HOTUBA YA MGENI RASMI-JOHN MNYIKA (MWENYEKITI WA MKOA WA KINONDONI KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM) KATIKA UFUNGUZI WA MAFUNZO YA VIONGOZI WA CHADEMA JIMBO LA UBUNGO YALIYOFANYIKA KATIKA HOTELI YA DELUXE DAR ES SALAAM TAREHE 31 JANUARI 2010.
Ndugu viongozi na wajumbe wa Kamati ya Utendaji;
Wawakilishi wa Kata mbalimbali;
Wageni Waalikwa, mabibi na mabwana;
Itifaki zote zimezingatiwa:
Nawashukuru kwa kunialika kuja kufungua haya mafunzo kuhusu uendeshaji wa chama na maandalizi ya uchaguzi ambayo yanafanyika Wilaya/Jimbo la Ubungo ndani Mkoa wetu wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es salaam.
Katika mafunzo yenu mzingatie mambo ambayo ni kipaumbele katika kushamiri kwa chama cha siasa na kushinda kwa wagombea wake. Kwa tafsiri rahisi; chama cha siasa ni jumuia ya watu wenye dhamira inayofanana wakilenga kuchukua dola kwa njia za kidemokrasia ili kuweza kutekeleza azma yao kwa ustawi wa jamii. Na kabla ya kuchukua dola, chama kinakuwa na wajibu wa kuiwajibisha serikali iliyoko madarakani na chama kinachotawala.
Kwa hiyo fursa hii ya mafunzo iwawezeshe kutafakari mambo ya msingi yanayounda chama cha siasa na dhima yake kwa taifa. Msingi wa kwanza ni watu ambao kwenye chama cha siasa ni pamoja na wanachama na wapenzi wa chama, hivyo lazima kujifunza ni kwa vipi CHADEMA katika ngazi zenu na maeneo yetu kinaweza kupata wanachama na wapenzi zaidi na kuwashirikisha katika michakato ya demokrasia lakini pia michakato ya kimaendeleo katika jamii zinazowazunguka.
Msingi wa pili ni dhamira inayofanana, hii ni pamoja na falsafa, itikadi, sera za CHADEMA lakini pia inajumisha malengo na maamuzi ya pamoja. Mafunzo haya yawawezesha kuilewa zaidi dhamira hiyo, kuitafsiri katika muktadha wa mazingira yenu ili kuweza kutekeleza malengo mliyojiwekea kwa kufanya kazi kama timu.
Msingi wa tatu ni kulenga kuchukua dola kwa njia za kidemokrasia; hivyo mafunzo haya yawawezeshe kujipanga zaidi kutimiza wajibu huu. Kwa bahati njema mafunzo haya yanafanyika mapema zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais mwaka 2010. Katika muktadha huo mafunzo yawawezeshe kuhamasisha watanzania waadilifu kutoka ngazi zenu kujitokeza kugombea nafasi hizo na kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya kupata kura na kulinda ushindi.
Nachukua fursa hii kutoa mwito kwenu kuwatangazia wananchi kwamba uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa upande wa Dar es salaam utafanyika kuanzia tarehe 22 mpaka 27 Machi mwaka 2010. Nawaomba watanzania wote ambao watakuwa wamefikia umri wa miaka 18 na kuendelea wakiwemo vijana na wanawake wajitokeze kwa wingi kwenda kujiandikisha. Mafunzo yawawezeshe kutambua njia za kidemokrasia za kutumia kuweza kushinda uchaguzi na kupata dhamana ya kuongoza serikali- njia kuu ikiwa kugombea, kupiga kampeni na kupiga kura. Katika kufanya kuiwajibisha serikali iliyo madarakani na hata kufanya kampeni za uchaguzi natarajia mtatumia njia za kawaida mathalani mikutano ya hadhara, kampeni za mtu kwa mtu, vyombo vya habari nk.
Hata hivyo, katika mazingira ya leo ambapo chama kilichopo madarakani kinaendesha siasa za rushwa na vurugu kikitumia pia vyombo vya dola na watumishi wa umma ni muhimu mkajipanga kuunganisha nguvu ya umma kukabiliana na hujuma ikiwemo kuzuia uwizi wa kura.
Katika mazingira hayo ya kutokuwa na uwanja sawa wa kisiasa ni muhimu mafunzo yakawawezesha pia kufahamu mbinu mbadala za kidemokrasia zinazoweza kutumiwa kushinikiza mabadiliko ya kweli ikiwemo mbinu ya kukataa utii wa kiraia hata pale haki za msingi zinapovunjwa (civil disobedience) mathalani kupitia maandamano nk. Natoa tamko rasmi kama Mwenyekiti wa Mkoa na muwafikishie salamu hizi CCM na vibaraka wao kwamba CHADEMA Mkoa wa Kinondoni hatutakubali kuibiwa kura katika uchaguzi wa mwaka 2010 ndani ya wilaya, jimbo na kata zetu na tunatoa changamoto kwa maeneo mengine ya nchi nayo kujipanga vilivyo kuwadhibiti mafisadi wa kisiasa na wote wanaotumika kuhujumu demokrasia wakati wa uchaguzi.
Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli, viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa ahadi kedekede kwenye uchaguzi lakini utekelezaji ni legelege kutoka na ombwe na uongozi na mfumo mzima wa utawala kuelemewa na ufisadi. Wakati nyinyi mmejumuika hapa kwa ajili ya mafunzo siku ya leo, viongozi wa CCM wamejumuika katika maeneo mbalimbali kuzindua sherehe za wiki nzima ya kile wanachokiita maadhimisho ya miaka 33 ya CCM.
Kwa kweli CCM imefikia kiwango cha juu sana cha kuwapuuza watanzania ambao iliwaahidi kuwaletea maisha bora badala yake imeweka mazingira ya gharama za maisha kupanda kwa Ari, Nguvu na Kasi mpya kupitia kupandisha kodi na bei za bidhaa zinatumiwa na wananchi walio wengi. Nyinyi hapa Ubungo ni mashuhuda wa namna gharama za maisha zimepanda zikiwemo bei za vyakula wakati kipato cha mtanzania wa kawaida wakiwemo watumishi wa umma kipo pale pale na kwa wengine kimeshuka.
CCM ina nini cha kusherehekea kwa wiki nzima? Ni vizuri badala ya kusherehekea CCM ikatumia fursa hiyo kutoa majibu ya kina kwa umma namna viongozi na chama hicho kwa umoja wao wanavyotuhumiwa kwa ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika msururu mrefu wa kashfa kuanzia fedha za Akaunti ya Madeni Benki Kuu (EPA) hususani kuhusu kampuni ya Kagoda, Tangold, Deep Green, Meremeta nk. Ni vizuri watanzania wakaendelea kufunguka macho na kutambua unafiki huu wa CCM na viongozi wake ambao wameamua kutumia maadhimisho hayo kufanya propaganda za kurejesha imani kwa wananchi kwa kuwa mwaka huu ni kipindi ambacho tunaelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kuliko kufanya propaganda zinazohusisha matumizi ya anasa ikiwemo ya fedha za umma zaidi ya bilioni mbili (milioni zaidi ya 2000) ambazo chama hicho kinachukua kila mwezi kutoka serikali zizotokana na kodi yako na yangu badala ya kuendelea kufanya ubadhirifu wapeleke fedha hizo kuwahudumia watanzania wenzetu walioathirika na maafuriko huko Kilosa.
CCM haina cha kujivunia sasa zaidi ya kufilisika kifalsafa, kiitikadi, kimaadili, kisera na hata kiuongozi. Ushahidi wa hali hiyo ni maandiko ya mwasisi wa chama hicho hayati Mwalimu Nyerere ambaye katika moja ya kitabu chake cha mwisho mwisho aliandika wazi kwamba CCM ina kansa ya uongozi kutoka na rushwa. Katika sherehe hizi za CCM zinazoendelea mtawasikia CCM wakijivunia kuwa chama hicho kinafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea lakini ukweli ni kwamba chama hicho kimeifanya nchi kuwa tegemezi lakini kubwa zaidi ni kwamba katika kitabu hicho Nyerere alieleza wazi kwamba CCM inawadanganya watanzania kwa kuwa misingi mikuu ya Azimio la Arusha ikiwemo miiko ya uongozi ilifutwa katika maamuzi ya Zanzibar ya mwaka 1991. Hivyo, kama sehemu ya kufuata wosia wa Nyerere natoa mwito kwa watanzania kupuuza kauli za kipropaganda za viongozi wa CCM katika maazimisho yao.
Ufisadi na uongozi mbovu ndani ya mfumo wa utawala chini ya CCM hauko kwenye ngazi ya taifa tu bali umejikita katika ngazi zote za chama hicho na serikali yake. Wakati viongozi wa kitaifa wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dr Wilbroad Slaa wakipambana na mafisadi na kutetea rasilimali za nchi yetu kwenye ngazi ya taifa nyinyi mnapaswa kutimiza wajibu huo kwenye ngazi yenu.
Manispaa ya Kinondoni ambayo jimbo letu la Ubungo na kata zake tupo ni halmashauri ambayo sehemu kubwa ya viongozi wakuu wa serikali na vyama vya siasa wanaishi; lakini pia ndio halmashauri kinara kwa tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Tuhuma hizo zikimhusu pia Meya wa Halmashauri hii Bwana Salum Londa ambaye alitajwa mpaka Bungeni kuwa analindwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba katika kashfa zake.
Kati tuhuma zinazomgusa ni pamoja manispaa kuuziwa matrekta 27 ya kuzoa takataka yasiyokuwa na viwango katika kashfa inayohusisha matumizi ya zaidi zaidi ya milioni 150 wakati ambapo uchafu umekithiri katika mitaa mbalimbali ya halmashauri. Dalili za kuwepo vitendo vya ufisadi zimeonekana wazi baada ya Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo ambalo ndilo lililopitisha zabuni hiyo kugawanyika katika makundi mawili na kuendeleza malumbano bila kuchukua hatua zozote za misingi. Lakini tuhuma dhidi ya halmashauri hii haziishii kwenye zabuni pekee bali uuzaji na umilikishaji wa ardhi kinyume cha taratibu mathalani Eneo la Ufukwe wa Coco (coco beach) na umegaji wa kiwanja cha shule ya Msingi Kawe nk.
CHADEMA Mkoa wa Kinondoni tunayo taarifa ya siri yenye mihutasari na saini za viongozi wa CCM na Halmashauri ya Kinondoni ambazo zinathibitisha wazi kabisa tuhuma hizo zikitaja kwa majina na viwango vya rushwa ambazo zilitolewa ikiwemo kwa madiwani katika kashfa hizo ili kupeleka mashtaka kwa umma katika maeneo yenu.
Ndani ya halmashauri hii ambapo ubora wa elimu katika shule za umma unazidi kuporomoka; huduma za afya zinazidi kuterereka hususani katika Hospitali ya Manispaa ya Mwanyamala; maji yanazidi kuwa adimu katika maeneo mengi ya kata za Goba, Kimara nk huku wanayoyapata wanapandishiwa bei kinyemela ama wanavutiwa maji kwa gharama kutokana na tuhuma za ufisadi; itakuwa ni aibu kwa CCM Kinondoni kuitisha sherehe za wiki nzima badala ya kuboresha huduma za kijamii ambazo chini ya sera mbovu na uongozi bomu zinaguezwa kuwa bidhaa ya bei mbaya katika soko holela.
Nimalize kwa suala moja ambalo linaendelea kujadiliwa sasa kutokana na mkutano ulioitishwa na SUMATRA kupata maoni ya wadau kuhusu utoaji wa huduma ya usafiri mijini kwa kutumia makampuni na mashirika ambao kwa kiasi kikubwa ulijadili mradi wa mabasi yaendeyo kasi mkoani Dar es salaam (DART).
Nyinyi kama viongozi na sehemu ya wananchi mzingatie kuwa mradi huu unawahusu sana kwa kuwa unatarajiwa pia kupita katika barabara za Jimbo la Ubungo hususani barabara ya Morogoro. Suala hili pia linahusu mustakabali wa magari ya usafirishaji wa abiria mkoani humu ambayo yanakadiriwa kufikia elfu sita (6,000), nyuma ya magari hayo huzungumzii tu abiria wanaotumia usafiri huo bali pia suala hilo linahusu mustakabali wa ajira za madereva na makondakta wa mabasi hayo pamoja na mazingira magumu ya kazi zao.
Jambo kubwa ambalo limejitokeza katika mchakato mzima ni dhamira ya serikali kufungua milango ya uwekezaji ikiwemo kuruhusu wawekezaji kutoka nje katika sekta ya usafirishaji na kuweka viwango na vigezo ambavyo kimsingi vitaweka pembeni wenye mitaji midogo. Kama kawaida ya Serikali ya CCM na mamlaka zake sababu zinazotolewa ni za kuvutia kisera mathalani kuondoa kero za usafiri kwa kupunguza msongamano ndani ya mabasi na kupunguza foleni za magari barabarani. Hatahivyo, nyuma ya kauli hizi za kisiasa upo ukweli mchungu ambao ni muhimu watanzania wakautambua na kuujadili.
Katika mazingira hayo natoa changamoto kwa SUMATRA na DART kuweka wazi ripoti zao za tathmini (feasibility study) pamoja na mikataba yote inayohusika na mradi huu ili umma wa watanzania hususani wakazi wa Dar es salaam uweze kujadili kwa kina kwa kuwa suala hili halihusu wamiliki pekee bali pia watumiaji wa daladala ambao ni wananchi wa kawaida.
Kauli ya SUMATRA kwamba tayari kuna makampuni toka nje ambayo yameonyesha nia ya kuwekeza katika mradi husika ukichunguzwa kwa kuzingatia kasi ya sasa ya DART kutaka mfumo tofauti wa uwekezaji katika mradi huo inazua maswali mengi. Ni kisingizio hiki kiki cha kutaka mitaji toka nje ndicho kilichosababisha hasara kwa taifa kwa miundo mbinu yetu ya usafirishaji kubinafsishwa kwa bei chee katika mazingira tata bila Tanzania kunufaika na hicho kinachoitwa mitaji mikubwa kutoka nje mathalani katika sekta ya reli (RTL), ndege (ATCL), bandari (TICTS) nk. SUMARTA wanatuhakikishia vipi kuwa DART haitakuwa TRL nyingine tena ndani ya mkoa wa Dar es salaam ikihusisha usafiri ambao unatumiwa na wananchi walio wengi?
Serikali ieleze wazi namna uchumi wa wawekezaji wazawa wenye daladala, na ajira za watumishi wa daladala hususani madereva na makondakta zitavyolindwa katika mchakato mzima. Serikali inapaswa kueleza wazi pia namna ambavyo haki za abiria wa daladala zitavyolindwa ikiwemo kupatiwa huduma bora lakini zenye bei ambayo mtanzania wa kipato cha chini anayeishi Dar es salaam anaweza kumudu.
Nakubaliana na ukweli kwamba foleni katika mkoa wa Dar es salaam ni tatizo lenye athari za kiuchumi ambapo taifa hupoteza takribani bilioni nne kila saa; lakini serikali izingatie kwamba mikakati mipana inapaswa kutekelezwa kukabiliana na hali hii badala ya kufikiri kwamba uwekaji wa makampuni makubwa ya kuendesha mabasi yaendayo kasi ndio suluhisho kuu. Fikra za namna hii za kuongoza kwa dharura ndio ambazo zilitumika kutekeleza mpango wa njia tatu katika baadhi ya maeneo mfumo ambao athari zake zinaendelea kuonekana mpaka sasa. Inashangaza jiji pana lenye takribani milioni nne lenye magari binafsi laki moja tu kuwa na foleni kwa kiwango cha Dar es salaam. Hii ni dalili kwamba tatizo letu la msingi ni udhaifu katika mipango miji. Sasa badala ya kushughulikia matokeo ni muhimu kutekeleza sera zenye kukabiliana na vyanzo vya matatizo.
Hivyo mkazo uwekwe katika kutekeleza sera zenye kupanua jiji kuelekea pembezoni (satellite towns) lakini pia kuheshimu ramani za muda mrefu badala ya kuendelea na mtindo wa ujenzi holela ambao unachochea pia migogoro ya ardhi na kuliingiza taifa katika kubeba mzigo mkubwa wa fidia za mara kwa mara. Pia serikali iwekeze katika barabara za kuchuja magari (filter roads) ili kupunguza msongamano kwenye barabara kuu. Mathalani, hapa jimboni Ubungo haiingii akilini kwamba mtu ambaye yuko Mbezi Loius akitaka kwenda Mbezi Beach upande wa Jimbo la Kawe analazimika kwenda na gari mpaka Ubungo mataa halafu Mwenge ndio anarudi Mbezi. Wakati kama barabara ya kutoka Mbezi Louis kwenda Mbezi Beach moja kwa moja kupitia Goba ingejengwa kwa haraka kiwango cha lami ingepunguza msongamano wa magari. Hivyo hivyo, mwendesha gari kutoka Kibamba kwenda Tegeta analazimika kupita njia hiyo hiyo na kuongeza msongamano wakati angeweza kukatishia Mpiji Magoe au maeneo mengine kama njia hizo zingelindwa dhidi ya uuzaji holela wa viwanja na pia barabara zake zingewekwa lami.
Wakati serikali ya CCM inazungumza kujenga barabara za hewani (flying overs) na mabasi na treni ziendazo kasi (rapid transport), serikali hiyo hiyo inashindwa kuweka mazingira ya huduma za msingi za kijamii kwa wananchi. Hii ni serikali inayojiita masikini inayoendeshwa kwa kuomba omba lakini inataka kuvunja rekodi za kimataifa katika ujenzi na manunuzi kuanzia bungeni, ndege ya rais, rada, majengo pacha ya Benki Kuu, nyumba ya gavana na sasa usafiri katika mkoa wa Dar es salaam.
Hali hii ya kushindwa kutambua vipaumbele kama taifa ndio inafanya kodi za wananchi wa vijijini kutokurejeshwa kuhakikisha maendeleo ya uwiano na hivyo kujenga matabaka yanayosababisha watanzania wengi zaidi kukimbilia Dar es salaam na kusababisha msongamano kuzidi kuongezeka. Kwa hiyo kuleta wawekezaji toka nje, na kuleta mabasi yaendayo kasi havitaweza kuondoa msongamano kama vyanzo vya msingi vya msongamano havitashughulikiwa kisera, kimfumo na kiuongozi.
Mwelekeo mzima wa mradi huu unadhihirisha udhaifu katika mfumo wetu wa utawala ambao serikali kuu na mamlaka zake inahodhi michakato yote ya msingi hata ile ambayo halmashauri zilipaswa kushirikishwa na kuchukua nafasi ya kuwa mstari wa mbele katika kutoa mwelekeo kama suala hili la usafiri katika mkoa wa Dar es salaam na manispaa zake. Lakini ni ishara pia ya uongozi wa muda mrefu wa CCM unaanzisha mipango tofauti tofauti inayoshindwa baada ya muda mfupi. Kwa hali hii badala ya CCM kusherehekea itumie fursa hii kuwaeleza watanzania ni nini kimefilisi kampuni ya Usafirishaji Dar es salaam (UDA) na pia waeleze wazi ilipokwenda michango iliyotolewa na wananchi mkoani Dar es salaam kwa ajili ya mradi wa mabasi ya wanafunzi ambao fedha zake inatuhumiwa kuwa zimeishia mikononi mwa vigogo wa UVCCM wakati walengwa wanaendelea kupata adha ya usafiri.
Katika mazingira haya ni muhimu kuhamasisha mabadiliko ya kweli katika taifa kwa wananchi kuchagua viongozi mbadala. Mwaka 2005 Mkoa wa Dar es salaam uliwaangusha watanzania kwa kuwa pamoja na kuwa na wasomi wengi, wananchi wenye kufikiwa zaidi na vyombo vya habari na pia wananchi ambao wanaelezwa kuwa na elimu ya kuridisha ya uraia ukilinganisha na wa vijijini; lakini mkoa huu wabunge wake wote 7 ni CCM na madiwani wake wote wa kuchaguliwa na wa viti maalumu katika manispaa zote tatu ni CCM. Wananchi wa Dar es salaam wakiwemo wajanja wa Kinondoni wanafurahia hoja za wabunge wa upinzani kama Dr Wilbroad Slaa bungeni ama kazi ya madiwani wa upinzani wanaongoza halmashauri kama kule Karatu lakini hawajui kwamba viongozi hawa mbadala wametokana na wenzao wa vijijini ambao waliamua kuunganisha nguvu katika uchaguzi uliopita kwa kupiga kura kwa wingi lakini pia kushiriki kulinda ushindi wao mpaka hatua ya mwisho. Natarajia mafunzo haya yatawawezesha kuwaunganisha wananchi wa Jimbo la Ubungo kurekebisha kasoro hizo na kusimamia mabadiliko kwani katika miji mingi mikubwa ya Afrika wananchi wanaunga mkono vyama mbadala.
Mafunzo haya yawawezesha kwenda kwa umma kuwaeleza udhaifu wa uongozi ulioko madarakani na ufisadi uliokithiri lakini msiishie kukosoa tu bali muweze kueleza kwa kina sera mbadala za CHADEMA na kuondoa upotoshaji unaofanywa kuhusu sera hizo.
Mathalani waelezeni watu kuhusu sera ya mfumo mpya wa utawala ya CHADEMA maarufu kama sera ya majimbo. Napenda kuchukua fursa hii kuwaeleza kwa maneno machache sana namna sera hii inavyoweza kuwa mkombozi kwa watanzania kwa kutoa mamlaka zaidi kwa umma katika kuleta maendeleo.
Kwa kutumia falsafa ya CHADEMA ya nguvu ya umma sera hii inalenga kupeleka mamlaka kwa umma ili kuepusha masuala yanayowahusu wananchi kuchelewa kushughulikiwa kwa urasimu wa serikali kuu badala yake serikali za majimbo na za mitaa zitapewa mamlaka zaidi kutatua kero za wananchi.
Sera ya mfumo mpya wa utawala inalengo la kupeleka madaraka zaidi kwa wananchi katika kuchagua viongozi wetu. Kama Tanzania ingekuwa inaongozwa kwa sera hii leo hapa Halmashauri ya Kinondoni msingekuwa na mkuu wa wilaya, maana CHADEMA imeshatangaza kufuta vyeo hivi. Haiwezekani kuwa na mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri na meya wa manispaa wote wakifanyakazi zinazokaribiana hali inayosababisha mwingiliano wa madaraka. Vyeo hivi vya mkuu wilaya na vya mkuu wa mikoa vilikuwa vikitumiwa na serikali ya mkoloni wakati wa ‘wagawe uwatawale’, wakati huo uteuzi ukifanywa na gavana. Ni mfumo huo huo umebakizwa leo ambao Rais anateuwa watendaji wake mpaka serikali za mitaa ambao hawawajibiki kwa wananchi wala serikali za mitaa bali serikali kuu. Madaraka haya ya serikali kuu yanaenda mbele zaidi mpaka katika uteuzi wakurugenzi wa halmashauri badala ya uteuzi wa watumishi hawa kufanywa na halmashuri zenyewe.
Pia, CHADEMA inataka mameya na wenyeviti wa halmashauri wachaguliwe na wananchi moja kwa moja badala ya kuchaguliwa na madiwani pekee. Kama Halmashauri ya Kinondoni ingeongozwa kwa sera hii ya CHADEMA basi msingekuwa hapa na Meya Londa ambaye hawajibiki moja kwa moja kwa wananchi kwa kuwa wananchi wote wa manispaa hawakushiriki katika kumchagua. CCM haiwezi kuteleza mabadiliko makubwa kama haya kwa hofu ya kupoteza vyeo vyao lakini pia izingatiwe kuwa mabadiliko haya yanahitaji katiba mpya suala ambao serikali wanayoiongoza imeshatangaza kuwa haikusudii kulifanya.
Hali hii inatufanya tukumbuke; mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale. Kwa falsafa ya chukua chako mapema; Tanzania yenye neema haiwezekani. Tuunganishe nguvu kubadili mfumo wa utawala; mabadiliko yanawezekana. Tunahitaji uongozi wenye dira na uadilifu wa kulikomboa taifa na tunaweza kufanya hivyo kwa kubadili mfumo wa utawala na kuiwezesha CHADEMA kuongoza dola ama kupunguza hodhi ya chama kimoja bungeni na kwenye halmashauri za wilaya/manispaa ikiwemo ya kwetu ya Kinondoni.
Nimefungua rasmi mafunzo haya na Asante sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment