Saturday, January 14, 2012

TANZIA

Mh. Regia Mtema; Mbunge wa Viti Maalum na 
Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira  
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani. 

Katika uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. 

Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum. 
Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu. 

CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema, wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa chama na kwa taifa. 

Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe. Ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama. 

Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.

Imetolewa na: 


John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments: