Sunday, April 5, 2009

Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia-1

Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia-1

Na John Mnyika

Tubadili mfumo wa uchaguzi tupate uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia; huu ni mwito wangu wa leo ambao unajikita katika eneo moja tu: “Mfumo wa Uchaguzi Tanzania”. Mfumo ni roho ya uchaguzi na chaguzi ndio msingi wa Siasa. Kama siasa(nikimaanisha siasa safi) ni hitaji muhimu la maendeleo kama alivyowahi kusema hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; basi uendeshwaji wa uchaguzi(kwa maana ya uchaguzi huru na haki); ndio njia ya kulipata hitaji hili. Uendeshwaji wa uchaguzi huru na haki hutupatia pia hitaji lingine la msingi kwa maendeleo- yaani “Uongozi Bora”. Suala kuu ni kuwa na mifumo ya kikatiba na kisheria na kiuwanja wa kisiasa ambayo inahakikisha uchaguzi huru na haki. Hili nitalijadili katika makala zangu zitakazofuata siku za usoni tukiwa tunaelekea katika uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2009 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Hata hivyo, mfumo wa uchaguzi ni moja ya masuala muhimu katika mchakato wa uendeshaji wa uchaguzi wa kidemokrasia. Kwa kuwa demokrasia ni utawala wa watu kwa ajili ya watu, uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii katika uongozi ni suala linalopaswa kuhimizwa. Uhusiano wa karibu baina ya hoja ya mfumo wa uchaguzi na haja ya uwiano wa kijinsia unajitokeza katika mazingira hayo.
Wakati suala la mfumo wa uchaguzi limeshawekewa sheria zinazosimamia kwa karibu katika nchi zilizoendelea ambapo demokrasia ya mfumo wa vyama vingi imekuwepo kwa miaka mingi; katika nchi zenye demokrasia changa bado tunaendelea kujiuliza maswali na kuibua masuala kwa lengo kupata mifumo ambayo itakidhi mahitaji yetu.
Shabaha ya makala hii ni kuchochea mjadala ambao utawezesha mapitio ya katiba na sheria zinazotawala siasa Tanzania katika muktadha wa mfumo wa uchaguzi na kuhamasisha marejeo ama mabadiliko yanayostahili. Ni lazima tuhakikishe tunaendelea kuwa na “uchaguzi” badala ya “uchafuzi”.

Masuala ambayo yameibuliwa katika mijadala mbalimbali kuhusu suala hili pamoja na mambo mengine ni tuhuma za uwepo wa ubaguzi, ukabila na upendeleo katika mgawanyo wa viti hivyo. Lakini masuala mazito zaidi, ni mjadala kuhusu dhana na dhima ya viti maalum hususani vya wanawake katika taifa letu katika muktadha wa mfumo wa uwakilishi wa kidemokrasia nchini wenye kuhakikisha uwiano wa kijinsia.

Mfumo unatotumika Tanzania ni Mfumo wa Wengi Wape; hata hivyo kuna Viti Maalumu vya Wanawake katika ngazi ya Ubunge na Udiwani ambavyo vinagawanywa kwa misingi ya uwiano. Mfumo wa Wengi Wape (Plurality-Majority) ni mfumo ambao hutumia wilaya/jimbo za/la uchaguzi na mgombea anachaguliwa kuwakilisha wilaya/jimbo husika. Tawi la mfumo huu linaloitwa kwa Kiingereza First-Past-the-Post (FPTP) ndilo lililo maarufu sana na hutumika katika nchi nyingi zilizo katika Jumuiya ya madola. Katika mfumo huu vyama huteua wagombea na kuwadhamini katika majimbo. Mgombea anaeshinda kwa kura nyingi kuliko wenzake hata kama hazifikii nusu ndio huwa amechaguliwa na kunyakua kiti kinachogombewa. Mfumo huu unatumika katika nchi kadhaa mathalani Uingereza, India, Kenya na Tanzania. Mfumo huu pia husababisha mara nyingi kuwa na chama kimoja chenye uwezo wa kuunda serikali peke yake bila ya kuhitaji vyama vingine na kuwa na mseto. Mfumo huu husaidia wananchi kuchagua watu na sio vyama vya siasa na hivo mpiga kura anaweza kutathmini utendaji wa mbunge au mwakilishi badala ya utendaji wa chama fulani. Mfumo huu ni rahisi kuutumia na unaeleweka miongoni mwa wananchi, wagombea huwa wachache na hata uhesabuji wa kura unakuwa ni rahisi.

Kwa upande mwingine ‘mshindi anachukua vyote’ huathiri ukuaji wa vyama na hivyo nchi kukosa vyama vingi vyenye nguvu. Hii ni kwa sababu, badala ya vyama kufanya kampeni kwa kutumia sera zao, hutumia majina ya watu ambao ni wagombea wao. Hivyo basi mfumo huu hupelekea vyama kuwekwa pembezoni na kushindwa kushindana na kutotoa mbadala. Vyama katika mfumo wa wengi wape huwa vigumu sana kuwajibika kwa wananchi kwani badala ya kurekebisha sera zao vyama hubadili wagombea tu na kuwarubuni wananchi na kushinda tena. Maoni ya wananchi yanakuwa hayaheshimiki kikamilifu na nchi inakosa maendeleo kwa sababu ya demokrasia duni inayosababishwa na mfumo wa wengi wape.

Mfumo wa wengi wape hupelekea kuminya nafasi za wanawake kuchaguliwa kuingia bungeni. Kwa tamaduni za nchi za kiafrika bado kuna imani kwamba mwanamke hawezi kushindana na mwanaume na pia gharama kubwa za uchaguzi katika majimbo, wanawake wanaochaguliwa kuingia bungeni wanakuwa ni wachache sana.

Hali hii inajihidhirisha katika bunge la sasa ambapo katika bunge la lenye wabunge 232 wa kuchaguliwa majimboni, kati yao wanawake waliochaguliwa majimboni hawafiki 20. Hii inaamaanisha kwamba katika bunge letu la sasa, ukiondoa wabunge wa viti maalum vya wanawake; bunge lina zaidi ya asilimia 90 wanaume na wanawake ni chini ya asilimia 10. Ili kufikia lengo la Umoja wa Mataifa(UN) na Umoja wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) lililowekwa na baadaye na Umoja wa Afrika(AU), Tanzania ilitenga viti maalum vya wanawake na kufanya uwakilishi wa wanawake hivi sasa katika bunge letu kuwa takribani asilimia 30 katika bunge zima lenye wabunge takribani 320.

Katika mchakato wa uteuzi wa mwaka 2005 ulianzia kwenye ngazi ya wilaya zao na baadaye kupitia kwenye Kamati Kuu ya chama. Mchakato huu uliongozwa na vipengele vya Katiba ya CHADEMA toleo la mwaka 2004 ambayo ilikuwa ikitumika wakati huo. Vigezo hivyo vilijikita katika kuangalia sifa za uongozi na mchango wa kila mwombaji katika kutimiza wajibu kwa CHADEMA na taifa. Hata hivyo kutokana na matarajio ya uchache wa viti, uamuzi wa kupanga orodha ya mwisho baada ya kupata mapendekezo kutoka ngazi za chini za chama ilibidi ufanyike katika ngazi ya taifa. Hata hivyo, uteuzi wa viti hivyo sita ulifuatiwa na shutuma zilizoelekezwa kwa chama kuhusu upendeleo katika uteuzi huo hoja kuu ikiwa ni tuhuma za ukabila katika uteuzi huo. Niliwahi kuandika huko nyuma uchambuzi wangu kuhusu uteuzi wa viti hivyo ikiwemo ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo katika mfululizo wa makala unapatikana kwenye http://mnyika.blogspot.com ambapo nimeeleza vigezo vigezo vilivyotumika, mafanikio na udhaifu uliojitokeza. Kwa kuwa na viti hivyo 6 kati ya wabunge wake 11, CHADEMA ina uwakilishi wa zaidi ya asilimia 50 wanawake katika timu yake bungeni.CCM kwa upande wake kwa kuwa ilikuwa na viti zaidi ya 50 iliweza kuvigawa viti hivyo kimikoa na kuwashindanisha wanawake katika maeneo yao. Pamoja na hayo bado pamekuwepo na tuhuma za upendeleo na rushwa katika kampeni za uteuzi ndani ya CCM na jumuia zake.

Jambo moja ambalo watanzania ni vyema wakalifahamu; CHADEMA kama chama kinachokua na kubadilika. Mwaka 2006 kilifanya tathamini ya chama, na kuandaa Mpango Mkakati wa chama 2006 mpaka 2010. Na kati ya mambo ambayo chama kiliyatazama ni mfumo wa uteuzi wa wanawake wa viti maalum. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, na mchango mzuri wa wabunge wetu bungeni ikiwemo wa viti maalum, palionekana changamoto- namna kati ya kuwianisha mfumo wa uteuzi kwa vigezo na mfumo wa uteuzi kwa kugombea pekee. Chama kiliona kuna haja ya kuboresha zaidi mfumo wake wa uteuzi wa wabunge hawa, na hivyo, CHADEMA ikabadili katiba yake. Sasa katiba imetoa fursa ya kuanzishwa kwa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), na pamoja na mambo mengine- BAWACHA ndio ambalo sasa linasimamia uteuzi wa wabunge wa viti maalum mwaka 2010, kupitia ushindani wa wanawake wenyewe. Taratibu za BAWACHA sura ya kumi zinaeleza bayana namna ya wabunge na madiwani wa viti maalum watavyopatikana ndani ya CHADEMA kwa kuteuliwa na wanawake wenyewe.

Hata hivyo kuwa na mfumo wa uchaguzi wenye uwiano katika viti vya wanawake pekee umesababisha viti hivyo kwa kuitwa ‘viti maalum vya wanawake’. Matokeo ya kuwa na mfumo usiotazama suala la jinsia kwa upana wake ni nafasi hizi kubebeshwa taswira ya upendeleo katika katiba na sheria kabla hata ya uteuzi wenyewe. Hivyo, hata mchakato wa uteuzi wake klwa mantiki hiyo, viti hivyo, vitaendelea kuonekana kama ni ‘maalumu’, vya ‘upendeleo’ na kwa ujumla vinagawiwa ‘kibaguzi’ kwa wanawake dhidi ya makundi vingine. Vinapatikana kwa ushindani ‘uliofungwa’ miongoni mwa wanawake wengine. Ni watu wenye mtizamo huu mpana ndio ambao wanamsimamo kuwa viti hivyo ‘vifutwe’. Watetezi wa viti hivi wamekuwa wakijenga hoja wakati wote kuwa viti hivyo ni muhimu, kwa kuwa wanawake wamekuwa wakishindwa kushindana na kushinda majimbo na hivyo kufanya uwakilishi wao kuwa duni. Na wanatoa sababu za kihistoria na sababu za vikwazo vya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kama vikwazo vya wanawake kupata nafasi za ubunge. Katika hali hiyo, watatezi hao wanaamini kama uwepo wa viti maalum, ni tiba na daraja la kuwawezesha wanawake kupata nafasi katika siasa.(Affirmative action). Lakini Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) na Wanaharakati wa Haki za Wanawake(FEMACT) wao wamefanya tathmini ya miaka kumi toka viti maalum viazishwe, wakati wa mapitio ya miaka kumi toka tamko la Beijing na kubaini kwamba viti hivi; havijasadia masuala ya wanawake kupewa kipaumbele katika vyombo vya maamuzi, wala havijasaidia kuwezesha wanawake wengi zaidi kuingia katika siasa na kushinda majimboni. Kwa ujumla, viti hivi vinaonekana kuzua ‘upendeleo’, ‘ubaguzi’ nk miongoni mwa wanawake wenyewe na kunufaisha tabaka la wachache. Wapo wenye mtizamo mkali zaidi, kuwa kwa kutengewa ‘viti maalum’, wanawake wanazidi kusukumwa pembezoni mwa mkondo na mfumo wa uwakilishi. Hivyo, mjadala huu unapaswa kuwa mpana zaidi ili kuhakikisha mfumo wa uwakilishi wa uchaguzi na kisiasa mwaka 2009, 2010 na kuendelea unatoa tija inayostahiki kwa makundi yote ya kijamii. Ndio maana kuna haja ya kubadili mfumo wa uchaguzi kupata uongozi bora wenye uwiano wa kijinsia. Katika makala yangu inayofuata nitachambua mfumo uliopitishwa na CCM na kupendekeza mfumo mbadala.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com

No comments: