Friday, January 29, 2010

Uhuru wa vyombo vya habari na utoaji wa elimu ya uraia vipewe kipaumbele katika marekebisho ya sheria za uchaguzi

Katika uchaguzi mkuu 2005 vyombo vya habari pamoja na mapungufu katika maeneo kadhaa vilifanikiwa kutoa taarifa kwa wapiga kura hususani kuandika habari za matukio mbalimbali ya kiuchaguzi. Hata hivyo havikufanikiwa kwa kiasi cha kutosha kutoa elimu ya uraia na kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mwelekeo wa uchaguzi ikiwemo kufichua ufisadi/rushwa wakati wa uchaguzi. (habari pekee kubwa kuhusu rushwa katika uchaguzi ni ile iliyoandikwa na Gazeti la RADI toleo la April 27 mpaka Mei 6, 2005 ambayo lilichambua kwa kina kwamba Mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete ameleta kwa siri toka Oman mamilioni ya dola za mafuta kwa ajili ya kampeni zake. Habari ambayo haikukanushwa na timu ya Kikwete badala yake toleo la gazeti husika lilinunuliwa kwa bei ya jumla na kuisha mitaani mapema).

Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010. Hatahivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe. Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi. Katika makala hii tutajadili suala moja la haja uhuru wa vyombo vya habari na utoaji wa elimu ya uraia kupewa kipaumbele katika marekebisho ya sheria za uchaguzi.

Kwa ujumla Vyombo kadhaa vya habari vilikiuka Maadili ya Vyombo vya Habari katika Uchaguzi ambavyo vyombo husika vilikubaliana kuyafuata ikiwemo ushabiki, upotoshaji na kutotoa nafasi sawa baina ya wagombea mbalimbali ( Ripoti ya Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari wakati wa Uchaguzi iliyotolewa na MISA-TAN na Ripoti ya Uchaguzi Mkuu iliyotolewa na TEMCO zimefafanua ukiukwaji huo). Hata hivyo, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010 nafasi ya vyombo vya habari katika siasa inaacha mengi kutokana na kuzuka kwa uandishi wa kushafuana na kushambuliana.

Midahalo ya wagombea urais kupitia vyombo vya habari ilipangwa mara tatu lakini haikuweza kufanyika kutokana na mgombea wa CCM kukataa kushiriki bila sababu kutolewa; hii imefanya historia kubaki kwamba mdahalo wa wagombea urais uliwahi kufanyika katika uchaguzi wa mwaka 1995 tu.

Ikumbukwe kuwa Tarehe 11 Disemba 2009 Serikali ilichapisha kwenye gazeti la serikali miswada miwili yenye kulenga kufanya marekebisho katika sheria za uchaguzi na kutangaza kupitia vyombo vya habari tarehe 21 Disemba 2009 maudhui ya miswada hiyo. Hata hivyo, marekebisho hayo yanayopendekezwa hayajagusa kikamilifu maeneo yanayoweza kuongeza mchango wa vyombo vya habari katika uchaguzi.

Masuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na Serikali, Tume ya Uchaguzi, Vyama Vya siasa na Wadau wengine kama sehemu ya marekebisho ya kisheria yanayokusudiwa kufanyika kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010:

Utaratibu wa kikanuni na kisheria uwekwe kusimamia matangazo katika vyombo vya habari; katika mazingira ya matangazo ya kulipia ya kisiasa ni vyema ukatolewa utaratibu wenye usawa. Gharama za malipo lazima ziwiane baina ya vyama mbalimbali pamoja na muda wa matangazo kutangazwa. Kama haiwezekani kuweka mfumo wenye usawa katika eneo hili basi ni vyema sheria ikakataza matangazo ya kisiasa ya kulipia kama ilivyo katika baadhi ya nchi.

Nafasi ya vyama katika vyombo vya habari itolewe kwa usawa wakati wote, si wakati wa uchaguzi pekee; muda wa bure unaotolewa kwa vyama vya siasa na vyombo vya habari hususani vya umma uendelee kutolewa kwa vyama hata baada ya uchaguzi. Uwepo uratibu wa kisheria wa kutoa idadi ya wastani wa dakika kwa kila chama kwa mwezi katika vyombo vya habari vya umma.

Vyombo vya habari viwe na mkakati na mwelekeo wa kuibua masuala muhimu kwa wananchi na rushwa za kisiasa wakati wa uchaguzi; pamoja na kwamba vyombo vya habari vimefanikiwa kufanya rushwa/ufisadi kuwa ajenda ya msingi inayojitokeza mara kwa mara wakati wa kawaida, vyombo vya habari havijafanikiwa kuibua masuala ya rushwa zinaozoendelea wakati wa uchaguzi. Hili ni eneo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi zaidi.

Sheria zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo wakati wa uchaguzi zinapaswa kufanyiwa marekebisho; baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria inayolipa Bunge madaraka ya kumtaka mwandishi atoe kwa bunge chanzo chake cha habari; Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 1945 kifungu 114(1) inayotoa mamlaka kwa mahakama kulazimisha chombo cha habari kutaja kufichua chanzo chake cha habari; Sheria ya Usalama wa Taifa ya Mwaka 1976 kipengele cha 15(2) inayotoa hukumu kwa yoyote anayekataa kutoa taarifa kwa usalama wa taifa; Sheria ya Magezeti ya Mwaka 1976 kinachotoa mamlaka ya kufungia chombo cha habari (kwa kutumia sheria hii gazeti la Tanzania Daima lilifungiwa kwa siku tatu wakati wa uchaguzi mkuu 2005). Tumeshuhudia hivi karibuni magazeti ya Kulikoni na Leo Tena yakifungiwa kwa kutumia sheria hiyo hali inayotoa ishara mbaya tunapoelekea uchaguzi mkuu. Hivyo, za miaka mingi ambazo zilianzishwa na wadau mbalimbali kutaka sheria ya uhuru wa taarifa na sheria ya vyombo vya habari ni muhimu zikapewa msukumo wa ziada ili miswada ya sheria hizo mbili itolewe na kupitishwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kwa upande mwingine, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Taratibu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi ziliipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kama chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa elimu ya mpiga kura na kwamba asasi/taasisi yoyote ilipaswa kuomba kibali/ridhaa ya Tume kutoa elimu ya mpiga kura.

Elimu duni ya uraia na ya kisomo miongoni mwa wananchi ni moja ya kasoro ambayo imekuwa ikijitokeza katika uchaguzi. Kiashiria cha haraka ikiwa ni jinsi ambavyo walikubali kurubuniwa na kunyanyaswa kwa sababu za kisiasa. Elimu ya mpiga kura badala ya elimu ya uraia iliyopana ilitolewa na tume na wadau wengine hususani asasi zisizo za kiserikali(AZISE) kwa kiasi ambacho hakikufikia wapiga kura walio wengi na ilichelewa kuanza kutolewa. Ukosefu wa elimu ya kisomo hususani kutokujua kusoma na kuandika ulitumika kuwakosesha wananchi wasiokujua hakusoma na kuandika uhuru wao kwa ‘kupigiwa kura’ kwenda chama tawala kupitia mikakati mbalimbali.

Katika muktadha huo masuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na Serikali, Tume ya Uchaguzi, Vyama Vya siasa na Wadau wengine kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuzingatiwa pia katika marekebisho ya sheria husika yanayokusudiwa.

Tatizo la wananchi wengi kutokujua kusoma na kuandika linapaswa kujadiliwa na kushughulikiwa kwani linaathiri uchaguzi huru na haki wa viongozi. Uwepo wa watu wengi wasiojua kusoma na kuandika unaathiri uhuru wa kupiga kura na umetumika kuhujumu upinzani wakati wa uchaguzi. Serikali kwa miaka mingi imeshindwa kuwawezesha watanzania walio wengi hususani vijijini kujua kusoma na kuandika na kuitumia fursa hii kushinda uchaguzi. Hivyo kuna haja ya kujadili kama kuna sababu ya wananchi wasiojua kusoma na kuandika kupiga kura kama uhuru wao utaendelea kutumika visivyo na hivyo kupoteza haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka. Hivyo kama serikali ina nia njema ya kisiasa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata uhuru na haki ya kupiga kura ni lazima kuweka mkazo kuhakikisha kuwa wananchi wote wanajua kusoma na kuandika.

Ni lazima kwa serikali, vyombo vya habari, asasi za kiraia na vyama vya siasa kutoa elimu ya kutosha ya uraia ili kuwezesha uchaguzi wenye amani ulio huru na haki. Mkazo uwekwe katika kuhakikisha elimu ya uraia inatolewa kwa wananchi walio wengi kama mchakato wa mapema na endelevu bila kusubiri wakati wa uchaguzi pekee. Elimu hii ya uraia ijumuishe pia elimu ya siasa, elimu ya mpiga kura, uzalendo, haki na wajibu wa mwananchi na haki za binadamu kwa ujumla. Ni muhimu kutambua kuwa ufahamu wa wananchi kuhusu michakato ya kisiasa katika mfumo wa vyama vingi ni muhimu kwa uchaguzi wa haki na kushamiri kwa demokrasia. Hii ni pamoja na kuboresha mitaala ya elimu ya uraia katika shule na vyuo iweze kukidhi mahitaji kwa pamoja na mambo mengine kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa. Pia wananchi wawezeshwe kutambua mchango wa upinzani na mfumo wa vyama vingi katika kuchochea maendeleo ikiwemo kwa kuboresha uwajibikaji wa viongozi walioko madarakani.

Masuala haya yenye kuweka uwanja sawa wa ushindani katika uchaguzi wa demokrasia ya vyama vingi yanahitaji jambo moja kuweza kuzingatiwa: dhamira ya kisiasa ya utawala ulioko madarakani. Pasipo na dhamira; panahitajika mjadala wa umma utakaowezesha kuunganisha nguvu za kidemokrasia na kimaadili ili kudai na kushawishi mabadiliko ya sheria za uchaguzi na mazingira ya kisiasa. Kuna haja ya serikali kufanya marekebisho mapana zaidi au vyama vya siasa na wadau wengine waelekeze jitihada bungeni na mahakamani kudai mabadiliko ama kufutwa kwa vipengele vya sheria nyingine ambavyo vinafanya mazingira ya kisiasa na kiuchuguzi yanayokwaza uchaguzi huru na wa haki.
SEHEMU YA MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA TOLEO LA TAREHE 27 JANUARI 2010

2 comments:

Anonymous said...

JJ,
Kuna mahali nimesoma hapo juu. Naona kuna haja ya kusaidiwa hili gazeti la RADI liendelee kuwepo. Naona linatoka kwa kusuasua, ninyi wenye sauti za ukweli hali lisaidieni gazeti hili. Naona kama ni gazeti lenye malengo lakini halina uwezo kwasababu halina pesa za mafisadi.

Anonymous said...

JJ,
Kuna mahali nimesoma hapo juu. Naona kuna haja ya kusaidiwa hili gazeti la RADI liendelee kuwepo. Naona linatoka kwa kusuasua, ninyi wenye sauti za ukweli hali lisaidieni gazeti hili. Naona kama ni gazeti lenye malengo lakini halina uwezo kwasababu halina pesa za mafisadi.