Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010. Hatahivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe. Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi; na katika kujadili muswada huo makala hii itachambua suala la uteuzi wa wagombea pekee.
Uteuzi wa Wagombea upo katika ngazi mbili: Uteuzi wa Wagombea katika Vyama na Uteuzi wa Wagombea katika Tume ya Uchaguzi. Uteuzi wa ndani ya vyama unasimamia na katiba, kanuni na taratibu za vyama husika. Ni kawaida katika siasa za uteuzi ndani ya vyama kutawaliwa na ushindani mkubwa; lakini ieleweke kuwa kuna tofauti kati siasa chafu na siasa za ushindani. Siasa zenye ushindani chanya zinasababisha uteuzi wa wagombea ambao wenye uwezo kiuongozi mathalani elimu, uzoefu na dira. Siasa za ushindani hasi hupelekea kupatikana kwa wagombea ambao ushindi wao umetokana na rushwa, upendeleo, kupakana matope, udini, ukabila nk. Kwa mfano, uteuzi wa ndani ya CCM uligubikwa na ‘takrima’ na siasa za kupakana matope katika maeneo kadhaa ikiwemo kuanzia ngazi ya udiwani mpaka ya Urais. Mathalani inatajwa jinsi Salim Ahmed Salim (aliyekuwa Katibu Mkuu wa OAU) alivyopakwa matope (kwa mujibu wa Ripoti ya Uchaguzi Mkuu 2005 ya TEMCO). Ilifikia hatua Fredrick Sumaye, mmoja wa wagombea (ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wakati huo), akiwa analaani jinsi ambavyo anapakwa matope alitamka bayana kwamba “anayesafisha njia kwa kalamu, atatawala kwa risasi”.
Uteuzi wa wagombea katika Tume ya Uchaguzi unasimamiwa na Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 1985. Katika uchaguzi Mkuu 2005 wagombea wengi walipitishwa na Tume ya uchaguzi na mapingamizi mengi yalitupiliwa mbali tofauti na chaguzi zingine zilizotangulia.
Katika kipindi cha mwaka 2006 mpaka 2009, pameibuka suala ambalo linahitaji kufanyiwa kazi na marekebisho yakafanyika kuhusu mapingamizi dhidi ya wagombea katika chaguzi. Tutatumia mfano wa suala la mapingamizi katika uchaguzi wa ubunge na udiwani Mbeya Vijijini lakini ipo mifano pia katika chaguzi zingine za marudio ikiwemo za madiwani, mitaa, vijiji na vitongoji. Mgombea wa CHADEMA aliwasilisha fomu zake kwa ajili ya uteuzi tarehe 27 Disemba 2008 na kuteuliwa kuwa mgombea.
Hata hivyo tarehe 28 Disemba, 2008 mgombea aliwekewa pingamizi na mgombea wa CUF na mgombea wa CCM. Misingi ya pingamizi ni pamoja na kuwa mgombea wa CHADEMA alijiapisha mwenyewe na kwamba mgombea aliapa kwa wakili badala ya kuapa kwa hakimu. Msimamizi alimtaka mgombea kuwasilisha maelezo yake, na mgombea aliwasilisha maelezo ya kukanusha kujiapisha, kutoa ufafunuzi kuhusu mpangilio wa majina na kueleza kwamba aliapa mbele ya wakili kwa kuzingatia tarehe ambazo alipaswa kuapa na kwa kuwa ipo sheria nyingine ya viapo inayoruhusu kuapa mbele ya wakili. Na kwamba sheria ya uchaguzi haikatazi moja kwa moja viapo vya waapishaji wengine.
Tarehe 29 Disemba 2008 Msimamizi wa Uchaguzi alikubaliana na eneo moja la pingamizi zilizowasilishwa na CCM na CUF la mgombea kuapa mbele ya wakili badala ya hakimu na kutupilia mbali maeneo mengine ya pingamizi.
Tarehe 30 Disemba 2008 mgombea wa CHADEMA aliwasilisha rufaa dhidi ya maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi kutokana na misingi ifuatayo: Kwamba Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini hakusoma kwa umakini maelezo ya mrufani na kuyazingatia kikamilifu kabla ya kufanya maamuzi ya kumuengua; Kwamba msimamizi wa uchaguzi hakuzingatia maelezo ya mrufani juu ya muda wa uchukuaji fomu na urejeshaji fomu uliojumuisha siku nyingi takribani tatu mfululizo zisizokuwa za kazi( za sikukuu na siku ya mapumziko ya mwisho wa wiki) ambapo mahakama hazikuwa wazi(operative) na kwamba aliweza kusaini mbele ya wakili tarehe 24 Disemba, 2008 jioni baada ya kumaliza kujaza fomu husika. Na kuomba tume izingatie kifungu 38(1)(4)(proviso) cha sheria ya uchaguzi namba ya mwaka 1985.
Kwamba msimamizi wa uchaguzi wa jimbo alikosea katika kuelezea kuwa sheria ya uchaguzi inasema “mgombea ubunge aape mbele ya hakimu na si vinginevyo” wakati maneno “na si vinginevyo” hayapo kwenye sheria bali ni nyongeza yake tu ili afikie maamuzi ya kumuengua mrufani. Kifungu cha 50 cha sheria ya uchaguzi (National Election Act CAP 343 RE 2002) kinahusika.
Kwamba msimamizi wa uchaguzi amekosea kisheria kwa kutosoma sheria za viapo na kwa kutozingatia maelezo yangu kwamba sheria ya uchaguzi inapaswa kusomwa pamoja na Oaths(Judicial Proceedings and Statutory Declarations Act) pamoja na Notaries Public and Commissiners for Oaths Act(CAP 12 RE 2002), sheria ambazo zinaeleza bayana nani anayepaswa kuapisha kisheria na maana ya kiapo au ‘declaration’. Kifungu cha 11 cha sheria ya viapo “Notary Public and Commissiners for Oath (CAP 12 RE 2002) inaeleza waziwazi kwamba hakuna kizuizi chochote dhidi ya kiapo cha wakili au kamishna yeyote wa viapo.
Kwamba msimamizi wa uchaguzi amekosea kisheria kwa maamuzi yanayoonyesha kuwa sheria ya uchaguzi ni ya kiubaguzi na kwamba inazuia sheria zingine kutumika katika nchi hii. Kwamba msimamizi wa uchaguzi alikosea kisheria kwa kutozingatia maelezo yangu kwamba hakimu anapofanya kazi ya kuapisha hawi hakimu bali anakuwa ‘commissiner for oaths’ kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 3 na 10 cha Notaries Public and Commissioner for Oaths Act na kwamba nani anapaswa kufanya jukumu hilo. Kwa maana ya sheria hiyo hakimu hawi tofauti na watu wengine waliotajwa na sheria hiyo wakati anaapisha. Kwamba msimamizi wa uchaguzi amekosea kisheria kwa kushindwa kuelewa hali halisi ya demokrasia ya vyama vingi na mahitaji ya wapiga kura wa jimbo la Mbeya Vijijini kwa kuwanyima haki ya kuwa na uwanja mpana wa uchaguzi kwa ridhaa yao. Kumuengua mrufani ni kulazimisha watu wa Mbeya Vijijini kuchagua vyama ama wagombea waliobakia ambapo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kuomba tume izingatie kifungu 38(1)(4)(proviso) cha sheria ya uchaguzi namba ya mwaka 1985. Tarehe 2 Januari 2009 Tume ilitupilia mbali rufaa ya mgombea wa CHADEMA kwa misingi mbalimbali na hivyo mgombea husika akaendelea kuenguliwa.
Taarifa za pingamizi zilifikia viongozi wa chama kabla ya mapingamizi kuwekwa zikieleza mawasiliano ya karibu baina ya viongozi wa waweka pingamizi katika uchaguzi wa Mbeya Vijini na Maofisa wa serikali. Kadhalika ilionyesha wazi kwamba palikuwa na mashinikizo la kutoka nje toka ngazi za juu za CCM na serikali katika kuamua kuhusu pingamizi hilo. Kwa hali ya kisiasa ilivyokuwa, pingamizi hilo lilionekana wazi kuwa ni njia pekee iliyokuwepo ya kuepusha CCM kushindwa na CHADEMA katika uchaguzi huo. Hivyo, tume haikutaka kabisa kuzingatia kwamba siku za kiapo hazikuwa zikitosha na tume haikutaka kabisa kutumia mamlaka yake ya kupokea fomu hata kama haina kiapo ama ina kiapo batili kutokana na mazingira hayo. Hata hivyo, maelezo ya Tume yanaashiria pia kuwa tume ilitambua uwepo wa udhaifu katika sheria ya uchaguzi wa kulazimisha kiapo kufanywa na hakimu pekee.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi uliochapwa kwenye gazeti la serikali tarehe 11 Disemba 2009 unaonyesha kwamba marekebisho ya sheria yanayopendekezwa hayatagusa kabisa vifungu vyenye utata kuhusu mamlaka za kuapisha wagombea wala masuala yenye kuwezesha haki na usawa katika uteuzi wa wagombea katika ngazi zote za uteuzi ndani na nje ya vyama.
Suala pekee ambalo Serikali kupitia Ofisi wa Waziri Mkuu imetangaza kuwa imeandaa marekebisho ambayo imeyaita ‘makubwa’ linalogusa uteuzi wa wagombea ni kuhusu utuezi wa mgombea urais au mwenza inapotokea mmoja wao akafariki katikati ya kampeni. Muswada wa marekebisho ya sheria unapendekeza kupunguzwa kwa muda wa kusubiri kabla ya kufanya uteuzi wa mgombea mwingine wa nafasi ya urais au umakamu inapotokea mmoja wao anafariki kabla ya uchaguzi ambayo imejinadi kuwa yanalenga pia kuipunguzia nguvu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Ibara ya 9 inapendekeza marekebisho katika fungu la 35A la sheria kwa lengo la kupunguza muda wa kusubiri kabla ya kufanya uteuzi wa mgombea mwingine wa urais au umakamu wa rais inapotokea wagombea hao wamefariki.
Masuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na Serikali, Tume ya Uchaguzi, Vyama Vya siasa na Wadau wengeni kama sehemu ya marekebisho ya kisheria yanayopaswa kufanyika kulinda haki wakati wa uteuzi wa wagombea.
Mosi; vyombo vya uangalizi na usimamizi viwezeshwe kisheria kufuatilia kuhakikisha uteuzi wa ndani ya vyama unakuwa huru na haki. Kuna haja ya vyombo mbalimbali viwezeshwe kutupia macho uteuzi ndani ya vyama kuhakikisha haki inatendeka. Mathalani Tume ya uchaguzi na ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa hawapaswi kuwa kimya siasa za kupakana matope zinaoendekezwa wakati wa uteuzi wa baadhi ya vyama hususani CCM. Pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) ifuatilie na kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na vitendo vya rushwa vinavyoendelea wakati wa mchakato wa uteuzi katika baadhi ya vyama; utawala wa sheria lazima uheshimiwa hata ndani ya mipaka ya Kikatiba za Vyama vya siasa nchini.
Pili; marekebisho ya sheria ya uchaguzi yahusishe pia kufuta vipengele vibovu vinavyotoa mianya ya mapingamizi yanayokwenda kinyume na haki za kikatiba za wagombea na vyama vyao. Ni vyema mchakato wa kurekebisha sheria ya uchaguzi ukahusisha kuondoa kigezo cha kulazimisha kiapo kwa hakimu pamoja na vigezo vingine ambavyo ni nje ya vigezo kwa kikatiba vya sifa za mgombea. Marekebisho haya yasipofanyika itakuwa ni ishara ya wazi ya kwamba Tume ya Uchaguzi imeacha mwanya kwa mapingamizi kutumika kama zana ya kuhujumu wagombea na vyama vyao katika chaguzi. Tume ya uchaguzi iondoe mianya ya wagombea kukwepa ushindani wa kwenye jukwaa la umma na kukimbilia kutafuta ushindi wa mezani.
SEHEMU YA MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA MAJIRA TOLEO LA TAREHE 20 JANUARI 2010
No comments:
Post a Comment