Wednesday, January 27, 2010

Marekebisho ya Sheria za uchaguzi yaondoe kasoro kwenye upigaji kura, kuhesabu na utangazwaji wa matokeo

Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ni muhimu kama taifa tuondoe kasoro kwenye upigaji kura, kuhesabu na utangazwaji wa matokeo. Methodolojia na taratibu zinazosimamia upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo vimefafanuliwa katika Sheria ya Uchaguzi na. 1 ya mwaka 1985 kutoka kipengele cha 61(1) mpaka 87 na taratibu zingine za uchaguzi zinazotolewa. Mambo ya kufanya na kutofanya katika uchaguzi yalifafanuliwa katika Taratibu za Uchaguzi za Mwaka 2005 sehemu ya IV kipengele cha 39 mpaka 61. Kwa upande mwingine Sheria ya Uchaguzi na. 1 ya mwaka 1985 kipengele cha 61 mpaka 69 na Taratibu za Uchaguzi za mwaka 2005 kifungu cha 45 mpaka 52 vinaelekeza taratibu zinazopaswa kufuatwa katika vituo vya kupigia kura. Hata hivyo, zipo kasoro kwenye mchakato mzima wa upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo ambazo ni muhimu zikajadiliwa.

Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010. Hatahivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe. Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi. Katika makala hii tutajadili suala moja la hoja na haya ya kuondoa kasoro kwenye upigaji kura, kuhesabu na utangazwaji wa matokeo.

Lipo tatizo la wananchi hususani wanachama wa vyama vya upinzani kunyimwa ama kuogopeshwa kwenda kupiga kura. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na hata katika chaguzi za marudio kati ya mwaka 2006 na 2009 palikuwa na utaratibu wa majina kubandikwa nje ya vituo ambapo katika maeneo mbalimbali baadhi ya wananchi wengi wao wakiwa ni wanachama wa vyama vya upinzani walizuiwa kupiga kura pamoja na kuwa na vitambulisho vya kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura(DKWK) ama kwa kukosa majina yao nje ya vituo au taarifa zao kuwa na mapungufu au kutokuwepo kabisa katika daftari. Ishara zinaonyesha kuwa pengine huu ulikuwa ni mkakati rasmi kwa kuwa siku kadhaa kabla ya uchaguzi watendaji wa chama tawala hususani wajumbe wa nyumba kumi walipita na kuandikisha namba za wapiga kura katika maeneo yao. Kwa kuwa wananchi wengi walikuwa na elimu finyu ya uraia na kwamba katika baadhi ya maeneo wajumbe hawa wanasikilizwa sana na/au hata kuogopwa, wapiga kura wengi waliorodheshwa na hata wengine kutishwa kuwa kura zao zitajulikana na hivyo wasipoipigia kura CCM watashughulikiwa. Vitisho hivi vilipata nguvu kutokana na utaratibu wa kuchukuliwa namba za shahada za wapiga kura na wasimamizi wa vituo wakati wa kupiga kura. Hii ilifanya uchaguzi usiwe huru.

Pia, vyama vingi havikuweza kuweka mawakala kwenye vituo vyote kutokana na changamoto ya rasilimali na pia mawakala hawakuwa na mafunzo yanayowiana, kila chama kilitoa mafunzo kwa mawakala wake kwa utaratibu wake kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Tume. Hivyo, kulikuwa na utofauti baina ya wasimamizi/wasaidizi wa vituo wa Tume na mawakala wa vyama katika utendaji wao.

Pia, zipo kasoro za moja kwa moja ambazo hujitokeza katika kuhesabu na kutangaza matokeo. Mathalani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 Jimbo la Ubungo matokeo ya ubunge yalitangazwa kwa shuruti bila kutangaza na kujumlisha kwa pamoja matokeo ya kituo hadi kituo hali iliyoashiria kuwa matokeo ya Ubunge yalikuwa na utata. Kutangaza huku kwa nguvu ilikuwa ni mkakati wa kutaka matokeo hayo yasihojiwe kama ilivyokuwa katika matokeo ya urais ambayo yalichelewa kutangazwa kutokana na kukutwa na mapungufu mengi. Kwa hali iliyodhihirisha wazi kuwa matokeo yalipikwa, waliopiga kura za Ubunge walikuwa 185,684 wakati waliopiga kura za Rais walikuwa 152,525 na hivyo kufanya tofauti ya kura za Ubunge na urais kufikia 33,159. Katika hali ya kawaida na katika uchaguzi uliofanyika kwa wakati mmoja ilikuwa ni vigumu kwa tofauti kubwa ya kura kiasi hiki. Na hata kama wananchi wangekuwa hawapendi kupiga kura za rais kwa kuwa mpiga kura alikuwa akipewa karatasi zote tatu kura hizi zilipaswa kuwepo katika kura zilizoharibika kitu ambacho hakikutokea. Mfano wa Jimbo la Ubungo unaibua hoja ya utofauti mkubwa baina ya jumla ya wapiga kura katika ubunge na urais katika majimbo mbalimbali Tanzania, suala hili linapaswa kujadiliwa. Ufanyike uchambuzi huo kujua utofauti katika kila jimbo ili kuweza kubaini chanzo cha hali hiyo na kukabilina nacho.
Katika kipindi cha mwaka 2006 mpaka 2009, kumeonekana tatizo lingine ambalo nalo linahitaji mjadala wa kina; mwitikio mdogo wa wapiga kura katika chaguzi za marudio. Mathalani chaguzi ndogo za ubunge: Tunduru (48%), Kiteto (47%), Tarime(46%) na Mbeya Vijijini(35%). Kwa upande wa chaguzi ndogo za madiwani hali ilikuwa mbaya zaidi katika baadhi ya kata mathalani: Upanga Mashariki-Dar es salaam (7%) na Sombetini-Arusha(14%) nk. Suala linahitaji kufanyiwa utafiti na chombo zaidi ya kimoja, ili kuwianisha matokeo ya sababu na mazingira yatayoanishwa. Maelezo ya wananchi mbalimbali ni kwamba ‘kadi za kupigia kura zinanunuliwa ama kuchukuliwa kabla ya kwenda kupiga kura’. Uchunguzi wa kina utasaidia kubaini tatizo hili ambalo linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa misingi ya uhuru na haki katika chaguzi zinazofuata.

Ikumbukwe kuwa Tarehe 11 Disemba 2009 Serikali ilichapisha kwenye gazeti la serikali miswada miwili yenye kulenga kufanya marekebisho katika sheria za uchaguzi na kutangaza kupitia vyombo vya habari tarehe 21 Disemba 2009 maudhui ya miswada hiyo. Miswada hiyo imeshajadiliwa na kamati husika za Bunge na inatarajiwa kujadiliwa ndani ya mkutano wa Bunge unaonza mwezi huu.

Hata hivyo, marekebisho hayo yaliyopendekezwa katika miswada hiyo hayajagusa kikamilifu maeneo yenye kasoro yanayohusu upigaji kura, kuhesabu na utangazwaji wa matokeo. Eneo pekee linaloguswa katika marekebisho ni lile linalohusu zoezi la uandikishaji wapiga kura, ambapo imependekezwa katika ibara ya 7 kuwa na fungu jipya la 15A katika sheria linatoa nafasi kwa vyama vya siasa kuteua mawakala wakaokuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura kama ilivyo wakati waupigaji kura.

Hivyo ni muhimu mjadala ukapunuliwa kuwezesha kasoro kushughulikia likiwemo tatizo la kupungua kwa idadi ya wapiga kura. Zipo nchi ambazo sheria ya uchaguzi inalazimisha wananchi kupiga kura ili kuondokana na tatizo la kupungua kwa idadi ya wananchi wanaojitokeza kupiga kura. Mazingira ya kisheria yanaweza kuweka bayana kwamba uhalali wa kiongozi kutangazwa mshindi unategemea asilimia ya wananchi waliopiga kura. Kiongozi aliyechaguliwa na wananchi ambao hawafiki hata asilimia kumi ya wapiga kura waliojiandikisha uhalali wake uko mashakani.
Sheria na taratibu ziwezeshe pia kuwe na mafunzo ya pamoja baina ya mawakala wa vyama na wasimamizi/wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura. Hii ihusishe pia serikali kugharamia mawakala wa vyama. Ni muhimu kwa Tume na wadau wengine kuwatambua mawakala wa vyama kama sehemu ya msingi ya mchakato mzima wa uchaguzi hivyo mafunzo yao yafanyike sanjari na mafunzo ya wasimamizi/wasimamizi wasaidizi wa vituo. Hii ihusishe pia kuwezesha upatikanaji wa rasilamili kwa ajili ya kugharamia mawakala.
SEHEMU YA MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA MAJIRA TOLEO LA TAREHE 25 JANUARI 2010

No comments: