Wednesday, January 15, 2014

Taarifa kwa Umma-Nishati ya Umeme


Kufuatia ukimya wa Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka nyingine tangu nitoe mwito kwao tarehe 9 Januari 2014 juu ya ongezeko la bei ya umeme; namshauri Rais Jakaya Kikwete katika mchakato wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kumtaka Waziri Prof. Sospeter Muhongo kujieleza kwake na kwa umma kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa.

Rais Kikwete akumbuke kwamba Waziri Muhongo alisema uongo kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 alipowahakikishia wananchi kwamba bei ya umeme haitapanda hata baada ya TANESCO kuwasilisha mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme.

Kinyume na kauli za Waziri Prof. Muhongo; Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), katika kikao chake cha tarehe 10 Desemba 2013 pamoja na mambo mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko la bei za umeme kwa viwango mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya wateja hatua ambayo itaongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi na itaathiri uchumi wa nchi.

Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwasilisha maombi ya kurekebisha bei ya umeme kwa EWURA. TANESCO ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1 Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17 kuanzia tarehe 1 Januari 2015.

Vilevile TANESCO waliomba kuidhinishwa kwa kanuni ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi ya kitanzania hatua ambazo nazo zina athari katika uchumi na maisha ya wananchi.


Katika muktadha huo; tarehe 9 Januari 2014 nilitoa taarifa ya awali kwa umma kuhusu ongezeko la bei ya umeme lililoanza kutekelezwa. Katika taarifa hiyo pamoja na mambo mengine niliomba maoni ya wadau katika kipindi cha wiki moja juu ya athari za ongezeko hilo na hatua ambazo wananchi wanapendekeza zichukuliwe kurekebisha hali hiyo.

Kabla ya kipindi hicho kumalizika tayari nimepokea maoni ya wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali nchini. Hakuna mwananchi yeyote mpaka hivi sasa kati ya waliotuma maoni kwa njia ya barua pepe aliyeunga mkono ongezeko hilo la bei ya umeme.

Badala yake wananchi hao wameelezea athari ambazo wameanza kuzipata na wamependekeza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kunusuru uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko la gharama za maisha linalotokana na ongezeko la bei ya umeme.

Wananchi wengi wamependekeza kwamba badala ya mamlaka husika kukimbilia kupandisha bei ya umeme ni muhimu kuchukua hatua za kupunguza mzigo mkubwa wa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na uendeshaji wa sekta ya nishati kwa ujumla.

Aidha, wananchi wamependekeza kwamba iwapo mamlaka husika hazitapunguza kiwango cha ongezeko la bei ya umeme; maandamano yaandaliwe kuishinikiza Serikali kuchukua hatua za haraka za kunusuru uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kutokana na ongezeko hilo. Naendelea kupokea maoni ya wananchi mpaka tarehe 17 Januari 2014 kwa barua pepe kupitia mbungeubungo@gmail.com na uchambuzi utakapokamilika nitaeleza hatua tutakazochukua. 

Aidha, pamoja na kuwatakia heri ya Maulidi nawahimiza mnaoguswa na ongezeko la bei ya umeme na hamjatoa maoni mpaka hivi sasa kufanya hivyo kwa maslahi ya umma.


Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 

14/01/2014

No comments: