Monday, January 11, 2010

Watanzania mlio nje ya nchi amkeni (Tanzanians in Diaspora Arise)


Watanzania mlio nje ya nchi amkeni (Tanzanians in Diaspora Arise): Wakati Tanzania Bara (wakati huo ikiitwa Tanganyika) ikiwa katika harakati za kudai uhuru; tunasimuliwa na wazee wetu, vijana wa wakati huo kwamba palikuwa na mchango mkubwa sana wa watanzania waliokwenda kupigana vita nje ya mipaka ya nchi yetu. Hawa waliwaelewa vizuri wakoloni wa wakati huo kuanzia udhaifu wao na hata mbinu za kuwakabili; na kwa ujumla walijifunza kwamba nchi kupata uhuru inawezekana.

Ni hakika kwamba wakati taifa letu linapoendelea kukabiliwa na changamoto za maadui ujinga, umasikini na maradhi huku ukoloni mamboleo ukiweka mirija katika rasilimali na maliasili; tunahitaji mabadiliko ya kweli yenye kuleta uhuru wa kweli.

Katika mazingira haya, kama ilivyokuwa wakati wa kuundoa ukoloni mkongwe, mchango wa watanzania mlio nje ya nchi (Diaspora) ni wa muhimu sana.

Watanzania nyie mnaelewa matunda ya mabadiliko katika kukabiliana na changamoto za ujinga, umasikini na maradhi na mbinu za kidemokrasia za kufikia mabadiliko hayo. Katika kukabiliana na ukoloni mamboleo, watanzania mlio nje ya nchi mnafahamu udhaifu wa mabeberu hivyo mnauwezo wa kusimama kidete kuunganisha nguvu kujenga taifa lenye uwajibikaji na kutoa fursa kwa watanzania wengine walio wengi.

Kwa sasa mchango mkubwa wa watanzania mlio nje ya nchi umekuwa katika kuleta rasilimali kwa wenzenu walio nyumbani (remittances); kwa wachache uwekezaji na wengine kutoa uzoefu wao wa kitaalamu.

Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010; ni wakati wa Diaspora kuchukua hatua kama ilivyokuwa wakati wa kudai uhuru ili kuweke madarakani uongozi wenye dira, uadilifu na uwezo kuifikisha Tanzania katika kipeo cha demokrasia, maendeleo na ustawi wa watu wake. Mnaweza kufanya hivyo kwa wengine kujitokeza kugombea lakini wengi kuunga mkono harakati za mabadiliko kwa njia mbalimbali; kwa kutoa mawazo, kuchangia rasilimali na kupiga kura.

Naotoa ujumbe huu wakati huu Taifa likiwa katika mjadala wa sheria mbili muhimu zenye taathira katika uchaguzi ambazo watanzania mlio nje ya nchi mnapaswa kuzitazama kama kikwazo kwenu na kutoa maoni ya kuzibadili ili ziwe fursa kwenu kuwezesha mabadiliko kupitia uchaguzi.

Mosi; muswada wa marekebisho ya sheria za uchaguzi; huu umekwepa kuweka mabadiliko ya msingi ya kuwezesha uchaguzi kuwa huru na haki ikiwemo kutokuwepo mfumo huru wa usimamizi wa uchaguzi kama wadau walivyohitaji. Lakini kwenu mlio nje ya nchi, muswada huu haujaingiza ombi lenu la muda mrefu la kutaka mruhusiwe kupiga kura. Inashangaza kwamba nchi masikini kama Msumbiji, na nchi iliyotoka vitani karibuni kama Rwanda; raia wake wanawekewa utaratibu wa kupewa haki ya kupiga kura kupitia balozi zao katika nchi mbalimbali, Tanzania inashindwa kuweka kifungu hiki katika marekebisho ya sheria na hivyo kuendelea kunyima haki hii muhimu ya kikatiba kwa watanzania walio nje ya nchi.

Pili; Muswada wa Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010; huu pamoja na kuweka vifungu kuminya wagombea kuchangisha fedha za uchaguzi ndani ya nchi, na kutoa mianya ya wagombea kufutwa bila kupewa haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa. Umelenga pia kudhibiti hata fedha za watanzania walio nje ya nchi kuchangia uchaguzi. Kama sheria hii itapita, watanzania mlio nje ya nchi, hamtaweza kuchangia vyama ama wagombea kwenye kampeni ya uchaguzi hata kama ni michango midogo midogo ya kuwezesha mabadiliko. Katika mazingira haya, uchaguzi wa mwaka 2010; mchango wenu utakuwa ni upi? Maana nyie ni raia halali, lakini hamtakuwa na haki ya kupiga kura wala hamtakuwa na haki hata ya kuchangia wagombea iwe ni fedha au rasilimali nyingine yoyote ile kwa chama ama kwa wagombea.

Amkeni sasa, wekeni msimamo wa kuwezesha taifa kuwa na sheria itayolinda uhuru wa nchi na kuweka uwanja sawa wa ushindani wa kisiasa wakati huo huo ikawawezesha kupata haki zenu za kikatiba muweze kutimiza wajibu wenu wa kidemokrasia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Ukimaliza kusoma ujumbe huu; tafadhali mtumie na mwenzako au usambaze katika majukwaa mbalimbali ya mijadala. Wako katika demokrasia na maendeleo: John Mnyika, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (CHADEMA); tuwasiliane- 0754694553, mnyika@yahoo.com au mnyika@chadema.or.tz.





1 comment:

ray05 said...

Asante kaka Mnyika kwa ujumbe huu.Watanzania tunapaswa kukumbuka tulikotoka na sio kujifanya tunajua kutoa comments kwa yanayotokea wakati sisi wenyewe tukiwa hatuhusiki.Nchi inajengwa na watanzania na sisi ndio watanzania wenyewe,huku tulipo sio kwetu na tukumbuke kuwa mpaka sisi kufika huku Tanzania ndio iliyotulea.

TUUNGANE KUJENGA NCHI YETU
RAYMOND MAUKI ALGERIA ray_mauki@yahoo.com