Wednesday, January 20, 2010

Mapendekezo ya serikali hayatawezesha kikamilifu uchaguzi huru wa viongozi


KWA kuwa siasa (nikimaanisha siasa safi) ni hitaji muhimu la maendeleo kama alivyowahi kusema hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; basi uendeshwaji wa uchaguzi (kwa maana ya uchaguzi huru na haki); ndio njia ya kulipata hitaji hili.

Uendeshwaji wa uchaguzi huru na haki hutupatia pia hitaji jingine la msingi kwa maendeleo - yaani “Uongozi Bora”. Suala kuu ni kuwa na mifumo ya kikatiba na kisheria na kiuwanja wa kisiasa ambayo inahakikisha uchaguzi huru na haki.

Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010.

Hata hivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe.

Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi.
Ikumbukwe kwamba tume ya uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa Aprili 21, 2009 mkoani Dar es Salaam mkutano ambao nilishiriki.

Katika mkutano huo nilieleza masikitiko yangu kwamba tangu baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2005, Tume ya Uchaguzi haikuitisha mkutano na vyama vya siasa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu hadi mwaka 2009, takriban mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi.

Hii inaacha maswali kuhusu dhamira ya tume katika kuhakikisha taifa linakuwa na uchaguzi huru na haki; hasa ukizingatia kwamba toka mwaka 2006; CHADEMA na wadau wengine tumekuwa tukihitaji kukutana na tume na pia tukihimiza mchakato wa mabadiliko ya kweli kuanzishwa.

Niliweka bayana mashaka yangu nikizingatia kuwa masuala ya uchaguzi mkuu yanahusu mabadiliko ya kisheria, kimfumo n.k, ambayo huchukua muda mrefu kuweza kupitishwa na kutekelezwa, hivyo kitendo cha kuanza majadiliano wakati huu, kinaashiria kuwa sehemu kubwa ya yatakayojadiliwa; hayataweza kutekelezwa.

Kwa upande mwingine nilishukuru kuitishwa kwa mkutano huo nikiwa na matarajio kuwa baada ya kukutana huko tume kwa kushirikiana na serikali ingeweza bado kuchukua hatua za haraka kuweza kufanya mabadiliko yanayokusudiwa katika kipindi kifupi kilichobaki.

Mkutano huo, baada ya kupokea maoni ya ujumla kutoka kwa vyama vya siasa uliahirishwa baada ya muda mfupi bila maamuzi yoyote ya msingi kufikiwa kwa maelezo kwamba ungeitishwa mkutano mwingine baada ya kufanya mapitio ya hoja na vielelezo vilivyotolewa na wachangiaji mbalimbali.

Takriban miezi minane, yaani zaidi ya nusu mwaka ukapita mpaka ikafika mwezi Desemba 2009; siku chache kuelekea 2010, si Tume ya Uchaguzi wala serikali ilikuwa imefanya kikao na vyama vya siasa kufikia makubaliano kuhusu marekebisho yanayokusudiwa.

Hata hivyo, katika mwezi wa Desemba 2009 vyombo vyote viwili; tume ya uchaguzi na serikali viliibuka na kutoa kauli zinazoashiria kwamba tayari maamuzi yameshafikiwa kuhusu suala hili nyeti linalohusu mustabali wa wananchi wote bila kujali vyama.

Ilianza Tume ya Uchaguzi ambayo Desemba mosi, 2009 ilifanya mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuelezea kile ilichokiita mkutano wa kubadilishana mawazo na kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu 2010.

Katika mkutano huo mada na hotuba zilionyesha bayana kwamba tayari yapo marekebisho ambayo tume kwa kushirikiana na serikali wameshakusudia kuyafanya; huku mabadiliko mbalimbali ya msingi yakiwa ni sehemu ya hoja zilizowasilishwa.

Siku chache baadaye Desemba 2009 11, serikali ikachapisha kwenye gazeti la serikali miswada miwili yenye kulenga kufanya marekebisho katika sheria za uchaguzi. Siku kumi baadaye serikali ikafanya kile kilichoitwa kuweka hadharani miswada hiyo miwili kupitia taarifa yake fupi kwa vyombo vya habari Desemba 21, 2009.

Serikali ilitangaza marekebisho hayo yakiwa na mapendekezo ya kufanyia marekebisho sheria ya uchaguzi sura ya 343 na sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292, lengo lililoelezwa kuwa ni kuondoa upungufu mbalimbali uliojitokeza katika chaguzi zilizopita kuiwezesha NEC kuendesha uchaguzi kwa ufanisi.

Serikali ikaeleza kuwa upungufu uaokusudiwa kurekebishwa katika muswada huo ni pamoja na NEC kutokuwa na madaraka ya kuteua waratibu waandikishaji wa mikoa.

Pia kushughulikia suala la kipindi cha kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kutotajwa bayana katika sheria na sheria kutoruhusu baadhi ya watendaji wa tume kuingia katika vituo vya kupigia kura ili kufuatilia zoezi la upigaji kura.
Ibara ya 6 imependekeza marekebisho katika fungu la 15 la sheria, ili kuweka bayana kipindi cha kufanya uboreshaji wa daftari la taifa la kudumu la wapiga kura kuwa mara mbili katika Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata.

Aidha, sehemu hiyo inasisitiza kwamba, kwa lengo la kuongeza uwazi katika zoezi la uandikishaji wapiga kura, imependekezwa katika ibara ya 7 kuwa na fungu jipya la 15A katika sheria linatoa nafasi kwa vyama vya siasa kuteua mawakala wakaokuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura kama ilivyo wakati waupigaji kura.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetangaza kuwa imeandaa marekebisho ambayo imeyaita ‘makubwa’ ya sheria za uchaguzi ambayo pamoja na mambo mengine, imependekeza kupunguzwa kwa muda wa kusubiri kabla ya kufanya uteuzi wa mgombea mwingine wa nafasi ya urais au umakamu inapotokea mmoja wao anafariki kabla ya uchaguzi ambayo imejinadi kuwa yanalenga pia kuipunguzia nguvu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Ibara ya 9 inapendekeza marekebisho katika fungu la 35A la sheria kwa lengo la kupunguza muda wa kusubiri kabla ya kufanya uteuzi wa mgombea mwingine wa urais au umakamu wa rais inapotokea wagombea hao wamefariki.

Sehemu ya muswada huo wa sheria ya uchaguzi imependekeza kufutwa kwa vifungu vya sheria vinavyoruhusu utoaji wa takrima.

Muswada unapendekeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ipewe mamlaka ya kuteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi au sifa zao tofauti na ilivyo ambapo tume huteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi pekee.

Marekebisho hayo pia yanapendekeza kuongeza muda wa rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika Mahakama ya Rufaa kwenye kesi za uchaguzi na kuongezwa kwa muda wa kufungua kesi kutoka siku 14 za sasa hadi siku 30.

Ibara ya 10 imependekeza marekekibisho katika fungu la 37 la sheria ili kuweka ukomo wa muda wa kufanya chaguzi ndogo za Bunge kama inavyobainishwa katika ibara ya 76(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.

Katika Ibara ya 3, muswada unapendekeza kuongeza tafsiri ya maneno mbalimbali katika sheria ya uchaguzi; unapendekezwa kurekebisha tafsiri ya maneno “nomination” na “Member of Parliament” ili kujumuishwa katika tafsiri ya uteuzi (nomination) uteuzi wa wabunge wanawake wa viti maalumu na katika tafsiri ya mbunge (member of Parliament) mbunge wa kuteuliwa wa viti maalumu vya wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ibara ya 13 inakusudia kufanya marekebisho katika sura ya V ya sheria kwa kuongeza sehemu mpya ya III inayohusu mchakato wa mamlaka ya tume kuwatangaza wabunge wanawake wa viti maalumu walioteuliwa na vyama vyao kuwa wabunge.

Marekebisho hayo ambayo serikali imeyapendekeza yanatarajiwa kujadiliwa katika kikao cha Bunge hivi karibuni ili yatumike kwenye uchaguzi wa mwaka 2010.

Hata hivyo, marekebisho hayo hayajitoshelezi kabisa ukilinganisha mapungufu yaliyopo, muda uliopo, hoja za wadau na rasilimali ambazo zimetolewa na wadau mbalimbali kuwezesha mchakato wa marekebisho ya kisheria na kitaasisi nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Hivyo mjadala utakaowezesha kuunganisha nguvu za kidemokrasia na kimaadili ili kudai na kushawishi mabadiliko ya sheria za uchaguzi na mazingira ya kisiasa ni muhimu uibuliwe na kuendelezwa.

Kuna haja ya serikali kufanya marekebisho mapana zaidi au vyama vya siasa na wadau wengine waelekeze jitihada bungeni na mahakamani kudai mabadiliko ama kufutwa kwa vipengele vya sheria nyingine ambavyo vinafanya mazingira ya kisiasa na kiuchuguzi yanayokwaza uchaguzi huru na wa haki.

Kwa muhtasari lazima kuzipitia sheria na/ama kufanya mabadiliko/marekebisho ya msingi yafuatayo ambayo hayajaguswa katika miswada iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mosi, tume lazima iwe huru na ya kudumu yenye kufanya kazi muda wote na kuwekewa bajeti maalumu na watumishi wa serikali wasitumike katika uchaguzi badala yake kuwe na watendaji huru wa tume katika ngazi zote kama ilivyo kwa mahakama.

Pili, kupanua wigo wa mfumo wa uwakilishi wa uwiano na kuweka mfumo mchanganyiko/mchanyato. Tatu; Kufuta vipengele katika sheria vinavyoruhusu mapingamizi yanayokwenda kinyume na misingi ya masharti ya kikatiba ya wagombea.

Nne, kuchunguza na kukabiliana na tatizo la mwitiko mdogo wa wapiga kura. Tano, kuhakikisha kwamba mafunzo ya pamoja yanafanywa baina ya wasimamizi/wasaidizi wa vituo na mawakala wa vyama; na kuhakikisha wgombea/vyama vinakuwa na rasilimali za kuwezesha kuwa na mawakala katika vituo.

Sita, kutoa uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo wakati wa uchaguzi; Kuweka usawa katika matumizi ya vyombo vya habari ikiwamo kuhusu matangazo ya kisiasa ya kulipia wakati wa kampeni.

Ni wazi: Sehemu kubwa ya mabadiliko haya yanahitaji kitu kimoja tu: mabadiliko ya katiba ya nchi.

Hakuna uhuru na haki kwa vyama vya siasa kushiriki kwenye chaguzi zijazo kama mazingira ya kisiasa na kiuchaguzi hayatabadilika katika nchi yetu!

No comments: