Monday, January 18, 2010

Uchaguzi Mkuu 2010: Kwa Pamoja Tutashinda


Kwa kuwa hii ni makala yangu ya kwanza kwa mwaka huu inayotoka katika toleo la kwanza kabisa la Mwanahalisi kwa mwaka 2010 nianze kwa kuitakia timu nzima ya gazeti hili na wewe msomaji wake heri ya mwaka mpya wenye upendo, furaha na mafanikio.

Mwishoni mwa mwaka 2009 paliibuka majadiliano ambayo yanaendelea mpaka hivi sasa kwenye mtandao kupitia www.facebook.com/john.mnyika kuhusu ‘Ubunge Ubungo 2010: Nigombee Nisigombee?’

Wachangiaji wote waliotoa maoni yao mpaka sasa wamenitaka nigombee huku wakitoa sababu mbalimbali. Wapo waliotoa hoja ya kutambua uwezo, haja ya kubeba harakati za kizazi kipya kushiriki kwenye uongozi wa taifa letu na kufanya vizuri mwaka 2005 wakati huo nilipogombea ubunge wa jimbo hilo nikiwa na umri wa miaka 24.

Mchangiaji mmoja alirejea mfano wa Barack Obama ambaye alikuwa na mashaka kuhusu kugombea kwake lakini mmoja wa washauri wake wa karibu akamweleza kwamba ‘usipogombea umechagua kushindwa; lakini ukigombea una chaguo la kushinda ama kushindwa’. Walatini wana msemo ‘Sauti ya watu ni sauti ya Mungu’; hivyo zitazijadili kwa sasa hoja husika.

Majadiliano hayo yalifanya nihitimishe mwaka 2009 kwa makala “Kuelekea 2010: Kwa Pamoja Tunaweza” kuwezesha tafakari ya wengine ambao ni sehemu ya wapiga kura ama wananchi kwa ujumla hawana fursa ya kushiriki majadiliano kwenye tovuti. Tafakari pana zaidi tunapoelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; nini kinawasukuma wagombea kujitokeza kugombea: dhamira binafsi ama msukumo wa umma au vyote?

Katika makala hiyo nilijenga hoja kwamba kwa mgombea ambaye utumishi wake bado haufahamika kwa umma anaweza kusukumwa kugombea kwa dhamira binafsi lakini kwa mgombea mtarajiwa ambaye anafahamika tayari: nguvu alizonazo, udhaifu alionao, fursa alizonazo na vikwazo vinavyomkabili; si vizuri naye asukumwe na dhamira binafsi pekee.

Kwa mgombea mtarajiwa ambaye anafahamika kwa wananchi ni muhimu pamoja na dhamira yake binafsi pawe pia na msukumo wa umma; hii ni kwa sababu nafasi za kuchaguliwa kama ubunge ni za kuwakilisha wananchi. Ni muhimu sehemu ya wananchi: iwe ni wanachama wa chama, wapiga kura ama baadhi ya watu katika jumuia waone haja hiyo na watoe hoja hiyo kwake au kwa wapiga kura wenzake.

Nashukuru kwamba wananchi karibu wote (isipokuwa mmoja) waliopiga simu ama kutuma ujumbe mfupi wa maneno waliunga mkono maudhui ya makala hiyo; maoni mbalimbali waliyoyatoa ndio yamenihamasisha kuandika makala hii kuendeleza mjadala.

Mtu mmoja (namba yake naihifadhi) alituma ujumbe mfupi ufuatao, namnukuu “unajisumbua tu huo ubunge wa Ubungo hatukupi, hili sio jimbo la dini yenu tu kila wakati, tunajitaji mwenzetu sisi”.

Ujumbe ukanipa hisia kwamba wapo watu wachache katika jamii yetu wanaotazama watu wengine- si kwa haiba yao, dira yao, maadili yao au uwezo wao; bali dini zao. Hali hii ikiendelezwa katika taifa letu inaweza kututumbukiza katika ubaguzi; iwe wa kidini, kikabila au wa aina nyingine yoyote.

Nilimjibu kwa ufupi tu kwamba “Mwenyezi Mungu akuwezeshe kutambua kwamba Bunge sio kanisa, msikiti wala sinagogi na kwamba mbunge sio padri, shehe au kasisi”; hakujibu tena chochote mpaka sasa.

Taifa letu dini (secular state) lakini inaheshimu uhuru wa kuabudu na watu wake wanadini zao; hii ni moja ya tunu katika katiba ya nchi yetu. Natambua nafasi ya dini zetu katika kujenga maadili ya wananchi, tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 tukiwa na haja na hoja za kufanya mabadiliko umoja wetu ni jambo la muhimu; kwa pamoja tutashinda.

Kugombea nafasi za kuchaguliwa zinazohusisha kuwakilisha umma hakupaswi kuwa suala la mtu binafsi pekee au maslahi ya wachache kwa kisingizio cha dini au kabila. Matokeo ya kuwaachia wagombea binafsi, au vikundi vyao ama vyama vyao pekee ni kuwa na viongozi ambao baada ya kuchaguliwa kwao; kwa sababu waliingia kwa dhamira zao na wakafanya kampeni ‘kivyaovyao’; hawawajibiki kwa umma.

Hivyo tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ni muhimu kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla kutambua kwamba suala la uongozi wa kuchaguliwa kuwakilisha umma ni wajibu wa pamoja (shared responsibility).

Ni wajibu wa yoyote (bila kujali chama, hali, dini au kabila) anayetambua kwamba Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu na watu wake rasilimali; iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu ama maliasili: hivyo tunawajibika kujenga taifa lenye kutoa fursa ya ustawi wa wananchi. Kwa pamoja tutashinda!.

Tuzingatie bila kujali chama, dini wala kabila kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale. Kwa falsafa ya chukua chako mapema; Tanzania yenye neema haiwezekani. Tunahitaji fikra mbadala za kuleta ukombozi kwa kuwa mabadiliko yanawezekana. Tuunganishe nguvu kubadili mfumo wa utawala; kwa pamoja tutashinda.

Wazazi, wanafunzi, wazee, wanawake na masikini kwa ujumla wenye kuathirika na kuongezeka kwa gharama za maisha na kuporomoka kwa huduma za kijamii nchini iwe ni elimu, afya, maji, mafao ya wastaafu kwa pamoja tutashinda na kuweka mifumo thabiti ya usalama na haki katika jamii (social security and social justice) ili kuepusha migogoro.

Hata mwenye uwezo na fursa anayeona hatari inayolinyemelea taifa kutokana na kuongezeka kwa pengo kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho, ukosefu wa ajira hususani kwa vijana nk ambayo ni mabomu ya wakati yenye athari vizazi hata vizazi yanayoweza kuepukwa ujumbe wangu kwake ni kuwa pamoja tutashinda ikiwa tutaweka pembeni ubinafsi na kujali maendeleo ya sekta zinazogusa mustakabali wa waliopembezoni.

Natoa rai kwa watumishi wa umma iwe ni walimu, polisi, wahudumu wa sekta ya afya nk ama wafanyakazi binafsi ambao wanataka mabadiliko kutoka katika mishahara midogo na mazingira magumu ya kazi, maslahi duni kwa kwa pamoja tutashinda na kujenga taifa lenye kuthamini utaalamu.

Watanzania wote waadilifu wanapaswa kukerwa na ufisadi mkubwa unaolitafuna taifa huku hatua zinazostahili kushindwa kuchukuliwa kutokana na ufisadi kutapakaa katika mfumo mzima wa utawala na kuteteresha hata utawala wa sheria. Hivyo pamoja tutashinda na kufanya mabadiliko ili turejeshe uwajibikaji na maadili ya taifa.

Hivyo, ni muhimu kwa yoyote anayetaka mabadiliko; mosi, ajiandikishe kupiga, ajitokeze kugombea au ashawishi wenye msimamo wa kuunga mkono mabadiliko ya kweli kujitokeza kugombea katika kata, majimbo, taifa na kupiga kura katika uchaguzi mkuu. Pili, ajiunge na harakati za kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu kwa hali na mali; pamoja tutashinda.

Tushirikiane katika kufikia azma ya kugombea kama njia ya kuunganisha nguvu ya umma hata katika kampeni za uchaguzi. Katika siasa za ushindani, ni muhimu harakati za uchaguzi zikaendeshwa katika mfumo wa vuguvugu (movement) hususani kwa wagombea wanaopitia vyama mbadala ambavyo havitegemei nguvu ya dola.

Ikumbukwe kuwa kushiriki kuleta mabadiliko ni zaidi ya matukio ya kugombea ama kupiga kura; ni pamoja na kushiriki katika mchakato mzima wa kuleta mabadiliko kwa njia mbalimbali. Kwa pamoja tutashinda hivyo tunahitaji nguvu yako katika kufanya mabadiliko; kama alivyosema Mahatma Gandhi ‘kuwa wakala wa mabadiliko unayotoka kuyaona’.

Tutashinda ikiwa wapenda demokrasia wote watatambua kwamba hujuma za kwenye uchaguzi zinaweza kudhibitiwa kwa kuunganisha nguvu ya umma kuweka uwanja sawa wa kisiasa ikiwemo kwa kujenga vuguvugu thabiti la ulinzi wa kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Tuwasiliane, tushauriane na tushirikiane kwa pamoja tutashinda.


Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.or.tz na http://mnyika.blogspot.com

No comments: