Thursday, December 29, 2011

Kuhusu matatizo ya maji kata ya Goba; uvumilivu unakaribia kikomo

Matatizo ya maji kata ya Goba ni matokeo ya udhaifu wa watendaji katika ngazi mbalimbali na natoa mwito kwa mamlaka zinazowasimamia watendaji hao kuchukua hatua stahiki na kutoa taarifa kwa wananchi katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.

Kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba na sheria ni kuwakilisha wananchi, kuisimamia serikali na kutunga sheria. Utekelezaji ni jukumu la mamlaka, vyombo na ngazi mbalimbali za kiserikali. 

Matatizo ya maji kata ya Goba yanafahamika kwa mamlaka zote husika kuanzia Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na vyombo vya dola kuanzia mwaka 2007 mpaka mwaka 2011 lakini hatua kamili hazijachukuliwa.

Wananchi wamepoteza uvumilivu na kama hatua hazitachukuliwa kwa haraka viongozi wa kuchaguliwa hatutakuwa na sababu ya kuendelea kuwaambia wavute subira; tutaungana nao katika kushinikiza uwajibikaji. 

Serikali itoe taarifa uchunguzi wa kashfa ya UDA

Serikali inapaswa kutoa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya ukaguzi na uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA).

Taarifa hiyo inapaswa kutolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, vyombo vya dola na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa umma umeanza kupoteza matumaini juu ya hatma ya ukaguzi na uchunguzi huo ambao serikali iliahidi ungefanyika katika kipindi cha mwezi mmoja lakini mpaka sasa miezi minne imepita huku ukimya na usiri ukitawala.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kutoa taarifa kwa kuwa alitoa agizo bungeni tarehe 4 Agosti 2011 wakati wa kipindi cha maswali kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 38 (4) ya kuelekeza vyombo vya dola hususan Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) , Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi ya Upepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma husika.

Toka agizo hilo litolewe umma wala wabunge hatujawahi kuelezwa hatua ambayo vyombo vya dola hususani TAKUKURU na ofisi ya DCI imefikia katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA).

Wednesday, December 28, 2011

Serikali itake Israel waombe radhi; tukijiheshimu, tutaheshimiwa

Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya CHADEMA inaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa tamko juu ya kauli ya Waziri wa Ulinzi wa Israel ya kwamba nchi yetu si ya muhimu wala ya maana.

Waziri Barak alifanya mahojiano na Radio Israel na kutoa kauli ambayo imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nchi hiyo wiki iliyopita kuwa “ Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania or Tripolitania…..these are very important, very relevant countries and we don’t have an interest in increasing tensions with them or making them bitter enemies”.

Kwa kauli hii serikali ya Israel inaiona Tanzania sio nchi ya muhimu wala ya maana hata kufikia hatua ya kuilinganisha na eneo tu ndani ya Libya linaloitwa Tripolitania.

Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Benard Membe kuitaka serikali ya Israel kuomba radhi kufuatia kauli hiyo au kueleza wazi iwapo mazungumzo hayo ya Waziri Barak ni msimamo wa nchi hiyo kuhusu uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa yetu.

Barua pekee ya balozi wa heshima wa Tanzania nchini Israel, Kasbian Nuriel Chirich kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Lieberman ya kulaani matamshi hayo ya Waziri Barak na kumkaribisha mwakilishi wa Israel kutembelea Tanzania haitoshi kuifanya serikali ya nchi hiyo kutambua athari za kidiplomasia za kauli iliyotolewa.

Monday, December 26, 2011

Waraka wa Pili wa Mbunge kwa Wananchi wa Jimbo la Ubungo


Uhuru na Kazi:
Nimekuja kuwatembelea kuona hali halisi ya uharibifu wa makazi yenu, mali zenu na miundombinu yetu kutokana na maafa ya maafuriko katika mitaa hii ya kata ya mabibo. Kuanzia maafa yatokee tarehe 20 Disemba mpaka tarehe 24 Disemba nimekuwa pamoja na wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo bega kwa bega katika jitihada za uokoaji na utoaji wa huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali mathalani Msewe, Ubungo, Kisiwani, Kibo, Mburahati, Sinza D, Sinza E, Uzuri, Manzese Chakula Bora, Mburahati Kisiwani, Msigani, Mbezi Kibanda cha Mkaa, Kimara B. Na pia, nimeenda kutoa misaada kwa majimbo jirani ya Kinondoni (Magomeni Sunna na Kigogo), Kawe (Msasani Bonde la Mpunga na Bunju) na Ilala (Mchikichini). Kutokufika Mabibo, katika hizo siku chache, kunadhihirisha ukubwa wa maafa yenyewe na ilikuwa vigumu kuwepo mahali pote wakati wote. Hata hivyo, katika wakati huo wote nilikuwa na mawasiliano na wananchi na viongozi kuhakikisha kwamba mamlaka zinazohusika na uokoaji zinafika katika maeneo haya. Nawashukuru wote mliotoa ushirikiano wakati wa uokoaji na nawashukuru pia mliotoa msaada wa hali na mali kwa majirani zenu katika kipindi hiki kigumu.

Saturday, December 24, 2011

Majina mapya bila mfumo mpya hauwezi kutuhakikisha ufanisi wa tume wala kuwa na chaguzi huru na za haki

Kufuatia Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wadau mbalimbali wametaka maoni yangu kuhusu watu walioteuliwa. Kwa maoni yangu hatupaswi kutoa maoni kuhusu watu walioteuliwa kwa sababu matatizo ya tume yetu ya uchaguzi ni ya mfumo mzima. Hivyo, uteuzi wa mwenyekiti na mkurugenzi mpya wa tume ya uchaguzi hauwezi kuleta mabadiliko yoyote ya maana katika utendaji wa tume ya uchaguzi wala hauwezi kuisaidia tume hiyo kuweza kuaminika na umma. Majina mapya bila mfumo mpya hauwezi kutuhakikisha ufanisi wa tume wala kuwa na chaguzi huru na za haki.

Uteuzi huu mpya hauwezi kuhakikisha watanzania kuwa na chaguzi huru na haki katika chaguzi za marudio zinazotarajiwa kufanyika, wala hauwezi kuleta uchaguzi huru na haki wakati wa kura za maoni za kufanya maamuzi ya kuhalalisha katiba mpya wakati wa mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011.

Pia, uteuzi wa mwenyekiti na mkurugenzi mpya wa tume ya uchaguzi hautaweza kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchaguzi huru na wa haki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hivyo, wananchi na wadau wote badala ya kupongeza uteuzi uliofanyika tunapaswa kuunganisha nguvu ya umma kuendelea kudai mabadiliko ya mfumo mzima wa uchaguzi ikiwemo utaratibu mzima unaoongoza uteuzi. Kwa sasa Rais Kikwete amepewa mamlaka makubwa ya uteuzi kwa mujibu wa katiba na mamlaka hayo ameyakuwa akiyatumia vibaya kufanya teuzi mbalimbali bila kuzingatia ridhaa ya umma na maslahi ya taifa kwa ujumla.

Heri ya Xmas, Tamasha la Injili na kutoa zawadi

Nachukua fursa hii kuwatakia heri katika sikukuu ya noeli. Kwa waumini siku hii ni kumbukumbu ya kwa mkombozi hivyo inapaswa kuleta mabadiliko ya kuzaliwa upya kiroho na kimaisha. Aidha nawahimiza kutumia siku hiyo kujumuika na waliokumbwa na matatizo mbalimbali katika jamii wakiwemo waathirika wa maafa ya maafuriko yaliyotokea Dar es salaam na maeneo mengine ya nchi yetu. Nawaalika kujumuika nami kwa hali na mali katika matukio ya tarehe 25 na 26 Disemba ambayo nitashiriki.

Katika kuadhimisha sikukuu ya mwaka huu pamoja na kujumuika na familia, tarehe 25 Disemba 2011 nitashiriki katika katika Tamasha la Muziki wa Injili na tarehe 26 nitatembelea nyumba za waathirika wa mafuriko eneo la Mabibo kutoa zawadi mbalimbali za sikikuu pamoja na kujumuika nao kwa chakula.

Katika kuadhimisha sikukuu hii nimealikwa kuwa Mgeni Rasmi katika tamasha la muziki wa Injili litakalofanyika katika Ukumbi wa Landmark Hotel-Ubungo siku ya Krismas kuanzia saa 8:30 mchana ambalo limeandaliwa na RudishaMusic ikishirikiana na WAPO Radio FM.

Lengo kuu la tamasha hili ni kusherehekea sikuku ya Noel-(Krismas) na kuendeleza jitihada za kukuza tasnia ya muziki wa Injili hapa nchini. Tamasha litahusisha vikundi mbalimbali vya muziki wa injli wa moja kwa moja (live performance) ambapo vikundi vitakavyoshiriki ni pamoja na Host of Praise, Glorious Celebration, Holy of Holies, Jackson Benty, Rachel Marlon na Mwanamapinduzi Band. (Maelezo zaidi kuhusu tamasha husika yanapatikana kupitia: www.XmasExtravaganza.co.tz.

Thursday, December 22, 2011

Hatua kuhusu maafa katika Jimbo la Ubungo

Jana na leo nimeshiriki katika jitihada za uokoaji na nimetembelea maeneo mbalimbali katika Jimbo la Ubungo kwa ajili ya kuchukua hatua za kibunge kufuatia maafa ambayo yamejitokeza kutokana na mvua na mafuriko yanayoendelea.

Kama sehemu ya kazi ya mbunge ya uwakilishi na kuisimamia serikali nimekuwa nikiwasiliana mara kwa mara na mamlaka zinazohusika na naomba kitengo cha maafa kuongeza nguvu zaidi katika kushughulikia matatizo yaliyojitokeza. Ingawa kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wetu mzima wa kukabiliana na maafa na dharura kwa ujumla, hata hivyo huu si wakati wa kulaumiana bali kuunganisha nguvu katika kuchukua hatua za haraka.

Aidha, natoa pole kwa wananchi wote waliofiwa au kuathirika kutokana na maafa yanayoendelea na kuwasihi waishi kwa tahadhari lakini wawe na utulivu katika kipindi hiki kigumu. Pia, natoa mwito kwa wadau wengine wote ikiwemo mashirika ya misaada ya kinadamu kutembelea katika maeneo ya maafa kuona hali halisi na kuchukua hatua zinazostahili kuunga mkono jitihada ambazo tunaendelea nazo hivi sasa.

Maeneo ambayo nimetembelea nyumba za wananchi na miundombinu ni pamoja na kata ya Ubungo (maeneo ya Ubungo Kisiwani na Msewe), Kata ya Sinza (Maeneo ya Sinza D na Sinza E) kata ya Mabibo (Maeneo ya Mabibo farasi na Loyola) na Manzese (maeneo ya Uzuri na Chakula Bora).

Monday, December 19, 2011

Kuhusu Serikali kulinda Viwanda vya ndani

Leo tarehe 19 Disemba 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwahakikishia wafanyabiashara kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete itaendelea kulinda viwanda vya ndani ili viweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza ajira.

Hata hivyo, kauli hiyo haipaswi kuleta matumaini ya kweli kwa wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha kuathirika kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na mfumuko mkubwa wa bei na kuporomoka kwa kasi kwa shilingi ya Tanzania ukilinganisha na dola kunakochangiwa pamoja na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa uzalishaji nchini katika kilimo na viwanda pamoja na ongezeko kubwa la uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Waziri Mkuu Pinda anapaswa kutoa kwa wafanyabiashara wenye viwanda na umma wa watanzania mpango wa haraka wa kukuza uchumi wa nchi na kupunguza gharama za maisha ambao pamoja na mambo mengine utajikita katika kuongeza uzalishaji nchini, kupanua wigo wa ajira, kupunguza kiwango cha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ili kuboresha urari wa biashara na kudhibiti bei ya bidhaa muhimu.

Friday, December 16, 2011

Taarifa ya Mkutano wa Kanda Maalum DSM

Taarifa inatolewa kwa viongozi, wanachama na wapenda demokrasia na maendeleo wa Jiji la Dar es salaam na Manispaa kuhusu Mkutano Mkuu wa CHADEMA wa Kanda Maalum Dar es salaam.

Mkutano huo utafanyika jumapili ya tarehe 18 Disemba 2011 kuanzia saa 4 kamili asubuhi katika Ukumbi wa Kilamuu ulioko Mbezi jijini Dar es salaam.

Washiriki wa mkutano huo ni viongozi wa chama wa Mikoa ya kichama ya Temeke, Ilala, Kinondoni na wajumbe wa mikutano mikuu ya majimbo yote ya jiji la Dar es salaam. Aidha, waalikwa katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa kuchaguliwa katika ngazi mbalimbali, viongozi wilaya, kata na wawakilishi wa matawi mbalimbali.

Taarifa zaidi kuhusu ushiriki wa wanachama na wapenda demokrasia na maendeleo katika mkutano husika zinatolewa katika ofisi mbalimbali za chama katika ngazi za mikoa, wilaya/majimbo ya kanda maalum ya Dar es salaam.

Ajenda za Mkutano huo ni waraka na. 1 na 2 wa chama wa mwaka 2011 kuhusu uchaguzi ndani ya chama na waraka na. 3 wa mwaka 2011 kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Mgeni rasmi katika Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbroad Slaa ambaye pia atashiriki katika kutoa mada.

Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya mpango mkakati wa CHADEMA wa mwaka 2011 mpaka 2016 ambapo umeweka mkazo kwa chama kufanya mikutano katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa chama pia kwa ajili ya kushughulikia masuala muhimu ya kitaifa.

Katika ajenda ya waraka namba 1 na 2 Mkutano utapokea na kujadili maelezo na maelekezo mbalimbali kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama katika ngazi mbalimbali.

Ajenda ya Waraka namba 3 ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Kamati Kuu la tarehe 20 Novemba 2011 ambayo iliwaagiza viongozi wote wa chama na wa kuchaguliwa wa ngazi zote nchi nzima kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata katiba mpya na bora kwa nchi yetu ili kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi. Kamati Kuu ilizingatia kwamba sheria husika ilisomwa na kujadiliwa kwa mara ya pili bila ya wananchi kushirikishwa kwa ukamilifu kutoa maoni yao na muswada kuboreshwa kwa kuzingatia makubaliano ya kitaifa kuhusu mchakato wa katiba mpya.

Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba CHADEMA itaendelea kutoa elimu kwa wanachama, wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na rasimu ya katiba mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki.

Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa waraka na. 4 wa mwaka 2007 chama kilielekeza kwamba Hoja ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi kuwa ya kudumu katika vikao vya kikatiba vya chama pamoja na mikutano na wananchi mpaka pale taifa letu litakapokuwa na katiba mpya.

Maandalizi ya Mkutano huo ni matokeo ya kikao cha pamoja cha viongozi wa Mikoa ya kichama, wilaya za kichama, na majimbo ya kiuchaguzi ya Kanda Maalum ya kichama ya Dar es Salaam.

John Mnyika (Mb)
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mikoa ya Kanda Maalu ya Dar es salaam
Na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama wa Kinondoni.
16/12/2011

Thursday, December 15, 2011

Mwigamba apata dhamana; tuepuke dola ya kipolisi

Hatimaye leo tarehe 15 Disemba 2011 Samson Mwigamba mmoja wa Waandishi wa Makala aliyefikishwa mahakamani tarehe 8 Disemba 2011 ametoka mahabusu kwa dhamana. Kuchelewa kutoka kwake kumesababishwa na ugumu wa dhamana iliyotokana na aina ya dhamana iliyotakiwa. Awali ilitarajiwa angeshtakiwa kwa kosa la uchochezi hivyo viongozi wa chama walijiandaa kwa dhamana husika. Hata hivyo, hata hivyo alifunguliwa kesi ya jinai namba 289 ya mwaka 2011 yenye mashtaka makubwa zaidi ya kudaiwa kushawishi askari na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoendelea kutii serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete (kosa lenye mwelekeo wa uhaini).
Mahakamani alidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 30 Novemba 2011 kutokana na Makala yake kwenye gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2553 ambayo inadaiwa kuwa maudhui yake yamekwenda kinyume na kifungu 46 (b), 55 (10)(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kutokana na mashtaka hayo alitakiwa kati ya mdhamini mmoja wapo aweke hati ya nyumba yenye thamani iliyotajwa na mahakama. Kwa kuwa sharti hili lilitolewa tarehe 8 Novemba na kesho yake ilikuwa sikukuu ya uhuru tarehe 9 Disemba hakukuwa na fursa ya kutimiza masharti yote kwa wakati pamoja na jitihada zote zilizofanywa na viongozi husika wa chama.

Hii ni kwa sababu taratibu za dhamana ya hati yenye mali isiyohamishika zinahusisha mali hiyo kufanyiwa uthamini (valuation) na baadaye kufanyiwa tena tathmini ya uthibitisho (verification) hatua ambazo huchukua muda kutokana na urasimu katika mamlaka mbalimbali.

Kwa heshima yake na kwa ajili ya kupanua wigo wa mjadala nimeona niwaletee ujumbe huu ambao nilichangia kwenye mtandao wa Wanabidii tarehe 7 Disemba 2011, siku moja kabla ya Mwigamba kufikishwa mahakamani.

“Nimesoma tena ujumbe ambao Mwigamba aliundika kwenu, najua wengine waliuchukulia kuwa ni mwito wa kawaida tu polisi kwa kuwa mhariri gazeti lililochapa makala yake hakuitwa.

Hata hivyo, vyanzo vyangu ndani ya Jeshi la Polisi vimenieleza kuwa kesho asubuhi Mwigamba anatarajiwa kupelekwa mahakama ya Kisutu kushtakiwa kwa kosa la uchochezi. Taratibu Tanzania inaelekea kuwa dola ya kipolisi (police state), hali ambayo ikifikia itakuwa na athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Sina hakika kama wakuu wetu kwenye vyombo vya ulinzi na usalama wanayafanya haya kwa kwa maelekezo ya Rais kwa mujibu wa ibara ya 33 na 35 ya katiba au ni matakwa tu binafsi.

Kwa vyovyote vile, Rais anapaswa kushauriwa: KAMATA KAMATA KWA ARI, NGUVU NA KASI ZAIDI (ANGUKA); Miaka 50 baada ya Uhuru, tumeanza kurudi katika zile zama za watu kukamatwa na kuwekwa kizuizini.

Tofauti ya wakati huo na sasa ni kwamba sasa hukamatwi kwa kificho, wala huwekwi mafichoni; ni rahisi tu, polisi wanakukamata halafu wanakupeleka mahakamani.
Wanajua baada ya hapo utakuwa tayari umepoteza sehemu ya uhuru wako, utapaswa kwenda mahakamani mara kwa mara. Kesi itachukua muda mrefu kwa polisi hao hao walikuona una kosa wakakupeleka mahakamani kutoa sababu kwamba ‘upelelezi haujakamilika’.

Kosa la Mwigamba linaelezwa kutokana na makala yake aliyoiandika “Waraka kwa Askari wa Tanzania”, anadaiwa kwamba kupitia makala hiyo amewachochea polisi kukaidi amri za viongozi wao na kuwachochea polisi kukataa kutimiza wajibu wao wa kisheria. Suala hili limenifanya noisome makala yake, na baada ya kuisoma naona sasa tunaelekea katika dola ya kipolisi (police state).

Ari, Nguvu na Kasi hii ya Jeshi la Polisi kusoma, kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua dhidi ya ‘wahalifu’ ningeiunga mkono kama ingekuwepo toka wakati Orodha ya Mafisadi (List of Shame) iliposomwa 15 Septemba 2007 pale viwanja vya Mwembe Yanga na baadaye kusambazwa na vyombo vya habari na mitandao mbalimbali. Lakini mpaka leo Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) hakuna hatua za maana alizochukua lakini ana ari, nguvu na kasi zaidi ya kuwakamata na kuwahoji waandishi wa makala nyingine za magazetini.

Kauli ya kwamba si lazima kwa askari kufanya kile ambacho wakubwa wake wanamuamrisha kufanya hata kama anacholazimishwa ni kinyume cha sheria na kinyume cha maadili na haki na kwamba askari polisi watumie pia akili zao kufikiri Mwigamba sio wa kwanza kuiandika au kuisema.

Tanzania inaelekea kuwa dola ya polisi, sio kwa baadhi ya wabunge na wapinzani tu bali hata kwa wananchi wengine na hata katika ya polisi wa juu dhidi ya polisi wa ngazi za chini.

Tukio hili limenifanya nikumbuke mambo kadhaa dhidi ya jeshi letu ya polisi yaliyojiri katika mkutano wa nne wa Bunge.

Mosi; Wakati wa bunge la bajeti nilihoji kuhusu jeshi la polisi juu ya polisi kuwa na maslahi duni, Serikali ikasema bungeni kuwa posho zao (ration allowance) zimeongezwa mpaka laki unusu. Ukweli ni kwamba askari hawalipwi kiwango hicho cha posho, hata hivi sasa pamoja na ufafanuzi kuhusu mgawo wa posho za askari tulioomba bungeni tarehe 28 na 29 Julai 2011.

Kufuatia kauli ya serikali bungeni askari wakaanza kuulizia kuhusu posho hizo na waliowaunganisha wenzao kuhoji wakaitwa ‘wachochezi’; wakuu wa vikosi na vituo wakapewa waraka wa ‘kufuta’ kauli hiyo ya serikali nje ya Bunge na kuchunguza askari wote wanaopandikiza ‘chuki’ kwa wenzao dhidi ya serikali kwa kutumia suala hilo la posho.

Polisi maeneo mbalimbali nchini wakaelezwa kwamba vitendo vya kushawishi askari aliyekula kiapo cha utii kwa serikali kufanya hujuma kama hizo za kudai posho ambayo imeahidiwa bungeni ni hujuma kwa serikali hivyo ni UHAINI.

Pili, kitabu kinachosambazwa na Jeshi la Polisi Mitaani na Vijijini cha “Utii wa Sheria bila Shuruti” ambacho kinaonyesha mwelekeo wa serikali kuanza kuandaa mazingira ya dola ya kipolisi (police state). Kitabu hicho chenye kueleza kuhusu “wajibu wa vyama na watu walioshindwa katika uchaguzi” kinawaasa watanzania dhidi ya wanasiasa na wanaharakati wenye kutumia ‘tabia ya kutumia shida na kero za wananchi kuchochea hasira, munkari na jazba dhidi ya viongozi halali’.

Aidha, kampeni ya “Utii wa Sheria bila Shuruti” inawakumbusha wananchi wajibu wa “Kuepuka kushiriki katika mikutano, maandamano na harakati za kuichokoza mamlaka ya dola, kwa uwasilishaji wa malalamiko au kero kwa njia ambazo zinasababisha bughudha na karaha kwa wengine”.

Kitabu cha “Utii wa Sheria bila Shuruti” kinaeleza kwamba ‘Sheria inampa mamlaka afisa wa Polisi wa himaya inayohusika kusitisha maandamano, mkutano au mkusanyiko wowote endapo atabaini kwamba kuna habari au taarifa kwamba kuendelea kufanyika kwa mkutano kunaweza kusababisha uvunjaji wa amani na kuhatarisha usalama. Na kwamba endapo amri hiyo itaonekana kuupuuzwa kwa namna yoyote hata kama maandamano, mkutano au mkusanyiko ulikuwa ni halali utahesabika kuwa ni haramu. Hivyo hatua za kuwatawanya kwa njia ya shuruti itafuata ikiwemo kuwakamata waandaaji na washiriki na kuwafikisha mahakamani”.

Kifungu hiki kilitumiwa kwenye Mkutano wangu na Wananchi tarehe 5 Novemba 2011 kwa kuvamia katika mkutano halali, kukata nyaya za vipaza sauti, kukamata viongozi waandaji na kuondoka nao pamoja na gari lenye nyaraka mbalimbali za katiba. Maelezo ambayo waliwaeleza awali viongozi hao ni kuwa mkutano haurusiwi kutokana na tishio la ugaidi wa Al Shabab.

Nilipoelezwa nikawaambia viongozi waendelee na maandalizi ya mkutano kwa kuwa Rais hajatangaza hali ya hatari, kama kuna tishio la kawaida la vurugu polisi waje wamejiandaa kufanya kazi yao ya kulinda amani kama ambavyo walikuwa wamejiandaa kulinda mechi zingine za mpira zilizofanyika siku hiyo hiyo ya tarehe 5 Novemba na matembezi ya Mke wa Rais yaliyofanyika DSM wiki hiyo hiyo.

Pamoja na viongozi kukamatwa na vipaza sauti kuchukuliwa kabla ya kufika uwanjani, nilipofika niliendelea kufanya mkutano wa kupata maoni ya wananchi kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba na masuala mengine muhimu ya jimbo na taifa kwa ujumla kabla ya kwenda mkutano wa tano wa Bunge ulioanza tarehe 8 Novemba 2011. Nawashukuru askari walioacha kunikamata pamoja na maagizo waliyokuwa wamepewa ya kunikamata.

Kwanini nimeandika yote haya? Sababu ya Mwigamba kuitwa mchochezi ni kuwa amewaambia askari watumie akili zao wasikubali kutumwa kukamata na kupiga watanzania wenzao katika hatua za maandamano ya kupinga sheria ya mabadiliko ya katiba wakati njia za kidiplomasia kupitia mikutano za kutaka sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko kabla ya kuanza kutumika zitakapopuuzwa na hatimaye kulazimika kuunganisha nguvu ya umma kupitia maandaamano.

Nimeamua kutafakari kwa sauti wakina Mwigamba wengine mnisikie, kwamba tusipoungana kuwakanya viongozi wetu tunaelekea kuwa dola ya kipolisi na kwenye mchakato wa katiba dola hiyo (Mungu apishie mbali) inaweza kutumiwa na watawala kuvuruga utulivu wetu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hiyo ni dola ya polisi wasiofikiri kabla ya kutenda; polisi wanaofikiri baada ya kutenda kwa kutumwa na watawala walioacha kufikiri na kujikita katika kutoa amri haramu.

Akili zao zinadhihirika kwenye kauli zao na za wataalamu wao mathalani kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni wakati wa kuhalalisha kifungu kwenye sheria ya Mabadiliko ya Katiba chenye kutoa adhabu ya faini isiyopungua milioni tano na isiyozidi milioni kumi na tano au kifungo kwa muda usiopungua miaka mitatu na isiyozidi miaka saba au adhabu zote mbili kwa kwenda kinyume cha sheria hiyo.
Makosa yenyewe ya hukumu hiyo ni pamoja na ‘kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi’ na ‘kuendesha elimu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria’ hiyo. Makosa ya kukusanya maoni na kutoa elimu sasa yametengewa hukumu kubwa kuliko ya mafisadi na ambao wameisababishia hasara serikali. Huo ndio “Utii wa Sheria bila Shuruti” wanaoutaka kwa watanzania. Kwa maneno ya Werema bungeni kuhalalisha kifungu husika “matatizo tuliyonayo sasa ambayo yanasababishwa na watu ambao hawataki kufuata utaratibu kwa mambo ya siasa, inatakiwa kutoa elimu ya kisiasa katika jambo hili la katiba kwamba wapewe adhabu kali; ndiyo maana yake”.

Nawaandikia kuwaomba mjiandae iwe ni wanahabari, wanaharakati, wanasiasa, viongozi wa dini, wanataaluma au wananchi wa kawaida; kuwa mkiwa na mawazo tofauti kuhusu katiba na polisi hawa wa “Utii wa Sheria bila Shuruti” wakaagizwa kuwakamata kwa kutoa elimu ama kukusanya maoni kinyume cha sheria adhabu yenu itakuwa kifungo cha hadi miaka saba au faini ya hadi milioni 15 au vyote. Na polisi jiandae, huu ni wakati wa pekee katika historia taifa letu; miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanganyika, muwafunge wananchi wenzenu wanaodai uhuru wa kweli dhidi ya ujinga, umasikini, maradhi na ufisadi kwa kudaiwa na serikali ya mkoloni kuwa ni wachochezi kama alivyofanyiwa Mwalimu Nyerere na TANU au msimame upande wa haki na ukweli.

Na hili halihusu tu maslahi ya taifa ambayo tunawaomba askari myasimamie popte pale mlipo, inahusu pia kusimamia maslahi yenu wenyewe. Wakiitisha mabaraza ya askari, wakiwaambia polisi kwamba mnapaswa kuendelea kulipwa ration allowance ya laki moja tu, kwa mujibu wa waraka wa idara kuu ya utumishi wa tarehe 26 May 2009 wenye kumb. Na. C/AB.129/271/01/E41 waambieni waje watuambia sisi bungeni kwa kuwa walitoa kauli kuwa mnalipwa laki na hamsini; waje waje wafute kauli bungeni tujadili msingi wa wao kukataa kuwalipa haki yenu hiyo kwa mwezi, wakati ni pungufu ya posho iliyoongezwa kinyemela ya mbunge ya siku moja pekee ya kukaa kwenye kikao (sitting allowance).

Mkitumwa kwenye kufanya operesheni haramu na kulipwa viwango duni vya posho kwa kuwapiga watanzania wenzenu kwa maelezo kuwa waraka mwingine wa tarehe 27 Januari 2009 wenye kumb. Na. C/BC. 129/271/01/18 umewaongezea posho kwa 15% waulizeni mbona serikali imeongeza posho haramu kwa wabunge ya kukaa kwenye vikao kwa zaidi ya 150%.
Wakiendelea kuwalipa mishahara midogo huku kima cha chini kikiwa kimeongezeka toka 219,170 mpaka 243,000 tu sawa na ongezeko la 10% huku bei za bidhaa na gharama za maisha zimeongezeka kwa zaidi ya 100% waulizeni uhuru na usawa tulioupigania miaka 50 uko wapi?

Najua wanaendelea kuwaeleza mkiwa kwenye maandalizi ya gwaride la sherehe za uhuru kuwa muendelee kuwa na ‘utii na uvumilivu kwa kuwa serikali haina uwezo’ na kwamba nyongeza hiyo ndogo kupitia waraka wa tarehe 13 Julai 2011 wenye kumbukumbu na. CAC/205/228/01/A/41 imetokana na hali halisi ya uchumi wetu. Muwakumbushe kiwango cha fedha ambacho kinakaribia kufika bilioni 50 kinachotumika kwenye ‘sherehe’ za miaka 50 ya uhuru toka maandalizi yake yaanze mpaka mwisho huku mkiidai serikali malimbikizo ya madeni.

Hali yenu ni sawa na ya walimu, watumishi wa sekta ya afya na kada nyingine za chini katika utumishi wa umma ambapo mtajumuika kwa ‘utii wa bila shuruti’ katika halaiki ya 9 Disemba ‘kusherehekea uhuru’. Hampaswi kugoma kwa kuwa kazi yenu ni wito, lakini msiache kuwafikishia ujumbe watawala; msikubali kutumiwa kuminya haki zenu wenyewe na za wenzenu.

Tekelezeni amri zote halali za ulinzi na usalama wa taifa letu, wakatalieni amri zote haramu zenye kuvunja sheria, kuvuruga amani na kukiuka haki za msingi za binadamu. Tenganisheni kati ya kusimamia maslahi ya taifa na kulinda matakwa ya mafisadi; tambueni kuna amri za watawala kudumisha utawala wao na kuna amri za viongozi kusimamia mahitaji ya umma.

Watawala wameapa kulinda katiba, ambayo ibara ya 8 (a) inatamka wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka kwa wananchi; ibara ya 9 inawataka wao na serikali wanayoongoza kulinda haki za binadamu, kuendeleza utajiri wa taifa kwa manufaa ya wananchi wote, kuhakikisha serikali na vyombo vyake vyote vinatoa nafasi sawa kwa raia wote bila ubaguzi na kwamba aina zote za dhulma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini. Waambieni wakumbuke kiapo chao, na wasiwalazimishe nyinyi kutii amri zinazokiuka kiapo chao wenyewe.

Msiwaogope wao kuliko wananchi wanaowalipa mishahara yenu kwa kodi zao na ndugu zenu mnaishi nao katika mazingira yenu ya ugumu wa maisha. Kama hamuwaogopi wananchi wenzenu basi walau muogopeni Mwenyezi Mungu anayetaka muenende kwa upendo, haki na ukweli. Sheria kuu kuliko zote ya kuitii sio ya Tanzania; bali ya nafsi zenu na Mungu wetu. Msiwatii wanapowataka mtende dhambi. Kwa maneno ya Mahatma Ghandi, ‘kuweni mawakala wa mabadiliko mnayotaka kuyaona’”.

Kama nilivyoandika miaka michache iliyopita wakati mwanahabari wa gazeti la Mwanahalisi Saed Kubenea aliposhambuliwa; shambulizi dhidi ya mwanahabari ni chambulizi dhidi ya ‘uhuru wa habari’. Hivyo, kamata kamata dhidi ya watoa maoni, ni kamata kamata juu ya ‘uhuru wa kutoa maoni’. Tukio hili lipaswa kuwa chachu ya kuendelea kutoa maoni na kudai uhuru wa kutoa maoni ikiwemo uliopokwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Kesi hii ni muhimu kwa taifa kuhusu haki ya msingi ya kibinadamu na kuwasiliana na kutoa maoni, hivyo tuifuatilie kwa karibu mwenendo wake. Aidha, ni wakati sasa wa kuunganisha nguvu ya umma kudhibiti nchi yetu kugeuzwa ‘dola ya kipolisi’.

John Mnyika (Mb)

Wednesday, December 14, 2011

Utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme

Tarehe 8 Disemba 2011 Wizara ya Nishati na Madini imetoa Taarifa kwa Umma kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Nishati na Madini. Tunaendelea kuipitia taarifa husika na tutatoa taarifa mbadala kwa umma kama sehemu ya wajibu wa kikatiba wa kuishauri na kuisamia serikali. Hata hivyo, nimeshangazwa na ukimya wa serikali mpaka hivi sasa kuhusu haja ya kutoa kwa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi kwa sasa zenye kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Kuanzia mkutano wa tano wa bunge ulionza tarehe 8 Novemba 2011 ilitarajiwa kwamba serikali ingetoa taarifa bungeni kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba kuhusu mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati; hata hivyo suala hilo halikuingizwa kwenye ratiba ya bunge. Baada ya taarifa kutokutolewa bungeni nilitarajia serikali ingetoa taarifa kwa umma lakini mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatoa taarifa husika hivyo natoa mwito kwa Waziri husika kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umema na maendeleo ya sekta ya nishati kwa ujumla.

Mpango wa Dharura uliwasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011, ahadi ya serikali ilikuwa kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011.
Kimsingi kauli iliyotolewa bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli hivyo ahadi ya kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana.

Ikumbukwe kwamba mpango mwingine wa muda mfupi ulioelezwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 ni mradi wa kununua mitambo ya MW 100 wa Jacobsen wa gesi asili ambao awali ulikuwa ukamilike 2009/2010 lakini kutokana uzembe ndani ya serikali mradi huo haukukamilika mpaka mwaka 2011. Kuchelewa kwa kununuliwa na kufungwa kwa mitambo hii ambayo ilikuwa ifungwe Ubungo ndiko kuliongeza makali ya mgawo wa umeme kuanzia mwishoni mwa 2010 mpaka mwanzoni mwa mwaka 2011.

Baada ya kuchelewa kwa mradi huu serikali ikakubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ukamilike Juni 2012. Kutokana na ahadi ya MW 150 za dharura toka NSSF kuthibitika kuwa ni hewa, serikali ikarudi tena mezani kufanya majadiliano na mkandarasi wa mradi wa Jacobsen ili kuharakisha utekelezaji uzinduliwe mwezi Disemba 2011 wakati wa ‘sherehe’ za uhuru. Hata hivyo, wataalamu hawakumueleza tena ukweli Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa matarajio waliyompa ya kuzindua mradi huo wakati wa sherehe za uhuru nayo yamethibitika kuwa hewa kwa kuwa sherehe zimepita bila umeme wa nyongeza. Kutokana na hali hii, Rais Kikwete alilazimika kurudia mara kwa mara kwamba asingetoa hotuba ndefu uwanja wa taifa kwenye maadhimisho tarehe 9 Disemba katika siku ambayo wananchi walitarajia mkuu wa nchi azungumze masuala makubwa ya kitaifa ikiwemo suala la umeme na sekta ya nishati wa ujumla.

Kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na takribani MW 660 unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei ambao hivi sasa umefikia zaidi ya asilimia 16. Hivyo, watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Pamoja na kuwa ahadi za mpango wa dharura bado hazijatekelezwa kwa ukamilifu wake serikali inaendelea kutumia zaidi ya bilioni 2 kila siku kama gharama za mafuta ya kuzalishia umeme suala ambalo linahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya fedha hizo na uhalali wa matumizi ya miradi ya Aggreko International, Symbion Power LLC na IPTL.

Nilionya bungeni kuhusu gharama kubwa za mpango wa dharura wa umeme na kupendekeza vyanzo mbadala vya fedha ambavyo serikali ilivipuuza. Uamuzi wa kukopa katika mabenki ya biashara kwa ajili ya kugharamia mpango wa dharura wa umeme tayari umeshaanza kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO), serikali na utaathiri maisha ya wananchi.

Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Julai 2011 nilieleza bungeni vyanzo mbadala vya kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bila kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.

Hata hivyo, tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Siku hiyo nilirudia kumsomea Waziri Mkuu kumbukumbu ya Bunge (Hansard) ya ahadi yake ya tarehe 18 Julai 2011 ambayo haikuitimiza, inaelekea serikali ilitoa ahadi hewa ndio maana haikutaka kabisa kubadili msimamo.

Matokeo ya hali hiyo ni hivi sasa serikali kutafuta namna ya kuinusuru TANESCO kwa kubebesha mzigo mkubwa wananchi kwa kuwa hivi karibuni imewasilisha ombi la kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu) ya bei ya sasa. Ombi hili likikubaliwa kwa ukamilifu wake litakuwa na athari kubwa sana katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi. Ikumbukwe kwamba Januari 2011 umeme ulipanda bei kwa 18.5% tu lakini kupanda huko kulisababisha mfumuko wa bei, sasa watanzania wajiulize itakuwaje ukipanda kwa 185%. Hata hivyo, ni vigumu kwa EWURA kukubali kupandisha bei kwa kiwango hicho kwa kuwa ikumbukwe kwamba Disemba 2010 TANESCO iliomba kupandisha bei kwa zaidi ya 30% lakini haikukabaliwa. Kukataliwa kupandisha kwa bei kubwa kutaiweka TANESCO njia panda kwa kuwa tayari imeshakopa kwa gharama kubwa katika mabenki ya biashara na pia gharama za uendeshaji wa TANESCO zipo juu kutokana na ufisadi katika mikataba mbalimbali na pia kutokana na madeni makubwa ambayo TANESCO inadai kwa serikali na wateja wengine.

Hivyo, upo uwezekano wa mikopo kushinda kulipwa kwa wakati na TANESCO na madeni kurudi kwa umma kupitia kwa dhamana za serikali. Katika hali hii hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa na Wizara ya Nishati na Madini kutoa taarifa ya kina ya hali halisi ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati ili kudhibiti mianya ya uchelewaji na ubadhirifu ambayo imeanza kujitokeza kwa kuzingatia pia mapendekezo ambayo tuliyatoa bungeni.

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
14/12/2011

Tuesday, December 13, 2011

Kuhusu migogoro ya UDSM, UDOM na MUHAS

Kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa aliahidi bungeni kwenye mkutano wa nne kwamba serikali imepata mkakati wa kumaliza migogoro na matatizo katika vyuo vikuu nchini na kwamba hatua za haraka zingechukuliwa kama sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2012/12.

Hata hivyo, badala ya migomo na migogoro kumalizika inaelekea kuongezeka. Katika siku za karibuni pamekuwepo na maandamano ya mara kwa mara katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS). Aidha, hali ya mambo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) haijatulia mpaka sasa, huku wanafunzi 567 wakiwa bado wamesimamishwa. Katika kipindi cha mwezi mmoja imekuwa ikijirudia rudia hali ya mvutano baina ya wanafunzi na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

Hali katika vyuo vikuu hivi na vingine haiendani na ahadi ambayo Waziri Kawambwa alizitoa bungeni na kwa umma miezi kadhaa iliyopita. Leo nimeingia ofisini jimboni na kukatizwa kazi za kufuatilia masuala mengine ya wananchi na habari za mgomo katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam Mlimani.

Pamoja na kuwa bado sijapokea taarifa rasmi ya toka kwa Utawala wa Chuo au kwa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO); wakati nikifuatilia taarifa zaidi nimeona nichukue hatua za kiutendaji za kuwasiliana na wizara yenye dhamana ili waweze kuingilia kati kama sehemu ya kutimiza ahadi iliyotolewa bungeni.

Katika kukabiliana migomo na migogoro katika elimu ya juu serikali imekuwa ikichukua hatua dhidi ya matokeo badala ya kushughulikia vyanzo vya matatizo hivyo natarajia wakati huu Waziri husika atajielekeza katika madai ya msingi ya wanafunzi na wahadhiri.

Serikali izingatie kwamba chimbuko la mgogoro wa MUHAS ni tofauti katika utekelezaji wa agizo la serikali la tarehe 12 Juni 2009 (GN. 178) ambayo limefanya mabadiliko ya makubwa kwenye uendeshaji wa serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu na hivyo kuanzisha mivutano baina ya wanafunzi na utawala katika chuo hicho na vyuo vingine nchini.

Serikali irejee kwamba chanzo cha migomo UDOM ni madai ya wanafunzi kuhusu mafunzo kwa vitendo na malalamiko mengine kutoka kwa wahadhiri. Toka wanafunzi wasimamishwe mwezi Juni 2011 mpaka sasa ikiwa imepita karibu miezi sita wanafunzi 567 bado wamesimamishwa masomo huku zoezi la kumhoji mmoja mmoja likisuasua na kutarajiwa likiwa limepangwa kumalizika mwishoni mwa Mwezi Machi mwaka 2011. Serikali inaweza kabisa kwa kushirikiana na chuo kuharakisha taratibu za kinidhamu wakati huo huo kushughulikia madai ya msingi ya wanafunzi ili kuepusha mazingira ya mivutano kudumu kwa muda mrefu.

Serikali itambue kwamba chanzo cha migomo ya hivi karibuni UDSM ni kugeuzwa kwa taratibu za utoaji mikopo na hatimaye kuchelewa kwa malipo ya wanafunzi na wengine kupata pungufu au kukosa kabisa. Katika mazingira hayo ni muhimu kwa Waziri Kawambwa kuweka wazi kwa umma ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Kuwekwa wazi kwa taarifa hii kutawezesha wawakilishi wa wananchi, wanafunzi, wazazi, vyuo vikuu na wadau wengine wote kuunganisha nguvu katika kushughulikia matatizo yanayoendelea kujitokeza katika elimu ya juu hivi sasa.

Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete aliahidi mwaka 2007 kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wanafunzi wa elimu juu nchini ili kupunguza migomo na migogoro. Katika Mkutano wake na wanafunzi wa vyuo vikuu mwezi Februari 2007 alikwenda mbali zaidi kwa kuwaeleza kwamba hakuna mtoto wa maskini atayeshindwa kuendelea na masomo kutokana na masharti ya mikopo.

Miaka mitano imepita toka ahadi hizo zitolewe migomo katika vyuo vikuu inaendelea na pia wapo watoto wa walalahoi ambao wamefaulu kidato cha sita lakini wemeshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo; hivyo Waziri asipochukua hatua za haraka itadhihirika kwamba ahadi za serikali zimekuwa za ‘kiini macho’.

John Mnyika (Mb)
13/12/2011

Sunday, December 11, 2011

Waziri Mkuu aeleze ufujaji wa sherehe za Uhuru

Vyombo mbalimbali vya habari vya leo tarehe 11 Disemba 2011 vimeeleza kwamba kesho tarehe 12 Novemba 2011 Waziri Mkuu Mizengo atakuwa mgeni rasmi katika shughuli maalumu ya kufunga Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru itakayofanyika kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Mkoani Dar es salaam.

Kwa makadirio ya vyanzo mbalimbali kiwango cha fedha kilichotumiwa mwaka huu kwa ajili ya ‘sherehe’ za miaka 50 ya uhuru kinazidi bilioni 50; hivyo natarajia kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiye mwenyekiti wa maandalizi ya maadhimisho hayo atatumia shughuli hiyo ya kufunga kueleza pia kiwango halisi cha fedha ambacho kimetumiwa hivi sasa na Serikali kupitia Wizara na taasisi zake.

Toka wakati wa bunge la bajeti nimekuwa nikisikitishwa na kiwango kikubwa cha fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya ‘sherehe’ za uhuru katika bajeti za Wizara mbalimbali huku kukiwa na upungufu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Gharama za maisha kwa wananchi ziko juu na uchumi wa nchi uko kwenye hali tete kwa sababu ya pamoja na mambo mengine mfumuko wa bei na kuporomoka kwa shilingi. Hali hii inachangiwa pia na ubadhirifu na matumizi ya anasa ya fedha za umma ambapo ‘sherehe’ hizi ni sehemu za matumizi hayo.

Wakati wa bunge la bajeti nilipiga kura ya HAPANA ya kukataa bajeti ambayo ilitenga fedha nyingi kwenye posho za vikao na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima huku mipango mingine muhimu ya maendeleo mathalani ya kuwezesha jiji la Dar es salaam kupata maji, ujenzi wa barabara za pembezoni kwa ajili ya kupunguza foleni, malipo ya madeni ya walimu, askari na watumishi wa umma pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa haijatengewa fedha za kutosha.

Majibu ya serikali wakati wote yamekuwa ni kwamba hakuna fedha za kutosha sasa ni muhimu Waziri Mkuu Pinda watanzania mabilioni ya ‘sherehe’ hizo yametoka wapi; kwa kuwa kiwango cha matumizi yaliyofanyika kinaonyesha kuwa juu hata ya kile ambacho kimekuwepo kwenye bajeti iliyopitishwa bungeni.

Kiwango hicho cha fedha kingeweza kugharamia masuala yafuatayo ambayo yangefanyika katika kipindi cha mwaka mmoja maadhimisho ya uhuru yangekuwa na maana zaidi kwa sababu tarehe 9 Disemba 1961 Mwalimu Nyerere akihutubia taifa alieleza kuwa ‘uhuru ni kazi’ wala hakusema ‘uhuru ni sherehe’.

Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yangekuwa na maana kama yangeacha kumbukumbu ya mwaka 2011 kwa kulipa madeni yote ya walimu, askari na watumishi wengine wa umma; pamoja na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi iliyotengewa fedha kidogo.

Mathalani ujenzi wa barabara za pembezoni za kupunguza foleni Dar es salaam umetengewa bilioni tano tu, ujenzi wa bwawa la maji la Kidunda umetengewa bilioni sita, na kuna watoto wa maskini ambao wamekosa mikopo na kushindwa kuendelea na elimu tofauti na ahadi ya Kikwete; fedha hizi zingetosha kufanya matumizi haya yote na mengine.

Aidha katika kufunga maonyesho hayo Waziri Mkuu Pinda afafanue pia sababu za maonyeshoya Wizara na Taasisi mbalimbali kufanyika zaidi mkoani Dar es salaam kama vile miaka 50 ya Uhuru ilikuwa kwa ajili ya watu wa Dar es salaam pekee. Fedha hizi za umma zingekuwa na maana kama zingetumiwa kuzunguka nchi nzima kuhamasisha maendeleo mitaani na vijijini ili kusonga mbele kama taifa kwa kuwa mafanikio ya miaka 50 ya Uhuru yanapaswa kujionyesha yenyewe katika maisha ya wananchi.

Wakati Wizara na Taasisi hizo zikiwa zinatumiwa fedha nyingi kufanya maonyesho kwa gharama za posho, machapisho na matumizi mengine yasiyokuwa na lazima; watumishi wa umma wako kwenye hali mbaya na mishahara katika taasisi zao imekuwa ikicheleweshwa. Hivyo, pamoja na kufunga maonyesho Waziri Mkuu Pinda anapaswa kufuatilia kwa kina matumizi ya wizara zote na taasisi zote zinazowahusu ili kuwa na uwajibikaji kutokana na matumizi haya.

Izingatiwe kwamba matumizi haya yamehusisha pia matumizi ya mara nyingi ya fedha za umma kwenye masuala yale yale ya maonyesho kwa kuwa toka mwaka huu uanze Wizara na Taasisi zimekuwa zikifanya maonyesho yao kila moja pekee na kutumia fedha za umma. Wizara na Taasisi hizo hizo nyingi zikashiriki tena maonyesho ya Saba Saba na Wizara na Taasisi hizo hizo zimerudia tena kushiriki maonyesho ya Uhuru katika viwanja hivyo hivyo; katika mkoa huu huu mmoja wa Dar es salaam.

Haya yanafanyika wakati wakina mama wajawazito na wagonjwa wengine wanafariki katika Hospitali ya Mwananyamala, Temeke, Amana, Muhimbili na Ocean Road kwa ajili ya kukosa madawa na huduma nyingine za msingi miaka 50 baada ya uhuru; haya yanafanyika wakati bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari katika Mkoa huu huu wa Dar es salaam ambazo hazina vifaa muhimu ikiwemo madawati miaka 50 ya Uhuru.

Hivyo, ili kushughulikia mianya ya ufujaji na ubadhirifu kutokana na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru ni kamati ya maandalizi iliyoongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda itoe taarifa ya mapato na matumizi. Aidha, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aingize kipengele maalum cha matumizi ya fedha za ‘sherehe’ za uhuru katika ukaguzi wake wa kila Wizara, Taasisi za Umma , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika ukaguzi wa Matumizi ya fedha za mwaka wa fedha 2011/2012.

John Mnyika (Mb)
11/12/2011

Wednesday, December 7, 2011

Msimamo wangu juu ya suala zima la Posho!

Kufuatia habari tarehe 28 Novemba kuhusu ‘kupanda kimya kimya kwa posho za wabunge kwa zaidi ya asilimia 150’ tarehe 29 Novemba 2011 nilitoa kauli yangu kama mbunge na katibu wa wabunge wa CHADEMA kuhusu suala husika.

Katika kauli hiyo nilieleza kuwa: “ Wabunge wa CHADEMA hatujapokea taarifa rasmi kwamba masharti ya kazi ya ubunge yamebadilika na kwamba viwango vya posho vimeongezwa. Wala kamati ya wabunge wa CHADEMA haijawahi kuridhia ongezeko lolote la posho ya vikao (sitting allowance) kwa wabunge. Napenda kutumia fursa kusisitiza msimamo wetu wa kutaka posho za vikao (sitting allowance) ziweze kufutwa kwa wabunge na katika mfumo mzima wa malipo ya wakati wa kazi miongoni mwa watumishi wa umma”.

Hivyo, kama mbunge na katibu wa wabunge wa CHADEMA nilitoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya Serikali na Spika Anna Makinda kwa niaba ya Bunge kutoa kauli kuhusu suala hili ili kuondoa hisia zinazojengeka kwamba ‘wabunge wote tumekaa bungeni na kukubaliana kujiongezea posho ya vikao’.

Kufuatia Spika Makinda kutoa kauli na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe leo tarehe 7 Novemba 2011 naomba kutoa msimamo wangu kama ifuatavyo:
“ Ongezeko la posho ya vikao lilofanyika linapaswa kusitishwa kwa kuwa limefanyika kinyume na taratibu na pia halina uhalali wowote kimantiki na halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla; nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni haramu (Illegitimate).

Bado narudia kutoa mwito kwa Rais Kikwete kutoa kauli wake na wa Ikulu na Ofisi ya Rais kwa ujumla unaacha ombwe lenye athari kubwa kwa serikali na kwa bunge mbele ya wananchi ambao kwa mujibu wa katiba ibara ya nane ndio wenye mamlaka na madaraka.
Aidha, kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo ya posho za vikao ni kwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo.

Nyongeza hiyo ya posho ya vikao ni matumizi mabaya ya madaraka na ni dharau kwa walipa kodi wanaohangaika na kupanda kwa gharama za maisha na athari za ubadhirifu wa fedha za umma. Ni udhaifu kufikiri kwamba suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha ni kuongeza posho za kikao; tatizo la kupanda kwa gharama za maisha linapaswa kushughulikiwa kwa kuchukua hatua dhidi ya matatizo ya kiuchumi katika nchi ili kuweza kuwa na tija kwa wananchi wengi ambao ni waathirika zaidi wa kupanda kwa gharama za maisha kuliko wabunge.

Pia, utetezi wa Spika Makinda kuhalalisha upandishaji wa kinyemela wa posho za vikao kwa wabunge haina maana kuwa kama sababu ingekuwa chanzo ni kupanda kwa gharama maisha ingepandishwa posho ya kujikimu (subsistence allowance) ambayo imebaki pale pale 80,000 .

Aidha kufuatia kauli ya Spika Makinda, hatua za kinidhamu zinapaswa zichukuliwe na Rais Kikwete dhidi ya Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashilillah ya kutoa taarifa potofu kwa umma kwa kukanusha kwamba ofisi ya bunge haijaongeza posho kwa wabunge na pia kwa kufanya malipo kinyume na taratibu.

Kugongana kwa kauli baina ya Spika na Katibu wa Bunge ni ishara ya kuwepo kwa jambo ambalo linafichwa kuhusu suala hilo la nyongeza haramu ya posho za vikao kwa wabunge na pia ni ushahidi wa taratibu kukiukwa hali ambayo inahitaji kauli kutoka kwa mwenye mamlaka kwa mujibu wa sheria kuhusu masuala ya posho za wabunge ambaye ni Rais.

Pia, katibu wa wabunge anapaswa kutuomba radhi wabunge kwa kauli yake kwamba mabadiliko ya posho za vikao yametokana na mkutano wa wabunge tarehe 8 Novemba 2011 kuiomba serikali ipandishe posho hizo za vikao.

Binafsi nilikuwepo kwenye mkutano huo wa tarehe 8 Novemba 2011 na hakuna uamuzi wowote ambao ulifikiwa wa kuiomba serikali ipandishe posho za vikao. Kilichotokea ni kwamba katika kuchangia maelezo ya serikali na ya bunge kuhusu masuala mbalimbali ya bunge na serikali yaliyojiri baada ya mkutano wa nne wa Bunge na mpangilio wa mkutano wa tano wa bunge, wabunge walipewa fursa ya kujadili taarifa hizo.

Katika kujadili taarifa hizo wapo wabunge wachache waliotoka nje ya hoja za msingi na kuzungumzia kuhusu nyongeza ya posho ya vikao; hata hivyo mkutano huo wa wabunge haukufanya maamuzi yoyote na wala haukukamilika. Kabla ya majina yetu wengine kufikiwa kuweza kuchangia Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kwa nafasi yake ya kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ni mwenyekiti wa mikutano ya wabunge alieleza kwamba muda umemalizika hivyo mkutano na kwamba tarehe nyingine ingepangwa kwa ajili ya kuendelea kujadili masuala mbalimbali yaliyohojiwa na pia kuweza kutoa fursa kwa wabunge wengine kuweza kutoa maoni yao kuhusu masuala hayo.

Katika hatua hiyo Waziri Mkuu Pinda alisoma majina yetu na kueleza kwamba mkutano huo wa wabunge ungeendelea katika tarehe nyingine lakini haukufanyika mkutano mwingine; hivyo katika mkutano wa tano wa bunge uliomalizika wabunge ambao mimi nilishiriki wabunge wote hatujawahi kukaa na kujipangia nyongeza ya posho za vikao kama inavyoelezwa hivi sasa wala.

Pia, wabunge hatujawahi kupatiwa nakala ya muktasari au kumbukumbu wa vikao vya kamati ya uongozi au vya tume ya bunge ambavyo vimekaa na kupitisha nyongeza ya posho ya vikao kutoka 70,000 mpaka 200,000 kama Spika alivyonukuliwa na vyombo vya habari. Ni muhimu watanzania wakazingatia kwamba mwenye mamlaka ya kupandisha posho za wabunge ni Rais na natoa mwito kwa Rais kukataa kupandisha posho za vikao kwa wabunge na badala yake azifute kabisa. Watumishi wote wa umma ikiwemo wabunge hatustahili kulipwa posho za kukaa kwenye vikao vyetu ambavyo mwisho wa mwezi tunalipwa mshahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Kufuatia hali hii, kwa kuwa sasa imeshatoka kauli rasmi ya bunge yenye kudhihirisha kwamba posho za vikao zimepandishwa kinyemela badala ya kufutwa kama tulivyotaka awali; tutaitisha kikao cha wabunge wa CHADEMA ili kukabaliana hatua za ziada za kuchukua kwa kuwa ofisi ya bunge na serikali wanaendelea kuingiza posho za vikao kwenye akaunti za wabunge hata baada za kuzipinga.”


Katika kauli yangu ya tarehe 29 Novemba 2011 nilieleza kwamba ni vyema umma ukafahamu kwamba Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais ataeleza kwa maandishi. Katika kipengele (d) sheria imetaja orodha (i) mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri, kujikimu na wasaidizi. Katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao (Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye akaunti za wabunge moja kwa moja ambayo kamati ya wabunge wa CHADEMA tunataka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.
Kifungu 19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu hiki kimetoa mwanya wa kutolewa kwa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010 wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya vikao (Sitting Allowance).

Hivyo, ofisi ya Rais na Ofisi ya Bunge zinapaswa kuwaeleza watanzania iwapo waraka huo umebadilishwa na sababu za wabunge kutojulishwa kuhusu mabadiliko hayo.
Aidha tarehe 29 Novemba 2011 nilieleza kuwa, iwapo mabadiliko hayo yamefanyika ni muhimu yakasitishwa kwa kuwa zitakwamisha utekelezaji wa mpango wa kufuta posho za vikao (sitting allowance) na kupunguza matumizi ya serikali kama ilivyoelezwa katika Ilani ya CHADEMA ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa bungeni mwaka 2011.

Izingatiwe kwamba uchumi wa nchi hivi sasa unasuasua, serikali ina hali mbaya ya fedha kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha kinachopatikana katika kodi na washirika wa kimaendeleo ukilinganisha na mahitaji ya bajeti; na hivyo kukopa kibiashara kwa ajili ya kuziba nakisi iliyopo.

Kupungua kwa uzalishaji, kiwango cha fedha pamoja na kuongezeka kwa ubadhirifu katika matumizi ya rasilimali za umma kunachangia katika mfumuko wa bei hali inayohitaji mpango wa dharura wa kunusuru uchumi wetu ukaohusisha pamoja na mambo mengine kubana matumizi ya serikali.

“ Binafsi natarajia serikali ije kwetu wabunge na mpango wa kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi badala ya kutuletea mpango wa kutuongezea wabunge posho za vikao huku mwelekeo wa uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ukiwa kwenye hali tete”.

Kamati ya wabunge wa CHADEMA ilikubaliana posho hizo zifutwe kwa kuwa Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imeeleza kwamba lengo la msingi ni kuondoa posho za vikao (sitting allowance ) hatua ambayo itaambatana na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi, nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya kwa haki. Uamuzi huu ungewezesha pia kuelekeza fedha zaidi katika miradi ya maendeleo.

Ofisi ya Rais na Ofisi ya Bunge zizingatie kuwa Serikali ya CCM imeridhia msimamo huo na kuuingiza kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2011/2012-2015/2016 uliosainiwa na Rais Jakaya Kikwete tarehe 7 Juni 2011 ambao kwenye ukarasa wa 17 unatamka bayana kwamba posho za vikao na nyinginezo zinapaswa kufutwa au kuwianishwa hivyo kuziongeza ni kupuuza mpango huo.

John Mnyika (Mb)
07/12/2011

Thursday, December 1, 2011

Jitokeze kesho, 2nd Dec, 2011 Ukumbi wa Makumbusho Dar(mkabala na IFM) ktk Mkutano wa wadau ulioitishwa na TANESCO!Kukataa ongezeko la bei ya umeme

Kesho tarehe 2 Disemba 2011 katika Ukumbi wa Makumbusho Dar es salaam (mkabala na IFM) kuanzia saa 4 asubuhi EWURA imeitisha Mkutano wa Wadau kujadili ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa 155% (zaidi ya mara tatu ya bei ya sasa).
Nawaomba wanamtandao wote tuhamasishe umma kwa kutumia TEHAMA (sms, facebook, twitter, email na njia nyingine) ili wananchi waweze kuhudhuria mkutano husika kwa wingi na kutoa maoni.

Mtakumbuka kwamba tarehe 23 Novemba 2011 nilitoa taarifa kwa umma kwamba Serikali inapaswa kusitisha ombi la dharura la kupandisha bei ya umeme kwa kiwango kikubwa ili kuepusha athari katika usalama na uchumi kutokana na mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha. Aidha, serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kulinusuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) dhidi ya mzigo mkubwa wa gharama unaotokana na ufisadi wa muda mrefu katika mikataba ya gesi asilia na gharama za mitambo ya kufua umeme wa dharura badala ya kuweka mkazo katika kuongeza bei ya umeme kwa wananchi wa kawaida.

Izingatiwe kuwa tarehe 9 Novemba 2011 Mamlamka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipokea ombi la dharura toka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kuidhinisha ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa (zaidi ya mara tatu).

Naomba umma wa watanzania uzingatie athari za maombi hayo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla hivyo mjadala wa kitaifa unahitajika na natoa mwito kwa wananchi kuweza kutoa maoni yao kuanzia sasa. Aidha ni muhimu kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau ulioitishwa na EWURA tarehe 2 Disemba 2011.

Umma wa watanzania ufahamu kwamba ongezeko hili sio ombi la TANESCO pekee bali ni agizo kutoka kwa serikali kwa kurejea maelezo ya Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja bungeni katika mkutano wa nne wa bunge na kusisitizwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwezi Septemba 2011 akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Mara.

Namshangaa Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa taifa tarehe 18 Novemba 2011 alipozungumzia utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme hakuwaeleza watanzania kwamba uwasilishaji wa ombi hilo ni sehemu ya mpango huo wa dharura ambao utawaongezea wananchi bei ya umeme na gharama na maisha na hivyo kuathiri utekelezaji wa ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania.

Wananchi wakumbuke kwamba hii ni mara ya pili katika kipindi cha takribani mwaka mmoja kwa TANESCO kupandisha bei ya umeme; mara ya kwanza ikiwa mwezi Januari 2011 ambapo umeme ulipanda kwa asilimia 18.5 na kuchangia katika kupanda kwa gharama za uzalishaji katika nchi na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Ombi la TANESCO la wakati huo la kupandisha umeme lilikuwa ni asilimia 34 likakataliwa na EWURA na kushushwa mpaka asilimia 18.5, sasa Rais Kikwete, Waziri Mkuu Pinda na Waziri Ngeleja wanapaswa kuwaeleza watanzania sababu za kufanya ombi hilo la dharura kuwa la wastani wa asilimia 155 ili wananchi waweze kutoa maoni kwa kuzingatia mzigo ambao umma unataka kubebeshwa.

Pamoja na matatizo ya kifedha ya TANESCO ambayo serikali inapaswa kuyashughulikia kwa pamoja na mambo mengine kutoa ruzuku katika kipindi hiki cha mpito; gharama kubwa za uzalishaji zinazolikabili shirika zinachangiwa na ufisadi wa muda mrefu katika mikataba ikiwemo ya uzalishaji wa gesi na ukodishaji wa mitambo ya kufua na pia maamuzi ya kukopa kibiashara katika kutekeleza mpango wa dharura wa umeme.

Kabla ya kuongeza bei ya umeme kwa watanzania wa kawaida, Serikali iwaeleze wananchi imewapunguzia mzigo kiasi gani kwa kupitia upya mikataba ya kifisadi inayolinyonya Shirika la Umeme Tanzania kama ilivyopendekezwa kwenye ripoti mbalimbali ikiwemo katika maazimio ya Bunge ya mwaka 2008 juu ya mkataba wa ukodishaji wa mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Richmond Develepment Company LLC ambapo orodha ya mikataba na makampuni mengine ilitajwa.

Aidha, umma uelezwe pia ukweli iwapo uamuzi wa kuchukua mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa umeongeza zaidi gharama za uzalishaji wa umeme na hivyo kuifanya TANESCO iongeze zaidi bei ya umeme kwa wateja ikizingatiwa kuwa tarehe 15 Julai 2011 na 13 Agosti 2011, nilisisitiza bungeni serikali ipunguze bajeti katika maeneo mengine yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi zaidi kwenye umeme bila kuongeza mzigo mkubwa wa riba utakaolipwa na wananchi kupitia ongezeko la bei.

Uamuzi huu wa kupandisha kwa kiwango kikubwa bei ya umeme utasababisha ongezeko la ziada la mfumuko wa bei hali ambayo ni tishio wa usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Serikali izingatie kwamba mfumuko wa bei nchini hivi sasa umefikia asilimia 17.9 na bidhaa zinazochangia mfumuko huo kwa kiwango kikubwa ni vyakula, mafuta na umeme. Kupanda kwa bei kwenye sekta ya nishati pekee kumekuwa kwa asilimia 37.4 na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha, sasa viongozi wajiulize itakuwaje umeme ukapopanda kwa wastani wa asilimia 155.

Wananchi wakumbuke kwamba katika hotuba yake kwa taifa tarehe 18 Novemba 2011 Rais Kikwete ameelezea kwamba mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola kwa ujumla kumetokana na uchumi wa nchi mbalimbali duniani hususani za Ukanda wa Sarafu ya Ulaya (Eurozone) kuwa katika kipindi kigumu na cha mashaka na kueleza kwamba suluhisho la matatizo la uchumi wetu litategemea uchumi wao.

Kauli hii imedhihirisha kwamba Serikali haina mpango wa haraka wa kukabiliana na mfumuko wa bei, kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa gharama za maisha. Hali itakuwa mbaya zaidi iwapo tutaruhusu pamoja na sababu za nje ya nchi yetu tukaongeza vyanzo vya ndani vya kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na bei za bidhaa kwa kupandisha bei ya nishati ya umeme ambayo chanzo chake ni hapa hapa nchini. Hivyo, mpango huu wa kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 unapaswa kusitishwa ama kubadilishwa kwa kulinda maslahi ya makundi mbalimbali kwa kuzingatia aina za matumizi.

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
1/12/2011

Friday, November 25, 2011

Juu ya hoja ya kutaka kupandishwa bei ya umeme!

Mnyika ataka bei ya umeme isipandishwe
Wednesday, 23 November 2011

MBUNGE wa Ubungo,jijini Dar es Salaam, John Mnyika, ameitaka Serikali kusitisha ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 155, ili kuepusha athari katika usalama na uchumi wa nchi, utakaozidishwa na mfumuko wa bei.


Mbunge huyo alisema hayo jana kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, kufuatia hatua ya Tanesco kutaka kupandisha bei ya umeme kwa kiwango hicho.

Mnyika alisema Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kuinusuru Tanesco dhidi ya mzigo mkubwa wa gharama unaoikabili, badala ya upandisha bei ya umeme kwa wananchi.

"Itakumbukwa kwamba Novemba 9 mwaka huu Mamlamka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ilipokea ombi la dharura kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuidhinisha ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa, bei ambayo ni zaidi ya mara tatu ya sasa" alisema Mnyika.

Mnyika pia alisema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kwa wingi katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau ulioitishwa na Ewura kuhusu upandishaji bei ya umeme ili nao, wapate fursa ya kutoa maoni yao ipasavyo.


"Wananchi wakumbuke kwamba hii ni mara ya pili katika kipindi cha takribani mwaka mmoja kwa Tanesco kupandisha bei ya umeme. Mara ya kwanza ilikuwa Januari mwaka huu ambapo umeme ulipanda kwa asilimia 18.5 na kuchangia katika kupanda kwa gharama za uzalishaji na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi" alisema.

Mnyika alisema kabla ya kuongeza bei ya umeme kwa wananchi, Serikali inapaswa kwanza kuwaeleza namna ilivyowapunguzia mzigo kwa kupitia upya mikataba inayoinyonya Tanesco.

Alisema uamuzi wa kupandisha bei ya umeme utasababisha ongezeko la mfumuko wa bei , jambo ambalo litatishia usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa jumla.

“ Serikali izingatie kwamba mfumuko wa bei nchini hivi sasa umefikia asilimia 17.9 na bidhaa zinazochangia mfumuko huo kwa kiwango kikubwa ni vyakula, mafuta na umeme. Kupanda kwa ya nishati ya umeme pekee kumekuwa kwa asilimia 37.4 na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha” alisema.

Alisema mpango huo wa kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 unapaswa kusitishwa ama kubadilishwa kwa kulinda maslahi ya makundi mbalimbali kwa kuzingatia aina za matumizi.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/51-habari-nyingine/17784-mnyika-ataka-bei-ya-umeme-isipandishwe

Wednesday, November 23, 2011

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Prof.Anna Tibaijuka katika Kata ya Sinza kukagua uuzwaji maeneo ya wazi


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Prof. Anna Tibaijuka akiongea na mkazi wa Sinza Ndahani Yohana ambaye amenunua eneo la wazi kwa utapeli kwa shilingi milioni 500 wiki mbili zilizopita, ambapo ramani halisi inaonyesha eneo hilo ni la wazi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Prof. Anna Tibaijuka akihakiki na kuonyesha kupitia ramani maeneo ya wazi yaliyouzwa na kuvamiwa katika Kata ya Sinza eneo la Sinza E

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Prof. Anna Tibaijuka wa pili kutoka kulia akiangalia ramani halisi inayoonyesha maeneo ya wazi wakati alipokagua maeneo ya wazi yaliyovamiwa na wananchi maeneo ya Sinza E wilaya ya Kinondoni, ambapo pia alikuwa akikagua mabango yaliyowekwa kwa ajili ya kuwataarifu wananchi na kuwaelimisha maeneo ambayo ramani inaonyesha yako wazi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya Serikali.

Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba akimwonyesha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Prof. Anna Tibaijuka maeneo ya wazi yaliyovamiwa na wananchi katika maeneo ya Sinza E

Nashukuru sana blogu ya http://www.hakingowi.com/ kwa kurusha habari hii!

Tuesday, November 15, 2011

Sheria ya Manunuzi!

Sheria ya Ununuzi: Wabunge wapunguza nguvu za Rais
Monday, 14 November 2011 21:41

Kizitto Noya, Dodoma
MUSWADA wa Sheria ya Ununuzi wa Umma jana ulipita kwa mbinde baada ya wabunge kuibana Serikali na kuilazimu kuufanyia marekebisho kwenye baadhi ya vipengele, ikiwemo kuondoa kipengele kinachotaka Rais athibitishe ununuzi.

Mbali na kuibana Serikali kubadili kipengele hicho, wabunge pia walitaka ufafanuzi wa kina kuhusu kifungu cha 104 kinachoelezea adhabu ya mtu anayeisababishia Serikali hasara katika mchakato wa ununuzi pamoja na kifungu cha 66 kinachopendekeza ununuzi wa vifaa vilivyotumika, hatua ambayo ilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuagiza vipengele hivyo kurudishwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo za Bunge, kwa ajili ya majadiliano zaidi.

Muswada huo ambao awali ulipangwa kupitishwa jana mchana, ulilazimika kusubiri katika kikao cha jioni baada ya kutokea malumbano makali ya hoja kati ya wabunge waliopinga vipengele hivyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye alikuwa akivitetea.Malumbano hayo yalijitokeza wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati kwa ajili kupitisha sheria hiyo mpya.

Wabunge waliotawala mjadala huo walikuwa John Mnyika wa Ubungo (Chadema), Luhaga Mpina wa Kisesa (CCM) na Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki (CCM).

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao walipinga adhabu iliyopendekeza mtu anayepatikana na hatia ya kuisababishia Serikali hasara katika mchakato wa ununuzi, kufungwa miaka mitano na kulipa faini ya kuanzia Sh5milioni hadi Sh10 milioni wakisema ni ndogo na inapaswa kuongezwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi naona adhabu hiyo ni ndogo, mtu wa aina hiyo anapaswa kufungwa siyo zaidi ya miaka 30 na baadaye afilisiwe mali zake kulipa hasara aliyoisababishia Serikali,” alisema Mpina na baadaye kuungwa mkono na wabunge wengine watano: Seleman Jafu (Kisarawe), Christina Mughwai (Viti Maalumu), Alphaxard Lugola (Mwibara), Dk Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini) na Mnyika.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, wabunge hao walisema si sahihi wala haki mtu aliyeisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kufungwa jela kwa kipindi kisichozidi miaka mitano na kulipa faini isiyopungua Sh10 milioni au zaidi wakisisitiza kuwa mtu huyo anapaswa kufungwa miaka isiyopungua 20 na isiyozidi 30 na baadaye afilisiwe mali zake zote kulipa deni.

Hata hivyo, Werema alipinga mapendekezo hayo ya wabunge kwa maelezo kuwa adhabu hiyo ni kubwa mno kwa watu ambao mfumo, uliwadhamini kuitumikia jamii.

“Waheshimiwa wabunge, katika kutunga sheria tusiwe na hasira kwa sababu hasira ni pango la shetani. Nakubaliana kwamba tatizo hilo linahitaji adhabu kali lakini, adhabu hiyo inapaswa kuwa ya uwiano na kosa lenyewe. Kosa tunalotaka kulifanya tuliwahi kulifanya mwaka 1983 katika Sheria ya Uhujumu Uchumi. Sheria ile tuliitunga kwa hasira, kwa ushauri wangu adhabu hiyo inatosha,” alisema Jaji Werema.

Kauli hiyo ya Jaji Werema, iliwaamsha wabunge kadhaa na Makinda kumchagua Mpina kuzungumza ambaye alisema: “Ninachoweza kusema hapa ni kwamba Mwanasheria Mkuu hana uzoefu na manunuzi.”

“Kwa nini tuwe na sheria za upendeleo? Tumetunga sheria kwamba raia akionekana kwenye mbuga za wanyama hata kama hana silaha, akamatwe na watu wanapigwa risasi. Lakini tunapokuja kutunga sheria kwa ajili ya watendaji tunataka ziwe laini, kwa faida ya nani?”

Malumbano hayo yalimfanya Spika Makinda ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge zima, kuifunga hoja hiyo akisema: “Sasa naagiza kifungu hicho kirudishwe kwenye kamati ili kikajadiliwe upya.”

Hoja nyingine iliyozua mjadala katika kikao hicho ni ile aliyoitoa Mnyika kutaka kanuni zitakazotungwa na waziri kwa ajili ya utekelezaji wa sheria hiyo, zipitiwe upya na Bunge pamoja na kutaka kufutwa kabisa kifungu cha 66 kinachotaka kuruhusiwa ununuzi wa vifaa vilivyotumika.

Mkulo
Awali, akifunga mjadala huo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema Serikali imeridhia mapendekezo ya wabunge kufanyia marekebisho kipengele kinacholihusisha Baraza la Mawaziri kushiriki katika kuidhinisha ununuzi wa umma.
“Tumekubaliana na mapendekezo ya wabunge kwamba Rais asihusishwe kuidhinisha ununuzi, badala yake sasa kazi hiyo itafanywa na Waziri wa Fedha baada ya kushauriwa na kamati maalumu atakayoiunda.”

Waziri Mkulo aliwaomba wabunge kuondoa hofu ya mwanya wa ufisadi katika sheria hiyo, akisema Serikali imejipanga vya kutosha kukabiliana na hali hiyo kwa kuja na kanuni zitakazodhibiti mianya yote ya rushwa.

Alitaja baadhi ya kanuni hizo kuwa ni zile zinazotaka wataalamu kukagua mali inayotaka kununuliwa, mmiliki kuwasilisha nyaraka zinazoonyesha kifaa husika kimetengenezwa lini, ulinganifu wa ubora wa vifaa pamoja na taasisi zisizoridhika na mchakato kutoa taarifa (Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).

Kupitisha muswada
Kabla ya kupitishwa kwa muswada huo jana jioni, Jaji Werema alifafanua kwamba Serikali imekubaliana na hoja ya Mpina ya kukifanyia marekebisho kifungu cha 104 kinachohusu adhabu kwa watuhumiwa ambacho kinatoa mamlaka ya mtuhumiwa aliyesababishia Serikali hasara katika ununuzi kuhukumiwa adhabu ya miaka zaidi ya saba na kufidia hasara hiyo au kukamatwa na kutaifishwa kwa mali zake.

Jaji Werema alisema anaamini kwamba adhabu hizo zitaongeza uwajibikaji na umakini katika kusimamia na kutekeleza Sheria ya Ununuzi ili kuliepusha taifa na hasara na kuongeza kwamba Serikali pia ilikubaliana na hoja ya Mnyika aliyeonyesha shaka juu ya mamlaka ya waziri katika utekelezaji wa kanuni ambayo pamoja na mambo mengine, ataweza kuunda timu ya wataalamu ambayo itamshauri katika baadhi ya vitu muhimu vinavyohitaji ununuzi kisha naye kuamua.

Hata hivyo, baadaye muswada huo ulipitishwa na utakapotiwa saini na Rais, Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2011 itachukua nafasi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004, inayotumika sasa.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/49-uchaguzi-mkuu/17501-sheria-ya-ununuzi-wabunge-wapunguza-nguvu-za-rais

Monday, November 14, 2011

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA

SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, 2011
(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZIMheshimiwa Spika,
Tarehe 11 Machi 2011, Serikali ilichapisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika Gazeti la Serikali la tarehe hiyo. Muswada huo ulipelekwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa Hati ya Dharura. Hata hivyo, baada ya upinzani mkubwa dhidi ya Muswada huo kujitokeza karibu nchi nzima, Bunge lililazimika kuondoa Hati ya Dharura na hivyo kufanya Muswada kushughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida wa kutunga sheria uliowekwa na kanuni za 80, 83 na 84 za Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano, 2007. Katika kufanya hivyo, Bunge – kwa kupitia Spika - liliiagiza Serikali kufanya mambo yafuatayo kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano Katika Bunge (Hansard) ya Kikao cha Nane cha Mkutano wa Tatu cha tarehe 15 Aprili 2011:


(a) “Muda zaidi utolewe kwa Kamati na wananchi kuufikiria Muswada huu. Katika kufanikisha hili, “... iandae Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ili wananchi wenyewe waweze kusoma yaliyomo kwenye Muswada huo badala ya kupewa tafsiri tu na watu wengine;


(b) “Muswada uchapishwe kwenye magazeti na kutangazwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari ili kutoa fursa ya kutosha kwa wananchi wengi kuuelewa na kuutolea maoni;
(c) “Utangulizi wa Muswada huu uwekwe vizuri zaidi ili wananchi waelewe madhumuni ya Muswada huu, kwani imeonekana wazi wananchi wengi wanadhani tayari tumeanza kuandika Katiba, kumbe lengo la Muswada huu ni kutunga Sheria ya Kuunda Tume ya Kukusanya Maoni tu.” (uk. 31-32)

Mheshimiwa Spika,
Katika kutoa maagizo haya, Bunge lilisitiza kwamba “... Muswada huu uko ndani ya Bunge, hauko serikalini.” (uk. 33) Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Bunge, Muswada ulikwishasomwa kwa mara ya kwanza na kupelekwa kwenye Kamati inayohusika kwa ajili ya kuanza kujadiliwa. Aidha, kwa mujibu wa kanuni ya 84(2) Kamati ilikwishaanza kupokea maoni ya wadau “... kwa lengo la kuisaidia katika uchambuzi wa Muswada huo.” Kazi iliyokuwa imebaki kwa Kamati ilikuwa ni kutumia mamlaka yake chini ya kanuni ya 84(3) “... kufanya marekebisho katika Muswada wa Sheria kwa kumshauri Waziri ... anayehusika na Muswada huo kufanya mabadiliko....” Ni baada tu ya kupata ushauri wa Kamati kuhusu mabadiliko ndio Serikali ingeweza kuleta Jedwali la Mabadiliko kwa lengo la kufanya mabadiliko katika hatua hii kabla Muswada haujaletwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa mara ya pili na kwa mjadala wa Bunge zima.

Mheshimiwa Spika,
Hakuna hata moja ya maagizo haya ya Bunge ambalo limetekelezwa na Serikali. Tafsiri ya Kiswahili ambayo imeletwa Bungeni – pamoja na kuonyesha imesainiwa tarehe 8 Machi 2011 sawa na Muswada wa Zamani uliopigiwa kelele sana na wananchi – ililetwa kwenye Kamati wiki mbili zilizopita, ikiwa ni wiki moja baada ya Kamati kukataa kuujadili Muswada Mpya kwa vile ulifanyiwa mabadiliko na Serikali bila kupata ushauri wa Kamati kama inavyotakiwa na kanuni ya 83(4) ya Kanuni za Bunge. Badala ya kutekeleza maagizo ya Bunge, Serikali imeleta Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ambao ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 14 Oktoba 2011.

Muswada huu mpya una tofauti kubwa na za kimsingi na Muswada wa Zamani kama nitakavyoonyesha hapa. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mabadiliko makubwa na ya kimsingi yaliyofanywa kwenye Muswada wa Zamani yalihitaji na bado yanahitaji mjadala wa kitaifa wa wananchi kama ambavyo wengi wamedai katika mijadala inayoendelea nchi nzima. Aidha, Bunge hili tukufu lilihitaji, na bado linahitaji, muda zaidi wa kuyatafakari mabadiliko haya makubwa nay a kimsingi katika Muswada wa Zamani. Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini ni busara na ni sound policy kwa Muswada huu Mpya kusomwa mara ya Kwanza ili kuruhusu mjadala unaohitajika kufanyika.

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, Muswada huu unapendekeza kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa mujibu wa Utangulizi wa Muswada, itawajibika “... kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba (na) kuainisha na kuchambua maoni ya wananchi....” Kwa mujibu wa ibara ya 5, Tume hii itaundwa na Rais “kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar, na kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar....” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 6(1), Rais atateua wajumbe wa Tume “... kwa kushauriana na kukubaliana na Rais wa Zanzibar....”

Ibara ya 6(2) inapendekeza kwamba “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Pendekezo hili linarudia, kwa njia iliyojificha zaidi, msimamo wa ibara ya 6(2) ya Muswada wa Zamani iliyokuwa imeweka wazi kwamba idadi ya wajumbe wa Tume itakuwa sawa kwa sawa kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano! Kama ilivyokuwa kwa Muswada wa Zamani, ibara ya 7(2) ya Muswada inapendekeza kwamba “uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti utafanyika kwa msingi kwamba iwapo Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Makamu Mwenyekiti atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano.”

Muundo wa Tume unakamilishwa na Sekretarieti ya Tume itakayoongozwa na Katibu. (ibara ya 13(1) Kwa mujibu wa ibara ya 13(2), Katibu huyo atateuliwa na Rais “baada ya kukubaliana na Rais wa Zanzibar.” Watendaji wengine wa Sekretarieti watateuliwa na Waziri “kwa makubaliano na Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Muswada unapendekeza kumpa Rais - baada ya makubaliano na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kutoa hadidu za rejea za Tume na muda wa kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(1) Na kama hali itahitaji kufanya hivyo, Rais – “kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar” – anaweza kuongeza muda usiozidi miezi mitatu ili kuwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti. (ibara ya 8(2) Hadidu za rejea, kwa mujibu wa ibara ya 8(3), “... zitakuwa ni hati ya kisheria ambayo Tume itaizingatia katika utekelezaji wa majukumu na utumiaji wa mamlaka yake kwa mujibu wa Sheria hii.”

Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 9(1) ya Muswada inaelezea kazi za Tume kuwa ni pamoja na:
(a) Kuratibu na kukusanya maoni ya wananchi;
(b) Kupitia na kutafiti usahihi na ulinganifu wa masharti ya kikatiba yanayohusu mamlaka ya watu, mifumo ya kisiasa, demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora;
(c) Kutoa mapendekezo kwa kila hadidu ya rejea; na
(d) Kuandaa na kuwasilisha ripoti.
Ijapokuwa haijaanishwa hivyo, ni wazi - kwa mujibu wa wa ibara ya 17(1)(d) na (2) ya Muswada - kwamba moja ya kazi za Tume ni kuandaa Rasimu ya Muswada wa Katiba mpya. Mapendekezo ya Muswada kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni muhimu na yanazua maswali mengi yanayohitaji mjadala wa kitaifa na maamuzi ya wananchi. Maeneo haya muhimu ni pamoja na nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano katika mchakato mzima wa kutengeneza Katiba Mpya.

MAMLAKA YA RAIS

Mheshimiwa Spika,
Kama ambavyo tumepata kusema ndani ya Bunge hili, kwa muda wote wa uhai wetu kama taifa huru, mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa umejengwa juu ya nguzo kuu ya Urais wa Kifalme (Imperial Presidency). Hii inatokana na ukweli kwamba katika mfumo huu, Rais ana madaraka makubwa sana ya kiutendaji na ya kiutungaji sheria. Vile vile Rais ana kivuli kirefu cha kikatiba juu ya mahakama kwa kutumia mamlaka makubwa aliyonayo katika uteuzi wa viongozi wote wa ngazi za juu za Mahakama. Urais wa Kifalme ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote za serikali na ndio kichocheo kikubwa cha rushwa na ufisadi wa kutisha ambao umefanywa kuwa ni sehemu ya kawaida ya maamuzi ya kiserikali. Sio vibaya, katika kuthibitisha jambo hili, kurudia maneno ya ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977: “... Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote....” Na kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwenye mahojiano ya mwaka 1978 na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kama Rais wa Tanzania alikuwa na mamlaka – kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi yetu – ya kuwa dikteta!

Muswada unaendeleza kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Mtu mwenye mamlaka ya kidikteta, kama Rais alivyo kwa mujibu wa Katiba ya sasa, hawezi kusimamia upatikanaji wa katiba ya kidemokrasia. Kwa kutumia mamlaka makubwa ya uteuzi wa Tume yanayopendekezwa na Muswada huu, ni wazi Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama tawala cha CCM, atateua wajumbe anaowataka yeye na Rais Ali Mohamed Shein, Makamu wake na pia Rais wa Zanzibar! Ni wazi vile vile kwamba watu watakaoteuliwa na Marais hawa ni watu wasiokuwa tishio kwa status quo kwa maana ya kupendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kikatiba na kiutawala na hivyo kuhatarisha maslahi ya CCM!

Mheshimiwa Spika,
Hali ni hiyo hiyo kwa Sekretarieti ya Tume ambayo ndio chombo cha kiutendaji na moyo wa Tume yenyewe. Kama Katibu, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Tume ni mteuliwa wa Rais na ni mtumishi wa Serikali; kama watendaji wengine wa Tume ni watumishi wa serikali walioteuliwa wa Waziri ambaye naye ni mteuliwa wa Rais baada ya kukubaliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar; na kama watumishi wengine wa Tume nao ni watumishi wa Serikali kama inavyopendekezwa na ibara ya 13 ya Muswada Mpya, ni wazi, kwa hiyo, kwamba mapendekezo haya yote ya uteuzi wa wajumbe, watendaji na watumishi wengine wa Tume yana lengo moja tu: kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.

Mheshimiwa Spika,
Badala ya mapendekezo haya ya Muswada Mpya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza utaratibu wa kidemokrasia zaidi katika uteuzi wa Tume. Kwanza, badala ya Tume hiyo kuwa ‘Tume ya Rais’ kama inavyopendekezwa katika Muswada, tunapendekeza iwe ‘Tume ya Vyama’ (multiparty Commission) kwa maana moja kubwa: wajumbe wa Tume wateuliwe kufuatana na mapendekezo na makubaliano ya vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni, vyama vingine vilivyosajiliwa pamoja na mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini. Hii haina maana kwamba wajumbe wa Tume hiyo hawatatakiwa kuwa na sifa zilizoainishwa katika ibara ya 6(3) ya Muswada Mpya. La hasha! Wajumbe wa Tume ya Vyama watatakiwa kuwa na sifa zozote za kitaaluma zinazotakiwa ili kuwawezesha kufanya kazi ya kitaalamu kama inavyopendekezwa na
Muswada Mpya.

Pili, baada ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Vyama, inapendekezwa kwamba wajumbe walioteuliwa kwa mashauriano na makubaliano kama tunavyopendekeza watatakiwa wathibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pendekezo hili litahakikisha kwamba wajumbe wa Tume wanakuwa vetted na chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi. Hili litajenga kuaminiana baina ya Serikali, vyama vya siasa, mashirika ya kijamii, taasisi za kitaaluma na za kidini na litaipa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uhalali mkubwa wa kisiasa, kitu ambacho ni muhimu katika mazingira ya sasa ya kisiasa.

Mheshimiwa Spika,
Tofauti pekee na muhimu kati ya pendekezo la Muswada Mpya na pendekezo letu kuhusu mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume ni locus ya uwajibikaji wao. Wajumbe wanaoteuliwa na Rais wanakuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha Rais au chama chake. Wajumbe wanaotokana na mapendekezo na makubaliano ya wadau wengi na wanaothibitishwa na chombo cha uwakilishi cha wananchi kama tunavyopendekeza hawawezi kuwa na shinikizo la kutoa matokeo yatakayompendezesha mmojawapo wa wadau hao. Faida kubwa na ya wazi ya Tume ya Vyama ni kwamba matokeo ya kazi yake yana nafasi kubwa zaidi ya kukubaliwa, kuheshimiwa na kutekelezwa na wadau mbali mbali kuliko matokeo ya kazi ya Tume ya Rais. Kwa lugha nyingine, kazi ya Tume ya Vyama itakuwa na uhalali wa kisiasa (political legitimacy) mkubwa zaidi kuliko Tume ya Rais.
Pendekezo hili linawahusu Katibu, watendaji na watumishi wengine wa Tume vile vile. Kutokana na uzoefu uliotokana na historia yetu na mfumo wetu wa kiutawala na kikatiba, watumishi wa serikali wamekuwa hawana uhuru wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia utashi wao na uadilifu wa kitaaluma bali hufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya mabosi wao wa kisiasa. Hii ni kwa sababu, kisheria na hata kivitendo, watendaji na watumishi karibu wote wa umma hujiona wanawajibika kwa mamlaka zao za uteuzi, yaani Rais na/au Waziri. Aidha, watendaji na watumishi hawa wanawajibika kinidhamu kwa mamlaka zinazoongozwa na watendaji wa Serikali ambao nao ni wateuliwa wa Rais na kwa hiyo wanakuwa na woga wa kufanya maamuzi yanayoweza kuhatarisha maslahi ya kisiasa ya Rais na chama tawala.

Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa watendaji na watumishi wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wawe huru dhidi ya mashinikizo yoyote ya kisiasa kutoka kwa Rais na Serikali yake na chama chake. Ili Tume iwe na mamlaka na uhuru unaohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na ili isiingiliwe kweli na mtu au mamlaka yoyote kama inavyosema ibara ya 10 ya Muswada, inabidi mamlaka ya uteuzi yaondolewe katika mikono ya Rais na/au Waziri ambaye ni mdau mmojawapo tu wa wadau wengi wa mchakato wa Katiba Mpya. Na namna ya pili ya kuhakikisha uhuru huu unakuwepo ni kuweka utaratibu wa kuwapata watendaji na watumishi hawa nje kabisa ya utumishi wa serikali kwa kuweka masharti ya kuwataka waombe kazi, kufanyiwa usaili na kuteuliwa na jopo la wataalamu walio huru.

Mheshimiwa Spika,
Namna ya tatu ya kuhakikisha uhuru wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ni kuhakikisha wajumbe wake wanapatiwa ulinzi wa ajira zao (security of tenure) sawa na wanaopatiwa majaji wa Mahakama ya Tanzania ili kuzuia uwezekano wa wajumbe kuondolewa kwa sababu zisizotokana na utendaji wao wa kitaaluma au ukosefu wa maadili. Kwa maana hiyo, mapendekezo ya ibara ya 10 Muswada Mpya juu ya uhuru wa Tume hayatoshelezi hata kidogo. Hii ni kwa sababu ibara ya 12 ya Muswada Mpya, ambayo inazungumzia ukomo wa ujumbe wa Tume, haijaweka utaratibu wowote wa namna ya kushughulikia nidhamu ya wajumbe pale kunapokuwepo tuhuma za ukiukaji wa Kanuni za Maadili zinazopendekezwa katika ibara ya 12(2) na Jedwali la Pili la Muswada. Kutokuweka utaratibu huu kuna hatari kubwa kwani, kisheria, mamlaka ya uteuzi huwa ndio mamlaka ya nidhamu pale ambapo sheria haijaweka utaratibu tofauti wa nidhamu. Hii ina maana kwamba bila kuweka utaratibu wa kisheria wa nidhamu ya wajumbe wa Tume, Rais ndiye atakuwa na uwezo wa kuwaondoa madarakani kwa sababu yeye ndiye aliyewateua!

Mheshimiwa Spika,
Pendekezo letu la tatu linahusu hadidu za rejea. Hapa kuna hoja za aina mbili. Kwanza, sambamba na pendekezo la kutompa Rais madaraka ya uteuzi wa wajumbe wa Tume, Rais asipewe mamlaka ya kutoa hadidu za rejea kwa Tume. Pili, kwa vile – kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya – hadidu za rejea ni hati ya kisheria inayotakiwa kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu yake, ni muhimu hati hii iwekwe wazi katika sheria yenyewe badala ya kubakia kuwa siri ya Rais. Watanzania lazima wajue Tume inapewa majukumu gani ya kisheria. Aidha, wajumbe wa Tume wenyewe lazima wafahamu wanapewa majukumu gani ya kisheria na wafahamu kwamba wanatakiwa kufuata matakwa ya sheria na sio maelekezo ya mtu mmoja hata kama ni Rais wa Kifalme. Hii itasaidia uwajibikaji wa Tume kwa wananchi kwani itakuwa rahisi kupima matokeo ya kazi ya Tume kwa hadidu za rejea zilizowekwa wazi katika sheria.
Ukweli ni kwamba badala ya kumsubiri Rais kutoa hadidu za rejea, tayari ibara za 9 na 16 za Muswada Mpya zimeshafanya hivyo kwa kuainisha kazi za Tume, mipaka ya Tume katika utekelezaji wa kazi hizo na utaratibu wa namna ya kuzifanya. Kwa ajili hiyo, zaidi ya kutaka kuonyesha kwamba Rais ana mamlaka makubwa katika mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya, mapendekezo ya ibara ya 8 hayana maana wala sababu yoyote na yanaweza kuondolewa bila kuathiri maudhui ya Muswada. Aidha, kwa kuzingatia mapendekezo ya ibara ya 9, haijulikani Rais atatoa maelekezo gani ya ziada yanayohusu kazi za Tume na namna ya kuzitekeleza. Kwa upande mwingine, mapendekezo ya ibara ya 8 yanaweza kuleta mkanganyiko na mgogoro wa kisiasa na kisheria usiokuwa wa lazima endapo Rais atatoa hadidu za rejea zinazotofautiana na matakwa ya kisheria kama yanavyopendekezwa na ibara 9 ya Muswada Mpya. Pendekezo letu, kwa hiyo, ni kwamba ibara ya 8 ifutwe yote na ibara za 9 na 16 zifafanuliwe vizuri ili kuweka wazi zaidi hadidu za rejea za Tume na namna ya kuzitekeleza.

Mheshimiwa Spika,
Kuna mapendekezo mengine yaliyoko kwenye Muswada yanayoonyesha hatari za Urais wa Kifalme. Kama tulivyoona, Tume inatakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kwa Rais wa Zanzibar. Baada ya hapo, kwa mujibu wa ibara ya 18(2) ya Muswada, “baada ya mashauriano na makubaliano na Rais wa Zanzibar na baada ya kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera, Rais atamwelekeza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba kwa ajili ya kupitishwa kwa vifungu vya Katiba.”

Pendekezo hili ni la hatari kubwa. Kwanza, ‘kumalizika kwa taratibu za ndani zinazohusu utungaji wa sera’ maana yake ni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kawaida wa kiserikali unaohusu utungaji sera na sheria. Chini ya utaratibu huu, rasimu ya muswada hupelekwa kwanza kwenye Kamati ya Watalaam ya Baraza la Mawaziri (Inter Ministerial Technical Committee of the Cabinet) kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho na Makatibu Wakuu kabla ya kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa maamuzi ya mwisho. Baada ya maamuzi ya mwisho ya Baraza la Mawaziri, rasimu ya muswada hurudishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuandikwa upya ndipo upelekwe Bungeni la Katiba.

Katika hatua zote hizi, muswada wa sheria huweza kufanyiwa marekebisho makubwa. Kwa maana hiyo, pendekezo la kuuwasilisha Muswada wa Katiba Mpya katika Bunge la Katiba baada ya kuupitisha kwanza kwa Makatibu Wakuu ambao wote ni wateuliwa wa Rais, na kwenye Baraza la Mawaziri ambalo wajumbe wake wote (ukiacha Makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar) ni wateuliwa wa Rais ni kutengeneza mazingira ya kisheria yatakayoruhusu uchakachuaji wa Muswada huo kwa lengo la kuhakikisha matokeo yake ya mwisho, yaani Katiba Mpya, yanakidhi maslahi ya Rais na chama chake cha CCM. Kwa vyovyote vile, pendekezo hili halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

SIFA ZA WAJUMBE

Mheshimiwa Spika,
Muswada Mpya unapendekeza sifa zifuatazo wanazotakiwa kuwa nazo wajumbe wa Tume:
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii;
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(c) Maslahi ya umma;
(d) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbali mbali ya kijamii; na
(e) Vigezo vingine ambavyo Rais ataona vinafaa. (ibara ya 6(3)
Zaidi ya sifa zilizotajwa, ibara ya 6(4) inakataza watu wenye sifa zifuatazo kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume:
(a) Wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, madiwani na viongozi wa vyama vya siasa wa ngazi zote kuanzia Wilaya hadi Taifa;
(b) Watumishi wa vyombo vya usalama;
(c) Watu waliowahi kuhukumiwa kwa kutenda kosa au wanaotuhumiwa mahakamani kwa mashtaka ya kukosa uaminifu au uadilifu;
(d) Watu wasiokuwa raia wa Tanzania.

Mapendekezo haya yana athari kubwa kwa mchakato mzima wa upatikanaji wa Katiba Mpya. Kwanza, kwa kukataza viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa kuteuliwa wajumbe wa Tume kunaondoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya kundi kubwa la watu wenye utaalamu na uzoefu katika masuala mbali mbali ya kisiasa, kikatiba, kisheria, kiuchumi, kiutawala, kifedha na kisayansi jamii. Vile vile, viongozi wa vyama vya siasa wanawakilisha makundi makubwa ya kijamii yenye mtawanyiko wa watu na wa kijiografia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wanawakilisha watu wa umri na jinsia zote kama inavyopendekezwa katika Muswada Mpya.

Aidha, kwa kuwa maneno ‘maslahi ya umma’ hayajafafanuliwa katika Muswada, hakuna anayeweza kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu na za kati wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa kisheria baada ya kutimiza masharti yote husika ya kisheria, na ambao wanaungwa mkono na mamilioni ya wananchi wa Tanzania kwa kupewa nafasi za uwakilishi katika taasisi za uwakilishi za umma kama Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri za Serikali za Mitaa hawajui wala hawazingatii maslahi ya umma na kwa hiyo hawafai kuwakilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba! Kama ingekuwa hivyo, Rais – ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na kwa hiyo kiongozi wa chama cha siasa – naye pia atakuwa hana sifa za kuteua Tume! Na wakati haja ya kutoshirikisha watumishi wa taasisi za ulinzi na usalama katika mchakato wenye ubishani wa kisiasa kama utungaji wa Katiba Mpya inaeleweka, ni matusi kwa watu waliochaguliwa na wananchi kuwa Wabunge, Wawakilishi au Madiwani au viongozi wa vyama vya siasa vilivyowapendekeza watu hao, kuwekwa pamoja na wahalifu na kutamkwa kuwa hawana sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba!

Inaelekea lengo kuu la pendekezo hili ni kuhakikisha kwamba vyama vya upinzani, hasa hasa CHADEMA, vyenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Bunge havipati fursa ya kuamua muundo na maudhui ya Katiba Mpya hasa katika hatua muhimu za uundaji wake. Pili, lengo kuu vile vile ni kuhakikisha kuwa Rais, na kwa hiyo chama chake cha CCM, wanadhibiti mchakato wa Katiba Mpya katika hatua muhimu ya uundaji wake. Endapo watafanikiwa katika hili, Rais na chama chake cha CCM watakuwa na nafasi kubwa ya kuamua aina ya Katiba Mpya itakayotokana na mchakato walioudhibiti kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya. Hii ni kwa sababu, kwa kutumia uzoefu wa Tume nyingine zilizopata kuteuliwa miaka ya nyuma, wajumbe wengi huwa ni watumishi au waliopata kuwa watumishi wa Serikali na/au taasisi zake. Wajumbe wa aina hii wamekuwa hawana uthubutu wa kupendekeza mabadiliko makubwa yanayohitajika katika mfumo wa utawala wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Badala ya kukataza viongozi wa vyama vya siasa kama inavyopendekezwa na Muswada Mpya, na kwa kuzingatia nafasi ya vyama vya siasa katika historia yetu na mfumo wetu wa utawala, na kwa lengo la kuhakikisha Tume inakuwa na utaalamu, uzoefu na uhalali wa kisiasa unaohitajika, watu wanaostahili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume wawe ni wale wenye sifa zinazopendekezwa na ibara ya 6(3)(a), (b), (c) na (d) ya Muswada. Kwa sababu hiyo, hakutakiwi kuwa na vigezo vingine visivyojulikana wazi kwa wananchi. Kwa maneno mengine, pendekezo la kuwa na ‘vigezo vingine ambavyo Rais ataona inafaa’ halikubaliki kwani linampa Rais mwanya wa kuteua marafiki zake au watu ambao hawana sifa zinazojulikana. Kwa maoni yetu vile vile, badala ya kuwa sababu ya disqualification, uongozi wa kuchaguliwa na wananchi katika taasisi za uwakilishi au katika vyama vya siasa unatakiwa kuwa an added advantage pale ambapo kiongozi husika ana sifa za kitaaluma zinazotakiwa!

MISINGI MIKUU YA KITAIFA

Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuwepo kwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ambayo Tume inatakiwa kuizingatia kwa lengo la kuihifadhi na kuidumisha. Misingi mikuu inayopendekezwa ni:
(a) Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano;
(b) Uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama;
(c) Mfumo wa kiutawala wa kijamhuri;
(d) Umoja wa kitaifa, amani na utulivu;
(e) Uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote kupiga kura;
(f) Ukuzaji na na uhifadhi wa haki za binadamu;
(g) Utu, usawa mbele ya Sheria na mwenendo wa sheria; na
(h) Uhuru wa kuabudu na uvumilivu wa dini nyingine. (ibara ya 9(2)
Kifungu hiki kimefanyiwa mabadiliko kwa kufuta maneno ‘Tume itahakikisha ... kutokugusika na utakatifu (inviolability and sanctity) wa mambo yafuatayo’ yaliyokuwa katika Muswada wa Zamani, na badala yake yamewekwa maneno mapya ‘... kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo....’ Mabadiliko haya yamefanywa ili kujaribu kuondoa hofu iliyojitokeza wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kwamba lengo la pendekezo hilo lilikuwa kuzuia mjadala juu ya masuala ya kikatiba yenye utata mkubwa kama vile suala la Muungano. Hata hivyo, hatari ya kuzuiliwa kwa mjadala juu ya misingi mikuu ya kitaifa bado haijaondolewa kwani, kwa mujibu wa ibara mpya ya 9(3), “... Tume itatoa fursa kwa watu kutoa maoni yao kwa uhuru kwa lengo la kuendeleza na kuboresha masuala hayo.” Tafsiri halisi ya maneno haya ni kwamba mjadala pekee utakaoruhusiwa juu ya ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni ule ambao lengo lake ni ‘kuendeleza na kuboresha masuala hayo.’

Kwa maoni yetu, lengo kuu la pendekezo linalohusu kuendeleza na kuboresha ‘misingi mikuu ya kitaifa’ ni kuzuia mjadala wenye kuhoji ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ ili kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wenye Serikali mbili. Hii ni kwa sababu katika mambo yote yanayopendekezwa kuwa misingi mikuu ya kitaifa, ni ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano’ yenye Serikali mbili ndio ambayo imekuwa na mgogoro mkubwa kwa muda wote wa maisha ya Jamhuri ya Muungano. Ukiacha ‘ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu’ ambalo lilikataliwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere kwa miaka yote ya utawala wake, mambo mengine yote yanayotajwa kuwa ‘misingi mikuu ya kitaifa’ hayajawahi kubishaniwa kwa miaka yote ya uhai wa Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la ‘misingi mikuu ya kitaifa’ linastaajabisha sana kwani, kwa mujibu wa ibara ya 98(1)(b) ya Katiba ya sasa, ‘kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Kamhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar, Orodha ya Mambo ya Muungano na idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar’ ni mambo yanayoweza kubadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ili mradi tu mabadiliko hayo yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa kutoka Tanzania Bara na wa Tanzania Zanzibar. Kwa sababu hiyo, pendekezo la ibara ya 9(3) ya Muswada kwamba ‘misingi mikuu ya kitaifa’ izungumzwe kwa lengo la kuiendeleza na kuidumisha tu halikubaliki kwa sababu linazuia uhuru wa kuhoji na/au kupinga mambo ambayo kwa Katiba ya sasa ni ruhusa kuyahoji, kuyapinga na/au hata kuyabadilisha! Tunapendekeza ibara ya 9(2) na (3) za Muswada zifutwe kabisa ili kuwepo na uhuru kamili wa kujadili, kwa kupinga au kuunga mkono, kila jambo linalohusika na Katiba Mpya.

NAFASI YA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika,
Pengine mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika Muswada ni mapendekezo yanayohusu nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Itakumbukwa kwamba moja ya masuala yaliyozua tafrani kubwa katika mchakato wa kukusanya maoni juu ya Muswada wa Zamani hasa katika kituo cha Zanzibar ni kuwepo hisia kwamba nafasi ya Zanzibar ilikuwa imepuuzwa katika Muswada huo. Muswada sio tu kwamba umetekeleza matakwa yote ya ushirikishwaji wa Zanzibar, bali umekwenda mbali zaidi kwa kuifanya Zanzibar mwamuzi wa mustakbala wote wa kikatiba wa Tanzania. Hii imefanyika kwa njia mbili: kwanza, kwa kumfanya Rais wa Zanzibar kuwa mshirika sawa wa kikatiba wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; na pili, kwa kuipa Zanzibar nafasi kubwa ya uwakilishi katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.

NAFASI YA RAIS WA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kwamba utekelezaji wa mamlaka yote ya Rais, Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano lazima ufanyike kwa ‘mashauriano na makubaliano’ na Rais, Waziri au Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kwa mfano, ibara ya 5 inayohusu kuundwa kwa Tume inamtaka Rais ‘kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar na kupata ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Vile vile, ibara ya 6(1) inayohusu uteuzi wa wajumbe wa Tume; ibara ya 8(1) na (2) inayohusu hadidu za rejea na kuongeza muda wa Tume; na ibara ya 13(2) inayohusu uteuzi wa Katibu wa Tume, zote zinataka kuwepo na makubaliano na Rais wa Zanzibar. Aidha, ibara ya 13(5) inayohusu uteuzi wa watendaji wengine wa Tume inalazimu makubaliano kati ya Waziri na Waziri mwenzake wa Zanzibar ambao nao ni wateuliwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar.
Mamlaka ya Rais wa Zanzibar hayaishii tu kwenye uteuzi wa wajumbe na watendaji wa Tume, bali pia yanaingia hata katika uwasilishaji wa ripoti ya Tume. Kwa mujibu wa ibara 18(1) ya Muswada, mara baada ya kumaliza kazi yake, Tume itawasilisha ripoti yake kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 18(2), mara baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais, ‘baada ya kushauriana na kukubaliana’ na Rais wa Zanzibar, “... atamuagiza Waziri kuwasilisha Muswada wa Katiba katika Bunge la Katiba.” Kwa mapendekezo haya pia, Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato wa Katiba Mpya. Maana yake ni kwamba Rais wa Zanzibar asipopatiwa nakala ya ripoti ya Tume au asipokubaliana na Rais wa Muungano, basi Muswada wa Katiba hautawasilishwa kwenye Bunge la Katiba!

Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanaashiria kuwepo kwa mtazamo ambao chanzo chake ni Makubaliano ya Muungano kati ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ya tarehe 25 Aprili 1964. Kwa mtazamo huo, Zanzibar ni nchi huru kama ilivyokuwa mwaka 1964 na kwa hiyo ni lazima sio tu ishirikishwe kwa usawa, bali pia lazima ikubaliane na mabadiliko yoyote ya kikatiba yanayopendekezwa na Muswada. Kama Profesa Palamagamba Kabudi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alivyosema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika tarehe 12 Novemba 2011: ‘Katika kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mtazamo huu sio sahihi. Kwanza kabisa, Zanzibar sio nchi huru tena kama ilivyokuwa mwaka 1964, kama ambavyo hakuna tena nchi inayoitwa Tanganyika wala serikali yake. Hii ni kwa sababu tangu kusainiwa kwa Hati za Muungano mwaka 1964, na kwa mujibu wa ibara ya 4(3) ya Katiba ya sasa, masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo pia imekasimiwa mamlaka juu ya masuala ya iliyokuwa Tanganyika. Masuala haya ya Muungano hayawezi kujadiliwa upya na kwa usawa kati ya nchi hizi mbili kwa vile moja kati ya nchi hizo haipo tena na iliyobaki imepoteza sehemu ya uhuru wake kutokana na Muungano huo! Hii ndio kusema hakuwezi tena kuwa na wabia wa Muungano bila kwanza kuirudisha Tanganyika kama nchi na bila kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yenye uhuru na mamlaka kama iliyokuwa nayo kabla ya Muungano!

Pili, kuna dhana kwamba Rais wa Zanzibar hakushirikishwa katika mchakato wa maandalizi ya Muswada wa Zamani. Dhana hii vile vile ni potofu. Kwanza, Rais Ali Mohamed Shein mwenyewe ametamka wazi kwa waandishi wa habari kwamba alishiriki katika hatua zote za maamuzi kwenye Baraza la Mapinduzi. Pili, mujibu wa ibara ya 54(1) ya Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar ni mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kwa hiyo ni mshiriki wa maamuzi yote ya Serikali hiyo. Kwa maana hiyo, maslahi ya Zanzibar yanawakilishwa ndani ya ‘chombo kikuu cha kumshauri Rais’ katika Jamhuri ya Muungano. (ibara ya 54(3) Hii ni licha ya ukweli kwamba, kwa mlolongo wa madaraka uliopo katika ibara ya 54(2), Rais wa Zanzibar sio mmoja wa wajumbe wanaoweza kuongoza mikutano ya Baraza hilo.

Aidha, ndani ya Baraza la Mawaziri, Zanzibar inawakilishwa pia na Makamu wa Rais ambaye – kwa mujibu wa ibara ya 47(1) ya Katiba ya sasa – “... ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano....” Kwa maana hiyo, mapendekezo ya Muswada yanayomfanya Rais wa Zanzibar kuwa sio tu mshiriki sawa lakini pia mwamuzi wa mustakbala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanaenda kinyume sio tu na Katiba ya sasa bali pia na Hati za Muungano wenyewe. Kwa mapendekezo haya, endapo Rais wa Zanzibar hatakubaliana na uteuzi wowote wa wajumbe wa Tume au Katibu wake au watendaji wake wengine, anaweza kusimamisha mchakato mzima wa kikatiba hata kama unahusu masuala ya Tanzania Bara yasiyo ya Muungano!

UWAKILISHI WA ZANZIBAR

Mheshimiwa Spika,
Ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake. Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vya maamuzi vinavyopendekezwa na Muswada. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya 6(2), “... muundo wa Tume utazingatia msingi wa kuwepo kwa uwakilishi ulio sawa kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano.” Hii ina maana kwamba wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake wanatakiwa wawe sawa kwa sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Ikumbukwe kwamba Tume hii inatengeneza Katiba inayohusu masuala ya Muungano, ambayo ni haki kwa Zanzibar kushirikishwa kwa usawa kabisa, na vile vile masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo Zanzibar haina haki ya kushiriki.

BUNGE LA KATIBA

Mheshimiwa Spika,
Eneo la pili ambalo Zanzibar ina ushawishi mkubwa kutokana na uwakilishi wake ni katika Bunge la Katiba linalopendekezwa katika Sehemu ya Tano ya Muswada. Kwa mujibu wa ibara ya 20(2), wajumbe wa Bunge la Katiba watakuwa ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano; wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar; mawaziri wa katiba na sheria wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; Wanasheria Wakuu wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar; na wajumbe mia moja kumi na sita wakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za kiserikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii. Inaelekea kwamba, kwa mujibu wa ibara ya 20(4), wajumbe wasiokuwa wabunge ama wawakilishi nao pia watateuliwa na Rais licha ya kutoka nje ya mfumo wa kiserikali!

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(a) ya Katiba ya sasa ya Muungano, wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni pamoja na wabunge wa majimbo ya uchaguzi. Kwa composition ya sasa ya Bunge, kuna jumla ya majimbo ya uchaguzi 239 ambayo kati yao majimbo ya Zanzibar ni hamsini. Vile vile, kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(c) ya Katiba, Baraza la Wawakilishi Zanzibar linawakilishwa na wabunge watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, kama inavyotakiwa na ibara ya 66(1)(b), kuna wabunge wanawake mia moja na mbili wanaojulikana kama ‘wabunge wa viti maalum.’ Kwa mgawanyo wa sasa wa wabunge hawa, idadi ya wanaotoka Zanzibar ni ishirini na tano kwa vyama vyote vyenye uwakilishi bungeni. Na mwisho, kuna wabunge wasiozidi 10 wanaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 66(1)(e). Hadi sasa, Rais ameshateua wabunge watatu ambao wote ni wa kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, katika Bunge la sasa lenye wabunge 353, wabunge wanaowakilisha Zanzibar ni themanini na tatu au karibu 23.5% ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Kwa mujibu wa Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Tano ya Katiba ya Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na wawakilishi wa majimbo hamsini ya uchaguzi, wawakilishi kumi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar na wawakilishi ishirini wa viti maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa hiyo, jumla ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa sasa ni themanini na moja. Kwa maana nyingine ni kwamba endapo mapendekezo ya ibara ya 20(1)(b), (c) na (d) ya Muswada yatakubaliwa, idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Zanzibar itaongezeka hadi kufikia mia moja sitini na nne kati ya wajumbe 545 wa Baraza hilo kwa mujibu wa ibara ya 20(2). Idadi hii ni sawa na 30% ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.
Idadi hiyo ya uwakilishi wa Zanzibar bado haitakidhi matakwa ya Muswada kwani ibara ya 20(3) inapendekeza kwamba “... idadi ya wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Tanzania Zanzibar ... haitapungua theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba”! Theluthi moja ya wajumbe wa Bunge la Katiba ni wajumbe 182. Kwa hiyo ili kukidhi matakwa ya Muswada kuhusu uwakilishi wa Zanzibar, itabidi wajumbe 18 kati ya 116 waliotajwa na ibara ya 20(2)(e) watoke Zanzibar ili kufikisha idadi ya wajumbe 182 ambayo ndio theluthi moja ya wajumbe wote wa Bunge la Katiba.

Mheshimiwa Spika,
Kuna maeneo mengine ya Muswada ambayo pia yanazua maswali mengi juu ya nafasi ya Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya. Kwa mfano, wakati ibara ya 21(1) inapendekeza kwamba Spika na Naibu Spika wa Bunge la Katiba wachaguliwe kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo, ibara ya 21(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano basi Naibu wake lazima atoke upande mwingine. Sambamba na pendekezo hili, ibara ya 22(1) inapendekeza Makatibu wa sasa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar watakuwa ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bunge la Katiba. Aidha, sawa na ibara ya 21(2), ibara ya 22(2) inapendekeza kwamba endapo Spika atatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi Katibu wa Bunge la Katiba lazima atoke upande mwingine.

Mapendekezo haya yanaonyesha sio tu nafasi na ushawishi mkubwa wa Zanzibar katika mchakato wa Katiba Mpya, bali pia ni mwendelezo wa dhana potofu kwamba Zanzibar ni mshirika sawa wa Jamhuri ya Muungano. Hii inathibitishwa pia na pendekezo la ibara ya 24(3) ya Muswada inayotaka Katiba Mpya ikubaliwe na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotoka Tanzania Bara na vile vile theluthi mbili ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba iwe ni kwa masuala ya Muungano yanayoihusu Zanzibar pia, au kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara ambayo hayaihusu, Zanzibar itakuwa na kura ya turufu kwa mujibu wa mapendekezo ya Muswada huu.

Mheshimiwa Spika,
Uwakilishi mkubwa wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano umetumika kihistoria kwa lengo la kuwatuliza Wazanzibari wakati Serikali ya Mwalimu Nyerere ilipokuwa inamomonyoa uhuru wa Zanzibar kwa kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano kwenye Katiba ya Muungano. Katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union, Profesa Issa Shivji, mwanazuoni mashuhuri wa kikatiba na mwanafunzi wa historia ya Muungano huu amemnukuu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati wa utawala wa hayati Sheikh Abedi Amani Karume, Bw. Wolfgang Dourado akimnukuu Sheikh Karume juu ya nafasi ya Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano: “‘Msiwe na wasi wasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwakilishwa katika Baraza letu la Mapinduzi’”!
Mheshimiwa Spika, Sababu nyingine inatokana na kuongezeka kwa ushawishi na nafasi ya Zanzibar katika siasa za ndani ya CCM, hasa hasa katika zama hizi za vyama vingi na vita za makundi mbali mbali ndani ya chama hicho. Katika mazingira haya, mtu yeyote anayetaka kupitishwa kuwa mgombea urais kwa kupitia CCM anakuwa anahitaji kura za CCM Zanzibar ili kushinda katika kinyang’anyiro hicho. Kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwenyewe katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, “sababu moja kubwa iliyofanya viongozi wetu wasitake kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ... ni umuhimu wa kura za Zanzibar katika kumteua mwanachama wa CCM kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano. Kwa kiongozi yeyote anayeliona jambo hilo kuwa ni muhimu kupita mengine yote, kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ni dhambi ambayo haina budi iepukwe kwa kila njia.” Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, hofu hii ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba upendeleo wa Zanzibar unaopendekezwa katika Muswada huu kuhusiana na uwakilishi katika Bunge la Katiba na katika vyombo vingine vya maamuzi juu ya mchakato wa Katiba Mpya sio wa haki na haukubaliki tena. Kwanza, ibara ya 64(2) ya Katiba ya sasa inaweka wazi kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina mamlaka ya kutunga sheria katika Zanzibar ‘... juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano....’ Hii pia ndio lugha ya ibara ya 78(1) ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka jana. ‘Katiba ya Tanzania’ ni jambo la kwanza katika orodha ya Mambo ya Muungano iliyoko kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa Muswada Mpya kupendekeza kwamba Baraza la Wawakilishi Zanzibar liwe sehemu ya Bunge la Katiba ni kukiuka wazi wazi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ya Katiba ya Zanzibar. Ni ajabu iliyoje kwamba wale wanaojifanya ni machampioni wa Muungano wanaweza kunyamazia ukiukaji huu wa Katiba!
Mheshimiwa Spika, Thomas Paine, mwandishi maarufu wa Marekani ya wakati wa Mapinduzi ya mwaka 1776, aliwahi kuandika kijitabu alichokiita Common Sense juu ya uhalali wa Uingereza kutawala Bara la Amerika ya Kaskazini ambako alisema: ‘... [T]here is something very absurd in supposing a continent to be perpetually governed by an island [for] in no instance hath nature made the satellite larger than its primary planet...’! Yaani, ni ujinga kudhani kwamba bara linaweza kutawaliwa milele na kisiwa kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya kitegemezi kuwa kikubwa kuliko sayari yake ya msingi. Hata kama ni kweli kwamba Tanganyika sio bara kama ilivyokuwa Marekani ya Kaskazini, bado tunakubaliana na Tom Paine kwamba ni ujinga kudhani kwamba Visiwa vya Zanzibar vitaendelea kuwa na maamuzi na ushawishi mkubwa katika masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika kwa sababu utaratibu wa asili haujawahi kufanya maslahi ya Visiwa hivyo kuwa bora zaidi ya maslahi ya Tanganyika!
Kwa maoni yetu, wakati umefika kwa Muungano kuwekwa kwenye msingi wa usawa na imara zaidi. Msingi huo unahitaji kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika ambayo ndio ilikuwa – pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – mbia mkuu wa Muungano wa mwaka 1964. Kurudishwa huko kwa Tanganyika kutaiwezesha Zanzibar kujadiliana nayo kwa usawa juu ya masuala yote yanayohusu Muungano. Haya yote yanawezekana tu endapo Muungano huu utawekwa mbele ya wananchi ili waamue – kwa kura ya maoni - kama wanataka kuendelea nao au la; na kama wanataka kuendelea nao ni muundo gani wa Muungano wanaoutaka.

Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya kurudishwa kwa Tanganyika na Serikali yake sio mapya. Miaka ishirini iliyopita, Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) ilipendekeza hivyo hivyo. Miaka saba baadae, Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper Na. 1 ya 1998 (Tume ya Kisanga) nayo ilipendekeza hivyo hivyo. Kuendelea kupuuza mapendekezo haya wakati Zanzibar inavunja Katiba ya sasa ya Muungano; kuendelea kukaa kimya kwa hofu ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’ wakati wao wanajitwalia uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe huku wakiendelea kushiriki katika maamuzi ya mambo ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano; kuendeleza kile alichokiita Mwalimu Nyerere falsafa ya ‘changu ni changu, chako ni chetu’ katika mahusiano ya Zanzibar na Tanzania Bara, ni kutulazimisha tuipinge dhana nzima ya Muungano kati ya nchi zetu mbili kitu kinachoweza kupelekea kuvunjika kwa Muungano wenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni isingependa tufike huko lakini ndoa hii ya kulazimishana haiwezi ikadumu muda mrefu kwa taratibu za aina hii.

UDHOOFISHAJI WA UPINZANI

Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya Muswada juu ya uwakilishi katika Bunge la Katiba yana athari nyingine kubwa katika majadiliano na maamuzi ndani ya Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na Profesa Issa G. Shivji kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, endapo mapendekezo ya ibara ya 20(2) ya Muswada yatapitishwa, CCM itakuwa na kati ya wajumbe 350 hadi 400 katika Bunge la Katiba ambalo lina wajumbe 545. Kwa upande mwingine Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina Wawakilishi 29 katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitakuwa na wajumbe 65 katika Bunge la Katiba. Kwa maana ya uwakilishi katika Bunge la Katiba, CUF itakuwa ndio chama cha pili kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge hilo, licha ya kuwa na wabunge wawili tu wa kuchaguliwa kwa upande wa Tanzania Bara na licha ya kupata kura chache sana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Na kama inavyojulikana, tangu Muafaka wa Kisiasa Zanzibar kati ya CCM na CUF wa mwaka 2010 na kuzaliwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, upinzani wa kisiasa Zanzibar umekufa na kwa upande wa Tanzania Bara, na hasa Bungeni na kwenye chaguzi ndogo kama ule wa Igunga, CUF imekuwa ikishirikiana na CCM kuipinga CHADEMA. Kwa mapendekezo haya, kambi ya CCM na CUF katika Bunge la Katiba inaweza kufika hata zaidi ya wajumbe 465 katika ya wajumbe 545 wa Bunge hilo! CHADEMA ambayo kwa sasa ndio chama kinachoongoza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, itabakia na Wabunge wake 48 na vyama vya kibunge vilivyobaki, yaani NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vitabaki na jumla ya Wabunge sita. Kwa hiyo, CHADEMA itakuwa chama cha tatu kwa nguvu za kisiasa ndani ya Bunge la Katiba licha ya kuwa ni chama kikuu cha upinzani chenye nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini!

Kwa maana nyingine, iwe ni kwa makusudi au bila ya kujua au kwa kunuia, athari mojawapo kubwa ya mapendekezo ya Muswada kuhusu uwakilishi katika Bunge la Katiba itakuwa ni kuiongezea nguvu zaidi kambi ya CCM/CUF na kupunguza nguvu na ushawishi wa CHADEMA ambayo ndio chama pekee kinachobeba matarajio na matamanio ya Watanzania wengi wanaotaka mabadiliko ya kimsingi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Haihitaji kuwa na shahada ya uzamivu kujua kwamba Bunge la Katiba lenye uwakilishi wa aina hii litapitisha Katiba Mpya ambayo pengine itatofautiana na Katiba ya sasa kwa jina tu! Na wala haihitaji kisomo kikubwa kujua kwamba Bunge la Katiba la aina hii halitagusa ‘msingi mkuu’ uliobaki wa Jamhuri ya Muungano, yaani Serikali mbili. Hapa pia ni wazi kuwa lengo halisi la mapendekezo haya ni kuhakikisha kwamba mchakato wa Katiba Mpya utazaa matunda yasiyokuwa tofauti sana na ya Katiba ya sasa!

‘UWAKILISHI’ WA BUNGE LA KATIBA

Mheshimiwa Spika,
Sio Bunge hili tukufu la Jamhuri ya Muungano wala Baraza la Wawakilishi Zanzibar lenye mamlaka kikatiba na kisiasa ya kutunga Katiba Mpya ya Tanzania. Hii ni kwa sababu sisi wote tulioko humu ndani tulichaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa na mamlaka yetu yote yako ndani ya kona nne za Katiba hiyo. Kama ni kweli, kama anavyodai Profesa Kabudi, kwamba kitendo cha kutunga Katiba Mpya vile vile ni kitendo cha kuua Katiba ya Zamani, basi sisi Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar hatuna mamlaka ya kuiua Katiba ya sasa kwa sababu sisi wote tulikula kiapo cha kuilinda, kuihifandhi na kuitetea.

Pili, sisi sote ni Wabunge na Wawakilishi wa vyama vya siasa kwa sababu, kwa mujibu wa Katiba ya sasa sheria zote husika, tumechaguliwa kwa sifa kuu ya kuwa wanachama wa, na tuliopendekezwa na, vyama vya siasa. Kuligeuza Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Bunge la Katiba ni sawa na kusema kwamba wasiokuwa wanachama wa vyama vya siasa hawana haki ya kushiriki katika kutunga Katiba Mpya kwa sababu ya kuwa na kilema cha kisheria kinachowakataza kuchaguliwa kuwa Wabunge na Wawakilishi! Ibara ya 20(4) ya Katiba ya sasa inatamka wazi kwamba “... ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote....” Sio kosa, kwa hiyo, kwa mamilioni ya Watanzania ambao wameamua kwa hiari zao kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikubaliani, na haiwezi kukubali, ubaguzi wa aina hii dhidi ya Watanzania walioamua kutumia haki zao za kikatiba ya kutokujiunga na chama chochote cha siasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitakubali Watanzania hao waadhibiwe kwa kunyimwa kushiriki katika Bunge la Katiba kwa sababu tu ya kutokuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Tatu, wajumbe 116 wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais. Pili, Bunge la Katiba ni chombo cha uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi na kwa mila na desturi zinazokubalika na kutumika kimataifa, wajumbe wa Bunge la Katiba huchaguliwa moja kwa moja na wananchi bila ya kujali vyama vya siasa na huwa na kazi moja tu: kutunga Katiba Mpya. Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wajumbe wa Bunge la Katiba wachaguliwe moja kwa moja na wananchi na kusiwe na masharti yoyote kuhusu uanachama wa vyama vya siasa.

UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA

Mheshimiwa Spika,
Muswada una mapendekezo ambayo yanaashiria kuachana na utaratibu wa kihistoria wa utungaji wa Katiba ambao umewaweka wananchi kando katika michakato wa kikatiba tangu miaka ya mwanzo ya uhuru. Kwa mujibu wa ibara ya 27(1), kutakuwa na kura ya maoni kwa lengo la kuihalalisha Katiba Mpya. Kwa mujibu wa ibara ya 30, watu wote walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, watakuwa na haki ya kupiga kura katika kura hiyo ya maoni. Aidha, kufuatana na ibara ya 32(2), matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa zaidi ya 50% ya kura zote zilizopigwa Tanzania Bara na kiasi hicho hicho kwa Zanzibar.

Mapendekezo ya ushirikishwaji wa wananchi katika kuipa Katiba uhai wa kisheria ni jambo la maana sana na linaonyesha kuwa tumeanza kuachana na urithi wa kikatiba wa kikoloni ulioanza na Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961. Hata hivyo, mapendekezo haya yamejaa mitego na vichaka vingi vya hatari. Kwanza, ibara ya 27 inapendekeza kwamba kura ya maoni itaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili – kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni. (ibara ya 28(1) na (2) Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 31, utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia kauli yake ndani ya Bunge hili wakati wa kujadili Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria tarehe 24 Agosti, 2011: “Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haina imani, sio tu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bali pia na mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi unaoendesha chaguzi za nchi yetu. Mfumo huu na watendaji wake wameonyesha wazi kutokuwa huru na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi kuchakachua matokeo ya chaguzi mbali mbali hapa nchini. Kwa maana hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, na ile ya Zanzibar, haiwezi kuachiwa jukumu kubwa la kuendesha kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Serikali ilete bungeni muswada wa mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba na ya sheria husika za uchaguzi kwa lengo la kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha inasimamia zoezi la kura ya maoni kwa uhuru na bila upendeleo kwa chama tawala.”

Kuna maeneo mengine ambayo nayo yanaonyesha kwamba lengo halisi la Muswada huu ni kupata Katiba ambayo haitabadilisha mambo ya msingi ila itakuwa mpya kwa jina tu. Kwanza, ibara ya 26(2) inapendekeza kumpa Rais mamlaka ya “kuliitisha tena Bunge la Katiba lenye wajumbe wale wale siku zijazo kwa ajili ya kutunga masharti ya katiba kabla ya kuizindua Katiba inayopendekezwa kwa lengo la kurekebisha masharti yaliyomo kwenye Katiba iliyopendekezwa.” Maana halisi ya maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.

Pili, wakati ibara ya 32(3) inapendekeza kurudiwa kwa kura ya maoni endapo kura za ‘NDIYO’ na ‘HAPANA’ zitalingana, ibara ya 32(4) inaelekeza kwamba “endapo wingi wa kura ya maoni utakuwa ni ‘HAPANA’, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, itaendelea kutumika.” Endapo pendekezo hili litapitishwa na kuwa sheria, hii itakuwa ni kualika maasi kwa vile, kwa vyovyote vile, wananchi wa Tanzania – baada ya kupitia mchakato mrefu wa kutengeneza Katiba Mpya – hawatakubali tena kuvishwa minyororo ya Katiba ya sasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba badala ya kurudi kwenye status quo ante kama inavyopendekezwa, mchakato wa Katiba Mpya uanze tena hadi hapo utakapopatikana muafaka wa kitaifa wa katiba.

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 2011 ni Muswada muhimu kuliko pengine miswada yote ambayo Bunge la Kumi litapata fursa ya kuijadili na kuipitisha. Ni muswada wa kihistoria kwa vile, tangu uhuru wa Tanganyika miaka hamsini iliyopita, na tangu Muungano miaka karibu arobaini na nane iliyopita, Watanzania hatujawahi kupata fursa ya kujadili na kuamua mustakbala wa taifa letu kikatiba kwa utaratibu kama unaopendekezwa katika Muswada huu. Hata hivyo, kwa jinsi ambavyo Muswada huu ulivyoandaliwa na kwa maudhui yake na kwa jinsi ulivyoletwa Bungeni kwa kukiuka makusudi Kanuni za Bunge, ni wazi – kama utapitishwa jinsi ulivyo – Watanzania tutakuwa tumekosa fursa ya kuamua mustakbala wa taifa letu kwa njia ya amani na maridhiano. Bunge hili tukufu lina wajibu mbele ya historia na kwa vizazi vya sasa na vijavyo, kuhakikisha kwamba tunapata muafaka wa kitaifa juu ya Tanzania tunayoitaka. Hukumu ya historia, endapo Bunge hili tukufu litaendekeza ushabiki wa kisiasa na kufanya maamuzi ya mambo makubwa kama haya kwa kupiga kelele au kwa kuzomea au kwa kugonga meza kwa nguvu, itakuwa ni kali sana. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haiwezi kuwa sehemu ya maamuzi makubwa kama yanayopendekezwa na Muswada huu bila kwanza wananchi wa Tanzania na Wabunge wenyewe kupata muda wa kutosha wa kuyatafakari masuala haya yote kwa uzito unaoyastahili na kuyafanyia maamuzi ya busara.
Kwa sababu hizi zote, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja chini ya kanuni ya 86(3)(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hili tukufu kwamba Bunge hili likatae Muswada huu Kusomwa Mara ya Pili kwa sababu Serikali imeleta Muswada Mpya na wenye mabadiliko makubwa na ya msingi bila kufuata masharti ya kanuni ya 84(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge; na pia kwa sababu Serikali haijatekeleza maagizo ya Bunge hili tukufu kuhusu kutoa muda zaidi kwa Kamati na wananchi kuufikiria, kuuelewa na kuutolea maoni Muswada huu kinyume na matakwa ya ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano juu ya uhuru wa wananchi kutoa maoni yao; ibara ya 21(1) na (2) juu ya haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi, na haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayowahusu wananchi, maisha yao au yanayolihusu Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI& WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERIA