Monday, January 10, 2011

Mnyika ahimiza wananchi kununua bidhaa za Tanzania

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amewahimiza wananchi wa jimbo hilo na Watanzania kwa ujumla kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa Watanzania hasa wanawake na vijana.

Mnyika alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wanawake wajasiriamali kwenye hafla ya kusherehekea mwaka 2011, Ubungo jijini Dar es Salaam sambamba na kutembelea miradi ya uzalishaji mali inayoendeshwa na kikundi cha Gide Women Group-GWG.

Alisema ongezeko la mfumuko wa bei hapa pamoja na kusababishwa kwa kupanda holela kwa gharama na mzigo mkubwa wa ufisadi unaochangiwa pia na kupungua kwa uzalishaji wa ndani katika taifa na utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

“Wazalishaji wetu wa ndani wapo lakini wanapata changamoto ya kukosa masoko kwa kuwa hapa nchini, kumejengeka utamaduni wa watu kukimbilia bidhaa za nje na pia wajasiriamali wengi kuacha uzalishaji na kujikita kwenye uchuuzi wa bidhaa hizo za kutoka ughaibuni,” alisema.

Mnyika aliongeza kuwa amefurahishwa na jitihada zinazoonyeshwa na wanawake kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya ufugaji kuku wa kienyeji, ushonaji wa vitambaa pamoja na utengenezaji wa sabuni za matumizi ya majumbani hali inayowaongezea kipato cha kujikimu na familia zao.

Naye Mwenyekiti wa kikundi hicho, Rita Paul, alimpongeza Mnyika kwa kushinda katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba ana changamoto kubwa ya kushirikiana na vikundi mbalimbali vya maendeleo katika jimbo hilo.

Aidha, alisema kikundi hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 2007, kimeweza kupokea hisa toka kwa wanachama wake ambazo thamani yake imefikia Sh. milioni 30 japo bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Mnyika alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanawake kushiriki katika mjadala wa katiba mpya kwani unagusa haki za msingi za makundi yote katika jamii na mustakabali wa vizazi mbalimbali.

“Ukifuatilia mjadala wa katiba utakuta umetawaliwa na sauti za wanaume, wanawake wachache sana wametoa misimamo yao, wengi wao ikiwa ni kutokana na nafasi zao kwenye utumishi mathalani, Waziri Celina Kombani, Spika Anne Makinda na wanaharakati kama Ananilea Nkya. Hivyo, nawahamasisha wanawake wa Ubungo kuwa mstari wa mbele kwenye mjadala huu,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema katiba ndiyo inayotoa haki za msingi kama za umiliki wa ardhi, huduma za msingi za kijamii na hata uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi hivyo, wanawake wanapaswa kushiriki kujadili kutokana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazolikabili taifa kuwagusa kwa kiwango kikubwa.

Chanzo: Nipashe (10/01/2011)

No comments: