Wednesday, August 10, 2011

Hatma ya Bajeti ya Nishati na MadiniLEO TAREHE 10 AGOSTI 2011 NILIOMBA MUONGOZO WA SPIKA BUNGENI KWA MUJIBU WA KANUNI 68(7) KUTAKA SERIKALI ITOE MAELEZO KWANINI AHADI YA WAZIRI MKUU YA KUZISHIRIKISHA KAMATI ZA BUNGE KATIKA KUANDAA MPANGO WA DHARURA WA UMEME NA MAELEZO KUHUSU NISHATI NA MADINI HAIJATEKELEZWA NA KUTAKA MUONGOZO KUHUSU UTARATIBU GANI UTATUMIKA KUENDELEZA MJADALA TAREHE 13 AGOSTI. UKIREJEA MAJIBU YALIYOTOLEWA UTABAINI KWAMBA SERIKALI INAKUSUDIA ‘KUFUNIKA KOMBE MWANAHARAMU APITE’ KUHUSU BAJETI YA NISHATI NA MADINI; REJEA HAPA CHINI TAMKO LANGU LA TAREHE 8/8 TUSHIKIRIANE KUISIMAMIA SERIKALI KUTIMIZA WAJIBU

Itakumbukwa kwamba tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa hoja bungeni ya kuahirisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za kudumu za bunge(toleo la 2007) kanuni ya 55 (3) (b) na 69 (1).

Waziri Mkuu alilieleza bunge kuwa serikali imetoa hoja ya kuahirisha mjadala wa bajeti ya Wizara husika ili kupata muda usiozidi wiki tatu wa kutoa maelezo kuhusu michango ya wabunge hususani kwa kuwasilisha mpango wa dharura wa kuondoa mgawo wa umeme kwa kuzishirikisha kamati za bunge.

Hata hivyo, ikiwa imesalia chini ya wiki moja kufikia tarehe ya kuendelea kwa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 13 Agosti 2011 serikali bado haijazishirikisha kikamilifu kamati za bunge hususani ya nishati na madini pamoja na fedha na uchumi kama ilivyoahidi. Hatua za haraka zisipochukuliwa na uongozi wa bunge, kamati husika na wadau wengine serikali italeta maelezo yake yakiwa yamechelewa na hivyo kukosekana kwa muda wa marekebisho ya msingi kufanyika.

Hivyo, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya Shughuli zote za Serikali Bungeni kwa mujibu wa katiba ibara ya 52 (2) hivyo anapaswa kuwajibika kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kutozihusisha kamati za bunge mpaka hivi na kutimiza wajibu wa serikali kuwasilisha mpango wa dharura pamoja na marekebisho mengine ya kibajeti kwa kamati zinazohusika mapema iwezekanavyo.

Aidha, kwa umma una matarajio makubwa kuwa serikali itafanya marekebisho ya msingi katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni muhimu kwa Spika wa Bunge Anna Makinda kutoa fursa ya mjadala kuendelea mara baada ya serikali kutoa maelezo na mpango wa dharura kwa kamati zitakazohusika za bunge pamoja na kambi rasmi ya upinzani kutoa maoni kabla ya mtoa hoja kupewa nafasi ya kujibu wa mujibu wa kanuni ya 99 (9). Hii italiwezesha bunge kutekeleza kwa ukamilifu wajibu wa kikatiba uliotajwa kwenye ibara ya 63 (3) (b) na (c).

Katika mpango wa dharura na maelezo yatayotolewa natarajia Serikali itazingatia mapendekezo tuliyotoa kambi rasmi ya upinzani kupitia Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini na kuongeza kiwango cha bajeti kwa kiwango kisichopungua bilioni 977 kwa bajeti ya maendeleo pekee kwa kutumia vyanzo vya nyongeza vya mapato tulivyovitaja. (tofauti na ile ambayo serikali ilitenga awali Sh. Bilioni 452 kwa maendeleo ya nishati na Madini-Fungu 58 na 50).


Baadhi ya vyanzo hivyo ni kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta Kampuni za Madini peke yake kutaongeza mapato ya shilingi bilioni 59. Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini peke yake tunaweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kupunguza fedha kwenye Wizara zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo hususani ya umeme na gesi. Wizara ya Nishati na Madini peke yake imepanga kutumia Sh. Bilioni 7.9 kulipana posho ambazo zinaweza kupunguzwa na kuongezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini.


Kama sehemu ya vyanzo vya mapato tunatarajia kwamba serikali itatoa maelezo ya kukamilisha majadiliano ya ubia ama mikopo toka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na washirika wengine isiyopungua bilioni 400 kwa ajili ya miradi ya umeme na gesi asilia. Pia, serikali itaeleza namna itavyoharakisha ufilisi wa IPTL ili kupata takribani bilioni 200 zilizohifadhiwa katika katika akaunti maalum (escrow account) na kuzielekeza kwenye kuliwezesha Shirika la Umeme (TANESCO) kuwekeza katika umeme na kukamilisha utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika. Aidha, zaidi ya bilioni 100 zingine zinaweza kuongezwa katika ujenzi wa miundombinu ya umeme kutoka kwenye fungu 98 kasma 4168 ya fedha za bajeti ambazo zimepitishwa bila kupangiwa matumizi halisi.


Tunaamini kwamba ongezeko hilo la bajeti litawezesha vipaumbele vifuatavyo kuzingatiwa kwa uzito unaostahili kwa kurejea mwelekeo wa matumizi ambao tuliuwasilisha kwenye bajeti mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011: Kuwekeza fedha za kutosha kwenye mpango wa dharura wa sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane kuwekeza katika Bomba la Gesi kutoka Mtwara, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani. Kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme katika mwaka wa fedha 2011/2012 ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Pamoja na ununuzi wa mitambo mingine kipaumbele kiwekwe pia kuanza kutekeleza miradi ya Kiwira, Stiggler Gorge, Ngaka na Mchuchuma Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini kama tulivyoshauri katika bajeti mbadala.


Aidha kufuatia Kamati Kuu ya CCM kutoa agizo lenye kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011 kuhusu ongezeko la kodi katika mafuta ya taa; serikali ipaswa kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha katika mkutano wa bunge unaoendelea ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa ongezeko kubwa lililofanywa kwenye kodi ya mafuta ya taa na pia kupunguza kodi zaidi kwenye dizeli na petrol kama tulivyoshauri.

Kwa upande wa sekta ya madini, pamoja na kushughulikia masuala ya mapato kama tulivyoyaeleza natarajia kwambaWaziri wa Nishati na Madini William Ngeleja atatoa maelezo na mpango wa kushughulikia masuala yote ya ufisadi na migogoro tuliyoyaeleza kwenye hotuba ya kambi ya upinzani tarehe 15 Julai 2011. Mathalani kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato.

Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Namtumbo) na Bahi Kaskazini (Dodoma) bila serikali kupata mapato yanayostahili wala wananchi wa maeneo husika kunufaika.
Pia Serikali itoe maelezo kuhusu kutokutekelezwa kikamilifu kwa ahadi ya kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo pamoja na kuepusha migogoro ya leseni mathalani mgogoro wa wachimbaji wadogo eneo la Winza wilaya ya Mpwapwa ambao serikali iliahidi bungeni tarehe 9 Julai 2010 kuumaliza ambapo mpaka hivi sasa wanaendelea kuhamishwa kwa nguvu.

Kadhalika Serikali itoa maelezo juu ya shughuli za New Alamasi Ltd iliyochimba almasi katika eneo la Luhumbo bila leseni stahiki, kiasi cha almasi iliyochimbwa kinyemela kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 (kwa miaka 35); zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo haramu ya almasi na hatua zilizochukuliwa kwa wahusika na ikiukaji wa sheria.

Wenu katika utumishi wa umma,


John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-08/08/20113 comments:

Anonymous said...

Mh Mbunge Mnyika. Hivi kwanini DAWASCO hawasimamiwi kidedea kama TANESCO?
Tuna vyanzo vingi vya maji, hawa jamaa wala hawachimbi, wala kusambaza na pia hata uwajibikaji wao wa kutusambazia huduma ya lazima wala hawana habari nayo.
Zaidi tu tunasikia wanaohusika kutajwa kuwania nafasi ya uraisi bila ya wao kutuonyesha wanatujali kivipi sie wananchi.
Huduma ya MAJI na UMEME, kwa wananchi Mh. Mnyika ni ya LAZIMA.
Ebu ipigie debe tuweze kufaidika.

Anonymous said...

Nitaanza harakati dhidi ya DAWASCO kuanzia wiki ijayo kuelekea bajeti ya Wizara ya Maji tarehe 22 Agosti 2011. Mnyika

Anonymous said...

Asante Mh Mnyika, kweli siku hizi tuna viongozi wa kisasa, nashukuru kwa majibu.
Sidhani kama wakina magamba wangethubutu hata kufanya mnayofanya (except Mh Makamba!).