Friday, November 7, 2008

TUBADILI MFUMO WA UCHAGUZI KUPATA UONGOZI BORA

TUBADILI MFUMO WA UCHAGUZI KUPATA UONGOZI BORA
Na John Mnyika

Makala yangu ya leo inajikita katika eneo moja tu: “Mfumo wa Uchaguzi Tanzania”. Mfumo ni roho ya uchaguzi na chaguzi ndio msingi wa Siasa. Kama siasa(nikimaanisha siasa safi) ni hitaji muhimu la maendeleo kama alivyowahi kusema hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; basi uendeshwaji wa uchaguzi(kwa maana ya uchaguzi huru na haki); ndio njia ya kulipata hitaji hili. Uendeshwaji wa uchaguzi huru na haki hutupatia pia hitaji lingine la msingi kwa maendeleo- yaani “Uongozi Bora”.

Wakati suala la mfumo wa uchaguzi limeshawekewa sheria zinazosimamia kwa karibu katika nchi zilizoendelea ambapo demokrasia ya mfumo wa vyama vingi imekuwepo kwa miaka mingi; katika nchi zenye demokrasia changa bado tunaendelea kujiuliza maswali na kuibua masuala kwa lengo kupata mifumo ambayo itakidhi mahitaji yetu.

Shabaha ya makala hii ni kuchochea mjadala ambao utawezesha mapitio ya katiba na sheria zinazotawala siasa Tanzania katika muktadha wa mfumo wa uchaguzi na kuhamasisha marejeo ama mabadiliko yanayostahili. Ni lazima tuhakikishe tunaendelea kuwa na “uchaguzi” badala ya “uchafuzi”.

Mfumo wa uchaguzi unaotumika sasa

Mfumo unatotumika Tanzania ni Mfumo wa Wengi Wape; hata hivyo kuna Viti Maalumu vya Wanawake katika ngazi ya Ubunge na Udiwani ambavyo vinagawanywa kwa misingi ya uwiano. Mfumo wa Wengi Wape (Plurality-Majority) ni mfumo ambao hutumia wilaya/jimbo za/la uchaguzi na mgombea anachaguliwa kuwakilisha wilaya/jimbo husika. Tawi la mfumo huu linaloitwa kwa Kiingereza First-Past-the-Post (FPTP) ndilo lililo maarufu sana na hutumika katika nchi nyingi zilizo katika Jumuiya ya madola. Katika mfumo huu vyama huteua wagombea na kuwadhamini katika majimbo. Mgombea anaeshinda kwa kura nyingi kuliko wenzake hata kama hazifikii nusu ndio huwa amechaguliwa na kunyakua kiti kinachogombewa. Mfumo huu unatumika nchini Uingereza, India, Kenya na Tanzania.Mfumo huu pia hupelekea kuwa na chama kimoja chenye uwezo wa kuunda serikali peke yake bila ya kuhitaji vyama vingine na kuwa na mseto. Mfumo huu husaidia wananchi kuchagua watu na sio vyama vya siasa na hivo mpiga kura anaweza kutathmini utendaji wa mbunge au mwakilishi badala ya utendaji wa chama fulani. Mfumo huu ni rahisi kuutumia na unaeleweka miongoni mwa wananchi, wagombea huwa wachache na hata uhesabuji wa kura unakuwa ni rahisi. Mfumo wa wengi wape hupelekea kuminya nafasi za wanawake kuchaguliwa kuingia bungeni. Kwa tamaduni za nchi za kiafrika kwamba mwanamke hawezi kushindana na mwanaume na pia gharama kubwa za uchaguzi katika majimbo, wanawake wanaochaguliwa kuingia bungeni wanakuwa ni wachache sana. Mfumo huu huua ukuaji wa vyama na hivyo nchi kukosa vyama makini. Hii ni kwa sababu, badala ya vyama kufanya kampeni kwa kutumia sera zao, hutumia majina ya watu ambao ni wagombea wao. Hivyo basi mfumo huu hupelekea vyama kubaki dhaifu na kushindwa kushindana na kutotoa mbadala. Vyama katika mfumo wa wengi wape huwa vigumu sana kuwajibika kwa wananchi kwani badala ya kurekebihsa sera zao vyama hubadili wagombea tu na kuwalaghai wananchi na kushinda tena. Maoni ya wananchi yanakuwa hayaheshimiki na nchi inakosa maendeleo kwa sababu ya demokrasia duni inayosababishwa na mfumo wa wengi wape.
Marekekebisho yanayotaka kufanywa na wanaCCM

Katika mtandao wa www.jamiiforums.com pamezuka mjadala kutokana na marekebisho yanayotarajiwa kusukumwa na wanaCCM kuhusu suala la mfumo wa uchaguzi. Marekebisho hayo yameshadokezwa pia na vyombo kadhaa vya habari. Mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo ametoa mchango ambao ni nimeona na vyema nikaukuu kama ulivyo kabla ya kutoa uchambuzi wangu.

Nanukuu: “CCM imebuni kete mpya ya kuizidi CHADEMA na kupunguza nguvu ya upinzani bungeni. Katika mkakati huo mpya ambao umeshapata baraka ya kamati kuu ya chama hicho ukisubiri kupitishwa na NEC hivi karibuni, katiba ya nchi itafanyiwa marekebisho kuweza kutekeleza mkakati huo. Chini ya marekebisho hayo, wabunge wa viti maalum hawatapatikana kwa kuteuliwa na vyama bali watagombea kupitia wilaya ambazo ndizo zitakazo kuwa majimbo ya wanawake pekee. Chini ya mfumo huo mpya, patakuwa na majimbo ya kawaida 232 ambayo yatagombewa na watu wote kwa kama ilivyo utaratibu wa sasa. Kwa upande mwingine viti maalum vya wanawake pekee 75 vitaondolewa na badala yake wanawake watagombea wenyewe kwenye wilaya 130 za Tanzania. Kwa hali hiyo, kutakuwa na ongezeko la wabunge ambalo litalazimisha taifa kupanua tena ukumbi wa bunge na pia bajeti ya matumizi ya wabunge ya mishahara na posho itabidi iongeze kwa zaidi ya bilioni 50. Kwa idadi hiyo ya wabunge, Tanzania itaingia katika kundi la nchi zenye wabunge wengi zaidi.Mkakati huo umebuniwa kupunguza nguvu za kambi ya upinzani hususani CHADEMA ambayo imepata kutokana na kupata wabunge wengi wa viti maalum kutokana na idadi ya kura ambazo chama hicho na vingine vya upinzani vimeokoteza nchi nzima.Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 CHADEMA ilipata wabunge watano tu wa kuchaguliwa lakini ikapata wabunge wa viti maalum sita kutokana na kura ambazo chama hicho kilipata katika uchaguzi. Kama viti maalum vingetolewa kwa idadi ya viti ambavyo chama kimepata chama hicho kingepata kiti maalum kimoja au viwili tu.“Unajua tumeweka sheria inayoisaidia CHADEMA, hawa chini ya Operesheni Sangara hata kama tukitumia nguvu kushinda majimbo bado watapata zaidi ya asilimia 20-40 ya kura katika majimbo mbalimbali hali itayofanya wapate kati ya wabunge 15 mpaka 30 wa viti maalum mwaka 2010. Lazima tutafute njia ya kuwadhibiti mapema kwa kubadili sheria”, alinukuliwa mmoja wa wajumbe wa Kamati kuu ya chama hicho.Timu ya kuandaa mpango huo iliundwa miezi michache iliyopita baada ya kujitokeza fursa ya marekebisho hayo kutokana na Rais Kikwete kutoa ahadi kupitia hotuba yake ya kuongeza uwakilishi wa wanawake bungeni kuwa 50 kwa 50.Timu hiyo ilifanikiwa kushawishi wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kuweka pembeni mapendekezo mengine ya Kamati ya Dr Ghalib Billal ambayo iliundwa baadaye kuchambua kuhusu suala hilo.Kamati hiyo ilikuja na mapendekezo mbalimbali ikiwemo kupanua idadi ya wanawake katika uwakilishi wa uwiano kuwa na orodha yenye uwiano wa majina kijinsia. Aidha pendekezo lingine la kamati hiyo lilitaka uchaguzi uhusishe wagombea wawili mwanamke na mwanaume katika majimbo ya uchaguzi na kupunguza majimbo ya sasa.Mfumo huu mpya unatarajiwa kupata upinzani mkali toka kwa makundi ya kijamii mathalani walemavu na asasi za kiraia.“Unajua mfumo wa sasa wa viti maalum, unatoa fursa ya uwakilishi wa makundi maalum ya wanawake. Kwa mfano, mimi nimechaguliwa kuwakilisha kundi la walemavu. Lakini kwa marekebisho hayo yanayopendekezwa, nitatakiwa nikagombee katika jimbo la uchaguzi. Tunaweza tukapoteza kabisa uwakilishi wa makundi mbalimbali bungeni”, alisema mbunge mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake.Chini ya mfumo mpya hakutakuwa na viti maalum vya makundi kama vijana, walemavu, wawikilishi wa elimu ya juu na mashirika yasiyo ya kiserikali ambavyo vimekuwa vikitengwa na vyama kutokana na uwingi wa viti ambavyo chama kimepata.Makubaliano hayo ya Kamati Kuu yanatarajiwa kuzua mjadala mkali katika kikao cha NEC kutoka kwa wabunge wa majimbo kuhusu hadhi yao katika mfumo mpya.“Inabidi tuelezwe wazi, kati ya wabunge wa wilaya, na wabunge wa majimbo. Ni nani watakuwa na hadhi na mamlaka zaidi chini ya marekebisho hayo”, alisema mbunge machachari wa kanda ya ziwa akitoa maoni yake kuhusu uamuzi wa NEC.Chini ya mapendekezo hayo, mathalani wilaya kama Ilala yenye majimbo mawili ya Ukonga na Ilala itakuwa na wabunge watatu; Mbunge wa Wilaya ya Ilala ambaye atakuwa ni Mwanamke na Wabunge wawili wa majimbo ya Ilala na Ukonga ambao watakuwa ni wa jinsia yoyote.Hata hivyo, ili kupunguza mjadala katika jamii kuhusu mkakati huo, tayari Mkuu wa Mawasiliano amekabidhiwa jukumu la kuundaa umma kukubaliana na marekebisho hayo kupitia propaganda za vyombo vya habari.Kama sehemu ya propaganda hizo imekubaliwa kwamba habari maalum zitolewe na vyombo vya habari kabla zikieleza kwamba marekebisho hayo yanalenga kuundoa migogoro katika vyama vya siasa inayotokana na upendeleo katika uteuzi wa viti maalum kwa kuweka mfumo huu mpya ambao utafanya wanawake washindane wenyewe kwa wenyewe.Habari hizo zitaeleza kwamba CHADEMA ni mfano dhahiri wa migogoro hiyo ya upendeleo wa viti maalum ambayo serikali ya CCM inalenga kuindoa kwa kufanya marekebisho hayo ya katiba ya nchi na sheria za uchaguzi katika upatikanaji wa wabunge wa viti maalum.Changamoto kubwa kwa serikali inatabaki kutumiza ahadi ya kuwa na wabunge kwenye uwiano wa 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume, ahadi ambayo mfumo huu mpya hauwezi kuitekeleza badala yake mfumo huo umeondoa mfumo wa kuthamini kura ambao umekuwa ukitumika katika nchi mbalimbali” Mwisho wa kunuu.

Mabadiliko yanayostahili kufanywa

Katika mazingira ya majadiliano niliyoyanukuu hapo juu, ni wazi suala hili sasa linahitaji mjadala mkubwa wa umma kwa sababu mabadiliko ya katiba na sheria za nchi si hodi ya chama chochote cha siasa au kikundi cha watu wachache; ni suala la maslahi na matakwa ya umma. Mjadala huo umegusia suala la uteuzi wa viti maalumu katika CHADEMA hoja ambayo nimewahi kuiandikia makala mbili mfululizo kama sehemu ya kuchambua vigezo vilivyotumika; makala hizi zinapatikana kupitia mtandao wa http://mnyika.blogspot.com.

Makala ya leo inalenga zaidi kutoa maoni yangu ya kutokubaliana na marekebisho hayo hapo juu ambayo yameanza kujadiliwa. Kwa maoni yangu mfumo wa Uchaguzi urekebishwe na kuruhusu mfumo mchanyato wa uwiano wa kura na mfumo wa “first-past-the-post” badala ya mifumo hiyo iliyotangulia. Mfumo wetu wa uchaguzi unataka Wabunge na Madiwani kupatikana kutoka katika majimbo na kata tu. Marekebisho yanayopendekezwa yanaturudisha nyuma zaidi. Kwa mfumo wa sasa wabunge wanawake hupatikana kwa uwiano wa kura za Wabunge nchi nzima na Madiwani wa wanawake kutokana na uwiano wa viti vya udiwani ambao kila chama kimepata. Lakini Wabunge Wanawake hawana mamlaka ya kisheria kwa eneo maalumu. Kwa sasa ni rahisi kusema kuwa wanatoka mikoani, lakini hii ni kwa sababu tuna chama kimoja kikubwa na hivyo kupata kura za kuenea mikoa yote. Huko mbele, tena na hawa wagombea binafsi, itatokea mikoa ambayo haitapata wabunge wanawake kwa sababu kura hazitotosha kwa chama kimoja kugawa wabunge kila mkoa. Umefikia wakati sasa kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchaguzi ili kuingiza uwakilishi wa uwiano. Kama nchi tutafakari mambo yafuatayo yanayohusu mabadiliko ya mfumo wa kisiasa wa nchi yetu: Mosi; Wabunge wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi watokane na Halmashauri za Wilaya za sasa. Mfano, badala ya Wilaya ya Manispaa ya Kinondoni kuwa na Wabunge watatu, iwe na Mbunge mmoja tu. Halmashauri ya Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji ndio iwe Jimbo la Uchaguzi. Katika ngazi hii wagombea wasio na vyama waruhusiwe pamoja na wale wenye vyama. Kwa hali ya sasa tutapata Wabunge takribani 130 kutoka kundi hili. Idadi yao itaongezeka kutokana na kuongezeka kwa Halmashauri zitakazoundwa pindi mahitaji yanapotokea. Ikumbukwe kwamba katika ngazi ya chini kitovu cha mamlaka ni halmashauri, ambao ni msingi pia hata katika upangaji wa bajeti taifa.

Haitakuwa tena kazi ya Tume za Uchaguzi kuunda Majimbo ya uchaguzi bali vile vigezo vya kuunda Halmashauri (Baraza la Madiwani) vilivyopo kisheria (Local Government Authorities Acts) ndio vitatumika. Pili; Wabunge kati ya 150 na 200 watokane na kura za uwiano (idadi tofauti inaweza kupendekezwa). Vyama vya siasa vitapata viti kutokana na uwiano wa kura ambao kila chama kimepata katika Mkoa.

Chama cha siasa ni lazima kiwe kimepata kwanza asilimia tano ya kura zote zilizopigwa katika Mkoa husika ili kigawiwe viti. Kwa hiyo kila chama kitatengeneza orodha ya wagombea wake kwa kila Mkoa na kuipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Orodha hii iwe katika hali ambayo kama jina la kwanza ni Mwanaume la pili awe Mwanamke, hali kadhalika kama jina la kwanza ni Mwanamke katika orodha la pili liwe la mwanaume. Mikoa itapata idadi ya Wabunge kutokana na vigezo maalumu, mfano idadi ya watu n.k. Kwa mapendekezo haya tuna uhakika wa kuwa na Wabunge wanawake zaidi ya theluthi moja katika Bunge. Lakini pia tutakuwa na uhakika kwamba kila Mkoa utakuwa na Mbunge au Wabunge wanawake. Ama kwa lengo la kuongeza idadi kubwa ya wanawake kuelekea uwiano wa hamsini kwa hamsini(50-50), robo tatu ya wabunge wa uwiano inaweza kuwa ni orodha ya wanawake na robo ikabaki kwa ajili ya wanaume. Lengo la kuwa na orodha ni kuwezesha pia vyama kutumia orodha hiyo kuhakikisha uwakilishi wa makundi ya kijamii mathalani walemavu, vijana na viongozi muhimu wa kijamii ambao ni muhimu kuwepo bungeni.

Mabadiliko haya ya mfumo wetu wa Uchaguzi yana faida nyingi sana. Moja ya faida ni kuvigeuza vyama vyetu vya siasa kutoka katika kushindanisha watu tu, bali pia kushindanisha sera. Kwa sababu wananchi watakuwa wanapiga kura mbili. Kura moja ya chama na kura nyingine ya ama diwani au Mbunge na Rais. Kura ya chama ndio itatufanya kupata wabunge wa uwiano. Wala hatutatumia mfumo mmoja kuzalisha mfumo mwingine. Bali kila mfumo utazalisha Wabunge kuunda Bunge letu. Sisi hatutokuwa wa kwanza kufuata mfumo huu wa uwiano-Msumbiji, Afrika ya Kusini, Ujerumani, Uswidi na hata India.

Vyama vikianza kushindanisha sera tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana kama nchi katika kuimarisha mfumo wa demokrasia na kwa kweli hatutokuwa na wasiwasi wa vyama kudhoofika kutokana na wagombea Binafsi kuruhusiwa. Demokrasia ndani ya vyama itaimarika kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha vyama vinapata wawakilishi wake katika Orodha ya Mikoa kidemokrasia. Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate viongozi bora!

No comments: