Thursday, October 2, 2008

Salam za rambi rambi za Vifo vya Watoto Tabora

TAARIFA KWA UMMA

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA VIFO VYA WATOTO TABORA

Vijana wa CHADEMA tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watoto na vijana wenzetu wadogo vilivyotokea wakati wa Sikuu ya Iddi mkoani Tabora Oktoba Mosi, 2008.

Kutokana na msiba huo mzito, kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) natuma salamu za pole kwa familia za marehemu wote na kuwaomba wawe na utulivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Aidha tunalitaka Jeshi la Polisi mkoani Tabora kuwajibika kwa uzembe wa kuruhusu watoto chini ya miaka kumi nane kuweza kuingia kwa wingi katika ukumbi wa muziki. Tunaamini kwamba Jeshi la Polisi, lina wajibu wa kusimamia sheria nchini zinazokataza watoto wa umri mdogo kuwepo katika mabaa na vilabu.

Ni vyema vyombo vya dola vikaendelea kuwashikilia wamiliki na waendeshaji wa ukumbi huo ili kuwezesha uchunguzi uweze kufanyika kwa uhuru na kwa ukamilifu na matokeo yake kuwekwa hadharani na hatua zinazostahili ikiwemo za kisheria kuchukuliwa.

Pamoja na kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa ajali hiyo imetokana na watoto kuingizwa katika ukumbi kwa wingi kupindukia; tunatoa mwito kwa timu iliyoundwa kuchunguza ajali hiyo kufanya kazi yake kwa undani na kwa uwazi ikiwemo kuchunguza ujenzi wa jengo hilo linalomilikiwa na asasi ya umma(NSSF) kama lilijengwa kwa ajili ya kumbi za burudani zenye kuweza kukabiliana na ajali kama hiyo iliyojitokeza.

Mwisho, uongozi wa vijana wa CHADEMA Mkoani Tabora utaelekezwa kushiriki maziko kuwakilisha BAVICHA pindi taratibu za maziko zitakapotangazwa.

Imetolewa 2 Oktoba, 2008:John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana Taifa
0754694553

No comments: