Friday, October 31, 2014

WAZIRI MUHONGO, WAZIRI MKUU PINDA NA SPIKA MAKINDA WAJITOKEZE KUTOA MAELEZO JUU YA HATUA WALIZOCHUKUA KUHUSU UFISADI NA UDHAIFU KATIKA WIZARA YA NISHATI NA MADINI; WASIPOFANYA HIVYO NITAUREJESHA MJADALA BUNGENI NOVEMBA 2014

Itakumbukwa kwamba tarehe 29 Aprili 2014 kupitia Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini (nimeambatisha nakala)  juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara tajwa kwa mwaka 2014/2015 nilieleza ufisadi na udhaifu uliopo katika Wizara hiyo na mashirika yaliyo chini yake.

Kutokana na kukithiri kwa ufisadi na udhaifu huo nilipendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa katika Mkutano wa 15 wa Bunge uliokuwa ukiendelea wakati huo, nanukuu:

Mosi, Spika aruhusu kabla ya mjadala huu kuendelea ziwekwe mezani nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi kwenye Sekta ya Nishati na Madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa bungeni mpaka sasa.

Pili, Wizara ya Nishati na Madini itakiwe kabla ya mjadala huu kuwasilisha kabrasha la majibu ya michango ya wabunge juu ya makadirio ya mwaka 2013/2014.

Tatu, mara baada ya hoja hii kuamuliwa naeleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kuundwe kamati teule ya kuchunguza masuala tete na tata tuliyoyaeleza katika maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Nne, Waziri Mkuu kwa mamlaka na madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba ya Nchi atakiwe katika mkutano huu wa Bunge kuelekeza Serikali iwasilishe Taarifa Bungeni juu ya maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanyika kwa nyakati mbalimbali juu ya masuala yanayogusa sekta za nishati na madini kama tulivyoyaeleza.”, Mwisho wa kunukuu.

Hata hivyo, katika majumuisho ya mjadala huo hatua hizo hazikuchuliwa na badala yake Waziri wa Nishati Prof. Sospeter Muhongo akaendelea kusema uongo Bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda akapindisha maelezo niliyoyawasilisha Bungeni na Spika Anna Makinda akaikinga Serikali dhidi ya usimamizi wa kibunge. Matokeo yake ni kuwa ufisadi na udhaifu huo katika Wizara ya Nishati na Madini na mashirika yaliyo chini yake umeendelea kulindwa mpaka hivi sasa.

Hivyo, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa Waziri Muhongo, Waziri Mkuu Pinda na Spika Makinda kujitokeza mbele ya umma na kueleza hatua ambazo wamechukua juu ya ufisadi na udhaifu toka kumalizika kwa Mkutano wa 15 wa Bunge mpaka wakati huu.

Aidha, iwapo hawatafanya hivyo ndani ya siku tatu kuanzia tarehe ya kutolewa kwa mwito huu nitaurejesha mjadala juu ya ufisadi na udhaifu huo katika Wizara ya Nishati na Madini katika Mkutano wa 16 wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 3 Novemba 2014 ili kuisimamia Serikali na kuchangia katika uwajibikaji kwa maslahi ya nchi.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)

27 Oktoba 2014.


No comments: