Friday, January 27, 2012

Kuhusu Msongamano wa Magari DSM na Ziara Kwembe

Nashukuru kwamba jana Serikali ilituma ujumbe wa kuonana ana kwa ana madaktari; hata hivyo ni muhimu ikayafanyia kazi yaliyowasilishwa jana ili leo kuwa na ujumbe mzito zaidi majadiliano yakamilike kwa haraka ili madaktari warejee kazini. Leo naendelea na kazi za kijimbo:

Mosi, nitashiriki mkutano wa wadau kuhusu tatizo la msongamano wa magari katika mkoa wa Dar es salaam. Serikali imeleta kwa dharura mwaliko wa mkutano huo jana hivyo sijapata wasaa wa kuomba maoni yenu kuhusu utekelezaji, mnaweza kuendelea kuyatoa hapa na tutayaunganisha pamoja na kuyawasilisha kwa mamlaka husika. Nimekosa pia fursa ya kuandika uchambuzi wangu kwa ajili ya kuchochea mjadala hivyo hoja zangu nitakwenda kuzitoa moja kwa moja kwenye mkutano papo kwa papo. Kwa ujumla, huu si wakati wa maneno bali matendo; mikutano kuhusu foleni katika jiji la Dar es salaam imeshafanyika kadhaa kati ya mwaka 2005-2010, maoni yametolewa na mipango imeandaliwa. Kinachotakiwa hivi sasa ni kuunganisha nguvu ya wadau katika kuhamasisha na kuharakisha utekelezaji. Na katika kufanya hivyo, kunahitajika nyongeza ya bajeti kwa kuwa kiwango kilichotengwa kwa ajili ya kupunguza msongamano katika jiji la Dar es salaam kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ni kidogo ukilinganisha na ukubwa wa tatizo, kiasi cha mahitaji na hasara ambayo wananchi na nchi inapata kila siku kutokana na msongamano katika Jiji la Dar es salaam.

Kuitishwa kwa mkutano wa leo kumefanya nikumbuke ujumbe wangu ambao niliuandika kwenye mtandao wa Wanabidii tarehe 14 Disemba mwaka 2011 nikichangia mjadala na kujibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa. Takribani mwezi mmoja na nusu umepita toka niandike ujumbe huo, ambapo yapo ambayo tayari nimeshayafuatilia mwezi huu wa Januari kupitia vikao vya bodi ya barabara, RCC, Jiji na Manispaa na hatua zimeanza kuchukuliwa kama sehemu ya kuchangia katika kupunguza foleni katika jiji la Dar es salaam hususani Jimboni Ubungo. Hata hivyo, nanukuu mchango wangu huo kwa kuwa kuna mambo bado ambayo niliyasema wakati huo lakini yanaweza kuendelea kujadiliwa na wadau katika mkutano wa leo:

“ Nitachangia tu kwa ujumla bila kutenganisha hatua kati ya za dharura, muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.


Kuhusu masoko ya jioni, chanzo ni kikubwa zaidi. Kiwango cha magari ni kikubwa ukianzia yanayosafirisha mizigo nje ya nchi, ya wananchi wanaotoka makaz ini na daladala kwa ujumla. hivyo, ni lazima suluhisho lihusishe ama kupunguza uwingi wa magari kwa wakati mmoja au kupanua ukubwa wa eneo la magari kupitia. Kwa sasa mpango uliokubaliwa na serikali ni wa kupanua njia kwa kujenga njia ya kupishana (fly over), hata hivyo kwa kiwango kikubwa ni kauli lakini kwenye bajeti ya 2011/2012 hakujatengwa fedha za ujenzi kwa hiyo ya Ubungo, isipokuwa kidogo kwa Tazara. Hii inafanya kwa mwaka huu mzima kubaki na hatua za kupunguza, nazo ni kuwa na ratiba tofauti baina ya magari ya mizigo ya nje ya nchi na muda ambao wananchi wanakwenda au wanatoka makazini, hili linapaswa kushughulikiwa kwa ushirikiano baina ya wizara ya uchukuzi, mambo ya ndani nk. Aidha, tunaweza pia kwa kuwa Tanroads wameshatangaza kuwa jengo lao liko ndani ya barabara pale Ubungo mataa linaweza kuvunjwa kupata njia ya mkato ya kufika kwenye kituo cha daladala ili kupunguza msongamano kwenye mataa.

Wakati barabara za hewani (fly overs) zikisubiriwa ni muhimu kuharakisha ujenzi wa barabara za mzunguko na mchujo (ring and feeder roads ). Mathalani hakuna sababu ya mtu anayetaka kwenda Mbezi beach ya kawe akitoka Mbezi luis ya Ubungo kwenda mpaka Ubungo mataa wakati ambapo anaweza kupitia njia ya Goba au ya Msakuzi /Mpiji Magohe. Au mtu anayetaka kwenda airport/ukonga toka Kibamba si lazima aende Ubungo Mataa anaweza akapita tu Malambamawili mpaka Kinyerezi. Hii iko hivyo vile vile kwa njia nyingine za mkato kama Msewe, Bonyokwa, Kilungule nk. Barabara zote hizi tayari zimeshafanyiwa upembezi yakinifu, hata hivyo hakuna hatua ya ujenzi iliyoanza zaidi ya ukarabati. Kwenye vikao vya bodi ya barabara nimetaka sana twenda hatua ya ziada kuhusu barabara hizi kwa kuharakisha kufanya tathmini ya fidia. Kwa bahati mbaya kwenye bajeti ya mwaka 2011/12 jumla ya fedha kwa barabara za aina hii ni bilioni tano tu ambazo ni fedha kidogo. Tunapoelekea kufanya mid term budget review mwezi Februari ni muhimu zikaongezwa. Kutakuwa na foleni mbaya zaidi Dsm ujenzi wa barabara za DART utakapoanza kama hatua hizi za dharura hazitachukuliwa. Walau tumeunganisha nguvu za pamoja daraja la Msewe limejengwa na sasa linapitika. Changamoto kubwa ni kwamba sehemu kubwa ya barabara hizi za pembezoni pamoja na umuhimu wake zipo chini ya Manispaa wakati fedha ziko kwenye vyombo vya serikali kuu. Tumeomba kwenye vikao kwamba barabara hizi zipandishwe hadhi kutokana na umuhimu wake katika kupunguza foleni. Hata hivyo, vigezo vya sasa vya upandishaji wa hadhi za barabara vimejikita katika barabara kuu, ndefu na kubwa hivyo ni vigumu kutumika. 

Nimeiomba Wizara na Tanroads kuweka vigezo maalum kwa Dsm kutokana na suala la foleni. Pia, kama katibu wa wabunge wa Dsm niwaeleze kwamba tulikwisha omba bungeni kukutana na Waziri Mkuu kuhusu masuala ya ardhi na barabara. Hivyo, mjadala huu ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kupata mambo ya ziada ya kuzingatia kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.

Kuhusu kituo kikuu cha mabasi ya Ubungo, wazo la njia mbili linatekelezeka kwa kuwa upo uwezekano wa kuwa na njia ya nyuma. Changamoto ni kuwa bado kuna kiwingu kuhusu mwelekeo wa kituo husika. Yapo mapendekezo ya kuwa sehemu ya mabasi iwe na kituo cha nje ya mji, pengine hata Bagamoyo baada ya kukamilika kwa upanuzi wa Barabara husika ili kupunguza msongamano Ubungo. Pia, sehemu kubwa ya kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo itakatwa kwa ajili ya miundombinu na kituo cha mabasi ya Haraka (DART). Hivyo, maamuzi yoyote lazima yatazame picha pana na mpango wa muda mrefu. Kuna mambo mengi bado tunaendelea kutofautiana kuhusu hili ambayo nisingependa kuyatolea maoni hadharani katika hatua ya sasa.

Kwa ujumla, hatua za kupunguza foleni, na hapa nijikite zaidi katika muktadha wa barabara ya Morogoro zinahitaji kushughulikia mfumo mzima.

Kuwe na usafiri wa umma ( mass transit) wa abiria kwa njia ya barabara na kwa njia pia ya treni/reli kwa Dsm. Utekelezaji wa mradi wa DART unaelekea kusuasua hivyo wananchi na wadau kwa ujumla tunahitaji kuunganisha nguvu za pamoja kufuatilia. Aidha, wakati wa mkutano wa nne wa bunge nilisisitiza haja ya ongezeko la bajeti ya uchukuzi kuzingatia pia kuwa na mabehewa kwa ajili ya safari za Dsm.


Barabara hizi za pembezoni zipewe uzito kutokana na matatizo ya foleni. Tubadili mifumo ya ujenzi na ukarabati wake; kama tunazibakiza kwa halmashauri basi bajeti za barabara kwa manispaa zetu toka serikali kuu ziongezwe kwa  sababu ya mahitaji lakini na kuzingatia pia Dsm inachangia kwa kiwango kikubwa mapato yanayotokana na kodi za barabarani na za mafuta. Mathalani sasa hivi kipande kidogo cha barabara toka ubungo maziwa mpaka makuburi external kupitia daraja la Ubungo Kisiwani kinahitaji ujenzi wa daraja kubwa zaidi na upanuzi, lakini ni rahisi kwa Tanroads kutoa jibu jepesi kuwa barabara hiyo iko chini ya Manispaa ya Kinondoni wakati ambapo pamoja na ufupi wake ina umuhimu katika kupunguza foleni. Au barabara ya Kijitonyama mpaka Manzese Chakula bora. Au ujenzi wa madaraja kama ya Golani, Msigani nk. Ni lazima ama serikali kuu iongeze fedha kwa Manispaa au miundombinu husika ijengwe na serikali kuu kupitia Tanroads.

Pia, lazima kupunguza idadi ya malori kwenye barabara ya Morogoro ili kupunguza foleni na ajali kwa kuharakisha matengenezo ya reli nchini ili mizigo mikubwa ibebwe kwa treni. Pia, kuharakisha upanuzi wa barabara ya Bagamoyo ili baadhi ya malori yapitie njia ya Msata badala ya Kibaha. Kwa miaka ijayo hatuwezi pia kuepuka kuipanua barabara ya Morogoro yenyewe.

Hatua za sasa zitasaidia kupunguza tatizo la wakati huu, lakini halitaleta suluhisho la kudumu bila kutazama masuala mapana zaidi ya mipango ya muda mrefu yanayohusu ukuaji wa jij la Dsm. Ni lazima jiji lipanuliwe kwa kuelekea pembezoni kuhakikisha kwamba msongamano unapungua katikati. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba maeneo ya pembezoni yanapimwa na watu kupewa hati ili wakati wote kuhakikisha kwamba ujenzi wetu wa nyumba unaacha barabara za kutosha kwa ajili ya kupunguza mzigo kwa barabara kuu. Aidha, miji ya pembeni yenye huduma za msingi (sattellitte towns) kama ile ya Luguruni Kibamba inabidi ifuatiliwe. Wengine tunaifuatilia, lakini ni jukumu la wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja. Katika vikao nimehoji sana kuhusu uboreshaji wa master plan ya Dsm, tutaendelea kupeana taarifa kuhusu hatua ambayo imefikia.

Kujenga miundombinu pekee, bila kupunguza kiwango cha mfumuko wa wananchi wa maeneo mengine ya nchi kuja DSM hakutaweza kuleta suluhisho la muda mrefu. Hivyo, ni lazima sisi kama viongozi na wananchi wa Dsm tuhakikishe tunachangia katika maendeleo ya maeneo mengine ya nchi ili kupunguza msongamano Dsm,; tushiriki katika kukuza miji mingine nchini. Ukiangalia eneo la Dsm na idadi ya watu, sio mji wenye msongamano ukilinganisha na miji mingine duniani. hata hivyo, kutokana na udhaifu wa muda mrefu katika mipango na miundombinu, gharama ya kulibadili jiji la Dsm ni kubwa sana. Ni muhimu kuweka uwiano baina ya kulibadili Jiji na kujenga majiji mengine.

Wakati hatua hizi za muda mrefu, kuna hatua za haraka zinaweza kuchukuliwa kwa kuboresha utendaji tu wa vyombo vyetu iwe ni serikali za mitaa au serikali kuu ili kwa rasilimali zinazotumika sasa miundombinu iendelezwe na isimamiwe vizuri. Mathalani, jambo dogo tu kama ukarabati wa barabara ya Sinza mpaka Tandale linasababisha sasa hivi foleni inaongezeka; naamini TANROADS wataharakisha zaidi walau hili. Au foleni ya Mbezi Mwisho, wakati ambapo kituo cha mabasi mbezi luis kilichojengwa kwenye eneo la barabara kinachelewa kufunguliwa kwa sababu ya kutokuwa na choo au maofisini. Au malori ya nafaka yanaendelea kuja mjini na kuongeza foleni, badala jiji kuharakisha kukamilisha ujenzi wa kituo na soko la nafaka pale Mbezi ambao umeanza muda mrefu. Tunaendelea kuyafuatilia haya, tunahitaji kuendelea kuyajadili ili kuwez a kuunganisha nguvu za pamoja."

Pili; baada ya mjadala huo nitakuwa na ziara ya kichama katika kata ya Kwembe Jimboni Ubungo. Nitakuwa na kazi ya uzinduzi wa ofisi za chama za matawi mbalimbali pamoja na kuzungumza na wananchi na wanachama katika mikutano ya ndani. Mitaa nitayotembelea ni Kwembe Kati, Kwembe Mpakani, Kwembe Luguruni, Kwembe Kati. Katika mikutano hiyo pamoja na kueleza kazi ambazo tumezifanya katika mwaka 2011 katika kusimamia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo, nitawajulisha pia wananchi na wanachama shughuli ambazo zinatarajiwa kufanyika katika mkutano wa Bunge unaonza tarehe 31 Januari 2012 ikiwemo miswada inayokusudiwa kujadiliwa ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kufanya mikutano kabla ya kila mkutano wa bunge. Hii ni ziara ya pili kabla ya mkutano huu wa sita wa bunge, ziara ya kwanza niliifanya tarehe 12 Januari 2012 kuhusu miundombinu ambayo niliifanya katika kata za Mbezi, Saranga, Kimara na Ubungo.

Nawaomba tuendelee kushirikiana katika kutimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 wa kuwakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia serikali ili kuwezesha maendeleo. Maslahi ya Umma KWANZA.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika(Mb)

No comments: