Katika kipindi cha karibuni kumeibuka kauli za mara kwa mara kutoka serikalini zikilenga kuwaonya na kuwatisha mabalozi na jumuia ya kimataifa katika muktadha wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kauli nzito zaidi zikiwa zimetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe Bungeni Dodoma mwezi Julai mwaka 2009 na kauli kama hiyo imerudiwa tena kwa maneno makali na Rais Kikwete mwanzoni wa mwezi huu wa Januari 2010.
Kauli hizi zinapaswa kujadiliwa na kutafakariwa na duru za kidiplomasia na kutolewa kauli mbadala kwa lengo la kudumisha mahusiano mema wakati huo huo kulinda haki kwa kurejea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mikataba Mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa nafasi yangu ya Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa CHADEMA nimeshangazwa na Hotuba ya Rais Kikwete ya Sherehe kati yake na Mabalozi ya mwaka mpya(New Year Sherry Party) ya tarehe 7 Januari 2010 ambayo badala ya Rais kuwaeleza utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwao kwenye hotuba yake ya mwaka katika tukio kama hilo mwaka 2006 mara baada ya kuingia madarakani ametumia nafasi hiyo kutoa kauli zenye kuonyesha vitisho kwa mabalozi.
Ikimbukwe kwamba mara baada tu ya kuingia madarakani, Rais Kikwete alitoa ahadi mahususi kwa mabalozi kwamba serikali yake ingefanya mabadiliko kwa lengo la kuweka uwanja sawa wa kisiasa, kudumisha demokrasia na majadiliano na vyama mbalimbali. Pia alitoa kwao ahadi mahususi za kubadili mazingira ya kiuchumi na kiuwekezaji na kuweka utaratibu wa kunufaisha watanzania walio wengi hususani masikini. Kwa upande wa diplomasia za kikanda na kimataifa, Rais Kikwete alitoa ahadi ya Tanzania kuwa kinara katika utatuzi wa migogoro eneo la maziwa makuu (great lakes) na Umoja wa Mataifa(UN).
Miaka minne imepita lakini Rais Kikwete na Serikali yake hawajatekeleza kikamilifu ahadi hizo kwa watanzania ambazo walizitoa mbele ya mabalozi; badala yake Rais Kikwete anatoa kauli mbadala zenye mwelekeo wa vitisho kwa mabalozi.
Nakubaliana na ukweli kwamba ni muhimu kwa mabalozi kuzingatia Mkataba wa Vienna na kwamba hawapaswi kuwachagulia watanzania mtu au chama tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; lakini ni kinyume kabisa kwa mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kuwaziba midomo mabalozi wasitoe kauli kwenye masuala yanayogusa demokrasia na maendeleo katika muktadha wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Rais Kikwete na serikali yake wakumbuke kwamba ni mabalozi hawa hawa na washirika wa kimaendeleo ndio ambao serikali imewaomba fedha na kupewa rasilimali za kutekeleza mipango mbalimbali mathalani mradi wa Deeping Democracy Programme pamoja na Mfumo wa Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2010(Busket Fund); miradi ambayo yote inaratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa(UN) kwa kushirikiana washirika mbalimbali wa kimaendeleo zikiwemo balozi mbalimbali.
Hata hivyo, mpaka sasa miezi michache kuelekea uchaguzi mkuu marekebisho ya msingi hayajafanyika ya kikatiba, kisheria, kitaasisi na kitaratibu kuweka mazingira ya uchaguzi huru na wa kidemokrasia kama ilivyoahidiwa.
Hivyo, natoa mwito kwa jamii ya wanadiplomasia kupuuza vitisho hivyo vya serikali na badala yake kuongeza nguvu zaidi ya kuhoji kuhusu utekelezaji wa ahadi ambazo Rais Kikwete na serikali yake wametoa kwao na kwa watanzania kwa kuwa serikali za nchi zao na taasisi zake zimetoa fedha na msaada wa kiufundi kutekeleza mipango husika. Mabalozi wazingatie kuwa wao ndio watakaohojiwa na walipa kodi wa nchi zao(sio Rais Kikwete wala Membe) kuhusu matumizi ya kodi zao kwa miradi hiyo ambayo kuna mashaka kama malengo yaliyokusudiwa yatatimia kwa wakati uliopangwa.
Pamoja na vitisho vya Waziri Membe na sasa Rais Kikwete ni muhimu kwa mabalozi na jumuia ya wanadiplomasia kuendelea kuurejea Mkataba wa Vienna sanjari na mikataba, itifaki na maazimio mengine ya kimataifa ambayo nchi zetu imeridhia.
Katika dunia ya sasa yenye changamoto mbalimbali ambapo udhaifu kwenye taifa moja una taathira kwa majirani zake na ubinadamu kwa ujumla wake; ni muhimu kwa msingi muhimu wa utetezi wa haki za binadamu unaovuka mipaka na mamlaka ya kinchi kuzingatiwa.
Haiwezekani jumuia ya kidiplomasia ikaendelea kukaa kimya wakati haki za msingi za binadamu zinavunjwa katika chaguzi kwa hofu ya vitisho vya Rais Kikwete ama Waziri Membe ya kwamba wanaingilia mambo ya ndani ya kisiasa ya nchi.
Msingi huu wa kuepusha watu wengine kutoa kauli zenye kuashiria kuingiliwa kwa mamlaka ya ndani ya nchi(sovereignity of the state) ingekuwa na maana kama serikali inayoongozwa na CCM ingekuwa inazingatia kikamilifu katiba ya nchi, sheria za nchi na mikataba ya kimataifa.
Hali ni tofuati, kwani pamoja na ahadi za Rais Kikwete kwa mabalozi mwaka 2006, Taifa limeshuhudia ukiukwaji wa haki za binadamu katika chaguzi za marudio za ubunge Tanzania bara mathalani Kiteto, Tarime, Busanda na Biharamulo ikiwemo vitendo vya viongozi wa CHADEMA kukatwa mapanga wakati wa kampeni za chaguzi husika. Hali hiyo hiyo imejitokeza Tanzania visiwani(Zanzibar) wakati wa uandikishaji wa wapiga kura hususani katika kisiwa cha Pemba.
Ni wazi kwamba vyama vya siasa hususani vya upinzani, mashirika ya kiraia na viongozi mbalimbali wa dini wamekuwa wakitoa kauli kama hizi; hivyo vitisho kwa mabalozi vinaweza kufanya jumuia ya kimataifa ikwepe kutoa kauli za kuunga mkono madai hayo ya haki kwa kuhofia kutafsiriwa kuwa wanaunga mkono 'chama' au 'watu' kwa lengo la kukiondoa chama tawala madarakani.
Ni muhimu kwa watanzania na jamii ya kidiplomasia kwa ujumla kuitafsiri kauli ya sasa ya Rais Kikwete katika muktadha wa matukio yanayotokea ndani Serikali na kwa umma tunaopoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuchapisha kwenye gazeti la Serikali la Disemba 11 na kutoa tamko kwa umma Disemba 22 kuhusu mapendekezo ya Miswada miwili ya sheria zinazogusa uchaguzi.
Muswada wa kwanza ni wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Uchaguzi ambao kimsingi haujagusa mabadiliko ya msingi yaliyohitajiwa na vyama vya siasa hususani vya upinzani, wadau wengine na mengine kuuungwa mkono hata na baadhi ya wanadiplomasia na Taasisi zao.
Muswada wa pili ni wa sheria mpya ya Matumizi ya Uchaguzi wa Mwaka 2010, ambao pamoja na malengo mazuri yanayotajwa ya kudhibiti fedha chafu na fedha kutoka nje kuingia katika uchaguzi Tanzania; maudhui ya muswada mpya ni mabaya ambayo kama yakipishwa kama yalivyo yanalenga kunyonga vyama vya upinzani, wagombea wa upinzani, makundi ya kiraia yakiwemo ya kidini na hata baadhi ya wagombea ndani ya chama tawala; jambo ambalo likiachwa lihujumu uchaguzi mkuu 2010 na demokrasia kwa ujumla wake.
Kitendo cha Rais Kikwete kutoa kauli hiyo wakati ambapo tayari baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ikiwemo wa CHADEMA wametoa kupinga maudhui ya miswada inaweza kutafsiriwa kuwa inalenga kuwatisha mabalozi wakwepe kutoa kauli za kuunga mkono misimamo hiyo kwa kuhofia kutafsiriwa kuwa "mabalozi wanaunga mkono 'chama' ama 'watu".
Hivyo, ni muhimu kwa washirika wa kimaendeleo kupuuza kauli hizo na kuunga mkono vyama, vikundi vya kiraia na viongozi mbalimbali kila wanapotoa kauli zinazoendana na misingi ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu(UDHR) na Mikataba ya Kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia.
Wakati huo huo; natumia fursa hii kutoa mwito kwa jumuia ya kimataifa kuzirejea ahadi za Rais Kikwete za Mwaka 2006 kuhusu ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa katika muktadha wa matukio yaliyojitokeza baadaye. Mathalani, inashangaza kwa Tanzania kuahidi kuwa mstari wa mbele kulinda Amani eneo la Maziwa Makuu (Great Lakes) na kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa(UN). Lakini miaka minne baadaye, serikali ya Rais Kikwete huyo huyo inatuhumiwa kwenye ripoti ambayo kwa taarifa tulizonazo tayari imeshawasilishwa kwenye Kamati ya Vikwazo ya Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa(UN) kwamba baadhi ya Raia wake wakiwemo Vigogo wa Serikali na taasisi zake wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika usafirishaji wa Silaha kwenda maeneo ya Vita ndani ya ukanda wa maziwa makuu na utoroshaji wa madini haramu toka maeneo hayo. Aidha Tanzania kama nchi imetuhumiwa pia kwa serikali kushindwa kusimamia kikamilifu maazimio ya UN ambayo Serikali yetu ilikubaliana nayo ya kuzuia madini na silaha haramu visipite katika ardhi ya nchi yetu bila kuchukua hatua.
Kutokana na hali hiyo, nachukua fursa kutoa rai kwa Mabalozi wa nchi za Maziwa Makuu na hata kundi la marafiki (Group of Friends) kutoa kauli kuhusu tuhuma hizi; kauli ambayo inapaswa kutolewa pia na Mkuu wa Mabalozi Tanzania (Dean Of Diplomatic Corps)-Balozi Juma Mpango (ambaye pia ni Balozi wa DRC nchini Tanzania).
Imetolewa na:
John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa(CHADEMA)
mnyika@chadema.or.tz, mnyika@yahoo.com na 0754694553
No comments:
Post a Comment