Wednesday, April 4, 2012

Matokeo ya Mkutano wa Mbunge na Wafanyabiashara Ndogondogo

Tarehe 04/04/2012 nilifanya mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500 walioondolewa katika kata ya Ubungo.

Nilianza kwa kuwaeleza wazi kwamba siungi mkono biashara kufanyika katika maeneo hatarishi na maeneo yasiyoruhusiwa kisheria; hata hivyo nimekutana nao kwa kuwa: Mosi; waliniita hivyo nimefika kuwasikiliza kwa kuwa kazi yangu ni kuwakilisha wananchi wote. Pili; kuwaeleza sijaridhika na namna ambavyo serikali imetekeleza zoezi hilo bila kutimiza ahadi zake kwa wafanyabiashara ndogondogo na bila kutushirikisha au walau kutupa taarifa yoyote wakati wowote viongozi wa kuchaguliwa wa eneo husika. Tatu; kukubaliana hatua za pamoja za kuchukua ili kupata mwelekeo muafaka kwa kuzingatia haki, utulivu na fursa kwa waathirika kuendelea na shughuli za kujikimu bila kuwa katika maeneo hatarishi.

Baada ya utangulizi huo niliwapa fursa ya kutoa hoja au kuuliza maswali ambayo masuala mengi yalielezwa au kuulizwa. Baadhi ya masuala na maswali hayo ni:

Stella Mbuba-Yeye alieleza kuwa hawajakutana na serikali na kukubaliana maeneo mbadala kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari. Anasema baada ya kusikia matangazo kwenye vyombo vya habari kuwa kuna maeneo mbadala wametengewa walikwenda kwa mtendaji tarehe 29 Machi 2012 lakini wakajibiwa kuwa ‘aliyewaleta eneo hilo ndiye atayewapeleka anakokujua na mkiendelea kuuliza tutawaitia polisi’.


Omari Cheka-Yeye anasema kwamba biashara ndogo ndogo katika eneo hilo zilipata baraka ya serikali kwa muda mrefu. Mvutano ulijitokeza tu pale wanaojiita ‘matembo’ walipoanza kufanya vitendo vya wizi na ubabe katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo mwezi Januari na Februari 2012 walikaa mikutano kati ya wafanyabiashara wote, serikali za mitaa na viongozi waandamizi wa jeshi la polisi na kuamua kuweka mfumo wa ulinzi shirikishi ili kulinda eneo husika. Katika mikutano hiyo walielezwa wazi waendelee na biashara kwenye eneo hilo kwa kuzingatia utaratibu waliopanga mpaka pale watakapopatiwa maeneo mbadala.

Mama Peter- Yeye anafafanua kwamba masoko yaliyotajwa wanayopaswa kwenda ya Shekilango na Mabibo tayari yamejaa wafanyabiashara wengine. Anasema kuwa sababu kuwa eneo hilo ni hatarishi ilipaswa pia kuhusu kituo cha mabasi ambacho kinamzunguko mkubwa zaidi wa watu siku nzima tofauti na biashara zao ndogondogo ambazo wamekuwa wakizifanya jioni mpaka usiku. Hivyo, hofu ya mitambo kulipuka haiwezi kuwa kwa wafanyabiashara ndogondogo bali hata kwa wananchi wengi wanaotumia kituo cha daladala mpaka sasa.

Rombo Mswaki-Yeye anaeleza kuwa baada ya kukubaliana na serikali na kuweka mfumo wa ulinzi na usafi walifanya pia zoezi la kuandikisha wafanyabiashara ndogo ndogo. Wakapata idadi ya wafanyabiashara waliokuwa na meza na walikuwa kila siku wanakaa na kufanya biashara ni 1440; hawa ni nje ya wafanyabiashara ndogo ndogo wanaoshika bidhaa mikononi. Wafanyabiashara wanachoomba ni kupatiwa eneo mbadala la kuendelea kujiajiri lenye kuwatosha na pia lenye ukaribu na wanunuzi.

Baada ya kuwasikiliza wafanyabiashara ndogondogo hao niliwaeleza kuwa kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi, kuisimamia serikali na kutunga sheria.

Matatizo ya wafanyabiashara ndogondogo katika Jiji na Dar es salaam ni maeneo mengine ya mijini nchini ni ya muda mrefu.

Mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni aliahidi kwamba serikali yake ingeyapatia ufumbuzi wa haraka, hata hivyo Oktoba 2006 mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa baada ya kushughulikia msingi wa matatizo aliongoza uamuzi wa siasa kanyaboya wa kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo kinyume na alichowaahidi wakati wa uchaguzi.

Maelezo aliyoyatoa Rais Kikwete wakati huo ni kuwa tunawaondoa maeneo yasiyorasmi ili kuwapeleka kwenye maeneo rasmi muweze kupata anuani, mafunzo na mitaji; ahadi ambayo haijatekelezwa kwa ukamilifu.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli sasa kuwa wafanyabiashara walioondolewa Ubungo waende Machinga Complex suala ambalo nalo ni propaganda kanyaboya kwa kuwa anafahamu kuwa eneo hilo lina uwezo wa kubeba wafanyabiashara takribani 4,500 wakati ambapo wafanyabiashara ndogo ndogo katika mkoa wa Dar es salaam walio katika maeneo kinyume cha sheria ni zaidi ya 150,000. Hivyo, Mkuu wa Mkoa anapaswa kuonyesha mfano wa kuwapeleka wafanyabiashara ndogondogo waliombele ya ofisi yake na maeneo jirani katika Machinga Complex, ambao pekee watajaza. Nimewaeleza kwamba kama suala ni kuvutia wafanyabiashara ili soko lizoeleke watekeleze ushauri niliowapa kwenye vikao husika wa kuongeza ruti za daladala kupitia eneo husika watoe likizo ya kodi kwa wafanyabiashara ndogondogo kwa muda maalum katika jengo husika kama inavyofanya kwa wafanyabiashara wakubwa kutoka nje wanapokuja kuwekeza nchini.

Nikawaeleza kwamba nilitarajia serikali iweke mkazo katika kukabiliana na vyanzo vya mgogoro wa muda mrefu katika serikali na wafanyabiashara ndogondogo badala ya kujikita katika kushughulikia matokeo pekee. Wafanyabiashara ndogondogo wajaibuka ghafla katika eneo la Ubungo, walianza taratibu huku serikali ikiwaachia na hata kuwatambua kwa njia mbalimbali; hivyo kuwaondoa lazima kutanguliwa na maandalizi ya maeneo mbadala ya kufanyia biashara.

Aidha, wananchi kufanyia biashara katika maeneo yasiyorasmi ni matokeo ya udhaifu wa muda mrefu wa serikali wa mipango miji na kushindwa kutenga maeneo ya biashara na kuuza kinyemela maeneo machache yaliyotengwa kwa huduma za msingi za kijamii. Hivyo, uamuzi wa kufungua ukurasa mpya kurekebisha hali hiyo lazima uambatane na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na huduma nyingine za msingi za kijamii.

Serikali ina wajibu huo pamoja na kuwa biashara inaweza kutazamwa kuwa ni suala la mtu binafsi kwa kuwa wanunuzi wa biashara hizo ni wananchi hususani wa kipato cha chini na hali hii ya kuongezeka kwa uchuuji ni sehemu ya athari za kupungua kwa uzalishaji nchini.

Hali ya taifa ya kiuchumi na kijamii ni chimbuko la ongezeko la wafanyabiashara ndogondogo Jijini Dar es salaam, mathalani kasi ndogo ya ukuaji wa ajira hasa katika viwanda na kilimo ikilinganishwa na idadi kubwa ya vijana wanaohitimu shule na vyuo; biashara hizo ni sehemu ya jitihada za vijana wenyewe ‘kujiajiri’ hivyo kuwaondoa bila mfumo mbadala ni kuchangia katika umaskini.

Hivyo; kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwao tuunganishe nguvu ya pamoja kwa kutumia ibara ya 8 na 63 za katiba kuisimamia serikali ili kuhakikisha wanapata maeneo mbadala ya kuendelea na biashara zao kwa:

Mosi; Tarehe 5 Aprili 2012 kila mmoja wao kwenda Manispaa ya Kinondoni saa 4 Asubuhi kufuatilia eneo mbadala ambalo manispaa imeahidi, kwa kwa maeneo yaliyotajwa yamejaa Manispaa ielekeze eneo ambalo imewatengea. Diwani wa kata husika pamoja na mimi mwenyewe tutawaongoza kufuatilia iwapo Manispaa haitatoa majibu ya msingi. Jimbo la Ubungo linayo maeneo katika eneo jirani na viwanda (Ubungo Industrial Area) ambalo lina baadhi ya viwanja wazi ama viwanda vilivyokufa baada ya kubinafsishwa kiholela; pamoja na mkakati wa ujumla wa kufufua na kuongeza viwanda serikali itekeleze mapendekezo niliyotoa kwa nyakati mbalimbali bungeni na kwa manispaa ya kutwaa au kununua sehemu ya maeneo hayo kwa ajili ya viwanda vidogodogo na biashara ndogondogo ili kuchangia katika ajira kwa vijana. Baada ya hatua hii tutaungana nao kufuatilia katika Mamlaka zingine mpaka kieleweke.

Pili; Nimetoa siku tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika kutekeleza ahadi waliyoniahidi wakati wa vikao vya kamati ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi na kufanya biashara katika maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme Jimboni Ubungo. Ikumbukwe kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo lakini mpaka sasa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa hatua za haraka kuhusu suala hili mara baada ya kuchaguliwa niliendelea kufuatilia kwa njia mbalimbali za kibunge na kuanzisha pia mazungumzo kuhusu umuhimu wa Wizara na TANESCO kuchangia katika azma ya kununua eneo mbadala kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo kama sehemu ya mkakati endelevu wa kuwaondoa karibu na mitambo. Sehemu kubwa ya operesheni inayofanyika hivi sasa inagharamiwa na TANESCO, hivyo ikiwa shirika hilo lina fedha kwa ajili hiyo njia bora zaidi ni kizielekeza kwenye kuchangia ununuzi wa eneo mbadala kwa ajili ya wafanyabiashara na pia kulipa fidia kama ambavyo serikali iliahidi.

Tatu; nimetoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kueleza hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ahadi yake ya aliyoitoa tarehe Oktoba 2010 wakati wa kampeni ya kujenga Machinga Complex nyingine tano; ili kuwe na maeneo ya namna hiyo ya biashara mawili kwenye kila manispaa. Kama serikali ingekuwa imetekeleza ahadi hiyo katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja toka Rais Kikwete aingie madarakani kungekuwa hivi sasa na eneo la wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya elfu saba katika Jimbo la Ubungo. Ahadi hii ingeweza kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kuwa Rais Kikwete alisema mwenyewe Oktoba 2010 kuwa tayari serikali ilikuwa imepata ufadhili wa bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo. Serikali inayokusanya kodi kwa wananchi wote ikiwemo wafanyabiashara ndogo ndogo inawajibu wa moja kwa moja kushughulikia chanzo cha mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati yake wafanyabiashara hao badala ya matokeo. Serikali inatumia nguvu kubwa kwenye kushughulikia vyanzo badala ya matokeo, kama nguvu hizo hizo zingetumika kushughulikia mafisadi wanaoua viwanda na kukosesha ajira kwa vijana au wanaohujumu ruzuku katika kilimo nchi ingepiga hatua kwa haraka zaidi. Hivyo, kusimamia utawala wa sheria kusiishie kwa wafanyabiashara ndogondogo bali nguvu kubwa hiyo itumike pia kuwaondoa katika maeneo yasiyoruhusiwa wafanyabiashara wakubwa ambao wengine wamepora viwanja vya wazi vya umma na wengine wamevamia maeneo ya hifadhi ya barabara.

Nne; Wafanyabiashara ndogondogo pamoja na kuungana nami katika kuisimamia serikali nimewaelekeza nao kwa upande wao waunganishe nguvu yao kutafuta eneo dogo ambalo wanaweza kulitumia wakati huu wa mpito tunaposhughulikia kupata eneo la kudumu. Wamekubali kuchangishana kufanikisha azma hiyo na tumekubaliana kwamba kwa hatua ambayo watakuwa wamefikia watujulishe kwa haraka na wengine ili tuweze kuchangia. Suala hili halihusu tu haki ya wafanyabiashara kujiajiri kwa kuuza bidhaa bali haki pia ya wananchi kupata bidhaa kwa urahisi ndio maana tunapaswa kuunganisha nguvu za pamoja kupata maeneo mbadala ya wafanyabiashara.

Tano; Nitaendelea kuungana na wafanyabiashara ndogondogo na wananchi kufuatilia masuala haya bila kujali kauli zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa kuwa ‘wanasiasa’ hawapaswi kuingilia masuala haya. Mkuu wa Mkoa amesahau kwamba na yeye ni mwanasiasa na hili ni suala la kisiasa linalohusu mgawanyo wa rasilimali za umma. Viongozi wa serikali wamesahau kwamba Mwalimu Nyerere alisema ili nchi iendelee inahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Nimekuwa nikifuatilia masuala haya kuanzia mwaka 2011 bungeni, jiji, mkoani na manispaa; yaliyojitokeza hivi sasa yatasaidia kuongeza msukumo wa hatua za haraka kuchukuliwa. Nitaendelea kufanya siasa safi katika suala hili kwa kuwa ndio kazi ambayo wananchi walinichagua kuifanya na sitaacha kuweka wazi pale wanasiasa au watendaji wa serikali wanapofanya siasa chafu za propaganda hewa bila kushughulikia masuala ya msingi yanayoyakabili makundi ya kijamii nchini na taifa kwa ujumla. Maslahi ya Umma Kwanza.

1 comment:

Anonymous said...

MNYIKA KI UKWELI UMETUSAHAU WAPIGA KURA WAKO, UMEKAA KITAIFA ZAIDI KULIKO KUHUDUMIA WAKAZI WA JIMBO LA UBUNGO, BARABARA ZETU ZOTE NI MBAYA TUNAZUNGUMZIA BARABARA ZA KIWANGO CHA CHANGARAWE KUANZIA YA UKUTA WA POSTA SINZA, MAENEO YA BONYOKWA, KING'ONGO SIJUI UNAWAZA NINI KUHUSU HILI MUHESHIMIWA TUNAHITAJI HUDUMA YA GREDA TU, KIMARA NDIO KABISA UMETUSAHAU.
MPIGA KURA WAKO