Friday, July 19, 2013

Kufuatia kauli za Serikali magazetini kuhusu mimi na kodi ya umiliki wa kadi za simu; nijibu tu kwa ujumla kwamba SITAACHA. Badala yake naomba kuwapatia namba zao: Makamba 0767783996 na Mgimwa 0754/0684765644, tunachohitaji ni kauli ya Serikali kuwa kodi imesitishwa na itaondolewa na sio siasa chafu.

Kwa mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba kwamba; “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:

Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha walau kidogo kwa maendeleo.

Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.


Aidha, sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi bali nilichukua hatua kwa mujibu wa kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la marekebisho ya kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta ya mawasiliano bali pia kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub sector) nyeti ya mafuta.

Mlioniuliza kwa SMS katika simu na kwenye mitandao ya kijamii sasa ni wakati wa Makamba kuhojiwa kwa njia hizo hizo (Simu yake ya Mkononi ni 0767783996) kwa kuwa yeye ni sehemu ya Serikali na Serikali ndiyo ambayo iliingiza suala hili kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge kupitia hotuba ya Bajeti Serikali na ikalirudia kuliingiza kupitia jedwali la marekebisho ya Sheria ya Serikali; ni wakina nani hasa kwa majina ndani ya Serikali na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni wakina nani hasa waliopigia kura ya ndio kuipitisha?

Aidha, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo tarehe 19 Julai 2013 akieleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita kwake ilikuwa na kuzidiwa nguvu. Hivyo, ataje kwa majina hayo waliozidi nguvu serikali kinyume na matakwa yake. Amenukuliwa akisema pia kwamba anajua kuwa suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima litabadilishwa kwa kuangalia eneo lingine la kutoza kodi. Ni vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha kodi hiyo ni nani na kwanini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati maandalizi yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo katika mkutano ujao?

Wakati Naibu Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa katika Serikali hiyo hiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hii hii ya leo ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao ya simu nchini na watanzania kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya sh 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu za kiganjani.

Na kwa kuwa amesema kwamba Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau, natoa mwito kwa wananchi kumtumia maoni kupitia namba zake za simu za mkononi 0754/0684-765644. Aidha, ni vizuri aeleze subira hiyo ivutwe mpaka lini? Na ni wakina nani hasa kwa majina waliomfanya akaingiza kodi hiyo katika kitabu cha Hotuba yake aliyosoma bungeni kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na hasa kwa majina waliomfanya arejeshe kodi hiyo ya kadi za simu kwenye jedwali la marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha alilowasilisha bungeni.

Nasisiza kuwa kauli za ujumla za Serikali bila kuwataja kwa majina wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge. Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Rais ama kiongozi mwingine mwenye mamlaka ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa kufuta kodi hiyo kuwasilishwa katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 27 Agosti 2013.

Majina ya wahusika yasipotajwa au mamlaka zinazohusika zisipotoa kauli katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki jumapili tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni nitatoa mrejesho kuhusu yaliyojiri katika mkutano uliopita wa Bunge na kueleza hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa kuwezesha majina ya wabunge hao kutajwa hadharani na hatua za kuondoa kodi hiyo kuchukuliwa. 

Uongozi bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi. Twende kazi.

John Mnyika (Mb)

19 Julai 2013

6 comments:

Anonymous said...

nakubali kazi zako john endelea hivyo hivyo tuko pamoja

Anonymous said...

Tuko pamoja Bro John.Endeleza mapambano

YOJAZE said...

KAKA KWANZA POLE SANA NA KAZI, MIMI NAKUUNGA MIKONO YOTE, TENA HATA HUKO AUGUST NI MBALI SANA MI NAONA WA-TAKE WAJIBU HIYO KODI IFUTWE MARA MOJA

Unknown said...

Mheshimiwa hongera kwa kazi nzuri unayoifanya pamoja na wenzako wote. Jipe moyo mkuu kututetea sisi wanyonge na Mola atakujalia baraka tele. Endeleza kazi nzuri unazozifanya kuhusu kuondolewa hii kodi ya laini za simu na usisahau pia suala zima la maji katika jimbo lako na maeneo mengine.

Anonymous said...

Nakupa big up ila ulichofanya kupublish no za mtu mwingine bila idhin yake sio fresh, ila big up endelea na msimamo wako kuwapigania wananchi

Unknown said...

Sisi kama wananchi hizo kodi hatuzitak na kama hawaelew bata hakieleweki