Tuesday, February 19, 2013

BAADA YA HOJA BINAFSI NA KUSUDIO LA MAANDAMANO; WAZIRI WA MAJI NA MKUU WA WILAYA WAENDA GOBA NA MAENEO MENGINE KUFUATILIA MIRADI YA MAJI

Nitafuatilia ahadi alizotoa Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe tarehe 17 Februari 2013 kuwa maji yataanza kutoka kata ya Goba tarehe 20 Februari 2013 na ziara ya Mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana kwenye kata hiyo. 

Hata hivyo, ni vizuri umma ukatambua kuwa pamoja na mabadiliko ya hoja kwa kuongeza maneno ya kupendekeza hoja kuondolewa yaliyofanywa na Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kinyume na kanuni za Bunge tarehe 4 Februari 2013, maelezo na hoja binafsi niliyowasilisha bungeni yameongeza uwajibikaji wa Waziri wa Maji, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni na Halmashauri kuhusu masuala ya maji. 

Siku chache baada ya kutangaza tarehe 10 Februari 2013 kwenye mkutano wa hadhara kuipa Serikali wiki mbili, Mkuu wa Wilaya na Meya wa Halmashauri ya Kinondoni waliitisha mkutano na viongozi wa mitaa pamoja na kamati za miradi ya maji ya jumuiya na leo tarehe 18 Februari 2013 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana ameanza ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya maji katika Jimbo la Ubungo. 

Katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au jumuiya za watumia maji. 

Itakumbukwa kwamba kwenye maelezo yangu ya hoja binafsi bungeni nilieleza kwamba katika Halmashauri nyingi nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au jumuiya za watumia maji na nilitoa mifano ya Halmashauri ya Kinondoni. 

Katika maelezo yangu Bungeni nilitoa mfano wa Halmashauri ya Kinondoni na kueleza kuhusu tatizo la maji katika kata ya Goba lililodumu sasa kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano, pamoja na kwamba serikali inaowajibu kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu mamlaka zinazohusika hazijaweza kutimiza wajibu ipasavyo kuhusu kata ya Goba. 

Jana tarehe 17 Februari 2013 Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kupitia mkutano wa hadhara wa CCM kama ambavyo imenukuliwa pia na baadhi ya vyombo vya habari leo tarehe 18 Februari 2013 ametoa ahadi kwamba kuanzia tarehe 20 Februari 2013 wakazi wa Goba wataanza kupata maji. 

Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali, hivyo nitaendelea kufuatilia ahadi hiyo ya Waziri ambayo ni sehemu ya ufumbuzi wa muda mfupi kwa watu wachache lakini bado narudia kutaka majibu ya Waziri wa Maji kuhusu ufumbuzi wa kudumu kwa Wizara kuchukua hatua za ziada ili kata ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na badala yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na DAWASCO ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu. 

Aidha, Waziri wa Maji, Mkuu wa Wilaya na Meya watoe majibu kuhusu malalamiko ya wananchi ya kushindwa kushughulikiwa kwa matatizo ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za Halmashauri iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na kamati za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha wananchi kukosa huduma ya maji. 

Kwa mujibu wa maelezo niliyoyawasilisha kwa Serikali na kwa Bunge kwa nyakati mbalimbali; historia ya tatizo hili inaonesha kuwa wakazi wa Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua ya tarehe 15/10/2009 ikieleza kero ya maji kwa wananchi na wakimtaka alipatie ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya Kinondoni pamoja na hayo bado tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku wakazi wa Goba wakiendelea kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha bila maji. 

Kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia kuandika barua ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua hiyo hakuna jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo. 

Utendaji mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya Kinondoni chini ya kamati za maji zilizosababisha maji kukatwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu wa maji kwa kipindi chote hicho. 

Katika kipindi cha karibuni, kamati ya maji Goba baada ya kukatwa kwa maji ilimwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe 30/08/2011 yenye kumbukumbu namba G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu Mkurugenzi kuhusu kusitishwa kwa huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya Goba. 

Katika barua hiyo ambayo mbunge nilipatiwa nakala yake, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi kwa kutozifanya kazi barua zao wakionesha mfano barua ya tarehe 22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua hatua za haraka ili huduma ya maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea kuchukua hatua zinazostahili. 

Mnamo tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011 yenye kichwa cha barua “Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa Maji Goba” . 

Kutokana na hatua stahili kutochukuliwa niliandika barua nyingine kwa Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na kupendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha kutoka mfuko wa Jimbo Tsh 3,000,000.00 zinapelekwa haraka katika Akaunti ya maji Goba ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa manispaa za kujenga uwezo wa mradi husika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alifanya ziara Goba tarehe 31/01/2012 katika ziara ile mkurugenzi aliwaahidi wakazi wa Goba kurejesha huduma ya Maji ndani ya wiki moja lakini hadi sasa ni zaidi ya mwaka wananchi bado hawajapata huduma hiyo. 

Tarehe 18/03/2012 niliwaandikia barua tena DAWASA yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/006/2012 kuhusu hatua ambazo DAWASA imechukuakuhusu matatizo ya maji katika kata ya Goba, katika barua hiyo nilitaka kujua hatua ambazo DAWASA imechukua kushughulikia matatizo ya maji Goba hususani juu ya kufanya majadiliano na Manispaa ya Kinondoni ili kuwa na mfumo endelevu zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata ya Goba ambayo ina ongezeko kubwa la wakazi, makazi na mahitaji mengine mengi kwa sasa. Wenu katika uwakilishi wa wananchi, John Mnyika (Mb) 

18/02/2013

No comments: