Tuesday, March 17, 2009

Ardhi na Maendeleo ya mgeni njoo mwenyeji akonde!

Ardhi na Maendeleo ya mgeni njoo mwenyeji akonde!

Na John Mnyika

Wahenga walisema, mgeni njoo mwenyeji apone. Msemo huu, ni ishara ya baraka njema inayoletwa na wageni chini ya ukarimu wa kiafrika. Hata hivyo, yapo maeneo ambayo ujio wa wageni ama wa mambo mageni umezua hasara kwa upande wa wenyeji. Tunayaona hayo katika maeneo ya uwekezaji ambayo wenyeji wameondolewa kwa shuruti kupisha wageni bila kupata manufaa ya kutosha kutokana na ujio wa wageni hao. Hayo yamejitokeza katika sekta za uchimbaji madini, uwindaji na maeneo mengine yanayohusiana na rasilimali za taifa. Hapo ndio unapoweza kuzuka msemo mpya wa mgeni njoo mwenyeji akonde. Si dhamira ya makala yangu ya leo kuzungumzia hayo ya wageni katika maeneo ya rasilimali wengi wao wakiwa kutoka nje, leo nataka nizungumze kuhusu wageni wa ndani katika sekta ya ardhi.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Ardhi ni msingi wa maendeleo. Hata hivyo, pamoja na kutambua hayo, mpaka sasa sera za serikali inayoongozwa na CCM zimejikita katika kuweka ardhi mikononi mwa serikali badala ya umma. Watanzania wanaoamini kwamba wanamiliki ardhi ni wapangaji tu katika ardhi husika kwa miaka ambayo imetajwa ndani ya hati za umiliki. Unahitajiika msukumo mbadala wa kubadili sera ili kuwe na mfumo wa kuwezesha raia kumiliki ardhi kikamilifu. Hii nayo, si hoja kuu ya makala yangu ya leo.

Chini ya mfumo huu huu tulionao sasa, wako watanzania ambao ni wamiliki wapangaji katika ardhi na kipindi chao cha kumiliki ardhi hiyo bado hakijamalizika lakini serikali inaitaka ardhi yao kwa sababu moja au nyingine.

Hawa wako maeneo mbalimbali ya nchi. Katika mkoa wa Dar es salaam pekee mijadala ya masuala kama haya imetapakaa katika maeneo ya Kigamboni, Tabata, Kurasini, Kibamba na kadhalika. Katika maeneo yote haya wananchi wanapaswa kuhamishwa kupisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Leo najadili eneo la Kwembe kwa kuzingatia msemo wa ‘mgeni njoo mwenyeji akonde’. Ama kwa hakika hakuna anayepinga maendeleo. Maendeleo yanavyopiga hodi kokote ni faida kwa wenyeji kama ambavyo ni faida pia kwa taifa kwa ujumla.

Kijiji cha Kwembe sasa kikiwa na hadhi ya mtaa, kiko katika kata ya Kibamba, Wilaya ya Kinondoni katika Mkoa wa Dar es salaam. Mjadala kuhusu yanayojiri katika mtaa huu unaweza kusaidia watanzania wengine wa maeneo mbalimbali ambayo wanakumbwa na masuala kama hayo hayo.

Izingatiwe kwamba mtaa huu uko katika kata ambayo huko nyuma palijitokeza mgogoro mwengine wa ardhi wakati wa uhamishaji na ulipaji fidia wa wananchi walioko katika eneo la Luguruni kupisha ujenzi wa mji mpya(satellite town).

Mgogoro huu wa awali ulifungua macho watanzania kuhusu ufisadi uliopo katika mfumo wa ardhi hususani katika tathmini na ulipaji fidia kwa wananchi. Ilibainika wazi kwa ushahidi wa nyaraka kwamba kuna watu walilipwa fidia zisizostahili, chini ya mtandao ambao ulihuisha maofisa wa ardhi. Waziri wa Ardhi wa wakati huo, John Magufuli, alipatiwa orodha kamili ya wahusika wa ufisadi huo na aliikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU). Hata hivyo, mpaka leo serikali haijaeleza hatua zilizochukuliwa kwa watu hao. Pengine sasa ni wajibu wa Waziri aliyefuatia wa Ardhi, Zephania Chiligati kueleza kuhusu hatua zilizochukuliwa. Lakini waziri mpya sasa anatuhumiwa kutumia nafasi ya kiserikali kutoa viwanja kisiasa kwa wafanyakazi wa taasisi zinazomilikiwa na CCM ambayo yeye ni Katibu Mwenezi, katika eneo hilo hilo. Kwa upande mwingine pia, ilibainika kuwa wapo wananchi ambao walipunjwa fidia zao kutokana na kutofahamu haki zao na kukiukwa kwa taratibu. Hii iliilazimu serikali kufanya tathmini na kulipa fidia upya. Wakati wananchi wa eneo hilo wakichekelea kulipwa fidia zao upya kwa mujibu wa haki, malipo hayo kwa upande mwingine ni hasara kwa mradi na serikali kwa ujumla kutokana na ulipaji wa fidia kufanyika mara mbili. Kwa vyovyote vile, sehemu ya hasara hiyo inabebwa kwa kodi yangu mimi na wewe. Mradi huo wa Luguruni pekee umeigharimu serikali shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ulipaji fidia pekee. Kiasi hiki ni mara tatu ya jumla ya fedha zote zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mikopo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo katika mkoa mzima wa Dar es salaam.

Kama vile taifa halijajifunza na hasara hii, jirani kabisa na Luguruni katika eneo la Kwembe pameibuka sakata lingine. Watendaji wa wizara ya Ardhi wameingia kisiri siri katika maeneo ya wananchi, na kuanza mchakato wa kuthaminisha mali za wananchi kinyume na taratibu ili kuwahamisha. Tayari wapo wananchi ambao walianza kulipwa fidia bila kufuata taratibu na bila haki zao kulindwa. Nyuma ya mchakato wote palikuwa na upokeaji rushwa na uporaji wa kitapeli wa ardhi ya wananchi. Suala hili lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kutokufahamu haki na wajibu wao katika masuala ya ardhi. Hivyo, baadhi ya wanasiasa na watumishi wasio waamininifu wakatumia mwanya huo kufanya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Ushahidi wa mambo hayo ulidhihirika wazi katika mikutano ya umma.

Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999(Namba 4 na 5 kwa mijini na vijijini) pamoja na kanuni zilizotokana na sheria hiyo zinaeleza bayana misingi muhimu ya kuzingatiwa katika masuala la ardhi. Ardhi inapaswa kutumika kwa ajili ya uzalishaji ama makazi kwa maendeleo endelevu. Katika hali hiyo, katika kuwaondoa wananchi katika ardhi yao, inapaswa kuzingatiwa kwamba ardhi ina maslahi kwao na maslahi yoyote yana thamani inayopaswa kurejeshwa. Hivyo, wananchi wanapopaswa kuhamishwa, uhamishwaji huo lazima uende na fidia kamili na kwa wakati. Sheria na kanuni husika zinataka pia raia wawezeshwe kushiriki katika kutoa mamuzi yanayohusika na umiliki wa ardhi. Kwa upande wa Kwembe hili nalo halikufanyika na hivyo kubatilisha mchakato wa fidia zilizoanza kulipwa.

Ili kutekeleza azma hiyo, kifungu namba 109 cha sheria kimempa mamlaka waziri husika kuandaa kanuni kuhusu ulipaji wa fidia. Mnamo mwaka 2001 Waziri wa Ardhi wa wakati huo, Gideon Cheyo alitunga kanuni kwa notisi namba 78 ya kwenye gazeti la serikali la tarehe 4 Mei mwaka 2001. Hii ni nyaraka ambayo kila mtanzania aliyopo katika eneo ambalo anapaswa kuhamishwa kwa sababu mbalimbali anapaswa kuisoma.

Kanuni hizo ambazo zinatumika mpaka sasa zimeeleza bayana kwamba msingi wa tathmini katika ulipaji na ulipwaji wa fidia ni bei ya soko, ya ardhi na maendelezo ambayo yamefanyika. Kwa maneno mengine, hii ni dhana ya mgeni njoo mwenyeji apone badala ya ile ya mgeni njoo mwenyeji akonde kama ilivyoanza kufanywa katika eneo la Kwembe.

Kanuni zimekwenda mbali zaidi kwa kueleza vigezo vya kukubaliana ‘bei ya soko’. Baadhi ya vigezo vilivyotajwa ni pamoja na mauzo ya karibuni ya ardhi inayoendena na ardhi inayotaka kuuzwa sasa, thamani ya uzalishaji unaofanyika na njia nyinginezo zilizoelezwa. Vigezo hivi havikuzingatiwa katika ulipaji wa fidia ulioanza Kwembe.

Fidia pia imeelezwa kwamba inapaswa kuhusisha si tu thamani ya ardhi bali pia mambo mengine kama usafiri wa kuhama, kodi ya miezi 36(miaka mitatu), faida iliyopotea na usumbufu. Katika eneo la Kwembe, wapo wananchi waliotuhumiwa kuwa waliwapa rushwa watumishi wa ardhi ili wawaandikie fidia kubwa. Lakini walikuja kubaini baadaye kwamba walipewa fidia ya ardhi pekee pamoja na rushwa yao, kiwango ambacho walipwa kupewa kwa haki yao kabisa kilikuwa kikubwa kuliko walichopewa kwa kutoa rushwa. Walidhani wamepata, kumbe walikuwa wamepatikana. Huu ni mfano halisi wa jinsi ambavyo, utamaduni wa ufisadi katika taifa letu unavyoathiri mifumo ya haki. Yaliyotokea Kwembe ni funzo kwa raia kuhusu umuhimu wa utamaduni wa uwajibikaji kama kimbilio la haki za msingi kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Matokeo ya ufisadi huo na matumizi ya madaraka ni baadhi ya wananchi kulipwa fidia kisirisiri kwa kiasi kidogo kwa ekari. Wakati hayo yakifanyike, jirani kabisa na Kwembe eneo la Luguruni thamani ya ardhi iliyofanyika kwa uwazi na kufuata taratibu baada ya nguvu ya umma kuanika ufisadi wa awali ilikuwa ni shilingi elfu 30 kwa mita moja ya mraba. Izingatiwe kwamba ekari moja ina mita za mraba takribani elfu nne. Ndio maana wapo wananchi wa eneo hilo la Luguruni ambao walilipwa takribani milioni mia moja. Pamoja na kuwa eneo la Kwembe si barabarani kama ilivyokuwa Luguruni, bado wananchi walistahili kulipwa fidia stahili inayoendana na thamani halisi ya ardhi na mali zao kwa wakati huu. Hata hivyo, kwa kuruhusu ufisadi, uvunjaji wa sheria/kanuni na matumizi mabaya ya madaraka, baadhi ya wananchi walikaribia kuzikosa haki zao.

Chini ya mchakato wa fidia unaofuata sheria na kanuni, wananchi wanapaswa kujaza fomu namba moja ya ukaguzi kwa ajili ya uthamini wa fidia. Fomu hii ipaswa kujazwa maelezo kuhusu kiwanja, nyumba, maendelezo, matumizi, mazao nk. Hivyo fomu hii inapaswa kujaziwa katika eneo la fidia ili mwishoni ijazwe mmiliki na kiongozi wa eneo. Fomu hii huambatana na picha na michoro. Lakini kwa upande wa Kwembe, watumishi wasio waaminifu, waliwaita wananchi wizarani na kujaza fomu hizo huko. Hatua ambayo inabaditilisha fomu zenyewe ambazo zilishaanza kutumika kulipia fidia. Fedha hizo zilizolipwa kwa njia hii ya kifisadi, ni wazi kwamba zinaweza kupotea na serikali kupata hasara kama ilivyotokea kwa Luguruni.

Maelezo ya fomu ya kwanza huhamishwa katika fomu ya kijani, ambayo nyuma huwa na mchanganuo wa uthamini. Fomu hii ni zana ambayo inaweza kutumiwa vizuri kulinda rasilimali za serikali. Kama fomu hii isipojazwa vizuri, raia anaweza bado kubaki na mali yake na wakati huo huo akawa shahidi upande wa serikali kulinda mali ya umma dhidi ya maofisa wanaotumia mianya kama hiyo kujinufaisha. Ili fomu hii iweze kutumika kutoa fedha za umma kwa ajili ya kulipa fidia inapaswa kuwa na saini za ngazi mbalimbali za utayarishaji na uidhinishaji. Ikiwemo saini ya mthamini mkuu wa serikali na muhuri wake. Kwa upande wa Kwembe, malipo ya awali ya fidia yalitolewa bila kuwa na saini za wahusika, kwa tafsiri ya haraka hizi fedha zilizotolewa pamoja na kuwa zilitoka kwenye mikoba ya umma, zilitolewa na watu binafsi sio serikali. Namna pekee ya kulinda ardhi ya wananchi, na fedha za umma katika mazingira kama hayo ni kufanya uchanguzi wa kina na kuchukua hatua kwa wahusika wote.

Baada ya mambo yote hayo kufunuka, viongozi wa serikali kama kawaida walianza kutumiana mipira. Wakati waziri husika akieleza kwamba mradi uko chini ya wilaya, mkuu wa wilaya yeye alitoa tamko la kutokuwa na taarifa zozote. Hata hivyo, fomu za fidia zilizotolewa zinaeleza kwamba zimetolewa na halmashauri ya manispaa ya Kinondoni. Taifa linaweza kujifunza mambo kadhaa kutokana na sakata linaoendelea Kwembe, na masakata kama hayo yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mosi, ufisadi ni adui wa haki. Wananchi wanaweza kukosa haki zao tu kutokana na mfumo wa rushwa ambao umeota mizizi katika jamii yetu. Hivyo, jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mmoja kwa manufaa yake yeye binafsi na kwa taifa kwa ujumla. Pili, wananchi kutokufahamu sheria na kanuni mbalimbali kunatoa mianya kwa viongozi wasio waadilifu kupitisha taratibu. Tatu; sera za zimamoto huleta mzigo mkubwa wa fidia katika taifa. Laiti kama sera za maendeleo ya makazi zingeweka mkazo katika mipango ya ujenzi wa miji ya muda mrefu na kulinda viwanja vinavyotengwa kwa kazi maalumu, nchi isingebeba mzigo mkubwa wa fidia zinazojitokeza mara kwa mara kwa ajili ya kupisha miradi ya maendeleo. Izingatiwe kuwa fidia hizi hulipwa toka fedha za za walipa kodi ambazo zingeweza kutumika kupeleka maendeleo katika maeneo mengi zaidi. Nne, nguvu ya umma ni nyenzo muhimu ya kukabiliana na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Hivyo, kila wanapopata kero ya msingi, wananchi wanapaswa kuungana pamoja, pale ambapo viongozi wa kuchaguliwa wanapoashindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatetea bado wananchi wanafursa ya kusukuma hatua kuweza kuchukuliwa kwa kutumia njia mbadala. Ushujaa wa wananchi wa Kwembe wa kwenda kutoa taarifa TAKUKURU kwa ajili ya kulinda mali zao na fedha za umma na kuwakataa viongozi wasio waadilifu, unapaswa kuigwa na wengine katika maeneo mengine. Maendeleo katika sekta ya ardhi yaje sambamba na kulinda haki za wenyeji. Wageni waje lakini wenyeji wasikondeshwe.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com

No comments: