadhaa kutumia madaraka yao vibaya ikiwemo kudhibiti uhuru wa wananchi katika kutoa maoni kwenye tume mbalimbali ambazo zimewahi kuundwa na serikali nyakati za nyuma kwa masuala mbalimbali ikiwemo yanayohusiana na marekebisho ya katiba. Aidha kati ya mambo ambayo wananchi wameanza kuyatolea maoni kwenye maudhui ya katiba ni pamoja na kutaka kufutwa au kupunguzwa mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya; hivyo kitendo cha kuwaweka mstari wa mbele katika mchakato ni dalili za serikali kutokuwa na dhamira ya kweli ya kutaka mabadiliko ya katiba.

Katika muktadha huo; na kwa kuwa serikali ilishawasilisha awali muswada wa katiba natoa mwito kwa Spika na Ofisi ya Bunge kuhakikisha kwamba bunge linachukua nafasi yake kuanzia hatua za msingi kuhakikisha suala hili la mchakato wa katiba mpya lipata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) yanayohusu kutunga sheria na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Hivyo, badala ya kusubiri mpaka mwishoni mwa mkutano huu wa bunge tarehe 29 mpaka 30 Agosti 2011 ndipo wabunge wapewe tena muswada wa mabadiliko ya katiba pamoja na marekebisho yake yaliyofanyika ikiwemo tafsiri katika lugha ya Kiswahili; utaratibu wa kikanuni ufanyike kuhakikisha taarifa ya serikali inatolewa mapema pamoja na muswada huo nyeti.

Kwa upande mwingine umma unapaswa kuzipokea kwa tahadhari kauli za Waziri Mkuu Pinda kuhusu mchakato wa katiba mpya kwa kurejea msimamo wa wake wa awali kuhusu mabadiliko ya katiba alioutoa wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 17 Disemba 2010 ulikuwa na kumshauri Rais aunde jopo shirikishi ili kuratibu na kusimamia mchakato husika.

Izingatiwe kuwa tarehe 9 Februari 2011 nilitoa tamko la kupokea kwa tahadhari uamuzi wa Serikali kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kubadili misimamo ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kuamua kukubaliana na mwito wa kutaka mchakato husika uanzie bungeni kupitia kutungwa kwa sheria ya bunge ya kuratibu na kusimamia mchakato husika kwa kuwa maneno ya kauli zilizotolewa hayaambatani na vitendo vya dhati vya kuweka mchakato mzuri wa katiba mpya.

Uthibitisho wa mwelekeo huo ni kwamba Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/2012-2015/2016) uliotiwa saini na Rais Kikwete tarehe 7 Juni 2011 haukuweka kipaumbele haja ya katiba mpya kwenye eneo la utawala bora na utawala wa sheria. Aidha, bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 haikuweka bayana na kwa kiwango cha kutosha rasilimali kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya suala ambalo pamoja na maelezo ya Waziri wa Fedha wakati wa kuhitimisha hoja bado serikali ina wajibu wa kulitolea ufafanuzi wa kina katika mkutano wa Bunge unaoendelea.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)

Mgawo wa Fedha za Mfuko wa Jimbo

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika anatoa taarifa kwa umma kwamba utekelezaji wa miradi iliyochangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) kwa mwaka wa fedha 2010/2011 awamu ya kwanza uko katika hatua za mwisho na kwamba mchakato wa uteuzi wa miradi ya awamu ya pili umeanza.

Ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu kwa mujibu wa Sheria namba 16 ya mwaka 2009 iliyounda mfuko husika, Mnyika ameitisha kikao cha kamati ya usimamizi wa mfuko wa jimbo ambacho kitafanyika tarehe 27 Juni 2011 katika ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni.
Pamoja na ajenda nyingine kikao hicho kitapokea taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika kukamilisha miradi iliyoteuliwa katika awamu ya kwanza.

Miradi inayoendelea kutekelezwa kutokana na fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo la Ubungo katika mgawo wa awamu ya kwanza iliyopangiwa jumla ya shilingi 70,245,433 ni pamoja na: Ukarabati wa Jengo la Kutoa huduma ya afya kwa wakinamama wajawazito na watoto Kata ya Kwembe Mtaa wa Msakuzi (27,245,433); Kuchangia ujenzi wa Kituo Kidogo cha Polisi Kata ya Ubungo Mtaa wa Msewe(6,000,0000); Ujenzi wa Vyoo katika Shule ya Sekondari ya Hondogo Kata ya Kibamba Mtaa wa Kiluvya (22,000,000); Ununuzi wa madawati 200 ya Shule ya Sekondari Mburahati katika kata ya Mburahati (13,000,000) na Kuchangia Vifaa vya Ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Kimara Mtaa wa Mavurunza.

Aidha, Mbunge anapenda kuwataarifu wananchi kwamba fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo zilizotengwa kwa Jimbo la Ubungo katika mgawo wa awamu ya pili ni shilingi 69,819,663. Fedha hizo zimetolewa toka Serikali Kuu kwa vipindi viwili; Mei 2011 (Tshs 34,910,000) na Juni 2011 (Tsh. 34,909,663) na kuingizwa katika akaunti ya mfuko inayoratibiwa na Manispaa ya Kinondoni.

Mnyika amesema kwamba kikao cha kamati ya kusimamia mfuko atakachokiongoza kitaanza uteuzi wa miradi itayochangiwa na mfuko huo kutokana na mambo mbambali yaliyowasilishwa. Mnyika amehimiza wananchi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa maendeleo ya jimbo.

“Pamoja na kuwa mfuko huu unachochea jitihada hizo za maendeleo, bado naendelea kuunga mkono harakati za wadau wengine za kutaka mabadiliko katika mfumo mzima wa sheria iliyounda mfuko husika kutokana na kuiingiliana na majukumu ya mbunge kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63(2) na (3). Hata hivyo wakati marekebisho hayo yakisubiriwa ni muhimu kuhakikisha uwajibikaji katika hatua zote” , amesema Mnyika.

Mnyika amesema kwamba maendeleo yenye kugusa watu wengi na sekta nyingi yanaletwa kwa kupitia uwajibikaji katika Baraza la Madiwani na Bungeni kwa kuzisimamia serikali za mitaa, serikali kuu na taasisi zake sanjari na kuunganisha nguvu ya umma ya sekta binafsi.

Imetolewa tarehe 26 Juni 2011 na:

Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge

Saturday, June 25, 2011

Mgawo wa kizembe wa umeme; serikali iwajibike

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja anapaswa kuwajibika na kutoa kauli kwa umma na bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 ya Bunge kuhusu mgawo mkubwa wa umeme uliotangazwa na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwa utaikumbuka mikoa 18 inayopata umeme kupitia Gridi ya Taifa.

Aidha kabla ya kusubiria kutoa kauli bungeni Waziri Mkuu anapaswa kuingilia kati kwa haraka kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na TANESCO ili kuharakisha maamuzi ya kupunguza muda wa mgawo unaoendelea hivi sasa.

Hii ni kwa sababu pamoja na kupungua kwa vina vya maji katika baadhi ya mabwawa zinazoelezwa; kwa sehemu kubwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa umechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia Rais, Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

Maelezo ya kwamba mgawo huu umesababishwa na mitambo ya IPTL kuzalisha MW 10 badala ya MW 100 kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) yanatosha kwa serikali kuwajibika kutokana uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua stahili kuchukuliwa.

Mara kadhaa tumetahadharisha kwenye vikao na hadharani mara kwa mara kuhusu suala hilo lakini inaelekea kuna ombwe na kiuongozi na kimaamuzi katika serikali ambalo linaambatana na hali mbaya ya kifedha ndani ya serikali inayoongozwa na CCM kutokana na fedha nyingi za umma kutumiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa pili wa Bunge kikao cha sita tarehe 15 Februari mara baada ya kauli za Mawaziri ambapo Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya umeme nchini na utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi kifupi na cha kati nilitoa hoja ya dharura kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (e) na kanuni ya 47 ili bunge lijadili jambo la dharura la mgawo wa umeme unaolikumba taifa.

Katika ya hatua za dharura ambazo zingejadiliwa kwa kina ni ufanisi katika matumizi ya mitambo ya IPTL ikiwemo kuboresha taratibu za upatikanaji wa mafuta mazito, kuharakisha mchakato wa kupata mitambo ya MW 260; kuharakisha kukamilisha mitambo ya MW 100 Ubungo, MW 60 Mwanza, kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya mitambo na hatua nyingine za dharura; iwapo hoja hiyo ingejadiliwa wakati huo bunge lingepitisha maazimio ya kuwezesha hatua za mapema kuchukuliwa kudhibiti mgawo mkubwa uliolikumba taifa mwezi Mei na unaoendelea kulikabili nchi hivi sasa.
Pamoja na bunge kutojadili suala hilo baadhi ya ushauri wa kurekebisha kasoro zilizoendelea ulitolewa kwa serikali kupitia kamati ya nishati na madini mwezi Februari 2011 hata hivyo kuna mwelekeo wa kutokuwa na uongozi thabiti katika serikali wa kukabiliana na tatizo la mgawo mkubwa wa umeme.

Tarehe 2 Aprili 2011 nilitoa kauli ya kuitaka serikali ieleze maandalizi ambayo yamekwishafanyika mpaka hivi sasa kukabiliana na tatizo la upatikanaji, usafirishaji na uhifadhi wa mafuta mazito (HFO) ambayo yatahitajika kwa kiwango kikubwa katika kuendesha mitambo ya kufua umeme wa dharura ikiwemo IPTL na ya MW 260 kufuatia hotuba ya Rais Kikwete ya Aprili Mosi 2011 akilihutubia taifa ambayo haikuonyesha namna ambavyo serikali imejiandaa ipasavyo kukabiliana na mgawo wa umeme unaolikumba taifa.

Tarehe 22 Mei 2011 wakati taifa likikumbwa na mgawo mkubwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukarabati wa visima vya gesi asilia inayotumika kuendeshea mitambo ya umeme nilitahadharisha kwamba mgawo mwingine mkubwa zaidi unaweza kutokea iwapo hatua zaidi na za haraka hazitachukuliwa kuhusu upatikanaji wa mafuta mazito, gesi asilia na uharakishwaji wa mchakato wa kupata mitambo ya dharura ya MW 260.

Kauli zilizotolewa na Serikali baada ya kumalizika kwa ukarabati wa visima vya gesi kwamba mgawo ulikuwa umemalizika bila ya serikali kuchukua hatua za haraka kuzirekebisha kasoro tulizozieleza ililenga kutoa matumaini hewa kwa wananchi ili kuvuta muda kwa ajili ya kutoa visingizio vingine mwezi Juni kwa matatizo ambayo yalifahamika mapema.

Aidha kutokana na udhaifu wa kiutekelezaji Waziri Mkuu Pinda amekwepa katika Hotuba yake ya Bajeti ya tarehe 24 Juni 2011 kuzungumzia tatizo la mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa badala yake ameeleza tu kwamba nishati ya uhakika itapatikana miaka michache ijayo. Hii ni kwa sababu Waziri Mkuu Pinda ameshindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi wa MW 100 Ubungo na MW 60 Mwanza ambayo aliiahidi kupitia hotuba yake ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 na mradi wa MW 200 Kiwira ambayo kama ingetekelezwa kwa wakati kuanzia ilipowekwa kwenye mipango ya serikali mwaka 2009 ingekuwa imekamilika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hivyo taifa lisingekuwa na mgawo mkubwa wa umeme na kuingia gharama kubwa za mitambo ya kukodi kama ilivyo sasa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kutoa majibu wakati wa majumuisho ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo kueleza kwa watanzania yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni sababu za serikali kutokutekeleza kwa wakati mipango ya kulinusuru taifa kutokana upungufu wa umeme unaochangiwa na ukame hali ambayo aliifahamu tangu mwaka 2008 alipoingia madarakani. Ikumbukwe kwamba Waziri Mkuu Pinda aliingia madarakani wakati huo baada ya Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa kujiuzulu kufuatia maamuzi ya kifisadi yaliyofanywa na serikali wakati wa mgawo wa umeme kati ya mwaka 2006 mpaka 2007.

Kupitia kauli bungeni serikali ieleze ukweli kuhusu sababu za mgawo mkubwa wa umeme uliotokea mwezi Mei na unaoendelea hivi sasa na hatua ambazo serikali imechukua kwa waliosababisha hali hiyo. Aidha Serikali ieleze ukweli kwamba Waziri Ngeleja alitoa kauli potofu bungeni tarehe 15 Februari na Rais Kikwete alitoa ahadi hewa kupitia Hotuba yake kwa Taifa tarehe 1 Aprili 2011 kuhusu ukodishwaji wa mitambo ya MW 260 kwa ajili ya umeme wa dharura kuanzia mwezi Julai mwaka 2011. Serikali iwaeleze watanzania ukweli kuwa imeshindwa kutekeleza mpango huo na kueleza hatua mbadala za kurekebisha hali hiyo ili kuepusha mgawo huu ulioanza mwezi Juni kuendelea mpaka mwezi Disemba mwaka 2011 hali ambayo itakuwa ni janga kwa taifa.

Aidha serikali ieleze mikakati mahususi ya muda mfupi ya kushirikiana na sekta binafsi iweke mazingira wezeshi ya kisheria, kikanuni na kibajeti ya kuweka msingi wa utekelezaji wa miradi ya Somangafungu (MW 230), Mnazi Bay (MW 300), Kinyerezi (MW 240), maporomoko ya Ruhudji (MW 358) ili ikamilike kwa haraka zaidi kuliko ilivyopangwa hivi sasa.

Katika kauli hiyo serikali iwaeleze watanzania kupitia bunge mkakati mahususi wa kuwekeza katika kuongeza upatikanaji wa gesi asilia kwa ajili ya kuendesha mitambo hiyo ya umeme na pia kama sehemu ya mpango wa nishati mbadala yenye kupunguza gharama za maisha zinazochangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na mzigo mkubwa wa kodi ambao utaendelea hata baada ya serikali kutangaza punguzo dogo la kodi na tozo.

Kwa uchumi na usalama wa nchi serikali ya Tanzania inapaswa kufanya maamuzi mazito na kuwasilisha maombi bungeni ya kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 131 ambacho kinahitajika kama sehemu ya kuchangia asilimia 15 ya mkopo kwa ajili ya mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na baadaye hadi Tanga. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 ambayo imepitishwa serikali haijatenga kiasi hicho cha fedha hali ambayo itakwamisha utekelezaji wa mradi huo unaohitaji kati ya mwaka mmoja na miaka miwili kuweza kukamilika. Mradi huo usipotekelezwa kwa wakati ipo hatari ya baadaye ya kuwa na mitambo ya umeme ya gesi lakini ikakosekana gesi asilia ya kuiendesha na pia taifa litashindwa kutumia vizuri fursa ya kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kutumia nishati mbadala ambayo inapatikana hapa nchini.

Hatua hizi zinahitaji sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni roho ya taifa letu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kwa ujumla KUWAJIBIKA. Kupungua kwa uzalishaji na kuishi gizani miaka 50 baada ya uhuru ndio mafanikio ambayo serikali inayoongozwa na CCM inataka tujivunie! Poleni wananchi, serikali inapaswa kutuomba radhi! Kambi rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, kupitia kwa Msemaji wake Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini itaendelea kupitia Mkutano wa Nne wa Bunge kuifuatilia Serikali iliyoko madarakani kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa maslahi ya umma wa watanzania.

Wenu katika utumishi wa umma;

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-25 Juni 2011

Tuesday, June 21, 2011

Mbunge awataka DAWASCO kutoa maelezo kuhusu kero ya maji

MBUNGE AWATAKA DAWASCO KUTOA MAELEZO KUHUSU HATUA AMBAZO WAMEZICHUKUA KATIKA KUSHUGHULIKIA MATATIZO YA UPATIKANAJI WA MAJI KATIKA MAENEO MBALIMBALI YA JIMBO LA UBUNGO

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ameandikia barua Kampuni ya Maji Safi na Maji taka Dar es salaam (DAWASCO) kuwataka kutoa maelezo kuhusu hatua ambazo wamezichukua katika kushughulikia matatizo ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.

Mnyika amesema kwamba iwapo DAWASCO haitatoa maelezo mapema ataeleza hatua za kibunge ambazo atazichukua ili kuhakikisha kampuni hiyo inatimiza wajibu wa kushughulikia kero ya maji katika kata mbalimbali za jimbo hilo.

Ifuatayo ni nukuu ya baadhi ya maelezo yaliyo katika barua ya Mbunge kwa DAWASCO:
“Tarehe 19 Januari 2011 niliiandikia barua ofisi yako yenye kumbu. Na. OMU/ MJ/004/2011 kuwaalika DAWASCO kuja kushiriki na kutoa mada katika Kongamano la Maji Jimbo la Ubungo; hata hivyo hakuna mtendaji yoyote toka ofisi yako aliyefika kutimiza wajibu husika wala barua tajwa kujibiwa.

Tarehe 15 Machi 2011 niliandika tena barua kwa ofisi yako kuwasilisha Ripoti ya Kongamano husika na kutoa mwito kwa hatua kuchukuliwa; hata hivyo ofisi yako mpaka sasa haijaeleza hatua ambazo imechukua au walau kutambua kupokea ripoti husika.
Tarehe 27 Februari 2011 na tarehe 6 Machi 2011 nilifanya mikutano na wananchi katika kata ya Goba kuhusu maji; pamoja na kuwa mradi katika eneo hilo uko chini ya wananchi vielelezo vilitolewa vya malalamiko ya muda mrefu kutaka hatua kuchukuliwa na DAWASCO kuhusu uharibifu wa mita na pia mapendekezo ya kutaka huduma katika eneo husika kutolewa na DAWASCO moja kwa moja.

Tarehe 26 Machi 2011 nilifanya ziara kata Kata ya Makuburi katika Mitaa ya Makoka, Muongozo na Kibangu na kubaini kwamba wananchi wa maeneo husika wamekuwa na ukosefu wa maji kwa miezi kadhaa hata katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yakipata maji na hivyo kutoa mwito kwa DAWASCO kuchukua hatua za haraka.

Tarehe 7 Mei 2011 nilifanya ziara kata ya Kimara na kubaini kwamba ujenzi wa visima katika mitaa iliyoanishwa na DAWASCO kwa mujibu wa ahadi ya Rais Kikwete ya tarehe 24 Mei 2010 haujakamilika kwa maeneo mengi.

Tarehe 8 Mei 2011 nilifanya ziara katika kata za Mbezi na kubaini upungufu mkubwa wa maji wakati kukiwa na upotevu wa maji katika maeneo ya Msigani.

Tarehe 22 Mei 2011 nilifanya ziara katika kata za Mabibo na Manzese na kubaini ukosefu wa maji katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata maji awali ikiwemo upungufu wa maji katika magati ya DAWASCO.

Tarehe 29 Mei 2011 nilifanya ziara kata ya Saranga na kubaini malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kuhusu kero ya maji ikiwemo kutokujulikana ama kutokufuatwa kwa ratiba ya mgawo wa maji.

Aidha katika kipindi husika nimepokea barua toka wateja na wananchi kuhusu maombi mbalimbali ambayo wameyawasilisha kwenu bila hatua stahiki kuchukuliwa au walau kupatiwa majibu kwa ukamilifu.

Mathalani maombi ya kuunganishiwa maji ya wananchi wa eneo la Burula (katika barabara ya Kimara Suca kuelekea Golani- barua yao ya tarehe 9 Agosti 2010), Mbezi Msakuzi (Hatua za utekelezaji baada ya barua ya DAWASCO/WSP/187/Vol III/42 ya 25/03/2009; Wananchi wa Msigani kwa ajili ya Wakazi wa kwa Mjanja ( Barua ya S/M/MSG/KN/001/2011 ya tarehe 10/01/2011 ambayo ilieleza mapendekezo yao mahususi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kuomba mkutano kati yao na DAWASCO ili kujadili maombi yao), Wananchi wa Malambamawili (kwa barua yao SM/MSG/MWL/KN/DWSC/02/2011 ya tarehe 3/2/2011).

Naelewa kwamba utatuzi wa kero ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo jimbo la Ubungo unahitaji hatua za muda mrefu, muda wa kati na muda mfupi. Hata hivyo, zipo hatua ambazo zingeweza kuchukuliwa kwa haraka kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na wananchi katika Kongamano na pia maombi ambayo yamewasilishwa DAWASCO bila kupatiwa majibu yoyote.

Nataka kupatiwa maelezo kuhusu shughuli ambazo zimetekelezwa na DAWASCO katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari 2011 mpaka Mei 2011 katika kuboresha upatikanaji wa maji kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo ikiwemo kuelezwa hatua mahususi ambazo zimechukuliwa kufuatia ripoti ya Kongamano na barua za wananchi.”

Pamoja na kuwa zipo hatua ambazo zimefanyika katika kupunguza kero ya maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo kufuatia Kongamano la Maji lililoitishwa na Mbunge tarehe 31 Januari, 2011; bado hali kwa ujumla wake hairidhishi suala ambalo limemfanya Mbunge kutaka maelezo ya kina kutoka DAWASCO kama sehemu ya kutimiza wajibu wake wa kusimamia serikali.

Imetolewa tarehe 14 Juni 2011:

Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge Ubungo

Sunday, June 19, 2011

TAMKO JUU YA KAULI ZA WAZIRI MKUU PINDA KUHUSU POSHO

TAMKO LA KATIBU WA WABUNGE WA CHADEMA JUU YA KAULI ZA WAZIRI MKUU PINDA KUHUSU POSHO

Katibu wa Wabunge wa CHADEMA nimeshangazwa na kauli za Waziri Mkuu Mizengo Pinda alizozitoa bungeni tarehe 16 Juni 2011 wakati akijibu maswali ya papo kwa papo.
Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli ya kuhalalisha posho za wabunge kwa hoja kwamba zinahitajika kwa ajili ya kuwapa watu wanaowaomba fedha nje ya ukumbi wa Bunge.
Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuifuta kauli yake, kwani inapotosha majukumu ya Bunge na Wabunge wake yaliyotajwa kwenye ibara ya 63 (2) na (3) ya kuisimamia serikali, kuwakilisha wananchi, kupitisha mipango na kutunga sheria. Kauli ya Waziri Mkuu Pinda inahamasisha siasa za fadhila (patronage) katika taifa, ambazo ndizo zimetumika na CCM kupandikiza mbegu ya rushwa katika uchaguzi kwa kisingizio cha takrima.

Kadhalika kauli ya Waziri Mkuu Pinda inadhihirisha hana dhamira ya dhati ya kutekeleza kwa ukamilifu na kwa haraka maagizo ya Rais Kikwete kinyume na Katiba Ibara ya 52 (3), ambayo inamtaka atekeleze au asababishe utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.

Aidha, Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli bungeni kuwa wabunge wengi wa CHADEMA wanazimezea mate posho hizo na kujaribu kuonyesha kwa umma kwamba hoja ya kutaka mabadiliko katika mfumo wa posho nchini ni ya wabunge wachache ndani ya CHADEMA.
Katibu wa Wabunge wa CHADEMA namtaka Waziri Mkuu Pinda aelewe kwamba suala la kutaka mabadiliko ya mfumo wa posho katika nchi yetu ni la pamoja kwa CHADEMA na natoa mwito aisome ilani ya CHADEMA kupata msingi wa msimamo huo.

Kama sehemu ya kuimarisha uchumi kwa kuondoa ubadhirifu Ilani ya CHADEMA ya Agosti 2010 kifungu cha 5.5.1 kipengele cha 5 imeeleza bayana kwa mifano kwamba serikali ya CCM imekuwa ikitenga kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya posho. Mfano katika mwaka 2008/2009 Serikali ya CCM ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 509 (Zaidi ya nusu trilioni kwa ajili ya posho mbalimbali) ambayo ilikuwa sawa na malipo ya mishahara ya mwaka mzima ya walimu 109,000. Aidha ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 ilieleza bayana kwamba Ofisi ya Rais Jakaya Kikwete ndiyo iliyoongoza kwa kujigawia posho ya zaidi ya Bilioni 148 kwa mwaka 2009/2010 huku Bunge likijagiwia Bilioni 36 katika kipindi hicho hicho.

Kipengele cha 6 kwenye Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 kimeeleza bayana kwamba Serikali ya CHADEMA itaweka utaratibu ili semina, warsha, mafunzo na vikao katika taasisi mbalimbali za umma zifanyike kama sehemu ya kazi bila uwepo wa posho maalum za vikao kwa siku (Sitting Allowances).

Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imefafanua kuwa lengo ni kupunguza posho hizi kwa zaidi ya asilimia 80 zikiendana na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya kwa haki. Uamuzi huu ungewezesha pia kuelekeza fedha zinazobaki katika miradi ya maendeleo.

Huo ndio msimamo ambao viongozi wa CHADEMA kwa umoja wetu ikiwemo wagombea wa nafasi mbalimbali tuliunadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa wabunge walioshinda wa majimbo na viti maalum ndio msimamo watakaoendelea kuusimamia ndani ya Bunge huku Chama kikihamasisha miongoni mwa jamii kwa kuunganisha nguvu ya umma. Suala hilo pia limejadiliwa katika vikao vya kamati ya wabunge ya chama na kuzingatiwa katika Bajeti Mbadala (Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012) ambayo imeeleza bayana namna ambavyo kiwango cha posho kimepanda kwenye bajeti ya serikali kwa ari, nguvu na kasi zaidi na kufikia takrikabani trilioni moja.

Nilitarajia kwamba baada ya Serikali ya CCM kuchukua msimamo huo na kuuingiza kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2011/2012-2015/2016 uliosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 7 Juni 2011 ambao kwenye ukarasa wa 17 unatamka bayana kwamba posho za vikao na nyinginezo zinapaswa kufutwa au kuwianishwa; Waziri Mkuu angeipongeza CHADEMA na wabunge wake kwa msimamo wao badala ya kubeza na kupotosha.

Kinyume chake na siku chache baada ya kauli ya Waziri Mkuu; Serikali ambayo yeye ndiye kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 52 (2) imefanya mkakati wa kupenyeza habari ya kuupotosha umma kwa kutumia orodha na saini za wabunge za mahudhurio ya vikao sanjari na habari ya kupindisha kutaka kuupotosha umma kwamba wabunge wa CHADEMA hawana dhamira ya dhati ya kutaka posho za vikao (Sitting Allowance) ziondolewe.
Ni vizuri Waziri Mkuu Pinda na watu wanaotumika ndani ya Serikali kutaka kuichafua CHADEMA na wabunge wake waelewe kwamba ambacho wabunge wa CHADEMA tunataka kwa umoja wetu ni kurekebishwa kwa mfumo mzima wa posho kama ambavyo tumeelezea katika Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Hali ya Uchumi na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Katika kushinikiza msimamo huo kutekelezwa wabunge kwa nafsi na nafasi zao wanauhuru wa kutumia njia mbalimbali kufikia lengo hili la pamoja. Wapo walioandika barua kutaka posho zao zielekezwe katika taasisi za kimaendeleo na wapo ambao wakizielekeza fedha hizo kuchangia shughuli za maendeleo katika majimbo yao kuanzia Novemba mwaka 2010. Hata hivyo, katika kuendeleza msimamo wa pamoja ikiwa Waziri Mkuu hatafuta kauli yake ama Ofisi ya Bunge kutoa ufafanuzi ikiwemo hatua mahususi kuelezwa bungeni kuhusu serikali itakavyoanza kufanya mabadiliko katika mfumo wa posho katika utumishi wa umma wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti; tutakaa kikao cha Kamati ya Wabunge wa chama (Party Caucus) kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu 109 na 110 kama sehemu ya kuweka msimamo wa pamoja kuhusu bajeti na kueleza hatua za ziada ambazo tutachukua kuhusu posho hizo za vikao (Sitting Allowance) na ubadhirifu mwingine katika serikali.

Aidha nachukua fursa hii kumtaarifu Waziri Mkuu Pinda kwamba posho ya kikao (Sitting Allowance) haijatajwa kwenye katiba wala kwenye sheria hivyo ni suala la kiutendaji ambalo yeye kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anapaswa kuwasiliana na Spika kuharakisha taratibu za kuziondoa bila kuleta visingizio vya kikakatiba na kisheria.

Napenda umma wa watanzania ufahamu kwamba Katiba Ibara ya 73 imetamka tu kuwa wabunge watalipwa mishahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na bunge lakini kifungu hicho hakitaji aina ya posho wala viwango.
Aidha Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais ataeleza kwa maandishi. Katika kipenge (d) sheria imetaja orodha (i) mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri, kujikimu na wasaidizi; katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao (Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye akaunti za wabunge moja kwa moja na CHADEMA imetoa tamko la kutaka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.

Kifungu 19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu ambacho kimefanya utolewe waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010 wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya vikao (Sitting Allowance).

Hivyo, kwa kuwa Rais Kikwete amesaini tarehe 7 Juni 2011 Mpango wa Miaka Mitano wenye kulenga kuondoa posho hizo Rais Kikwete anapaswa kufuta posho hizo haraka kwa kutoa waraka badala ya kusubiri mabadiliko ya kisheria na kikatiba kama Pinda alivyoeleza bungeni. Aidha, hatua hiyo iende sambamba Rais Kikwete kuonyesha mfano kwa kupunguza gharama za posho mbalimbali za vikao na safari za nje ambazo zinatumiwa na ikulu.

Imetolewa tarehe 19 Juni 2011 na:

John Mnyika
Katibu wa Wabunge wa CHADEMA
Na Kambi Rasmi ya Upinzani

Majibu kwa Maswali yenu kuhusu POSHO

Kutokana na maswali ya mara kwa mara toka kwa wananchi kupiti mtandao na simu ya mkononi kutaka kujua msimamo wangu kuhusu mjadala wa posho unaoendelea hivi sasa. Naomba niwakumbushe tu kwamba msimamo wangu nimekuwa nikiuweka bayana kuanzia kampeni za mwaka 2005 na hata za mwaka 2010; ambapo nimekuwa nikiahidi kwamba nikichaguliwa nitataka mabadiliko katika mfumo wa posho na mishahara ya wafanyakazi.
Nimekuwa nikieleza bayana kwamba siridhishwi na pengo la mishahara katika utumishi wa umma kati ya kima cha chini na kima cha juu, na niliahidi kwamba wakati nikiendelea kutaka mabadiliko katika mfumo wa mishahara na kuboreshwa kwa mishahara ya watumishi wa umma binafsi nitaonyesha mfano kwa kukata asilimia 20 ya mshahara kuelekeza katika kuchangia masuala ya elimu jimboni. Aidha, nimekuwa nikikosoa mfumo wa malipo ya posho za vikao (Sitting Allowance) na kutaka ubadilishwe na kama sehemu ya kutaka mabadiliko hayo nilitangaza hadharani kuelekeza posho hiyo katika masuala mbalimbali ya maendeleo. Kauli zangu hizo zimewahi kunukuliwa na vyombo kadhaa vya habari kwa nyakati mbalimbali. Nashukuru pia msimamo huu pia ni msimamo rasmi wa chama uliopo pia kwenye Ilani ya Chama ya Uchaguzi Mkuu 2010.

Mara baada ya kuchaguliwa nimekuwa nikitekeleza ahadi hiyo kwa kutoa asilimia 20 ya mshahara kuchangia elimu jimboni kupitia ofisi ya mbunge na Taasisi ya Maendeleo Ubungo (Ubungo Development Initiative). Nimekuwa pia nikizielekeza fedha hizo za posho ya vikao (Sitting Allowance) kwenye masuala ya kimaendeleo jimboni ikiwemo ya kuchangia mipango ya maji ya wananchi katika baadhi ya mitaa.

Na iwapo Serikali itaacha kuzifuta posho hizo kwenye mwaka huu wa fedha nitawasiliana na ofisi ya bunge kuweka utaratibu rasmi zaidi wa fedha hizo kuelekezwa moja kwa moja katika miradi ya maendeleo jimboni Ubungo hususani kupitia CDCF (ingawaje naungana na wanaharakati kupinga mfuko huo); lakini nitazingatia pia makubaliano ya pamoja kuhusu suala husika katika chama. Kabla ya kubadilishwa kwa mfumo mzima wa posho si jambo lenye maslahi ya umma kuziachia posho hizo zikatumiwa kiubadhirifu na serikali inayoongozwa na CCM badala yake ni lazima kuweka mazingira ya kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwenye masuala ya kimaendeleo kinyume na hapo itakuwa ni sawa sawa na ‘kumsusia fisi bucha’. Nilichukua pia msimamo kama huo kwenye suala la mikopo ya magari ya wabunge, wakati wa kampeni nilipinga kiwango cha mikopo kinachotolewa cha milioni 90 kwa ajili ya gari kuwa ni kikubwa; na baada ya kuchaguliwa nilipewa mkopo huo na kuupokea. Hata hivyo, niliendelea na msimamo wa kutonunua gari la milioni 90 na badala yake sehemu ya mkopo huo niliuelekeza kwenye mfumo wa kutoa mikopo kwa madiwani wa jimbo la Ubungo kwa ajili ya kazi zao. Naamini kwamba madiwani wanapaswa kuwekewa utaratibu bora zaidi wa kuwezesha utumishi wao; wakati tukiendelea kusukuma ajenda pana zaidi ya kuongeza mamlaka ya serikali za mitaa na uwajibikaji katika halmashauri niliona nianze kwa kuongeza ufanisi na madiwani wa jimbo letu kwa njia mbalimbali ikiwemo mfumo huo wa mikopo.

John Mnyika (Mb)

Friday, June 17, 2011

Mchango wangu Bungeni kuhusu Mpango

MCHANGO WANGU BUNGENI TAREHE 14 JUNI WAKATI WA KUJADILI RASIMU YA MPANGO WA TAIFA WA MIAKA MITANO

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya kwenye Mpango kwa mujibu wa Kanuni ya 57 na Kanuni ya 58 ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 63, Bunge ndiyo chombo kikuu kwa niaba ya wananchi chenye wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali na katika kutekeleza wajibu huu, Ibara ndogo ya (3) inatamka kwamba, kazi mojawapo ni kujadili na kupitisha mipango ya muda mfupi na muda mrefu na huu ndiyo wajibu tulionao mbele hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye maeneo mahususi ambayo nimewasilisha mabadiliko ambayo nitaomba yazingatiwe kwa mujibu wa Kanuni ya 57 na 58 kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza ni eneo ambalo liko ukurasa wa 117 wa nyaraka hii wa mpango wa miaka mitano. Hili ni eneo linalohusu miradi ya maji, sababu ya kuwasilisha mabadiliko haya ni kwamba huko nyuma kumekuwepo na miradi ya maji ikiwemo miradi mbalimbali katika Jimbo ambalo wamenituma kuwawakilisha la Ubungo. Miradi ambayo ilihusisha ulazaji wa mabomba ambayo yanajulikana zaidi kama mabomba ya Wachina, lakini pamoja na mabomba kuwekwa kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo mengi sana ukienda King’ong’o, Mbezi, Mavurunza, Makoka na kwingineko. Serikali imetumia pesa nyingi sana ikiwa kiasi kikubwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, lakini maji hayatoki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kuna mpango ambao unalenga kuchangia katika kurekebisha kasoro zilizotokea kipindi cha nyuma, lakini mpango wenyewe kama ukiachwa kama ulivyo utarudia kasoro za kipindi cha nyuma na kasoro kubwa iliyoko kwenye mpango huu ni kwamba ukitazama kwenye hilo jedwali la miradi hii ya maji ya Ruvu juu, Ruvu chini pamoja na ujenzi wa mabwawa Kidunda na visima Kimbiji na Mpera ambayo yangeongeza vilevile uzalishaji wa maji Dar es Salaam, yamegawanywa rasilimali zake katika kipindi cha miaka mitano. Kwa hiyo, ukianza utekelezaji mpaka utakapokamilika, kitakachotokea ni kama kinachoendelea sasa Ubungo, mradi wa mabomba wa Benki ya Dunia umewekwa, maji hayafiki, mabomba yameanza kuharibika, miundombinu imeanza kuharibiwa kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafahamu, ndani ya Baraza la Mawaziri, ndani ya Serikali, baada ya mijadala ya umma na sisi kule Ubungo tulifanya kongamano la wananchi la maji, Serikali ikaamua kwamba miradi hii ya Ruvu juu, Ruvu chini, ujenzi wa bwawa Kidunda na visima Kimbiji, Mpera ikamilike kwa ukamilifu wake ifikapo mwaka 2013 na Serikali kwa maana ya Rais akatoa kauli, Waziri wa Maji akatoa kauli hadharani, sasa kilichopo kwenye mpango, kinapingana na Kauli ya Waziri na Rais ya kumaliza miradi hii ifikapo mwaka 2013.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ya mabadiliko kwenye kifungu hiki ili kurekebisha hii hali, rasilimali zilizotengwa hapa kwa mwaka wa fedha 2014/2015 na mwaka wa fedha 2015/2016 zipunguzwe bila kuathiri jumla, zirudishwe nyuma kwenye miaka mitatu ya kwanza na nimewaeleza kwenye mapendekezo ambayo Wabunge mnayo nakala yake, kiwango cha pesa kinachopaswa kuhamishwa ili miradi ikamilike kwa wakati kuepusha hasara kama iliyoko hivi sasa kutokana na mradi wa mabomba ya Wachina na ili kutimiza kauli ya Rais na Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinyume cha mapendekezo haya ni kutengeneza bomu lingine la wakati la kutumia rasilimali nyingi sana, lakini mradi ukachukua miaka mingi kukamilika, miundombinu ikaanza kuharibiwa kabla hata maji kuanza kupatikana. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge hii ni kauli ya Mheshimiwa Rais, Waziri na Wabunge. Humu kuna Wabunge wa Majimbo mbalimbali ili si kwa ajili ya Jimbo la Ubungo tu, kuna Wabunge wa Mkuranga, Kigamboni, Wabunge wote wa Dar es Salaam na Wabunge wa maeneo mbalimbali ambao wanaamini katika usimamiaji wa kauli hizi kwa ukamilifu wake. Kwenye eneo hili nitaomba niishie hapa nihamie eneo lingine la mabadiliko ninayoyapendekeza. Hili lilikuwa linahusu ukurasa wa 147 kifungu cha A.1.4 ambacho kinahusiana na Kifungu cha 3.4.4 cha Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili liko ukurasa wa 127 ambao ni kifungu cha A1.2.2 ambacho kinatokana na Kifungu cha 3.4.1.1 cha kuhusiana na kupunguza foleni Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Mpango huu, yale mapendekezo ambayo wadau wamekuwa wakiyatoa na tumekuwa tukiyatoa kwa muda mrefu kwamba ili kupunguza foleni Dar es Salaam, lazima kuwekeza sana kwenye barabara za pembezoni. Humu kuna barabara zimeingizwa, mapendekezo yale yamekubalika, barabara ya kutoka Goba mpaka Mbezi, Mbezi Malambo Mawili mpaka Kinyerezi, Changanyikeni kwenda Chuo Kikuu kupitia Msewe na nyinginezo. Kabla sijasema pendekezo mahususi ambalo liko hapa kuhusiana na hii barabara nyingine, niombe tu katika kutekeleza Mpango huu ili jambo liharakishwe kwa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa litalikumba jiji la Dar es Salaam wakati wa utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi utakapoanza. Barabara ya Morogoro itakapoanza kutengenezewa njia maalum ya mradi wa mabasi yaendayo kasi, foleni ambayo itakuwepo kwenye barabara ya Morogoro, itakuwa ni foleni ya kihistoria kwa sababu barabara ni nyembamba lakini kutaanza construction pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maamuzi ya kujenga barabara za kuchuja magari, barabara ya kutoka External kupitia Kilungule mpaka Kimara na nyinginezo inabidi yaharakishwe, naelewa kwamba hizi barabara zote zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu, nipendekeze katika utekelezaji tathmini ya fidia ufanyike haraka ili zoezi lifanyike haraka kabla ya kuanza kwa ujenzi wa mabasi yaendayo kasi. Lakini kuna hoja mahususi iko hapa mbele ya barabara hii ambayo naomba iingizwe kwenye schedule, barabara ya kutoka Kimara kwenda Mavurunza mpaka Bonyokwa mpaka Segerea. Hii barabara ni muhimu iingizwe kwenye schedule hii niliyoisema ya barabara, katika ukurasa wa 127, kuna orodha ya barabara na hii barabara haipo, iingizwe kwa sababu ni ahadi ya Rais ya tarehe 24 Mei 2010 alivyokwenda kutembelea Mavurunza na alisema kwamba barabara hii ndani ya miaka mitano itajengwa kwa kiwango cha lami ili kupunguza foleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa isipokuwepo kwenye mpango wa miaka mitano maana yake ni kwamba hii ahadi itakuwa ni ahadi hewa. Sasa ninachosema tu hapa ni kwamba, wengine wanachambua, wanasema ahadi zote za ujumla za Rais zinafikia takriban trilioni 95, sasa hizi za hapa jumla ni trilioni kama 42 plus. Sasa ili kupunguza ule mzigo wa lawama kwamba kuna ahadi nyingi ambazo haziko kwenye Mpango, naomba kutoa pendekezo hapa kwa mabadiliko kwamba barabara hii ya kutoka Kimara kupitia Bonyokwa mpaka Segerea ambayo itaunganisha Majimbo haya mawili na kupunguza foleni iingizwe kwenye hii orodha kama ambavyo nimewasilisha kwenye jedwali la mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la nishati, Kifungu cha 3.4.1, kuna mambo mengi ambayo tungeweza kuzungumza kuhusu nishati, lakini hapa kuna pendekezo mahususi sana kwenye ukurasa wa 135, kwenye ile miradi ya umeme. Kuna mradi mmoja ambao Mheshimiwa Rais aliuzungumza Bungeni na baadaye aliuzungumza alipotembelea Wizara na baadaye kukatangazwa kuundwa Kamati ya kushughulikia mradi huo, mradi wa Stigler’s Gorge, lakini mradi huu pamoja na kutangazwa kwamba ndani ya miaka hii mitano utekelezaji wake unaanza, mradi huu kwenye miradi ya umeme inayozungumzwa haupo kwenye orodha ya miradi. Kwa hiyo, mabadiliko ninayoyapendekeza hapa ni kwamba, kwa ajili ya uzalishaji mwingi wa umeme wa Taifa letu na huu ni mradi mkubwa sana utekelezaji wa mradi huu, maandalizi yake ya kirasilimali na kifedha uingizwe ndani ya mpango huu wa miaka mitano ili tuweze kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ukurasa wa 112, mabadiliko mahususi yanahusiana na uzalishaji, manufacturing ya Kifungu 3.4.3, lakini hapa narejea kifungu 1.12, kwanza nashukuru kwamba concept ya Special Economic Zone imeingizwa kwenye Mpango. Nitaomba tu katika utekelezaji wake huko nyuma tumewahi kuwa na mipango ya kuanzisha viwanda, tukiondoa hivi viwanda ambavyo vina motisha maalum na Ubungo ni moja kati ya maeneo ambayo yalikuwa industrial area yaani ukizungumza kuhusu viwanda vya Dar es Salaam unazungumza UFI, uzalishaji wa Zana za Kilimo, unazungumza Ubungo Maziwa, uzalishaji wa maziwa, Ubungo Garment, Urafiki na kadhalika lakini viwanda vile vingi vimefungwa, vingine vinafanya biashara tofauti, hatimaye watu wanakosa ajira. Sasa wakati tunafufua vile viwanda tumeanzisha mkakati mwingine wa maeneo maalum ya viwanda likiwemo hili la Benjamin Mkapa Special Economic Zone lililopo pale Mabibo na kule kuna viwanda vinakusudiwa kuanzishwa. Sasa naomba, vitakapoanzishwa vichangie kwenye ajira lakini tufufue viwanda vile vile vilivyokufa ndani ya Jimbo la Ubungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa kuna hoja mahususi sana ambayo naomba izingatiwe ni sehemu ya 1.1.2 ambapo ndani ya Mpango huu inakusudiwa kama sehemu ya Benjamin William Mkapa Special Economic Zone kujenga bomba maalum la mtaro kutoka eneo la viwanda kupeleka kwenye mabwawa ya kumwaga uchafu yaliyoko pale Mabibo yanaitwa Mabibo oxidization ponds. Sasa naomba hili pendekezo lizingatiwe, hii hoja ni hoja hatari sana. Kwa sababu kwa mtu anayefahamu jiografia ya Dar es Salaam, mabwawa yale ya Mabibo yameshazusha zogo sana kutokana na uchafuzi wa mazingira usio wa kawaida. Sasa hii ni waste ya kawaida tu imezusha zogo, fikiria uwe na eneo la viwanda lenye viwanda zaidi ya kumi, halafu industrial sewage ijengewe bomba lipeleke kwenye mabwawa ambayo yako katikati ya community ya watu ni janga litakalokuja kutokea baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa hoja yangu ninayopendekeza hapa ni kwamba, mabadiliko yafanyike kwenye hiki kifungu na nimeandika text ya Kiingereza sitasoma kwa Kiingereza iingie kwenye rekodi rasmi kwa sababu ni nyaraka rasmi, lakini hoja yangu ni kwamba huu mtaro wa maji machafu uelekezwe, uungane na sewage system inayo-service viwanda badala ya kupelekwa Mabibo oxidization ponds na kwa kiwango cha pesa kilichotengwa technicalities, tutazungumza baadaye, ni jambo ambalo linawezekana ili kuepusha hiyo hatari ya baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwenyewe kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira kwenye mto unaoitwa Mto Ubungo pale eneo la Kisiwani kutokana na uchafu wa majitaka kutoka Hosteli za Mabibo kuishia njiani na kumwagwa mtoni badala ya kumwagwa kwenye mabwawa kwa sababu ya huo udhaifu wa mtandao wa sewage system. Kwa sasa kama hali iko hivyo, je, itakuwaje kama industrial waste ikienda kuelekezwa kwenye eneo kama hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nimalizie rekebisho lililoko kwenye ukurasa wa 146, linahusu kifungu cha…

(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iingie kwenye kumbukumbu rasmi kwa sababu nimeshawasilisha kuhusu Chuo cha Butiama ambacho kipo kwenye hotuba ya Waziri kwamba kitajengwa Chuo cha Butiama, lakini kwenye Mpango wa miaka mitano hakipo. Kwa hiyo, naomba kutoa hoja kwamba hicho Chuo nacho kiingizwe kwenye Mpango pamoja na maelezo mengine ambayo nimeyatoa lakini kutokana na Kanuni…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

Nakala ya Mabadiliko yaliyosambazwa kwa wajumbe bungeni ikiwa ni sehemu ya mchango wangu inapatikana kupitia: http://mnyika.blogspot.com/2011/06/mabadiliko-ya-mbunge-kuhusu-mpango-wa.html

Mabadiliko ya Mbunge kuhusu Mpango wa Miaka Mitano

YAH: KUWASILISHA MABADILIKO KATIKA HOJA YA SERIKALI KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO (2011/2012 – 2015/2016) ULIOWASILISHWA KWA HATI YA MEZANI TAREHE 13 JUNI, 2011 KATIKA KIKAO CHA NNE CHA MKUTANO WA NNE WA BUNGE.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu 57 (1) – (a), (b), (c) na 58 (1), napendekeza mabadiliko katika Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano kama ifuatavyo;
Katika Kiambatanishi namba 1

Page 117: Water and Sanitation (A.1.1.4)

In the row of “Rehabilitate and expand water supply scheme of Upper Ruvu for Dar es Salaam”

1. Insert 62,500 in the fiscal year 2012/13 and 43,000 in the fiscal year 2013/2014.

2. Insert 16,000 in the fiscal year 2014/2015 and 3,700 in the fiscal year 2015/2016.

Jumla ya fedha za bajeti ya mpango haijabadilishwa, bali kinachopendekezwa ni kupunguza fedha zilizotengwa kwenye miaka ya mbele ya mpango, yaani 2015/2016 na kuzijazia kwenye miaka ya mwanzoni ya 2012/13 na 2013/2014 ili utekelezaji wa miradi ufanyike mapema kwa kuzingatia pia ahadi alizotoa Rais na Waziri wa Maji za kukamilisha miradi ifikapo mwaka 2013.

In the row of “Rehabilitate and expand water supply scheme of Lower Ruvu for Dar es Salaam”

1. Insert 62,000 in the fiscal year 2012/2013 and 43,800 in the fiscal year 2013/2014.

2. Insert 8,800 in the fiscal year 2014/2015 and 1,300 in the fiscal year 2015/2016.

Jumla ya fedha za bajeti ya mpango haijabadilishwa, bali kinachopendekezwa ni kupunguza fedha zilizotengwa kwenye miaka ya mbele ya mpango, yaani 2015/2016 na kuzijazia kwenye miaka ya mwanzoni ya 2012/13 na 2013/2014 ili utekelezaji wa miradi ufanyike mapema kwa kuzingatia pia ahadi alizotoa Rais na Waziri wa Maji za kukamilisha miradi ifikapo mwaka 2013.

In the row of “Drill 20 high yielding boreholes at Kimbiji and Mpera in Kigamboni and Mkuranga areas”

1. Insert 49,200 in the fiscal year 2012/2013 and 30,000 in the fiscal year 2013/2014.

2. Insert 6,800 in the fiscal year 2014/2015 and 3,600 in the fiscal year 2015/2016.

Jumla ya fedha za bajeti ya mpango haijabadilishwa, bali kinachopendekezwa ni kupunguza fedha zilizotengwa kwenye miaka ya mbele ya mpango, yaani 2015/2016 na kuzijazia kwenye miaka ya mwanzoni ya 2012/13 na 2013/2014 ili utekelezaji wa miradi ufanyike mapema kwa kuzingatia pia ahadi alizotoa Rais na Waziri wa Maji za kukamilisha miradi ifikapo mwaka 2013.


Page 127: Roads Schedule:( A.1.2.1)

In the sub –part of De-congestion of DSM

1. Insert “Kimara –Mavurunza –Bonyokwa - Segerea” in the list of roads
Barabara hii iliahidiwa na Rais tarehe 24 Mei 2010 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami kama sehemu ya kupunguza foleni katika jiji la Dar salaam.

Page 135: Energy(A.1.3)

In the row of “Increase electricity generation to 2,780 MW by 2015, insert “Stiggler’s Gorge” in the list of activity.

Tayari serikali ilitangaza kwamba mradi huu utapewa kipaumbele maalum cha utekelezaji kuanza katika kipindi cha miaka mitano ya sasa kwa ahadi ya Rais Kikwete Bungeni na pia serikali ilitangaza kuunda kamati ya kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi husika.

Page 112: In the row of “Benjamin William Mkapa Special” (1.1.2)

1. Remove “Construction of Sewerage line from BWM-SEZ to Mabibo oxidation ponds”, and then insert “Construction of sewerage line from BWM –SEZ to the nearby “major industrial wastes disposal system”.

Mabwawa ya Mabibo ni madogo na yako katika hali mbaya na hivyo kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira. Mabwawa haya yakiongezewa uchafu wa viwandani toka BWM-SEZ eneo la Mabibo litakuwa na mazingira hatari kwa binadamu. Tayari hivi sasa kuna uchafuzi mkubwa wa maji taka ya toka Hosteli za Chuo Kikuu za Mabibo kumwagwa katika Mto eneo la Ubungo Kisiwani kutokana na kushindwa kusukumwa kuelekea katika mabwawa ya mabibo.

Hivyo, kuna haja ya mfumo wa BWM-SEZ unaokusudiwa kujengwa uunganishwe kwenye mfumo wa maji taka unaohudumia maeneo ya viwanda.

Page 146: In the row of Higher Education(A.1.5)

In the list of Activity

1. Remove “to facilitate construction of 2 higher learning institutions” and then insert “to facilitate construction of 3 higher learning institutions”.

Page 147: In the list of Location

1. Insert “Chuo Kikuu cha Kilimo Butiama”

Pamoja na kuwa kwenye hotuba ya Waziri ya kuwasilisha mpango ametaja Chuo Kikuu cha Kilimo Butiama katika Ukurasa wa 16 hata hivyo Chuo hicho hakijaingizwa katika mpango miaka mitano. Pamoja na kuingiza chuo hicho; serikali iangalie uwezekano wa kuongeza vyuo vikuu zaidi mathalani Chuo Kikuu cha Mafuta Mtwara na kukigeuza Chuo Cha Madini kuwa Chuo Kikuu.
Naomba kuwasilisha;


John John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
13 Juni 2011