Tuesday, July 31, 2012

Maoni yangu katika Sekta ya Afya: Bajeti na uhalisia!

Jana tarehe 30 Julai 2012 baada ya Hotuba ya Waziri wa Afya ya Ustawi wa Jamii kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii kuhusu Wizara husika na Maoni ya Kambi ya Upinzani nilitaka mjadala usiendelee mpaka kwanza wabunge tupewe nakala ya ripoti ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia mgogoro kati ya Serikali na madaktari na kuandaa mapendekezo ya kuboresha Sekta ya Afya nchini.

Nilifanya hivyo kwa kunukuu Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii ambayo pamoja na kuwa mwezi Februari 2012 bunge lilikataliwa kujadili masuala husika mpaka kwanza kamati hiyo ikapate ukweli wa pande zote mbili na kuwasilisha mapendekezo kwa bunge, taarifa ya Kamati hiyo kuhusu bajeti iliyowasilishwa jana haikueleza chochote nini kamati ilibaini baada ya kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya wala haikueleza ni ushauri gani iliutoa kwa serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro uliokuwepo wala haikuwasilisha bungeni mapendekezo yoyote yaliyotokana na kazi waliyopewa na bunge. Aidha, Nilinukuu pia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo yalieleza bayana kuwa mwezi Juni yalitolewa majibu yasiyokuwa ya kweli bungeni kuwa Taarifa ya Kamati hiyo iliwasilishwa bungeni.

Kufuatia hali hiyo, na kutokana na bajeti hiyo ya afya kuwa finyu huku ikiwa na utegemezi wa fedha kutoka nje kwa ziadi ya asilimia 90 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 wakati ambapo katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango cha fedha ambazo wahisani walileta ni asilimia 36 pamoja na kuahidi kuchangia zaidi ya 90 kwenye fedha za maendeleo; hali ambayo itaendeleza migogoro kwenye sekta ya afya.

Nikataka ili bunge liweze kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro kwenye sekta ya afya nchini; Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia madai ya madaktari iwasilishwe na kujadiliwa bungeni, majibu ya Naibu Spika aliyoyatoa ni kwamba taarifa hiyo haiwezi kuwasilishwa kwa bungeni kwa kuwa kuna kesi mahakamani baina serikali na Madaktari. Majibu hayo yamenifanya niwakumbushe taarifa hii ambayo niliitoa tarehe 29 Julai 2012 ili wadau wa afya mshiriki katika kutaka hatua muafaka toka kwa Serikali na Uongozi wa Bunge:

Sunday, July 29, 2012

Kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:

Kwa maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.

Ukiondoa tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.

Hivyo hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.

Hata baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.

Friday, July 27, 2012

HOTUBA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI; WIZARA YA NISHATI NA MADINI

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

UTANGULIZI


Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za kuhamasisha mabadiliko katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni. Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com tutaendelea nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.

Sunday, July 22, 2012

PICHA ZA ZIARA ZA VIONGOZI WA CHADEMA, Ndago Mkoani Singida

Mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar-es-salaam,John
Mnyika,akihutubia wakazi wa kijiji cha Ndago jimbo la Iramba magharibi.

Baadhi ya Viongozi wa CHADEMA waliokuwa
katika mkutano huo ,kulia Dr Kitila Mkumbo
 

Saturday, July 21, 2012

Singida:Polisi wasogeza muda.

Polisi wamesema tuongeze muda wa kusubiri kwa kuwa gari la kikosi chao toka  Dar es Salaam imepata tatizo. Tumewaeleza ikifika saa 11 jioni ama RPC aliyetuita atuhoji au turudi Dodoma hicho kikosi kilichokuja kitufate. Nimepata  hapa ushahidi wa nyaraka kuwa pamoja na vijana kikundi kidogo cha vijana wa CCM Ndago,Iramba waliofunguliwa jalada wakamatwe kwa kurusha mawe mkutanoni kuna vijana wengine toka Dar Es Salaam na maeneo mengine ya Singida ambao ni sehemu ya watuhumiwa na viongozi wa CCM wanahangaika kuwawekea dhamana. Taratibu ukweli unazidi kuibuka. Kuna njama zilipangwa na baadhi ya viongozi wa serikali, polisi na CCM juu yangu. Nasubiri nikiona kama wana muelekeo wa kuzitekeleza wakati wa mahojiano na polisi nitaweka mambo hadharani hatua kwa hatua.

Maslahi ya Umma Kwanza

John John Mnyika,
Mbunge Jimbo la Ubungo (CHADEMA)
18.07.2012

Wednesday, July 18, 2012

Mwito wa Polisi, Singida: Yanayojiri!

Nimefika Singida kuitikia mwito wa Polisi kutoa maelezo kuhusu mkutano nilioalikwa Iramba kwa nafasi yangu ya Mkurugenzi wa Habari na Uenezi.

Nimekutana na RPC, amesema kwamba nisubiri mpaka saa 10:30 alasiri ndiyo nikutane nao kwa kuwa kwa sasa kuna kikosi cha upelelezi toka Dar Es Salaam kimekwenda eneo la tukio. Nimemuuliza RPC maswali mawili;

1. Wameniita kutoa maelezo kama mtuhumiwa au shahidi?

Amenijibu kuwa ni mahojiano ya kawaida.

2. Kwanini mpaka sasa watuhumiwa 12 waliofunguliwa jalada NDG/RB/190/2012 kwa kurusha mawe kwenye mwanzo wa mkutano wakati Bwana Waitara akitoa hotuba ya utangulizi huku polisi wakiachia hali hiyo. Baada ya kufungua jalada na polisi wa juu kupigiwa simu kuwa kuna njama kati ya Polisi na CCM hali ilitulia, Waitara akamaliza hotuba yake, Dkt Kitila akasalimia name nikahutubia kwa amani na kwenda kwenye mkutano mwingine. Mauaji yalitokea baadae mbali na tulipohutubia.

John John MNYIKA,

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA)

18 Julai, 2012

Monday, July 16, 2012

Tutibu kiini cha tatizo Sekta ya Nishati ya Umeme!

Kwa nafasi ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini,nafahamu kuna ufisadi na ubadhilifu ndani ya TANESCO ambao uchunguzi ni muhimu kwa ajili ya uwajibikaji.Kusimamishwa kwa Mkurugenzi wa TANESCO na maafisa wengine wa shirika hilo kupisha uchunguzi ni muhimu,lakini si muarubaini wa uozo wa kimfumo katika sekta ya nishati nchini nitatoa vielelezo vya kina wakati nitakapo wasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni katika wizara ya Nishati na Madini.

Hata hivyo ni vyema nikatahadharisha mapema kuwa tukio hili linapaswa kutafakariwa kwa upana kwa kuwa linahusisha masuala mengi ambayo mengine Bodi ya Wakurugenzi imeyaacha nyuma ya pazia.Ukweli wote utakapotoka hadharani wengine zaidi watapaswa kuwajibika au kuwajibishwa kwa maslahi ya Taifa!

Kwa nyakati mbalimbali toka mpango wa dharura wa umeme uwasilishwe bungeni,nimekuwa nikiitahadhalisha na kuihoji serikali(kama sehemu ya jukumu langu la kibunge) kwa uzembe,ufisadi na udhaifu wa kiutendaji katika serikali ambao hasara yake utairejesha nchi katika mgao wa umeme hali ambayo imedhihirika hivi sasa!

Sunday, July 15, 2012

Majibu juu ya MAJI na hoja binafsi

Jana tarehe 13 Julai 2012 niliuliza swali la nyongeza bungeni kuhusu mtandao wa mabomba maarufu kama mabomba ya wachina kutokutoa maji kwa miaka mingi kwenye maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla; nilihoji hatua za dharura za serikali za kuhakikisha mabomba hayo yanatoa maji badala ya kusubiri mpaka Disemba 2014 kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Wizara ya Maji, nilihoji pia hatua zilizochukuliwa  kwa waliosababisha uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa kuwa mabomba hayo yameanza kuharibika.

Katika majibu serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maji Dkt. Binilith Mahenge ilieleza kuwa upo uwezekano wa sehemu ya miundombinu kuharibika au kuharibiwa na ili kuepusha hali hiyo serikali inatekeleza miradi ya kuongeza uzalishaji kutoka Ruvu chini, Ruvu juu na vyanzo vingine. Aidha, baada ya miradi hiyo kukamilika mtandao wa mabomba utahakikiwa na kama kuna kasoro zitarekebishwa na pia kama kuna ubadhirifu wowote utakao bainika Serikali itachukua hatua.

Ninachoweza kusema kwa sasa ni kuwa Hotuba ya Waziri wa Maji Prof, Jumanne Maghembe akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya matumizi ya fedha za Wizara ya Maji kwa mwaka 2012/2013 tarehe 9 Julai 2012 na majibu haya ya Naibu Waziri ya tarehe 13 Julai 2012 yanadhihirisha haja ya hoja binafsi niliyoiwasilisha ya kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Ikumbukwe kwamba Rais Jakaya Kikwete na mawaziri mbalimbali kwa nyakati mbalimbali waliahidi kwamba tatizo la maji kuwa historia katika mkoa wa Dar es salaam mwaka 2013;  kinyume na ahadi hiyo kauli mpya ya Waziri bungeni ni kuwa sasa miradi hiyo inakamilika mwaka 2014. Hata hivyo, uchambuzi wangu kuhusu bajeti iliyopitishwa mwaka 2011/2012 na 2012/2013 inaonyesha kwamba hata lengo hilo la 2014 haliwezi kufikiwa kwa kuwa kiwango cha fedha kilichotengwa ni kidogo pungufu ya kilichopaswa kutengwa kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa maendeleo, hivyo kama mwelekeo wa utekelezaji utakuwa wa kusuasua kama ilivyo sasa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es salaam yatadumu mpaka zaidi ya mwaka 2016 tofauti na ahadi zinazotolewa na serikali.
Ikumbukwe kwamba Mwezi Februari 2011 Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri lakini kiwango cha fedha kinachotengwa na serikali hakizingatii waraka huo na maazimio ya baraza la mawaziri kwa ukamilifu wake hali ambayo inahitaji bunge kuisimamia serikali kwa haraka.

Aidha, Wizara ya Maji haionyeshi kuichukulia kwa uzito unaostahili kashfa ya Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji; hivyo hatua za kibunge zinahitajika katika kuwezesha ukaguzi stahiki.
Kwa upande mwingine, wakati miradi ya muda mfupi ikiendelea kusubiriwa, wananchi wanahitaji maji ya haraka hivyo Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kuwa Oktoba 2012 katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa tofauti na ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa Kimara mwezi Mei mwaka 2010.
Nashukuru kwamba baada ya kueleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi tarehe 8 Juni 2012 hatua zifuatazo zimechukuliwa na Wizara ya Maji: Mosi, kwa mara ya kwanza Wizara imejibu barua yangu na kueleza hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa za kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji katika Jimbo la Ubungo. Pili, Wizara imetoa mrejesho wa utekelezaji wa Mpango wa dharura wa Maji kwa jiji la Dar es salaam.
Hata hivyo, kwa kuwa maelezo na majibu yaliyotolewa hayajashughulikia kwa ukamilifu hatua saba ambazo nilipendekeza Wizara ya Maji ichukue nitaendelea kuchukua hatua katika mkutano huu wa nane unaoendelea kuwasilisha hoja binafsi kuomba bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Izingatiwe kwamba tarehe 8 Juni 2012 nilieleza kwamba nimewasilisha  kwa katibu wa bunge taarifa ya hoja pamoja na maelezo ya hoja; hivyo ninachosubiri hivi sasa ni kujulishwa iwapo hoja husika imekubaliwa kuwasilishwa bungeni katika mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa.
Kati ya hatua hizo saba amabazo bunge ni muhimu likapitisha maazimo ya kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 63 (2) na (3) ni pamoja na ; Mosi,  kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya kashfa ya taifa ya kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 ambapo Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Pili; kuwasilisha  bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti kamili ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa ipasavyo kwa msukumo wa kibunge badala ya ahadi za ujumla za kwenye ziara.
Tatu; Serikali kueleza hatua zilizopangwa kuchukuliwa kufuatia ziara ya Wizara ya Maji kuhakikisha Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 unawekewa muda wa ukomo wa kukamilika ndani ya miezi mitatu katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
Nne; Serikali kukubaliana na pendekezo nililotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
Tano; Serikali kuhakikisha Wizara ya Maji inaisimamia EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, Serikali ihakikishe EWURA inaharakisha kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.
Sita; Serikali iwezeshe Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 iliyotolewa na CAG kwa haraka ili maoni na mapendekezo yazingatiwe mapema iwezekanavyo.
Saba; Serikali ihakikishe inawasilisha kwenye mkutano wa tisa wa bunge muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Imetolewa Dar es salaam tarehe 14 Julai 2012 na:

John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
Bungeni-Dodoma
Thursday, July 12, 2012

OFISI YA WAZIRI MKUU HAIKUJIBU UKWELI BUNGENI SWALI LANGU KUHUSU MGOGORO KATI YA SERIKALI NA WALIMU


Ofisi ya Waziri Mkuu imejibu uongo  bungeni kuhusu uwepo wa mgogoro kati ya Serikali na walimu hivyo nakusudia kumwandikia Spika aagize swali hilo lijibiwe kwa ukweli na ukamilifu.
Tarehe 11 Julai 2012 wakati nikiuliza swali la nyongeza kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya walimu watumishi wa umma katika Jimbo la Ubungo na nchi kwa ujumla kuwa ni lini serikali itakamilisha kushughulikia madai ya walimu kwa kuwa matatizo walimu yamedumu kwa miaka mingi kwa kiwango cha kufikia hatua ya walimu kutangaza mgogoro na serikali.
Akijibu swali langu kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Majaliwa Kassim Majaliwa hakueleza kwa ukamilifu ni lini serikali itakamilisha kushughulikia madai ya walimu badala yake akatoa majibu ya uongo kuwa walimu hawajatangaza mgogoro  na serikali.
Hata hivyo, ukweli ni kuwa walimu wametangaza mgogoro na serikali na ushahidi ni tamko la Serikali  yenyewe kuhusu migomo sehemu za kazi lililotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira tarehe  9 Julai 2012 ambalo limeeleza kuwa tayari Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kwa niaba ya walimu nchini kimeishawasilisha mgogoro katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi- Dar es salaam wenye usajili CMA/DSM.ILA/369/12.
Hivyo, naendelea kusisitiza serikali ichukue hatua ya kushughulikia vyanzo vya migogoro na watumishi wa umma badala ya kusubiri mpaka matokeo ya migogoro kama migomo na madhara mengine kwa nchi na wananchi ndio ianze kutumia nguvu kuidhibiti.
Migogoro kati ya serikali na watumishi wa umma ina athari kubwa; wakati migogoro ya madaktari huchangia katika kuathiri hali na uhai wa wagonjwa, migogoro kati ya serikali na walimu inachangia katika kudidimiza ubora wa elimu na kuathiri maisha ya wanafunzi.
Na wabunge  tupewe nafasi ya kuishauri na kuisimamia serikali kwa mujibu wa mamlaka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) kwa kuletewa taarifa sahihi na pia kujibiwa maswali kwa ukweli na ukamilifu kabla ya serikali kwenda mahakamani baada ya majadiliano yake na watumishi wa umma kukwama kama ilivyotokea kwa madaktari.
Aidha, Spika aliwezeshe bunge kupokea taarifa maalum ya kamati ya bunge ya huduma za jamii kuhusu madai ya watumishi wa umma ambayo mengi chanzo chake ni ufinyu wa bajeti ili katika mkutano huu wa bunge la bajeti unaoendelea bunge liweze kujadili na kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro badala ya matokeo.

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
13/07/2012

Saturday, July 7, 2012

Barabara za Kupunguza Msongamano na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi

Jana usiku tarehe 6 Julai 2012 Bunge limepitisha mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/2012. Mtakuwa mmeona wakati bunge lilipokaa kama kamati nilishika mshahara wa Waziri kutaka maelezo ya kisera juu ya mkakati wa serikali katika kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika barabara ya Morogoro inayopita Jimbo la Ubungo.


Nilitaka maelezo hayo kwa kuwa pamoja na kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2016 au zaidi.

Nilitaka maelezo ni kwanini Serikali isizingatie vipaumbele vya mwaka wa kwanza wa mpango wa miaka mitano katika kuandaa bajeti ili pamoja na miradi hiyo niliyoitaja iwekeze kwa haraka kwenye barabara za pete/mzunguko (ring roads) za pembezoni ambazo zinaweza kujengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuchangia kwenye kupunguza foleni katika barabara kuu ifikapo mwaka 2013.

Kufuatia majibu ya Waziri nilihoji tena wakati bunge linapitisha vifungu vya miradi ya maendeleo kwenye kasma ya kuondoa foleni Dar e salaam ambayo imetengewa shilingi bilioni 10.5 tu, wakati ambapo mpango wa taifa wa miaka mitano uliopitishwa umeelekeza kifungu hicho kitengewe jumla ya fedha kwa miaka miwili 2011/2012 na 2012/2013 kiasi cha shilingi bilioni 100.1. Ikumbukwe kwamba mwaka jana serikali ilitenga bilioni 5 tu wakati mpango uliitaka serikali itenge bilioni 68 na nilipohoji wakati huo nilijibiwa kwamba ilikuwa ni kipindi cha mpito hivyo fedha zote zingeunganishwa mwaka huu kitu ambacho hakikufanyika.

Majibu ya kwamba Dar es salaam na Pwani kwa ujumla zimetengewa bilioni zaidi ya 900 yanajumuisha fedha za maendeleo kwa miradi iliyoanza 2010/2011, 2011/2012, 2012/2013 na ni miradi ya muda mrefu ya barabara kuu na madaraja makubwa kwa mikoa yote miwili.

Kwa hiyo bilioni 10.5 imegawanywa kidogo kidogo kwa barabara zifuatazo: Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine ya Dar es salaam kama zilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri. Kwa kasi hii ndogo, itachukua takribani miaka kumi kuweza kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara hizo ambazo jumla ya urefu wake ni kilomita 96 tu.

Nashukuru kwamba fedha zimetengwa kumalizia pia barabara ya Ubungo Maziwa- Bus Terminal na pia za kuanza ya kuelekea External, na pia bilioni zaidi ya 240 za mradi wa DART; hata hivyo, tuendelee kuungana katika kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi wakati tukisubiri utekelezaji wa miradi ya muda wa kati na muda mrefu.

Tuendelee kuishauri Tume ya Mipango ambayo Mwenyekiti wake ni Rais kuingiza kwenye Mpango wa Mwaka wa Maendeleo Mwezi Februari 2013 ili hatimaye kiwango hicho cha fedha kiingizwe katika bajeti. Izingatiwe pia kuwa sehemu ya Barabara hizo ni ahadi za Rais alipotembelea Jimbo la Ubungo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010 na kurudia tena ahadi hizo wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2010. Tuendelee kushirikiana katika kufuatilia kazi za maendeleo.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,John Mnyika (Mb)

7/7/2012-Bungeni, Dodoma

Sunday, July 1, 2012

MAONI YA MBUNGE WA UBUNGO KUHUSU HOTUBA YA MH. DKT. JAKAYA KIKWETE RAIS WA TANZANIA KWA WANANCHI TAREHE 30 JUNI 2012
Leo tarehe 1 Julai 2012 kumesambazwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari hotuba ya Mh. Dkt. Jakaya Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi inayotajwa kutolewa tarehe 30 Juni 2012.

Kufuatia hotuba hiyo na kufuatia mwito kutoka wachangiaji wa mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kutaka maoni yangu kuhusu hotuba husika, naomba nichukue fursa hii kutoa maoni kwa nafasi yangu ya ubunge kuhusu hotuba tajwa kama ifuatavyo:

Hotuba hiyo ya Rais imeibua mjadala na masuala ambayo yanahitaji kujadiliwa bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge unaoendelea hivyo, serikali isiendelee tena kutumia kisingizio cha mahakama kulizua bunge kujadili masuala husika wakati yenyewe inayajadili na kuyatolea maelezo na maelekezo pamoja na kuchukua hatua hususani kuhusu suala la mgomo wa madaktari.

Hotuba hiyo ya Rais ukindoa suala la usafirishaji haramu wa watu nchini inaelekea kuwa ndiyo kauli ya Serikali ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliahidi kwamba ingetolewa bungeni lakini baadaye serikali ikasema haitatoa kauli. Uamuzi wa Serikali kuitoa kauli hiyo kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge wasijadili hotuba husika na pia wasitimize wajibu wa kikatiba wa ibara 63 (2) wa kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.

Hivyo, Ofisi ya Rais na Ikulu wanapaswa kutoa maelezo kwa umma sababu za Rais kutolihutubia taifa tarehe 30 Juni 2012 kama ilivyotangazwa katika baadhi ya vyombo vya habari vya kielectroniki na badala yake hotuba ya Rais kusambazwa tarehe 1 Julai 2012 kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari na iwapo masuala ya hotuba hiyo kuhusu mgomo wa madaktari ndiyo yale ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikusudia kuyaeleza bungeni.

Aidha, kwa kuwa bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia kesho tarehe 2 Julai 2012 na kuendelea ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ni vizuri hotuba ya Rais imeeleza wazi kwamba tukio la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si la kwanza kutokea hapa Tanzania kwa kuwa kwa kipindi cha miaka kumi kumekuwa na ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu katika taifa letu kupitia mipaka ya mikoa mbalimbali hapa nchini. Kwa mbinu yoyote ile ambayo imetumika, matukio haya yanaashiria kwamba mipaka yetu haipo salama kwa kuwa kama malori na vyombo vingine vya usafiri vyenye watu wasio na hati za kuingilia nchini wanaweza kuingia kwa wingi kwa nyakati mbalimbali tafsiri yake ni kwamba nchi iko kwenye hatari ya kuingiziwa pia vitu vingine haramu ikiwemo madawa ya kulevya na silaha hali ambayo ni tishio kwa usalama wa nchi na maisha ya wananchi. Ni vizuri Rais amekutana tarehe 27 Juni 2012 na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuzungumzia tukio hilo; hata hivyo, zaidi ya kuwapongeza vyombo vya dola kwa kazi nzuri ya kudhibiti shughuli za biashara haramu, nilitarajia kwamba Rais kwa mujibu wa mamlaka yake ya ibara ya 33 (2) ya mkuu wa nchi, kiongozi wa serikali na amiri jeshi mkuu angeagiza uchunguzi ufanyike kuhusu udhaifu uliojitokeza na kuagiza hatua kuchukuliwa kwa walishindwa kudhibiti hali hiyo katika mipaka ambayo biashara haramu ya usafirishaji wa watu inapitia. Izingatiwe kwamba mianya hii katika mipaka yetu ina athari pana sio katika suala hili tu bali pia katika usalama wa maisha ya wananchi kama ilivyo katika mikoa ya Kigoma, Kagera na kwingineko ambapo uhai wa wananchi na mali zao uko mashakani kutokana na uvamizi toka kwa wahamiaji haramu. Aidha, athari za hali hiyo zimejitokeza katika usambazaji wa chakula toka kwenye hifadhi ya taifa ambapo pamoja na Serikali kutumia zaidi ya bilioni 27 kusambaza mahindi na nafaka nyinginezo bei za bidhaa hizo katika Soko la Dar es salaam ikiwemo katika Jimbo la Ubungo hazikushuka kutokana na vyakula hivyo kutoroshwa na kuuzwa nje ya nchi kutokana na udhaifu katika ulinzi kwenye mipaka.

Hivyo, ni muhimu wabunge wakati wa mjadala wa bajeti ya ofisi ya Rais wataka kuongezeka kwa uwajibikaji na usimamizi wa utawala wa sheria ili kudumisha amani nchini.

Hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa ni pamoja na bunge kuisimamia serikali kuhakikisha idara ya usalama wa taifa inafanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kuvisaidia vyombo vingine vya dola kulinda mipaka ya nchi na pia matatizo ya maslahi katika vyombo vya ulinzi na usalama yanatatuliwa ili vyombo husika viweze kufanya kazi bila baadhi ya maofisa wake kujihusisha na vitendo vya ufisadi na kuruhusu biashara haramu za aina mbalimbali.

Kuhusu Mgomo wa Madaktari

Kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa; hotuba ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielezo vya upande wa pili; hivyo kuwa serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani, ni muhimu pia taarifa ya kamati ya bunge ya huduma za jamii iliyoshughulia suala hilo na kukutana na pande zote mbili itoe taarifa yake bungeni na kwa umma.

Katika hotuba yake Rais amewaeleza kwa kiwango kikubwa wananchi namna ambavyo madaktari wanasababisha mahangaiko kwa wagonjwa wengi na kusababisha vifo kwa wengine lakini hakueleza kabisa mchango wa serikali katika kusababisha hali hiyo. Hivyo, kwa kuwa pande zote mbili zinachangia katika athari zinazoikumba nchi na wananchi kutokana na mgomo; ni muhimu chombo cha tatu kikaingilia kati kuwezesha ufumbuzi kupatikana na chombo hicho ni bunge ambalo ndilo lenye wajibu wa kuisimamia serikali. Jitihada za kuwalazimisha madaktari kurejea kazini bila majadiliano ya pande mbili mbele ya chombo cha kuisimamia serikali kushughulikia chanzo cha mgogoro huo zinaweza kuleta ufumbuzi wa muda mfupi na athari za muda mrefu.

Ieleweke kwamba hata madaktari wakisitisha mgomo wa wazi kutokana na amri ya mahakama na agizo la Rais, migogoro katika ya serikali na watumishi wa umma wenye kusababisha migomo baridi ya chinichini ina madhara ya muda mrefu kwa taifa.

Mathalani, kutokana na migomo baridi na huduma mbovu katika sekta ya afya wananchi wa kawaida wamekuwa wakifa kutokana na magonjwa yanayotibika.

Migomo ya chini kwa chini ya walimu na mazingira mabovu yamekuwa yakisababisha kudidimia kwa elimu katika shule za umma; mwanafunzi aliyehitimu masomo yake bila kujua kusoma na kuandika hana tofauti na mgonjwa anayekufa kwa kukosa huduma.

Hali hii ya kugoma kusiko kwa wazi imeenza kujipenyeza mpaka kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuachia mianya ufisadi na kushindwa kusimamia utawala wa sheria kama ivyodhihirika kwa kuongezeka kwa vitendo vya biashara haramu katika taifa letu.

Rais amewaeleza wananchi kuwa kati ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari na kwamba katika mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa na pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. Hata hivyo, katika masuala matano yaliyobaki, Rais hakueleza kwa wananchi nini ambacho serikali ilikuwa tayari kutoa kwa kila madai na kwa kiasi gani badala yake ameonyesha tu kwa ujumla kwamba madai hayo hayatekelezi.

Aidha, kufuatia hotuba hii ya Rais Madaktari nao wana wajibu wa kuueleza umma msingi wa madai yao na kwa kiwango gani walikuwa tayari kushuka kutoka katika madai yao ya awali, kinyume na hayo itaonekana kwamba madaktari waliingia katika majadiliano wakiwa na msimamo wa kutaka madai yao pekee ndiyo yakubaliwe wakati ufumbuzi wa mgogoro wa pande mbili hupatikana kwa win win (give and take).

Ni vizuri ikafahamika kwamba katika majadiliano, pande zote mbili huwa na mapendekezo yake; hivyo upo uwezekano kwamba yapo madai ambayo madaktari wameyatoa ambayo serikali haina uwezo wa kuyatimiza kwa kiwango walivyopendekeza na yapo ambayo serikali imeyakataa wakati ambao ina uwezo wa kuyatekeleza hata ikiwa kwa kiwango pungufu ya kile kilichopendekezwa na madaktari.

Suluhu katika mgogoro kama huo ambao kila upande una mapendekezo yake linapaswa kufanywa na vyombo vya usuluhishi; hata hivyo kuwa suala hili linahusu mgawanyo wa rasilimali za nchi na bajeti ya serikali, chombo chenye mamlaka ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi ni bunge.

Na kwa kuwa kamati ya bunge ya huduma za jamii ilikutana na pande mbili, ilikuwa muhimu kwa serikali kabla ya kupeleka shauri mahakamani kurejesha kwamba suala husika bungeni ambalo ndilo lenye wajibu wa kupendekeza vipaumbele vya mpango wa serikali na ndilo lenye kuidhinisha bajeti ya matumizi ya serikali.

Uamuzi wa serikali kukimbilia mahakamani kabla ya majadiliano ya bunge umechangia katika kusababisha mgomo wa madaktari, hivyo ushauri wangu kwa Rais Kikwete ni kwa serikali kufuta kesi iliyoko mahakamani ili bunge lipewe fursa ya kujadili ripoti yake kamati yake na kupitisha maazimio ya kuwezesha suluhu kati ya serikali na madaktari.

Mahakama iwe ni hatua ya mwisho baada ya mihimili miwili muhimu ya serikali na bunge kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.

Rais Kikwete ameeleza taifa kwamba Serikali imeongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12; hata hivyo serikali inapaswa pia kulieleza taifa namna ambavyo kiwango hicho cha fedha kinapungua ukiweka kizio (factor) cha kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumumo wa bei ukilinganisha mwaka 2005 na 2012.

Ukweli ni kwamba bajeti ya Sekta ya Afya bado ni ndogo kwa kuwa serikali haijatimiza bado azimio la kutenga asilimia 15 kwa ajili ya bajeti ya afya pia, hata kiwango hicho cha ongezeko la fedha hakijaleta matokeo ya kutosha kutokana na matumizi kuelekezwa kwenye baadhi ya maeneo yasiyokuwa ya kipaumbele na kuwa na utegemezi wa kiwango kikubwa cha fedha za wahisani ambazo kwa mwaka huo wa 2011/2012 aliourejea Rais Kikwete hakikutolewa kwa kiwango kilichoahidiwa. Hivyo, Rais Kikwete awezeshe kuongezwa kwa fedha za ndani kwenye bajeti ya afya kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika madai mengine Rais Kikwete ameeleza kwamba pande mbili zilifikia makubaliano nusu nusu, hali ambayo inaashiria kwamba madaktari wana hoja ambazo zinahitaji majadiliano hivyo, ni muhimu bunge likapewa nafasi ya kujadili kuweza kuwakilisha pande zote mbili za serikali na madaktari kuhusu nini kinawezekana na nini hakiwezekani ili kulinusuru taifa na mgogoro unaoendelea.

Rais Kikwete ametumia kwa kiwango kikubwa madai ya madaktari ya ongezeko la mshahara kujaribu kuwachonganisha wananchi na madaktari kwa kuwa na madai yasiyotekelezeka. Hata hivyo, ni muhimu ikafahamika kwamba sio madaktari pekee ambao wana mgogoro na mwajiri wao yaani serikali kuhusu kiwango cha mshahara bali pia watumishi wengine wa umma ikiwemo walimu.

Nyongeza iliyotolewa na serikali ya kati ya asilimia 15 na 20 kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 ni tofauti na ahadi ambazo serikali imekuwa ikitoa kwa wafanyakazi za kuongeza mishahara na kupunguza kodi katika mishahara. Rais Kikwete na serikali warejee maoni na mapendekezo ya kambi rasmi ya upinzani kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/2013 kuhusu nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma na vyanzo mbadala vya mapato vya kuongeza kwa ajili ya kuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji. Uwiano wa sasa wa matumizi ya mishahara kuwa asilimia 48 ya bajeti badala ya uwiano mzuri wa asilimia 35 kuwa mishahara na na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa; ni matokeo ya udhaifu wa serikali katika kupanua vyanzo vya mapato, kupunguza matumizi ya kawaida yasiyo ya lazima na kuongeza fedha katika miradi ya maendeleo hali ambayo Rais Kikwete kuliwezesha bunge kuisimamia serikali na kuirekebisha.


Kuhusu Suala la Dkt. Steven Ulimboka

Rais Kikwete ameeleza wananchi kuwa ameelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane; hata hivyo kauli hii inaashiria kukubaliana na hatua iliyochukuliwa na jeshi la polisi kuunda jopo la kuchunguza.

Nilitarajia Rais Kikwete kwa kutambua uwepo wa madai ya polisi kutuhumiwa kuhusika katika jaribio la mauji ya Dr Ulimboka angetangaza kuunda tume huru ya uchunguzi au walau angeongeza nguvu katika jopo la uchunguzi lililoundwa kwa kuunda timu ya maafisa waandamizi wa vyombo vya ulinzi na usalama na usalama pamoja na wadau wengine kutoka taasisi huru.

Rais Kikwete anapaswa kutumia madaraka yake kwa mujibu wa katiba kuunda tume huru ambayo inadhihirisha kwa vitendo kwamba watuhumiwa hawajichunguzi wenyewe na kuwezesha matokeo ya uchunguzi kuaminika.

Narudia kuwasihi madaktari kuendelea kuokoa maisha ya wananchi katika kipindi hiki kigumu lakini wakati huo huo Rais Kikwete aiongoze serikali kuepusha athari zaidi katika sekta ya afya ya kuwa na mgogoro na madaktari kwa kuliwezesha bunge kujadili suala hili na kulipatia ufumbuzi ikiwemo kupitia nyongeza ya bajeti ya Wizara ya Afya. Nimemwandikia barua Spika Anna Makinda akiwa ni mkuu bunge kama muhimili mmojawapo wa dola kuweza kuchukua hatua stahili, naomba pande zote zizingatie maoni yanayotolewa na wabunge kwa niaba ya wananchi kwa maslahi ya taifa.

Maoni haya yametolewa leo tarehe 1 Julai 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma