Tuesday, September 18, 2012

KAULI KUHUSU TAARIFA YA TANESCO JUU YA MAAMUZI YA MAHAKAMA KUU KWENYE KESI YA DOWANS

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 7 na 8 Septemba 2012 haijatoa ufafanuzi kuhusu masuala niliyotaka Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuyatolea majibu hivyo bado nasubiri kauli zao kuhusu maamuzi ya mahakama kuu kwenye kesi ya TANESCO na Dowans na kuhusu matumizi katika kesi ya IPTL.

Aidha, taarifa hiyo imeibua tena mjadala kuhusu ufanisi wa makampuni binafsi ya wanasheria yanayoishauri TANESCO na kuiwakilisha mahakamani hivyo narudia kutoa mwito kwa Serikali kuagiza ukaguzi na uchunguzi unaoendelea kuhusu tuhuma za ufisadi na ubadhirifu ndani ya TANESCO kuhusisha pia ukaguzi na uchunguzi wa matumizi ya fedha na ufanisi wa huduma za kisheria ambazo TANESCO ikitumia katika kesi za Dowans na IPTL.

Jana tarehe 7 Septemba 2012 nilitoa kauli kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ya kuitaka serikali isitumie kizingizio cha maamuzi ya Mahakama Kuu ya juzi tarehe 6 Septemba 2012 kuharakisha mpango wa kuilipa Dowans kwa fedha za walipa kodi watanzania au kubebesha mzigo huo kwa wateja wa TANESCO.


Badala yake niliitaka Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kueleza hatua zilizochukuliwa toka TANESCO ilipowasilisha mahakama ya rufani taarifa ya kusudio la kukata rufaa na kutaja kiasi cha fedha za umma zilizotumika kulipa makampuni binafsi ya uwakili katika kesi ya Dowans, IPTL na zingine kubwa zenye kubebesha mzigo TANESCO kutokana na mikataba mibovu iliyoingiwa.

Tarehe 7 na 8 Septemba 2012 Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kwa Ofisi ya Uhusiano Makao makuu limetoa taarifa kwa umma kuhusu maamuzi ya mahakama kuu kwenye kesi ya Dowans kuwa ‘hakuna hukumu iliyotolewa ya kuamuru TANESCO kuilipa Dowans dola za kimarekani milioni 96’.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kilichoamuliwa ni kuwa mahakama kuu haina mamlaka ya kusikiliza ombi la kuzuia utekelezaji wa hukumu ya ICC na kuwa mamlaka hayo yapo katika mahakama ya rufaa.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya TANESCO kwa umma haijatoa majibu kwa masuala niliyotaka Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iyatolee ufafanuzi kwa umma na inaibua mjadala zaidi kuhusu ufanisi wa makampuni binafsi yanayoiwakilisha Serikali na TANESCO katika kesi mbalimbali zinazoendelea.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa TANESCO kupitia kwa mawakili wake ikiwemo Kampuni ya Wanasheria ya Rex Attorney ilifungua maombi mawili mojawapo likiwa ombi la kusitishwa utekelezaji wa hukumu ya ICC, hata hivyo tarehe 6 Septemba 2012 mahakama kuu ilitupilia mbali ombi hilo la TANESCO kwa misingi kuwa mahakama kuu haina uwezo wa kisheria kutoa uamuzi unaohusu ombi la rufaa ambalo limeshawasilishwa mahakama ya rufaa.

TANESCO inapaswa kutoa ufafanuzi wa ziada wa sababu za Wanasheria wake kutoa ushauri wa kufungua maombi kwenye mahakama kuu wakati huo huo ikiwa imetoa taarifa ya kukata rufaa (Notice to Appeal) katika mahakama ya rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa tarehe 28 Septemba 2011.

Izingatiwe kwamba hii si mara ya kwanza kwa maombi ya TANESCO yaliyofunguliwa kufuatia ushauri wa Kampuni ya Wanasheria ya Rex Attorney kutulipiwa mbali kwa kurejea kuwa tarehe 20 Februari 2012 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilifanya uamuzi wa kutupilia mbali ombi la Shirika la Umeme (TANESCO) lililotaka mahakama iwaruhusu kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu tuzo ya Kampuni ya Dowans isajiliwe hapa nchini.

Katika muktadha huo, nasisitiza kauli yangu ya tarehe 7 Septemba 2012 ya kuitaka Serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo kueleza ni hatua gani ilichukua kutoka TANESCO ilipowasilisha mahakama ya rufani taarifa ya kusudio la kupinga hukumu iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi Septemba 28 mwaka 2011 iliyoruhusu tuzo hiyo isajiliwe.

Aidha, narudia kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni kiasi cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali.

Izingatiwe kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee jumla ya shilingi bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi hizo kwa kuilipa kampuni ya Rex Attorneys na Makampuni mengine ambayo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa yakiiwakilisha serikali na TANESCO na kushindwa katika mahakama za kitaifa na kimataifa.

Kufuatia mfululizo wa TANESCO kushindwa mahakamani huku mabilioni ya walipa kodi na wateja wake yakitumika, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ahakikishe kuwa ukaguzi Maalum unaoendelea kufanywa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) na uchunguzi unaofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhusu tuhuma za ufisadi na ubadhirifu katika Shirika la Umeme (TANESCO) uhusishe pia ukaguzi wa mabilioni ya matumizi ya fedha za idara ya sheria na ununuzi wa huduma za kisheria kutoka makampuni binafsi unaofanywa na TANESCO.

Ukaguzi na uchunguzi huo ufanywe kuhusu matumizi na ufanisi wa huduma za kisheria ambazo TANESCO imekuwa ikizipata kutoka kwenye makampuni binafsi katika kesi kubwa za kimataifa ikiwemo ya Dowans na IPTL kwa kurejea pia maoni niliyoyawasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012.

Katika hotuba yangu bungeni nilitaka Serikali itakiwe kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kama gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya kuilipa kampuni ya Mkono &Co. Advocates .

Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati ya mwaka 1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha ya makampuni hayo.

Aidha, niliitaka Serikali ieleze mkakati wa kudhibiti ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu wachache. Nilitaja Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.

Waziri wa Nishati na Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanapaswa kutoa kauli sio kuhusu Dowans pekee bali pia kuhusu kesi ya IPTL ambayo mzigo wake wa tozo na gharama za kesi ni mkubwa kuliko hata wa Dowans iwapo TANESCO itashindwa katika kesi zinazoendelea.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya Mkono ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala hilo.

Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama, na kuwa na mfululizo wa utata wa ushauri kama unaojitokeza katika kesi za Dowans unaohusisha Kampuni ya Wanasheria ya Rex Attorneys.

Masuala haya ni muhimu yakazingatiwa wakati TANESCO ikiendelea na hatua ilizozieleza za kupeleka ombi la kuzuia utekelezaji wa hukumu ya mahakama ya ICC kwenye mahakama ya rufaa ya Tanzania na hatimaye kuendelea na taratibu za kukata rufaa.

Pamoja na TANESCO kuendelea na taratibu za kukata rufaa, bado ipo haja kwa Serikali kuzingatia mapendekezo niliyoyatoa nilipowasilisha hoja binafsi kwa Katibu wa Bunge mwaka 2011 kutaka utekelezaji wa maazimio yote yaliyobaki kuhusu mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC ili hatua zaidi zichukuliwe kwa mafisadi na wahujumu uchumi waliohusika na Richmond, Dowans na masuala mengine ya kisheria yanayosababisha mzigo mkubwa kwa TANESCO na wananchi.

Kutokana na rekodi za maamuzi mbalimbali ya kimahakama kuanzia mwaka 2010 mpaka 2012 sasa inajulikana wazi kuwa Mkataba wa TANESCO na Richmond ulirithishwa kinyemela Oktoba 14, 2006 kwenda kwa Dowans huo kama inavyoononekana katika nyaraka za mahakama ambapo Dowans na Richmond zinadaiana huko Marekani; na kwa kuwa hilo lilifanyika bila kuitaarifu TANESCO kinyume na kifungu cha 15.12 cha Mkataba huo.

Kutokana na hukumu ya Dowans ushahidi umepatikana na kuwa mashahidi mbalimbali walioitwa mbele ya Kamati Teule ya Bunge na wakiwa chini ya kiapo walitoa taarifa za uongo kuwa mkataba kati ya Richmond na TANESCO ulihamishwa kwenda Dowans Disemba 23, 2006 na hivyo wahusika hao mbalimbali – wakiwemo wamiliki wa Richmond; walidanganya au kuficha ukweli mbele ya Kamati Teule na hivyo kuonesha dharau dhidi ya Bunge.

Kufichwa kwa taarifa hizo muhimu ndiko kulichangia kukubaliwa kwa kampuni ya Dowans kuchukua Mkataba wa Richmond; wakati tayari ilikuwa imerithishwa kinyume cha mkataba wenyewe hivyo kuliingiza taifa katika deni kubwa linalotaka kugeuzwa kuwa mzigo mkubwa migongoni mwa walipa kodi wa Tanzania katika utekelezaji wa maamuzi ya mahakama iwapo TANESCO ikishindwa kukamilisha taratibu za rufaa au ikishindwa katika hukumu ya rufaa husika.

Imetolewa tarehe 8 Septemba 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

1 comment:

Unknown said...

Pongezi Mnyika kwa kuwajibika vena kama mbunge na kutumia taaluma yako ya sheria kwa moyo wa kizalendo. Hali halisi wanasheria mafisadi wanaipeleka nchi yetu kuwekwa rahani kwa madeni ya kutengenezwa. Wanashirikiana na viongozi na wafanyabiashara kufisidi taifa kwa kiwango cha kustaajabisha. Mabadiliko makubwa yanahitajika kwenye uongozi wa kisiasa nchini ili kulinusuru taifa.