Friday, October 31, 2014

WAZIRI MUHONGO, WAZIRI MKUU PINDA NA SPIKA MAKINDA WAJITOKEZE KUTOA MAELEZO JUU YA HATUA WALIZOCHUKUA KUHUSU UFISADI NA UDHAIFU KATIKA WIZARA YA NISHATI NA MADINI; WASIPOFANYA HIVYO NITAUREJESHA MJADALA BUNGENI NOVEMBA 2014

Itakumbukwa kwamba tarehe 29 Aprili 2014 kupitia Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini (nimeambatisha nakala)  juu ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara tajwa kwa mwaka 2014/2015 nilieleza ufisadi na udhaifu uliopo katika Wizara hiyo na mashirika yaliyo chini yake.

Kutokana na kukithiri kwa ufisadi na udhaifu huo nilipendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa katika Mkutano wa 15 wa Bunge uliokuwa ukiendelea wakati huo, nanukuu:

Mosi, Spika aruhusu kabla ya mjadala huu kuendelea ziwekwe mezani nakala ya ripoti zote za kamati za uchunguzi kwenye Sekta ya Nishati na Madini zilizoundwa na matokeo yake kutowasilishwa bungeni mpaka sasa.

Thursday, October 23, 2014

Pata hapa nakala ya muswada wa Baraza la Vijana la Taifa; boresha tupate baraza bora

Katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.

Narudia tena kuwashukuru vijana na wadau tulioshirikiana kuandaa muswada huo na naomba kuendelea kupata ushirikiano wenu wa karibu katika hatua zinazoendelea.

Kuanzia tarehe 21 Oktoba 2014 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeanza vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo. Nakala tete ya muswada huo inapatikana hapa, tafadhali pakua pitia na wasilisha maoni yako sasa.

Unaweza kuandika maoni yako kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com au kutuma kwa barua pepe kwenda mbungeubungo@gmail.com na nakala kwa Kamati husika ya Bunge kupitia tanzparl@parliament.go.tz.

Ikiwa unataka kutumia njia nyingine kuwasilisha maoni yako tafadhali wasiliana na Gaston Garubimbi 0715/0767-825025 kwa maelezo zaidi. Mdau wa masuala ya vijana zingatia kwamba  zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza  la Vijana la Taifa zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji kamili na wa haraka.

Wednesday, October 8, 2014

Maharamia wamepitisha Katiba haramu: wameanzisha mgogoro chanya na mwanya wa mabadiliko

Dira ni kuwa na katiba bora itakayojenga Tanzania yenye demokrasia ya kweli, uhuru wa kweli na maendeleo endelevu kwa watu wake wote. Lakini uharamia katika mchakato wa katiba mpya umelipasua taifa. Mpasuko huu unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au mgogoro chanya utakaoleta mabadiliko nchini. 

Maharamia wanashangilia kilevi katika Bunge Maalum baada ya kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata theluthi mbili kwa njia kiharamia. Katiba iliyopendekezwa kiharamia ni katiba haramu.

Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi, katiba ya CCM wahafidhiana na mawakala wake inapaswa kupingwa mtaani na mahakamani kwa mbinu mbalimbali. 

Iwe ni kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika sanduku la kura. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba mchakato huu wa mabadiliko ya katiba ni mwanya wa mabadiliko katika taifa letu.

Saturday, September 27, 2014

TAARIFA KWA UMMA

Katika Mkutano wa 14 Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 uliowasilishwa na John Mnyika (Mb).
Baada ya muswada huo kusomwa, Bunge lilielezwa na Mheshimiwa Spika, naomba kununukuu “ Waheshimiwa wabunge, muswada binafsi…. sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.

Hata hivyo, mpaka sasa maelekezo hayo ya Spika hayajatekelezwa hivyo; Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo inataka Spika wa Bunge Anna Makinda kutoa kauli ya: Mosi, kuueleza umma sababu ya maelekezo yake ya muswada huo kuwepo kwenye tovuti ya bunge kwa ajili ya kuwa wazi kwa umma mpaka sasa kutokutekelezwa, Pili, ni lini muswada huo utapangiwa tarehe ya kujadiliwa; Tatu, ni kwanini mpaka sasa muswada huo haujapelekwa kwenye kamati zinazohusika;  Nne, ni upi wakati muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Katika Mkutano wa 14 Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 uliowasilishwa na John Mnyika (Mb).
Baada ya muswada huo kusomwa, Bunge lilielezwa na Mheshimiwa Spika, naomba kununukuu “ Waheshimiwa wabunge, muswada binafsi…. sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Hata hivyo, mpaka sasa maelekezo hayo ya Spika hayajatekelezwa hivyo; Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo inataka Spika wa Bunge Anna Makinda kutoa kauli ya: Mosi, kuueleza umma sababu ya maelekezo yake ya muswada huo kuwepo kwenye tovuti ya bunge kwa ajili ya kuwa wazi kwa umma mpaka sasa kutokutekelezwa, Pili, ni lini muswada huo utapangiwa tarehe ya kujadiliwa; Tatu, ni kwanini mpaka sasa muswada huo haujapelekwa kwenye kamati zinazohusika;  Nne, ni upi wakati muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Ofisi ya Jimbo la Ubungo inawakumbusha vijana na wadau wote wa maendeleo yao kwamba kutokuwepo kwa chombo kinachowaunganisha vijana wote bila kujadili itikadi kufuatilia masuala ya maendeleo ya vijana  kunafanya Wizara mbalimbali za kisekta kutokuzingatia masuala yaliyokipaumbele kwa maendeleo ya vijana.
Mathalani, katika Mkutano huu wa Bunge katika Fungu la 65 la Wizara ya Kazi na Ajira Kitabu cha Nne Cha Miradi ya Maendeleo Kifungu cha 2002, pamoja na wabunge na vijana kupewa matumaini kwamba zimepitishwa bilioni tatu kwa ajili ya mikopo na mitaji kwa vijana ukweli ni kwamba fedha hizo zimepangiwa matumizi ambayo kusipokuwa na chombo cha kuyafuatilia kutakuwa na udhaifu, ufisadi na ubadhirifu kama ilivyojitokeza katika fedha za mifuko ya maendeleo ya vijana  kati ya mwaka 1993/1994 mpaka 2013/2014.
Kwa mujibu wa Kasma za Kifungu hicho cha 2002 cha Bajeti iliyopitishwa ya Fungu 65 Wizara ya Kazi na Ajira, fedha hizo zinazopaswa kuwa za mikopo na mitaji kwa vijana zitatumika milioni 700 kwa ajili ya kulipia utaalamu elekezi (consultancy fees) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana 200 tu; milioni 150 zitatumika kununulia magari Wizarani, milioni 60 zitatumika kwenye matangazo na orodha ndefu nyingine ya  matumizi yasiyo ya lazima ambayo kutokana na ufinyu wa muda sitaendelea kuyataja.
Aidha, katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge waliweka bayana kwamba kiwango kinachotengwa katika Mifuko ya Maendeleo ya Vijana iwe ni kwa Serikali Kuu na hata Halmashauri ni kidogo ukilinganisha na uwezo wa nchi, mahitaji ya vijana na mafungu mengine yasiyo na matumizi muhimu yanavyotengewa fedha nyingi katika baadhi ya Wizara.
Hivyo, ili Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo ni vyombo muhimu kwa maendeleo ya vijana viweze kuanzishwa kwa wakati, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inamkumbusha Spika wa Bunge kuelekeza muswada binafsi uliokwisha wasilishwa kwa Bunge kwa kamati zinazohusika kwa ajili ya kuanza  kuujadili. Suala hili ni muhimu likapata majibu ya mapema ili muswada huo uweze kuwasilishwa Bungeni katika Mkutano wa 16 wa Bunge unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka 2014.
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inatoa mwito pia kwa vijana na wadau wa maendeleo ya vijana kuingilia kati suala hili na kuisimamia Serikali kwa kuzingatia kwamba katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara yenye dhamana ya vijana kwa mwaka 2013/2014 tarehe 21 Mei 2013 mkutano wa 11 kikao cha 30; Serikali ilitumia kisingizio kwamba ‘ni bunge la bajeti’ kukwepa kuwasilishwa kwa muswda Bunge. Hata hivyo, ahadi ya Serikali ya kuwasilisha muswada haikutekelezwa kwenye mikutano mitatu uliyofuatia ya 12, 13, 14 na 15; hivyo mkutano huu wa 16 ni muafaka kuwezesha maamuzi kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.
Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inaukumbusha umma kwamba Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa  Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikiwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.
Imetolewa tarehe 24 Septemba 2014 na:

Aziz Himbuka
Katibu wa Mbunge

Jimbo la Ubungo

Monday, September 8, 2014

Kinondoni Vijana Saccoss (KIVISA) yakabidhiwa Komputa na Kasiki (safe) na Mbunge Mnyika

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika akikabidhi kompyuta na Kasiki (Safe) kwa Kinondoni Vijana Saccoss (KIVISA) ikiwa ni sehemu ya milioni 10 za CDCF tulizotenga kwenye kuchochea vijana na wanawake kujiajiri.

Uzinduzi wa rasimu ya ripoti ya matokeo ya utafiti kuhusu kuongeza ushiriki na uwakilishi wa wanawake,vijana na wenye ulemavu


John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Ubungo Akizindua rasimu ya ripoti ya matokeo ya utafiti kuhusu kuongeza ushiriki na uwakilishi wa wanawake, vijana na wenye ulemavu katika uongozi uliofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)

Monday, September 1, 2014

Mnyika akabidhi vyerahani kutimiza ahadi ya ajira kwa wanawake


Mnyika akibidhi vyerehani na mashine kudarizi kwa VICOBA viwili vya wanawake Kimara na Matete ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya kutoa vifaa vya kuwawezesha kujiajiri vyenye thamani ya jumla ya milioni 10 kwa vikundi mbalimbali jimboni kutoka katika CDCF;

(Kutoka kushoto Diwani Manota, anayekabidhiwa ni Mwenyekiti wa Kikundi na anayeshuhudia ni Mtendaji wa Kata)

Rais Kikwete, Waziri wa Maji Prof Maghembe na Bodi mpya ya DAWASCO

Tarehe 13 Agosti 2014 Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe alizindua Bodi mpya ya Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam (DAWASCO) na kutoa kauli mbalimbali mbele ya vyombo vya habari ambazo zinaendeleza udhaifu ule ule badala ya kuchukua hatua za haraka kunusuru wananchi katika shida kubwa ya upatikanaji wa maji.

Ni suala lililo wazi kwamba kuzindua bodi mpya ya DAWASCO pekee haitoshi, kwa kuzingatia kuwa majukumu makuu ya kuwezesha hatua za haraka yapo chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam (DAWASA) ambayo nayo inahitaji bodi mpya.

Natoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuvunja bodi iliyopo ya DAWASA na kuunda bodi mpya. Aidha, namkumbusha Rais Kikwete kuitisha kikao ikulu pamoja na DAWASCO, DAWASA na Wizara ya Maji kama alivyoahidi mbele ya wananchi mwezi Machi mwaka 2013.

Thursday, July 31, 2014

Kuhusu uongozi mpya wa wilaya ya CHADEMA Ubungo

Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Ubungo, Goodluck Justine (wa kanza kushoto) akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
UONGOZI mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya kichama Ubungo unatarajiwa kujulikana Agosti 3, 2014 baada ya uchaguzi wa ngazi za chini katika wilaya hiyo kukamilika. 

Mbali na viongozi wa wilaya hiyo kujulikana siku hiyo, pia chama hicho kimeeleza kuwa, kimejiandaa vema kuwadhibiti mamluki wasijipenyeze katika uongozi huo. 

Hayo yalibainishwa na Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Ubungo, Goodluck Justine, wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana katika uchaguzi wa ngazi za msingi, matawi na kata. 

Nafasi zitakazowaniwa ni ya mwenyekiti, katibu, katibu mwenezi na mhazini na kwamba, kwa ngazi ya mabaraza ni vijana, wazee na wanawake. 

Monday, July 28, 2014

Mnyika ataka matengenezo ya barabara ya Sinza-Tandale-Magomeni yaharakishwe

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amemtumia mjumbe Meya wa Manispaa ya Kinondoni kutaka afuatilie kwa karibu matengenezo ya Barabara ya Sinza-Tandale-Magomeni (Barabara ya Mlandizi) kuharakishwa.

Mbunge amechukua hatua hiyo baada ya kupita katika barabara hiyo kuanzia maeneo ya Sinza Kijiweni-Mtogole hadi Makanya na kubaini kwamba bado ukarabati haujaanza na hali ya barabara ni mbaya.

Mnyika amewasiliana pia na Mkurugenzi wa Halmashauri kutaka Ofisi yake itoe taarifa kupitia vyombo vya habari tarehe ngapi matengenezo hayo yataanza na lini yanatarajiwa kumalizika.

Mnyika amekumbusha kwamba pamoja na kero ambazo wananchi wanapata hivi sasa Serikali inapaswa kutambua kwamba barabara hiyo ni muhimu katika kupunguza msongamano kwenye Barabara ya Morogoro na inapaswa kupewa kipaumbele wakati huu ambapo ujenzi wa mradi wa mabasi ya haraka (DART) unaendelea na hivyo kuhitajika kwa barabara mbadala.

Sunday, July 20, 2014

Mkutano wa naibu waziri wa maji waingia dosari katika kata ya Goba.


Mnyika amnusuru Waziri Makala

16 Julai, 2014 Na Abdallah Khamis

Naibu Waziri wa Maji, Amos MakalaMBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemnusuru Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala asiendelee kuzomewa na wananchi wakati wa  ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu ya maji jimboni humo.
Mapema wanachama wa CCM wakiwa na bendera zao, walionekana kupangwa ili kumzomea Mnyika ambaye hata hivyo hakuwajali, badala yake aliendelea kuhutubia mkutano huku Makala akionekana kufurahishwa na hali hiyo.
Mnyika alieleza jinsi alivyowapigania wakazi wa Kimara Mavurunza na maeneo mbalimbali ya jiji kupata maji pasipo kujali itikadi zao za vyama.
Alisema ziara hiyo ya naibu waziri ni matokeo yake ya kumbana Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, pamoja na watendaji wa Kampuni ya kusambaza maji ya Dawasa kuhakikisha maji yanapatikana kwa wakazi wa Dar es Salaam.

CCM,Chadema wafanya vurugu ziara ya Makalla, Mnyika

Na Mary Geofrey 16th July 2014
Print
Ujumbe ulioongozana na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ukiwa ndani ya tenki la maji lililopo Chuo Kikuu cha Ardhi jana.
Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walifanya vurugu katika ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla na Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika ya kukagua miradi ya maji katika jimbo hilo.

Mbali na kukagua miradi ya maji, Makalla na Mnyika alitumia ziara hiyo pamoja na kuzungumza na wananchi juu ya mipango na mikakati ya serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa maji jimboni humo.

Vurugu hizo zilianza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mavurunza, Kata ya Kimara, baada ya Mnyika kusimama na kutaka kuzungumza na wananchi kuhusu ujio wa Makalla pamoja na juhudi alizozifanya za kuhakikisha maji yanapatikana.

Baada ya Mnyika kusimama wafuasi wa CCM walianza kumshambulia kwa maneno ya kumtaka kuwa muda wake wa kukaa katika jimbo hilo umekwisha na kwamba, hana kazi nyingine anayofanya zaidi ya kutoa hoja bungeni na kuomba mwongozo wa Spika.

Waziri anusurika kichapo


Imeandikwa na Sharifa Marira

*Aondolewa chini ya ulinzi baada Chadema, CCM kuzusha vurugu

*Ni baada ya kudaiwa kuingiza u-CCM katika ziara ya kiserikali


KITENDO cha Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, kumkaribisha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, kusalimia wananchi kwenye mkutano wa kiserikali, jana kilizua balaa na kulazimisha nguvu za dola kuingilia kati kumnusuru mteule huyo wa Rais.

Tafrani hiyo ilizuka jana mchana huko Goba, wakati Makalla, ambaye yupo kwenye ziara ya siku nne kukagua miradi ya maji jijini Dar es Salaam, alipokuwa katika mkutano wa mwisho wa hadhara kwa siku hiyo.

Kitendo cha kada wa CCM, Madenge, kuitwa jukwaani, hakikuwapendeza wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwapo kwenye mkutano huo, kwa madai kuwa huo haukuwa mkutano wa kisiasa, ndipo wanachama hao walipokumbana na wenzao wa CCM na kuzusha vurugu kubwa zilizodumu kwa takriban dakika 30.

Habari Picha: Ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla katika Jimbo la Ubungo

ZIARA KATA YA KIBAMBA







Tukikagua ujenzi wa tanki la maji katika kata ya Kibamba


John Mnyika, Mbunge wa Ubungo akaiwa amebebwa na wafuasi wa chama chake wakati akiingia eneo la mkutano Kibamba




Diwani wa Kata ya Kibamba akizungumza jambo la Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla


Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akihutubia wananchi wa kata ya Kibamba


Naibu Waziri, Amos Makalla na John Mnyika, Mbunge wa Ubungo wakiondoka katika eneo la tanki-Kibamba

ZIARA KATA YA KIMARA


Naibu Waziri wa Maji Amos Makalla, akimsikiliza kiongozi wa ujenzi wa Tanki la maji lililopo Kimara jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni mbunge wa jimbo la ubungo John Mnyika.


Tanki hili litavunjwa na kujengwa jipya





Mbunge wa Jimbo la Ubungo akizungumza na vyombo vya habari katika ziara hiyo ya kukagua miradi ya maji kata zilizopo Jimboni Ubungo

MKUTANO NA WANANCHI KATIKA UWANJA WA SEKONDARI YA MAVURUNZA


Diwani wa Kimara Pacal Manota, akizungumza katika mkutano huo uliofanyika viwanja vya Sekondari ya Mavurunza


Askari Polisi akiwambeleleza wanaCCM kusikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa meza kuu katika mkutano uliofanyika uwanja wa Sekondari Mavurunza


Wakutanapo Chadema na CCM 


John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Ubungo akizungumza katika mkutano huo na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla uwanja wa Sekondari Mavurunza





Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla akizungumza katika mkutano wa hadhara








Katika hati hati ya kutaka kunusuru fujo zilizoanza kutokea katikati ya mkutano wa hadhara







Ujumbe wa wananchi kwa njia ya mabango





Polisi akijaribu kuwasihi wanaCCM kutulia ili mkutano uweze kuendelea


WanaCCM na WanaCHADEMA akutanapo


Ujumbe katika mabango












Naibu Waziri, Amos Makalla na John Mnyika tukijaribu kuwasihi wananchi toka katika pande zote za vyama kutulia ili mkutano uweze kuendelea









Idd Azzan, Mbunge wa Kinondoni akijaribu kuwatuliza Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge na Diwani wa Kimara, Pascal Manota














Mama Sanare akishauriana na Naibu Waziri, Amos Makalla na John Mnyika, Mbunge wa Ubungo baada ya mkutano kuingiwa na vurugu. Huku Idd Azzan, Mbunge wa Kinondoni akiendelea kuwasihi Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge na Diwani wa Kimara, Pascal Manota


Mama Sanare akishauriana na Naibu Waziri, Amos Makalla na John Mnyika, Mbunge wa Ubungo baada ya mkutano kuingiwa na vurugu


Shukrani kwa picha: Blogu ya Mzuka Kamili (www.mzukakamili-mzuka.blogspot.com)



Tuesday, July 8, 2014

Mnyika adai kutishiwa maisha

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amewaomba wapiga kura wake kumuombea kila siku kutokana na madai kuwa amekuwa akiwindwa na watu wanaotishia uhai wake.
Mnyika alitoa kauli hiyo juzi jioni katika eneo la Mbezi mjini Dar es Salaam, wakati akihutubia mkutano wa hadhara.
“Nimekuwa nikizungumza mambo mengi ninapokuwa bungeni Dodoma, hasa ninapowatetea wananchi na wapiga kura wangu, lakini kuna watu hawafurahishwi kabisa…sasa wamefikia hatua ya kunitishia maisha yangu.

Tuesday, July 1, 2014

Maghembe awasilisha nyaraka za kuhusu Mnyika

Na Mary Geofrey

Prof. Jumanne Maghembe, Waziri wa Maji
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amepokea barua kutoka kwa Katibu wa Bunge ikimjulisha kwamba Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, hatimaye amewasilisha nyaraka na ripoti za utekelezaji wa miradi ya maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Msaidizi wa Mnyika, Aziz Himbuka, inasema kuwa taarifa hiyo imepelekwa katika Ofisi ya Mshauri Mkuu wa Mambo ya Sheria wa Bunge ili iweze kusomwa na hatua zitakazohitajika zichukuliwe.

Alisema Mnyika ataanza kazi ya kuzipitia taarifa hizo katika Ofisi Kuu ya Bunge Dodoma na baada ya kazi hiyo atarejea kuanza ziara ya kikazi jimboni kwake kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu (Julai), 2014.

Mnyika anatarajia kufanya ziara katika kata zote 14, ambayo pamoja na mambo mengine atakagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji.

Saturday, April 12, 2014

MAONI YA WAJUMBE WALIO WA WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA [Kanuni ya 32(4) ya Kanuni za Bunge Maalum, 2014]


UTANGULIZI
Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”[1]

Mafuriko yanayoendelea katika jiji la Dar es Salaam

Nipo bungeni lakini nimepokea taarifa za mafuriko katika maeneo mbalimbali jimboni kama Kibamba, Malambamawili, Makoka nk Nimeshatoa maelekezo kwa Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Mbunge Ubungo kufatilia kwa ukaribu na kuzitaarifu mamlaka husika kwa hatua za haraka. Kwa maeneo mengine yenye mafuriko tafadhali mpeni taarifa kupitia: 0715-379542 au 0784-379542

Sunday, April 6, 2014

Sijaridhika na majibu ya Mkuu wa Mkoa kuhusu mgogoro unaoendelea juu ya usafiri wa pikipiki/bodaboda na bajaji katikati ya jiji la Dar es Salaam

Tarehe 4 Aprili 2014 Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Said Meck Sadiq amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba hawezi kusitisha kwa muda agizo lake la kukataza pikipiki/bodaboda na bajaj kuingia katikati ya Jiji. Mkuu wa Mkoa amenukuliwa akisema kwamba hawezi kufanya hivyo kwa kuwa agizo hilo si la kwake bali la sheria ambayo ameamua kuisimamia.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo kufuatia taarifa yangu ya tarehe 2 Aprili 2014 niliyoeleza kuwa nimemwandikia ujumbe kutaka asitishe kwa muda utekelezaji wa tamko alilotoa tarehe 3 Machi 2014 ili kupisha mazungumzo baina ya Serikali, wahusika wa Bodaboda na Bajaji na wadau wengine muhimu ili kupata ufumbuzi.

Kufuatia kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa nimeipitia kwa mara nyingine tena kifungu kwa kifungu Sheria inayohusika ambayo ni The Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act; sheria namba 9 ya mwaka 2001. Hakuna kifungu chochote katika sheria hiyo kinachokataza pikipiki/bodaboda au bajaj kuingia katika maeneo ya katikakati ya jiji. Hivyo Mkuu wa Mkoa anapaswa kutoa ufafanuzi kwa umma ni sheria ipi hiyo ambayo anaitumia na kifungu kipi hicho cha sheria ambazo kinamzuia kutengua agizo lake.

Ujumbe kwa Wananchi wa Chalinze:

Leo jumamosi 05 Aprili 2014 ni siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze na kesho jumapili 06 Aprili 2014 ni siku ya wananchi kupiga kura. Kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze wa kata mbalimbali mnaoweza kupata ujumbe kwa njia ya mtandao nawajulisha kwamba nitazungumza nanyi katika mkutano wa hadhara leo. 

Kampeni za Chalinze zilizinduliwa na Katibu Mkuu Dr Wilbroad Slaa na zitafungwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Said Issa Mohamed (ZNZ) akiwa na Dr Slaa. Kwa wapenda demokrasia na maendeleo popote mlipo ziungeni mkono timu za viongozi, wanachama na wapenzi kwenye kata na vijiji mbalimbali. Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mratibu Mohamed kupitia 0784246764 au 0784246764.

Wasiokuwa na mtandao naamini timu zetu za kampeni ya chini kwa chini na zenye magari ya matangazo kwa pamoja zitakuwa zimeshawaalika kwa kuzingatia ratiba ya kampeni. Tutahutubia kufunga kampeni kupitia mkutano utakaofanyika eneo la Chalinze Mjini (Sokoni) kuanzia saa 8 mchana na mpaka 12 Jioni nikiwa na viongozi wengine wa kitaifa.

Thursday, April 3, 2014

TAARIFA KWA UMMA

Tangu tarehe 3/3/2014 Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Meck Sadiq ilipotoa tamko la kupiga marufuku biashara ya kusafirisha abiria maeneo ya mijini kwa kutumia usafiri wa bodaboda na bajaji kumekuwa na mgogoro baina ya vijana wanaofanya kazi hiyo kwa upande mmoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa upande mwingine.

Aidha, kufuatia kauli hiyo watumiaji wa kawaida wa pikipiki na bajaji nao wamekuwa wakipata usumbufu wa kukamatwa kamatwa na kusumbuliwa wakidhaniwa kwamba ni sehemu ya biashara ya usafiri kwa kutumia bodaboda na bajaji.

Kadhalika, kuanza tamko hilo limezusha usumbufu kwa abiria ambao walikuwa wakitumia vyombo hivyo vya usafiri kama mbadala wakati huu ambapo ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo kwa Haraka (BRT) imeambatana na ongezeko la foleni katika barabara zinazoelekea mjini.

Kwa upande mwingine pamekuwepo na utata kuhusu mipaka ya Eneo la Katikati ya Mji (Central Business District- CBD) linaloguswa na amri hiyo.

Kwa kuwa mwezi mmoja umepita bila mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi na Serikali yenyewe, nimeamua kuingilia kati ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.

Wednesday, March 26, 2014

Mnyika: Dawasco toeni taarifa mtambo wa Ruvu

26/03/2014 | Posted by Shehe Semtawa

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, ameitaka Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), kutoa taarifa kwa umma kuhusu kuchelewa kukamilika matengenezo ya mtambo wa Ruvu Juu, kunakosababisha upungufu wa maji katika maeneo ya jiji hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano jana, Mnyika alisema baada ya kutokea tatizo hilo aliwasiliana na Dawasco ili kujua hatua walizochukua.

Alisema maelezo waliyompatia ni kuanza kwa matengenezo, hivyo hatua ya kuchelewa kukamilika kwa matengenezo hayo ilipaswa Dawasco kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari, matangazo ikiwemo tovuti yake.

Monday, March 24, 2014

Kuhusu Kituo Kipya cha Daladala Ubungo, Uendelezaji wa Kiwanja na. 2005/2/2 Sinza (Former Simu 2000) na fursa kwa Wafanyabiashara Ndogo Ndogo

Leo 25 Machi 2014 Ofisi ya Mbunge wa Jimbo Ubungo itafanya kazi ya kufuatilia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na Kamati ya Wafanyabiashara ndogo ndogo kuhusu utekelezaji wa mapendekezo niliyotoa tulipofanya ziara ya kikazi katika Stendi mpya ya Daladala ya Ubungo tarehe 6 Januari 2014.

Aidha, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo itatumia nafasi hiyo kufuatilia kwa mamlaka mbalimbali juu ya masuala ambayo mbunge aliyahoji jimboni na bungeni kuhusu wafanyabiashara ndogo ndogo na wazalishaji wadogo ambayo yako katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ikumbukwe kwamba tarehe 6 Januari 2014 nilipofanya ziara ya kikazi ya kufuatilia ujenzi wa Kituo kipya cha daladala katika Kiwanja na. 2005/2/2 Kitalu C Sinza eneo ambalo zamani lilikuwa chini ya “Simu 2000” uendelezaji ulikuwa umefanyika katika ekari nne.

Saturday, March 8, 2014

Ujumbe wangu kwenu siku ya Wanawake: Dhima ni mabadiliko kutimiza dira ya usawa kwa maendeleo ya wote

Tarehe 8 Machi ni Siku ya Wanawake Duniani (IWD). Ujumbe wa siku hii kwa mwaka huu wa 2014 kwa mujibu wa internationalwomenday.com ni “inspiring change” (kuhamasisha mabadaliko). Wakati kwa mujibu wa unwomen.org ni “equality for women is progress for all” (usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote”.

Mchango wa wanawake katika taifa letu unapaswa kuheshimiwa na kila mtu; wanawake ni wazazi, walezi na ni wengi katika jamii yetu. Hata hivyo, ni kundi linalokabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni muhimu kuunganisha nguvu za pamoja katika kuzikabili.

Katika kuadhimisha siku hii ofisi ya mbunge jimbo la Ubungo inafanya kazi nne mahususi zenye kuhamasisha mabadiliko na maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.

Mosi; kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano Ofisi ya Mbunge inapokea mapendekezo toka kwa wanawake na wadau wa masuala ya jinsia ya kuboresha rasimu ya katiba kwenye ibara zenye kasoro. Mkazo haupaswi kuwa kwenye uwiano wa kijinsia na haki za wanawake za ushiriki kwenye chaguzi na uongozi wa kisiasa pekee au kupata ujira sawa kama ilivyo sasa katika rasimu ibara ya 47, bali kuwezesha ushiriki wa wanawake katika uchumi, kumiliki mali na maendeleo kwa upana wake.

Thursday, March 6, 2014

Taarifa kwa Umma: “Kuendelea kwa ‘Kashfa ya IPTL’ mpaka hivi sasa ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa uongozi wa Bunge, ufisadi wa baadhi ya viongozi wa CCM na uongo wa Waziri Muhongo”.

Kwa nyakati mbalimbali kati ya tarehe 27 Februari 2014 na tarehe 5 Machi 2014 vyombo mbalimbali vya habari vimeandika habari na kuchapisha matangazo juu ya TANESCO na IPTL.

Umma uzingatie kwamba ‘kashfa ya IPTL’ ni ya miaka mingi katika taifa letu na inaendelea mpaka hivi sasa kutokana na udhaifu, uzembe, ufisadi na uongo unaotawala. 

Kumbukumbu zangu zinanionyesha kwamba wakati wa kuanzishwa kwake IPTL ilikuwa ni ubia wa kampuni mbili; Mechmar Corporation ya Malysia Bhd na VIPEM ya Tanzania. 

Udhaifu wa Rais unaendeleza ‘kashfa ya IPTL’:

Mwaka 1994 IPTL ilikutana na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini wakati huo Jakaya Kikwete na aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO wakati huo Simon Mhaville. 

Thursday, February 27, 2014

Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum hizi hapa; na masuala yanayohitaji kuungwa mkono ni haya:

Itakumbukwa kwamba tarehe 19 Februari 2014 Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum Pandu Kificho aliteua Kamati ya Wajumbe ishirini yenye uwakilishi wa makundi yote yanayounda Bunge Maalum kwa ajili ya kumshauri kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.

Rasimu ya kwanza ya Bunge Maalum iliandaliwa na Kamati ya Maandalizi chini ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (nakala yake niliwapa hapa: http://goo.gl/hEI4aw ).

Kazi ya mjumbe ni kuwakilisha na kuwasilisha; katika kutekeleza wajibu huo, jana 26 Februari 2014 tulikuwa na Semina ya Bunge Maalum kuhusu Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum toleo la 2014. 

Katika mjadala wa jana niliunga mkono mapendekezo ya rasimu katika sehemu ya nne kuhusu kupunguzwa kwa mamlaka na madaraka makubwa ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum, tofauti na rasimu ya kwanza; sasa maamuzi ya mwenyekiti hayatakuwa ya mwisho. Mjumbe asiporidhika anaweza kukata rufaa na pia rasimu sasa inapendekeza kwamba mwenyekiti au makamu wanaweza kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani.

Niliunga mkono kuruhusiwa kwa utaratibu wa kuwasilisha Taarifa ya Maoni Kinzani (dissenting opionion); hii ni kwa sababu rasimu ya kwanza haikuwa na utaratibu wa uwasilishaji bungeni wa hoja za wabunge, hoja zote ilikuwa ni kamati. Njia pekee ya kuwezesha mawazo mbadala kuweza kufika katika ukumbi wa Bunge kwa ukamilifu ukiondoa michango ya wabunge ni kupitia Taarifa za Maoni Kinzani.

Sunday, February 23, 2014

Pata nakala ya rasimu ya kanuni za Bunge Maalum la Katiba hapa, na shiriki mkutano wa mtandaoni leo tuijadili kutoa maoni na mapendekezo

Ratiba na utaratibu wa Bunge Maalum la Katiba haujatuwezesha kurejea kupata maoni ya mliotutuma au walau kuwekwa utaratibu wa Mwenyekiti wa Muda kuitisha mkutano wa kusikiliza umma/wadau (public/stakeholders hearing) hapa Dodoma.

Nilitoa pendekezo hili kwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge na kwa wadau; rejea: http://mnyika.blogspot.com/2014/02/kwanini-ni-muhimu-tushirikishe-wananchi.html na http://www.ippmedia.com/frontend/?l=64919

Hata hivyo, mjadala wa bungeni unaanza kesho na hatimaye kanuni kupitishwa kwa kile ambacho vyanzo vyangu vimenidokeza kuwa msimamo wa wenye madaraka ni kwamba “mamlaka ya kujitungia kanuni ni ya bunge maalum lenyewe, kutunga kanuni ni suala la ndani la wajumbe wenyewe”.

Kutokana na ukuu na upekee wa kanuni hizi katika uendeshaji wa Bunge Maalum, ni wazi kasoro katika kanuni zitaacha mianya ya maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya katiba kuchakachuliwa badala ya kuboreshwa. 

Aidha, yapo mambo katika rasimu ya kanuni yanayohusu haki, kinga na maslahi ya wajumbe wa Bunge Maalum ambayo katika mizania ya utawala bora ni vyema katika kuyatunga maoni na mapendekezo ya wadau wengine wa nje ya Bunge la Maalum yakatolewa.

TAARIFA KWA UMMA: SAKATA LA FIDIA YA ENEO LA MLOGANZILA

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ameendelea kufuatilia kuhusu fidia ya ardhi ya wananchi wa kata ya Kwembe waliohamishwa baada ya kulipwa fidia ya maendelezo pekee kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila.

Kwa upande mwingine, Mbunge Mnyika ameendelea pia kuhoji katika mamlaka mbalimbali juu ya kauli za viongozi wa Serikali kutamka kwamba eneo hilo lipo katika Mkoa wa Pwani badala ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar Es Salaam.

Tarehe 19 Januari 2014 Mbunge Mnyika alifika katika kata ya Kwembe na kukutana na wananchi kusikiliza malalamiko yao na mara baada ya mkutano huo alizikutanisha kamati mbili zinazofuatilia suala hilo.

Kufuatia hatua hiyo, Mbunge Mnyika aliwasiliana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwakumbusha kutekeleza ahadi zao za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo kufuatia hatua ya mbunge kuhoji suala hilo bungeni kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2011 mpaka 2013. (Baadhi ya rejea kutoka Kumbukumbu Rasmi za Bunge-Hansard zimeambatanishwa).

Saturday, February 22, 2014

Maoni yangu kuhusu matokeo ya kidato cha nne wa mwaka 2013


Maoni yangu kuhusu matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne wa mwaka 2013 yaliyotangazwa na kuelezwa kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.17 yamedhihirisha tahadhari niliyotoa kuhusu mabadiliko ya viwango vya ufaulu yaliyotangazwa na Serikali tarehe 30 Oktoba 2013.

Serikali kwa barakoa (veil) ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) imeamua kulificha taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa (Bad Results of Now). Hivyo, wachambuzi wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili nchi ijue hali halisi kwa manufaa ya wananchi.

Aidha, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuweka wazi kwa umma ripoti za uchunguzi zilizoundwa kuwezesha wananchi kuihoji Serikali iwapo kupanda huko kwa ufaulu ni matokeo ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza au ni kiini macho cha mabadiliko ya wigo wa alama na madaraja?

Ukweli ni kuwa hali ya mazingira ya kujifunza na kujifunzia katika shule nyingi za msingi na sekondari hasa za umma sio nzuri kutokana na kutokuwa na vitabu vya kutosha, maabara za kutosha, waalimu wenye sifa wapo wa kutosha na kuboresha maslahi ya waalimu ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa siku nyingi.

Thursday, February 20, 2014

Rasilimali na mchakato wa kuandika Katiba Mpya

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa wadau wote wa masuala ya rasilimali kuzingatia kwamba rasimu ya katiba haijazingatia masuala ya msingi kuhusu haki ya wananchi kumiliki na kunufaika na rasilimali za nchi. Hatua hii ni kinyume na mapendekezo niliyoyatoa bungeni tarehe 22 Mei 2013 na maoni yangu niliyoyatoa mbele ya tume ya mabadiliko ya katiba pamoja na maoni yaliyotolewa na wadau wengine mbalimbali. 

Katika hotuba yangu ya Bungeni nilitaka Serikali isitishe kuendelea kunadi leseni za vitalu vya gesi mpaka kwanza mchakato wa katiba mpya ukamilike na pawepo sera na sheria zitazoongozwa na katiba mpya. Nilieleza kwamba katiba mpya inapaswa kuwa na ibara mahususi ya haki za wananchi kuhusu rasilimali ikiwemo ardhi, madini, gesi, mafuta, maji, misitu na maliasili zingine. Hata hivyo, katika rasimu ya katiba sura ya nne sehemu ya kwanza inayohusu haki za binadamu hakuna haki yeyote iliyotolewa kwa wananchi kuhusu kumiliki na kunufaika na rasilimali. Nitapendekeza kwa Bunge Maalum ibara mahususi kurekebisha udhaifu huo