Friday, January 29, 2010

Muundo wa tume uboreshwe rasilimali zitengwe kuwezesha usimamizi huru wa uchaguzi

Kwa mara ya tatu chini ya mfumo wa vyama vingi; Tume ya Uchaguzi ilisimamia na kuratibu uchaguzi mkuu mwaka 2005 kwa kutumia uzoefu ilioupata katika chaguzi za mwaka 1995 na mwaka 2000. Pia Tume imesimamia chaguzi ndogo 4 za bunge na chaguzi ndogo 75 za udiwani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2005. Kwa ujumla Tume ya Uchaguzi iliendesha vizuri zaidi uchaguzi uliopita ukilinganisha na chaguzi zilizotangulia lakini bado mchakato wa uchaguzi haukukidhi vigezo vyote vya uchaguzi huru na haki.

Katika siku za karibuni pamekuwepo na mjadala kuhusu sheria za uchaguzi uliotokana na uamuzi wa serikali kutoa miswada miwili: Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Fedha za Uchaguzi wa mwaka 2010. Hatahivyo, mjadala huo kwa kiasi kikubwa umejikita katika mapendekezo ya serikali yaliyomo kwenye sheria mpya ya fedha za uchaguzi na kufunika mjadala kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi ambayo kwa maoni yangu ndio msingi wa uchaguzi wenyewe. Hivyo, katika makala hii sitachambua muswada mpya wa fedha za uchaguzi bali nitajikita katika maudhui ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi; na katika kujadili muswada huo makala hii itachambua suala la muundo na utaratibu wa tume ya uchaguzi pekee.

Ni muhimu tuijadili mifumo ya kisheria na kiuchaguzi kwa ajili ya uchaguzi na Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sheria mbalimbali zimekuwa zikisimamia uchaguzi hususani: Sheria ya Uchaguzi na. 1 ya mwaka 1985; Sheria ya Vyama vya siasa na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo zimetoa mamlaka kwa tume kusimamia na kuratibu uchaguzi ikiwemo kutoa maelekezo na taratibu mbalimbali.

Muundo wa Tume ulichukua mfumo ule ule ambao ulitumika katika uchaguzi mkuu 2005 unatokana na Katiba Kifungu 74(1) kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria na. 4 ya 1992 na Sheria na. 7 ya mwaka 1993; Tume inateuliwa na Rais(Katiba na Sheria husika zimeeleza sifa za wanaoweza kuteuliwa). Mkurugenzi wa Uchaguzi naye anateuliwa na Rais kwa mapendekezo ya Tume. Katiba kifungu 74 imebainisha majukumu ya Tume ya Uchaguzi. Vyama vya siasa viliendelea kudai tume huru ya uchaguzi wakati wa marekebisho ya 14 ya katiba yaliyofanyika karibu na uchaguzi mkuu. Hata hivyo suala la muundo wa tume huru ya uchaguzi halikujadiliwa wala kuingizwa kama sehemu ya marekebisho hayo. Matokeo yake maandalizi ya uchaguzi yalifanywa na tume ile ile ambayo ilisemwa kipindi chote kwamba haiko huru. Kamati mbalimbali ziliundwa na kufanya kazi kipindi cha uchaguzi pekee. Hali hii haijabadilika kati ya kipindi cha 2006 mpaka 2009, pamoja na vyama vya siasa na wadau wengine kutaka mapema marekebisho yaweze kufanyika.

Ni muhimu kujadili kuhusu rasilimali kwa ajili ya usimamizi wa uchaguzi na Usimamizi wa Uchaguzi kama sehemu ya kuwezesha usimamizi huru wa uchaguzi. Tofauti na chaguzi za 1995 na 2000, katika uchaguzi mkuu 2005 fedha za uchaguzi kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa Tume ya Uchaguzi zilitolewa katika wakati mwafaka na sehumu kubwa zilitolewa na serikali. Kupungua kwa utegemezi kwa wahisani katika kutoa fedha za kusimamia uchaguzi pamoja na kutoa fedha mapema vilisaidia kuboresha uendweshwaji wa uchaguzi kwa kiwango Fulani. Hata hivyo, hali hii iliwezekana kutokana na ukweli kuwa serikali katika chaguzi zilizofuata baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 ilijivua jukumu la kugharamia kampeni za wagombea na mawakala wa vyama vya siasa.

Uhusiano katika ya vyama vya siasa na Tume ya Uchaguzi katika ngazi ya Taifa kwa kiwango fulani; vyama vilialikwa katika vikao mbalimbali na vilikuwa na wajumbe katika kamati mbalimbali za tume ya Uchaguzi. Hata hivyo malalamiko yalitolewa baadhi ya maeneo mengi hususani yale yaliyokuwa na upinzani mkali kwamba vyama havikushirikishwa ipasavyo na watendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi ngazi ya wilaya, majimbo na kata. Wakati wa kampeni watendaji hawa wameonekana kuegemea chama tawala. Hali hii iliendelea katika maeneo mengi hata katika hatua za kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo hususani katika ngazi za majimbo. Katika mfumo wa tume hakuna utenganisho kati ya usimamizi na utekelezaji katika muundo wa tume ngazi za chini ya makao makuu ya tume. Uteuzi wa watendaji wa chini ulifanywa na wasimamizi wa uchaguzi ambao ni watekelezaji(ambao walikuwa ni watumishi wa serikali) badala ya chombo huru cha kusimamia uchaguzi hivyo walitumiwa na dola kupika ama kuchezea matokeo.

Muswada kuhusu marekebisho ya sheria ya uchaguzi uliochapwa kwenye gazeti la serikali tarehe 11 Disemba 2009 unapendekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ipewe mamlaka ya kuteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi au sifa zao tofauti na ilivyo ambapo tume huteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi pekee. Upenyo wa tume kuachiwa kuamua kati ya vyeo na sifa unatoa mianya ya kuruhusu hujuma. Mathalani, katika uchaguzi wa serikali ya mitaa wa mwaka 2009 pamoja na kuwa haukusimamiwa na tume; kanuni za uchaguzi huo zilitaja kwamba wasimamizi wa uchaguzi wangeteuliwa kwa cheo au kwa sifa; matokeo yake idadi kubwa iliteuliwa kutokana na vyeo ndio maana uchaguzi husika kwa sehemu kubwa ulisimamiwa na watendaji wa serikali kwa nafasi zao. Kama mapendekezo hayo ya muswada wa sheria yakaachwa kama yalivyo maana yake ni kwamba; kwenye chaguzi tume inaweza kuamua kuangalia vyeo na kuteua wakurugenzi na maafisa watendaji wa kata kusimamia uchaguzi badala ya uteuzi kuegemea zaidi katika sifa na kuepuka kuwateua watendaji wa serikali.

Masuala yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa na Serikali, Tume ya Uchaguzi, Vyama Vya siasa na wadau na kuingizwa kama sehemu ya marekebisho ya sheria za uchaguzi katika miswada ambayo imetolewa:

Pawepo na Sheria ya Tume ya Uchaguzi ili kuipa uhuru na mamlaka zaidi tume ya uchaguzi kama ilivyo katika nchi kadhaa za Kusini mwa Afrika.(Pendekezo hili limetolewa pia na Tume ya Uchaguzi na Vyombo mbalimbali vya Ufuatiliaji/Uangalizi wa uchaguzi).

Katiba na Sheria vifanyiwe mabadiliko/marekebisho ili kutoa uhuru na mamlaka ya Tume ya Uchaguzi wa Kuzingatia vigezo vya Kanuni/Matamko na Misingi mbalimbali ya Uchaguzi ya Kimataifa ambayo taifa letu limeridhia. Baadhi ya masuala mahususi ni pamoja na: Tume iwe nje ya mfumo wa kiutendaji wa kiserikali(Watendaji wa Serikali kama Wakurugenzi na Watendaji wa Kata wasiwe watumishi wa Tume ya uchaguzi hata wakati wa uchaguzi); Wajumbe wa Tume wachaguliwe kwa mashauriano na Wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa na baadaye wathibitishwe na Bunge; Utumishi wa Wajumbe waandamizi wa Tume wa ulindwe(durability and security of tenure) kisheria na kikatiba kama walivyo majaji; Uwakilishi wa Tume uzingatie jinsia, uwakilishi wa kijamii na makundi rika; Tume ya Uchaguzi iwajibike kwa Bunge badala ya Kuwajibika kwa Serikali; Tume ya Uchaguzi iwe na Bajeti inayojitegemea itakayopitishwa moja kwa moja na Bunge. Kamati za Tume ziwe ni za kudumu; ziendelee na kazi hata baada ya uchaguzi. Vitengo vya TEKNOHAMA (ICT) na Elimu ya Uraia viwe sehemu ya vitengo vya kudumu vya Tume. Tume ya Uchaguzi iwe na watendaji wa Kudumu katika ngazi mbalimbali; utaratibu wa kuwatumia maofisa wa serikali kama wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi usitishwe. Hii ihusishe kuwezesha bajeti ya Tume ya uchaguzi iwekewe fungu pekee kutoka katika mfuko mkuu wa fedha za umma(consolidated fund) badala ya kuwa sehemu ya bajeti za kawaida za wizara.Hivyo mjadala utakaowezesha kuunganisha nguvu za kidemokrasia na kimaadili ili kudai na kushawishi mabadiliko ya sheria za uchaguzi na mazingira ya kisiasa ikiwemo wenye kuboresha usimamizi wa uchaguzi ni muhimu uibuliwe na kuendelezwa. Kuna haja ya serikali kufanya marekebisho mapana zaidi kuhusu muundo wa tume au vyama vya siasa na wadau wengine waelekeze jitihada bungeni na mahakamani kudai mabadiliko ama kufutwa kwa vipengele vya sheria nyingine ambavyo vinafanya mazingira ya kisiasa na kiuchuguzi yanayokwaza uchaguzi huru na wa haki. Sehemu ya marekebisho hayo yanahitaji kwanza marekebisho ya katiba ili muundo wa tume uboreshwe rasilimali zitengwe kuwezesha usimamizi huru wa uchaguzi.

No comments: