Saturday, April 26, 2008

Nimekumbuka ya Aprili Kumi

TAARIFA KWA UMMA
Wabunge wa upinzani wasilaumiwe kususia kikao; waungwe mkono
Spika, Waziri Mkuu, Bunge- Toeni uzito unaostahili kwa suala la Zanzibar
Muafaka si wa CUF na CCM pekee; watanzania tushirikiane kuziba nyufa

Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tunawapongeza wabunge wa kambi ya upinzani kwa juzi kuungana pamoja katika kususia kikao cha Bunge kutokana na serikali inayoongozwa na CCM kuchelewesha kulipatia ufumbuzi suala la mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar.

Aidha kwa namna ya pekee tunawapongeza wabunge wa CHADEMA kwa kuamua kuwaunga mkono wabunge wenzao katika suala hili la kitaifa. Pamoja na kuwa wabunge wa CHADEMA wamerejea kwenye vikao kama ilivyopangwa; tunaamini wabunge wa CUF ambao bado wameendelea kuwa nje ya vikao mpaka 14 Aprili, 2008 nao wanafanya shughuli muhimu tu kwa maendeleo ya demokrasia nchini. Hivyo, tunawataka wasivunjwe moyo na kauli ya Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samuel Sitta kwamba hawatapatiwa posho katika kipindi hicho watakachokuwa nje ya Bunge.

BAVICHA tunaamini kwamba kususia kikao ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa wananchi na wadau wote wa maendeleo kwamba mustakabali wa demokrasia upo mashakani.

Aidha Vijana wa CHADEMA tumeshangazwa na kauli ya Spika wa Bunge, Mheshimiwiwa Samuel Sitta(Mb) aliyoitoa jana ya kubeza uamuzi wa wabunge wa upinzani kutoka kwenye kikao; pamoja na kauli ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda. Tumeshangazwa na kauli za viongozi mbalimbali zilizoelezea kwamba suala hilo bado halikuwa limefikia ngazi ya kibunge, kwamba bado ni suala la vyama viwili vya CUF na CCM. Tumeshangazwa na kauli za viongozi wote hawa kwani tunaamini kwamba wanaelewa kabisa kuwa Rais Kikwete alitoa ahadi bungeni kuhusu kulipatia ufumbuzi tatizo la mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar lakini pia tunaamini kuwa wanatambua suala hilo ni la kitaifa. Tumeshangazwa kwa kauli za viongozi hawa ambao tunaamini wanakumbukumbu zote za yaliyotokea Zanzibar mwaka 1995, 1996, 2000 na 2001 na matokeo yake kwa Taifa kwa ujumla. Tunapenda kuwakumbusha viongozi na watanzania kwa ujumla kwamba katika kushughulikia migogoro mbalimbali katika taifa letu; ni heri ‘kuziba nyufa, kuliko kujenga ukuta’.

Kuhatarishwa huko kwa mustakabali wa demokrasia Zanzibar kumechochewa na maazimio ya Halmashauri Kuu ya CCM iliyoketi Butiama kwenda kinyume na rasimu ya makubaliano ya pande mbili ambayo Kamati za Vyama vya CUF na CCM vilikuwa tayari vimeshayakubali.

Kitendo cha CCM kuzusha mambo mapya, ni ishara ya wazi ya kutafuta mwanya wa kuchelewesha muafaka kuweza kupatikana; na kitendo hiki kimepata baraka ya Serikali kupitia Hotuba ya Rais Kikwete kwa Taifa ambapo alizungumza kwa kofia zote mbili ya chama na serikali na hivyo kuweka wazi msimamo wa serikali pia.

Tunatoa rai kwa Bunge kulichukulia uzito unaostahili suala hili kwa kuwa ahadi ya kulipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo suala la mpasuko wa kisiasa Zanzibar ilitolewa na Rais Kikwete Bungeni miaka kadhaa iliyopita; na ni wajibu wa Bunge kuhakikisha ahadi za Serikali zinatekelezwa. Kama spika Sitta, angekuwa na dhamira ya dhati ya kuona wabunge wa upinzani wanarudi bungeni kuendelea na vikao basi angetangaza wazi kwamba atahakikisha suala hili la mpasuko wa kisiasa Zanzibar, linapewa nafasi ya kujadiliwa katika mkutano huu wa Bunge ama katika maswali na majibu ama katika hoja binafsi.

Vijana wa CHADEMA tunaamini kwamba suala la mpasuko wa kisiasa Zanzibar halihusu vyama vya CUF na CCM tu; linahusu watanzania wote. Hali yoyote inayotokea Zanzibar inagusa vile vile mustakabali wa taifa letu; na kwa kuwa Bunge ni chombo cha juu kabisa cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania- ni lazima bunge na wabunge wote walione suala hili kwa uzito wake mapema na kuchukua hatua zinazostahili.

Vijana wa CHADEMA tunaamini kwamba suala hili la Zanzibar, haliwahusu wabunge wa Zanzibar tu; linahusu wabunge wote Tanzania na wananchi wanaowawakilisha hii ni kwa sababu kitisho kwa demokrasia mahali pamoja na kitisho cha demokrasia mahali pote. Kama demokrasia itaendelea kuminywa Zanzibar na haki kutopatikana kwa ukamilifu wake; basi demokrasia itaendelea kuminywa pia katika majimbo mengine nchini. Kama Serikali ya CCM ikichelewesha kuweka misingi ya kupatikana suluhisho za kisiasa Zanzibar; basi misingi kama hiyo itacheleweshwa katika maeneo mengine. Kama uwanja wa kisiasa Zanzibar hautasawazishwa; basi uwanja wa kisiasa maeneo mengine ya Muungano nao hautasawazishwa kikamilifu kwa ajili ya chaguzi zingine zinazofuata hapa nchini. Matokeo yake yanaathari kwa wabunge wote, hususani wa upinzani na wanachi wanaowawakilisha katika maeneo mbalimbali. Hivyo, tunaamini uamuzi wa wabunge wa upinzani kususia kikao umetokana na kuitambua hali hii na ni sehemu ya kuchukua hatua mapema.

Vijana wa CHADEMA tunatumbua kwamba kwa misingi ya Ripoti ya Kamati ya CCM iliyoshiriki kwenye majadiliano ya Muafaka kati ya CCM na CUF suala la kutaka kufanya kura za maoni halikuzuka katika kikao cha Halmashauri kuu ya chama hicho tu; lilipangwa mara baada ya kukukamilika kwa rasimu ya makubaliano kati ya vyama hivyo. Kutokana na kamati kusema wazi kwamba hoja hiyo imeongezwa ili kuwapiku CUF, ni wazi tunahoji dhamira ya kura hizo za maoni; na dhamira ya CCM katika kulipatia ufumbuzi suala hili; na kuwa kwa kuwa suala hili limepata pia baraka za Rais Kikwete; tunahoji dhamira ya serikali kwa ujumla kulipatia ufumbuzi suala hili.

Vijana wa CHADEMA tunaamini kwamba maamuzi ya CCM ya Butiama yalijaa unafiki wa kisiasa na dhamira hewa; yasipopingwa na wapenda haki na ukweli kote nchini- ni wazi yatarudisha nyuma jitihada za kulipatia ufumbuzi tatizo la mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Lakini pia, yatatengeneza msingi wa CCM na serikali yake kuendeleza pia unafiki wa kisiasa na dhamira hewa katika masuala mengine nyeti yanayolikabili taifa letu ikiwemo ufisadi. Itakumbukwa pia ni Halmashauri Kuu hiyo hiyo, iliyoshindwa kuwashughulikia kikamilifu watuhumiwa wa ufisadi- wale waliofanya ufisadi serikalini na wale waliothibitika kufanya ufisadi ndani ya chama hicho ambao wengi wao ni viongozi waandamizi wa chama hicho. Hivyo, tunawapongeza wabunge wa upinzani kwani uamuzi wao ni ishara ya kususia aina zote za ufisadi na kupinga ubakaji wa demokrasia. Ni ishara ya kutaka umma wa watanzania utambue kwamba kuna tatizo zito la kitaifa ambalo linapaswa kutazamwa na umma. Hivyo, tumefadhaishwa na kauli za baadhi ya watu kwamba kwa kususia kikao kwa siku moja, wabunge wa CHADEMA hawakuwatendea haki wananchi wa maeneo yao. Tungependa kuwakumbusha wananchi wa majimbo mengine nchini kuwa lolote litakalotokea Zanzibar ama eneo lingine nchini, linaathiri pia michakato mingine ya kitaifa na hatimaye kuwaathiri wanachi kwa ujumla katika maeneo mbalimbali.

Vijana wa CHADEMA tunaelewa maana ya kura za maoni na tunaamini katika haja ya ushirikiswaji wa umma chini ya falsafa ya chama chetu ya “Nguvu ya Umma”. Lakini hatua ya kwanza kabla ya kura za maoni; ni wadau walioko kwenye majadiliano kukubaliana na kuyaleta makubaliano yao kwa umma ama moja kwa kwa moja kwa kura za maoni ama kupitia kwenye chombo cha uwakilishi wa umma. Kitendo cha CCM cha kukwepa kupitisha makubaliano hayo katika Halmashauri Kuu yake, na badala yake kuitisha kura za maoni bila kwanza chenyewe kusaini makubaliano hayo; ni ishara ya kwamba chama hicho hakina dhamira ya kweli ya kufanya maamuzi badala yake kinatafuta mwanya wa maamuzi tofauti. Vijana wa CHADEMA tunapenda kuitaahadhariisha serikali na jamii kwa ujumla kwamba kura yoyote ya maoni itakayojaribiwa kufanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ambayo imethibitika kuwa si huru, chini ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo bado baadhi ya watu wanahoji uhalali wake; ni wazi kwamba kura hizo zinaweza zikaibua tena makovu ya chaguzi zilizopita na kuchochea mpasuko mwingine wa kisiasa Zanzibar.

Vijana wa CHADEMA tunaomba umma wa watanzania kuunga mkono jitihada zote za kutoa shinikizo kwa serikali ya CCM kutoa tamko tofauti katika kipindi hiki hiki cha Mkutano wa Bunge.

Vijana wa CHADEMA tunapenda kuona vyama vya CUF na CCM vinarejea katika majadiliano kwa misingi ya rasimu ya makubaliano ya awali na kuridhia makubaliano hayo na hatimaye makubaliano hayo kuletwa kwa umma katika masuala yoyote yale ambayo pande mbili hizo zitakubaliana yanayogusa watanzania kwa ujumla. Wakati umefika sasa wa wadau wengine kuingilia kati na kuhakikisha serikali ya umoja wa kitaifa inaundwa Zanzibar kama hatua ya awali na hatimaye kuweka misingi muhimu ya kuhakikisha chaguzi zijazo katika nchi yetu zinakuwa huru na haki, si Zanzibar tu bali Tanzania kwa ujumla.

Wakati huo huo; vijana wa CHADEMA tunasikitishwa na utamaduni unaonza kukua Afrika wa Vyama vinavyotawala kung’ang’ania madarakani hata pale vinapokataliwa; kwa kuvuruga chaguzi au kukimbilia kuunda serikali za mseto hali ambayo imejitokeza katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya na sasa Zimbabwe. Mwelekeo unaonyesha kwamba watawala wa Afrika baada ya kutoka katika zama za kufanya mapinduzi ya kijeshi na kuchochea vita barani Afrika sasa wanapeleka bara letu katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiraia kupitia kuvuruga chaguzi na kuminya demokrasia. Hali hii imeanza kututisha kama vijana na tungependa mjadala uibuliwe katika taifa letu kuhusu suala hili ili kutuepusha kupitia katika madhila ambayo mataifa mengine yanapitia hivi sasa. Vijana wa CHADEMA tunaamini kwamba ili kujikinga na hali hii ni vyema katika taifa letu tukajenga misingi ya haki, maelewano na amani ambayo inahitaji uwepo wa Taasisi muhimu za kidemokrasia ikiwemo Katiba Mpya na Tume Huru za Uchaguzi.


Imetolewa 10 Aprili mwaka 2008:


John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana
0754694553

No comments: