Thursday, October 15, 2009

Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-1



Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-1

Na John Mnyika

Septemba 2009

Mwishoni mwa mwezi Julai niliandika makala kuhusu uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa yenye kuchokoza mjadala kuhusu kanuni za uchaguzi husika. Makala hiyo ilibeba kichwa na maudhui yenye kuulizwa swali: Pinda kupindisha kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa? Niliandika makala hiyo, kabla ya kutolewa kwa kanuni za uchaguzi husika kwa lengo la kuibua mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba kanuni za uchaguzi na taratibu zake zinatolewa kwa kuzingatia makubaliano yaliyotiwa saini kwa pamoja kati ya ofisi yake, vyama vya siasa na asasi za kiraia mnamo mwezi Februari 20 mwaka 2009 kuhusu masuala yanayopaswa kuzingatiwa katika kanuni na taratibu za uchaguzi husika.

Izingatiwe kuwa chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda. Katikati ya mwezi Agosti baada ya kimya cha muda mrefu, kilichoambatana na shinikizo toka kwa wadau kutokana na serikali kuchelewesha kutoa kanuni tofauti na ahadi yake, hatimaye Waziri Mkuu Pinda alitoa kanuni na maelekezo kuhusu taratibu za uchaguzi husika yaliyotolewa kwa nyakati mbalimbali. Sasa ni wakati muafaka kutoa jibu la swali nililolitoa kwa wadau kuibua mjadala.

Ikumbukwe kwamba mwanya huu wa kisheria wa Waziri kutunga kanuni ulitumiwa vibaya mwaka 2004 na kufanya kanuni hizo kutungwa kupendelea chama kinachotawala kwa kuweka mianya ya hujuma za kiuchaguzi. Matokeo yake ni uchaguzi uliopita wa vitongoji, vijiji na mitaa kutokuwa huru na haki kutokana na mapungufu mengi ambayo hata serikali yenyewe iliyakiri.

Mathalani upigaji kura haukuwa wa siri, fujo katika mikutano ya uchaguzi, matayarisho kuwa hafifu, kuingiliwa na maafisa na watendaji wa kata na vijiji ambao walifikia hatua ya kuwatisha wananchi na kutotoa taarifa za muhimu za uchaguzi, kukosekana kwa daftari la wapiga kura na uchaguzi kusimamiwa na chombo kisicho huru cha kiserikali moja kwa moja(Wizara ya TAMISEMI).

Kutokana na mapungufu hayo CCM ilishinda kwa asilimia 96 na kupata mtaji haramu wa kisiasa ambao ilianza nao kama hujuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kufanya uwanja wa ushindani wa kisiasa usiwe sawa. Na hivyo, CCM ikashinda kwa takribani asilimia 80 katika uchaguzi mkuu mwaka mmoja baadaye.



Ilitarajiwa kwamba marekebisho ya haraka yangefanyika, hata hivyo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kati ya mwaka 2005 mpaka 2008. Kesi iliyofunguliwa na vyama vya upinzani mwaka 2004 kuhusu kanuni na taratibu za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa mpaka sasa bado ni kizungumkuti. Kwa upande mwingine, Serikali ilikuwa ikiitisha mikutano na vyama na kuiahirisha bila maamuzi ya msingi kufikiwa kuhusu marekebisho yanayostahili kufanywa katika sheria na kanuni zinazosimamia chaguzi husika.


Mwaka 2009, mwezi Februari ndipo serikali imesaini makubaliano na wadau kuhusu uchaguzi huu. Kwa kisingizio cha ufinyu wa muda, masuala ya msingi yaliyopaswa kufanyiwa marekebisho mengi hayapo kama sehemu ya makubaliano hayo. Kwa mara nyingine tena, serikali imechelewesha muda na baadaye kutumia kisingizio cha muda kukwepa kufanya mabadiliko ya msingi ya kisheria ya kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki.

Kama ilivyotarajiwa kutokana na makubaliano hayo, yafuatayo iliamuliwe yasifanyiwe marekebisho kutokana na sababu mbalimbali zilizotolewa na serikali ikiwemo ufinyu wa muda. Kuhusu kilio cha miaka mingi cha wadau cha kutaka uchaguzi usimamiwe na Tume ya uchaguzi kama ilivyo katika baadhi ya nchi nyingine duniani; makubaliano yameweka bayana kuwa uchaguzi utaendelea kusimamiwa na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa. Ndio maana kanuni zimeendelea kutungwa na waziri badala ya chombo huru. Katika kanuni hizo umri wa kugombea; umebaki kuwa miaka 21 badala ya kushuka mpaka 18. Wagombea binafsi; hawajaruhusiwa.

Mwito wa Vyama vya siasa kutaka viwezeshwe kutoa elimu ya uraia nao haujazingatiwa. Serikali imeendelea kuweka msimamo kupitia maelekezo ya taratibu za uchaguzi husika kuwa jukumu la kutoa elimu ya uraia litaendelea kuwa la serikali. Hoja ya kutaka uchaguzi wa madiwani uende sambamba na chaguzi zingine za mitaa nayo haipo katika kanuni zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda. Uchaguzi wa madiwani utaendelea kuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2010; hii ni kwa sababu suala hili linahitaji marekebisho ya kisheria na serikali ilishatamka wazi kwamba muda umeshakwisha wa kufanya marekebisho husika.

Haya ni masuala nyeti ambayo wadau wengi walipenda yafanyiwe marekebisho lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo Serikali imeyafanya kuhusu masuala hayo katika kanuni zilizotungwa ambazo Waziri Mkuu Pinda ameshazitangaza. Shabaha ya makala hii si kuyajadili masuala hayo ambayo hayakuwemo katika makubaliano ya wadau ya mwezi Februari 2009; masuala haya yanapaswa kutafakariwa na taifa kwa ajili ya marekebisho ya muda mrefu ili kuhakikisha yanazingatiwa katika uchaguzi unaofuata wa vitongoji, vijiji na mitaa wa mwaka 2014. Safari hii, wadau wasikubali serikali itoe visingizio vya ufinyu wa muda kwa kuwa kuna muda wa kutosha kuanzia sasa mpaka wakati huo kuweza kufanya mabadiliko yanayokusudiwa.


Dhima ya makala hii ni kutafakari iwapo masuala kwenye makubaliano ya wadau yameingizwa katika kanuni na taratibu zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 304 ya tarehe 21 Agosti 2009. Tafakari hii inaendeleza mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba marekebisho ya msingi walau yanayogusa mambo ambayo serikali ilishakubaliana na vyama vya siasa na asasi za kiraia yanafanyika kabla ya uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao umetangazwa kufanyika tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka 2009.

Waziri Mkuu Pinda ameweza kuingiza baadhi ya masuala kwenye kanuni na taratibu alizozitoa kama makubaliano ya wadau yalivyohitaji. Mathalani kanuni zimeelekeza kwamba kutakuwa na karatasi maalum za kura zenye nembo ya halmashauri husika; karatasi hazitakuwa na majina ya wagombea, majina yatabandikwa sehemu ya wazi baada ya uteuzi. Maelekezo ya taratibu yanaeleza kuwa uteuzi wa wagombea ni tarehe 5 Oktoba 2009; hivyo wagombea wanaweza kuchukua fomu za kiserikali kuanzia tarehe 28 Septemba mpaka 4 Oktoba, 2009.

Kwa mujibu wa Kanuni Uchaguzi utafanyika kwenye majengo ya umma, kama hakuna msimamizi atashirikiana na vyama kupata sehemu muafaka. Kanuni zimeelekeza kuwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri za Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji utafanyika katika kitongoji ili kuwafanya wapiga kura wengi kuweza kufika na kupiga kura zao; suala hili limewezakana baada ya Bunge kubadili sheria husika katika mkutano wake uliomalizika hivi karibuni. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za Mitaa utafanyika katika mitaa husika, vituo vitakuwa zaidi ya kimoja kulingana na wakazi wa mtaa.

Kwa mujibu wa kanuni Kampeni zitafanyika kwa muda wa siku saba kama ilivyo kwa kanuni za 2004; na maelekezo ya taratibu yameweka bayana kuwa ni kuanzia tarehe 6 mpaka 24 Oktoba 2009.

Orodha ya wapiga kura(Local Voter register) itaandaliwa siku 21 kabla ya uchaguzi ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kukagua orodha na kuweka pingamizi. Orodha itaandaliwa na watumishi wa umma lakini wasiwe watendaji wa vijiji, mitaa au kata. Uthibitisho wa mpiga kura utatokana na jina lake kuwepo katika orodha ya wapiga kura, vitambulisho vitavyotumika kumtambulisha chochote kati ya vifuatavyo- kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha chuo/shule, leseni ya uderava au wakazi kama mpiga kura hana kitambulisho chochote.

Kanuni zina kifungu cha kamati ya rufaa kama ilivyohitajiwa na wadau, wajumbe wake wanatajwa kuwa ni Katibu Tawala wa wilaya, afisa yoyote kutoka Taasisi ya Umma aliyoko katika wilaya husika na afisa yoyote wa umma anayefanya kazi katika ofisi ya katibu tawala wa wilaya ambaye atakuwa katibu na hatakuwa na haki ya kupiga kura. Kanuni pia zimeweka bayana kuwa wafuatao hawatateuliwa kuwa wajumbe wa kamati ya rufaa; afisa anayehusika na uteuzi wa wagombea, msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, kiongozi wa ngazi yoyote wa chama cha siasa na mtumishi wa halmashauri.




Hata hivyo, kwa upande mwingine Waziri Mkuu Pinda na ofisi yake wamepindisha Kanuni na taratibu za uchaguzi wa vitongoji na mitaa na kinyume na misingi ya chaguzi huru na haki ambayo ni mhimili wa utawala bora. Ama kwa hakika mambo haya yanahitaji kutazamwa kwa kina na kwa haraka na wadau wowote ili kuepuka uchaguzi huu kugubikwa na vurugu zenye kutishia amani na demokrasia.

Tayari vyama mbalimbali vimeshaanza michakato ya uteuzi na uchukuaji wa fomu za ndani ya vyama. Katika hali inayoibua maswali mengi, CCM ilianza mchakato wa uteuzi ndani ya chama chao kabla hata ya kanuni za uchaguzi kutolewa na Waziri Mkuu Pinda. Hali hiyo imeelezewa na wachambuzi mbalimbali kuwa ni ishara ya kuwa chama hicho kilipewa kanuni husika mlango wa nyuma na serikali kukipa fursa ya kujiandaa mapema kabla ya kanuni kutolewa kwa vyama vingine. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba kura za maoni katika chama hicho vimetawaliwa na rushwa na vurugu katika maeneo mbalimbali, hali ambayo mpaka sasa imesababisha kifo cha mtu mmoja huko wilayani Serengeti. Kwa upande wa CHADEMA, fomu hizo za uteuzi wa ndani ya chama zimeanza kutolewa kuanzia Agosti 25 na michakato ya uteuzi inaendelea mpaka Oktoba Mosi, 2009 kutegemea na ratiba ya ndani ya mamlaka zinazotoa fomu katika ngazi mbalimbali za chama.

Kama ilivyodokezwa awali, kanuni zimeelekeza kwamba karatasi za kura hazitakuwa na majina ya wagombea na kwamba mpiga kura atalazimika kuandika mwenyewe. Hali inaweza kuchochea kuchelewa ama kuvurugika kwa mchakato wa upigaji na uhesabuji wa kura. Katika nchi ambayo zaidi ya nusu ya wananchi wake hawajui kusoma na kuandika na sehemu kubwa ya wanaojua bado si kwa kiwango kizuri, uamuzi wa kutunga kanuni ambazo zinalazimisha kwamba wapiga kura waandike wenyewe majina kamili ya wagombea umetoa mianya ya kuvurugika kwa uchaguzi.

Waziri Mkuu Pinda pia amepindisha kanuni katika kifungu cha 20(8) ambapo inatamkwa kwamba mpiga kura atapatiwa kura nne; wakati ambapo uchaguzi huo unahusisha mafungu ya nafasi tatu: Mwenyekiti, wajumbe wa ujumla na wajumbe wa viti maalum wanawake. Hivyo, kwa vyovyote vile marekebisho yanapaswa kufanyika ili Oktoba 25 mpiga kura apatiwe kura tatu; hali hii ikiachwa bila ufafanuzi inaweza kuzua mzozo siku ya kupiga kura.

Kwa upande mwingine, yapo maeneo ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imekiri mnamo 11 Septemba 2009 kupitia barua yenye kumbukumbu Na. HB.114/126/01 kwamba maelekezo ambayo imeyatoa yamepindisha kanuni. Mathalani, maelekezo yanasema wajumbe wa Halmashauri ya vijiji wanawake wa viti maalum watakuwa si chini ya 25%. Wakati ambapo Sheria Na. 19 ya mwaka 2009 inatamka kwamba idadi ya wanawake viti maalum katika halmashauri ya kijiji inatakiwa kuwa si chi ya theluthi moja ya wajumbe ambayo kwa vyovyote vile sio chini ya wanawake nane(8). Wakati kanuni zinazungumza kwamba ukomo wa utumishi wa wenyeviti na wajumbe wao walioko madarakani hivi sasa ni siku tatu kabla ya uteuzi ambayo ni tarehe 02 Oktoba 2009; tayari ofisi ya Waziri Mkuu ilishatoa maelekezo kwamba utumishi wao ulikoma toka tarehe 2 mwezi Septemba 2009. Kitendo cha Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi tarehe 11 Septemba kubatilisha maelekezo ambayo waliyatoa kabla kinaacha maswali mengi kuhusu uhalali wa wenyeviti wa mitaa na wajumbe walioko madarakani hivi sasa ambao walishatangazwa kujiuzulu nyadhifa zao toka mwanzoni mwa mwezi Septemba. Katika makala inayofuata nitaeleza hoja zaidi zinazodhirisha mapungufu zaidi yaliyopo kwenye kanani na maelekezo na hatua zinazohitaji kuchukuliwa na wadau kwa haraka ili kuhakikisha uchaguzi husika unakuwa huru na haki.


Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na http://mnyika.blogspot.com













No comments: