Thursday, October 15, 2009

Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-2

Waziri Mkuu Pinda kapindisha kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa-2

Na John Mnyika

Septemba 2009

Katika makala iliyopita nilianza kutafakari iwapo masuala kwenye makubaliano ya wadau yameingizwa katika kanuni na taratibu zilizotolewa na Waziri Mkuu Pinda kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 304 ya tarehe 21 Agosti 2009. Makala hii inaendeleza mjadala wa wadau kuhakikisha kwamba marekebisho ya msingi walau yanayogusa mambo ambayo serikali ilishakubaliana na vyama vya siasa na asasi za kiraia yanafanyika kabla ya uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao umetangazwa kufanyika tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka 2009.

Izingatiwe kuwa chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu Pinda amepindisha kanuni na taratibu kuhusiana na uandikishaji wa Orodha ya wapiga kura. Kwa mujibu wa Kanuni, Waziri Mkuu alipaswa kutoa tangazo kwa umma kupitia magazeti yanayosambazwa nchi nzima ya kiingereza na Kiswahili si chini ya siku tisini kabla ya uchaguzi ili umma uweze kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi. Kama sehemu ya kutekeleza kifungu hicho cha kanuni, Waziri Mkuu Pinda alitangaza ratiba ya uchaguzi na shughuli zinazohusika kupitia Tangazo ambalo alilichapa katika baadhi ya magazeti Julai 25 mwaka 2009. Katika tangazo hilo pamoja na mambo mengine ratiba ya uchaguzi ilieleza kuwa uandikishaji wa wapiga kura ungefanyika kwa jumla ya siku 21 kuanzia tarehe 4 mpaka 24 Septemba, 2009.

Hata hivyo, takribani mwezi mmoja baadaye Waziri Mkuu Pinda akaamua kupindisha Kanuni na Taratibu kwa kutoa maelekezo ya uchaguzi yenye kuelekeza kuwa uandikishaji utafanyika tarehe 4 mpaka 10 mwezi Oktoba. Ikifuatiwa na uhakiki na hatimaye Orodha ya mwisho ya wapiga kura imepangwa kubandikwa kati ya tarehe 23 na 25 Oktoba 2009. Tafsiri ya maamuzi haya ni kwamba siku za uandikishaji wa wapiga kura, zimepunguzwa kutoka ishirini na moja(21) mpaka siku saba(7) tu; na pia orodha haitaandaliwa siku ishirini na moja(21) kabla ya uchaguzi kama makubaliano ya wadau na kanuni zinavyohitaji. Hiki ni chanzo kingine cha vurugu, kwani wasimamizi wamepewa mamlaka ya kuendelea kubandika orodha za wapiga kura mpaka siku yenyewe ya uchaguzi!. Suala hili ni nyeti kwa uzoefu katika chaguzi mbalimbali unakumbusha kuwa orodha ya wapiga kura ni moja ya zana inayotumika kuhujumu uchaguzi ama kwa kufanya wapiga kura wa upinzani majina yao yasionekane kwenye orodha za nje ya vituo au kwa kupenyeza wapiga kura wa nyongeza.

Waziri Mkuu Pinda pia amepindisha makubaliano ya wadau kwa kutoa kanuni zinazoeleza kwamba Kamati ya Rufaa itakuwa na wajumbe watatu, kati yao mmoja hatakuwa kura. Hii ni sawa na kuwa na kamati ya watu wawili, ambayo maamuzi ya kutumia kura ambao kura zitakuwa zinagongana na hakuna kifungu kinachompa yoyote kura ya turufu. Kanuni na maelekezo havitoi fursa kwa vyama kuweza kufahamishwa majina ya wajumbe wa kamati ya rufaa na kuwaweka pingamizi kama itahitajika. Marekebisho ya haraka yanastahili kufanyika kuongeza idadi ya wajumbe wa kamati ya rufaa lakini pia kutoa ratiba yenye kutoa fursa kwa vyama kuweza kufahamishwa kwa majina wajumbe wa Kamati ya rufaa na kuwawekea pingamizi kama vyama vitahitaji.

Kwa upande mwingine, yapo maeneo ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu imekiri mnamo 11 Septemba 2009 kupitia barua yenye kumbukumbu Na. HB.114/126/01 kwamba maelekezo ambayo imeyatoa yamepindisha kanuni. Mathalani, Wakati Kanuni zinasema kwamba siku ya kura watu wawe mita 300 kutoka kituo cha kupiga kura, maelekezo yanasema mita 200. Kwa upande mwingine, unaweza kujiuliza dhamira ya Waziri Mkuu Pinda na jopo lake wakati wanapanga umbali mrefu kiasi hicho hasa ikizingatiwa kuwa katika uchaguzi mkuu umbali kwa mujibu wa sheria ni mita 100 tu!. Pengine uzoefu wa chaguzi ndogo za Tarime, Busanda, Biharamulo na kwingineko umeisukuma serikali kutaka watu wasiosogee kabisa karibu na vituo baada ya kupiga kura; hali ambayo inaacha maswali mengi kuhusu dhamira ya serikali ya kuzuia watu kushuhudia kinachoendelea kama sehemu ya uwazi wa mchakato wa uchaguzi. Uamuzi wa Waziri Mkuu Pinda kuweka umbali mrefu kiasi hicho unaweza kuzua mivutano baina ya raia na vyombo vya dola kwa kuwa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa unafanyika kwenye ngazi ya chini sana na vituo vya kura viko karibu na makazi ya wananchi; swali la kujiuliza, ni je wananchi itabidi waondolewe umbali huo wa mita 300 ili wasije wakakamatwa kwa kukiuka kanuni, na je watakubali bila kuwa na hisia kwamba wanaondolewa ili wakae mbali kuruhusu mianya ya hujuma za kiuchaguzi?

Hata hivyo, kifungu husika pia kina utata kwa kuwa hakitamki kuhusu ‘kusimama’ kama ilivyo katika sheria ya uchaguzi inayohusu uchaguzi mkuu, bali kinazungumzia kukataza kuvaa sare au kuonyesha ishara za chama ndani ya umbali huo. Hivyo, ufafanuzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliotolewa kwa barua yake ya Septemba 11, 2009 kuhusu suala hilo ni batili kwa kuwa unarejea maelekezo ambayo kanuni hazijayatoa. Kama tutasoma na kuzifuata kanuni mstari kwa mstari basi ukweli ni kuwa wananchi hawajakatazwa kusimama karibu na vituo ili mradi wasiwe wamevaa sare za chama chochote cha siasa!.

Pia maelekezo ya uchaguzi yaliyotolewa na Waziri Mkuu Pinda yanapingana na kanuni ambazo ofisi yake imezitoa kuhusiana na dhamana ya wagombea. Kanuni zitaka mgombea awe amedhaminiwa na chama cha siasa. Hata hivyo, katika maelekezo Ofisi ya Waziri Mkuu imekwenda mbali zaidi kwa kuongeza maneno mengine ambayo hayapo kabisa kwenye kanuni ya kwamba mgombea lazima awe amedhaminiwa na ‘ngazi ya chini kabisa ya chama chake’. Mathalani katika CHADEMA ngazi ya chini kabisa ya chama ni msingi, ambayo ikifuatiwa na ngazi ya Tawi. Kwa upande wa CCM ngazi yao ya chini ni mashina halafu ndio matawi yanafuata. Kwa maelekezo hayo ya Ofisi ya waziri mkuu, dhamana ya mgombea ikiwa ni ngazi ya chini maana yake ni kuwa mgombea anapaswa adhaminiwe na msingi kwa CHADEMA na shina kwa CCM. Maelekezo hayo yanapingana kabisa na katiba za vyama shiriki ambazo zimeeleza bayana ni ngazi zipi zenye mamlaka ya kudhamini wagombea. Maelekezo hayo yanafunga pia milango kwa ngazi za juu za chama mathalani kata na kuendelea kudhamini wagombea kama ikibidi. Hivyo kwa ujumla, maelekezo hayo yanapaswa kubatilishwa mara moja kwa kuwa yanapingana na kanuni na katiba za vyama na yanatoa mianya kwa wagombea kuwekewa mapingamizi kutokana na utata kuhusu udhamini wao.

Yapo maneno muhimu ambayo yametumiwa kwenye kanuni na maelekezo ambayo hayajapatiwa tafsiri ya kuridhisha kuzuia mianya ya kupindishwa kwa kanuni na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao. Maneno hayo ni “Mkazi” na “Kipato halali”. Neno “Mkazi” limetafsiriwa kuwa ni raia wa Tanzania ambaye kwa kawaida anaishi katika kaya au taasisi iliyopo katika eneo husika. Tafsiri hii inaacha maswali mengi, kwa kuwa bila tafsiri kamili mpiga kura ama hata mgombea anaweza kuwekewa pingamizi kuwa hastahili kupiga kura au kugombea katika eneo Fulani. Maswali ya kujiuliza ni nini maana ya mkazi wa kawaida? Je mtu aliyehamia siku ya kujiandisha katika eneo Fulani anaweza kuhesabika moja kwa moja kuwa mkazi wa eneo hilo? Je, mtu aliyeishi miaka mingi katika eneo hilo akahama kwenda kwingine, akirejea kujiandikisha je bado anaweza kutambulika kuwa mkazi wa eneo husika? Nani mipaka ya vitongoji, vijiji na mitaa inatambulika kikamilifu na wananchi? Maana mtu anaweza kuwekewa pingamizi kwa kuambiwa tu kuwa kaya au taasisi anayoishi haiko ndani ya mipaka ya mtaa aliotaka kujiandikisha au aliojiandikisha. Jambo hili nalo linaweza kuwa chanzo cha mivutano hasa ukizingatia mambo yanayoendelea Zanzibar katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, ambao vitambulisho vya ukazi vinatumika kama kigezo cha kuamua nani aandikishwe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Kwa upande mwingine, kanuni zimetaja sifa mojawapo ya mgombea kwamba awe “ana kipato halali kinachomwezesha kuishi”. Hata hivyo, hakuna mahali popote, hata kifungu cha tafsiri ambapo maneno ‘kipato halali kinachomwezesha kuishi’ yamefafanuliwa. Jambo hili linaweza kutazamwa juu juu, lakini katika taifa ambao sehemu kubwa ya wananchi wamejiajiri katika sekta isiyo rasmi, na katika mazingira ya hujuma za kiuchaguzi; mgombea anaweza kuwekewa pingamizi kwa kuelezwa kuwa hana kipato halali kinachomwezesha kuishi. Mgombea ambaye amejiajiri kwenye ngazi ya chini kabisha hana kitambulisho cha kazi yake, anategemea hisani ya viongozi wa kiserikali kumuandikia barua za kumtambulisha hali ambayo ina mianya ya hujuma. Utata huu wa kukosekana kwa tafsiri unaweza kutoa mwanya kwa wasimamizi kukubaliana na mapingamizi yasiyokuwa na msingi wowote na kuwaengua wagombea, katika mazingira ambayo uchaguzi unasimamiwa na watumishi wa umma ambao hushinikizwa kuegemea matakwa ya chama tawala. Hivyo, ni lazima ufafanuzi utolewe ambao utahitaji mzigo wa kutoa ushahidi (burden of proof) uwe kwa anayeweka pingamizi badala ya anayewekewa pingamizi. Ielezwe wazi kuwa ni jukumu la mweka pingamizi kuonyesha kwamba Fulani hana kipato halali, ama ana kipato haramu au hana kipato kabisa. Ama sivyo, ufinyu wa tafsiri uliopo unatoa mwanya wa kupindishwa kwa kanuni na kuchochea mivutano katika mchakato wa uteuzi.

Kwa ujumla, kama kuna eneo ambao Waziri Mkuu Pinda amepindisha kanuni za msingi za uchaguzi huru na haki basi ni kuhusu uteuzi wa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi. Kwa mujibu wa kanuni, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa, wilaya ama afisa mwingine wa umma atayeteuliwa kwa ajili hiyo. Hata hivyo, si kanuni hazielezi mchakato wa uteuzi ambao ungetoa fursa kwa vyama kuweza kuweka pingamizi kama havikubaliani na uteuzi wa msimamizi wa uchaguzi. Kinachoshangaza zaidi ni kuwa maelekezo yaliyotolewa yamechukulia moja kwa moja tu tayari wakurugenzi ndio wasimamizi na moja kwa moja wamepewa mamlaka ya kuteua wasimamizi wasaidizi.

Kwa upande wa wasimamizi wasaidizi kanuni zimetaja kuwa ni maofisa watendaji wa vitongoji, vijiji, mitaa ama maofisa wengine watakaoteuliwa kwa ajili hiyo; kwa upande wao pia mchakato wa uteuzi haujatoa fursa ya kuwawekea pingamizi. Hii imeondoa uhuru wa mchakato mzima kwa kuwa uchaguzi unaposimamiwa na msimamizi au msimamizi msaidizi ambaye wadau hawamkubali tayari uhalali wa mchakato mzima unakuwa mashakani kwa kuruhusu mianya ya hujuma. Lakini pia, kuruhusu watendaji ambao kwa mujibu wa kanuni hizo hizo ni wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Kamati za Mitaa kusimamia uchaguzi ni kinyume kabisa na utawala bora. Katika maeneo mbalimbali ya nchi, watendaji hao ndio ambao wameshirikiana na wenyeviti kufanya ufisadi ama kutumia madaraka vibaya, kanuni zilizotungwa na Waziri Mkuu Pinda zinawapa mamlaka watu hao hao kusimamia uchaguzi. Inakuwaje pale wenyeviti waliokuwa madarakani, ambao kimsingi ndio ‘mabosi’ wao na washirika wao wa karibu katika kipindi chote walichoongoza? Hali hii inatoa fursa ya kuvurugika kwa uchaguzi. Lakini hata baada ya uchaguzi, kwa mujibu wa kanuni ni watendaji hao hao ndio ambao kwa nafasi yao ni makatibu wa Halmashauri za Vijiji na Kamati za Mitaa; unategemea kweli utawala bora baada ya heka heka za ama kupendeleana au kukomoana wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi? Kama ilikuwa ni lazima kutumia watendaji wa vitongoji, vijiji na mitaa; basi walau wangefanya kazi hiyo katika maeneo ya jirani yao badala ya kufanya kazi hizo kwenye maeneo yao. Ingewezekana kabisa kwa Waziri Mkuu Pinda kuweza kutunga kanuni ambazo zingetumia watumishi wengine wa umma pekee; nje ya watendaji wa mitaa ili kuweka uwanja sawa wa kisiasa na kuzingatia misingi ya utawala bora.

Izingatiwe kuwa mfumo wa utawala wa nchi yetu unaanzia katika vitongoji, vijiji na mitaa ambayo ina mamlaka kadhaa ya kiutendaji na kimaamuzi. Kuruhusu uchaguzi huu kuvurugika ama kuleta viongozi wabovu, kama taifa tutakuwa tumeweka msingi legelege wa utawala na demokrasia na athari zake zitaonekana katika kukwama kwa jitihada za kimaendeleo. Awali kabla ya kanuni kutoka niliweka bayana kwamba njia kuu ya kuzuia upindishaji wa kanuni, ni kuwashirikisha wadau kupitia rasimu ya kanuni kabla ya kuchapwa kwenye gazeti la serikali ili kuhakikisha kwamba makubaliano yote yamezingatiwa. Lakini Waziri Mkuu Pinda ametunga kanuni moja kwa moja bila walau kuitoa rasimu kwa vyama ndio maana udhaifu huu haukuweza kurekebishwa mapema. Katika muktadha huo, jibu la swali langu ni kuwa Waziri Mizengo amefanya ‘mizengwe’ na kupindisha kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Ameweka uwanja usio sawa wa kisiasa hivyo ni wajibu wa wadau wote kuingilia kati kwa haraka kurekebisha hali hii ili tusije kuwa uchafuzi wa amani na demokrasia. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha nchi yetu inakuwa na uchaguzi huru na haki kuanzia kwenye vitongoji, vijiji na mitaa. Bado kuna fursa ya kurekebisha kanuni, bado Waziri Mkuu Pinda anaweza kurekebisha hali ya mambo na kutoa ufafanuzi na maelekezo mbadala.


Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na http://mnyika.blogspot.com



No comments: