Monday, September 29, 2008

C/HQ/ADM/BV/20

19 Agosti, 2008

Mhariri,RAI,Da es salaam.

Ndugu,

Malalamiko juu ya gazeti la RAI kukiuka maadili ya uandishi wa habari na kunichafua

Utakumbuka kwamba tarehe 2 Agosti, 2008 wakati Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe(Mb) akiwasilisha malalamiko ya chama chetu kuhusu jinsi vyombo kadhaa ya habari vilivyoripoti tarehe 1 Agosti, 2008 kuhusu yaliyojiri kwenye msiba wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wetu na Mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe; uliibua tuhuma nzito juu yangu. Katika Mkutano huo wa Jukwaa la Wahariri, wewe kama mhariri wa RAI ulinilaumu kuwa mimi ndiye niliyekuwa chanzo cha sintofahamu iliyotokea katika taifa kutokana na msiba huo na kwamba nastahili kubeba lawama kwa yaliyotokea.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Sakina Datoo aliponipa nafasi ya kufafanua kuhusu madai yako; nilikanusha madai yako na nilidokeza kusudio langu la kutafakari na kuchukua hatua zinazostahili kutokana na gazeti la RAI kukiuka maadili ya uandishi wa habari na kunichafua.

Kinyume na madai yako niliweka bayana kwamba kuwa gazeti la RAI ndio lililopotosha na kuudanganya umma, na kuliingiza taifa kwenye hisia tenge kuhusu Kifo cha Chacha Wangwe.

Nikaeleza kuwa gazeti la RAI la alhamisi ya 31 Julai, 2008 lililokuwa na Kichwa cha habari “Wangwe kauwawa” ni moja ya mambo yaliyochochea hisia miongoni mwa wananchi kuhusu ‘kuuwawa’ kwa aliyekuwa kiongozi wetu. Siku hiyo hiyo ya kutoka kwa habari hiyo, ilitokea sintofahamu kwenye msiba Tarime na kupelekea magazeti ya 1 Agosti, 2008 kubeba habari zisizo za kweli kuhusu Mbowe kukaribia kukatwa mapanga nk na kuhusisha kifo hicho na ‘risasi’.

Nilifafanua zaidi kwamba habari hiyo ya ukurasa wa mbele ambacho ilikuwa na kichwa kingine kinachosema “Wataka Polisi iwabane Mnyika na Mallya”, ililenga kujenga hisia kwa wasomaji za kunihusisha na kifo cha Wangwe. Hii ilidhihirika wazi kwa kuwa pamoja na kichwa cha habari kutaka polisi wanihoji, ndani ya habari yenyewe hakukuwa mahali popote ambapo chanzo chochote kimesema nihojiwe na polisi.

Hata aya za ndani za habari yenyewe zilionyesha wazi kukiuka maadili ya uandishi wa habari. Mathalani aya ya kwanza na ya pili za habari hiyo, ambazo zinaeleza kuwa msimamo wa “wazawa wa Tarime” kwamba “chacha ameuwawa’ ulichochewa na kauli zangu; nilikuhoji mbele ya Jukwaa la Wahariri kwanini Habari yenyewe haitaji kauli yangu iliyolalamikiwa na ‘wazawa’ hao. Pia katika habari husika haielezewi popote wazawa hao kutamka bayana kuhusisha kauli zao na msimamo wangu.

Katika habari hiyo, paliwekwa aya, ambayo inataja kwamba msimamo wa Dr Slaa ulikuwa ni kutaka uchunguzi ufanyike wakati mimi nilitoa taarifa kwamba vyombo vya habari kuwa kifo hicho hakitokani na mgogoro ndani ya CHADEMA. Mara baada ya maneno ya habari hiyo, gazeti la RAI likaongezea maswali yafuatayo: “Kwanini Mnyika akimbie kutoa kauli hii? Je, Mnyika ni polisi kutangaza mazingira ya kifo cha Wangwe?Je, Mnyika alikuwepo eneo la tukio?, Je, Ni kinga ipi anayotaka kuweka Mnyika?”

Kutokana na habari hiyo kuongezewa maswali hayo ni dhahiri kuwa maswali hayo yaliongezwa na gazeti la RAI kuibua hisia kwa msomaji za kunihusisha na kifo cha Wangwe.

Gazeti la RAI limekiuka maadili ya uandishi wa habari kwa kushindwa kunihoji na kunipa haki ya kutoa majibu; na katika kipindi chote cha msiba huo gazeti la RAI halikuwahi kufanya mahojiano ya moja kwa moja na mimi kuhusu maswali na masuala ambayo wameandika kwenye toleo hilo yanayonigusa moja kwa moja.

Nikakueleza wewe kama Mhariri wa RAI mbele ya Jukwaa la Wahariri kwamba sisi kama CHADEMA tunafanya kazi kama timu kwa kwamba tulipozipokea tu taarifa za msiba tumekuwa tukibadilishana mawazo na kutoa misimamo ya pamoja. Nikakujulisha kwamba Jumanne 29 Julai, 2008 waandishi wa habari walinifuata ofisini kutaka kujua jinsi CHADEMA tulivyopokea msiba huo.

Waandishi wengi walifika baada ya kikao cha sekretariati ya chama ambacho mimi kama kaimu katibu mkuu(wakati huo), nilikuwa Mwenyekiti wa Kikao. Niliwajulisha waandishi hao jinsi ambayo wamekipokea kifo hicho kwa mshtuko na masikitiko makubwa na kwamba tutaendelea kumkumbuka Chacha kama kiongozi jasiri aliyesimamia yale aliyoyaamini na kuwaeleza taratibu za maombolezo ikiwemo bendera kupepea nusu mlingoti na kufungua daftari la maombolezo.

Baada ya kuhitimisha kutoa taarifa hiyo, kwa nyakati tofauti Mwandishi wa Habari wa Mtanzania, na wa TBC1 waliuliza maswali. Wakati yule wa Mtanzania akiuliza swali kwamba habari za mitaani zinasema kwamba CHADEMA ndio ‘imemuua’ Chacha nini kauli ya chama kuhusu suala hilo? Yule wa TBC1 aliuliza kama kifo hicho hakitokani na mgogoro ndani ya CHADEMA? Wote wawili niliwaeleza kwamba CHADEMA haihusiki na kifo hicho wala hakihusiani na mgogoro ndani ya chama chetu, na kwamba taarifa za awali tulizokuwa tumezipokea toka kwa Kamanda wa Polisi ni kwamba kifo hicho kimetokana na ajali. Nilisisitiza kuwa waandishi wasianze kuitazama CHADEMA badala yake vyombo vya ulinzi na usalama ndio vinawajibu wa kutoa taarifa kamili.

Huu ndio uliokuwa msimamo wa pamoja ambao ulitolewa pia na viongozi wengine wa CHADEMA siku hiyo akiwemo Katibu Mkuu, Dr Slaa. Hata viongozi wa kiserikali akiwemo Spika wa Bunge na Rais wa nchi katika salamu zao na taarifa walieleza kwamba kifo hicho kimetokana na ajali.

Katika Mkutano huo wa Jukwaa la Wahariri nilikuhoji wewe kama Mhariri wa RAI kwamba ni kwanini kati ya watu wote walionukuu taarifa ya polisi kuwa kifo hicho kimetokana na ajali hawakuandikwa na RAI kwamba wamekurupuka kujikinga; na ni kwanini gazeti la RAI halikuandika wahojiwe na polisi kama nilivyoandikwa mimi?

Nilikueleza masikitiko yangu kuwa pamoja na kuwa Jumatano ya tarehe 30 Julai, 2008 mimi mwenyewe nilimwandikia Barua Mkuu wa Polisi(IGP) kutaka uchunguzi wa utata wa mazingira ya ajali uliotokana na kauli tofauti tofauti ambazo zilitolewa na Deus Mallya ukilinganisha na watoto wa marehemu kuhusiana na ajali hiyo; gazeti la RAI halikuitumia kabisa barua hiyo ambayo nilipeleka nakala kwa vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kwa njia ya mtandao na vyombo vingi vya habari vilitoa habari hiyo.

Kwa mtiririko wa mambo ya mwelekeo wa habari hiyo, nilikueleza wazi wewe kama Mhariri wa RAI mbele ya Jukwaa la Wahariri kwamba, habari hiyo ililenga kunichafua jina langu na kunihusisha na kifo cha Chacha Wangwe.

Nimeshangazwa kwamba hata baada ya kutoa maelezo hayo kwako, mbele ya wahariri wenzako; gazeti lako katika matoleo yake yaliyofuata mpaka leo, halijafanya tendo la kiungwana la kurekebisha upotoshaji na upungufu nilioueleza.

Kutokana na hali hiyo, nakuandikia barua rasmi ya malalamiko na kukutaka ufanye yafuatayo katika toleo lako la RAI la tarehe 21 Agosti, 2008:

Gazeti lako liwaombe radhi watanzania kwa kukiuka maadili ya uandishi wa habari; kwa kuandika habari isiyokuwa na ukweli, isiyo sahihi, iliyoegemea upande mmoja, yenye mwelekeo wa uchochezi, yenye kuleta majonzi nk.

Gazeti lako liniombe radhi kwa kunichafua na kunihusisha na “kuuwawa kwa Chacha Wangwe”; liniombe radhi ukurasa wa mbele kwa kiwango na uzito ule ule ambao upotoshoji, uchafuzi na ukiukwaji wa maadili ulifanyika katika toleo lililotoka tarehe 31 Julai, 2008.

Kwa kuwa Vichwa vya Habari vya toleo hilo vilisomwa na vyombo vingine vya habari hususani redio na televisheni siku hiyo, napeleka nakala ya malalamiko yangu kwao ili waweze kuyatoa kwa uzito ule ule ambao ambao walisambaza habari hiyo iliyonichafulia jina langu.

Kadhalika, napeleka nakala ya malalamiko haya kwa menejimenti ya Kampuni ya New Habari Corporation wamiliki wa gazeti la RAI na Imprint Limited wachapishaji wa gazeti kwa ajili ya hatua ambazo wataona zinastahili kuchukuliwa.

Aidha napeleka ya barua hii kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari(MCT) na Katibu Mkuu wa CHADEMA kwa taarifa yao.

Natarajia gazeti lako litatoa ushirikiano wa haraka katika kulinda maadili ya uandishi wa habari nchini kwa kuyafanyia kazi malalamiko yangu.

Wako katika demokrasia na maendeleo.
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana

No comments: