Friday, January 29, 2010

Mchakato wa Uboreshaji Daftari na Uhakiki wa Wapiga kura urekebishwe

Katika uchaguzi orodha ya wapiga kura ni kitu muhimu. Katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hapakuwa na orodha ya kudumu ya wapiga kura badala yake wananchi waliandikishwa karibu na uchaguzi na kupewa shahada za mpiga kura badala ya kadi za kudumu. Ili kuruhusu mchakato wa kuanzisha Daftari na Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu 5(3) na kipengele cha 12 cha sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 vilifanyiwa marekebisho January 2000. Lakini hili halikufanyika na matokeo yake DKWK halikuweza kutumika katika uchaguzi wa 2000; hata hivyo June 9, 2004 Bunge la Muungano lilifanya marekebisho mbalimbali ambayo yaliwezesha mchakato wa kuandaa DKWK kuanza. Mchakato wa kuandikisha wapiga kura kwa upande wa Tanzania bara ulianza 7 Oktoba 2004 na kukamilika 18 April 2005.
]
Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010. Hatahivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe. Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi. Katika makala hii tutauchambua mchakato wa uboreshaji na uhakiki wa daftari la kudumu la wapiga kura pekee.

Ni muhimu nikiri kuwa daftari la kudumu la wapiga kura limeongeza ufanisi kiasi katika mchakato wa uchaguzi. Wananchi wengi hususani vijana walijitokeza kujiandikisha na wengi wao kwa matarajio kuwa kadi ya mpiga kura inaweza kutumika kama kitambulisho. Uwezekano wa watu kupiga kura zaidi ya mara moja ulipunguzwa isipokuwa kwa Zanzibar ambapo ulivurugwa na unaendelea kuvurugwa.

Lakini ni muhimu zaidi tuchambue mapungufu ya chaguzi zilizopita hatua kwa hatua na kuhusisha na marekebisho yanayopendekezwa ili kubaini kama mabadiliko yanayokusudiwa yanakidhi haja ya kuondoa kasoro husika.

Mwaka 2004 yapo mapungufu katika mchakato wa uandikishaji; mapungufu ambayo yamejirudia tena katika mchakato wa uboreshaji wa daftari katika awamu ya kwanza ya pili miaka ya 2007 na 2009.

Vituo vya kujiandikisha vilikuwa mbali na hivyo baadhi ya watu kushindwa kuandikishwa.(Vituo vilikuwa vichache hata kuliko vituo vya kujiandikisha vya mwaka 2000). Pia wananchi wa maeneo mapana waliandikishwa katika eneo moja na hivyo kufanya utaratibu wa kugawa vituo na wananchi kufahamu vituo vyao kuwa mgumu.(Mifano halisi imetolewa hata katika ripoti ya uchaguzi ya TEMCO, 2006).

Ushiriki wa vyama vya siasa katika kuhakikisha kuwa mawakala wa vyama wanakuwepo siku zote za uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura(DKWK) ulikuwa mdogo. Pia vifaa vilikosekana katika baadhi ya maeneo kabla ya siku ya mwisho ya uandikishaji na hivyo wengine kukosa fursa ya kuandikishwa. Zoezi la kuhakiki daftari nalo lilikuwa duni. Vyama vilipewa DKWK kamili siku chache kabla ya kwenda kupiga kura na taratibu hazikutoa fursa ya wapinzani kuhakiki. Wananchi hawakujitokeza kwa wingi kwenda kuhakiki majina yao baada ya daftari la awali la wapiga kura(provisional voter registry) kutolewa. Hivyo watu mbalimbali wengi wao wakiwa wanachama wa upinzani walinyimwa kuandikishwa na wengine waliofamika kuwa ni wana CCM hata wasio na sifa waliandikishwa hasa Zanzibar. Mapungufu haya yaliyojitokeza wakati wa uandikishaji mwaka 2004 mpaka 2005, hayakufanyiwa kazi kikamilifu wakati wa zoezi la Uboreshaji wa Awamu ya Kwanza lililofanyika kati ya Oktoba 2007 na Disemba 2008.

Tarehe 11 Disemba 2009 serikali imechapa muswada wa marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambao umegusa pia marekebisho yanayohusiana na mchakato wa daftari la kudumu la wapiga kura. Baadhi ya mapungufu yanayokusudiwa kurekebishwa katika muswada huo ni pamoja na NEC kutokuwa na madaraka ya kuteua waratibu waandikishaji wa mikoa. Pia kushughulikia suala la kipindi cha kuboresha daftari la kudumu la wapigakura kutotajwa bayana katika sheria na sheria kutoruhusu baadhi ya watendaji wa tume kuingia katika vituo vya kupigiakura ili kufuatilia zoezi la upigaji kura. Ibara ya 6 imependekeza marekebisho katika fungu la 15 la sheria, ili kuweka bayana kipindi cha kufanya uboreshaji wa daftari la taifa la kudumu la wapiga kura kuwa mara mbili katika Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata. Aidha, sehemu hiyo inasisitiza kwamba, kwa lengo la kuongeza uwazi katika zoezi la uandikishaji wapiga kura, imependekezwa katika ibara ya 7 kuwa na fungu jipya la 15A katika sheria linatoa nafasi kwa vyama vya siasa kuteua mawakala wakaokuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura kama ilivyo wakati waupigaji kura.

Hata hivyo; kasoro za msingi kuhusu uboreshaji na uhakiki wa wapiga kura bado hazijashughulikiwa kikamilifu kisheria katika muswada uliopendekezwa na hata kiuendaji katika zoezi la uboreshaji linaloendelea hivi sasa. Ili kurekebisha hali hiyo asuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na Serikali, Tume ya Uchaguzi, Vyama Vya siasa na Wadau wengeni kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010(hususani katika Uboreshaji wa Daftari katika Awamu ya Pili DKWK unaondelea na unaotarajiwa kukamilishwa mapema mwaka 2010).

Kwa ujumla daftari la kudumu la wapiga kura(DKWK) liboreshwe zaidi. Uanzishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unasaidia kupunguza gharama za uandikishaji wa wapiga kura mara kwa mara. Pia uwepo wa kumbukumbu za kudumu unasaidia kuondoa utata wa upotevu au kuharibika kwa nyaraka. Hata hivyo daftari hili linapaswa kuhakikiwa upya kwa kuwashirikisha kikamilifu wananchi na wadau muhimu hususani vyama vya siasa mapema sana kabla ya uchaguzi mkuu ujao kukaribia. Pia uwepo mfumo na mtandao wa kudumu mpaka ngazi za wilaya wa kuendelea kuingizia takwimu za wapiga kura wapya na kuondoa za ambao wamepoteza sifa za kupiga kura katika mahali husika. Orodha za wapiga kura zipangwe upya ili ziweke makundi ya wapiga kura kwa kuzingatia maeneo yao ya makazi mathalani mitaa midogo na vitongoji ili mpangilio uwezeshe daftari litumike katika chaguzi za ngazi ya chini. Kila raia atambue kuwa ana haki na wajibu wa kujiandikisha na kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura. Nichukue fursa hii kuhimiza wapiga kura wapya kwenda kujiandikisha na wale waliopoteza kadi zao ama kuhama maeneo yao nao kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari linaloendelea katika maeneo mbalimbali. Kwa upande wa Dar es salaam zoezi hilo kwa mujibu wa ratiba tuliyopatiwa na Tume litafanyika kuanza 22 Machi mpaka 27 Machi.

Pia uwepo utaratibu wa kuwezesha vyama kupata rasilimali ikiwemo mafunzo ili kuhakikisha kwamba mawakala wa vyama wanasimamia kikamilifu na kuhakiki zoezi la uandikishaji. Aidha mkazo uwekwe kwa vyama vya siasa ili kuhakikisha vinashiriki kutoa elimu ya uraia na ya mpiga kura ili kuhamasisha wanachama wao na wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Kadhalika pawepo na utaratibu utakaowezesha vyama vya siasa kupata DKWK wakati muafaka linapohitajika badala ya kutokupewa daftari hilo mpaka uteuzi wa wagombea unapofanyika (Rejea Tarime, Mbeya Vijijini, Busanda nk). Izingatiwe kuwa Daftari la Wapiga Kura, si nyaraka ya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi tu bali ni nyaraka ya mpiga kura na wadau wengine ikiwemo waangalizi wa uchaguzi. Hivyo, Tume inapaswa kuwa na mfumo wa kuwezesha daftari hilo kuwa wazi kwa pamoja na mambo mengine kuliweka katika tovuti (website) kila uboreshaji unapofanyika. Mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu na uhakiki wa wapiga kura ujadiliwe kama moja ya misingi muhimu ya marekebisho mapana ya kisheria kuwezesha uchaguzi huru na haki nchini ili kupata uongozi bora.
SEHEMU YA MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA NIPASHE TOLEO LA TAREHE 27 JANUARI 2010

No comments: