Wednesday, September 26, 2012

Shiriki mkutano wa EWURA na wananchi kuhusu udhibiti wa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi kesho 27 Septemba, 2012; toa maoni kuandaliwe kanuni za kudhibiti ubora na kuwezesha kutolewa kwa bei elekezi


Natoa mwito kwa wananchi wa Jimbo la Ubungo kuhudhuria mkutano wa wadau, wananchi na watoa huduma ya maji kwa magari na visima binafsi katika Jiji la Dar es salaam ulioitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) tarehe 27 Septemba 2012 katika Ukumbi wa Land Mark Hotel River Side Ubungo kuanzia saa 3 asubuhi.

Aidha, katika kujadili ajenda za mkutano huo zilizotolewa naitaka EWURA kuweka mkazo katika kupokea maoni ya wananchi ili kuwezesha kuandaliwa kwa haraka kwa kanuni za usimamizi na bei elekezi ya maji katika jiji la Dar es salaam ikiwemo katika visima na malori binafsi kwa kuzingatia kuwa katika ziara yangu katika kata nane za Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba 2012 nimepokea malalamiko mengi juu ya ongezeko la bei ya maji ambayo imefikia mpaka shilingi mia tano kwa dumu moja la lita 20 bila udhibiti wowote.

Kwa mujibu wa Tangazo la EWURA lililotolewa mwezi Septemba 2012 Mkutano huo ambao wadau wote wa maji ikiwemo wananchi wanaalikwa kushiriki utajadili haki na wajibu wa watoa huduma ya maji Jijini Dar es salaam; mwongozo wa watoa huduma ya maji kwa visima na magari binafsi na utaratibu utakaotumiwa na DAWASCO kusajili watoa huduma wa maji ya visima na wasambazaji wa maji kwa magari binafsi.

Izingatiwe kuwa katika mikutano yangu na wananchi ya awamu ya pili katika kata nane za Jimbo la Ubungo kati ya Agosti na Septemba 2012 nilisisitiza kuwa EWURA ina wajibu kama ilivyo kwenye mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma tu hata binafsi, hata hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande wa mamlaka za umma.

Hivyo, nilitoa mwito kwa wananchi kuungana kuitaka EWURA kueleza hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011 suala ambalo lipaswa kuzingatiwa na wadau watakaoshiriki kwenye mkutano unaofanyika tarehe 27 Septemba 2012.

Itakumbukwa tarehe 2 Machi 2012 nilifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo masuala mengine niliitaka EWURA kutoa kauli ndani ya kipindi cha wiki moja kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya kanuni husika pamoja na udhibiti wa bei ya maji ikiwemo kwenye sekta binafsi katika jiji la Dar es salaam.

Katika mkutano wangu na wanahabari tarehe 2 Machi 2012 nilieleza kuwa kupitia ziara ya kikazi katika kata saba za Jimbo la Ubungo nilibaini kwamba  kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es salaam katika sekta binafsi; bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi biashara haramu yenye kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi wenye kuharibu ratiba ya mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela.

Tarehe 8 Machi 2012 Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa EWURA Titus Kaguo alinukuliwa vyombo vya habari akinijibu kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi kwenye maji kwa kuwa tayari ilishafanya hivyo mwaka 2010 bila kuzingatia kuwa bei elekezi pekee iliyotolewa na EWURA ni katika visima, maghati na mabombo ya umma yanayoendeshwa na DAWASA na DAWASCO.

Kufuatia majibu hayo tarehe 8 Machi 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa kauli ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iliyonukuliwa na vyombo vya habari tarehe 8 Machi 2012 kuwa mamlaka hiyo haiwezi kutoa bei elekezi ya maji kwa kuwa imekwishatoa tayari mwaka 2010 haipaswi kukubaliwa na wananchi na wadau wa sekta ya maji katika Jiji la Dar es salaam.

Katika taarifa hiyo niliitaka EWURA kutimiza kwa ukamilifu wake wajibu wake kwa mujibu wa Sheria mbili muhimu za usimamizi wa sekta ya maji nchini (Water Supply and Sanitation Act of 2009 and The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act)

Katika taarifa hiyo nilitoa mwito kwa EWURA kutoa maelezo ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011.

Pamoja na kutoa taarifa hiyo kwa umma niliiandikia  barua EWURA itimize wajibu wake wa kusimamia ubora na bei hata hivyo nilipokea majibu kuwa muongozo bado haujaandaliwa, hivyo mkutano huu wa tarehe 27 Septemba 2012 ni fursa muhimu ya kuharakisha maandalizi ya kanuni na utaratibu husika.

Ufumbuzi wa kudumu wa kushusha bei ya maji ni DAWASA na DAWASCO kuongeza uzalishaji, usafirishaji na usambazaji hata hivyo udhibiti wa EWURA kuhusu ubora na bei katika kipindi hiki cha upungufu ni muhimu kuepusha madhara kwa umma ya kuuziwa maji yasiyo na ubora na kwa bei ya kuruka hali ambayo inawathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini.

Imetolewa tarehe 26 Septemba 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo


No comments: