Tuesday, July 5, 2011

Maji Mavurunza, Kilungule, King'ongo kata za Kimara na Saranga

Nawahimiza DAWASCO/DAWASA kusimamia vizuri wakandarasi ili kukamilisha haraka taratibu za uwekaji wa miundombinu na ufungaji wa vifaa ikiwemo kushirikiana na TANESCO kufikisha umeme katika visima vya maji ili kuwapunguzia kero ya maji wananchi wa kata za Kimara na Saranga.

Hivi karibuni nimefanya ziara katika kata za Kimara na Saranga na kubaini kwamba ukamilishaji wa visima katika mitaa ya Mavurunza, King’ong’o na Kilungule unasuasua kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa nyakati mbalimbali nimekuwa nikifuatilia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa kwa DAWASCO tarehe 24 Mei 2010 la kuchimbwa kwa visima vinane ili kupunguza kero ya maji kwa wananchi wa baadhi ya mitaa ya pembezoni mwa kata za Kimara na Saranga.

Visima hivyo vyenye mtandao wa maji ni suluhisho la mpito la tatizo la maji katika maeneo ya King’ong’o, Kilungule na Mavurunza wakati tukiendelea kufuatilia suluhisho la kudumu linalopaswa kuhusisha pamoja na mambo mengine kuongeza ufanisi wa DAWASCO katika kuwahudumia wateja, kudhibiti ufisadi unaofanywa katika mtandao ikiwemo kukabiliana na upotevu wa maji unaondelea, kuongeza kiwango cha maji toka Ruvu juu kupitia ujenzi wa bomba jipya na Bwawa la Maji Kidunda.

Kupitia kongamano la maji Jimbo la Ubungo la tarehe 31 Januari 2011 tulibaini kwamba ahadi hiyo ilikuwa imesahauliwa na watendaji wakuu wa mamlaka husika hivyo tukakubaliana na wananchi wa maeneo husika kwamba tuunganishe nguvu ya umma katika kuifuatilia itimizwe kwa wakati.

Kwa upande mwingine natoa mwito kwa wananchi wa maeneo husika kuendelea kufuatilia kwa karibu miradi hiyo ili kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Kisima cha King’ong’o namba moja iliahidiwa kwamba kitakamilika mwanzoni mwa mwezi huu na kuzalisha lita 13, 200 kwa saa na kuhududimia wakazi 3100; ujenzi wa matanki na uwekaji wa pampu unapaswa kuharakishwa.

Kisima cha King’ong’o namba mbili uchunguzi wa miamba wa eneo husika ulikamilika toka mwezi Mei 2011 hivyo utaratibu wa zabuni unapaswa kuharakishwa kwa majibu wa sheria hili huduma ya maji iweze kupatikana kwa wananchi.

Kisima cha Kilungule A uchimbaji wake ulianza toka mwezi Oktoba mwaka 2010 kikitarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 19,800 na kuhudumia wastani wa wakazi 4,000; hata hivyo ujenzi wa mtandao, tenki na vioski vitatu ulichelewa kuliko kawaida. Katika hatua ya sasa tayari TANESCO wamekamilisha uchambuzi kwa ajili ya makadirio ya gharama za umeme hata hivyo bado taratibu za kufikisha umeme kwa ajili ya wananchi kupata huduma ya maji zinasuasua.

Kisima cha Kilungule B taratibu zake zilichelewa kuanza mpaka msukumo wa ziada ulipotolewa na eneo na kuchimba kutafutwa mwezi Machi 2011. Hata hivyo, hatua za uchimbaji zimekwama kutokana na wataalamu kuchagua eneo ambalo maji yake hayana ubora wa kutumiwa na binadamu. Hivyo, taratibu za kupata eneo mbadala zinapaswa kuharakishwa ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji.

Kisima cha Mavurunza namba moja ujenzi wake ulianza mwezi Agosti 2010 kikikadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 19,800 na kuhudumia wakazi wapatao 4700. Hata hivyo ujenzi wa mtandao pamoja na ufungaji wa pampu ulisimama kwa muda mrefu. Mnamo mwezi Mei ulikamilika kwa majaribio lakini ulishindwa kuanza kazi kutokana na makosa ya TANESCO ya kufunga umeme wa njia moja (single phase) badala ya njia tatu (three phase); hivyo hatua zinahitajika kurekebisha hali hiyo.

Kutokana na ziara nilizofanya nimebaini kwamba visima ambazo taratibu za ujenzi zinaendelea mpaka sasa ni vitano; wakati ahadi ya Rais Kikwete ilikuwa ni ya visima nane. Hivyo, nahimiza DAWASCO kuanza ujenzi wa visima vingine vitatu katika maeneo ya pembezoni ya kata ya Kimara na Saranga kwa kushirikiana na manispaa ya Kinondoni.

Aidha ni muhimu kwa Wizara ya Maji kuwa na mfumo wa kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu miradi inayoendelea kwa kuwa wakati Rais Kikwete alipotembelea Wizara hiyo yenye makao yake makuu katika jimbo la Ubungo tarehe 24 Machi 2011 alipewa taarifa potofu kuhusu hatua ambayo imefikia katika ukamilisha wa ahadi zilizotolewa kuhusu uchimbaji wa visima. Suala hili ni muhimu kwa kuwa miradi mikubwa inayotaka kuanza kutekelezwa ya ujenzi wa bwawa la Kidunda na ujenzi wa bomba kubwa la maji kwa upande wa Ruvu juu litakaloongeza uwezo wa kusambaza maji kwa wananchi wa kata mbalimbali za jimbo la Ubungo na maeneo mengine unahitaji ufuatiliaji makini na ushirikishwaji mpana wa umma.

Nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Vuai Nahodha kwa kushirikiana nami kuwakumbusha mawaziri wenzake kuhusu ahadi za maji na barabara alizozitoa Rais Kikwete kata ya Kimara kama nilivyomuomba wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza mwezi Mei mwaka 2011.

John Mnyika (Mb)
Bungeni, Dodoma-4/7/2011

No comments: